Bunge Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge la Tanzania

Habari

WENYEVITI WA KAMATI ZA BUNGE WAKUTANA ZANZIBAR


Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema kamati za kudumu za Bunge ni muhimili muhimu wa utekelezaji wa majukumu ya kuisimamia Serikali na kuona ufanisi wa utendaji na uwajibikaji unafikiwa.

Mhe. Abdulla amesema hayo tarehe 16 Februari, 2026 katika Ofisi ndogo za Bunge, Tunguu-Zanzibar wakati akifungua mafunzo kwa Kamati ya Uongozi, Tume ya Utumishi wa Bunge na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge.

Amesema mafunzo ya aina hiyo kwa kamati za Bunge kwa kiasi kikubwa huongeza ufanisi wa kazi na majukumu kwa wabunge wapya kupata mbinu zitakazofanikisha utendaji wa kuisimamia Serikali.

Ameongeza mabadiliko mapya na mageuzi yanayofanyika yanahitaji mbinu na kujifunza kwa hivyo aliwataka wabunge hao kuwa makini na mafunzo hayo ambayo watayatumia katika kuendesha kamati zao na hivyo kuleta ufanisi wa uwajibikaji unaohitajika.

“Nimefurahishwa kuona mafunzo haya yanafanyika Zanzibar ambapo matarajio yetu wenyeviti wa kamati na wasaidizi wao kwa kiasi kikubwa mtakuwa makini kupokea mafunzo ambayo yataendeshwa na viongozi waliobobea katika masuala ya mabunge ya jumuiya ya madola.”alisema.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amesema mafunzo hayo ya siku tatu (3) yanawakutanisha wenyeviti na makamu wenyeviti wa kamati za Bunge pamoja na Tume ya Utumishi wa Bunge.

Amesema mafunzo hayo ni muhimu yatawasaidia kujifunza mbinu mbalimbali za uongozi na utendaji katika mabunge pamoja na masuala ya diplomasia ya kibunge katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku katika uendeshaji wa chombo hicho.

“Tumekutana hapa kwa siku tatu ambapo wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge pamoja na wasaidizi wao watapata mbinu za utendaji na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao zinazoendana na wakati uliopo sasa ambapo nashukuru wapo walimu wangu hapa na magwiji katika uendeshaji wa shughuli za Bunge.”amesema.