Bunge Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge la Tanzania

Habari

SPIKA ZUNGU: TANZANIA TAYARI KUCHANGIA UZOEFU HUDUMA ZA MAMA NA MTOTO


SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema Tanzania ipo tayari kuchangia uzoefu wake katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za mama na mtoto mchanga, afya ya uzazi, lishe na ustawi wa vijana.

Mheshimiwa Zungu ameeleza hayo Oktoba 8, 2026, wakati akitoa hotuba ya ufunguzi katika mdahalo kuhusu masuala ya afya ya mama na mtoto uliondaliwa na Serikali ya Tanzania kwa wajumbe wa Mkutano wa 153 Umoja wa Mabunge Duniani. Mkutano huo unaoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).

Mheshimiwa Spika amesema afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana ni msingi wa maendeleo ya Taifa na kwamba Tanzania inatarajia kuchangia uzoefu wake na kufanya kazi na washirika kugeuza dhamira ya kisiasa kuwa matokeo ya kudumu.

“Kila kifo kinachozuilika, kila hitaji la kiafya lisilotimizwa na kila kikwazo cha kupata huduma,kinahitaji umakini na hatua endelevu za kisiasa.

“Ndio maana Rais wangu Mhe. Rais Hassan ameweka kipaumbele cha kupunguza vifo vya wajawazito, kupunguza vifo vya watoto na idadi ya watoto wasiochanjwa hadi sifuri, si tu nchini Tanzania bali pia kuchochea hatua hizi kote barani Afrika kupitia wadhifa wake kama Kinara wa Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika,” amesema.

Amesema Bunge lina jukumu la kuendeleza sheria, kuhakikisha fedha za kutosha zinatengwa na kusimamia utekelezaji kuhakikisha rasilimali zinafika kwenye huduma za mstari wa mbele na kwa jamii.

“Kipaumbele chetu kiwe kwenye upatikanaji sawa wa huduma, ikiwemo huduma za mama na mtoto mchanga, afya ya uzazi, lishe, na afya na ustawi wa vijana.

“Kupitia Mtandao huu, tunaweza kujifunza kutoka kwa kila mmoja, kuimarisha uwajibikaji wa kibunge na kuendeleza hatua za vitendo katika nchi zetu.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais anayeshughulikia masuala ya afya, ustawi wa jamii, wanawake na watoto, Ummy Mwalimualiyemwakilisha Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, alisema Afrika imepiga hatua katika kupunguza vifo vya kina mama japo bado haijatosha.

Amesema vifo vya kina mama katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika vilipungua kwa asilimia 42 kati ya mwaka 2000 na 2023, lakini Afrika bado inachangia takribani asilimia 70 ya vifo vya kina mama duniani.

“Kwa kasi iliyopo sasa Afrika haitaweza kufikia lengo la Maendeleo Endelevu la kuwa na vifo vya kina mama 70 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi karibu mwaka 2050,” amesema Mwalimu.

Mwenyekiti wa Kundi la Kijiografia la Afrika la IPU, Mhe. Ali Kolotou Tchaïmi amesema Wabunge wana wajibu wa kuhakikisha ahadi za afya zinawafikia wananchi wa kawaida.

Amesema watunga sheria wana jukumu la kutunga sheria, kuidhinisha bajeti na kusimamia serikali, hususan katika kulinda makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.

Akitoa mchango wake katika mkutano huo, Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Angela Thokozile Didiza, ametoa wito wa kuimarishwa kwa uongozi wa kisiasa, akibainisha kuwa vifo vya kina mama na chanjo za watoto bado ni changamoto kubwa za afya ya umma.