Bunge Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge la Tanzania

Habari

SPIKA ZUNGU AKUTANA NA SPIKA WA BUNGE LA INDIA, WAHIMIZA USHIRIKIANO WA KIBUNGE NA TEKNOLOJIA


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu, amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la India (Lok Sabha), Mhe. Shri Om Birla, wahimiza ushirikiano wa Kibunge na Teknolojia.

Mazungumzo hayo yamefanyika  katika ofisi ya Spika Bungeni Jijini New Delhi nchini India wakati wa Mkutano wa 28 wa Maspika na Wenyeviti wa Bunge wa Jumuiya ya Madola (CSPOC) unaoendelea nchini humo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mhe. Zungu alielezea kuwa matumizi ya Akili Unde (AI) yatakuwa na manufaa endapo Nchi zitakuwa na uhuru wa kidijitali yaani ‘’Digital Sovereignty” katika kuzalisha, kutunza na kuhifadhi data ili kulinda usalama wa data hizo dhidi ya mashambulizi ya kimtandao.

Kuhusu Ushirikiano wa Kibunge Mhe. Zungu alizungumzia kuhusu umuhimu wa kuendeleza Kundi la Urafiki wa Kibunge ( Parliamentary Friendship Group) kati ya mabunge hayo mawili ili kuimarisha uhusiano uliopo.

Aidha, Mhe. Zungu alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya India na Bunge lake kwa mapokezi mazuri na maandalizi ya kiwango cha juu ya mkutano huo wa Maspika na Wenyeviti wa Bunge wa Jumuiya ya Madola (Conference of the Speakers and Presiding Officers of the Commonwealth-CSPOC).

Kwa upande wake Spika wa Bunge la India, Mhe. Shri Om Birla alimpongeza Mhe. Zungu kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 13 na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Mabunge ya India na Tanzania.

Ameongeza kuwa nia ya India ni kuendelea kuwa mshirika wa Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha eneo la Akili Unde (AI). Aidha, Bunge la India litaendelea kutoa fursa za mafunzo na kujenga uwezo kwa watumishi na wabunge wa Tanzania ili kuongeza ufanisi.

Mkutano huu ni mwendelezo wa juhudi za Tanzania kuimarisha diplomasia ya kibunge na mataifa rafiki duniani.