Bunge Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge la Tanzania

Habari

SPIKA MHE. ZUNGU AHUTUBIA MKUTANO MKUU WA 153 WA IPU


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu amesema Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) si fursa pekee ya Wabunge kukutana kama wawakilishi wa Mabunge, bali pia ni wakati muhimu wa kutathmini jinsi mabunge yanavyoweza kukidhi matarajio ya wananchi na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika jamii.

Mheshimiwa Spika ameyasema hayo wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Mkutano huo unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), leo Oktoba 6, 2026.

Amesema wawakilishi wa wananchi wana wajibu wa kuhakikisha kuwa ahadi za kitaifa zinatafsiriwa kuwa matokeo yanayoonekana na yenye tija.

“Kupitia utungaji wa sheria, uwakilishi, na usimamizi ni lazima mabunge yaendelee kuwa na uhusiano wa karibu na uhalisia wa maisha ya kila siku ya wananchi tunaowawakilisha," amesema.

Amesema Mkutano huo unafanyika wakati ambapo dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ambazo ni pamoja na kupungua kwa imani katika taasisi za umma, ukosefu wa usawa, migogoro na ukosefu wa usalama.

“Watu duniani kote wanadai uwajibikaji zaidi, taasisi zinazojali na kuitikia mahitaji ya wananchi, fursa sawa na ushiriki wenye tija katika maamuzi yanayohusu maisha yao,” amesema.

“Mambo haya yanatukumbusha kuwa utawala bora si suala la taasisi na mifumo pekee bali ni suala linalowahusu watu,” amesisitiza.

Ameongeza kwamba changamoto zilizopo ni mtambuka kiasi kwamba hakuna Bunge, Serikali au taasisi yoyote inayoweza kuzitatua peke yake.

“Mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya kiteknolojia, ukosefu wa usawa, shinikizo la kiuchumi, migogoro na matarajio yanayobadilika ya wananchi wetu yanahitaji ushirikiano mkubwa na hatua za pamoja,” amesema.

Kufutia changamoto hizo, Spika Zungu ametoa wito kwa Mabunge Duniani kutunga sheria zinazolinda haki za watu hasa wale ambao mara nyingi sauti zao hazisikiki.

“Nikirejelea kauli zangu za jana, ili kubadilisha uhusiano kati ya nchi za Kaskazini na Kusini mwa dunia ni lazima tuvuke hatua ya matamko tu na kugeuza malengo yetu kuwa mifumo madhubuti ya utekelezaji,” amesema.

Amesema matarajio yake ni kwamba Mkutano wa 153 wa IPU utatoa matokeo ya kivitendo yanayoweza kutekelezeka na yenye mtazamo wa mbele.

“Tunaamini kujifunza kutokana na uzoefu wa mabunge mengine, kubadilishana mbinu zilizofanikiwa katika nchi zetu na kubaini masuluhisho yanayoweza kutumika katika mazingira tofauti,” amesema.

“Hivyo basi, Mkutano huu uwe jukwaa la kurejesha imani, kuimarisha uwajibikaji, kuwawezesha wananchi na kuleta fursa kwa wote,” amesisitiza.