Kazi
Kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 63, Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake. Katika kutekeleza majukumu na Madaraka, Bunge linaweza:-
- Kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;
- Kujadili utekelezaji wa majukumu ya kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa Bajeti wa kila mwaka;
- Kujadili na kuidhinisha Mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;
- Kutunga sheria pale ambapo suala husika utekelezaji wake unahitaji kuwapo sheria; na
- Kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.
Hivyo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linafanya kazi kuu zifuatazo:-
- Kusimamia na kuishauri Serikali;
- Kuwakilisha maslahi ya wananchi;
- Kutunga sheria; na
- Kuridhia Mikataba ya Kimataifa.