Bunge Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge la Tanzania

Habari

SPIKA MUSSA ZUNGU AHIMIZA UFANISI KUELEKEA BUNGE LA BAJETI


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb), amefunga mafunzo maalum yaliyolenga kuwajengea uwezo viongozi waandamizi wa Bunge katika utekelezaji wa majukumu yao kitaifa na kimataifa.

 

Mafunzo hayo yamefungwa leo, Februari 18, 2026, katika Ofisi Ndogo za Bunge zilizopo Tunguu, Zanzibar, ambapo yamewakutanisha wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Tume ya Utumishi wa Bunge, pamoja na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge.

 

Akizungumza wakati wa kilele cha mafunzo hayo, Mhe. Spika alitoa shukrani za dhati kwa wajumbe wote kwa nidhamu na ushiriki wao madhubuti tangu siku ya kwanza. Aidha, aliwapongeza watoa mada kwa kuandaa maudhui yaliyoenda sambamba na mabadiliko ya sasa ya kiutendaji katika Bunge na Serikali.

 

Amesisitiza kuwa weledi uliopatikana utakuwa nguzo muhimu katika kutekeleza majukumu ya msingi ya Bunge na kuiwakilisha nchi vyema katika medani za kimataifa.

 

“Niwaombe Waheshimiwa Wabunge kuyashika mafunzo haya yaliyofundishwa ili iwe chachu tunapoelekea katika Bunge lijalo la Bajeti,” alisisitiza Mhe. Spika, akiashiria kuwa maarifa hayo ni silaha muhimu katika kuchambua na kusimamia mpango wa matumizi ya nchi.

 

Mafunzo haya yanatazamwa kama hatua ya kimkakati ya kuhakikisha viongozi wa Kamati wanakuwa na uelewa mpana wa kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na uelewa wa kidiplomasia, jambo litakalosaidia kuimarisha usimamizi wa Serikali na uwakilishi wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.