Utaratibu wa Kutembelea Bunge
UMUHIMU WA WANANCHI KUTEMBELEA BUNGE
Bunge ni Chombo cha Uwakilishi wa Wananchi kwa mujibu wa Ibara ya 62 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Hivyo kimsingi Bunge ni Chombo cha Uwakilishi wa Wananchi. Kwakuwa haiwezekani wananchi wote kukusanyika mahali pamoja na kufanya maamuzi muhimu katika uendeshaji wa nchi, uwakilishi hauna budi kuwepo. Hii inamaanisha kwamba Wabunge wanapokuwa Bungeni wanafanya kazi ya kuwawakilisha wananchi.
Ofisi ya Bunge kwa kutambua hilo imeweka utaratibu maalumu ambapo jamii huruhusiwa kuhudhuria na kushuhudia namna ambavyo Wawakilishi wa Wananchi wanavyotekeleza majukumu yao.
Bunge hufanya mikutano yake mara nne kwa mwaka Jijini Dodoma, wakati wa mikutano hivyo watu mballimbali huruhusiwa kutembelea Bunge na kujionea linavyoendesha shughuli zake. Wageni wanaweza kuruhusiwa kuingia Ukumbi wa Bunge katika sehemu yoyote ya Ukumbi huo ambayo imetengwa kwa ajili yao.
UTARATIBU WA KUTEMBELEA BUNGE
Fursa ya kutembelea Bunge ipo wazi ambapo watu binafsi, vikundi, watumishi wa taasisi za Serikali, Mabalozi wanaowakilisha mataifa yao nchini, mashirika ya kidini, asasi za kiraia, taasisi za kijamii, wanafunzi wa shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu na wageni kutoka Mabunge nje ya Tanzania au taasisi za kimataifa hutumia fursa iliyopo kutembelea Bunge na kuona jinsi linavyoendesha shughuli zake.
Utaratibu mzuri unaopaswa kufuatwa kwa wanaotaka kutembelea Bunge ni kuandika barua ya maombi ya kutembelea Bunge. Barua hiyo ni vyema ikaelekeza tarehe inayokusudiwa, idadi na madhumuni ya kutembelea Bunge na kutuma kwa anwani ifuatayo:
Katibu wa Bunge
Ofisi ya Bunge,
10 Barabara ya Morogoro,
S.L.P. 941,
40490 Tambukareli,
DODOMA.
Katibu wa Bunge,
Ofisi Ndogo ya Bunge,
S.L.P. 9133,
Barabara ya Shaaban Robert
DAR ES SALAAM.
Katibu wa Bunge,
Ofisi Ndogo ya Bunge,
S.L.P. 362,
ZANZIBAR.
Baruapepe: cna@bunge.go.tz
Ofisi ya Bunge hujibu barua zote za maombi ya kutembelea Bunge. Maombi yote hukubaliwa kama yalivyo, isipokuwa tu kama maombi mengi yamegongana tarehe na idadi ya watu ni kubwa kuzidi uwezo wa maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya wageni. Ikitokea hivyo, ushauri hutolewa kwa baadhi ya waombaji kupanga tarehe nyingine muafaka.
Njia nyingine kwa wageni kutembelea Bunge ni kupitia kwa Wabunge wao. Mbunge anapokuwa na wageni wanaotaka kutembelea Bunge, hutakiwa kujaza fomu maalumu ambayo ataandika idadi ya wageni, tarehe wanayotaka kuja kutembelea Bunge na uhusiano wake na wageni anaowaombea. Aidha, Mbunge anaweza kuwasilisha maombi ya wageni ya kutembelea Bunge kwa kupeleka barua kwa Katibu wa Bunge. Ombi la Mbunge hushughulikiwa kama ombi lingine la wananchi.
Ni haki ya kila mtu kutembelea Bunge ili kujionea shughuli za uwakilishi zinavyotekelezwa. Hivyo, wageni wanaombwa kutumia fursa hii kutembelea Bunge lao.
MAMBO YA KUZINGATIWA KWA WAGENI
Vikao vya Bunge huanza saa 3.00 asubuhi na kwa kawaida huendelea hadi saa 7.00 mchana ambapo husitishwa. Wabunge hurejea tena saa 11.00 jioni na kikao huendelea hadi saa 1.45 usiku ambapo Bunge huahirishwa mpaka siku inayofuata. Hivyo basi, wageni wote wanapaswa wawe wameketi katika maeneo husika kabla ya saa 2.45 asubuhi na saa 10.45 jioni kabla ya vikao kuanza.
Kwa kuzingatia Kanuni za Kudumu za Bunge, wageni wote wanapaswa kuvaa mavazi ya heshima. Baada ya kufika katika milango ya kuingilia, wageni wote husajiliwa na kupatiwa vitambulisho maalumu vitakavyovaliwa wakati wote wawapo katika maeneo ya Bunge.
UTARATIBU WA UKAAJI NDANI YA UKUMBI
Ndani ya Ukumbi wa Bunge wageni wanapaswa kufuata na kuzingatia masharti yafuatayo: -
- Kukaa kimya na kwa heshima inayostahili hadi watakapotoka nje ya Ukumbi huo;
- Kuingia na kutoka ukumbini kwa staha;
- Hairuhusiwi kusoma kitabu chochote, gazeti, barua au hati nyingine ambayo si Orodha ya Shughuli za Bunge;
- Hairuhusiwi kuandika wala kurekodi jambo lolote
,linalozungumzwa, isipokuwa tu kama ni wawakilishi wa vyombo vya habari au maafisa wa Serikali; - Hairuhusiwi kuvuta sigara au kiko wakati wowote wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge au mahali popote nje ya ukumbi huo ambapo kuna mahali pa kukaa wageni;
- Kuzima simu za mikononi;
- Hairuhusiwi kuingia na kamera wala kupiga picha kwa kutumia kifaa chochote kile;
- Hairuhusiwi kufanya jambo au kitendo chochote ambacho kinaweza kuvuruga amani na utulivu Bungeni; na
- Kurejesha kitambulisho wakati wa kuondoka maeneo ya Bunge.
Taratibu hizi zimewekwa ili kulinda utulivu na amani katika maeneo ya Bunge. Mara baada ya kushuhudia Vikao vya Bunge vinavyoendeshwa, wageni wanaotembelea Bunge hupata fursa ya kupewa elimu kuhusu ya Historia ya Bunge, Muundo na Majukumu ya Bunge, nafasi ya Kambi Rasmi ya Walio Wachache Bungeni ikiwa ni pamoja na kutembelea maeneo mbalimbali katika viwanja vya Bunge kujionea mandhari ilivyo.