Bunge Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge la Tanzania

Habari

Mkataba wa ujenzi wa Hoteli ya Nyota Tano ya CPA Kanda ya Afrika wasainiwa


Umoja wa Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika (CPA Africa Region) umesaini Mkataba wa Ujenzi ya Hoteli ya Nyota Tano na Kampuni ya CRJE (East Africa) Limited kutoka nchini China.

Mkataba huo umesainiwa na Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uwekezaji ya CPA-Afrika (Commonwealth Investment Company Limited - CICL) Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson na Mwakilishi wa Mkandarasi kutoka kampuni ya CRJE (East Africa) Limited, Ndg. Lu Chunbao.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Mheshimiwa Dkt. Tulia aliishukuru Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa kwa kutoka ardhi pamoja na vibali vyote vya ujenzi wa Hoteli hiyo itakayojengwa eneo la Njedengwa katika Jiji la Dodoma.

“Ujenzi wa Hoteli hii ya kwanza ya Nyota Tano Jijini Dodoma unaendana na mpango wa Serikali wa kukamilisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, hivyo wageni wengi watashuka na kufikia katika hoteli hiyo ikiwemo wageni wanaokuja kuonana na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Alisisitiza Wakandarasi kuhakikisha wanamaliza kazi ndani ya muda wa miezi 22 kama ambavyo wamekubaliana katika Mkataba uliosainiwa.

Aidha, alisema CPA Kanda ya Afrika inatambua mchango wa Spika Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi mstaafu wa Kampuni wa CICL Hayati Job Ndugai katika ujenzi wa hoteli hiyo.

Alisema akiwa mwenyekiti wa Bodi ya CICL ndiye alishawishi ujenzi wa kitega uchumi hicho kufanyika nchini Tanzania ambako ndipo yalipo Makao Makuu wa CPA Kanda ya Afrika.

Aliishukuru benki ya CRDB kwa kukubali kushiriki katika ujenzi wa hoteli hiyo.

Kwa upande wake Mweka Hazina wa CPA Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mbunge kutoka Bunge la Uganda, Mheshimiwa Enos Asiimwe alisema Hoteli hiyo ni mradi wa kwanza kutekelezwa na umoja huo na kwamba ni matumaini yao mradi huo utakuwa na mafanikio makubwa.

Alisema anatarajia kampuni ya CRJE haitawaangusha katika kutekeleza mradi huo na kwamba utamalizika kwa wakati.

Awali Katibu wa Bunge ambaye pia ni Katibu wa Kampuni ya CICL, Ndugu Baraka Leonard aliwashukuru washiriki wote wa hafla hiyo ya kutiliana saini na kwamba mradi huo wa hoteli utaacha alama kubwa ndani ya CPA na pia utaimarisha umoja huo na kuongeza mapato ya CPA.