Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliwaongoza washiriki mbalimbali kushiriki katika Azania Benki Bunge Bonanza ambalo lilihusisha Mashabiki wa Timu za Simba na Yanga. Bonanza hilo lilianza kwa matembezi kutoka eneo la Chuo cha Mipango hadi katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlini iliyopo Jijini Dodoma ambapo mashindano ya michezo mbalimbali kati ya Mashabiki wa Simba na Yanga ilifanyika. Bonanza hilo liliofanyika tarehe 1 Februari, 2025 lilidhaminiwa na Benki ya Azania na lilihusisha mashabiki wa Timu ya Simba na Yanga kutoka Ofisi ya Bunge (Waheshimiwa Wabunge na watumishi), watumishi kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DUWASA) na Wizara ya Maji. Taasisi nyingine ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Watumishi wa Umma (PSSSF), Chuo cha Mipango Dodoma, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mashabiki wa Timu za Simba na Yanga wa Mkoa wa Dodoma na viongozi wao. Mashabiki wa Timu ya Simba (Wekundu wa Msimbazi), waliibuka mshindi wa jumla katika Bonanza hilo.