Bunge Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge la Tanzania

Habari

Mkutano wa Pili wa Bunge Waanza Jijini Dodoma


Mkutano wa Pili wa Bunge la Kumi na Tatu (13) umeanza Siku ya Jumanne tarehe 27 Januari, 2026 Jijini Dodoma. Shughuli zitakazofanyika katika Mkutano huo ni pamoja na:-

Kiapo cha uaminifu

Kutakuwa na kiapo cha uaminifu na ahadi ya uzalendo kwa Wabunge wateule ambao hawakupata fursa ya kuapishwa katika Mkutano wa Kwanza wa Bunge.

Maswali

Kama ilivyo ada katika kila Mkutano wa Bunge kunakuwa na kipindi cha Maswali Bungeni kila siku ambapo jumla ya maswali 160 yataulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Mawaziri. Aidha, kutakuwa na kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu siku ya Alhamisi ambapo takriban maswali kumi na sita (16) yataulizwa na Waheshimiwa Wabunge.

Hoja za Serikali

Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge watajadili Hotuba ya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akifungua Bunge la Kumi na Tatu ambayo ilieleza muelekeo wa Serikali yake.

Kamati ya Mipango

Vilevile Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango kujadili Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027 – 2050/2051, Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027 – 2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Uchaguzi

Katika Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa watafanya uchaguzi wa Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge pamoja na wawakilishi wa vyama mbalimbali vya Kibunge.