Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kenneth Ernest Nollo (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kutumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwani hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili Tukufu. Vilevile niwashukuru zaidi Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Bahi na niwashukuru wananchi wa Bahi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais inaonesha dira ya namna gani taifa letu linapotaka kwenda. Tumeshuhudia nchi yetu imefanya uwekezaji katika sekta mbalimbali. Serikali imewekeza kwenye afya, elimu na sasa inawekeza kwenye miundombinu ya reli na umeme, ni mabilioni ya shilingi yanatumika katika uwekezaji. Katika nchi yetu takribani asilimia 75 ya wananchi wetu wako kwenye kilimo, kwa maana hiyo unavyowezesha afya, elimu, ni ili uwe na productive force ambayo itaweza sasa ku-engage kwenye uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu kilimo kwa maana ya uhai wa taifa lakini kilimo tangu historia ndiyo habari ya national security. Serikali nyingi duniani zimeangushwa kwa sababu ya kulegalega na kukosa chakula. Sote tunafahamu historia ya mkate ulivyoangusha utawala pale Ufaransa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia hivi na hili nasisitiza siyo kwamba tulete wawekezaji kwenye kilimo, tunataka Serikali iwekeze kwenye kilimo. Maana yangu ni kwamba tumekuwa na Benki ya Kilimo lakini bado haijawasaidia wakulima. Mchango mwingi wa wenzangu waliopita wamechangia kwamba tunaagiza kwa kiasi kikubwa ngano, mafuta lakini hata sukari yenyewe bado hatujakaa sawasawa kuhimili utoshelevu katika taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilo moja ya korosho mkulima anaiuza kwa dola moja, lakini kilo moja hiyohiyo ikishakuwa processed inakwenda kuuzwa kwa dola 20. Ireland walianza na model inaitwa vertical forward integration kwamba mkulima wa alizeti atapeleka alizeti kwenye kiwanda cha kukamulia mafuta kwa huduma ya kukamuliwa mafuta, siyo kwenda kuuza alizeti yake. Ikishatoka pale sasa ile alizeti inakwenda katika mlolongo wa kwenda kuuzwa na hela ile mkulima ndiyo anaipata. Pamoja na hilo, kwenye kiwanda kile mkulima anapata hata mashudu. Kwa hiyo, ni vyema Serikali ikawekeza hasahasa kwenye ushirika, kwamba kama tunaitumia Benki ya Kilimo tuweze kuwa-empower watu wetu kwa kuanzisha vyama vya ushirika ambavyo vitakuwa na mashine za kufanyia processing.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, suala la ngano; tunatumia takribani shilingi milioni 300 kwa mwaka, hivyohivyo kwenye mafuta. Kwa hiyo, bado soko la ndani ni kubwa kwa hiyo ni vyema sasa Serikali iwekeze yenyewe si kuleta wawekezaji kwenye kilimo. Bado tuna nafasi ya sisi wenyewe kuwekeza kama Serikali ili tupate utoshelevu wa bidhaa hizi ambazo tunaagiza kwa kiasi kikubwa kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, total importation ya chakula katika Bara la Afrika ilikuwa ni dola bilioni na zaidi kwa mwaka kwa takwimu za mwaka 2018. Maana yake nini? Maana yake ni kwamba hata soko la Afrika bado ni kubwa kwa sisi Watanzania tukaweza ku-export. Tumeshuhudia tani na tani za mchele zinapita hapa kwenda Kongo, mchele kutoka Asia unapita kwenye nchi yetu kwenda Kongo. Kongo wame-import mchele kwa thamani ya dola milioni 65 lakini fedha hizi za Wakongoman zilitoka hapa na kwenda katika Bara la Asia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwenye export. Nchi ya Vietnam ni ndogo kwelikweli katika Bara la Asia, ni nchi ya tatu duniani lakini kwa ujumla wake ina-export mchele kuliko Bara la Afrika, yaani chukua nchi zote za Bara la Afrika, ziunganishe, hazifikii kiwango cha Vietnam inacho-export. Vietnam ina-export kiasi cha 1.4 billion dollars kwa mwaka; hizo ni takwimu za mwaka 2019 lakini kwa combination ya Afrika hawaifikii Vietnam, Vietnam ni nchi ndogo sana. Niliwahi kwenda Hanoi, ukitoka kidogo kama hapa ukienda Area C tayari kuna majeruba ya mpunga. Kwa hiyo, wenyewe mpunga is everywhere lakini kama navyosema, ni aibu kwa Bara zima la Afrika kwamba tunashindwa na nchi kama Vietnam.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kilimo cha mpunga kwenye Jimbo langu la Bahi.Bahi tuliwahi kujengewa skimu na FAO na IFAD. FAOwalitujengea skimu mwaka 1997; hakujawahi kufanyika tena ukarabati tangu kipindi hicho. IFAD walitujengea skimu mwaka 2004, mvua ya kwanza ilikuja ikavunja tuta, hakujawahi kufanyika tena repair na kilimo hakiendelei katika skimu ile ya Mtita.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu Bodi ya Mikopo. Nataka tubadilishe model ya kuwafadhili vijana wetu. Vijana wetu tukiwapa hela, hela ile hawawezi kuitunza, ndani ya wiki mbili, tatu wameshazimaliza na hela zinavyotoka wengi wanajaa mjini huku kwa ajili ya kugonga bia. Sasa kwa nini tusiwe na mfumo, kwa mfano nchi ya Japan, anakuwa na kadi ya kwenda ku-swipe kwenye chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itarahisisha ku-manage economy, hasa vijana wetu wasiweze kushinda njaa kwenye vyuo vikuu. Badala ya kuwapa hela washike sasa tufanye utaratibu wa ku-swipe katika huduma mbalimbali, iwe kwenye chakula, hostel, hii itarahisisha vijana wetu wasome, hata book allowance siku hizi kuna vitabu electronic, wataweza ku-swipe na kununua vitabu. Suala hili litatusaidia kwanza Watanzania wengi wapata mkopo lakini vilevile itasaidia zaidi vijana wetu waweze kusoma kwa uhakika.

Mheshimiwa Niabu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nafurahi kupata nafasi hii niweze kuchangia kuhusu Mpango huu uliowasilishwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu zaidi nataka nijikite kwenye suala zima la kilimo. Wachangiaji wengi wameonesha namna gani tunaweza kuendelea kwenye suala zima la kilimo. Ni dhahiri kwamba, nchi za Afrika tumekuwa tuna-export zaidi madini kwa maana ya extractive lakini tumekuwa hatufanyi vizuri katika ku-export mazao ya kilimo. Kwa hiyo, nataka nirudie na kusema kilimo tunahitaji wawekezaji lakini vilevile tunahitaji Serikali iwekeze kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nataka nijikite zaidi kwa Mkoa wa Dodoma. Mkoa wa Dodoma unachukuliwa ni mkoa ambao hauwezi kustawisha mazao na kilimo kiko chini lakini tujiulize ni kiasi gani cha maji kinachopotea katika mkoa huu. Nianzie tu karibu pale Kibaigwa, lile bonde linavyotoa maji kwenda kule. Nenda Mpwapwa ile milima na mabonde yale, nenda hadi Mto Ruaha pale, anza kushuka njoo huku Dodoma, ingia Chalinze hapa uende hadi Bahi kule na swamps zote zile, lakini maji haya miaka nenda rudi yamekuwa yanapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kwenda Egypt. Ukifika Egypt huwezi ukadhani kama uko kwenye jangwa. Egypt baadhi ya watu hawajawahi kuiona mvua maana mara nyingi inanyesha mara moja tena ni vinyunyu kwa mwaka na kama umelala huioni tena, lakini ni nchi ambayo it is very green kuanzia Cairo mpaka Alexandria, nchi yote imestawishwa kwa umwagiliaji. Naichukulia Dodoma iko sawasawa na Egypt na Israeli. Tena nazilinganisha tu basi lakini sisi hatuwezi kulinganishwa na Israel na Egypt, sisi tuko better off.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu za mwaka 2017, export value ya Egypt katika mazao ya kilimo ilikuwa ni Dola bilioni 2.2. Ukija Tanzania export ya mazao ya kilimo ilikuwa ni Dola 8,000,030 na hiyo siyo kwenye hotculture products ni mazao ya pamba, chai na kahawa. Kwa hiyo, nachotaka kusema ni kwamba tuna nafasi kubwa ya sisi kuweza kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Dodoma hapa tuna zao la zabibu lakini hatujalitendea haki. Nchi ya Israel imeweza ku-export ule mchuzi kwa thamani ya Dola milioni 240 kwa mwaka lakini zabibu ya Dodoma ndiyo zabibu ambayo unaweza kui-train izae muda wowote unavyotaka. Zabibu ya Dodoma wanasema ni nzuri katika dunia nzima kwa maana ya sukari lakini na namna ya ku-train kwamba iweze kuzaa. Unaenda hivyo hivyo Egypt, wenzetu wako mbali kwenye kuuza mchuzi wa zabibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye hoja yangu kwanini nataka kusema kwamba Serikali iwekeze kwenye kilimo. Tunahangaika kuchimba maji ya chini, tunatafuta maji underground huko kwenye miamba maji ambayo hatuyaoni ndiyo tunahangaika nayo, lakini maji yanayopita kila mwaka hapa mwaka huu yatapotea na mwakani yatapotea, hivi hatuwezi kweli tuka-tap maji haya yakutosha na tukaweza kulima kwa uhakika muda wote. Naamini kabisa Mkoa wa Dodoma huu unaweza hata ukalisha kwa kiasi kikubwa kulisha hata nchi yetu kwa maana ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ardhi nzuri, ina rutuba lakini tunaenda hadi lini kwa utaratibu huu, maji yanapotea muda wote na nataka niseme wenzetu wamejikita zaidi kwenye hotculture ambayo kwanza hutakiwi kutumia maji mengi, ni maji yanaenda kwa utaratibu,acha hii massive kama tunavyomwagilia katika mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, nataka niishauri Serikali kwamba hebu tutoke kwenye kutafuta maji chini ya ardhi, tutumie maji haya ambayo tunayo kwenye mito.Wakati tuko Egypt nilikuwa kwenye delegation, mkuu wetu wa msafara aliulizwa kwanini Tanzania mna maji lakini bado hamfanyi vizuri kwenye kilimo. Tulienda kwenye shamba la ng’ombe 35,000 jangwani Egypt, kwanza yule mwenye shamba alihojiwa akaulizwa na Waziri wetu kwamba...

MWENYEKITI: Ng’ombe 35,000?

MHE. ERNEST K. NOLLO: Ndio ng’ombe 35,000.

MWENYEKITI: Kongwa Ranch ng’ombe hawafiki 10,000, endelea tu Mheshimiwa.

MHE. ERNEST K. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo shamba lile linalima nyasi kwa umwagiliaji jangwani na sera ya Egypt ni kwamba unaweza ukapata maji kwenye Mto Nile, lakini mtu wa Egypt anasema unatakiwa uchimbe kama hujayapata hujachimba. Kwahiyo mtu wa Egypt ataenda chini miles na mile lazima ayapate maji. Hii spiritna maji tuliyonayo hata Mwenyezi Mungu nataka niseme anatushangaa na atatushangaa kweli kweli.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka miujiza gani na maji haya tuliyonayo, ile pale nimetoa mfano pale Kibaigwa, kuna kipindi utadhani ni bahari, lakini maji yale yanapotea. Njoo kwetu Bahi sasa tuna-swamp ambayo imejaa maji kwelikweli, lakini hatuwazi kulima nyasi kwa kumwagilia, tupate maziwa yakutosha muda wote, hatuwazi maji yenyewe yatutosheleze, hatuwazi maji kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tungefanya hata anasa kama Kazakhstan, walichofanyawalihamia mji mpya ule wa Almaty, wakasema sasa tutengeneze kabahari, wakatengeneza bahari, maana waliona watu wengi wakiwa wana-relaxkama ilivyo Dar es Salaam wanaona bahari, ikaja kujengwa bahari, ni matumizi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa uwekezaji kama wa umeme na reli ni gharama kubwa sana, lakini na hili nalo tulifanye, hivi kweli Serikali kwa maana tumetoa sasa ma- exavetor mwezi mzima wanachimba, hatuwezi kupata bwawa kubwa ambalo tutaweza kumwagilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo wenzangu wengi wamesema kwa habari ya mafuta,edible oil. Tumeongea sana, hivi ukatoa viwanda viwili tu pale Singida viwe vya bilioni 700, bilioni 500 tunamaliza kabisa habari ya edible oil kwenye nchi hii. Tuache habari ya kwamba tukuze michikichi baadaye tuanze kupata mafuta, lakini alizeti tukiamua miaka miwili hii tunamaliza habari yaku-import edible oil.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii,lakini kwa kweli nataka niseme Serikali jambo hili la uwekezaji kwenye kilimo tulichukulie serious, kwa maana ya kwamba hatuwezi kuwekeza kushindana kama alivyosema muwasilishaji alisema tunataka tuwe na ushindani wa kibiashara, lakini nashindana na nani katika sekta ipi? Sisi mashindano yetu yawe kwenye kilimo, tulikuwa na wenzenu akina Malaysia, akina Hongkong na akina Singapore, wale walikuwa ni wenzetu, lakini sasa wameshatoka kwenye uzalishaji wa kilimo wako kwenye teknolojia lakini sasa sisi tuko na wenzetu washindani kwenye sekta ya kilimo bado tuna lag behind, kwahiyo tunashindana vipi? Nataka niseme kwenye mambo elekezi seriouskwa maana ya kwamba sisi tuko kwenye stage ya uzalishaji kwenye teknolojia hatupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio kile ulichokuwa unasema kwamba ku-exportbrain, ile ni serviceindustryambayo sasa dunia ya wajanja na wameshafikia hapo tunawapataje akina Heron Max, tunawapataje hawa jamaa wa facebook,kile ndiyo kitu cha msingi sasa, unatengeneza kitu kidogo lakini unatoa bilions of money, sasa huko sisi hatujafika, lakini mambo mengine haya kwa mfano ya uwekezaji wa watu wetu, tunaweza tukafanya na tukaweza kupiga hatua kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. KENETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi. Nilitaka nichangie katika maeneo mawili. Kwanza nichangie kuhusu bandari yetu ya Dar es Salaam na vile vile nitachangia kuhusu suala zima la barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari yetu ya Dar es Salaam ni bandari inayohudumia nchi sita katika ukanda wetu huu, lakini bandari yetu hii imekuwa na changamoto nyingi kwa maana ya efficiency ya vitu vinavyokuja kuweza kutoka sasa kwenda kwenye nchi wanazotegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Benki ya Dunia, inasema nchi majirani wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam, kwa ujumla wanapata hasara ya dola milioni 830 collectively kutokana na; niite ni uzembe unaotoka kwenye bandari yetu, kwa maana ya kuchelewa kwa muda wa vitu kutoka na hata urasimu usio wa lazima pamoja na udokozi unaofanyika bandarini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, World Bank wanasema bandari yetu ukilinganisha na bandari washindani katika ukanda wetu, ya kwetu inaonekana iko expensive kwa vigezo vyote hivyo. Vile vile wanasema Tanzania ikiamua kusimamia bandari yake, inaweza kuondoa loss ya shilingi almost bilioni 175 ambayo ni total loss kwenye economy pamoja na loss ya revenue tunazozikosa kwenye bandari yetu. Kwa hiyo, ninachotaka kusema kwa wenzetu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, ipo haja kubwa sana ya kusimamia bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia, sijui kuna kigugumizi cha nini? Tumeona nchi kama Singapore wanatumia bandari na viwanja vya ndege, wameendelea, sisi tunataka tupate miujiza ya aina gani? Pamekuwa na mizengwe mikubwa sana kwenye bandari yetu. Kwa hiyo, nataka Wizara hii na Mheshimiwa Waziri anasikiam hebu wakijite kwa ajili ya kuiboresha bandari yetu kwa kuondoa tu urasimu ambavyo ni vitu vya kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la barabara, Wizara hii imeonekana kufanya kazi nzuri kwa kutumia agency ya TANROADS, lakini hawapati fedha ya kutosha. Kwa miaka mitano mfululizo, bajeti hii haijaongezeka, lakini kazi walioifanya ni kubwa. Sasa tunategemea miujiza gani kama chombo hiki kinachotusaidia kwa kuunganisha nchi yetu katika barabara, lakini bado wanapata fedha kidogo? Kwa hiyo, hili tuliangalie, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iongezewe fedha za kutosha na hata bajeti yenyewe basi iweze kutekelezwa kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, alipokuwa kwenye kampeni pale Manyoni, aliahidi kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami kutoka Manyoni kuja Itigi - Heka - Sanza - Chali kwenye Jimbo langu la Bahi Kijiji cha Chali; na barabara hii ni muhimu sana, maana yake ukija Halmashauri ya Manyoni na Bahi, tunaitegemea sana kwa maana ya shughuli za kiuchumi katika Mji huu wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, barabara hii ikitengenezwa kwa kiwango cha lami kama nilivyotaja, kuanzia Manyoni - Itigi - Heka kuja - Chali Igongo - Chali Makulu - Chali Isanga, unakuja unatokezea Chipanga unakuja Mpalanga – Bihawana, utakuwa umetengeneza link kubwa sana ambayo itachochea uchumi katika Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi barabara zimeonyeshwa, lakini kuna vitu vingine ambavyo ukiangalia huwezi ukaelewa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)


MHE. KENETH E. NOLLO: Naunga Mkono hoja Ahsante sana.


Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara hii ya Kilimo ambayo ndiyo Wizara mama na ni tegemeo katika uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza mimi niseme kwa masikitiko makubwa matarajio niliyokuwa natarajia bajeti hii kutoka kwa Profesa Mkenda si kwa kiwango hiki ilivyokuja.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na matarajio makubwa sana, nilijua Wizara hii bajeti yake itakuwa na transformation lakini ukiiangalia na bajeti zilizopita it is all most the same. Sioni picha kubwa ambayo nilikuwa nayo ya Profesa Mkenda. Kwa kweli bajeti hii binafsi sijaridhika kutokana na nilivyokuwa na matarajio makubwa kutoka Profesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bajeti hii kwenye miradi ya maendeleo imetengwa shilingi bilioni 150 ukiacha matumizi mengine. Hivi kweli kilimo cha nchi hii unakipangia bilioni 150 Tanzanian shillings, kwa kweli hatuendi mbele.

Mheshimiwa Spika, nikija Kanda ya Kati kupitia kwenye bajeti huoni strategic vision kwamba hapa Kanda ya Kati kilimo kinakuja kuwekwa sawasawa, huoni programme, huoni chochote. Ukiisoma bajeti imegusagusa tu kwa kudonyoadonyoa na ni story kwamba hapa tulifanya hivi na pale tulifanya vile, lakini picha hasa kubwa ya Wizara ya Kilimo tunaelekea wapi huioni kwenye bajeti.

Mheshimiwa Spika, mimi nataka niseme na nashauri Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri tukimaliza bajeti hii hebu waende nje; Waziri aende Egypt lakini Naibu Waziri aende Zimbabwe. Zimbabwe wamenyang’anya mashamba kutoka kwa Wazungu na dunia nzima ikajua sasa Zimbabwe inaenda kufeli lakini wamefanya mapinduzi makubwa sasa kwenye kilimo, kwetu hapa hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu hailimi, tuko strategically positioned kwa ajili ya kuilisha Middle East na Uarabuni…

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Maji unakatiza kati ya mzungumzaji na Kiti lakini pia nilishazuia watu kumfuata Waziri Mkuu, ulikuwa haupo ndiyo maana, endelea Mheshimiwa.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, sisi tumekaa katika position nzuri ya kuilisha Middle East na nchi za Kiarabu ambazo wenzetu kule ni jangwani, lakini ukienda kwenye masoko ya Doha na Abu Dhabi vitu vyote vinatoka South America hadi ndizi na mchicha sasa hii nchi tunaenda huko lini? Ukiwa kwenye ndege unatua hata tu barabarani unakwenda Arusha unakwenda wapi hakuna plantation zozote katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, matreka yanayoingia hapa huwezi kulinganisha na Zimbabwe ambao Waafrika wenzetu wameingiza. Kwa hiyo, mimi nachoona bado tunapiga mark time, ASDP I&II zilifadhiliwa sana na donner partners walivyojitoa kwenye basket fund ile ya kusaidia kilimo sasa hivi hakuna ni story tu, ASDP II haina kitu.

Mheshimiwa Spika, nadhani kwenye kilimo tuwe serious, aligusia Mheshimiwa Kandege hapa hakuna kitu ndugu zangu tuseme ukweli kama tunataka kweli twende kwenye kilimo hatujaamua ndugu zangu. Wenzangu wameongelea Minjingu na maeneo mengi hatufanyi vizuri. Sasa nchi hii tunataka kuendelea, lakini tunaendeleaje kilimo tunakipuuzia? Kwa kweli nataka niseme bajeti hii imekuja chini ya kiwango hai-reflect hasa tunataka twende wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu kama nilivyosema tumejaaliwa tunalima sana mahindi na nchi zinazotuzunguka wanatutegemea sisi lakini bado hatujakaa sawasawa. Hatuwezi kulisha South Sudan, kuna watu tu wametu-block hapo karibu basi hatuwezi kwenda South Sudan. Congo walikuja wanataka…

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa.

SPIKA: Ndiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri tafadhali.

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji rafiki yangu Nollo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema sana ya maelezo yake juu ya mchango wa sekta ya kilimo, naomba nimpe comfort kidogo, najua baadaye Mheshimiwa Waziri ataeleza, lakini katika bajeti hii ya mwaka 2021/2022 ASDP II kupitia mradi utakaofadhiliwa na IFAD, Wizara ya Kilimo (mazao na mifugo na uvuvi) tutapata zaidi ya shilingi bilioni 150. Pesa hizi zitakwenda moja kwa moja katika vikundi kusaidia mambo ya mbegu na mengineyo. Kwa upande wa mifugo huko tutakapofika katika Wizara yangu pia vilevile itaonekana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimpe comfort na ikimpendeza baadaye nafikiri kupitia Mheshimiwa Waziri atamuonyesha kwa undani zaidi.

SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Nolla unapokea taarifa hiyo?

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa hiyo kwa sababu hatujapata hizo fedha kutoka IFAD, tunaanza kujadili kwamba tukiokota fedha tugawane, sasa ni story hiyo.

MBUNGE FULANI: Maoteo.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Hatuwezi kujadiliana maoteo. Mheshimiwa Spika, kwa kweli nachotaka kusema Serikali iwe serious kwenye kilimo kwani bado hatujawa serious. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye Jimbo langu la Bahi tuna skimu za mpunga za umwagiliaji, hazijafanyiwa ukarabati muda mrefu. Mara ya mwisho zimefanyiwa ukarabati mwaka 1998. Skimu ya Ntitaa mwaka 2004 IFAD walitujengea ilifanya kazi mwaka mmoja lile tuta likavunjwa mabilioni ya shilingi hatujawahi tena kuendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nachotaka kusema hebu tuichukulie Wizara hii kama MSD inavyofanya kazi. Kilimo kikianza kufanya kazi kama MSD tutaendelea. Tuchukulie kwamba huu ni uhai wa nchi. MSD inaleta dawa na ndiyo maana tunaendelea kuwa na afya, lakini kwenye kilimo bado tunacheza.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Mambo ya Nje. Nchi yetu imekuwa inaheshimika katika sura ya kimataifa kwa muda mrefu sana. Lakini heshima ambayo tumekuwa nayo tangu enzi ya awamu ya kwanza ni kutokana na nchi yetu kuwa na misimamo thabiti katika kutetea haki na unyanyasaji wa aina yoyote katika nchi mbalimbali hapa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatukujipambanua tu kwa kutetea haki kwa kutetea waafrika wenzetu wanavyosanyanyaswa au kuonewa lakini tumeenda nje kabisa ya Afrika na kutetea kokote duniani ambako tunaona haki inabinywa. Nataka niseme hili kwa kuangalia kwamba nchi yetu sawa inaingia kwenye uchumi wa dipomasia, lakini tunafika mahali sasa tunaanza kwenda kama watu wanaotaka kujiuza, tunapoteza heshima yetu, tunapoteza sisi tusema maskini ambaye sasa hana aibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana sasa unaweza ukawa maskini, lakini aibu unayo, una heshima yako unalinda heshima yako. Nalisema hili kwa sababu moja, wiki mbili zilizopita dunia nzima imeona namna Palestina ilivyoshambuliwa kwa kiasi kikubwa ambacho binadamu yeyote hawezi akasema hiki ni kitu gani kinatokea. Nchi yetu hatujatoa hata tamko la kulaani, hata kusikitika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mwingine anaweza aka-justify akasema mbona nao Hamas walikuwa wanarusharusha mawe upande ule, lakini ukiangalia kulichofanyika pale nchi yetu tulitakiwa tuweze kufanya condemnation kwa namna gani Palestina walivyofanyiwa. Hata Mwalimu alikuwa na msimamo thabiti kuhusu Palestina na msimamo wa nchi yetu ilikuwa ni kwamba pale inatakiwa mataifa mawili na juzi Rais wa Amerika huyu mpya amesema pale panatakiwa mataifa mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nisema ni kwa nini tunaanza kupoteana, Waziri atuambie msimamo wetu kuhusu Palestina ni nini? Anachofanyiwa Palestina sisi msimamo wetu Tanzania ni nini? Hili Waziri atuambie na ikiwezekana basi leo alaumu kilichotokea juzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na msimamo mkali kuhusu Morocco, alijitangazia kwa west sahara anaitawala na sisi Tanzania tukawa wakali hata tukatoa influence yetu kwenye Umoja wa Afrika na Morocco akajaribu kuingia pale akazuiwa, lakini hili nalo tumepoteana kwanza tumefungua ubalozi wetu Algeria ambao ulikuwepo, lakini tume-extend na Morocco sasa tuna ubalozi ambao tunautumia ule wa Algeria. Lakini na hili nalo Waziri atuambie msimamo wetu kuhusu West Sahara ni nini? Tumekubali kwamba tunakuja kujengewa kiwanja basi imekuwa give and take tunawaacha West Sahara ambako ulikuwa msimamo wetu tangu awali. Hili nalo Mheshimiwa Waziri atuambie msimamo wetu kuhusu West Sahara ni nini sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kuhusu economic diplomacy ambayo wengi wameisema kwamba sisi tuangalie nchi yetu tunapata nini, ndio maana nikasema sasa ile ni maskini anayejirahisisha na nchi yetu imekuwa na heshima kubwa na watangulizi wetu walitumia damu na nguvu zote kutetea hili, lakini hatuwezi tukatumia kitendo cha uchumi wa diplomasia tuweze sasa kusema hili sisi walau kwa vile tunapata pesa basi hili tuliruhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, balozi zetu tunazifungua, lakini ni lazima tuangalie kwamba tunapata nini pale. Economic diplomacy isichukuliwe kwamba sasa tumekubali ubeberu ututawale tunavyotaka na vyovyote itakavyoenda lakini lazima tuseme hapana kwa imperialism, ni nchi yetu lazima iseme bado kuna shida ya ubeberu na ubeberu wa namna yoyote ile nchi yetu lazima isema hapana, tusipoangalia tutakuwa ma-purpet wa mabeberu na tutasema kila kitu tutakabiliana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme hili kwa sababu moja wakati corona inaingia nchi yetu watu waliishangaa na tulionekana hatufai kwa nini atufungii watu wetu ndani, na hili tulisimama kidete, lakini majirani zetu na Afrika wakaanza kuwaambia sasa chukueni package ya kujinusuru na ya kunusuru uchumi wenu na majirani zetu wamekopa IFM, World Bank, nani hela nyingi sana, lakini sisi msimamo wetu tulisema kwamba kwenye hili hapana kama wanataka kutusaidia basi watupunguzie riba ya madeni haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninataka niseme na wizara waelewe tunakoelekea tunajipeleka kwenye chanjo, sawa, lakini kwenye jambo hili tuangalie tuwe na msimamo thabiti kwamba chanjo ile bado inazungumzwa kwa tofauti. Mheshimiwa Rais ameunda Kamati na imeshauri lakini ni lazima ndugu zangu wa Tanzania tuendelee kuliangalia hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado twendeni kwa kushtukastuka, tusiingize miguu yote, kama tulivyostuka hatua za awali za kufungia watu wetu bado na hili lazima twende kwa kustukastuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu balozi zetu kama nilivyogusia tusipekele tu watu ambao wamesoma international relations, tupeleke watu mbalimbali wenye ujuzi, wataalam wa masoko, biashara, wa uwekezaji, lakini kwamba balozi anakuwa na afisa mmoja tu pale halafu mnategemea mpate chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unateuwa balozi kwenda Lubumbashi unamchukulia kwa minajili kwenda kusuluhisha tu migogoro, lakini bado tunanaangalia kwamba balozi wetu huyu atuletee nini Tanzania. Kinachotushinda ni kwamba tunashindwa sasa kuangalia potential zilizopo za kibiashara tuweze kuzileta hapa kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilitaka nishauri, nchi yetu inavutia wawekezaji lakini tutaweza kupata wawekezaji wengi, lakini baadae tunaweza tukasema hawa watu wamekuja kutuibia kwa sababu moja tu, ukienda Malaysia kwamba mwekezaji lazima awe na mzawa, hapa kwetu tunasema lakini hatulifanyi, hata mzawa akiwepo anakuwa na ka-minor share na anakuwa diluted. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili tuliwekee mkazo kwamba ni lazima Mtanzania awepo kwenye kampuni ile na ashiriki kikamilifu, lakini kingine tuzalishe na sisi matajiri wa kwenda kuwekeza nje, Dangote yupo kwetu hapa ametengenezwa, lakini mkakati wa kumpeleka Bakhresa nje upo wapi, matajiri wetu mkakati wao huko wapi? Nataka nishauri kwamba Wizara ya Fedha na ninachukulia mfano wa nchi ya Ufaransa ina department ya Private Sector for Overseas Investiment na sisi tuwe na hicho na kitengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zetu wa China wakija hapa wawekezaji wao wanakopa hela kwenye Exim Bank ya China ndio maana inakuwa rahisi kuwekeza hapa kwetu. Sasa na sisi ni lazima tuwe na Overseas Department kwa ajili ya private sector ambayo itaweza kuwatafutia masoko, oppotunities na hata kuangalia namna gani Serikali iweze kufanya business negotiations badala kuwaacha waende namna hiyo walivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivi tutasaidia nchi yet una kwa maana hiyo tutakuwa washindani katika biashara, katika shughuli za uwekezaji zinazofanyika na namna hiyo tutaweza kweli kusema tunatekeleza economic diplomacy.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa utaratibu iliyochukua wa kutoa fedha shilingi 500,000,000 kwa kila jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu nauona una tija zaidi tofauti na ilivyozoeleka. Kwa upande wa Jimbo langu la Bahi, shilingi 500,000,000 hizi zimenisaidia kutatua changamoto kubwa ya barabara inayotoka kwenye Kata ya Chifutuka ambayo iko kilometa 90 kutoka kwenye Makao Makuu ya Wilaya na wakati mwingine imekuwa inajifunga haipiti. Lakini kwa 500,000,000 hizi tulizozipata tunaenda kutatua kwa kiasi kikubwa tatizo hili la barabara na hatimaye kuweza kuleta maendeleo ya wananchi kupitia kata ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka niipongeze sana Serikali. Bajeti hii ina ahueni kubwa katika kuleta maendeleo lakini pamoja na hilo, tunakuja kwenye matumizi ya bajeti. Bajeti yetu imekuwa mara nyingi haifiki asilimia 70 katika matumizi hususan katika miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hasa Wizara wa Fedha aelewe na atambue hili kwamba bajeti yetu iwe ni rural centered development. Iangalie zaidi katika kutatua shida zaidi za wananchi waliopo vijijini na kwa kweli tuna shida kubwa sana vijijini. Tuna shida ya zahanati, kwa mfano Jimbo langu la Bahi sina zahanati 16, sina ambulance, hata ambulance zinazokuja ugawaji wake bado haueleweki. Ukigawanywa kama hivi tulivyopewa 500, 500 italeta ahueni. Kwa hiyo, nadhani hii model iliyotumika ya 500,000,000 tuiangalie katika bajeti iweze kutumika katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya bajeti kupitishwa imekuwa tunasubiria kudra za Hazina ndiyo ziweze kutupatia katika maeneo yetu. Wakati mwingine unasikia upande fulani wamepewa, huku kwako hujapewa, kigezo hakieleweki. Ili twende sawa sawa, kuwe na equal distribution, ni lazima tuone namna gani. Kama tunaamua kutoa milioni 600 kwa ajili ya kumalizia maboma kwenye majimbo yote, ziende kote. Namna hii tunaweza tukaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishie pale kwenye conclusion ya Waziri wa fedha kuhusu kadi ya njano na kadi nyekundu. Maneno yale yana busara kubwa ya kuonesha namna gani kiongozi wetu wa Taifa hili alivyosheheni uzoefu wa kuweza kuliongoza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hivyo tu ni kwamba Mheshimiwa Samia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Chama hiki kina utajiri wa rejea katika uongozi. Ni chama ambacho kimepita katika vipindi vingi tangu kuanza mapambano ya uhuru lakini baada ya nchi yetu kupata uhuru. Lakini, hata hivyo vile vile kupambana na mifumo mbalimbali ili kujiletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama chetu cha Mapinduzi kimekuwa kinafanya reform kila wakati. Iwe katika kipindi kile sasa tunaanza kuimarisha viwanda Watanzania tuweze kujitegemea. Lakini hata hivyo, tuwe tumekuwa tunaangalia tunaenda na sera gani, tunajibadilisha kila mara kutokana na matakwa ya jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwahi kutoa Sera za CCM katika miaka ya 90. Lengo letu lilikuwa ni namna gani sasa tunaanza kwenda katika mageuzi ambayo yanatokea katika Dunia na sisi tuweze kuendana na namna Dunia inavyoenda. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Watanzania, Mheshimiwa Samia anarejea kubwa ya uongozi na ninataka niwaambie hakuna shaka ya kuwa na wasiwasi kwamba Mheshimiwa Samia hatalivusha Taifa hili. Atafanya vizuri zaidi kwa sababu ana msingi mkubwa ambao msingi umetengenezwa na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imetokea kasumba ya baadhi ya Mwenyekiti wa chama kimoja kuonesha kwamba kama ana kauli ya kuweza kulazimisha kila anachotaka yeye. Nataka tu niseme kama nilivyosema Samia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Mwenyekiti huyu ambaye kidogo anataka kujipa ahueni kwamba eti anataka kuja 25 ashike dola alianza tangu enzi za Mzee Mkapa, Mzee Mkapa akaondoka yeye bado ni Mwenyekiti, akaja Mzee Kikwete yeye bado Mwenyekiti, amekuja Hayati Magufuli yeye bado Mwenyekiti. Sasa mtu ambaye amekosa pumzi kabisa amechoka hoi bina taaban anataka kuja kupambana na Mwenyekiti ambaye ni mpya kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia Mwenyekiti wetu ni Mwenyekiti ambaye ameonesha, Rais wetu ameonesha ni mtu anayejua hata Dunia inavyoenda. Ninyi mmeshuhudia hata mitazamo yake, juzi amesema kwamba sasa Taifa letu liangalie kuna mageuzi makubwa sana ya kidijitali yanatokea. Sasa hatuwezi kubabaishwa na Mwenyekiti huyu ambaye ni Mwenyekiti wa enzi na enzi, amekosa mvuto, amepauka na anajinasibu anasema wao ni makamanda. Kwanza nataka niwaambie, sisi tulikomboa nchi nyingi za Afrika katika kupigania uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameanza kuvaa makombati hayo wanayoyavaa sisi tunawaona. Sisi tulishapigania uhuru na chama chetu kina heshima kubwa katika Bara la Afrika na ninataka niseme Mheshimiwa Samia sio wa kufanyiwa mashinikizo, yuko kwenye chama imara, anajiamini na nataka niseme tunaendelea kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi hii kwa dhati niipongeze Serikali kwa kuja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Kupambana na Ugaidi. Zaidi jambo hili linatoka kwa pendekezo na muktadha kutoka Umoja wa Mataifa kwamba nchi katika Kanda mbalimbali na dunia kwa pamoja tuweze kushirikiana kupambana na ugaidi. Bahati mbaya, dhima na dhana hasa ya ugaidi bado inatofautiana kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. Vilevile bado kuna ulegevu mkubwa wa Umoja wa Mataifa wenyewe kutoa definition kamili ya nini maana ya ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugaidi umekuwa unafadhiliwa na baadhi ya mataifa makubwa waziwazi na UN ipo. Ugaidi umekuwa kama unataka kuua mbwa mpe jina baya, baadhi ya nchi zimejaribu kutengeneza ugaidi kwenda kudhuru nchi zingine. Siwezi kuzitaja nchi hizo lakini ipo sponsored terror groups na jambo hili linatokana na mtofautiano wa kiitikadi kwamba huyu ni gaidi, kwa hiyo anaweza kuwa gaidi kwa mtizamo wa mwenzangu lakini kwangu vilevile asiwe gaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika historia wakati wa mapambano ya Kusini mwa Afrika, kikundi cha Nelson Mandela na Wapigania Uhuru wote wa South Africa waliitwa magaidi. Jambo hili bado linaendelea hata duniani, Mwalimu Nyerere alikwenda ziara Iraq mwaka 1979, wakati wanatoa ile inaitwa International Communiqué sasa maazimio ya pamoja na Iraq; Rais Sadam Hussein akataka waweke na kipengele kwamba kwa pamoja wamekubaliana kupinga uonevu unaofanyika kwa Wamarekani Weusi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alikataa akasema we don’t subscribe to that conflict; japo kuwa sisi ni PAN Africanism. Kwa hiyo na sisi tunapoingia katika muktadha huu wa kupambana na ugaidi lazima kuwa na maeneo tusi-subscribe; lazima tuseme sawa lakini hili bado haturidhii kama ule ni ugaidi. Tukienda hivyo, tutaondoa ile dhana ya sisi kutumiwa, kwa maana ya kwamba mataifa makubwa na mengine yanayotufadhili katika mambo mbalimbali yanaweza yakatumia mwanya huu sisi kuingizwa kwenye migogoro ambayo haituhusu na kwa sababu tumeingia katika Itifaki hii, basi tutaonekana kwamba na sisi tuweze kuwa pamoja katika migogoro ambayo wanayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesema kwa maana ya kanzidata ambayo ipo Algeria kwenye security na kwa maana ya ku-share information ni jambo la msingi; lakini siyo kila information utataka uitumie. Kwa hiyo, naiomba Serikali katika jambo hilo kwamba ni lazima tuseme kuna maeneo tunakubaliana kwamba huu ni ugaidi na kuna maeneo mengine lazima tukatae tuseme huu siyo ugaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kutaja baadhi ya nchi na baadhi ya vikundi, lakini jambo hili linaendelea. Ukienda nchi kama Qatar kuna vikundi vipo pale lakini nchi zingine wanasema wale ni magaidi; lakini wamewa-host wanakaa pale. Ukienda Palestine inachukuliwa ni magaidi, lakini kuna nchi hata sisi wenyewe tunasema Wapalestine siyo magaidi. Kwa hiyo, muktadha huu usitupeleke moja kwa moja katika Azimio hili, sasa katika context ya Afrika na sisi hata Kikanda bado kuna maeneo tunakubaliana hatukubaliani. Serikali zetu lazima tuchukue wajibu kwamba tusitumie mabavu ya Serikali kunyanyasa vikundi vingine na tukavipa nembo ya ugaidi. Jambo hili katika SADC na Afrika kwa ujumla ni lazima tuliangalie, kupitia hili Azimio tuwe na model nzuri ya kusema ugaidi ni nini na namna gani tuna-combat nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu hapa yalitokea pale Rufiji ilikuwa ni ugaidi, lakini tumeona Msumbiji imekuwa ni ugaidi, wenzetu wa West Africa wanasumbuliwa sasa na ugaidi nchi karibu tatu zote zile. Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba lengo letu tuwe katika nyanja zaidi ya kiusalama badala ya kushabikia ugaidi hasa kwa maana ya context ya dunia ambapo bado hatujakubaliana gaidi ni nani katika mtazamo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nchi zetu na Serikali zetu ni lazima ziangalie mipasuko katika jamii kwa kuwapelekea rasilimali, mgawanyo wa rasilimali uwe unakwenda sawasawa; moja ya maeneo yanayozalisha ugaidi ni baadhi ya jamii kutengwa, ni baadhi ya jamii kuona sasa hawafaidiki. Vilevile nchi zetu zina utajiri wa madini, baadhi ya maeneo ugawaji wa rasilimali haujakaa sawasawa; kwa hiyo, Tanzania kama kioo na kama kiranja wa ugawaji sawa wa rasilimali, ni lazima tuzikumbushe nchi zingine za Afrika ambazo tunaingia nazo katika Itifaki hii kwamba, lazima kuwe na usawa wa kugawanya rasilimali ili kuondoa minong’ono katika vikundi vingine katika jamii na hasa kuzalisha ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ni lazima sote tukubaliane kwamba mitazamo ya kidini imetumika katika ugaidi na kwa bahati mbaya yapo maeneo ambayo wamepata indoctrination hasa katika watoto wadogo na baadaye kuingia katika stage kubwa ya ugaidi. Pamoja na hilo lazima na Tanzania iendelee kuwa mfano katika hizi nchi nyingine za Afrika kwamba sisi tumewezaje kukaa na dini mbalimbali, tumewezaje kuishi pamoja na tumewezaje kuvumiliana katika kuwa makabila zaidi ya 127. Kwa hiyo, tunavyoingia kwenye Itifaki hii tuna kazi ya kuwaonesha wenzetu, tuna kazi vilevile ya kutoa somo kwamba ni namna gani katika jamii nyingi kwa ujumla na namna gani una in grace zile differences ili uweze kuwa na jamii ambayo haina mikwaruzano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo kama nilivyosema pamoja na kuingia katika itifaki hii sisi tuwe kiranja katika kuonesha wenzetu ni namna gani wanaweza wakakumbatia zile tofauti zilizopo, tumefanya hivyo katika miaka mingi, tumekuwa wasuluhishi migogoro ya Maziwa Makuu. Kwa hiyo, kama nilivyosema tuna jukumu kubwa lakini kikubwa zaidi tusitumie ugaidi katika context ambayo baadhi wanazo tofauti zao za kisiasa na baadhi ya vikundi vinafadhiliwa na Serikali za nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana. (Makofi)