Parliament of Tanzania

Mhe Spika: Nitaunda Kamati ya kuchunguza uchimbaji wa Madini ya Almasi hapa nchini

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai amesema ataunda Kamati ya Bunge itakayochunguza suala la uchimbaji wa Madini ya Almasi hapa nchini.

Mhe Spika aliyasema hayo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea ripoti ya Kamati maalum ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wa Madini unaosafirishwa nje ya nchi.

Mhe Spika alisema Kamati hiyo ambayo ataiunda kabla ya Bunge hili la Bajeti kwisha itakuwa ya pili baada ya ile ya kuchunguza suala ya uchumbaji wa Madini ya Tanzanite, huko Mererani, Wilayani Simanjiro ambayo pia aliunda wakati wa Bunge hili la Bajeti.

“Lengo la luunda Kamati hizi ni ili kuhakikisha kuwa tunashirikiana bega kwa bega na Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kuwa tunafika kwa haraka kule tunakotaka kwenda katika kuona kwamba raslimali za Madini zinawanufaisha Watanzania wote,” alisisitiza Mhe Spika.

Akizungumzia ripoti ya machanga wa Madini unaosafirishwa nje ya Nchi Mhe Spika alisema “ripoti hizi zimetuuma sana Watanzania, tupo katikati ya dhiki wakati ni dhiki ambayo hatustahili”.

“Ni mambo ya ajabu sana, huwezi kuamini katika akili ya kawaida, na hiyo yote imesbabishwa na mikataba ya ovyo, amabyo kwa kweli hatuwezi kuendelea namna hii,” aliongeza Mhe Spika.

Kufuatia ripoti hizo Mhe Spika alitoa wito kwa Watanzania kumuunga Mkono Mheshimiwa Rais katika jitihada zake za kuhakikisha kuwa raslimali zilizopo nchini zinawanufaisha Watanzania.

“Wito wangu mmoja, tumuunge Mkono Mheshimiwa Rais, tumepata bahati hii tuitumie nafasi hii vizuri”, alisema Mhe Spika.

Aidha Mhe Spika alimhakikishia Mhe Rais kwamba Bunge litaifanyia kazi kwa haki na uamininifu mkubwa sheria zote zitakazopelekwa Bungeni za uchimbaji wa Gesi na Madini.

“Nikuhakikishie tu Mheshimiwa Rais kuwa Mimi na Wabunge wenzangu tukiongozwa na Kiongozi wa shughuli za serikali bungeni ambaye ni Mheshimiwa Waziri Mkuu tutazirekebisha na kuziweka sawa Sheria zote zitakazoletwa kwa haraka za madiliko ya uchimbaji Gesi na Madini kwa maslahi ya Watanzania,” alisema Mhe Spika.

Awali akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo Mheshimiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli alimtaka Waziri wa Sheria na Madini kuunda timu itakayopitia sheria zote za Madini kabla ya kuziwasilisha Bungeni kwa ajili ya kuzifanyia mabadiliko haraka kadri itakavyowezekana.

Mhe Rais aliongeza kuwa ikibidi yupo tayari kuliongezea siku Bunge hili la Bajeti linaloendelea Mjini Dodoma kwa ajili ya kuzipitia na kuzifanyia marekebisho sheria za uchimbaji Madini na Gesi.

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's