Bunge Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bunge la Tanzania

Habari

MHE. ZUNGU:TANZANIA IMEWEKA HISTORIA KATIKA MKUTANO WA 153 WA IPU


Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu amesema Tanzania imeweka historia Kimataifa katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuendeshwa na Viongozi wawili wa Tanzania.

Mhe. Zungu ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), leo Oktoba 6, 2026.

Spika wa Bunge la Tanzania amechaguliwa kuwa Rais wa Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU wakati Rais wa Umoja huo ni Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge hili ambalo lilianzishwa mwaka 1889, linaendeshwa na Watanzania wawili; Rais wa IPU wa dunia, Dkt. Tulia, na Spika wa Bunge la Tanzania. Hii ni historia kwa Tanzania,” alisema.

Aidha, alisema historia hiyo itaendelea kuwekwa katika kumbukumbu za Tanzania, akimtaja Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa sehemu muhimu ya hatua hiyo kwa kuifikisha Tanzania katika nafasi ambayo dunia sasa inaitambua.

Akimzungumzia Spika wa Bunge la Uingereza Sir Lindsay Hoyle ambaye ndiye aliyempendekeza achaguliwe kuwa Rais wa IPU, amesema ushiriki wa Spika huyo katika Mkutano wa 153 wa IPU ni jambo la kihistoria.

“Jambo jingine kubwa la kihistoria ni ushiriki wa Spika wa Bunge la Uingereza, Westminster House of Commons katika mkutano wa 153 wa IPU unaoendelea jijini Arusha.

"Katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 , Spika wa Bunge la Uingereza, hajawahi kuhudhuria kikao kamili cha IPU. Amekuja nchini Tanzania, jambo hili ni historia kubwa na somo kwa dunia kuhusu hatua ambayo taifa letu limepiga,"amesema.

Amesema kuteuliwa na kupendekezwa kwa Tanzania kuendesha Mkutano huo na Spika wa Bunge la Uingereza, ni ishara ya diplomasia kubwa kwa Tanzania katika medani ya kimataifa.

“Kupendekezwa na Spika wa Uingereza kuwa Rais wa Mkutano huu; ni suala la diplomasia kubwa sana duniani. Hii inajenga uhusiano mkubwa kati ya Tanzania, mabunge na mataifa mbalimbali,” alisema.

Amesema fursa ya Tanzania kuandaa mkutano huo, inapaswa kutumiwa kujenga uhusiano na ushirikiano zaidi kati ya Tanzania na mabunge ya mataifa mbalimbali duniani.

Kutokana na mafanikio hayo, Spika Zungu, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa afya na nguvu alizonazo za kuendelea kuliongoza taifa, pamoja na juhudi zake katika maandalizi ya mkutano huo nchini Tanzania.

Amesema wajumbe wote waliokuja Tanzania wamepokelewa vizuri, huku Tanzania ikionesha uwezo mkubwa wa kushirikiana na mataifa na mabunge mbalimbali duniani.

“Tanzania imejenga jina kubwa sana katika dunia. Dunia yoyote sasa hivi inaitazama Tanzania kupitia mkutano huu. Tumepokea sana Mheshimiwa Rais, lakini pamoja na nchi Tanzania na viongozi wake, kwa kushirikiana na Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maandalizi ya mkutano huu,” amesema.