Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Boniphace Mwita Getere (67 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza shukrani zangu za awali kwa wote walioandaa hotuba hii ya Wizara ya Elimu na hasa Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Naibu Waziri.
Matatizo ya Jimbo langu la Bunda Vijijini; moja ni kutoa kibali cha ufunguzi wa sekondari ya (High School) ya Makongoro (Makongoro High School). Tunahitaji msaada wa Wizara, wananchi wamejenga vyumba vya madarasa, mabweni na jengo la utawala, tunahitaji shilingi 72,000,000 ili kumaliza ujenzi wa high school hii. Tunaomba msaada ili kupunguza makali ya michango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili ni upungufu wa walimu wa sayansi, (kemia, fizikia, biolojia na hesabu). Zaidi ya sekondari 30 wanahitajika walimu 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni matatizo ya mazingira ya vyoo. Zaidi ya shule za msingi 40, zina matatizo ya vyoo vibovu vya shule na tatizo la maji shuleni, hivyo naomba Wizara ya Elimu kupitia mashirika yake ya kutoa huduma za msingi na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tatizo la vyoo magonjwa ya watoto shuleni yameongezeka sana, (typhoid, kuhara, U.T.I). Naomba msaada wa suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba nne, matatizo ya maabara, madarasa na nyumba za walimu. Wizara iangalie namna ya kusaidia Jimbo hili jipya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia Wizara hii kwa maeneo yanayohusu Jimbo langu la Bunda Vijijini. Jimbo la Bunda lina Vijiji 39. Matatizo ya umeme ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, REA I vijiji vilivyopata umeme ni Kyandege, Migeta, Mariwanda, Salama „A‟ na Hunyuri Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo umeme wa REA Phase I uliwekwa katika maeneo ya center (Barabara kuu). Aidha, maeneo yote ya Taasisi; Mashuleni, Hospitali, Ofisi) hakuna umeme. Aidha, katika Vijiji vya Mariwanda, Hunyari, umeme uliwekwa katika volt ndogo (muhimu). TANESCO Bunda wanajua.
REA II: Vijiji vilivyopata umeme ni Kiloreli, Kambubu, Nyamuswa, Marambeka, Salama Kati, Kurusanga, Mikomariro na Mibingo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo vijiji vya REA II nilivyovitaja kuanzia cha 1 – 6 umeme umewaka katika maeneo ya center tu. Taasisi zote za Umma hakuna umeme. Wizara imetoa agizo kupitia Mheshimiwa Muhongo (Waziri) kuwa Taasisi zote za Umma zipate umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, REA III; vijiji ambavyo vinahitaji umeme ni Manchimaro, Tingirima, Nyangiranga, Rakana, Tiringati, Bigegu, Nyaburundu, Mahanga, Mmagunga, Nyariswori, Sarakwa, Majengo, Nyangere, Nyabuzame, Mmuruwaro, Nyang‟ombe, Nyanungu, Rubimaha na Bukoba,
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kuwa maeneo yote hayo yatapewa umeme wa REA Phase III kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni.
N.B. Vijiji vya Bukoba na Samata vimewekewa transformer, tunahitaji umeme uwake. Mungu ibariki Wizara, Mungu ibariki Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nitangulize shukrani zangu za dhati kwa Serikali yangu ya CCM. Nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Fedha na Sekretarieti yake kwa kuthubutu kutoa mapendekezo yao kwa Mpango huu wa Maendeleo wa Mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo haya ni mazuri kwa sehemu kubwa. Mchango wangu katika mapendekezo yangu upo katika sehemu tatu:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni Elimu ya Bure Shule za Msingi na Sekondari. Kwa maoni yangu, fedha hizi zinazotolewa mashuleni na hasa shule za msingi, hazifanyi kazi iliyokusudiwa. Mfano, Shule ya Msingi „A‟ kwa mwezi itapata shilingi 230,000/=. Fedha hizi hugawanywa kwa asilimia ishirini ishirini. Kwa maoni yangu, fedha hizi hazitoshi hata kununua mpira.
Kwa mahitaji makubwa ya shule ni chaki, mitihani na utawala. Kwa nini Serikali isifungue akaunti maalum kila Halmashauri na fedha hizi zikawa katika akaunti hii na kila shule ikapewa mahitaji muhimu ya wanafunzi na utawala. Napendekeza style iliyokuwa inatumika enzi za Mwalimu, kila mwanafunzi alikuwa anapewa vitabu, madaftari, chaki na vitu vingine muhimu kuliko fungu la fedha hizi ambazo sehemu kubwa hazifanyi kazi. Fanyeni utafiti.
(b) Nashauri Serikali itenge fidia ya wakulima kwa mazao yaliyoharibiwa na wanyama waharibifu (ndovu) Jimboni kwangu. Wakulima wanadai zaidi ya shilingi milioni 400. Serikali ihakikishe fidia kwa wakulima, inalipwa.
(c) Malambo kwa wafugaji. Maeneo mengi ya hifadhi ya Taifa hayana maji kwa mifugo. Serikali iwe na mpango maalum wa kuchimba malambo Jimbo la Bunda.
(d) Vile vile Serikali iwe na mpango maalum wa kujenga vyumba vya madarasa, vyoo na nyumba za Walimu kwa shule za msingi na sekondari. Mfano, Jimbo langu la Bunda lina upungufu wa vyumba vya madarasa 586 vyenye thamani ya shilingi milioni 687. Serikali iwe na mkakati maalum wa kujenga/kutatua kero hii.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni ya leo.

Nachukua nafasi hii kuwashukuru Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na wafanyakazi wote wa Wizara hii wakiongozwa na Katibu Mkuu wao. Nachukua nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa nguvu na juhudi kubwa anazozifanya katika kuokoa mali ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili iko dhana inajengwa hapa kwamba Rais Magufuli anafanya kazi yake bila kuhusisha Chama cha Mapinduzi. Sasa leo nimekuja hapa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuonesha wenzetu kwamba Rais hafanyi mambo yake, anafanya ya Chama cha Mapinduzi. Baadaye kama kuna mtu anahitaji Ilani hii tutampa aisome.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kunukuu maandishi ya Chama cha Mapinduzi kwa ujumla wake. Na. 4 inasema:-

“Katika miaka mitano ijayo 2015 - 2020, CCM ikiwa madarakani itaelekeza Serikali zake kutumia nguvu zake zote kuendeleza na kupambana na changamoto kubwa nne.

(i) kuondoa umaskini; kupambana na makinikia, kuzia wizi ni kupambana na umaskini;

(ii) Kupunguza tatizo la kukosefu wa ajira hasa kwa vijana wetu. Kutafuta fedha zinazoibiwa ni kuleta ajira ambayo tutaitumia baadaye kwenye viwanda; na

(iii) Kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hii ni ilani inayozungumza mambo hayo, maana yake CCM tunaelekeza kwamba Rais wa kwetu atakayepatikana atatekeleza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikutosha tukasema, sambamba na kupambana na tatizo la rushwa, Serikali pia zinaelekezwa na CCM, zinatakiwa kushughulikia kwa ukali zaidi tatizo la ubadhirifu na wizi wa mali ya umma. Kwa hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John PombeMagufuli anatekeleza yale tuliyomwelekeza Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ile dhana inayojengwa kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli anafanya yake, siyo kweli na yako mengi humu ndani. Mkitaka tutawapa mwendelee kusoma hayo mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo nayashangaa humu ndani, nayashangaa sana. Leo duniani kote, Korea Kusini pamoja na vita waliyonayo na Korea Kaskazini wamemfukuza Rais wao kwa sababu ya ubadhirifu; leo Brazil pamoja na umaskini ambao umekithiri, wamemfukuza Rais wao. Leo Urusi pamoja na juhudi kubwa za Putin lakini leo wanaandamana kwamba anakula rushwa. Sasa leo Rais wetu anapopambana kutoa rushwa na ubadhirifu, Venezuela nao wamemtoa Rais, naambiwa hapa. Rais wetu anapopambana kwenye mambo ya ubadhirifu, tunashindwa kumshangilia na kumpa na pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba siyo jambo jema, ni vizuri Waheshimiwa Wabunge wote tukaungana pamoja, tukashughulikia ubadhirifu huu na bahati nzuri sasa taarifa zilikuwa hewani kwamba wale watu ambao mlikuwa mnasema watatupeleka Mahakamani, wameshakubali kulipa. Sasa shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelekezo haya sasa, niende kuchangia, nijielekeze kwenye mambo ya viwanda na kilimo. Tunapozungumza viwanda maana yake tunazungumza kilimo; tukiendeleza kilimo chetu, ni lazima tubadili kilimo chetu cha mazao mbalimbali ili kupata nakisi ambayo itasaidia kwenda kuendeleza viwanda. Ni lazima ufugaji wetu tuubadili ili tuweze kupata mazao bora kwa ajili ya kupata viwanda. Malighafi itakayopatikana katika kilimo na katika mifugo isaidie kwenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji kwenye Jimbo langu la Bunda ni tatizo kubwa sana na namshukuru Mheshimiwa Rais kwamba anapopambana na ufisadi huu hela zitapatikana ili zije kwenye maji katika Jimbo la Bunda. Tuna miradi mitatu ya maji; kuna mradi wa Nyamswa wa World Bank, mradi wa Kiloleli na Salamakati. Miradi yote hii haijaenda kwa sababu fedha hazijaenda kwenye maeneo yangu. Mheshimiwa Waziri anapokuwa kwenye bajeti yako, naomba ufikirie namna ya kupeleka fedha Bunda kwa ajili kuendeleza miradi yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya barabara. Tuna barabara ya Nyamswa – Bunda, barabara ya Makutano
– Sanzati – Nata na tuna barabara ambayo inakwenda kukasimiwa kuwa barabara ya TANROAD ya Mgeta – Siolisimba – Mikomalilo. Kwa hiyo, naomba maeneo haya tuzingatie wakati tunapokuwa tunafanya bajeti hiyo waone namna gani mnasaidia miradi yangu kwenye Wilaya ya Bunda na Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Hospitali yetu ya Kongwa Mkoa wa Mara, ni ya muda mrefu sana na tumeisemea sana. Tunaomba kipindi hiki cha bajeti waikumbuke Hospitali ya Kongwa ambayo ni Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Bandari yetu ya Musoma, hii ni bandari ya muda mrefu sana na kwa sasa hivi imechakaa. Tunaomba waitengee fedha na niliona wanaenda kuishughulikia. Kwa hiyo, waone namna gani ya kusaidia ili Mkoa wa Mara nao upate bandari na iweze kutumika vizuri. Bahati nzuri kuna meli ya MV Butiama ambayo iko Mwanza inatengenezwa. Kwa hiyo, ikitengemaa tuone namna ya kuifikisha Musoma kwa ajili ya kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna reli ya kutoka Tanga – Arusha – Musoma, tumeizungumza sana. Pamoja na kwamba tuna reli ya kati ambayo tunaipigia upatu, lakini hata reli hii inayotoka Tanga – Arusha – Musoma inaweza kusaidia katika maeneo yetu na kuendeleza uchumi wa watu wetu katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa tunazungumzia mambo ya wakulima, lazima tukubaliane namna ya kuboresha zao la pamba. Katika Mkoa wa Mara hakuna zao lingine la kibiashara, ni zao la pamba ambalo liko pale. Kwa hiyo, tunapokuwa tunazungumza haya mambo, ni lazima tuone ni namna gani tunapandisha bei ya pamba. Miaka mingi sana tumekuwa tukitegemea Soko la Dunia, lakini lazima tutegemee viwanda vyetu vya ndani ili tuweze kukuza bei ya pamba katika Mkoa wa Mara na Kanda ya Ziwa kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya wafugaji. Tumekuwa na Kamati mbalimbali; kuna Kamati zimeundwa kwa Wizara tatu. Tunaomba zile Kamati zifike Mkoa wa Mara na hasa eneo moja linaitwa Kawanga kwenye Jimbo langu la Bunda ambako kuna migogoro mikubwa sana ya wafugaji kati ya Pori la Akiba la Ikorongo na eneo langu na Vijiji 15 vilivyopo kwenye maeneo haya ili tuweze kuona namna gani tunaweza kusaidia katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo mengi sana ya ndovu kwenye maeneo yetu. Tunaomba zile fidia ambazo zinahitajika kwenye maeneo haya; kuna Kijiji kimoja ama Vijiji vitatu vimebaki vya Maliwanda, Mgeta na Kyandege. Tuone namna ya kuvisaidia hivyo vijiji ambavyo havikupata fidia ya kifuta jasho ambapo vijiji vingine vimepata lakini vyenyewe havikupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda viwili vidogo vidogo vya maziwa, havifanyi kazi muda mrefu sana; kimoja kipo Kyandege na kingine kipo Mgeta. Kwa hiyo, tunaomba waone namna gani hivyo viwanda vinaweza kusaidiwa ili viweze kutoa mazao yao kwa ajili ya kuwapa faida wakulima wa maeneo hayo. Hivi viwanda vilijengwa enzi hizo za miaka ya nyuma tukiwa na Kiwanda cha Maziwa Musoma ambacho kimekufa, sasa tuone namna gani ya kuvifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda vya pamba viwili; Ushashi na Bramba. Kwa hiyo, tunaomba tuweze kusaidiwa kuvifufua viwanda hivi kwa ajili pia ya kuongeza zao la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii zana inayozungumzwa ya tozo ya road license. Gharama za mafuta kwa miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikishuka sana, lakini hatujawahi kuona nauli ya kutoka Bunda kuja Dodoma inapungua. Kwa hiyo, hata tukipunguza habari ya mafuta, wala hawa watu wanaofanya biashara ya usafirishaji hawapunguzi gharama zao za nauli. Kwa hiyo, naona kwamba hii Sh.40/= tuliyoiweka tungeongeza Sh.10/= ili tuipeleke kwenye maji kwa ajili ya kusaidia akinamama wanaohangaika na maji kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tukiwa tunazungumza suala la walemavu, ni vizuri tukaona namna gani ya kupunguza baadhi ya gharama. Pamoja na kwamba zimepungua, lakini bado. Tuwasaidie walemavu katika maeneo mbalimbali na hasa wale watoto wanaotakiwa kusoma ili wapewe vifaa bora kwa ajili ya kujifunza na kwa ajili ya kupata manufaa katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hapa ni kuhusu umiliki wa akinamama katika suala la ardhi. Sasa ni vizuri tukiwa tunazungumza hapa, tuone kama bajeti hizo zinawekwa kwenye maeneo haya ili tuweze kuona, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze kwa kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi na kwa Mkuu wake, jemedari wetu Mkuu Dokta John Pombe Magufuli, kwa kuongoza kazi nzuri anazozifanya, anatekeleza vizuri Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na hili niliseme tu, kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ninavyomuona namkumbukia sana Simba wa Nyika, Marehemu Mheshimiwa Mfaume Kawawa ambaye enzi hizo alikuwa akiagizwa kutekeleza jambo anatekeleza, Mungu amrehemu mahali alipo. Waziri Mkuu kila anapopewa nafasi ya kutekeleza mambo anatekeleza vizuri sana. Nimpongeze kwa kweli kwa mambo yote hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza mambo madogo tu kwenye hii bajeti na kwenye hii hotuba ninayotaka kuitoa hapa au kwa maelezo ninayotaka kutoa; kwamba, hivi mtu akipata nafasi ya kuchangia kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, hivi mwaka ujao yale aliyoyasema atayaona mawili, matatu yametendeka au ni kusema tu halafu yanaishia hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kusema kwamba kwa nafasi hii nitakayokuwa nayasema hapa nataka kuyapima kwamba mwaka ujao nitakuja kuona nafasi nilichangia kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, yale niliyoyasema japo mawili matatu yametendeka? Kwa hiyo, nafikiri hili jambo litakuwa bora zaidi kwa Bunge kuchangia hii ofisi kwa sababu ndiyo eneo kubwa ambalo Waziri Mkuu analiongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijielekeze kwenye miradi ya Jimbo langu la Bunda. Tuna miradi ya maji, katika miradi ya maji ya Jimbo la Bunda iko miradi mingi sana. Nimpongeze Waziri wa Maji, amekuja pale mara nyingi sana, kuna Mradi mmoja unaitwa Nyang’alanga – Mgeta ambao ulianza kwa bajeti ya milioni 495, sasa una milioni 910 mradi haujaisha na maji hayajatoka. Kila siku ripoti zinakwenda na hakuna ukaguzi unaofanyika wa kutoa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,ahati nzuri Naibu Waziri wa Maji amesema wale wote wanaohujumu fedha za maji watakipata cha moto. Namwomba afike pale sasa aone namna ya kuwashughulikia mradi wa maji Nyang’alanga ili kuweza kumuondoa mtu ambaye amekaa pale kwa muda mrefu na hakuna kazi inayofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mradi wa Malambo. Bunge lililopita nilizungumza hapa malambo 12 yaliyokuwa yanataka kutengenezwa ya zamani kuyafufua. Tunayafufua kwa sababu kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye Jimbo langu ni kilometa 25 lakini sisi maji hatuna tuna tabu sana ya maji katika Jimbo la Bunda. Tunataka kufufua malambo ya zamani yaliyochimbwa na Mtemi Makongoro na tumeleta bajeti kwenye Wizara ya Maji na Katibu Mkuu Wizara ya Maji alipokea huo mradi wetu na tunaomba aushughulikie, ninashauri haya mambo yafanyike mapema ili tuweze kupata maji kwenye Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza habari ya wanyama waharibifu kwenye Jimbo langu. Jimbo langu lina vijiji 11 ambavyo wanyama waharibifu wapo kila siku, kila mazao yanayolimwa yanaliwa, hata katani zinazopandwa zinaliwa, hata pamba inayolimwa sasa hivi inaharibika. Tunaomba Serikali sasa ichukue hatua za kutosha za kuzuia wale wanyama wasiwe wanakuja kuharibia wananchi mazao ili wananchi waweze kujineemesha kwa sababu yale mazao ndiyo kipato chao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu fidia. Toka haya mazao yameanza kuliwa tunadai zaidi ya milioni 360, kulikuwa na milioni 400 wameshalipa karibu milioni 182, kwa hiyo bado milioni 360 zinadaiwa, tunaomba Serikali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na nimwombe Waziri Mkuu ahimize hii fidia ya wakulima iweze kupatikana kwa Jimbo la Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya afya katika Jimbo langu. Tumejenga zahanati tano na mpaka zahanati zingine tumeshaezeka, tunaomba Serikali, kwa sababu Bunge lililopita Wabunge walisema hapa, maboma yote ya zahanati zote na maboma ya vituo vya afya wakasema na Bunge la Bajeti hapa tulizungumza na Bunge lililopita tulizungumza, kwamba maboma yote yashughulikiwe na yaletwe hapa Bungeni na tuweze kutengeneza mkakati maalum wa kuyamaliza, sasa sijui hatua imefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa maboma matano ya vijiji vilivyotengeneza kwenye jimbo langu, Kijiji cha Kambubu, Chiling’ati, Komalio na Malambeka ili waweze kupewa fedha za kuweza kumalizia majengo haya. Nimuombe Waziri wa Afya aweze kutusaidia na Wizara ya TAMISEMI iweze kutusaidia katika jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza habari ya barabara, habari ya barabara ya lami kutoka Makutano kwenda Nyamswa hadi Sanzati, inaitwa makutano ya barabara ya lami kutoka Makutano – Sanzati. Ninavyozungumza hii barabara bila unafiki, Mheshimiwa Waziri Mkuu namshukuru sana alikuja Mkoa wa Mara na akapita kwenye ile barabara akaiona, ni vitu vya aibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayopita kwenye maeneo ya kaburi la Baba wa Taifa imekaa miaka zaidi ya sita haimaliziki na wale watu wanaotengeneza hiyo barabara wale wakandarasi hawaguswi, hivi ni akina nani hawa? Barabara ipo kila siku na vumbi zinakwenda kwenye kaburi la Mwalimu pale, hakuna mtu anamaliza hiyo barabara, why?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii tupo tunavuta upepo, huu upepo tunaovuta ni wa Mwalimu. Jamani mambo gani hayo? Aibu hii. Mheshimiwa Waziri Mkuu ameliona hilo, nadhani atalishughulikia haraka iwezekanavyo ili tuweze kuzungumza haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara ya Nyamswa – Bunda, tuliahidiwa kupewa mkandarasi lakini hajaenda. Tuna Barabara ya Sanzati – Nata, mkandarasi hajapatikana, na kuna barabara ya kutoka Bunda kwenda Buramba na Buramba – Kisoria, mkandarasi bado naye anasuasua hajawa kwenye uwezo mzuri. Tunaomba Serikali ione namna gani ya kumaliza zile ahadi zake na hasa ile miradi ya muda mrefu ambayo inahitaji kumalizika. Barabara ya Makutano – Nyamswa – Sanzati ni ya muhimu sana, imeleta kero kubwa sana kwa wananchi wa Butiama na wananchi wa Kata ya Nyamswa na maeneo mengine yaliyopakana na barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi; namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja Mkoa wa Mara, amezungumza na ametusaidia mambo mengi, lakini migogoro ya Vijiji vitatu vya Silolisimba, Lemuroli na Mkomalilo bado vina matatizo ingawaje Mkuu wa Mkoa anajitahidi kumaliza tatizo hilo, lakini bado, tunamuomba na bahati nzuri siku moja Mheshimiwa Naibu Spika alitamka hapa Bungeni kwamba Serikali ishughulikie namna ya kumaliza tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuone namna gani ya kulimaliza ili wananchi waweze kukaa vizuri kwa sababu kila siku ni mapanga. Bahati nzuri miezi miwili iliyopita wananchi wawili walikufa kwa ajili ya mapigano ya hiyo mipaka, kwa hiyo tunaomba tuone namna ya kulimaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya Watendaji; katika jambo ambalo Wabunge tunashauri kwa kila mara na kama tuko Kikatiba katika kushauri jambo hili, hili suala la Watendaji hawa ambao tumepanga kuwafukuza, nadhani katika jambo ambalo tunaweza kulihimiza Bunge lifanye ni namna gani ya kuwaacha wale Watendaji wamalize muda wao, kwa sababu wengi wamemaliza miaka miwili, mitatu, minne, mitano, kuna haja gani ya kuwatoa sasa hivi? Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri tuone namna gani na tupate majibu mapema ili tujue namna ya kuwasaidia hao Watendaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina miradi ya REA vijiji 21, Jimbo langu katika Mkoa wa Mara ndiyo Jimbo lenye vijiji vingi ambavyo havijafikiwa na umeme ingawaje Mheshimiwa Waziri amenisaidia vijiji vingine huko nyuma vilikuwa 32 sasa vimebaki 21. Tunamwomba yule mkandarasi wa REA kwenye Jimbo langu na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alifungua mradi wa REA kwenye Jimbo langu, ajitahidi kumhimiza mkandarasi aweze kuimaliza ile miradi kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia habari ya Bandari ya Musoma, kuna miradi mikubwa pale ya Kimkoa, kuna mradi wa bandari na kuna mradi wa kiwanja cha ndege Musoma na mradi wa Hospitali ya Kwangwa. Kwa hiyo, Mkoa wa Mara kuna miradi mikubwa kimkoa, tunaomba Serikali iangalie namna ya kuimaliza ili wananchi wa pale waweze kupata huduma za kutosha katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo langu la Bunda na Bunda nzima na Jimbo la Bunda, ardhi yetu imechoka sasa, tunaomba kama kuna uwezekano wa kupata pembejeo kwa ajili ya wakulima sasa na sisi tuingizwe kwenye mradi huo wa kupewa pembejeo ili wakulima waweze kupata mazao mazuri kwa sababu ardhi yao imechoka kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya Walimu wa sayansi shule za msingi na sekondari. Katika maeneo mengi ya Jimbo la Bunda kuna sekondari zaidi ya tisa hakuna Mwalimu hata mmoja wa sayansi. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri sasa Waziri anayehusika aweze kuona namna gani ya kutusaidia Walimu wa sayansi kwenye sekondari tisa katika Jimbo la Bunda ambazo hazina Walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vingine naviona hapa nikivisoma huwa vinanitia kichefuchefi kidogo. Kuna deni la watumishi wa Serikali, lakini ukiangalia deni la watumishi wa Serikali kuna vitu vingine vya kujitakia. Hivi inawezekanaje leo tuna watumishi wanaokaimu wengi katika Wizara mbalimbali na kila mtumishi anayekaimu anapewa nusu ya mshahara wa mtu aliyekuwepo katika nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kama Mkurugenzi aliyetoka alikuwa anapokea mshahara wa milioni tano na yeye anaenda kukaimu anapokea milioni mbili na nusu na anakaa miaka kumi, mitano, saba, kumi na tano. Sasa hii kwa nini tunaitafutia Serikali madeni, kwa nini tusibadili sheria hizi za utumishi za kukaimu na sheria zile za kwenda kwa wakati wanakaimu kama ni mtu kwenda kukaimu tumwambie akaimu bure, sio akaimu kwa kulipa mshahara, tunatia madeni Serikali bure na tuangalie ile sheria namna ya kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kuangalia sheria ndogo hizi au sheria za Wanyamapori, Maliasili na Utalii na hasa zile sheria za fidia. Fidia imekuwa ndogo sana lakini mbaya zaidi kuna sheria zile za fidia ambazo hazijakaa sawa. Kwa mfano, kutoka mpaka wa wanyamapori kwenda kwa wananchi wanasema iwe ni mita 500, mita 500 ni nusu kilometa, lakini kutoka hiyo nusu kilometa buffer zone kwenda mpaka kilomita 1000 mkulima anatakiwa kulipwa kama amelima shamba heka 20 halafu tembo amekwenda amekula mazao yote, anatakiwa kulipwa heka tano tu, heka 15 nyingine ni sadaka, hii sheria ya wapi tena? Nafikiri kwamba ni vizuri wakaangalia hiyo sheria...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, niwapongeze Maprofesa wawili, Profesa Katibu, Waziri na Naibu wake Mheshimiwa Aweso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui nianze wapi kwa sababu kuna vitu vingine niliwaza wakati hawa watu wameteuliwa, nikamwona Profesa Kitila, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na Mheshimiwa Aweso wote wajanja. Kwa lugha ya kilaini kabisa na ya kitaalam na ya watu wale waliosoma wanasema, is software siyo hardware. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuja kutazama mambo yanavyokwenda, hivi kweli kwenye Wizara ya Maji ambako kuna wataalam leo wanapotuambia kwamba kufika Aprili katika nchi yetu kuna watu asilimia 64.08 wamepata maji vijijini, kweli? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Uongo mtupu.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa lugha nyingine maana yake ni kwamba katika vijiji 1,000, at least vijiji 650 vina maji safi na salama na vijiji 350 ndiyo havina maji safi na salama. Kwa hao watu ambao tuko nao hapo ofisini kwa nini tunakariri vitu ambavyo havipo? Hivi Wabunge walioko hapa sasa wakisimama leo kila mtu aseme kijijini kwake kuna nini, kuna haja hiyo kweli jamani? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hakuna maji.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunapewa takwimu ambazo hazipo? Kwa hiyo, wakati fulani vitu vingine vinachanganya kidogo. Kwa nini watu ambao tunawaamini wanaotumia kompyuta siyo maneno ya zamani, kompyuta halafu tunapewa takwimu siyo sahihi? Leo REA wanaweza kukuambia Bunda kuna vijiji 15 havina umeme na vijiji 20 vina umeme. Leo maji wanaweza kutuambia kila mkoa, wilaya, halmashauri, Jimbo la Mbunge lina vijiji vingapi vina maji, takwimu ikaja hapa. Jamani nyie bado vijana tupeni maji hakuna lugha nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema wazi hapa, katika kitabu hiki kuna changamoto zimetolewa. Changamoto ya kwanza nzito sana iliyotolewa ni ukosefu wa fedha za kutekeleza miradi ya maji, ndiyo iko humu jamani. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli amepita kila mkoa anawaambia viongozi sisi sometimes hatusaidii matatizo ya wananchi. Sasa leo Wabunge tunasema tunataka kusaidia mambo ya maji yaende, shida iko wapi sasa? Tunataka maji sasa yaende, tunataka aidha fedha shilingi 50 inatoka wapi lakini Kamati ya bajeti ikae ituletee, kwamba jamani eeh ili twende huko fedha ni hii hapa, nchi yetu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani aliyechagua watu wachafu wakae vijijini halafu watu wasafi wakae mjini? Watu wanasema watu wamesongamana sana mjini, nani anayekaa kwenye uchafu huko vijijini, sisi wasafi tuko huku ndani. Mimi kijijini kwangu dampo ambalo ng’ombe na mbuzi wanakunywa maji ndiyo binadamu naye anakunywa yaani kila kitu kinakunywa mle ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki ni kipindi cha kuamua tu kwamba tunataka kusaidia nchi yetu iende, tupeni maji, tutafutie fedha. Mmetuletea wenyewe hapa, mmesema kikwazo ni fedha na sisi Wabunge tunasema fedha iko hapa, sasa shida iko wapi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi mnafanya kazi nzuri lakini ndiyo hivyo sasa mmesema matatizo ni haya na sisi tunataka kuyasema. Mheshimiwa Waziri alipokuja Mheshimiwa Rais tarehe 09/9/2018, alipofika pale Nyamswa alikusimamisha Mheshimiwa Prof. Mbarawa kukuambia matatizo ya Jimbo la Bunda na mimi nilimwambia Mheshimiwa Rais matatizo yaliyopo na bahati nzuri nishukuru Wizara yako imetuma wataalam, wametembelea vijiji 30, wameleta mchanganuo lakini toka asubuhi nikasema labda miwani sina, nimenunua miwani nimetazama humu ndani sikuona hata kitu kimoja. Mheshimiwa Rais kasema, Waziri maliza matatizo, Waziri katuma wataalam wakaenda kufanya tathmini, wataalam wamekuja sioni Jimbo la Bunda hapa, sioni Bunda DC kuna nini kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwamba wakati fulani labda mtakuwa mmesahau lakini najua mtalikumbuka mtaniwekea hivyo vijiji ambavyo vina Kata za Unyali, Bungeta, Mihingo, Kitare, Salama, Nyamswa na ya Nyamang’uta. Wataalam walitembelea kote huko, nadhani mtaniambia kuna kitu gani kimetembea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza vizuri na naendelea kuzungumza vizuri kwamba nyie ni software, haiwezekana tukakariri gharama kubwa za kuendesha maji, gharama ni kubwa kuliko kawaida, kubwa sana. Leo mradi mmoja shilingi bilioni 20, shilingi bilioni 3, shilingi bilioni 4, tumefanya majaribio ya kujenga Hospitali za Wilaya na vituo vya afya kwa kutumia Force Account, gharama ni ndogo sana. Ninyi kwa nini msikae mkasema tufanye kama Malawi, tutandaze bomba kutoka Ziwa Victoria lipite barabarani tu, kila kituo, kila kijiji mnaweka toleo, barabarani tu. Vijiji vingine vilivyoko huko porini vitakuja kuchota maji pale kwa sababu vitakuwa na uhakika wa maji. Bomba lipite liende, inakuwa maajabu leo Bunda kilometa 15 kwenda kilometa 15 nyingine kutoka Ziwani hakuna maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnafanya wananchi wanakuwa watu wa ajabu. Hivi kama tunasema tunahurumia wananchi hawa, wanaendaje kupiga kura wakati wote hawana maji? Saa 12 akina mama ndiyo wanapiga kura, hawaendi kupiga kura maji hayapo, tupeni maji tuache

maneno jamani, tupeni maji. Tumechoka tupeni maji, haiwezekani. Mheshimiwa Aweso bado kijana mdogo unaweza ukatoa maji, tupeni maji. Kwa hiyo, nisema gharama za uendeshaji wa maji ni kubwa mno, tutumie akili tutengeneze namna ya kuwa na gharama ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimewaambia pale Bunda, kama mnaweza kunipa shilingi bilioni 10, nipeni mimi nipeleke maji nakotaka. Wataalam wa MUWASA wako pale, tutengeneze gharama. Tumeshatengeneza bomba, kiasi gani, wachimbaji ni wanakijiji wenyewe, ufundi unakuwepo tunaweka maji, kila mahali patakuwa na maji. Kama hiyo RUWASA hatuwezi kuiwekea mazingira mazuri itakuwa na hela kutokea wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo liko hapa, haiwezekani tukasema tunatafuta fedha, haiwezekani Mawaziri mkahangaika, haiwezekani Mheshimiwa Rais akahangaika mpaka anaomba misaada ya fedha kutoka nje, halafu watu wanaitwa sijui watumiaji maji, MUWASA, DUWASA, wanakula fedha. Tumeona kwenye ripoti ya CAG maeneo yote haya ya maji hasa ya majiji wamekula fedha. Tusisubiri ripoti kwamba PAC na LAAC wafanye kazi, hapana. Tukiona kuna chokochoko mahali, watu wanakula fedha za maji wakamateni waondoeni kwenye nafasi, mnasubiri Kamati za nini? Hatuwezi kukusanya fedha halafu watu wengine wanakula. Kwa hiyo, naomba tuangalie tunakwendaje kwenye suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili sasa nitaongea kwa upole, polepole tu msikie. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni karne sijui ya ngapi, sijui ni 21 au 22 sielewi.

MBUNGE FULANI: Hiyo ndiyo polepole?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Hiyo ndiyo polepole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekanaje leo eti mtu anakuja pale hodi, hodi, nani? Mimi mpima mita, jamani! Anakuja kuangalia bili apelike ofisini. Kwa nini tusiwekewe mita mtu alipie maji kadri anavyotumia, kuna shida gani? Hili nalo mpaka Mheshimiwa Rais aje aseme ndiyo mfanye? Kwa nini watu wanatumia bill kwa ajili ya kula fedha? Kwa nini wanaletea watu bili kwa maji ambayo hawajatumia? Kwa nini tusitumie mita kila mtu anakunywa analipa, shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie hili tena polepole ili muelewe vizuri. Mheshimiwa Waziri, Naibu Mheshimiwa Aweso, Katibu Mkuu katika jambo ambalo hatuwezi kufanya mchezo wa kuigiza au wa kupiga siasa ni suala la maji, watu wana hali mbaya sana. Wakati fulani naenda kijijini nasema huu Ubunge wa nini sasa, si bora nitoke tu. (Makofi)

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri ni vizuri mkafanya kazi ya kutusaidia kupata maji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Muda wake umeisha, Mheshimiwa Getere muda wako umemalizika.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu wa bajeti. Michango hii watu wengi wameizungumza vizuri lakini nilikuwa naangalia katika nchi yetu hapa kwamba uchumi wake unakuwaje, unakuwa kwa 6.8 mpaka seven point. Wanauchumi wanasema uchumi ukikua lazima uendane na mipango ya wananchi katika maeneo yao. Nilikuwa naangalia maeneo mbalimbali sijui kwa nini nchi yetu haiendi kwenye vyanzo halisi vya kupata uchumi wetu unavyokwenda. Ukiangalia katika maziwa yetu, Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria, ukinda Norway, ukienda Algeria, nilikuwa naangalia hapa Algeria ni nchi kama ya tatu hivi kiuchumi, lakini maeneo mengi inayotegemea katika uchumi wake ni suala la samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi uki-invest milioni 40 katika samaki unaweza ukapata samaki 200 na samaki 200 ukipata unaelekea kuzungumza habari ya bilioni mbili. Kwa hiyo nafikiri kwamba, sasa uchumi wetu uende sana kutafuta fedha za ku-invest katika maeneo ambayo tunaweza kupata faida kwa wakati muafaka. Vijana wetu wengi hawana ajira, lakini maeneo yetu mengi yana ajira. Tuna suala la kilimo, ukiangalia sasa Misri ndiyo nchi inaenda kwenye uchumi ambao uko juu kwenye uchumi wetu, lakini uchumi wao mwingi unatokana na hot culture, Kenya hivyo hivyo, Angola nayo imeenda kutuzidi kwenye uchumi ingawaje wana mafuta. Kwa hiyo, naomba Wachumi wetu waelekee sana kwenye namna ya kupata fedha ku-invest katika maeneo ambayo tunaweza tukapeleka vijana wetu wakafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naiona JKT kama ni eneo ambalo tungelitumia sana kupata uchumi wetu vizuri. Tuna maeneo mengi vijana wetu wanaenda JKT, tungetumia vijana hawa kuwapa mikopo katika maeneo, tuna maeneo mengi mazuri sana. Wale vijana wote wanaokwenda JKT wakitoka pale wameiva kwenye shughuli za kilimo, watu wote tume-invest kwenye shughuli za kazi za ofisini kazi ambazo sasa hazipo. Kwa hiyo tubadilishe mind set zetu twende kwenye maeneo ambayo tutanufaika nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi yalikuwa yanazungumzwa hapa, watu wanazungumza good governance (utawala bora), lakini utawala bora haujajikita kwenye election peke yake, umejikita kwenye mambo mengi. Kuna effective, kuna transparency, kuna accountability, kuna mambo mengi yamejikita humo ndani lakini watu wameng’ang’ania mambo ya utawala bora utawala bora, kama vile ni uchaguzi. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi za Ulaya sasa zinaangalia uchumi wao, kuna watu wanafikiri kwamba Tanzania haiko kwenye mpango wa kwenda mbele. Sasa hivi tunaangalia kwamba uchumi wa China mwaka 2030 utakuwa umezidi Marekani mara mbili, kuna watu wanaangalia hata Mexico nchi maskini inapokwenda 2030 inakwenda kuikaribia Marekani. Kuna watu wanafikiri kwamba kila wakati sasa sijui ni kuzungumza mambo ya uchaguzi, mambo ya kugombana. Kuna wasomi wamesema haya mambo ya uchaguzi pia yaliletwa na watu ambao wameleta kuvurugana kwenye nchi za Kiafrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia nchi nyingi nyingine zipo nchi za utawala wa kifalme hazina uchaguzi. Leo mtu anazungumza uchaguzi umekuwaje, uchaguzi umekuwaje ili mradi wapate msaada. Nataka niwaambie wenzetu nchi za Ulaya sasa hivi kila nchi inagombana, ukienda Marekani wanagombana juu ya utawala bora, sasa Marekani si nchi ya demokrasia, ni nchi ya utawala wa sheria. Ukienda Uingereza inagombana na Black City, ukienda kila mahali wanagombana kwa hiyo wasipokwenda kwenye uchaguzi wajue hakuna mtu atawasaidia, wao waende kwenye uchaguzi, tufanye uchaguzi mambo yaishe tuendelee na wakati wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanafikiri Mheshimiwa Magufuli amejiweka tu kuwa Rais, Mheshimiwa Magufuli ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyetokana na Chama cha Mapinduzi. Nilisikia siku moja mtu anasema ndege zimekuja nikaona mapambio, nikaona nini, nikamshangaa. Ukisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 70 inaeleza jinsi gani tumefanya mipango mikakati ya kuwa na viwanja vya ndege vingi na kupata ndege kwa ajili ya mambo yetu hapa. Sisi tunapoona…(Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere tatizo siyo uchaguzi, watu wanaangalia matokeo, wameshaangalia wanapigwa ile mbaya. (Kicheko/Makofi)

Sasa wanakamatia hapa chini lakini wanajua kimbembe kiko, si tarehe 24 Novemba wewe utaona matokeo tu! Mheshimiwa endelea. (Kicheko)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza…

MWENYEKITI: Nilikuwa namchokoza Frank hapa!

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli! Kwanza mimi naona hiki Chama cha Upinzani ndani ya Tanzania kinaitwa CHADEMA, hiki chama kinakokwenda kwanza wanazungumza transparency, wao wenyewe wanapata mabilioni ya fedha hapa kutokana na ruzuku lakini mpaka today wameandikiwa barua mbili na Msajili wameshindwa kufanya uchaguzi. Sasa huu utawala bora wanaouzungumza ni upi? Utawala bora wa CCM peke yake au utawala bora mwingine? (Makofi)

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwakajoka, Mwakajoka ametoka pangoni. Jamani tumempa ruhusa Mwakajoka.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, kwanza anasema kwamba mambo ya uchaguzi haya hayafai na sisi pia tulishawaambia kwamba mko wengi ndani ya Bunge leteni Muswada hapa tufute vyama vingi vya siasa ili mbaki na chama kimoja. Mtakaotaka kubaki CCM mbaki na sisi wengine ambao tutakuwa hatutaki tuendelee na mambo yetu. Ahsante. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Kaa chini, kaa chini wewe!

MWENYEKITI: Jamani aliyepewa taarifa ni Mheshimiwa Mwita Getere, unaipokea taarifa Mheshimiwa Mwita!

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza vyama vyenyewe vitajifuta kama vinavyojifuta sasa hivi, kwa hiyo mimi sioni haja ya kuendelea na mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze, kuna watu wamezungumza hapa fedha haziendi kwenye maeneo yetu ya majimbo, fedha haziendi huko kwenye halmashauri, fedha haziendi wapi, sasa mimi najiuliza; fedha haziendi wapi? Ukienda sekta ya elimu tunatoa bilioni 24 kila mwezi zinakwenda shuleni, ukienda kwenye afya…(Makofi)

MWENYEKITI: Kila halmashauri inapata.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kila halmashauri inapata. Ukienda kwenye afya hospitali zinajengwa kila mahali hata Mwakajoka juzi alisema imejengwa kwake, ukienda kwenye reli fedha zinakwenda, ukienda kwenye barabara za changarawe na lami zinakwenda, ukienda kwenye shughuli za kila mahali zinakwenda. Kwenye madini wamezungumza hapa, watu wanasema Private Sector, tushirikiane na Private Sector kutengeneza uchumi, sasa mtu anasema tupeleke fedha kwenye madini. Badala ya kusema wale wa madini tuwape nafasi ili Private Sector zituletee fedha, yeye anataka tupeleke tena fedha kwenye madini. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita na kwenye ruzuku ya CHADEMA zinaenda pia.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ruzuku ya CHADEMA pia zinaenda huko huko ndani. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoona sasa hivi suala la hawa wenzetu wamejichanganya kuhusu Mheshimiwa Rais wetu. Rais wetu amejiongeza kukusanya mapato ya kutosha kwa ajili ya kupeleka maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja, siku moja tumekwenda pale Muhimbili, mtu anasema hapa panadaiwa bilioni nne hazijaja hapa, bajeti haijaja ya bilioni nne. Bilioni nne kabla ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuwa madarakani walikuwa wanakusanya bilioni tano, sasa hivi katika sekta ile ya Hospitali ya Muhimbili inakusanya bilioni 11, sasa kama zimeongezeka unapeleka za nini wakati hela zimeongezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawajui kubana matumizi pia ni sehemu ya kuongeza fedha kwenye maeneo mbalimbali. Kwa hiyo nafikiri kwamba wenzetu wanajichanganya na hali halisi ilivyo na katika huo utawala bora wako watu wanasema ile Citizen, Watanzania wanategemea nini. Kama wameona Rais aliyepo na chama kilichopo kimebadilika kinaenda kuwaletea matumaini wawe na vyama vingine vya kufanya biashara gani! Leo hata mngepeleka Polisi Ngorongoro, hata mngepeleka polisi pale Monduli kuna maeneo hata ungepeleka fomu 300 hazichukuliwi. Maana pale hawachagui vyama, wazee ndiyo wanasema, ukienda Ngorongoro wao walishamaliza uchaguzi wanasema wewe ni Mwenyekiti, wewe utakuwa Diwani, wewe utakuwa Mbunge, sasa unaenda kufanya biashara gani kule ndani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona chama kinaitwa sijui ni NCCR Mageuzi, hakipo. Yule mzee naye ampumzike aende pole pole tulishampa na madaraka siku nyingi hapa ndani, naye anang’ang’ana kwenda kwenye sehemu ambayo haipo. Atulie mahali pake sisi tumuone bora hata tuweze kumpa Ubalozi, anaanza tena maneno ya kuleta matatizo kwenye nchi yetu hapa. Kwa hiyo tukubaliane kwamba CCM pamoja na kwamba Rais wake...

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita kuna taarifa.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mwita Getere kwamba hata kwangu Serengeti, nimeshangaa sijawahi kuona, vijiji vingi wamepita bila kupingwa hata kwenda kuchukua fomu imeshindikana, wametafuta wagombea wamekosa kabisa. Sijawahi kuona hii, sijawahi kuona kabisa. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita unapewa taarifa hiyo, unaipokea?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa kwa sababu mimi ninavyoona, labda kama tunataka, nakuomba, pengine tukae tukubaliane hawa wenzetu walioko humu ndani tunaweza kuwasaidia labda kajimbo kamoja, viwili wakarudi humu ndani. Maana yake hali ya hewa ni mbaya kuliko ilivyo kawaidia, kwa hiyo, ndiyo maana wamekuwa na hali hiyo (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ukweli kama tunataka kuwa na upinzani tutengeneze mazingira ya kuwabakiza wenzetu, vinginevyo wote hawatarudi hapa ndani. Kwa hiyo, tukubaliane na mazingira hayo, vinginevyo tukubali sasa Tanzania imebadilika, watu wanataka Chama cha Mapinduzi, lakini wasimhusishe Mheshimiwa Rais na uchaguzi. Mheshimiwa Rais anafanya kazi za Serikali, Chama cha Mapinduzi kina viongozi wake, Chama cha Mapinduzi kina Katibu, kuna viongozi, kuna Wabunge sisi tupo tunapambana na mambo yetu. Wenzetu wameshindwa kwenda kupambana kule chini, wanapambana na hali ya hewa ya kwao humu ndani. Wameshindwa kwenda kupambana kwenye majimbo yao wameachia maeneo yameenda, watu wanaogopa. Kwa hiyo, naomba mazingira yatengenezwe, tuone namna gani tutaendelea na upinzani Tanzania, vinginevyo hautakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE.BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia katika bajeti hii. Kwanza niishukuru Wizara na Waziri wa Fedha, amefanya na Idara yake yote, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Fedha, wamefanya kazi nzuri sana, tumeona bajeti hii katika maeneo mengi sana wamepunguza vitu vingi sana na kwa maana hiyo bajeti yenyewe imekwenda katika kukidhi mahitaji ya watu kwenye maeneo mbalimba na makundi mbalimbali, mimi kwa maoni yangu naona wamefanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumza miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mara. Nilikuwa naomba sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, katika bajeti tuliyokuwa nayo, katika ile miradi ya kimaendeleo katika majimbo yetu, katika miradi ambayo imekuwepo kwa muda mrefu, mradi wa hospitali ya Kongwa ya mkoa wa Mara, mradi wa barabara ya kutoka Makutano kwenda Sanzate; Sanzate - Nata - Mugumu; mradi wa barabara ya kutoka Nyamswa - Bunda - Buramba, mradi wa bandari ya Musoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba katika bajeti hii ambayo mmeiweka basi hiyo miradi iweze kutimilizika na kwa wakati muafaka, ni vizuri sana tunapoweka bajeti tuwe tunaweka vitu ambavyo vinakuwa halisia. Tusiwe na bajeti ambayo inakera wananchi na miradi ambayo nakera wananchi. Tumekuwa na miradi ya muda mrefu kwa Mkoa wa Mara ambayo haiishi. Pamoja na kwamba tunafanya jitihada sana ya kushukuru Serikali kwa kutupa miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze zao la pamba, sasa sijui kama kuna Waziri yuko hapa Waziri wa Kilimo ananisikiliza vizuri. Zao la pamba kwa sasa hivi kwa maeneo yote yanayolima pamba sasa imekuwa kama sumu, kwanza bei yake sasa haijulikani ni shilingi 2,000 na shilingi 1,200, lakini ukienda vituoni kuna watu wananunua pamba shilingi 850, lakini pia haina uhakika kwamba mtu akipeleka pamba apate fedha yake kwenye kituo cha kununulia pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mwaka jana, unakumbuka kwenye bajeti hapa alikuja Waziri wa Kilimo enzi hizo Mheshimiwa Tizeba, akasema wakulima watakatwa shilingi 100, hata kama mkulima huyu hakukopa pembejeo, lakini kwa msimu huu 2019/2020 huyo mkulima hatakatwa pembejeo zitakuwa bure, lakini mpaka tunapozungumza hapa pembejeo zinakatwa! Watu wanajiuliza, mimi nilikatwa fedha yangu bila kukopa, lakini bado leo nakatwa pembejeo tena ya shughuli gani na Bunge hili liliridhia kukata shilingi moja ya wakulima wa pamba, kwa hiyo, tukafikiri kwamba ni jambo la msingi kuwa katika hali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, yamezungumzwa mengi, nilikuwa nazungumza, mtu anazungumza mambo ya magazeti, mambo ya nini, jamani magazeti ni uhuru wa kila mtu anavyoona. Magazeti yako wazi na ndiyo maana huwa nawauliza waandishi wa habari, wakati fulani waandishi wa habari ukienda, ukiwanyima taarifa, wanasema wanakushitaki, ukiwapa taarifa, wanakwambia nipe vizuri. Kwa hiyo, nafikiri kwamba magazeti ni uhuru wa kila mtu kufanya anavyotaka. Sasa kusema kwamba gazeti fulani ni la wahuni au la nini, mimi sielewi!

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hapa wakati wa bajeti Waziri anahitimisha hapa, tumeona hapa tunataja viongozi wa kitaifa wa nchi hii. Wamemtaja Mheshimiwa Pinda, wenzetu wa upande huu hata makofi hawapigi, wakitajwa wazungu wanapiga makofi, kwa hiyo, kuna watu wameshakuwa colonized kwenye mambo kama hayo wanaweza kuwa…(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wahuni ni wapi! Wanaoshangilia watu wa nchi yao au wahuni wanaoshangilia watu wa nje. Kwa hiyo, nafikiri kwamba kuna vitu vingine humu ndani tuviangalie vizuri watu wanapokuwa wanafanya kazi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza hoja watumishi, kuna sheria za kimataifa za International Labor Organization ( ILO) ambazo zinamruhusu mtumishi wa Serikali kukopa moja ya tatu ya mshahara wake, lakini tunavyoenda mabenki kwa kushirikiana na watumishi mbalimbali, wamevunja, hiyo sheria wanaivinja. Sasa hivi mshahara wa mtumishi unaweza kukuta shilingi milioni moja, anapata shilingi 100,000; shilingi 400,000 anapata shilingi 50,000; watumishi wengine wanapata sifuri.

Sasa nimeona hapo tunazungumza habari ya kubana matumizi na kupitia sheria mbalimbali ili zilete nafuu.Tutazame hali ya watumishi wanavyokopa katika mabenki, hii sheria ya mataifa ambayo tumeridhia sisi tuitazame tuone watumishi wanapata kwa kiasi gani zile fedha ambazo..., imekwenda. Sheria inasema, kama utamkopesha mtumishi zaidi ya hapo, maana yake unamuua huyo mtumishi, sasa watumishi wamekopa zaidi na kama atakopa zaidi aoneshe vyanzo vya mapato ambavyo wanaweza kukopea, lakini watumishi wengi, hata leo tungeongeza mshahara milioni moja, bado wanapata sifuri. Kwa hiyo, naomba tuliangalie hiyo sheria ambayo inaweza kuwaruhusu watumishi wakaishi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ...

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere kuna taarifa, Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nipe taarifa mzungumzaji kwamba siyo watumishi tu, hata Wabunge wamefanya hivyo hivyo, sasa nashangaa anawapigia jembe watumishi, wakati Wabunge wamekopa zaidi ya asilimia 80 ya mshahara wao! (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere unaipokea taarifa hiyo?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa yake lakini namkumbusha tu Wabunge nao ni watumishi sawa na watumishi wengine tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza habari ya vitambulisho, sijui katika suala hili kwanini watu wameling’ng’ania sana. Vitambulisho ilikuwa kumuokoa machinga aliyekuwa anafukuzwa kila mahali anapoenda anafukuzwa, tukaweka vitambulisho kumuokoa kwenye mazingira mabovu. Sasa leo kama kuna watu wanatenda vibaya huko, sasa inakujaje kwa Rais, kuna watu wanatenda vibaya huko, inakujaje? Ni wajibu wa Mbunge kwenye Halmashauri yake kumwambia Mkuu wa Wilaya, kumwambia Mkurugenzi, kuwaambia wale waliopewa kazi kwamba Rais hakuagiza kufanya hivyo. Hakuna haja ya kuja kupiga kelele humu ndani, Rais alitoa vitambulisho, anauza, anafanyaje, vitambulisho vilijulikana toka mwanzo, kwamba vitambulisho ni shilingi 20,000.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere kuna taarifa, Mheshimiwa Cecil Mwambe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa ndugu yangu anayeongea kwamba labda hasomi na kufuatilia. Karibuni ilikuja taarifa kwamba TAMISEMI wamekaa na kupitia upya list ya watu wanaostahili kupata vitambulisho. Kwa mfano, Mkoa wa Lindi, Mtwara na kwingine kwenye bahari, wakiwemo pamoja na wapaa samaki, akina mama wanaouza matembele barabarani na wengine. Sasa nataka tu nimpe taarifa, kama watu hawa hawako jimboni kwake na kwamba atoe sasa ufafanuzi vizuri na aichukue hiyo taarifa aseme exactly huko kwenye jimbo lake waotozwa ni nani?

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge,...

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, unajua kuna watu wanakariri siasa, ndiyo hawa hawa!

NAIBU SPIKA:Mheshimiwa Mwita Getere tafadhali.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa sikubaliani nayo kwa sababu huyu amekariri siasa.

NAIBU SPIKA: Subiri kwanza Mheshimiwa Mwita Getere.

Waheshimiwa Wabunge, tukumbushane tena, uvyotoa taarifa huulizi maswali, kwa sababu siyo kazi yake Mbunge kukujibu wewe, ndiyo maana kanuni zetu zinasema unampa taarifa halafu anaulizwa kama anaikubali au hapana. Sasa ukimuuliza swali maana yake unataka akujibu wewe, kwa hiyo, tukumbushane tu hilo. Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea taarifa hiyo?

MHE.BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu huyu naye anakariri tu mambo ambayo hayapo. Tumesema makundi mbalimbali yameainishwa, yanaweza kuchukua vitambulisho vya taifa, kadri wanavyoviona vinawafaa, sasa mambo mengi yakitekelezwa vibaya, hayo ni jambo lingine tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuona mwanamke, unaweza sisi kwa kabila letu wa huko tunaozwa na baba, lakini suala la ku-deal ndani huko kama mna matatizo ni ninyi tu mnaokaa humo ndani, si suala lingine tena baba aje kusema kwamba kulikuwa na nini, angalia sana ndugu yangu mambo mengine unayazungumza uone yanavyokwenda huko kwenye maisha yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza, bajeti hii, nimuombe Waziri sasa, tumekuwa tunaweka bajeti kila mara, lakini bajeti yenyewe haiendi vizuri kwenye miradi yetu. Nirudie katika hilo, katika mwaka huu wa bajeti tunaouweka...

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa mchangiaji huyu hiyo itakuwa taarifa ya mwisho, Mheshimiwa Ryoba Chacha.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka kumpa mzungumzaji taarifa kwamba, vitambulisho vya shilingi 20,000 vimewasaidia wafanyabishara wadogo sana. Zamani kwenye Halmashauri zetu, kila siku mfanyabiashara anatozwa shilingi 500, ukichukua shilingi 500 mara siku 365 ni shilingi 182,000. Leo anaoa shilingi 20,000. Kwa hiyo, ni faida, anayepinga huyo hajitambui, hajui hesabu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere unapokea taarifa hiyo?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa yake.

Mimi narudia tu kusema kwamba bajeti ya mwaka 2019/2020 izingatie miradi muhimu ambayo tumeiweka, itenge kama kuna mradi wa stiegler’s gauge, kuna mradi wa reli, kuna miradi ya kujenga bandari, kuna miradi mbalimbali ya Kitaifa iweke bajeti yake lakini katika miradi yetu pia ya maendeleo katika majimbo yetu, ile miradi ambayo tunakuwa nayo ya barabara, ya maji, ya kila kitu nayo iwekwe miradi yake. Tuhakikishe kwamba bajeti inayowekwa inakuwa na uwiano na even distribution, isiwe sasa sisi tunakuwa na barabara, tunakuwa na maji, tunakuwa na maendeleo bajeti yetu inakuja kidogo halafu inatuumiza sana kwenye maeneo ya wananchi kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo tuweke bajeti ambayo inaweza kuwa sahihi kwneye mambo ya maeneo ya Wabunge, lakini maeneo ya Kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie hii Wizara ya Viwanda na Biashara. Nakushukuru wewe mwenyewe kwa kumuomba Mwenyezi Mungu amekuleta hapa Bungeni, lakini umekaa maeneo yako yale yale kama ulivyo kawaida, tunakuombea uendelee vizuri. Nashukuru Wizara yangu Wizara ya Viwanda ambayo mimi ni mwanakamati, namshukuru Profesa na crew yake yote Naibu Waziri na Katibu, kazi zinaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea ni kwamba naomba nchi yetu hii Mungu anaipenda sana na nadhani tuendelee kumuomba Mungu atuepushe na haya magonjwa mabaya yanayokuja na mimi naamini kama tutaendelea kumuomba Mungu hali itaendelea kuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Na niombe tu kwenye mikutano yetu yote tunayokuwa tunakuwa nayo tuwe tunaanza na yale mambo yetu ambayo ni ya Mungu kwa mfano, Bunge letu huwa tunaanza kuomba Mungu kwanza ndio tunaingia, hata kwenye mikutano tuombe kwa kuomba kwamba Asalaam Aleykum, Tumsifu Yesu Kristo, Bwana Asifiwe, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kazi Iendelee. Kwa hiyo nadhani hili nalo ni jambo kumtanguliza Mungu kila tunapokuwa tunafanya shughuli zote ambazo tunataka kuzifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie kwenye Wizara hii kwenye upande wa Mchuchuma na Liganga. Mimi kama mwanakamati nilivyoona ile hali na wakati sisi humu tunajipa matumaini kwamba Mchuchuma na Liganga itakuwepo, mimi kwangu naona kama hatutatafuta mwekezaji mwenye uwezo wa kuendesha ule mradi itakuwa ni majina tu tunaita kila siku mpaka tunafia humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili Liganga na Mchuchuma iwepo lazima tutafute mwekezaji mwenye uwezo wa kuendesha ule mradi, maana Serikali haiwezi kuendesha ule mradi. Kama Serikali haiwezi kuendesha ule mradi, tutafute mwekezaji mwenye uwezo wa kuendesha ule mradi na mwekezaji mwenyewe tukishampata mikataba yake tuisome wazi ionekane kwamba, anashughulika na miradi miwili mradi wa madini na mradi wa chuma aelewe mapema kutoka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa kaka yangu kwa mchango wake mzuri kwanza wa Liganga na Mchuchuma. Ningependa kumpa taarifa kwamba, kwanza huo mradi umechukua muda mrefu takribani miaka 20, lakini Serikali imeingia ubia na mwekezaji Mchina, amekaa zaidi ya miaka nane, ameshindwa kufanya chochote, wako kwenye hatua ya kulipa fidia, mbaya zaidi wanaenda ku-review mkataba na mwekezaji yule yule.

Sasa taarifa yangu nakupa kwa nini wasimfukuze na naungana na wewe watafute mwekezaji anayeweza kwenda kuwekeza kwenye Liganga na Mchuchuma ili tuweze kupata faida katika Taifa letu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, taarifa yake naikubali nadhani dada yangu sasa hivi yuko vizuri sana, kwa hiyo, naikubali taarifa yake. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua tusiwe tunazungumza mambo humu Bungeni kama kujifurahisha. Nchi yetu inahitaji kupata viwanda ule mradi ni mradi mkubwa sana, mkubwa sana. Kwa mwekezaji aliyopo kama ana-tender nyingi maana yake anataka afanye mradi mmoja yeye kwa mradi mmoja huo hataki ku-separate mambo ya madini na chuma. Kwa hiyo, mimi nione kama ni kazi, kwa hiyo, nimesema tutafute, kama yeye yupo, kama mikataba yake inaeleweka, tuilete hapa Bungeni tuione, tuizungumze humu Bungeni tuione kama anaweza kuifanya ile kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hawezi kama alivyosema Mheshimiwa Ester tumuondoe, tutafute mwekezaji mwingine mwenye uwezo. Sasa siku hizi nako nimesikia Tanzania kuna matatizo, tunaweka makandarasi, tunawaondoa, sijui ni kienyeji sijui ndio ujanja wao, wanarudi nyuma kinyume nyume kutudai tunalipa mabilioni. (Makofi)

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa muangalie tena mambo haya yanavyokwenda ili tuwe tunaweka hii mikataba na mambo mapya tusiwe tunaingia tena kudaiwa mabilioni ya watu wanaokuwa wanaweka mikataba…

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita subiri kidogo, Taarifa Mheshimiwa Mhagama.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukupongeza kwa kurudi katika nafasi yako, naomba nimpe taarifa mzungumzaji mzuri sana Mheshimiwa Getere kwamba commitment ya Serikali ya kuendeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma haupo tu kwenye kuingia mkataba na mwekezaji, bali pia kujenga mazingira ya kuanza kutekeleza mradi huo kitu ambacho hakijafanyika mpaka leo kwamba ilipaswa tuwe na reli ya Kusini ambayo itasafirisha chuma, tulipaswa tumalize barabara ya Madaba – Mkiu kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe na chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yake ni ya msingi na hata mazingira yetu ambayo tulitakiwa tuwe tumeyafanya hatujafanya. Kwa hiyo, hata wakisaini mkataba wa kuchimba kile chuma hawana baraba raya kusafirisha wala reli ya kubeba chuma. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashukuru leo naona kila point ninayokwenda mtu anaichangia namshukuru sana kwa point hizo ambazo ameenda nazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa Liganga na Mchuchuma, kulipa fidia lazima wananchi wa maeneo yale waambiwe, mwenye fedha ya kuwalipa wale wananchi ni nani ni mwekezaji au ni Serikali? Kama ni Serikali itoe maandalizi ya kulipa fidia kwa wananchi, kama ni mwekezaji tuwaambie wananchi kwamba sisi fidia hatutalipa mpaka mwekezaji atakayekuja hapa ndio atalipa ili wananchi wale wajue kinachoendelea pale. Sio wanakaa wanasubiri fidia, fidia, fidia kumbe inasubiri mwekezaji na mwekezaji anaweza kuja mwaka 2030 tumeshatoka humu Bungeni kwa hiyo, wawaambie wananchi kwamba nani anapaswa kulipa hiyo fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihame hapo niende kwenye viwanda vya Wilaya ya Bunda. Wilaya ya Bunda inaenda kuwa maskini kama ilivyokuwa huko nyuma kwamba sisi tulikuwa maskini kwenye Wilaya ya Bunda. Viwanda vilivyokuwepo Bunda kulikuwa na Kiwanda cha Kibara Ginnery, kuna S & C Ginnery, kuna Mount Meru Ginnery, kuna Olam Ginnery, kuna Mara Lint Ginnery, kuna Ushasi Ginnery, vyote vinaenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilikuwa viwanda vya pamba na Wilaya ya Bunda ndio inazalisha pamba nyingi kwa maeneo yote ya Mkoa wa Mara. Ndio eneo bora viwanda vimekufa, Kibara Ginnery imekufa, Ushasi msimu wa mwaka 2019/2020 Serikali tulilazimisha watu wanunue pamba kwa bei ambayo ni kubwa, wakasema yale makampuni yakinunua watapata refund kutoka Serikalini, hawakurudishiwa. Makampuni yamekufa, Olam ilikuwa inafanya kazi imefungwa, S & C inakwenda kufungwa, viwanda vingine Ushasi Ginnery imefungwa miaka mingi, Mara Lint imekufa, Bunda inaenda kuwa maskini ya mwisho katika Mkoa wa Mara na katika maeneo yote ya Tanzania. Kwa hiyo tuombe sasa Waziri…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa ya mwisho hiyo Mheshimiwa Ester.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa kaka yangu Boni mbali na mchango wake huo mzuri wa ginnery, lakini pia Mkoa wa Mara tuna kiwanda pale Musoma cha MUTEX, Serikali bado inashindwa ku-invest ili wakulima wetu wa pamba, mbali tu ya Mkoa wa Mara na maeneo mengine wawe wana uhakika wa soko. Lini pia Serikali itaenda kuwekeza fedha kwenye kile Kiwanda cha MUTEX. Nilikuwa nampa kaka yangu taarifa Mheshimiwa Boni.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante namshukuru sana Mheshimiwa Ester yuko sasa hivi nadhani amebadilika yuko vizuri sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza haya mambo, hatuwezi kuwa na Wilaya kubwa ambayo inazalisha pamba kwa wingi halafu viwanda vyote vimekufa. Kwa hiyo, Wizara ya Viwanda na Wizara ya KIlimo nadhani wakutane sasa waende waangalie vile viwanda msimu wa mwaka huu haijulikani pamba itauzwa wapi! Kwa hiyo, waende wakutane waone kiwanda kipi kama ni Mara Lint kama ni Kiwanda cha S & C wawalipe fedha waliyolipa ambayo wanadai Serikali, kama ni Olam wawalipe waliyokuwa wanalipa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vya mafuta, mimi hii nchi sijui ina miujiza mimi sielewi. Kama leo tuna alizeti ambayo tukiamrisha mwaka kesho au msimu unaokuja, kwa miezi mitatu tunauwezo wa kupata mafuta mengi na yakabaki ziada tukauza nje hatushughuliki nayo! Tunashughulika na michikichi iive baada ya miaka miwili, mitatu ndio ipatikane tunaendelea kuagiza mafuta kutoka nje.

Naomba Serikali tuwe tuna sehemu mbili, tuwe na long term kwa maana ya kupata viwanda vya mafuta na mazao ya mafuta kwa maana ya michikichi ambayo ni long term tutakuwa nayo, tuwe na short term ambayo ni alizeti ambayo leo Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda wakikubaliana kwamba wanatoa mbegu bora, wanasimamia masoko inapatikana kwa wakati na mafuta yanapatikana kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Kwanza niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Bunda na kwa bahati nzuri nina Kata saba, kwa hiyo, niwashukuru wapiga kura wa Nyamang’uta, Nyamswa, Salama, Mihingo, Mgeta na Hunyali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Wabunge wote nikiwemo mimi mwenyewe, hatua ya kufika hapa ni ndefu sana. Kwa kweli, Mwenyezi Mungu ametusaidia tumefika hapa wote, jambo la kwanza naomba tupendane, hii habari ya kushabikia vyama na kunyoosheana vidole itakuwepo, lakini iwe kwa wastani, kwa sababu wote tunaishi kama binadamu na tukifa au tukifiwa tunaenda kupeana pole, kwa hiyo tunapokuwa humu ndani naomba tupendane.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba Wabunge wa CCM wajue kwamba, nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumekabidhiwa sisi, hawa jamaa zetu wapo tu kwa kupinga na kupiga kelele. Kwa hiyo, tunatakiwa tufanye kila la maana kuwatendea haki Watanzania ili tunapofika 2020 hawa watakwenda kuuliza, tuliwaambia CCM hamuwezi sasa mnaona mmefanya nini? Kwa hiyo, tufanye kila la maana ili nchi yetu iweze kupata maendeleo ikifika 2020 tuwaoneshe kwamba tumefanya nini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais, sijui huwa najiuliza mara mbili mbili hivi kuna nini? Kwa sababu kabla ya mambo yote tunasema nchi inaliwa, nchi mbovu, hali mbaya, tunalia kila mahali, leo tumepata jembe, tingatinga anapiga kila upande bado watu wananung’unika nini? Hivi nchi hii tusipopata Rais nje ya Magufuli tunapata Rais wa aina gani? Kilichobaki ni kusahihishana tu pale na hapa mambo yanakwenda sawa, lakini Rais anafanya kazi nzuri sana.nn(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye utawala bora. Katika utawala bora naangalia mafunzo ya Halmashauri za Vijiji, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata. Tumekuwa na tabia ya kuchagua viongozi halafu hatuwapi mafunzo, hata humu ndani Wabunge tumo tu, hatukupata mafunzo bora, juzi nilikuwa namuuliza mwenzangu hapa, hivi maana ya mshahara wa Waziri ni nini? Ananiambia na mimi sijui! Unashika mshahara wa Waziri, mshahara uko benki wewe unaushikaje? Anasema sijui. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulitakiwa kuelezwa kwamba hivi vitu vinakwendaje, kuna Vote, kuna sub-vote, kuna program tulitakiwa tupewe mafunzo. Mafunzo kwa Watendaji wa Vijiji ni jambo la msingi sana, lakini imezungumzwa hapa habari ya Wenyeviti wa Vijiji kulipwa mshahara au kupewa posho. Serikali za Halmashauri au Halmashauri za Wilaya haziwezi kutoa posho, hilo tukubaliane!
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote tumetokea maeneo hayo, tumetoka kwenye vijiji, tumetoka kwenye Kata tunakuwaje hatuwatetei watu hawa wapate posho nzuri? Tunapaswa kufanya kila namna Watendaji wa Halmashauri za Vijiji, Wenyeviti wa Vijiji wapate posho nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo nizungumzie habari ya migogoro ya mipaka. Kuna migogoro ya mipaka ya Wilaya na Wilaya, kuna migogoro ya mipaka kati ya Kata na Kata, kuna migogoro ya mipaka kati ya Vijiji na Vijiji na ni mingi sana, kwenye Jimbo langu ipo katika kila eneo. Tunaomba Wizara zinazohusika na maeneo hayo, TAMISEMI na Ardhi washirikiane kumaliza migogoro hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Shule za Msingi, jambo ambalo Bunge la Kumi na Moja tutafanya na tutapata heshima ni kupata madawati ya watoto, madawati ya wananfunzi katika shule za msingi. Ukienda shule ya msingi ukiingia darasani watoto wanaamka wanakusalimia shikamoo mzazi, unasema marahaba, halafu unawaambia kaeni chini au unafanyaje? Wanakaa kwenye vumbi! Huwa najiuliza, naomba Waziri Mkuu afanye kazi mmoja, tufanye kazi moja au kazi mbili tu na nitoe njia. Kwanza, tukubaliane kwamba Bunge hili Bajeti yoyote kutoka Wizara mbalimbali ikatwe tupate bilioni 150 za kuweka madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepiga hesabu hapa yamepungua madawati 1,500,000 kama milioni nne, kwa hiyo, tukipata bilioni 160 au 170 maana yake madawati nchi nzima yanakuwepo. Waheshimiwa Wabunge tukitoka hapa tutakwenda kupambana na tatizo la madawati hamtakwepa, saa hizi kuna meseji zinazotoka kwa DED ooh! Mheshimiwa Mbunge hela yako ya Mfuko natengenezea madawati, nani kakutuma utengeneze madawati mimi sijafika huko?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tukubaliane kwamba madawati ni jambo la kwanza katika Bunge hili. Tutoke humu tujue kwamba tunakwenda kupata madawati nchi nzima, tukisema hii ya Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa tumetofautiana kipato katika Mikoa. Dar es salaam watatengeneza, Arusha watatengeneza, Bunda je, ambayo ni Wilaya ya maskini? hawawezi kutengeneza madawati! Kwa hiyo, nafikiri kwamba jambo la msingi sana kufanya mambo kama haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kama hatuwezi kuweka bajeti bilioni 160 kutoka Wizara mbalimbali, tukubaliane na Waziri Mkuu aunde Kamati ihusishe Kambi zote, Kamati itafanya kazi moja ya kujua idadi ya madawati nchi nzima, lakini kujua mashirika mbalimbali. Kwa mfano, tukasema hivi ukiweka shilingi tano katika Makampuni ya Simu, ukiweka shilingi tano kwa Makampuni ya Mafuta, ukiweka taasisi mbalimbali tulizonazo, hatuwezi kupata bilioni 160? Inawezekana! Waziri Mkuu aunde Kamati ili tuweze kupata watu, wafanye tathmini, watuletee hapa, wote tuchange.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Bunge letu limechanga, tumechanga bilioni sita au uwongo jamani?
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, tumechanga bilioni sita kutokea Bungeni humu ndani, tunataka Mashirika mengine yote na Taasisi zingine zichange.
Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo yangu kwa leo yalikuwa hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie hoja hii ya Wizara ya Nishati, binafsi nimefurahi kumuona Senator wetu Mheshimiwa George Mkuchika kwa kweli tuwe wakweli mwanadamu ni roho tu kama roho zetu zipo salama tunatakiana mema humu ndani, tunatakiana mema kwenye roho, roho tu ndio Mungu anaitaka iendelee kuwepo hiki kiwiliwili ni cha hapa hapa duniani lakini roho ni ya Mungu ikiendelea kuwepo tunashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niipongeze Wizara ya Nishati wanafanya kazi nzuri sana sana. Wizara hii sisi ambao tulikuwa wabunge wa CCM tulikuwa tunatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kusema kweli sehemu kubwa ya vijijini ya utekelezaji wa Ilani hii Wizara ndio imetekeleza, kura nyingi tulizozipata katika CCM kwa utekelezaji wa Ilani ni pamoja na hii Wizara ya Nishati, na hasa mradi wa REA vijijini kwa hiyo mradi wa REA vijijini ni muhimu sana Wizara imefanya kazi lakini Waziri wake na watumishi wengine wote na Naibu, ila tunamfahamu Waziri zaidi kwa sababu tumekaa naye muda mrefu kidogo nidhamu yake haina mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haina kabisa katika watu wanaotaka kupewa nidhamu baadhi ya Mawaziri wanaotaka kupewa nidhamu kwa utendaji na kwa kumpigia simu na kupokea na kunyenyekea na kufanya kazi huyu bwana anafanya kazi kweli sio utani. Anafanya kazi nzuri sana. Sasa niombe, kwamba huko tunakokwenda huko mbele mimi naona kama Wizara imekuwa na shughuli nyingi mno na hili unaweza kulisimamia hii Wizara inapokwenda nimesikia juzi tunatafuta mafuta, kutafuta mafuta ya kuchimba baharini ashughulike Mheshimiwa Dkt. Kalemani Bomba la kutoka Uganda lije Tanzania Mafuta ashughuliye huyo huyo, gesi inayotoka NLG aende yeye sun NLG wanaiita aende yeye wewe msukuma acha, bwawa la Mwalimu Nyerere aende yeye ashughulike sijui na vinasaba na mafuta kutoka Bandarini yeye. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naona tufanye kama wenzetu tuwe na Wizara mbili Wizara ya maendeleo ya Nishati na Wizara ya Maendeleo ya Petrol kwani kuna shida gani kama hizi Wizara zina fedha za kutosha mambo ya mafuta ni mabilioni ya fedha, mambo ya umeme yajitegemee hivi leo umeme unakatika kila mahali, umeme wa REA hauendi Kalemani ataendaje Bunda, ataendaje Kongwa ataendaje huko wakati wamembana kwenye mikataba ya kwenda Uganda, kusaini Mikataba, tukubaliane Mheshimiwa Rais alione hili tutenganishe hii miradi ya kimkakati iwe na mtu mwingine na hii mradi ya umeme ibaki na watu ambao tunashughulika nao kila siku.

Mheshimiwa Spika, wananchi wanataka kuona umeme habari ya kuchimba mafuta, habari sijui ya gesi inatoka kwenye mabomba ipewe mtu mwingine kuna shida gani, tuliangalie hilo naona sasa tukiliona hilo vizuri nchi yetu itaenda kwenye jambo la namna hiyo. Nimshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri jana nimemuona kule Sokoni anahangaika na matatizo ya wananchi, amesimamia vizuri bomba la mafuta la kutoka Uganda ule ni mradi wa kimkakati wa muda mrefu lakini wenye faida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamezungumza Wabunge wengi hapa ushauri wangu kwenye huu mradi Wabunge tuelimishe kuhusu huu mradi, huu mradi una mikataba mitatu mimi leo nikiambiwa mradi ule unafanyaje nitasema utapata ajira nyingi, utafanya nini lakini sijaelewa mikataba ya miradi hiyo ikoje. Kwa hiyo, Wabunge tuelimishe juu ya mikataba mitatu ya huu mradi ukoje, unafanyaje tupate Semina ya kutosha ili na sisi tueleze faida ya mradi huu itaendaje kwenye shughuli za kila siku huko mbele tunapokwenda.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la vinasaba sasa ninashindwa kuelewa wakati fulani ukisoma hadithi au ile tips za wakubwa wale watu waliokuwa wanatafuta uhuru akina Stephen Biko, anakwambia akili ya mwanadamu, akili ya mtu anayedhulumiwa yaani mtu anayedhulumiwa ili ajielewe anafanya kazi gani ya kudhulumiwa umpe akili wala usimpe silaha. Sasa ninashindwa kuelewa vinasaba ni nini, vinasaba ni vitu ambavyo mtu ameleta ili kutibu tatizo na nchi hii inaweza kuendeshwa bila vinasaba lakini leo kuna watu wamejipanga vinasaba vinasaba vinasaba.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema jambo moja vile vinasaba sasa hivi vinatozwa shilingi 14,000 mafuta yanayoingia nchini, mafuta tunayotumia sisi ni mafuta yanayotumika hapa nchini ni bilioni 14 ukizidisha na 14 ni bilioni 56 matumizi yake yakitoka super profit ni bilioni 40.

Mheshimiwa Spika, kwanini watu wasiseme kwanini wati doubt bilioni 40 unaipeleka wapi? Kwa hiyo niseme kwamba TBS inauwezo wa kupima ubora wa mafuta lakini haina uwezo wa kuweka vinasaba mambo ya ajabu duniani hapa ubora wa mafuta TBS inauwezo wa kupima lakini kupima kuweka vinasaba haiwezekani vitu vya ajabu sana hapa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninajiuliza madawa yanayotumika hapa nchini, madawa ya wanadamu sisi tunatengeneza hapa si tunaagiza yaani kuagiza madawa ya kutibu wanadamu hapa nchini ni jambo dogo kuliko kuagiza vinasaba, mambo ya ajabu hapa duniani hapa, mambo ya ajabu sana hapa tunaagiza mbolea tunaagiza madawa tunaagiza kila kitu tunafanya operation za binadamu vinasaba ni kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe nishauri niombe vinasaba visimamiwe na TBS na TBS wachukue shilingi saba kwa sababu vile vinasaba ni shilingi nne unaweza ku-handle, shilingi saba nyingine ije TARURA tunahangaika hapa na mambo ya TARURA mambo ya Barabara na mambo ya nini tuna hela zipo hapa…

SPIKA: Mheshimiwa Getere nilichokielewa so far kwa sababu niko nawasikiliza wote wanasema hawa waliochangia kuhusu kinasaba mpaka sasa wanasema kuipa TBS sio tatizo ila tunajukumu sisi Wabunge wa kuirekebisha sheria ya TBS kwa kuwaongezea hilo jukumu ndani ya sheria, ili wafanye kisheria jambo ambalo nafikiri tumuhimize Waziri endapo linakubalika ili sasa lifanyike hilo ili TBS wafanye ndicho nilichoelewa endelea tu lakini kuchangia. (Makofi)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante, nadhani hii suala la sheria hivi ngoja nikuulize sisi wote ni Wabunge hapa na wewe ni Mbunge hapa hivi tulipoamua kununua ndege tulileta sheria gani? Si tulileta ndege zikawepo,

Mheshimiwa Spika, mimi ninachokisema umezungumza vizuri sheria ziletwe wakati huo TBS iendelee ku-handle kwa sababu wale watu hawana mkataba TBS iendelee kuwa nalo hilo eneo wakati sheria zinafanya nini, zinaletwa shida iko wapi? Tusiwe watu wa kunyonywa mimi mambo ya kunyonywa ndio siyapenda humu ndani, tuhangaike kwamba hili neno linaendaje ili liweze kuleta mahusiano yetu kwenye mambo kama haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani umeshauri vizuri sheria iletwe haraka, lakini wakati huo huo TBS iendelee kufanya hiyo kazi kwa sababu jamaa wale hawana Mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninazungumza kukatika kwa umeme wa REA sasa mimi nashindwa kuelewa ni umeme wa REA ndio unakatika au Umeme mwingine ya mjini haukatiki, kwasababu vijijini umeme wa REA unakatika mara 10 kwa siku shida ni nini kama sisi tunaumeme wa kutosha wa megawatt za kutosha katika nchi hii leo shida ni nini umeme unakatika mara kumi kuna watu hawafanyi kazi shinda inatokea wapi kwenye jambo kama hili. Kwa hiyo, ndio maana nimesema hii Wizara tuiangalie upya tuweze kuigawanya ili iweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine nililotaka kuzungumza ni suala la mradi wa mikakati tuna bwawa la Mwalimu Nyerere tuna mradi SGR suala zuri duniani ambalo Marehemu Dkt. Magufuli tutamkumbuka miaka nenda rudi ni kwamba bwawa la Nyerere mradi ule unaendeshwa kwa Mkopo ambao hautulazimishi kuchukua bwawa wenzetu wa nchi jirani miaka ya karibuni hivi inayokuja miradi mingi ya mikakati itakuwa ya watu Zambia tayari na maeneo mengine tayari, lakini bwawa letu la Nyerere na niombe kwa style mliyotumia ya kukopa kwa fedha ya hiyari tusiingie tena watu waje kuleta uhifadhi yaani kufadhili ile Rambo lile bwawa la Nyerere halafu liwe la watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hilo ndio jambo, marehemu amefanya jambo kubwa sana kwamba mradi ule sasa hata ukiisha madai yake sisi hatudaiwi kwa nguvu, tutadaiwa kwa hiyari, na hivyo hivyo kwenye reli wenzetu wanaojua miradi ya namna hiyo ya mikakati huko mbele sio yao itakuwa ya watu kwa hiyo ninafikiri kwamba tuendelee kufanya na mimi naona Mama amejitahidi sana kuwa karibu na Miradi ya Mikakati tumuombee Mungu aendelee kuilinda miradi ya mikakati ili nchi yetu iende salama, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa mambo mengi tu, lakini nimkumbuke aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli. Kama huko aliko duniani na huku nje mambo yakaharibika sisi tutamlaumu yeye aliyetuachia watu wazuri kwenye safu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Magufuli alikuwa utatu mtiifu, Wakristu msinielewe vibaya nikasema Utatu Mtakatifu, utatu mtiifu. Wa kwanza ni huyu Rais wetu wa sasa ambaye alikuwa Makamu wa Rais, Mama Samia, ndiye aliye wa kwanza kwake. Wa pili alikuwa naye Waziri Mkuu ambaye bado anaye Rais wa sasa. Makamu wa Rais wa sasa alikuwa Waziri wake wa Fedha ambaye naye yupo. Hivi nchi inayumbaje, nchi ambayo Magufuli ameiacha kwenye watu waliokuwa utatu wake mtiif inaachaje? haiwezi kuacha. Kwa hiyo mimi naamini katika hili tunaloendanalo nchi itaenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme maneno, na kwa maneno haya msini-quotet mkasema sasa wewe mgombea ukamishna, a’ a’, ni maneno yangu. Nchi yetu inatakiwa iwe na watu watakatifu, watu wakumuogopa Mungu, watu wasio na mapenzi ya kujipendekeza kumbe roho zao zipo tofauti. Wakitokea watu wa namna hiyo na Mama Samia ambaye sasa ni mtiifu wakati wote nchi itakwenda salama; lakini kama kuna watu wala rushwa, watu wabadhilifu watakao mzunguka mama akiwa kwenye jukwaa wanampamba huku ndani wanafanya mambo mengine nchi itakwenda chini.. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niseme tumuombe Mungu, watakatifu mawaziri wake wote wafuate watu wale watatu ambao Hayati Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alituachia. Alituachia Makamu wa Rais ndiye amekuwa Rais wa sasa, alituachia Waziri Mkuu bado yupo na anafanya kazi, yaani huyu si wa kusema tena. Hivi nchi inawezaje kwenda nje ya Majaliwa? haiwezekani, nchi inawezaje kwenda tofauti na Mpango? Haiwezekani. Kwa hiyo tuwaombe viongozi wetu, mawaziri wetu na viongozi wote wawe watiifu, roho zao ziendane na wanavyosema kwenye majukwaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi inanishangaza sana kumuona mtu yupo jukwaani anazungumza mambo mazito, lakini huku chini ana mambo ya ajabu sana, mla rushwa mkubwa, kwa nini sasa inakuwa hivyo? Tuombe watu wetu Mungu awasaidie waende upande ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili nalizungumza polepole maana hili lilikuwa la nchi. Nilikuwa naangalia PAYE ile kodi ambayo inalipwa na watumishi wa Serikali. Waheshimiwa Wabunge nataka hili mlielewe vizuri. Tuna madaraja manne ya PAYE. Daraja la kwanza ni wale watu wa 270 mpaka 540 ambao wanalipa asilimia tisa, maana yake ikipunguzwa sasa itakuwa asilimia nane. Daraja linalofuata ni 540 mpaka 740, hawa wanalipa asilimia 20, ikipunguzwa itakuwa asilimia 19. Daraja linalofuata ni 740 mpaka 1,000,000, hawa wanalipa asilimia 25. Daraja la mwisho ni kuanzia 1,000,000 na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge nimesikia watu wengine wanazungumza huko mitaani kwamba Wabunge wanazungumza haya mambo hawalipi kodi; jamani, hii Pay As You Earn maana yake makundi yote sisi ndio tunalipa. Mbunge analipia milioni moja na kitu kwenye makundi yote. Kwa formular hii kundi la kwanza litalipiwa na kundi la pili, kundi la pili litalipiwa na kundi la tatu, kundi la tatu litalipiwa na kundi la nne, kwa hiyo sisi Wabunge makundi yote tunayalipa hela. Sisi ndio tuna kodi kubwa katika watumishi wa Serikali ambao wanalipa Serikalini hapa, kwa hiyo tuseme kwamba tunalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nilikuwa na ombi langu hapa, Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba unisikilize hapa kidogo. Mimi naona badala ya kupunguza asilimia moja ya hii kodi hili kundi la kwanza la 270 mpaka 540 tuliondoe, tuliondoe hilo kundi lisilipe kodi kwa sababu ukipiga hesabu yake ni kama bilioni saba au bilioni nane. Tuliondoe tubaki na kundi la pili na kundi la tatu na kundi la mwisho ili hawa ambao wana hela kidogo waendelee kupata kidogo waendelee kuishi. Kwa hiyo ushauri wangu kwa hapo nilikuwa naona hapo inakuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie TRA; na Mheshimiwa Mwigulu kama ni jambo la kutufanyia sisi Watanzania ili tukukumbuke masaa yako yote ni kuangalia mfumo wa TRA kwa sababu mfumo wa TRA si rafiki kwa kukusanya hela, mfumo wa TRA unakupa nafasi ya kwenda kukadiria. Mimi naleta makontena ya bilioni tatu halafu tunakubaliana sasa nilipe ngapi. Mimi ninaduka unakuja kunipigia mahesabu ya bilioni mbili, milioni 500 au milioni 100 au bilioni 50 tunakubaliana nilipe ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tutafute mifumo mizuri ya TRA ili hela zetu ziweze kupatikana, vinginevyo hakuna hela tutakayokusanya hapo. Kwa hiyo tuangalie mifumo ya TRA kwenye maduka, kwenye bandari na kwenye maeneo yote tuweze kuona kwamba tunaifanye mifumo hiyo ili tuweze kuishi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kodi ya majengo. Mimi hii kodi kwangu naona kama ni jambo gumu sana, na hasa kwa watu wa vijijini. Naiomba Serikali, Mheshimiwa Mwigulu wewe ni mtaalam wa hesabu hizi. Hii kodi wala msiipeleke kwenye umeme huko, hii kodi pelekeni kwenye Wizara ya Ardhi. Mtu mwenye kiwanja mumuongezee kakodi hako alipe, si ni mali yake, kuna ubaya gani? Hii kodi msiipeleke popote ipelekeni kwenye Wizara ya Ardhi walipe kupitia Wizara ya Ardhi, mimi nadhani hapo itakuwa nzuri zaidi kwenye upande huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie Deni la Taifa. Deni la Taifa ni himilivu, na tunasema ukiangalia nchi ambazo ni ten bora zenye madeni makubwa ni pamoja na Tanzania, ni ya kumi. Ni kweli tuna deni kubwa, lakini kukopa si dhambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi tajiri duniani ni Marekani, lakini nchi yenye madeni makubwa duniani ni Marekani. Sasa sijui kama watu mnaliona hilo, nchi tajiri duniani ni Marekani na nchi yenye madeni makubwa duniani ni Marekani; kwa hiyo kukopa si dhambi, mimi nafikiri tunakopa kufanyia nini ndiyo hoja. Kwamba tunakopa kulipa mishahara, tunakopa kufanya vitu ambavyo havina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nishauri kwenye Serikali hii ya Awamu ya Sita, Mama asiogope kukopa, akope kwenye malengo maalum. La muhimu hapa sana ninachoomba ni kwamba sisi Wabunge sasa ufike wakati tupewe taarifa, kwamba tumekopa wapi na tunadaiwa wapi, na hili deni tunalipa lini na likoje. Ije taarifa rasmi hapa Bungeni tujue tunadaiwa kiasi gani na tunadai kiasi gani na nani anatudai, tujue ili sisi Wabunge tuwaeleze watu huko, kwamba deni letu ni himilivu, lakini tunadaiwa na watu fulani, lakini kukopa si dhambi; kwa sababu hakuna kitu kinaitwa good debt, madeni yote ni mabaya hakuna deni zuri, hata sisi madeni yetu ni mabaya tu hakuna deni zuri hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie mifumo ya usimamizi wa fedha za bajeti zetu, na hapa ndipo patamu. Kuna watu wanaitwa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Ma-DAS, Makatibu Tarafa, Wakurugenzi, Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji; ni nani anasimamia vizuri miradi inayopelekwa kwenye Vijiji huko na kwenye Kata? Ni nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana. Akienda Naibu Waziri kwenye Wilaya anakutana na Mkuu wa Mkoa, anakutana na Mkuu wa Wilaya. Kama kuna hela zimeliwa kwenye Wilaya hiyo Mbunge analalamika, Wananchi wanalalamika, Waziri aliyeenda pale kama ni Naibu au Waziri wa Wizara analalamika, Mkuu wa Mkoa anamwambia Mkuu tuachie hilo tutatekeleza, mwaka wa kwanza. Anakwenda pale Waziri Mkuu mradi ule ule kwenye sehemu nyingine umeliwa, Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wanamwambia tuachie Mkuu hilo tutatekeleza. Sasa najiuliza, hivi nchi yetu imekuwa ya kurugenzi ya matukio?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi inatokeaje mkoa au wilaya fedha zinaliwa milioni moja, milioni mbili, milioni mia tatu, milioni mia nne, kila siku tunapoenda kwenye mikoa na wilaya kuna madeni na kuna hela zimeliwa, Wakuu wa Wilaya ukikutana nao wanakwambia mkuu tuachie, tunatekeleza mkuu tuachie tunatekeleza, watamaliza lini? (Makofi)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe taarifa mchangiaji, hapo anapoongea ni penyewe sasa, maana tunapitisha bajeti nyingi kubwa lakini ukiangalia kiuhalisia hela zinaliwa na hakuna mtu anayefungwa. Nilikuwa napenda kumpa taarifa mchangiaji yupo vizuri sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea taarifa hiyo.

MHE. BONIPHACE W. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Unajua humu ndani tupo tofauti, wapo Wabunge wanaoishi kwenye lami huko na kuna Wabunge tunaishi vijijini, sisi wa vijijini ndio tuna shida. Hivi Mbunge kama mfano Mheshimiwa Zungu, Mwenyekiti wetu ana shida gani kule, kule atazungumza watu wake tu wakawaida wale, lakini ukiangalia magorofa yamejaa, lami imejaa, kila kitu kimejaa; umeme upo vizuri, atazungumza mambo mengine yapo ya kibinadamu lakini si kama ya kwetu vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mfumo wa utendaji wetu ukubalike ili Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wawe na mikataba. Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ambaye eneo lake lina wizi, lina ubadhilifu watuambie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tukawe na Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Watendaji wa Kata, Makatibu Tarafa, Ma-DAS, Ma-RAS miradi inaliwa wapo, ukienda mkuu tuachie, ukienda mkuu tuachie, wanamaliza lini?

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpe taarifa kaka yangu ninaye mheshimu sana, Mheshimiwa Getere. Siyo nchini kote Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wanafanya ubadhilifu. Mimi kwa Wilaya ninayotoka, ya Ikungi Mkuu wetu wa Wilaya Mpogoro pamoja na Mkurugenzi wake Kijazi wanafanyakazi iliyotukuka ambayo hata Waziri Mkuu alipokuja kwenye ziara ndio moja ya wilaya alizisifia ambazo hazikuwa na makando makando katika utendaji. (Makofi)

Kwa hiyo, tunapowazungumza kwa u-general tuwatendee haki baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi ni waadilifu sana na wanaitumikia nchi kwa moyo wa uzalendo sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita malizia dakika yako.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mtaalam amezungumza, mimi nimezungumza toka awali hakunisikia, nimesema baadhi, labda Kiswahili cha kikurya hukusikia vizuri. Kwa hiyo, mimi nataka niombe kusema hivi, unajua tunavyozungumza uhalifu wa jambo tunazungumza in terms of average. Kama tuna watu Wakuu wa Mikoa 100 wanaofanya vizuri au kwa mfano sisi Wabunge tuulizwe kwenye Majimbo yetu ni Wabunge wangapi wana miradi iliyoliwa? Wataweza kunyoosha juu Wabunge hapa, miradi ambayo ipo ambayo haitekelezeki ni mingapi? Hivi tujiulize swali, Mtendaji wa Kata akiamka asubuhi anaenda wapi? Ana ratiba gani, Katibu Tarafa anaenda wapi? Tutengeneze utaratibu ambao mtu akiamka asubuhi kama ni mtumishi wa Serikali ana kazi ya kufanya, anaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hilo nataka nikuambie tukitengeneza mfumo mzuri, maana yake Serikali yetu itaenda vizuri. Kila mtu atakuwa anaamka na kitabu tuwe tuna-search umeenda kufanya kazi gani leo? Leo tuna wale maafisa ugani anaweza kuishi Dodoma, anakaa Singida. Tunataka kuwajua asubuhi wanaamka wanaenda wapi? Kazi gani wanafanya? Watoe taarifa ya kila siku wanafanya kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti: kwa hiyo, mimi nilikuwa nafikiri kwamba niunge mkono.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nizipongeze hizi Kamati tatu za PAC, LAAC na PIC na nimpongeze CAG wote kwa pamoja ametuonesha njia ya kupita na njia ya kusemea.

Mheshimiwa Spika, nakuwa na maneno magumu sana ya kusema lakini hata lugha ya kutumia naikosea, sijui nitafanyaje, yaani najiuliza maswali mengi sana kwamba hivi hizi nyimbo tunaimba tunamwimbia nani? Yaani tunaimba ili iweje?

Mheshimiwa Spika, nitatoa ripoti baadaye kwa kutumia mfano wa halmashauri yangu, lakini najiuliza wewe unasoma na sisi tunasoma vitabu kwamba, kazi ya Mbunge ni kuishauri Serikali, sasa na wewe ni mtaalamu wa sheria utakuja uniambie tukishauri, tukishauri miaka thelathini tunafanyaje, yaani sisi kazi yetu ni kuishauri Serikali sasa tumeshauri,tumeshauri,tunafanyaje? (Makofi)

SPIKA: Wacha nikusaidie, kazi yetu siyo tu kuishauri Serikali; kuna muda wa kuishauri Serikali, kuna muda wa kuisimamia Serikali. (Makofi)

Wakati tutakapokuwa tunajadili Mpango yale mapendekezo ya Mpango, tutakuwa tunaishauri Serikali, wakati huu wa kujadili ripoti ya CAG tunaisimamia Serikali. Kwa hiyo kama kuna jambo limeshauriwa, likashauriwa, likashauriwa, wewe umeliona ambalo unaona Bunge lifanyie maamuzi fulani ndio wakati wako huu. kwa sababu Serikali kwenye jambo hili na wao watakuwa wachangiaji kama mwingine, yaani haya yote yeliyosemwa na Kamati, yanayosemwa na Wabunge hapa watakaokuja kuhitimisha hoja ili Bunge lifanye maamuzi ni Kamati zetu, kwa maana ya Wenyeviti. Kwa hiyo saa hizi tunaisimamia Serikali, kwa hiyo endelea na mchango wako, hatushauri tu tunaisimamia pia. Karibu.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante, umenipa ufafanuzi mzuri. Sasa nitoe mfano wa Halmashauri ya Bunda ambayo ukienda kwenye chati ya kwanza kabisa kwenye jedwali la kwanza la ripoti hii ya LAAC, ni halmashauri moja tu kati ya halmashauri 184 yenye hati chafu ambayo ni hati mbaya. Sasa juzi wakati LAAC inaendelea nilienda kwenye Kamati ya LAAC nikakuta kwenye ile ripoti ya Kamati ya LAAC wameandika Bunda imepata hati isiyoridhisha, nikajiuliza mbona CAG amesema ni hati mbaya? Mkaguzi aliyekuja kutoka Ofisi ya CAG akaniambia kwamba hiyo hati mbaya hatutumii, tunatumia lugha nzuri ya kutoridhisha, lakini ripoti ya CAG nimeisoma na ripoti ya Kamati nimeisoma imeandika Bunda hati mbaya. Sasa najiuliza ukaguzi wa CAG wanaenda kule halmashauri, wanakuta mambo mabaya, wanakuja kwenye Kamati halafu wanaanza kulemba, hiyo nayo hapana. Kwa hiyo tuache, kama mambo ni mabaya ni mambo mabaya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilitaka nitoe mfano…

SPIKA: Mheshimiwa Mbunge wa Bunda, acha nikusaidie, siyo hati mbaya ni hati chafu ama inaitwa mbaya? Ama mbaya na chafu ni sawa? Hii inaitwa hati chafu na ndiyo ilivyoitwa huku, ndiyo inavyoitwa huku, kwenye taarifa, ni hati chafu maana mbaya na chafu ni vitu viwili tofauti. Endelea.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, sasa sitaki kwenda kwenye hiyo lugha kwa sababu nimesoma ripoti ya CAG imesema hati mbaya, nimesema ripoti ya LAAC imesema hati mbaya iliyoko hapa sasa hivi, kwa hiyo Kiswahili tuachane nacho tuendelee na ambayo nataka kusema mimi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, 2000 ni majedwali hapa nasema utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi miaka iliyopita 2012/2013, ripoti kama hii ilienda Bunda kukawa na hoja moja ya kujibiwa, haikujibiwa 2012/2013. Mwaka 2013/2014, hoja moja haikujibiwa; mwaka 2014/2015 hoja mbili hazikujibiwa; mwaka 2015/2016, hoja moja haikujibiwa; mwaka 2016/2017, hoja tatu hazikujibiwa; mwaka 2017/2018, hoja mbili, ikajibiwa moja; mwaka 2019/2020, hoja kumi na tisa, zikajibiwa tisa; jumla kutoka miaka yote hiyo tuna hoja 27 Bunda. Tukitoka hapo wanasema hati ya ukaguzi zilizotolewa miaka mitatu iliyopita, mwaka 2018, hati isiyoridhisha; mwaka 2019, hati yenye mashaka; mwaka 2020/2021, hati isiyoridhisha.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kujenga hoja yangu kutokea hapo, kwamba sasa tukisoma ripoti za 2012/2013, 2013/2014 na 2014/2015, zote zina ushauri wa CAG na Wabunge na matatizo yako palepale. Sasa niseme tuchukue uamuzi mgumu sasa tuseme, kwa ushauri huu sasa, kabla sijaenda Bunda, tuseme hivi katika hoja za LAAC na PAC, Bunge liseme hivi idara yoyote, wizara yoyote, taasisi yoyote ya umma ambayo haikutekeleza maagizo ya CAG na Wabunge mpaka tarehe 30 mwezi wa bajeti zao tusipitishe, si ndio tunasimamia au tunasemaje sasa, kwa sababu sasa tunamwambia nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme maneno mazuri hapa, kwamba CAG anaenda mbele ya Rais, anasema maneno mazito mazito umma unasikiliza, rais anatoa maelekezo tunasema vikao vya PAC na LAAC vitaangalia. Vikao vinakuja vinaangalia, vinaleta ushauri hapa, tunatoa ushauri miaka inapita, tunatoa ushauri miaka inapita, tunatoa ushauri, miaka inapita, ni lini sasa tutafanya maneno ambayo wananchi wanaweza wakasema tumechukua hatua.

Mheshimiwa Spika, naomba kwenye Bunge hili tuchukue hatua, ndiyo maamuzi yangu, popote ambapo kuna fedha imeliwa, ukisoma fedha zilizoliwa katika idara mbalimbali ni kichefu chefu. Watoto wetu hawana madawati sasa hivi, watu wanalilia shule za msingi kuna maboma, bado tuna matatizo ya maji, tuna matatizo mengi, tunamhurumia nani anayekula fedha za umma? Kwa nini watumishi wa Serikali wa Tanzania hawaogopi hela ya umma? Wenzetu waliotutawala hapa juzi tu, siyo tu kula hela ukisema uongo Bungeni umeondoka, ukileta kabajeti hakana faida umeondoka, hapo uongee nini sasa? Sisi watu wanaokula hela ni walewale, wanaokula hela ni walewale, wanaendelea tu, kuna nini kinaendelea hapa? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa niende Bunda, Bunda nimekwenda kwenye LAAC, bahati nzuri Mwenyekiti aliyekuwepo ni aliyekuwa anaongea hapa, ukienda kwenye zile fedha za ile 4.4.2 haikwenda 41,461,000,000. Ukienda kwenye 20% za vijiji kurudishwa kwenye maendeleo 11,465,000,000 haikwenda; ukienda fedha za maendeleo 260,000,000 hazikwenda; ukienda fedha mbichi 96,000,000 zimeliwa kabla hazijaingia benki; tumepewa 1,000,000,000 na mama ya kujenga Halmashauri ya Wilaya, 626,62,000 wamepewa wazabuni, hawajaleta vifaa, yaani wamepewa tu nenda mkanunue, nenda mkanunue, bila ukaguzi wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, LAAC imeomba kwenda Bunda, naomba uwape ruhusa waende, wasimamie watakuletea madudu. Leo tunapozungumza hapa mama ametoa fedha 467,000,000 kwa sekondari mbili, karibu milioni mia sita na kitu, wamekwenda kwenye kiwanda cha dragoni, wamenunua bati moja 69,140 badala ya 52,000 tumeenda Madiwani, tumekwenda mpaka tumepata vielelezo vyote vya kutosha, tukawaambia watumishi rudisheni hela, hawajarudisha wanasema eti TAKUKURU imechukua taarifa inapeleka. Hivi hizi hela za umma zitaliwa mpaka lini?

Mheshimiwa Spika, leo ukimwambia mwananchi wa kawaida kwamba fedha yake ya hospitali imeliwa shilingi laki moja ni tofauti na kumwambia bandari imekula 30,000,000. Wananchi wanapopelekewa fedha na mama inawauma sana kuliwa kwa sababu miradi yao haitaenda. Sasa hivi vitu tunafanyaje kweli kama tuna Mawaziri, tuna nani, tunafanyaje? Hivi kweli tunamlilia nani kila siku hii Serikali? Mimi si nimwombe mama aniteue hata Waziri wa TAMISEMI jamani hata siku moja? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hivi tunafanyaje sasa vitu vinaliwa vinaenda tunaangalia kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ya kwangu ndio hayo machache tu. Ahsante. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushuru kwa kunipa nafasi hii, namshukuru Ndugu yangu Mheshimiwa Lukuvi; Mheshimiwa Mabula ambaye ni jirani yetu Kanda ya Ziwa. Tumshukuru Rais kwa kuwapa nafasi hiyo, mnafaa kupewa nafasi hiyo na Mungu awasaidie muweze kutongoza vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti,nimeangalia taarifa hizi za Kamati ya Ardhi na Kambi Rasmi ya Upinzani wamesema vizuri sana. Wametofautiana kitu kimoja tu, hawa waCCM wameunga mkono, wale wa upinzani wameunga mkono kwa kushauri kwamba Serikali ikae pamoja itatue migogoro, jambo zuri sana.
Namshukuru rafiki yangu wa Bukoba Town na leo ni mnada, kwa hiyo, tutajua namna ya kufanya huko. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye mambo muhimu na naomba niulize maswali ambayo natakiwa wakati unakuja hapa ku-wind up uweze kuyatolea ufafanuzi. Ni nani anapima mipaka kati ya vijiji na hifadhi za wanyamapori? Kama ni Wizara ya Ardhi inapima, inakuwaje mpaka huo buffer zone moja iwe na kilometa kadhaa na buffer zone nyingine au kutoka mpaka wa wanyamapori kwenda kwa binadamu ni nusu kilometa; lakini kutoka mpaka wa wananchi kwenda porini ni zero. Nani anapima mipaka hiyo na kwa upendeleo gani wa aina hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanapima wataalamu wa wanyamapori, kweli wanaweza kutenda haki? Mipaka ya Jimbo langu la Rubana, kwa Mto Rubana, ukiingia mtoni, ukivuka tu, umekamatwa. Ukivuka mto tu, umekematwa; lakini wao kutoka mpakani, mita 500 ambayo ni nusu kilometa. Kwa hiyo, ina maana mita 500 hizo kama kuna mazao yakiliwa na wanyamapori, hakuna kulipwa. Hakuna malipo! Hawa jamaa wamejiwekea sheria, unalipa kutoka kilometa moja mpaka kilometa tano ndiyo unalipwa na unalipwa kwa heka moja shilingi 100,000. Kwa hiyo, kama tembo amekula mazao heka 20, unalipwa heka tano, heka 15 ni sadaka ya Serikali. Nani alifanya maneno ya namna hii? Tunataka kujua nani anapima hii mipaka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nani anatatua migogoro kati ya hifadhi ya wanyamapori na wananchi? Maana yake wamelalamika mika nenda-rudi, hakuna mtu anaenda. Tuna eneo moja linaitwa Kawanga; mpaka uchaguzi wa mwaka 1995 ulimtoa Waziri Mkuu, hiyo Kawanga. Aliuliza swali, nani atatatua mgogoro wa Kawanga? Akasema hii ni sheria, tutakwenda kufanya. Wakasema hapana, sisi tumeshachoka. Mpaka leo mgogoro upo, Mawaziri wameenda watano, sita, wapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Mawaziri wengine mlioko humu ndani, hebu tuambieni, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi; Waziri wa Ardhi, wametamka humu Bungeni kwamba watakaa vizuri na Wizara ya Maliasili na Utalii watatue migogoro ya wakulima, wafugaji na Hifadhi za Taifa, mtakaa mtatue. Uchaguzi tumetoka juzi! Mheshimiwa Rais wetu mtiifu amesema wafugaji sitawangusha. Tumetoka juzi tu, lakini operation zinaendelea kukamata watu. Hii maana yake nini hasa? Migogoro haijatatuliwa, watu wanakamatwa, watu wanatolewa; nani sasa amesema wewe uko sahihi kutoa watu? Tupo tu tunaangalia. Mheshimiwa Lukuvi, nafasi yako naitaka, ikifika miaka miwili na nusu miaka ijayo kama migogoro haijaisha angalau hata robo, wewe toka tu mimi niingie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mgogoro wa Jimbo la Bunda, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri, ameandika vizuri sana hapa. Mgogoro wa Bunda kati ya Wilaya tatu; kuna Serengeti, Bunda na Musoma Vijijini. Mgogoro wa mwaka 1941 mpaka leo haujaisha. Watu wanapigana, wanauana mgogoro upo tu. Mheshimiwa Mabula, wewe ulikuwepo Mkuu wa Wilaya ya Butiama, unaujua mgogoro. Mara uko TAMISEMI, mara uko Ardhi, mara uko wapi, toka miaka hiyo mpaka leo. Mimi sitaunga mkono hoja hii kama kweli mgogoro huu hautaniambia unaisha lini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la Kyandege na wameliandika vizuri hapa. Sasa haya ni mambo ya ajabu. Wakati fulani hawa wenzetu wakisema maneno hapa, ingawaje sisi hatuna mpango wa kutoka madarakani, lakini wana maneno yao mazuri. Hivi inakuwaje? Kwa mfano, inakuwaje GN ya kijiji imetoka; na imetoka Makao Makuu ya Ardhi, imekwenda kijijini; imeandika mpaka kati ya kijiji ni kaskazini na kusini, lakini anayekwenda kukata mipaka kutoka Halmashauri au sijui kutoka wapi, anaenda anakata Magharibi Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamelalamika toka 2007 mpaka leo; eneo hilo tu moja, Muliyanchoka kweli hii? Hapana, hii hapana! Kwa hiyo, naomba kujua hili tatizo litaisha lini? Kwa kweli kusema kweli yapo mambo ya msingi ya kufanya, lakini vinginevyo nakushukuru sana unajitahidi kufanya. Tatizo tulilokuwa nalo, Waziri ulielewe na Mawaziri wote mlielewe, mnafanya kazi sana ya kutumikia watu lakini watumishi wenu wakati fulani wanasema ninyi wanasiasa tu. Watumishi wenu wanawaangusha sana ninyi. Kila ukisema maneno wanakwambia huyu ni mwanasiasa tu. Sasa muangalie, hao wanaosema wanasiasa waondoeni kwanza mbaki ninyi ambao mnafanya kazi. Nashukuru sana.
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia hizi Wizara. Kwanza nawapongeza Wenyeviti wote wa Kamati ya Viwanda na Kamati ya Maliasili na Utalii, wamefanya vizuri na wametupa taarifa za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa dhana yake ya Royal Tour. Maana tunapozungumza Maliasili sasa Watalii wamesukuma hela za kutosha kwenye nchi yetu na maeneo yetu ya hoteli porini kule yamejaa. Zamani wakati Mheshimiwa Rais anafanya hili jambo, watu wengi waliona mchezomchezo lakini matokeo yake sasa mwenye macho haambiwi tazama. Iko wazi kabisa kwamba ile dhana imetoa matunda ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kitendo chake na dhana yake ya kuanzisha ile Tume ya Haki Jinai ambayo sasa itatazama utendaji kazi wa maeneo mbalimbali ya taasisi zetu Polisi, Magereza,TAKUKURU na Kitengo cha DPP. Kwa hiyo, hii dhana ni nzuri sana tutazame kitu gani tunapata haki kwa namna gani. Kwa hilo wazo tu la kuanzisha hiyo Tume ya Haki, nampongeza sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijikite kwenye hoja zetu na sasa nianze na TANAPA, TAWA na Ngorongoro. Toka Awamu ya Kwanza ya Urais ambayo yote ni ya Chama cha Mapinduzi suala la TANAPA, TAWA na Ngorongoro tumekuwa tukiwaachia mapato yao kwa ajili ya kulinda hifadhi zetu za Taifa ambao ni urithi wetu wa Taifa. Kwa sababu ya Corona hiyo 2019 ikabidi mapato yao yarudishwe kwenye Hazina kwa maana kwamba watawasaidia kupeleka bajeti, kwamba mapato yao yamepungua kutokana na Watalii kutokuja nchini. Sasa naona ni wakati muafaka wa kuwapa mapato yao kwa sababu vitendo vinavyoendelea sasa hivi, hata ule wingi wa mifugo kwenda porini, lakini pia kutolipa vizuri malipo ya kifuta machozi, hii dalili kwamba mapato kutoka Hazina kwenda TANAPA, TAWA na Ngorongoro imekuwa shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wao umekuwa wa shida mno, hawawezi kufanyakazi kwa kusubiri takwimu zitoke na hela zitoke Hazina waandike voucher, waende wapige sijui mfumo umekataa, sijui kitu gani, mambo mengi tu yametokea. Kwa hiyo, tunaomba sasa bajeti hii inayokuja na Wizara ya Fedha ielewe wazi kwamba bajeti yao itapita endapo watakubali fedha za TANAPA na TAWA ziende zikafanye kazi ya kulinda maliasili zetu ambazo ziko pale ndani. Kwa hiyo nafikiri kwamba hili ni wazo ambalo Kamati imelileta na sisi tunaliunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la pili, ninataka nizungumzie pongezi za watu wa Ngorongoro kuhama kwa hiari lakini kwa kuwapa haki zao. Sasa wakati naipongeza Ngorongoro kwa haki hizo, niende kwenye vijiji vitatu vya Wilaya ya Bunda ambavyo ni Nyatwali, Serengeti na Tamao vinahamishwa na TANAPA kwa hiari, kwa sababu vile vijiji vina registration ni haki yao kukaa pale. Lakini style inayotumika kuhamisha vile vijiji haifanani kabisa na style inayohamisha watu kutoka Ngorongoro, wakati wazo ni lile lile. Kwa hiyo, mimi naomba sasa vile vijiji vitatu vipewe haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, juzi wamekuja Mawaziri nane kwenye maeneo yale. Wale watu wanadai tuwape milioni 3.5 badala ya Milioni Mbili kwenye heka moja, kwa hiyo tunaomba kama haki zote haziwezi kufanana lakini at least bei halisi, thamani ya ardhi yao ipande kutoka milioni mbili kwenda milioni nne ili wapate haki sawa waweze kuhama kwenye maeneo yao ambayo ni haki yao, registration wamepata na ni haki yao kuishi pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia, ni Serikali yetu ya CCM ninaomba sana ifikirie jambo hili, kutoa watu kwenye maeneo waliokaa kwa miaka mingi na kuwapa thamani ndogo ya ardhi, wanahama wanalia, wanatoa machozi siyo vizuri sana kufanya jambo kama hili, tunaomba tufikirie namna ya kuongeza thamani ya valuation ya ardhi yao ili wapate haki sawa na watu wengine walivyohamishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye chombo kinaitwa ETS, sasa hapa niende kwa sauti ndogo. ETS wanaita ni Electronic Tracking System ambayo inaendeshwa na kampuni ya SICPA. Kampuni hiyo ililetwa na TRA kwa maana ya Serikali kwamba isaidie kukusanya mapato yetu, mimi naipenda sana ile kampuni kwa sababu inatuonesha mapato yako wapi! Lakini system inayotumika kuilipa ile kampuni ndiyo siipendi. Kwa sababu ile kampuni inapata bilioni 75 kwa mwaka na ina watumishi 15 tu na hakuna mahali bilioni 75 inaenda. Bilioni 75 inakusanywa na kampuni inaenda, inapelekwa nje hakuna mahali hiyo hela inaenda kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo matatizo makubwa ya madawati kwenye shule za msingi, bilioni 75 zinaenda, kwa nini ziende? Kama ni hivyo, hizo hela kwa nini sasa tusitengeneze mpango ikawa Serikali inatumia kidogo kwa ajili ya kufanya maendeleo? Mbaya zaidi hizi fedha zinalipwa na makampuni ya kwetu. Makampuni ya uzalishaji, makampuni ya Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kampuni inaingia kulikuwa na kampuni 19, wakaongeza bei ikawa bei kubwa kiasi hicho, sijui dola 18.6, sijui wanaita kwa track 1,000, lakini kwa sasa tunayo makampuni yamefika karibu 51, naambiwa ni 27, kama ni hivyo mpango wa hiyo kampuni ilikuwa ilete vile vifaa, ile mitambo iliyokuwa nayo baadae baada ya miaka mitatu ibaki na Serikali, ibaki na TRA ndiyo wakusanye. Kwa nini mpaka sasa hiyo mitambo ipo na inakusanywa na mtu wa SICPA, kuna nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukigusa maeneo hayo unataka kuuawa kuna nini hapo? Nataka kuuliza Mwenyekiti kuna nini hapo? Kwa nini watu wanakusanya bilioni 75 wanapeleka nje sisi tuna matatizo makubwa kiasi hicho. Nilikuwa nafikiri tulitazame hili jambo vizuri tuone linakwendaje.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu kumpa taarifa mzungumzaji ya kwamba TCRA walikuwa wanamfumo unaitwa TTMS kwa ajili ya kuratibu simu zinazoingia hapa nchini na kuratibu kazi zote za kampuni za simu. Mtambo huo uliwekwa na mwekezaji baada ya muda ameukabidhi Serikalini. Alichozungumza mzungumzaji hapa nakiunga mkono kabisa hawa walioweka mtambo wa ETS, kama muda umefika wauwasilishe Serikalini na Serikali ndiyo waendelee kukusanya kama walivyofanya TCRA.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea hiyo taarifa?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikubali kwa mikono mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba ni kwamba kampuni ile kwa maana ya mfumo wao wanafanya kazi nzuri sana lakini fedha inayolipwa na wawekezaji, makampuni halafu mbaya zaidi mpango wa kulipa hiyo fedha unapangwa na TRA. Wao wanapanga wameleta mtu atusaidie kukusanya mapato ni sawa, lakini malipo yao hata hawa-share. Unapanga na TRA na ela zinakusanywa zinaenda kwenye hiyo kampuni, sasa tunajiuliza kwa nini hiyo Kampuni kama imemaliza muda wake, hizo fedha zisikusanywe ziingie Serikalini halafu Serikali ione namna ya kumlipa huyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini akusanye yeye, kuna mpango gani kwa huyu mtu mkataba wake umeisha halafu bado anakusanya hela? Kwa hiyo, mimi nasema mpango wake na kampuni yenyewe, mfumo wenyewe ni mzuri sana, system ya kukusanya hela ndiyo tunaiwekea mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye upande wa ardhi, ninaiomba tu Serikali iiongeze Wizara ya Ardhi hela, suala la migogoro ya ardhi ni mingi sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri ambao Mheshimiwa Getere anautoa, isije ikaenda kwenye public kama vile fedha hii ambayo kampuni hii inalipwa ni fedha ambayo ilitakiwa ilipwe Serikali, isije ikaenda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kimsingi ETS inasaidia kudhibiti productions ya products nyingi zinazozalishwa kwa mara moja kama soda au juice au bia zile ‘tatatata’ inagonga zile alama. Kwa hiyo, ile inamsaidia kwanza mwenye kiwanda kuweza kujua bidhaa zake amezalisha kiasi gani kwa ajili ya usalama na kujua kiwango alichozalisha, kwa hiyo inadhibiti. Ni system ambayo inadhibiti, pia inaisaidia Serikali kujua kilichozalishwa ili iweze kuchukua kodi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, isije ikaonekana kwamba fedha hii ambayo inalipwa ilikuwa ni fedha ya Serikali, ni fedha ambayo Serikali kwanza inapata faida ya kujua kilichozalishwa ili iweze kudai kodi yake, pia mwenye kiwanda anapata faida ya kudhibiti uzalishaji wake. Kwa hiyo, siyo fedha ya Serikali ila tu hoja yake inabakia tu kwamba mbona hizi fedha zinachukuliwa na makampuni na zinapelekwa nje kutoka ndani ya viwanda vyetu? Sasa hilo ni jambo jingine.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere unapokea hiyo taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa ameeleza vizuri, hoja hatujasema kwamba hiyo kampuni haifanyi vizuri, inafanya vizuri. Hoja ya kujiuliza ni kwamba ni kwa nini Serikali imeleta hiyo kampuni kusaidia mapato ya Serikali lakini mipango yake ya malipo inatokana na wazalishaji wenyewe? Kwa nini wawawekee wazalishaji mzigo mkubwa wa kulipa malipo ambayo wao hawakushiriki kufanya malipo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kampuni zingine zenye bei nafuu zinazoweza kufanya kazi kama hiyo hazitakiwi kwenye hii nchi, kwa nini? Kwa hiyo hilo jambo liwe hivyo? Tunayo mashaka na hilo eneo lifuatiliwe. (Makofi)

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ole-sendeka taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kumpa taarifa rafiki yangu humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie mahusiano yaliyopo kati ya SICPA na baadhi ya Wizara ambayo inafanya kazi nayo ni mahusiano ambayo siyo ya kawaida. SICPA ilishindwa tenda kadhaa katika vinasaba ilipokuwa inashindanishwa na kampuni zingine ikabebwa mara mbili na muda wake ulipoisha wameendelea na fedha walizokuwa wanazikusanya hawajalipa kodi na Serikali haioni, ni uchochoro mwingine katika swala la vinasaba vya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili lilizungumzwa na Mbunge wa Gairo na hakuna mtu aliyetoa maelezo yaliyojitosheleza. Pale kuna ufisadi, Serikali iangalie na ilete taarifa kwenye Bunge hili juu ya ufisadi wa SICPA na walivyokuwa wanabebwa kama watoto wapendwa katika mradi huo na mkitaka ushahidi nitawaletea walivyoshindwa tenda zote na zote wakabebwa, SICPA hiyo! (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea taarifa hiyo.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikubali kwa mikono miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna vitu vinaletwa, yaani sijui kuna nini sasa! Kwa sababu tumeshakaa Kamati ya Viwanda, Kamati ya Fedha, Kamati ya Sheria tukazungumza hilo tatizo, tukalitolea maamuzi kwamba huyu mtu aangaliwe upya...

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa ya mwisho hiyo.

T A A R I F A

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba mkataba wa SICPA pia uliisha muda wake na Kamati tulishauri Serikali kwamba wasitishe kuendelea kupata huduma kutoka kwa SICPA kwa ajili ya gharama zao ni kubwa, zipo kampuni ambazo zinazo uwezo wa kufanya huduma kama hiyo kwa bei ya punguzo la asilimia 70 chini ya ambayo SICPA anaendelea kuitoa. Kwa masikitiko makubwa ushauri wa Kamati yetu haukuzingatiwa SICPA muda wake umeisha lakini mpaka sasa hivi bado wanaendelea kufanya huduma hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni zetu nyingi za Kitanzania zinalia sana, kila mtu analia hawana msaada. SICPA wanaiibia nchi yetu, wanasababisha mfumuko mkubwa wa bei kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea hiyo taarifa?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea lakini kwa maelezo kwamba hatutaki SICPA itoke, ila kama kuna mbadala wake uje. Tunataka bei ya SICPA ipungue kwa wazalishaji wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa heshima na mimi kuchangia Wizara ya Mifugo. Kwanza naishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi, namshukuru Mheshimiwa Ulega, bajeti yake kwakweli ameisoma kwa uchungu sana, na ameonesha kwamba ni kijana ambaye amedhamiria kufanya kazi kubwa, nakushukuru sana. Na mimi nadhani Mama Samia hatua anayoenda nayo kuna watu anawaona moyo wao unataka nini. Nadhani alikuona moyo wako unataka kuimarisha na kuwakomboa wafugaji kwenye mateso waliyonayo sasa hivi na watu wa uvuvi, nadhani unafanya kazi vizuri. Kwa maana hiyo moja kwa moja naunga mkono hoja yako kabla sijaendelea, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kufanya kazi kubwa ya kuwaamini Mawaziri wake. Mimi nadhani katika uongozi huu kama Waziri hata perform huyo atakuwa na shida yake binafsi. Mheshimiwa Rais anawaamini sana, anawapa ninyi mumpelekee mawazo. Kwa hiyo Mheshimiwa Ulega mpelekee mawazo ya wafugaji; kwamba kama tuna kopa kwa ajili ya mambo mengi hakuna eneo la kukopea kama kukopa kwa ajili ya kuimarisha mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Rais anaweza kukopa popote, kwa sababu ukichukua wafugaji wote, mali zote za wafugaji ng’ombe, mbuzi na kila kitu ulichotaja hapa ni trioni 25, na ukichukua samaki peke yake ni trioni 846. Sasa, trioni zote hizo manashindwaje kukopa kuimarisha, tuna shida gani ya kukopa ili kuimarisha trioni za fedha? Sasa unapewa milioni 200 ndugu yangu, sijui bilioni mbili, sijui bilioni tatu inatosha wapi? Haitoshi. Kama nchi inaweza kukopa ikope kwa ajili ya kuimarisha ufugaji na uvuvi. Mimi nadhani hilo ni jambo zuri sana la kufanya katika nchi yetu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda mbali nataka nizungumze jambo moja tu. Mheshimiwa Waziri umesema habari ya kupeleka mizani kwenye minada; na umezungumza kwa uchungu sana nimeiona moyoni mwako. Nataka nikupe tahadhari, tena tahadhari kubwa. Usipokuwa makini ukipeleka hiyo mizani bila kuwapa elimu wafugaji utakuta minada iko mitupu, na hasa minada ya vijijini. Mauzo ya ng’ombe hayategemei mizani peke yake. Nataka nikupe mfano; mimi nikiwa na maksai kumi inawezekana maksai sita ndizo zenye uwezo wa kununua milioni moja, maksai nyingine zote zinakuwa chini ya milioni moja, labda inakuwa laki nane au laki saba. Mimi nikikutana na mfugaji anayenunua ng’ombe yule mnunuzi namuuzia maksai kumi zote kwa milioni moja, zile zingine zote zinabebwa na maksai sita. Kwa hiyo ukienda kwa mizani inawezekana mtu asiuze ng’ombe zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, achunge sana hili neno; kama anakwenda huko afanye utafiti kwanza kabla hajapeleka mizani vinginevyo atakwenda kuua minada; watu watauzia majumbani hakuna mtu atakayepeleka ng’ombe mnadani. Lazima twende tuwaelimisha wafugaji juu ya hasara anayoweza kuipata kutokana na hili jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri amezungumzia habari ya mashamba darasa. Mashamba darasa maana yake ni kwamba uwe na maafisa ugani wa kutosha. Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeseme 2025 tuwe na afisa ugani kwa kila kijiji. Tuna vijiji 12,319, unao? Unao wa mashamba darasa? Asilimia 35 ya maafisa ugani ndio walioko vijijini sasa hivi; unao hao wa mashamba darasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani imesema tupeleke majosho kwa kila kijiji. Tuna vijiji 12,319. Kwenye jimbo langu katika vijiji 35 ambavyo vina wafugaji wa kutosha ni vijiji 10 tu ndivyo vina majosho, na majosho yenyewe mnaenda kufanya nyie watu wa Wizara. Siku hizi mna mtindo mnapeleka milioni 22 mnaenda kuchimba majosho. Unachimba josho la milioni 22 halina kisima, halina kibanio halafu unaliacha hapo, halafu fedha yenyewe inatoka Wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemuona hapo Mheshimiwa Waziri, aende akafumue huo mtindo. kwa nini fedha ya kijijini ikae Wizarani? Walaji gani wanakaa Wizarani na fedha haiji kiasi kwamba josho linajengwa kwa miaka miwili hadi miaka mitatu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kata ya Salama kuna josho limebomoka, naomba aende alitengeneze. Kwenye Kijiji cha Salakwa hamna josho, kwenye Kijiji cha Maliwanda hamna josho, vijiji takriban 20 havina josho. Nitamletea aweze kuangalia kwamba kwanini inafanyika hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuzungumze mashamba ya NARCO; sasa najiuliza, NARCO ni biashara au ni nini? Mashamba ya Serikali ya NARCO na mashamba mengine ya Serikali mliyonayo ni ya biashara au ni ya watu? Ni ya watu au ni ya Serikali au? Mimi sielewi sasa Kwa sababu kama mna ng’ombe, mashamba yenye kutunza ng’ombe milioni 42 leo mnatunza ng’ombe 19,000. Sasa mimi nashindwa kuelewa haya mashamba ni ya nani? Kila mtu shamba lake, kila meneja shamba lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri, kama anaweza kama anaitendea haki hii Wizara aanzishe mamlaka ya wafugaji. Mimi nashindwa kuelewa, hivi leo nchi yetu inashindwa kuwa na mamlaka ya Samaki na ng’ombe ilhali tuna Mamlaka ya TAWA, tuna TARURA, tuna RUWASA na tuna TFS. Mna mali ya kutosha kutoka kwa wafugaji lakini mnashindwa kuweka mamlaka, kwa sababu gani? Sijawahi kuona nchi ina mamilioni ya fedha kwenye maeneo kama hii…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Chumi uko salama hapo? (Kicheko)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, niko salama kama ambavyo Singo yuko salama.

NAIBU SPIKA: Nashukuru, nashukuru. (Kicheko)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipunguza sauti sawa. Kwa hiyo naomba nchi yetu itengeneze mamlaka ya wafugaji ili iwalinde wafugaji, wafugaji wanashida. Waheshimiwa Wabunge wa CCM na wale wa NEC mliomo humu ndani, katika eneo ambalo hatujafanya vizuri Tanzania ni la wafugaji. Wafugaji hatuwafanyii vizuri, hatuwatendei vizuri kabisa. Tunaomba hii Wizara mama aitendee vizuri, tunamuomba sana Mheshimiwa Rais na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa. Mimi nimekuja na kitabu hapa, ninacho hapa. Katika eneo la wafugaji hatujafanya vizuri; tuna ilani hapa hatujafanya vizuri katika eneo la wafugaji. Tuwalinde wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuja hapa na lile suala la herein; sasa katika ilani inasema hivi, tuwatambue wafugaji wenyewe, mifugo yao na wafugaji yenyewe. Sisi hereni tunawekea ng’ombe tu mfugaji hatujui tunamwekea nini, au na yeye tuna mwekea hereni? Sasa unawezaje kumwekea herein, is not sustainability. Unawekaje hereni kwenye mfugo, uweke leo kesho usijue unaweka nini? Ndama anazaliwa leo hakuna hereni. Tunaanzisha vitu ambavyo havina maana. Hata kama tungeuza hereni kwa bei nafuu lakini where is sustainability? Iko wapi sasa? Leo mtu anazalisha ng’ombe unampa hereni moja kesho kutwa anauwezo gani wa kuangalia?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa, ni wapi taarifa. Haya Mheshimiwa Tabasam.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Anazungumzia suala la heleni hawa ng’ombe wako madume na majike, sasa heleni wanatakiwa wavikwe. Je, watavishwa madume peke yake au na majike? Kwa sababu wakivishwa majike…

NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Getere.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: …akivishwa dume inakuwa ni hatari kama atavaa heleni.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa heleni sio mbaya, ni mzuri kwa maeneo yaliyoandaliwa, ni mzuri kwenye ranchi ni mzuri kwa maeneo yaliyoandaliwa siyo vijijini. Mtu hana simu hana nini eti unamlazimisha kununua heleni halafu anaiona ng’ombe wake…

MBUNGE FULANI: Taarifa, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa mnamchukulia muda wake, endelea Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili jambo la hereni nalo tuliwekee utaratibu mzuri ili tuweze kwenda nalo.

Mheshimiwa Waziri umezungumza habari ya mikopo ya wafugaji; ni kweli benki ya NMB inakopesha wafugaji kwa asilimia tisa, ni kweli, lakini masharti ya kupata mkopo eh! kazi ipo; kupata mkopo kazi ipo. Ni kweli benki ya NMB inafanya kazi nzuri, hata kwenye jimbo langu inafanya kzi nzuri sana ya kukopesha mikopo lakini nani anawasimamia wafugaji wapate mikopo. Kwanza unapewa masharti uwe na clearance, uwe sijui na vitu gani. Unatumia kama laki tano laki sita halafu unaomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naomba kujengewa majosho katika Kijiji cha Nyaburundu, Mekomariro, Nyansirori, Nyangere, Hunyari, Sanzate, Rakana, malambo mawili Nyaburundu na Rakana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Wizara ya Ardhi.

Kwanza nawashukuru Wizara kwa maana ya Waziri, Naibu, Makatibu wake na wote walioko hapo kwenye maeneo ya ardhi kwenye Wizara ya Ardhi. Nimshukuru Mheshimiwa Rais, kwa kweli kimsingi toka Rais amekamata hii nchi imekaa vizuri sana na inakaa vizuri inaendelea vizuri. Mheshimiwa Rais amefuata misingi ya Baba wa Taifa, anaijenga nchi katika misingi isiyo ya matabaka na wale wanaohubiri matabaka watakuja kuona kwamba hii nchi imejengwa kwa matabaka na haiwezi kuwa matabaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mtaniwia radhi tu yaani tu, yaani kusema lazima niseme tu. Katika Wizara sielewi kabisa ni Wizara ya Ardhi yaani sielewi, yaani sielewi, yaani sielewi naanza moja/mbili wapi, sielewi yaani ni Wizara ya Ardhi na kusema kweli kipindi hiki naunga mkono ila bajeti ijayo nitakuja na hoja binafsi ya kuichunguza Wizara ya Ardhi. Kabisa yaani sielewi, haitokei kichwani yaani. Wizara ambayo ina Mkurugenzi wa Ardhi, Kamishna wa Ardhi, Katibu Mkuu Ardhi, msaidizi gani - ardhi. Wana mipango, wana wasomi, wana maprofesa, wana makamishna wa mikoa, wana wa ardhi wa wilaya. Hakuna migogoro mahali popote imeisha, yaani hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mabula mimi niulize swali; hivi kweli kwa mfano ulikuwa Naibu, umekuwa Waziri, hivi kweli hata kwenye majiji yetu basi, tuseme leo Dar es Salaam migogoro imepungua imebaki asilimia labda 10, 15; Jiji la Mbeya imebaki lazima asilimia ngapi; Jiji la Mwanza yaani hakuna mahali unaenda ukute ardhi sasa imepunguza migogoro. Sasa tunajiuliza, sasa humu ndani kuna nini kinaendelea? Nenda kwenye mipaka ya nchi migogoro, mipaka ya vijiji migogoro, kila mahali migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jamani mambo gani haya? Kwa kweli mimi niombe na nikuombe mama yangu nikuombe kwa kweli ujitahidi. Mimi nadhani kuna matatizo kwenye hii Wizara na matatizo makubwa ni mipango ya Wizara hii. Sijui kama inaenda vizuri, sielewi yaani sielewi kama inaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa mfano mimi nikienda benki nataka kufanya biashara, mimi ni mfugaji labda nataka kufanya biashara ya ng’ombe wakanipa shilingi milioni 300 halafu milioni 300 nikapita barabara nimetoka Dar es Salaam nikatamani gari nikanunua shilingi milioni 200. Jamani, mambo ya ajabu haya. Mmepewa shilingi bilioni 350, badala ya kwenda kupima viwanja mpewe hela za kudumu miaka yote, mnajenga majengo. Hayo majengo si yapo? Yako pale Bunda yamejengwa, majengo ya ardhi yapo, yako kila mahali. Juzi juzi hapa mmejenga mmetengeneza mtandao pale Dar es Salaam mzuri kabisa mmepewa sijui mkopo kutoka nje. Migogoro imeisha? Mimi nadhani kuna shida, kuna shida.

Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri ufanye kazi ya kutosha kwenye Wizara yako. Ukiona imekushinda, hivi kwetu hapa hakuna mtu kujiuzuru? Si inakuwa imekushinda tu unasema Mheshimiwa Rais hii Wizara imenishinda basi. Kwa hiyo mimi nikafikiri kwamba hii hali ni hali ngumu sana ya Wizara hii.

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere namomba upokee taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilitaka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba naomba tukumbuke kwamba migogoro hii haijaanza hivi karibuni na mnakumbuka kabisa kuna Kamati ya Mawaziri nane iliundwa kwa ajili ya kutembelea kila eneo kuangalia changamoto zilizopo za migogoro ya ardhi na sasa kamati hii iko kwenye utekelezaji. Sasa inapofika mahali inaonekana kwamba kipindi hiki ndiyo migogoro imekuwa mikubwa, siyo kweli. Migogoro hii ni chimbuko la kuundwa kwa Kamati ya Mawaziri nane. Nataka hili Waheshimiwa walitambue, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere unapokea taarifa?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niendelee na uchangiaji wangu kwa sababu mimi sijazungumza hakuna Wizara inaitwa Kamati ya Mawaziri. Wizara inaitwa Wizara ya Ardhi, hakuna Wizara ya makamati ya Mawaziri. Kwa hiyo, mimi niendelee na mchango wangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunapozungumza ukweli kwenye jambo hili tunataka Waziri au Wizara hiyo ijirekebishe basi au kama kuna matatizo imalize. Kuna migogoro ya kudumu ya muda mrefu ni kweli, lakini kuna migogoro ya viwanja kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa yale yote ambayo Wabunge wamejadili humu wamemuomba aende atekeleze ikiwa ni pamoja na kutazama hizi fedha za kujenga majengo badala ya kwenda kupima viwanja. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa kweli hili ulitazame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongea haya kusema kweli kwa sababu hatuwezi kuwa na miaka 60 tuna Wizara halafu hakuna eneo, hakuna hata mkoa mmoja ambao tunasema sasa huu mkoa uko nafuu labda twende Dodoma hapa iko nafuu. Hata tunakoishi hapa ni shida. Nenda pale kwenye Wizara ya Ardhi hapo, watu wanazunguka tu wamejaa kila mahali, ni shida. Kwa hiyo, nafikiri kwamba hili nalo tulitazame tuone tunafanyaje ili tuweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Bunda nimeomba nimeandika barua ya kupima vijiji 30, sijawahi kupata majibu, lakini Mheshimiwa Waziri wewe ulikuwa Mara na mimi nakujua ni mkakamavu, mimi sijui Mawizara humu yanakuwaje mimi sielewi, lakini wewe ni mkakamavu kweli kweli yaani sasa sielewi ukifika Wizara fulani sijui ni watu wamekushinda akili sijui nieleweje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara ulikuja pale unajua mgogoro wa Mkomariro, siyo mgogoro sasa hivi ni changamoto; za Mkomariro, Sirorisimba, Mgonyamirwa na Kijiji cha Mahanga na Manchimweru kuna migogoro ile ambayo iko kwenye mipaka. Siyo sana kama ilivyo huko nyuma lakini tupeni fedha, wanahitaji shilingi milioni 60 tu kupima hata hati za kimila wawape ili kila mtu awe na ardhi yake wapunguze migogoro. Nikuombe kwenye hilo nitakuja ofisini kwako niweze kukuomba ili uweze kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumza hapa ni suala la Nyatwali. Sasa Mheshimiwa Waziri ulikuja Nyatwali nikakusikiliza na tukakufuata, tukakuuliza kwa nini wananchi wa Nyatwali ambao wana GN ya vijiji vyao mnawahamisha kinyemela tu bila kuwapa fedha shilingi bilioni mbili au laki mbili au laki ngapi wafanye kazi. Mheshimiwa Waziri ukasema unajua Sheria za Valuation zinasema hivi, zinasema hivi.

Sasa nataka nijiulize, hivi wananchi wa Nyatwali wao ni Warundi au ni watu gani? Wana tofauti gani na watu wa Ngorongoro waliohamishwa ambao tena hawakuwa na registration yoyote, wakapewa fedha, wakapewa nyumba, wakapewa mashamba, wakapewa vitu vya, wakapewa umeme, wakapewa, yaani wana tofauti gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli hivi Mama Samia analijua hili kweli? Mimi nimuombe mama kwa sababu mama watu wote ni watu wake. Aliwaonea huruma watu wa Ngorongoro wanavyoteseka na leo wanasifia sana kila mahali. Kwa nini hatuwaonei huruma watu wa Nyatwali? Hivi unamhamishaje mtu Mheshimiwa Waziri unasema Sheria ya Valuation inasema hivyo? Pale ni shilingi laki saba, sijui heka laki ngapi? Hivi Ngorongoro hakuna hiyo sheria? Hapo Ngorongoro sheria ilipotea? Ni watu ni wale wale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo hata mimi ungeniuliza Nyatwali wahame wasihame, ningewaambia wahame kwa sababu si tunataka tuweke Hifadhi ya Serengeti iwe mbuga ya maajabu? Si unataka ishikane na Ziwa Victoria? Sasa wale watu tumekwenda kuwahamisha kwa hiari yao, kwa nini tulete kutumia sheria na wamekubali kuhama, kwa nini? Nikuombe Mheshimiwa Waziri unajua mimi huwa najiuliza swali moja huwa najiuliza sana, hivi Wabunge mbona Wabunge mkiwa siyo Mawaziri naona kama vile mna-act vizuri, mkiwa Mawaziri mnakaa pembeni. Mkitenguliwa mnaanza na maneno, hivi mkoje ninyi? Kwa nini msihurumie watu? Yaani mkitenguliwa ndiyo mnajua huruma ya wananchi, mkiwa kwenye Uwaziri huruma hamuioni. Hivi mkoje ninyi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini msione huruma ya wale watu? Nenda kawatembelee mama wale watu. Wale watu wa shilingi milioni moja, milioni mbili, milioni tatu waone. Wale waliopata mabilioni, mabilioni achana nao. Muone basi wa kuwaona. Kwa nini huwaonei huruma, hivi siku nyingine mama wewe ni wa pale. Hivi siku ile unapita pale watu wanalia machozi, wanajigaragaza, mmekwenda kuwahamisha kwa hiari yao halafu mnawalipa shilingi laki moja, laki mbili, laki tatu? Jamani kwa kweli hii kwamba hiyo haiko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Rais hili kwa kweli alione, mimi sijui kama analifahamu vizuri, mimi sifahamu. Mimi nadhani kwamba sasa tumebaki tutafute alternative mtuombee wananchi na wazee sisi wa kule tumuombe tumwone mama na tumwambie mama watuongeze basi badala hata ya shilingi milioni mbili iwe milioni tatu. Hivi shilingi milioni mbili unaenda kununua; kiwanja bure ni shilingi milioni nne, unaenda kununua nini? Huna mahali pakwenda, hujapewa eneo, hujapewa chochote, yaani wahame tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe kwa kweli hiki kitu hakiko sawa. Nikuombe tutamuomba Mheshimiwa Rais hili ataliona aweze kutusaidia kwamba hii hali itakwendaje kwenye jambo hili ambalo siyo zuri kwa kweli, halina wema wowote.

Mheshimiwa Waziri hivi mipaka hii sasa, mipaka ya vijiji mimi niwaombe na nikuombe na Wizara yako, wakati fulani msitumie ramani kwa sababu unaweza kutumia ramani kwa sababu walikuja siku moja kutumia ramani Kijiji cha Tiling’ati wakakuta kijiji hicho kiko Butiama, siyo Bunda. Ukaenda sehemu nyingine kuangalia ramani kijiji kiko Serengeti siyo Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani kwenye migogoro ya muda mrefu nendeni mkajiridhishe, wewe unaishi hapa mwaka gani? Miaka fulani, wewe unaishi hapa miaka gani? Miaka fulani basi mnapima mnaachana nao. Kwa nini hatufanyi hiyo akili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna mtu mmoja anaitwa Albert Einstein alisema akili ni kile ambacho wewe umetolewa vitu vyote ulivyojazwa kichwani ukabaki nacho, hicho ndiyo akili. Kwa nini watu wazito wa busara? Kwa hiyo muende kwenye maeneo ambayo watu wamekaa kwa muda mrefu muwasaidie, muangalie uhalisia wao siyo kufuata ramani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia Wizara hii ya Nishati. Namshukuru Waziri na Naibu Waziri na viongozi wote, Katibu Mkuu wa Wizara na wote wanafanya kazi nzuri, wengi tumewapongeza wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa najiuliza mambo mengi, nikichangia hapa huwa mnaniona. Najiuliza kuhusu Waziri Makamba, wakati Mheshimiwa Makamba anawania Urais mwaka 2015 nilisoma sana hotuba yake. Moja ya hotuba yake aliyokuwa anaisema ni kwamba akiwa Rais atashughulikia mafisadi na wala rushwa katika nchi hii, akasema nchi yetu inaweza kwenda mbele au ikarudi nyuma kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikuombe kwa hilo ambalo ulilokuwa unalisema kipindi hicho, kwenye Wizara yako tunataka kukuona kwa miaka hii ambayo mama amekupa, tuone unatekeleza yale ambayo ulitaka kuwa Rais, leo nilikuwa nataka nikupe ushauri. (Makofi)

Lingine ambalo nikuseme Mheshimiwa Makamba ni kwamba ni moja ya vijana bora wa Afrika waliosoma chuo kikubwa duniani Harvard University ni vijana bora waliosoma na Watanzania na wale ambao walipelekwa na CCM. Umekaa Harvard miaka mingi, nategemea sasa ukija hapa uta-apply mambo makubwa ingawa Watanzania hawayaoni, lakini wanayaona hiki ulichotutengenezea hapa leo ni jambo kubwa sana na mabanda uliyoleta juzi hapa ni jambo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu yangu Makamba umesoma Harvard, Harvard ambayo ina vitabu ma-cover yake yamefunikwa na ngozi ya binadamu unaogopa nini? Harvard ambayo ina watu ambao wanafanya sayansi jumla ya miili iliyoko pale ni 23,000 unaogopa nini Harvard ambayo maraisi saba wa Amerika wamesoma pale, unaogopa nini kutekeleza mambo haya? Nina imani na wewe kwamba sasa tumepata mtu wa kutupeleka kwenye mwanga ni wewe, ukishindwa ni uzembe wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nishauri tu sasa wasomi hawa wakisoma sana wanataka kila kitu wafanye sayansi ndio shida sasa, kwa mfano hivi karibuni wakati unatoa hotuba yako umetuambia mambo mazuri sana, lakini moja umesema utaunda tume ya kwenda kuchunguza maeneo ya mjini yanayofanana na vijijini uyape umeme. Uunde tume miezi sita, hayo ndio matatizo ya wasomi. Kumbe sisi Wabunge tunaweza kuwa tume, ukasema baada ya hapa kila Mbunge alete maeneo ambayo yanafanana na vijijini yanayohitaji umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenyewe ni tume hapa, hizo hela za tume tupe sisi tuweke mafuta mzee, halafu baadaye wewe tuma watu wako wilayani na mkoani wakachunguze haya maeneo. Nakujua msomi kazi yake ni kuhakikisha kwamba hawezi kufanya jambo lazima alifanye kwa utafiti, sasa u-apply geopolitics ya Marekani na Tanzania ni vitu viwili tofauti, sisi hapa hatuna hela, wenye hela ambazo ungezitumia kuunda tume ungetupa sisi tuunde pale kwenye Jimbo langu nina vitongoji zaidi ya 37 havina umeme, hizo hela zingekuja upande wa pili.

Kwa hiyo, mimi nakushauri uangalie upya kwamba tume ya nini, sisi wenyewe Wabunge ni tume, leta makaratasi hapo leta fomu hapo tujaze halafu fuatilia uone kama ni ukweli ama sio ukweli, kwa hiyo jambo litakuwa liko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri nimeangalia hivi vipaumbele vyako kweli nimesikitika sana yaani kabla sijafanya utafiti nimesikitika mno, hivi najiuliza vipaumbele viko 12 Bwawa la Nyerere liko wapi ambalo lina shilini trilioni 6.55 liko wapi kwenye vipaumbele hivi ambavyo umevitoa? Lakini nikajua kwamba pengine umejumlisha kwenye kipaumbele Na. 1 haiwezekana, kwa sababu political is all about perception unaweza ukasema mtu akaangalia akasema Bwala la Nyerere limeachwa haliko kwenye vipaumbele tutasemaje sisi watu wa CCM tutasemaje, lakini kumbe umeliweka humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipofunua ukurasa wa pili nikakuta unasema miradi ya kusafirisha umeme, ukasema miradi ya uzalishaji wa umeme iliyopo katika hatua za utekelezaji; Bwawa la Nyerere ambalo umelitaja hapa shilingi trilioni 6.55 umelitengea shilingi trilioni 1.44 maana yake hili bwawa fedha yake imechukuliwa ni karibu ya nusu ya bajeti yako yote ambayo ina shilingi trilioni 2.9. Kwa hiyo hapa umelifanya vizuri, lakini nikuombe kipaumbele cha kwanza ni Bwawa la Nyerere, hili bwawa likiwepo maana yake matatizo ya umeme yanaisha, nikuomba hii karatasi ibadilishwe iwekwe upya Bwawa la Nyerere liwekwe la kwanza, lifanane na hiyo tunayokuwa tunazungumza hapa, lakini kwenye bwawa hili mimi najiuliza mambo mengi sana, nimesikia kuna changamoto ya Bwawa la Nyerere, najiuliza ni changamoto gani hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kama kuna changamoto tuletee, sisi tunaamini wataalam na wanasheria nguli wa Tanzania waliokwenda kufanya mikataba ya ujenzi wa Bwawa la Nyerere wamejiridhisha na kila kitu. Kwa hiyo mkandarasi anapaswa kufuata ile mikataba waliyoweka, sasa kama kuna changamoto zinatoka wapi?

Mimi nikuombe kama inawezekana waite wote waliofanya mikataba, wanasheria wote nguli, kaa nao na mkandarasi pengine mkandarasi ameona sasa wewe umeenda anakupa mambo mapya, mikataba iliyoko pale walioifanya wamefanya kwa uhakika zaidi, ifuate na mkandarasi afuate mikataba atekeleze mradi. Akikuzingua na wewe mzingue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa nirudi kwenye jimbo langu, mimi nakushukuru sana tena sana na Watanzania na Wabunge niwaambie huyu Makamba ni moja ya vijana ambao tunatakiwa kumtumia sana, tatizo tu kwamba ana-apply geopolitics ya Marekani, sasa arudi kwenye polepole ya Tanzania, asiwe na magharama makubwa ya kutekeleza miradi lakini ana uwezo wa kutengeneza vitu vyovyote vile, ana uwezo wa kufanya jambo hilo, nikushukuru kwa sababu ya mabanda yako uliyoleta hapa tumetembelea mabanda yote, nimekutana na TANESCO mkoa nilikuwa na Wajumbe wa Serikali za Vijiji nilikuwa na Wenyeviti wa Vijiji karibu 30 wamejiridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo maeneo yote ya Kurusanga, Kata ya Salama Kurusanga na maeneo yote ya Mgeta, Gogea, Bukoba na maeneo yote ya Machimolo pale Janungu na maeneo yote ya Nyamswa yote kwenye vijiji vyote ambayo tumeleta utaenda kuyatekeleza na bahati nzuri wamenipa uhakika huo. Kwa hiyo wananchi wa Jimbo la Bunda, wananchi wa Tarafa ya Chamliho wajiandae kupokea umeme wa Makamba ambao sasa utatuweka kwenye mambo mazuri katika mwanga utakaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho ambalo naliona hapa ni suala la kuweka umeme vijijini, hivi tuna kitu kinaitwa REA, kuna ka mradi kanaitwa densification, kamradi kale kalikuwa kanafadhiliwa na watu wa nje hivi kamekufa au kapo? Maana yake siku hizi sikaoni sana kanaendelea labda ukija hapa utanipa majibu kale kamradi ka-densification kamefia wapi? Kalikuwa kanaenda kama kamradi kanatelekeza umeme kwa msaada wa hela za nje, sasa tujue kamradi kanaenda wapi, kanakuja au kanaenda sehemu nyingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine ambacho nakiona hivi tunapeleka umeme vijijini, unaenda unaweka transfoma ya volti 50 halafu inabeba watu 20, sasa watu wanafika mpaka 50, mpaka 70 transfoma ni hiyo hiyo haibadilishwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, transfoma ya kilovolti 100 inabeba watu mpaka 300 haibadilishwi, sasa kwa nini umeme usikatike? Lazima ukatike tu, haiwezekani kuweka transfoma ya kubeba watu 20 halafu watu wakatumia 60, wakatumia 100 haiwezekani. (Makofi)

Kwa hiyo, kama ni tume ya kuunda ni hiyo sasa kaunde tume ya kutazama maeneo gani ya transfoma zina matatizo ambazo zinafanya umeme unakatikakatika. Sasa umeme unapokatika unatuletea shida sana na mimi Mheshimiwa Makamba nikuambie sasa watu wa REA na watu TANESCO uwaambie siku Yanga na Simba zinacheza umeme usikatike na siku tukienda kule Arusha umeme usikatike, siku tunaenda kucheza na Coastal umeme usikatike, sasa hilo liwe agizo kwamba sasa siku tunafanya mambo yetu umeme usikatike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namkushukuru sana Mheshimiwa Waziri Makamba kwa kweli uwezo unao, sasa ukishindwa kutekeleza hii Wizara wakati mama amekupa amekuamini na sisi tumejilizisha na kisomo chako....

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mnenaji hapa anazungumza kwamba January Makamba ana uwezo mkubwa, lakini ningependa nimuongezee taarifa kwamba hata Mkurugenzi wa TANESCO Maharage Chande ni mmoja ya vichwa vigumu tulivyokuwa navyo hapa Tanzania, kijana mbunifu, lakini pia yupo Mwenyekiti wa Omary Issa mwanzilishi wa Celtel Tanzania namfahamu vizuri, ni mmoja ya vichwa vigumu sana tulivyonavyo hapa nchini ahsante sana, nataka nimuongezee tu kwamba hilo TANESCO ipo salama, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere, unapokea hiyo taarifa?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea lakini nilitaka kujua labda analeta Simba ambaye imemfukuza kocha kumbe ameleta mambo mazuri, naipokea. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwneyekiti, nashukuru kwa yote hayo na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nianze kwa kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Bunda, kwa kunipa nafasi ya kuja hapa Bungeni na mimi nijumuike na wenzangu katika kuwatetea Watanzania wenye matatizo mengi. Nianze kwa migogoro ya moja kwa moja, migogoro ya wafugaji na hifadhi za wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi hapa, lakini kwenye Jimbo langu la Bunda kuna eneo maarufu linaitwa Kawanga, na mimi niombe kwa kusema wazi tu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, ng‟ombe ana laana, toka mmetunga Sharia hii ya wanyama pori ya kukamata ng‟ombe mnamfanya kama nyara, mnamkamata porini hachungi na mnampiga risasi, Mawaziri zaidi ya tisa wamesha toka humu ndani; ng‟ombe ana laana. Kwa hiyo, yeyote anayeshughulika na ng‟ombe vibaya ajue mambo yake yatakwenda vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano tu eneo la Kawanga. Eneo hili mwaka 1974 alikuja Mwalimu Nyerere pale kama kijiji cha ujamaa, akawashauri wananchi wa maeneo yale kwamba jamani acheni maeneo ya malisho. Wakavuka Mto Lubana wakaacha eneo la Kawanga, wakawa wamechimba malambo mawili makubwa ya Chifu Makongoro, wananywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1994 ukaja ujanja ujanja eneo hili likachukuliwa kama game reserve, Ikolongo Game Reserve na Grumeti Game Reserve, pori la akiba.
Mheshimiwa Mwwenyekiti, kwanza huwa najiuliza hivi pori la akiba maana yake ni nini? Mwalimu alisema hivi vitu vya akiba viwepo pale ambapo wananchi wana shida wapewe nafasi.
Sasa inavyoonekana mapori ya akiba yote ni ya wanyama pori, ikija kwa binadamu nongwa. Leo ikitokea operation ya kuzuia tembo asiende kwenye mashamba ya watu na operation ya kwenda kuzuia ng‟ombe wasiende porini, operation ya ng‟ombe inachukua nafasi. Kwa sababu ng‟ombe wanakuwa na faida ukiwatoa kwenye operation unawakamata unawatoza, wanatoa hongo na mnawauza sijui hela za ng‟ombe zinazouzwa zinaenda wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Kawanga wakahama watu, mkalifanya Pori la Gruneti, malambo mawili yako upande ule, mpaka wetu ni mto, na mto ule maana yake ng‟ombe akivuka tu, amekamatwa ndivyo mpaka ulivyo. Lakini kutoka kwenye mpaka wa Mto Rubana kwenda kwenye watu, unatembea nusu kilometa kwenda pale mbele, ndiyo buffer zone yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi najiuliza kama wananchi wa maeneo yale tembo wanakula mazao yao, ngo‟mbe hawavuki kwenye Mto Rubana, malambo yao mmechukua na hamkufidia halafu mnasemaje tuna mahusiano mabaya na ninyi? Profesa Maghembe mimi naomba nikuambie hivi, pengine kule Mwanga ninyi Ubunge wenu wakati fulani akisema fulani mnapata. Sisi Ubunge wetu ni wa kazi, kuna maeneo mengine Ubunge akisema mkubwa fulani watu wanapewa, lakini sisi Ubunge wetu mpaka utoe jasho ndipo upate. Sasa naomba uje Kawanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina ugonvi na wewe, na mimi nikuambie wazi wala huna ugonvi na Wabunge, tatizo lako ni kwamba una-attack ng‟ombe, kwa nini una- attack ng‟ombe sisi tunaolea ng‟ombe. Mimi mke wangu ametoka ng‟ombe namuita Nyabulembo, sasa wewe una-attack ng‟ombe mara kwa mara kwa nini? Tunataka ng‟ombe kweli watoke porini sawa, lakini watoke kwa mpango maalum. Hivi kwa nini majangili wamewashinda porini mnang‟ang‟ana na ng‟ombe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hapa kwenye ripoti ya wapinzani hapa, anasema kwamba ujangili ni mfupa uliowashinda CCM. Na kila siku asubuhi, hata leo asubuhi nimesikia, kwamba kiongozi mmoja mhifadhi wa wanyama pori sijui amekamatwa na pembe za ndovu. Sasa kwa nini msishughulike na hawa mnashughulika na ng‟ombe? Profesa achana na mambo ya ng‟ombe watakulaani hapa. Naomba uje Kawanga uangalie mpaka ulivyo ni mbovu. Lakini ndugu zangu Wabunge tunaotoka kwenye maeneo ya wafugaji, naomba niwaambie wazi, hizi kanuni na sheria za wanyama pori zitaua watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zitaua humu ndani, sheria hii imeandika ng‟ombe ni kama nyara, akikamatwa anapelekwa mahakamani, akionekana ameingia porini auzwe. Ng‟ombe wa Usukumani, ng‟ombe wa Jimbo la Bunda, ng‟ombe wa Tarime na maeneo mengine ana tofauti gani na ng‟ombe wa Ngorongoro? Ng‟ombe wa Ngorongoro anachunga na wanyama, kwani ile sheria ya Ngorongoro imekuwa ni sheria ya Mungu haibadiliki? Sheria ya Ngorongoro ambayo ng‟ombe wanachunga na wanyama haibadiliki imekuwa ni sheria ya Mungu? It’s too rigid haiwezi kubadilika. Tuone maeneo mengine ambayo yanahitaji uhitaji wa Ngorongoro wapelekewe hiyo sheria. Profesa nakuomba uje Bunda, uangalie eneo la Kawanga tuone ni namna gani tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo. Nakupongeza kwa maana ya kwamba msimu mdogo uliopita umenisaidia sana, tembo kidogo, watu wamevuna. Lakini ndugu zangu Wabunge na ndugu zangu Watanzania, mnyama tembo, mama mmoja tulienda kwenye mkutano akatuuliza hivi, hivi hao tembo hawana uzazi wa mpango? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana kama wamezidi tuwafanyie uzazi wa mpango, tembo siku hizi wanakwenda kwenye maghala, wanaangusha maghala wanakula mazao. Maeneo ya Bunda, Unyari, Kiumbu, Mariwanda na kwa Mheshimiwa Ester Bulaya pale Bukore na Mihale wanakula mazao asubuhi na mchana na Profesa upo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipiga kelele hapa mnasema tumekuwa wabaya, watu hawa wanaozunguka wanyama pori hawa, mazao yao yanaliwa fidia haipo. Tunadai fidia zaidi ya milioni 400 hamjalipa kutoka mwaka 2012 mpaka leo, na wanakula mazao kila siku na magari mnayo, watu mnao, mkiambiwa mnasema kwamba Halmashauri ndiyo ilinde wale wanyama. Halmashauri ina askari pori mmoja na gari bovu halipo na Halmashauri hazina own source. Halmashauri hazina hela unawaambia walinde tembo watalinda saa ngapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mbaya zaidi Halmashauri alinde tembo, asipolinda tembo anakula mazao, wakila mazao mnalipa nyie hivi kwa nini mpo hasara sasa? Kwa hiyo nilikuwa nafikiri kwamba ni vizuri ukaangalia. Lakini mambo mengine niseme mapambano ya kuzuia ujangili yaendelee kuwepo, kuimalisha misitu yetu muendelee kuimarisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nizungumze kidogo juu ya TFS. Hao TFS ulionao nikushukuru kwanza umewashughulikia, ni jipu. Haiwezekani kwenye makusanyo yao, kila mwaka asilimia 100, asilimia 200, asilimia 150 uliona wapi? Yaani kila makusanyo ya TFS asilimia 100, asilimia 250, asilimia 300 uliona wapi? Angalieni makusanyo yao asilimia walizokusanya kila mwaka, asilimia 120, asilimia 110, asilimia116 kila mwaka, wao makadirio yao yanakuwaje mpaka wapate hizo asilimia? Kwa hiyo, mliangalie hili nalo hao watu inawezekana wakawa jipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia ya shilingi milioni 400 watu wa Bunda unawalipa lini? Hii fidia sijaiona kwenye bajeti yako. Profesa ukija hapa uniambie kwamba hii kitu unalipa lini. Lakini naomba kuanzia leo na kwenda muda unaokwisha, kwa muda wa mwezi mmoja na nusu naomba mtusaidie kupata magari ili watu wale wapate mavuno yao. Wamebakiza mwezi mmoja tu, tembo leo wanaenda usiku na mchana na kama hamuwezi, Profesa ngoja nikuambie, Marekani ni wanjanja sana lakini wanaishi na Mexico. Waliona haiwezekani kuishi na Mexico maskini na wao wakiwa matajiri, ikabidi wawafadhili wao wapate hela. Hamuwezi mkafanya wananchi wanaozunguka maeneo ya pori, mkasema eti mtakuwa marafiki wakati ninyi mnawanyonya haiwekani, lazima muwafadhili ili waweze kuishi na wanyama vizuri. Na ninyi niwaambie huku Serikalini… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia uhaba wa chakula. Kwanza niwashukuru watoa hoja wote, Kamati ya Ardhi na Kamati ya Kilimo, wamezungumza vizuri kwenye vitabu hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua tu kwa Mawaziri wanaohusika na Wizara hizi au wa Serikali sijawahi kuona kwamba kwa nini kila siku tunazungumza hivi vitu vinavyohusu mifugo, vinavyohusu ardhi kutopimwa na sina hakika kwamba hivi muda huu toka Wabunge wamekuja toka mwaka 1961, haya mambo ya kupima ardhi yalikuwa hayajazungumzwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba kwa Wabunge wenzangu mkitaka Bunge hili tulitendee haki tuondoeni maneno yanayohusu U-CHADEMA na U-CCM. Mkiondoa haya maneno haya mtajenga Bunge ambalo ni imara na litasimamia Serikali. Tukifika humu tumebaki kubishana tu, tunabishana upande huu mara mwingine azushie Magufuli maneno, mara sijui Rais amefanya nini hatutafika hiyo. Tuzungumze mambo yanayohusu wananchi tuwaulize Serikali kwa nini kila siku tunazungumza migogoro ya mifugo na haitatuliki. Kama hakuna majibu tuseme sasa itakuaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila siku tunakuja hapa maneno tu kama ngonjera tu, tukubaliane kwamba kama sisi ni wasimamizi wa Serikali, tuiulize Serikali kwa nini sasa mipango hii ya ardhi ambayo wakulima na wafugaji wanauana, kwa nini haifiki mwisho? Tutapata majibu siku hiyo. Kama haifiki mwisho hatuendi kwenye bajeti, tutapata majibu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kwenye eneo langu la Bunda. Amekuja Waziri Mhagama, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Ndugu yangu hapa Ramo Makani, amekuja Naibu Waziri Kilimo, Mheshimiwa Ole-Nasha wamejionea hali halisi ya uharibufu ya wanyama tembo katika maeneo yangu, kata saba na Bunda Mjini. Wameona hali ilivyo, ikaahidiwa kwamba watapeleka chakula hakijaenda. Sasa nimeona humu wanaandika tupeleke mbegu bora, unaipanda wapi? Unapanda mbegu bora lakini tembo anaishi pale kila siku, wale Wazanzibar wanaita ndovu, anaishi pale pale kwenye shamba, tunapeleka mbegu bora ya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hao tembo au ndovu hawawezi kutoka kwenye Jimbo lile watu watalima lini? Nawashukuru siku hizi wanajitahidi wapeleke na magari, lakini tembo au ndovu zimewashinda kutoa. Wanaishi pale pale kila siku, wamepeleka tochi imeshindikana. Kwa hiyo, nafikiri kwamba ni vizuri Serikali ituambie kama mpango wa eneo langu, vijiji vya Unyali, Maliwanda, Kihumbu, Nyamang’unta, Tingirima, Mgeta na kule kwa neighbour wangu Mheshimiwa Ester Bulaya, vijiji vya Nyamatoke na Mihale, watuambie kama maeneo haya hayawezi kulimwa basi Serikali ijiandae kwenda kuwapa chakula cha bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tembo sasa hivi wamefika wakati sasa wanavunja maghala, wanachukua chakula wanakula, hawana uwezo sasa wakulima pale, ngombe hawaendi porini wanakamatwa, sasa tunafanyaje? Kwa hiyo, tunaiomba Serikali katika hili kuwa wepesi wa kupeleka chakula cha msaada au chakula cha bei nafuu wapeleke katika Kata Saba za Jimbo langu. Hali ni mbaya na Kata Tatu za Jimbo la Bunda Mjini. Hali ni mbaya sana kwenye maeneo haya, njaa ni shida.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimpa rafiki yangu, jirani yangu anaitwa Ryoba dakika tano uwe unanichunga kama zikizidi itakuwa mbaya zaidi. Kwa hiyo, niseme tu kitu kimoja…
MWENYEKITI: Mheshimiwa zimekwisha dakika tano zako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo yangu yote ya Ofisini kwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu yazingatiwe.
(i) Kukasimu barabara ya Mugeta – Misingo – Mekomariro (Bunda) hadi Sirorisimba (Butiama) na Serengeti.
(ii) Kutangaza mkandarasi wa barabara ya Nyamuswa – Bunda (ahadi ya Mheshimiwa Waziri 31/12/2016) aliposimama Kata ya Nyamuswa na kuahidi kutangaza mkandarasi ifikapo Februari, 2017.
(iii) Kutangaza mkandarasi kipande cha Sanzate hadi Nata. Nasikitika kuona kipande hiki kimerukwa badala yake Wizara ilitangaza barabara ya Nata. Kwangu naona kama sikutendewa haki na hasa ikizingatiwa hii Lot ilitakiwa kwisha kabla ya kutangaza huku. Naomba haki itendeke.
(iv) Uwanja wa Ndege Musoma, Mheshimiwa Waziri alishasema anatafuta shilingi bilioni 10 za ukarabati wa uwanja huu mapema 2016/2017. Nasikitika kuona bajeti iliyotengwa ni shilingi bilioni tatu badala ya shilingi bilioni 10. Naomba suala hili lizingatiwe.
(v) Reli ya Arusha – Musoma. Reli hii toka mwaka 1975 inapewa ahadi hadi leo. Tunaomba kwa miaka mitano watu wa Musoma waone jitihada ya Serikali katika kujenga reli hii.
(vi) Bandari ya Musoma ilikuwa ikipokea meli ya MV Victoria, MV Butiama na MV Umoja. Nimeona juhudi za Wizara za kutengeneza meli hizo, tunaomba meli hizo zikitengenezwa zifike Musoma. Matengenezo ya Bandari ni kidogo sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwnyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwashukuru Waziri na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Niendelee kutoa pongezi kwa Jemedari wetu, Rais wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya, sina mashaka na yeye. Wasiwasi wangu ni kwamba akimaliza miaka yake kumi atakuja mtu mzuri kama yeye au vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Hospitali ya Mkoa wa Mara. Sijajua kwa Mkoa wetu wa Mara ni kitu gani kinatokea kwa sababu vitu vingi haviendi vizuri. Hospitali hii imechangiwa karibu miaka 32 na haijaisha. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kongwa, imekuwa ikitengewa fedha kidogo kila mwaka na mpaka leo haijulikani itaisha lini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atueleza kwa mwaka huu wa fedha imetengewa kiasi gani na ni lini hospitali inaweza kwisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri, nadhani ukurasa wa 149, anazungumzia habari ya kupeleka fedha za vijana na akina mama katika vikundi. Katika Wilaya ya Bunda wameandika kwamba imepeleka shilingi milioni 106, nikashangaa! Sasa nataka kujiuliza haya maandishi humu ni ya kweli au mtu ameyabandika tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi nimempigia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kumuuliza hii hela mmepeleka ninyi? Anasema sisi tumepeleka shilingi milioni 20 tu. Maana Bunda yenyewe kukusanya shilingi milioni 100 ni kesi. Sasa nataka kujiuliza hizi fedha zimetoka Wizarani za muda mrefu au za namna gani? Kwa hiyo, kama ni za Wizarani ni sawa lakini kama ni za kutoka kwenye Halmashauri na ni own source, hizi fedha hazijatoka. Kwa hiyo, nataka kuuliza suala hili limekaaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nizungumzie habari ya watumishi katika Jimbo langu la Bunda. Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ametembelea katika Jimbo langu la Bunda ameona katika kila kituo nurse ni mmoja-mmoja tena wale wa daraja la chini na akaahidi mtakapopata nafasi mtatuletea watumishi katika Jimbo la Bunda. Zahanati zote zina nurse mmoja-mmoja na Naibu Waziri ameshuhudia mwenyewe. Kwa hiyo, naomba katika nafasi zitakazopatikana mnisaidie kupata watumishi wa maeneo hayo. (Makofi)

Lakini pia mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii. Tumetembelea Muhimbili, Ocean Road na maeneo mengine mengi, fedha haziendi kwenye vituo vyote vikuu. Tunaiomba Serikali katika bajeti inazotenga fedha ziende kwenye maeneo muhimu ambayo imezitengea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeona Mloganzila, tumeambiwa kile Kituo cha Ufundishaji cha Tiba kimeisha lakini hakina watumishi. Kinahitaji fedha kiasi cha shilingi bilioni nne ili kianze kazi. Tunaomba Serikali ipeleke pale madaktari na kituo kile kiweze kuanza kazi mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Hospitali yetu ya Benjamin Mkapa iko hapa, tunaomba watumishi waende maeneo hayo ili waweze kusaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna Hospitali ya Nyamuswa, ni kituo ambacho tumekijenga kiko kwenye hali nzuri. Tunaomba pale mtakapopata x-ray na nimesikia Waziri anasema mtapata x-ray basi mtupelekee kwenye Kituo cya Nyamuswa ili watu waweze kupata huduma katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika haya mambo ya vijana mimi nadhani sasa kuwepo na mkakati maalum kupitia hii Wizara na Wizara ya Kazi tujue sasa hizi fedha za taasisi za kijamii zinazoenda kwa ajili ya kuwakopesha akina mama na vijana zina mfumo mzuri ambao unaeleweka. Maana inaonekana kwamba kuna maeneo mengine yanapata fedha kutoka makao makuu na wengine wanapata kutoka own source sasa haijulikani ni wapi wanapata manufaa. Nashauri tuweke mfuko mmoja wa hizi fedha zijulikane kwamba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wanyama waharibifu. Serikali iwe na mikakati ya wazi katika kuzuia wanyama waharibifu katika Vijiji vya Hunyari, Kisambu Nyangere, Mariwanda, Sarakwa, Mugeta Kyandege na Tingirima. Maeneo haya kwa muda mrefu yameathirika sana kwa wanyama kula mazao yao ya chakula na biashara toka msimu wa 2011/2012 hadi leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia ya kifuta jasho. Tunaomba Serikali kulipa fidia ya kifuta jasho na kifuta machozi zaidi ya shilingi milioni 360 zinadaiwa na wakulima wa Vijiji vya Nyangere, Mariwanda, Kihumbu, Sarakwa, Tingirima, Mugeta na Sarakwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msaada wa kumalizia majengo matatu ya zahanati, kuna maeneo yaliyo mbali na huduma za afya, wakazi wa vijiji husika wamejenga zahanati ili kusaidia kupata huduma za afya. Majengo matatu yameezekwa bado samani, lipu, floor, nyumba ya Mganga katika Vijiji vya Tiring’ati, Kambubu na Mihingo. Tunaomba Serikali kusaidia vijiji hivi ambavyo vipo mbali na huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya maji katika Jimbo langu kuna uhaba mkubwa wa maji ya binadamu na mifugo na hapa ieleweke kuwa katika vyanzo vya maji katika Jimbo langu maji ya malambo na mabwawa ndio maji ya binadamu na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali kukarabati malambo ya zamani ya Kyandege, Mugeta, Tingirima, Nyang’aranga, Manchim, Wero, Mahanga, Salama A, Sarzate, Rakanaa, Mihingo, Mekomariro (Malambo mawili) na Sarakwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malambo haya yalipangwa kuchimbwa sana budget ya 2016/2017 hadi leo hakuna dalili, Mheshimiwa Waziri wa Maji aliahidi humu Bungeni, Bunge la Mwezi wa Pili, 2018 na kwamba Bunda imetengewa bilioni moja kwa kazi hiyo. Malambo yanatumika zaidi kwa maji ya binadamu kwa visima kukauka kila kiangazi. Suala la Malambo katika Jimbo langu yana umuhimu zaidi kuliko visima, maana visima hukauka kila kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Kitengo cha SENEPA wamekubali kutoa vifaa na ufundi kusaidia kukarabati malambo haya, tunaomba Serikali ikubali kusaidiana na Wizara ya Maji kukarabati malambo haya yaliyochimbwa miaka ya 60 lakini ni chanzo cha uhakika cha maji katika jimbo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kabla sijatoa hoja yangu ya kuunga mkono niwape pole wakazi wa Jimbo langu la Bunda kwa taabu kubwa waliyonayo ya upungufu mkubwa wa chakula na niwahakikishie kwamba Serikali kwa maelekezo yake hivi karibuni inaweza kuwasaidia kupunguza tatizo walilonalo.

Suala la pili, niwape pole wanavijiji wa barabara ya Bukama, Salamakati, Mihingo na Mgeta ambayo imevunjika daraja zake kwasababu ya mvua na mkandarasi wiki ijayo au wiki mbili zijazo atakuwa kwenye site, kwa hiyo wategemee watapata huduma, kwamba Serikali inawasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme tu kwamba humu ndani pamoja na kwamba tupo Wabunge wengine wa miaka mingi lakini pia kuna wazee humu ndani, hili suala la bajeti ya maji tumelisema sana, watu wameonyesha njia, lakini iko hoja ya msingi kwamba sasa litakwenda kwenye Kamati ya Bajeti ambayo itakaa na kulitazama upya. Sasa kama hiyo ndiyo hoja basi hakuna haja ya kulipinga ni kuliunga mkono tu kwamba pengine katika ongezeko litakalokuja litatusaidia kufanya mambo.

Kwa hiyo, mimi nitaiunga mkono hii bajeti mkono kwa sababu itakwenda na itarudisha majibu ambayo yataleta neema. Mambo mengine haya ya kuota kwamba CCM itakufa lini, unaweza ukakaa miaka mingi tu hujapata jambo hilo kwa sababu CCM pia ni nembo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye hoja ya msingi ya Jimbo langu la Bunda. Haihitaji kusoma sana kujua kwmana asilimia 72.6 ya huduma ya maji inayopatikana vijijini haihitaji kwenda darasa la saba wala la ngapi. Hivi kwa mfano, kama asilimia 72.6 ndiyo huduma ya maji vijijini, kwa lugha nyingine ni kwamba kama una watu milioni moja maana yake watu 726,000 wanapata maji vijijini. Yaani kama tuna vijiji 1,000 ina maana vijiji 726 tu vinapata maji sasa jamani hivi ni kweli? Maana yake ni kwamba vijiji 274 ndivyo havipati huduma ya maji. Hivi Waziri, wazee wangu hawa mmetoka sijui engineer sijui nini inahitaji hilo kutuuliza? Hivi takwimu hizi tunazipata wapi? Waheshimiwa Wabunge sisi wote tuko humu ndani, kwanini usituambie kila Mbunge atuletee vijiji vyenye huduma ya maji na wewe ukaviona kwenye asilimia? Msikariri bajeti hizi kwa mambo ya kukariri kwenye vitabu jamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazee wangu nyie ndiyo mnamalizia hivi, mkishatoka hapa na uwaziri unaacha. Kwa hiyo naomba mjikite kutusaidia sisi. Mbona Waziri wa Nishati na Madini ametuambia leteni vijiji ambavyo havina umeme, tumempa na ameviona vijiji vinaonekana, ninyi kwa nini hamfanyi hivyo? Mnakariri bajeti sio wataalam? Mimi ninawaambia kumekucha hali si nzuri sana. Kwenye Jimbo la Bunda amezungumza mwenzangu hapo, lakini niseme tu nimeandika barua tarehe 26/10/2016, utata wa miradi ya Jimbo la Bunda nikataja mradi wa maji Mgeta-Nyangaranga. Nashukuru kwa sasa hivi mkandarasi yupo lakini bado anasuasua tu, anaweka leo bomba moja kesho haweki, hakuna kinachoendelea pale, mradi una miaka sita unahangaika tu, haiendi vizuri. Barua hii haikujibiwa; hata sikujibiwa mimi kama Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupewa nilichoandika jamani ni sawa? Mheshjimiwa Waziri nimekuja kwako, Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuja kwako, kwa Katibu nimeenda, sasa mnataka tuende wapi? Wazee wangu mnataka tuende wapi tuseme? Mradi wa Maji Mgeta matatizo, Mradi wa Nyamswa Salama Kati mmetenga shilingi 367,291,127, wanasema mradi umetengenezwa kwa asilimia 55 umekufa una miaka mitatu; mnataka twende wapi? Nimezungumza mkasema mtarekebisha miradi ya zamani iendelee, lakini hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mradi wa Kilolei shilingi milioni 400, vijiji vya Nyabuzume, Kiloleni na Kambugu shilingi milioni 400, ile mnasema visima kumi. Nimewaambia ofisini hakuna kinachoendelea, mnasema tuseme nini sasa kwenye hili? Ameandika Mhandisi wa Wilaya ya Bunda tarehe 1 Juni, 2016 miradi ya viporo vya madeni ya wakandarasi wa mradi wa maji Wilaya ya Bunda; mmeleta shilingi bilioni tano. Miradi karibu asilimia sabini na kitu asilimia haifanyi kazi, ninyi mkija kwenye asilimia hapa mnaandika maji yanapatikana Bunda, hayapo, hayapo Bunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu wamekuja watu wa JICA tumewapa taabu kubwa sana, tumewaambia watusaidie kwa sababu kwenye Jimbo langu la Bunda lina ukame mkubwa, wametuambia tufanye bajeti tumewapelekea bajeti ya dola 63,879 ya ukarabati ya marambo yaliyoingiliwa na magugu maji.

Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri mliwahi kujibu hapa Bungeni kwamba mwaka huu mtafanya ukarabati wa malambo sita, iko wapi mzee wangu? Sasa mnafikiria sisi Wabunge tufanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, JICA hawa hawa wamesema tutengeneze malambo, tumewapa bajeti ya dola 255,237.17 tusaidieni basi, tusaidieni kwenye JICA hawa ambao wametuona kwenye tatizo mtusaidie kutusemea watusaidie. Jimbo la Bunda lina ukame wa kutisha, Jimbo hilo hilo ndio lina tembo wanaokula mazao ya watu kila siku, lina watu wana taabu zao kule; tunaomba mtusaidie kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona mradi wa umwagiliaji Bunda. Mradi wa umwagiliaji maji wa Nyatwali hauko Jimbo la Bunda, haupo Wilaya ya Bunda uko Bunda Mjini. Bunda DC kuna mradi wa umwagiliaji wa Maji unaoitwa Mariwanda pamoja na mradi wa Kasugutwa wa Buramba, haiku kwenye bajeti yanu; na kwenye takwimu zenu mnaonesha kwamba Mradi upo Bunda DC lakini upo Bunda Mjini. Kwa hiyo, naomba mlirekebishe hili na mradi wetu wa Mariwanda muufanyike kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu hebu tusaidieni, kama mmepewa hiyo Wizara na hali ndio hii inaenda miaka miwili sasa inaenda miaka mitatu na ninyi wazee ma-engineer mpo hapo, watu wazima ambao tunawategemea mtusaidie na hamna plan mpya ya kukomboa mambo ya maji, tunakaa na ninyi humu kufanya biashara gani? Maana sasa lazima tuwaambie kwamba miaka mitatu ijayo mtuambie mmeingia humu ndani mmekomboa nini au ndiyo zile asilimia mnazoimba tu asilimia 72 wakati hazipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nimeandika kwenu, nimewaleta, kwenye Jimbo langu mnasema kwamba miradi ya zamani iendelee kuwepo; na kwangu miradi ya zamani ipo, endeleeni kunisadia au mnampango wa kuniondoa huko ndani? Mniambie sasa mapema nijue.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuchangia katika Wizara hii. Nianze tu kwa kuipongeza Wizara, Waziri, Mheshimiwa Profesa Maghembe; Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Ramo na watendaji wote wakiongozwa na Katibu, Mkuu Meja Jenerali Milanzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa nchi yetu kwa kuwateua hawa lakini kwa kulinda maliasili ya nchi yetu na kuonesha kwamba ana nia nzuri ya kuendeleza utalii kwa kununua ndege ambazo zitakuwa zinatoa watalii maeneo mbalimbali na kuwaleta hapa kwa ajili ya kuongeza mapato ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze leo kwa kutumia hotuba zote hizi mbili ya Waziri na Kamati, yote ambayo tulitegemea kusema humu ndani hasa mimi naona wamezungumzia maeneo mengi. Nianze kwa kuangalia kitabu cha hotuba ya Waziri, ukurasa wa 17, ibara 36 wanasema:-
“Dhana ya ushirikishwaji jamii katika uhifadhi wa wanyamapori ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanashiriki katika uhifadhi na kunufaika kwa mujibu wa Sera ya Wanyamapori ya mwaka 2007”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye maeneo yangu ya Bunda na kwa bahati mbaya lugha inakuwa tofauti nikisema tembo inakuwa kosa basi niseme ndovu. Nimshukuru Waziri katika msimu wa kilimo wa mwaka jana na mwaka huu wametusaidia kuleta magari na askari ili kuzuia ndovu wasije kwenye maeneo ya makazi ya watu na kula mazao yao. Nina ombi maalum kwa Waziri kwamba kwa sasa wakulima wale wamelima sana na mazao yao yako kwenye hatua nzuri, kwa mwezi wa Tano, Sita na Saba watusaidie kupeleka magari na askari wa wanyamapori ili wananchi waweze kuvuna kwa msimu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu hiki cha hotuba ukurasa wa 19, ibara ya 39 inasema, jumla ya shilingi milioni 567.5 zimelipwa kwa wananchi ambapo shilingi milioni 504 ni kifuta jasho. Miongoni mwa Wilaya zilizolipwa hizo hela ni Bunda, nikushukuru Waziri kwa sababu amewakumbuka watu wa Bunda kwa Vijiji vya Unyari na Kiumbu. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Kijiji cha Maliwanda ambacho kimeathiriwa sana na wanyamapori lakini kwa bahati mbaya katika malipo haya hawakupata na Kijiji cha Sarakwa. Nilishaenda Ofisi kwao wakaniahidi kwamba watafanya marekebisho na hawa watu watapata malipo yao ya kifuta jasho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo nizungumzie hili la kifuta jasho. Mwaka jana katika hotuba hii ya bajeti tumezungumzia marekebisho ya kanuni za wanyamapori kuhusu kifuta jasho. Wanasema kutoka kwenye mpaka, mpaka kwenye eneo ambalo ni kilomita tano kutoka kwenye mpaka ambao wananchi na wanyamapori wanaishi, mwananchi atakayeliwa mazao yake zaidi ya kilomita tano analipwa shilingi laki moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuseme ndovu amekula mazao kilomita arobaini kutoka eneo la mpaka analipwa shilingi laki moja kwa heka moja. Iko sheria pale kwamba kama umelima heka arobani halafu ndovu wamekuja kwenye shamba lako wamekula heka arobaini unalipwa heka tano tu kwa shilingi laki moja. Kwa lugha nyingine unalipwa shilingi laki tano, kwa heka 40 unalipwa heka tano tu heka 35 inakuwa sadaka. Sasa ni vizuri tukaangalia namna gani ya kurekebisha sheria hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia kwenye kitabu hiki namna gani watu wanaozunguka wanyamapori wananufaikana nao. Katika eneo langu la Unyari miaka mitatu iliyopita ndovu walivunja jengo la watoto na akina mama wajawazito. Tukajitahidi kujenga jengo hilo na Serikali ikaahidi kwamba itaezeka na kufanya finishing. Niishukuru Wizara imetoa shilingi milioni 50 jengo lile linaendelea vizuri lakini alipokuja Waziri wa Afya amesema jengo lile kwa sababu tumelijenga vizuri liwe kituo cha afya. Kwa sababu ya sera yetu, nafikiri Mheshimiwa Waziri ni vizuri sasa akatusaidia hela nyingine kwa sababu inahitajika pale shilingi milioni 50 nyingine ili kubadilisha maeneo yale yote yawe kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba tutasaidiana katika jengo hili ili kiwe kituo cha afya na ikiwezekana hata kama litaitwa Profesa Maghembe siyo mbaya ili mradi tu umetutengenezea eneo limekuwa zuri zaidi kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo ya mipaka kati ya vijiji kumi na tano na Pori la Akiba la Grumeti. Mgogoro huu ni wa muda mrefu, tumesema sana na tunafikiri ile Kamati iliyoundwa ya Wizara tatu itafika kwenye eneo letu na kuweza kuangalia mipaka hii. Ipo hoja kwamba mwaka 1994 wakati eneo hilo linachukuliwa kutoka open area kuwa game reserve (pori la akiba), wananchi hawakushirikishwa. Kwa hiyo, tunafikiri kuwa sasa ni muda muafaka kuangalia mipaka hiyo na Kamati imesema ili tuweze kujua ukweli uko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ni kwamba wakati hilo pori la akiba linachukuliwa ambalo maarufu kule kwenye maeneo yangu kama Kawanga kulikuwepo na malambo mawili yaliyochimbwa na wananchi kwa ajili ya kunywesha mifugo. Yale malambo mawili sasa wanyamapori ndiyo wanakunywa maji lakini sisi huku chini hatuna maji ya kunywa. Mheshimiwa Waziri anajua mpaka wetu ni Mto Rubana, sasa watu wakienda katika maji yale wanafukuzwa kwa sababu wakivuka Mto Rubana tu wameenda porini. Kwa hiyo, tulifikiri ni muhimu sana Serikali kuja kuangalia namna ya kuchimba malambo upande wa pili ili ng’ombe wawe wanapata maji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia kero ya mipaka ambayo ni ya muda mrefu lakini kuna vijiji vya Mgeta, Tingirima, Kandege na vyenyewe havikupata huu mgao wa kifuta jasho. Ni vizuri sasa tukaona ni namna gani wanaweza kuzingatiwa, lakini Maliwanda ni kijiji cha kwanza kuzingatiwa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilitaka nichangie hayo, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia. Kwanza nawashukuru Wenyeviti wa Kamati, Mawaziri wote wa Wizara hizi tatu na Watendaji wao na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wanatufanyia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia nijielekeze kwenye Wizara ya Nishati. Wizara ya Nishati kuna maeneo mawili; kuna eneo la Densification na eneo la REA III, lakini yote inatoka kwenye REA. Kasi ya utendaji kazi wa Wakandarasi katika Jimbo la Bunda kwa upande wa densification ni mdogo sana, ninavyozungumza hapa, wako site lakini wanaenda pole pole sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, REA katika vijiji, kasi yake nayo imekuwa ndogo ingawa Mheshimiwa Waziri anafanya kazi kubwa sana ya kuanzisha hii miradi katika maeneo mbalimbali. Nami wakati fulani namhurumia, anatembea sana, lakini Wakandarasi wanaenda slow sana. Sasa, sijui ni upungufu wa hela au ni nini, sielewi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri sasa awahimize hawa Wakandarasi katika maeneo na hasa Wilaya ya Bunda, hususan Jimbo la Bunda katika maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri alikuja akafanya uzinduzi wa Mradi wa REA III katika eneo la Maiwanda katika Jimbo la Bunda. Kwa hiyo, nafikiri ni vizuri Mheshimiwa Waziri akahimiza wakaja kwenye kutenda hiyo kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika REA kuna mambo huwa siyaelewi vizuri. Moja, ni kitu kinaitwa kilometa. Unakuta kuna upungufu kati ya watu wa survey ya TANESCO na survey ya Mkandarasi, TANESCO ukiwauliza, nani amefanya survey ya kumpa Mkandarasi aende kujua Kijiji ‘A’ kila kilometa tatu, kina kilometa moja na Kijiji ‘B’ kinawekewa transfoma mbili na Kijiji ‘A’ kinapewa transfoma tatu au kilometa mbili. Sasa ukiuliza TANESCO, wanasema ni REA; ukiuliza REA, wanakuja na takwimu, hawahusishi wanakijiji wale kujua toka mwanzo kwamba kijiji hiki kitapata kilometa mbili au mtandao wa umeme wa kilometa mbili na transfoma tatu na voti ngapi katika hiyo transfoma. Kwa hiyo, hilo nalo ni tatizo liko hapa, Mheshimiwa Waziri naomba uliangalie vizuri ili tuweze kwenda vizuri katika suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Wizara ya Miundombinu. Kuna masuala ya barabara ya lami kutoka Nyamswa kwenda Bunda na kutoka Bunda kwenda Bramba na Bramba kwenda Kisorya, imechukua muda mrefu sana. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri anayehusika aweze kuiangalia kwa makini zaidi kwenye hiyo barabara. Kuna barabara ambayo inatoka Sanzati kwenda Mgeta na Mgeta kwenda Nata, nayo tunaomba Mheshimiwa Waziri anayehusika aweze kuiangalia vizuri hiyo barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema mambo yafuatayo:-

Kwanza, ni kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Mkoa wa Mara. Sisi Mara hatuna upungufu wa kupata Rais, tumewahi kupata Rais miaka 24, kwa hiyo, hatuwezi kulalamika kwamba Rais amefanya nini kwa miaka miwili iliyokuwepo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kwenda India kumshuhudia mtu anafanyiwa operesheni; kuna operesheni ndogo na kubwa. Operesheni kubwa ni zile zinazohusisha matumbo kwa ndani; unatoa labda figo na vitu vingine. Mtu yeyote atakayekatwa kisu kwa operesheni kubwa lazima agune na lazima arushe miguu. Kwa hiyo, ninachoona wenzangu hapa wanarusharusha miguu, naona kama operesheni ya Mheshimwia Dkt. Magufuli imewafikia. Kwa hiyo, sioni matatizo ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa mambo yote anayoyafanya. Kwanza, ni kutupa Mkoa wa Mara shilingi bilioni 10 za uwanja wa ndege. Kwa mara ya kwanza Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli akiwa madarakani, juzi Waziri Mkuu ametua pale na ndege kubwa. Sasa tunamlaumuje kwa mambo haya? Tunapozungumza, site watu wanaendelea na kazi. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuletea Mkoa wa Mara shilingi bilioni nne kwa ajili ya Hospitali ya Kongwa ambayo imekuwepo toka mwaka 1975. Inaendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Niabu Spika, kwa hiyo, sisi Mara tunamlaumu kwenye jambo gani? Kwa hiyo, mambo mengine yapo, yanaendelea. Naona watu wanarusha miguu tu, lakini hali ya hewa ni nzuri. Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais pia kwa kudhibiti rushwa, kuweka nidhamu ya kazini, kudhibiti wazembe na wala rushwa, kutoa elimu bure, kuanzisha miradi mikubwa ya Stigler’s Gorge na miradi mingine inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunachokiona hapa ni kitu kimoja; wenzetu wameshaona Messi wa CCM ni Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Kwa hiyo, ni lazima mshikeshike miguu. Wana-CCM lazima tukae tayari kumlinda Messi wetu asiumizwe, asilete madhara katika mambo hayo. Kwa hiyo, nafikiri kwamba haya ni mambo ya msingi ya kufanya, lakini naomba Wizara zinazohusika ziangalie Jimbo la Bunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nianze tu kwa kuwashukuru na niseme tu kwamba Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wanafanya vizuri. Nimefuatilia mambo mengi wanayoyafanya na nchi nyingi zinazofanya mambo ya barabara, wanafanya vizuri sana, tunatakiwa kuwashukuru sana. Tumpongeze Waziri Mbarawa, Katibu wake, Naibu Waziri na wote wanaohusika na Wizara hii kwa kweli wanafanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nianze tu na barabara za Mkoa wa Mara na niseme wakati fulani huwa najiuliza sijui kwa sababu mtangulizi wa Taifa hili alitoka Mkoa wa Mara na kwa sababu alikuwa anajumuisha Taifa hili kwa kuliona kama mtoto wa nyumbani kwake na akahusika kufanya maendeleo kwa kila eneo la nchi hii, lakini sasa Mkoa wa Mara kwa maeneo mengi hayaendi vizuri kwa kweli. Ukitazama barabara zetu barabara ya Nyamswa - Bunda tumeahidiwa toka mwaka juzi na iliwekewa shilingi bilioni nane mpaka leo iko kwenye utafiti tu hakuna kinachoendelea hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Buramba inatengenezwa haiendi, barabra ya Makutano - Sanzati haiendi, barabara ya Sanzati - Makutano - Mugumu haiendi, reli ya Arusha - Tanga - Musoma haiendi na Uwanja wa Ndege Musoma hauendi. Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli Mheshimiwa Waziri uutakapokuja hapa uje na majibu kamili kwamba hizi barabara tulizozitaja hapa zinakwenda vizuri na unaandaa namna gani unaweza kusaidia vinginevyo tunaweza kung’anga’ania shilingi yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mawasiliano, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuzungumzia masuala ya mawasiliano, niliomba kata tano, kwa maaa ya mawasiliano, nimepata kata moja kwa mtandao wa Halotel. Kuna vijiji vya Nyangere, Tingirima, Nyabuzume, Marambeka, Nyagurundu vyote havina mawasiliano. Kwa hiyo, nafikiri ni vizuri mnapokuja hapa muone ni namna gani ya kutusaidia, na ndugu yangu Nditiye uko hapo nadhani utanisaidia katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kusema mambo mengine madogo madogo haya lakini ni makubwa kwangu, nashangaa kuona vitu vingi vinazungumzwa hapa, sijui kuna shilingi trilioni 1.5, kuna ngapi, lakini sisi ambao tumeingia humu bado ni wageni kwenye Bunge hili tunajua utaratibu wa CAG unafuata kanuni ya kwenda kwenye Kamati ya PAC ambayo ndiyo inaita watu wote wanaohusika na ile mijadala kule ndani na kuona kile kinachohusika na kama uthibitisho utakuwa haupo ndipo tunajua kwamba hizi hela zimepotea au hazijapotea. Sasa naona watu hapa mishipa imewatoka, trilioni zimepotea, wapi sasa? Nani amekwenda kuthibitisha kwamba hela zimepotea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika report ya CAG tumeona mengi, tumeona kuna vyama hapa vimepoteza hela nyingi, tumeona kuna vyama vingine vimeshindwa kupeleka hela hatusemi wameiba, tunasema ni vitu vimo ndani, kwa nini watu wameshupaa? Lakini mbaya zaidi inaonekana ni kama kwamba hizi hela ni kama vile zimechukuliwa na Rais wakati Rais si mtu wa masuhuli sasa ni maneno gani haya? Yaani kuna vitu vingine vinanga’ang’aniwa kiasi kwamba wakati mwingine huwezi kujua kama vina maana gani hivi. Jamani katika mtu ambae atakuwa wa mwisho kuhukumiwa katika Taifa hili kwamba ni mdhulumati, kwamba ni mwizi, kwamba ni mtu anayekula rushwa ni Rais John Pombe Magufuli, wananchi wanamjua ndiye namba moja kwa uaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara hii sana kwa mambo mazuri sana waliyowatendea wakazi wa Jimbo langu, kama vile ujenzi wa nyumba vya madarasa primary na secondary. Wizara hii imesaidia sana ujenzi wa sekondari ya Makongoro kwa mabweni na nyumba. Shule hii ina kidato cha kwanza na cha sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba shilingi milioni 72 kumalizia ujenzi wa bwalo la Chalanda, watoto wanalia nje, mvua na jua lao. Sekondari ya Mekomariro tunajenga bweni, tunaomba samani za bweni (vitanda, meza na kadhalika).

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni sekondari za Nyamangita, Salama Rihingo na Chamriho, Nyamangutu. Naomba ujenzi wa maabara. Kwa upande wa Salama, jengo la maabara lipo katika kata, tunaomba fedha za kumalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chamriho na Mihingo watoto wanasafiri kilometa 17 kutoka eneo la shule ya sekondari. Tunaomba Wizara mtusaidie maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii, akiwepo Naibu Katibu Wizara ya TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, nilitoa taarifa ya kubomoka na kuanguka kwa shule za msingi Sarawe na Stephen Wasira ambapo watoto wawili walifariki.

Mhshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi kutoa msaada wa dharura kwa shule hizi mbili. Naomba ahadi hii itekelezwe, kwani mwakilishi na Serikali (Mkuu wa Mkoa) kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Elimu waliahidi kusaidia kutoa msaada wa dharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo sugu ambalo liko kimya, tatizo la mikopo ya watumishi na hasa walimu ambao ndio wengi. Walimu wanakopa kuliko uwezo wao, hakuna limit ingawa zipo sheria za mikopo, lakini hazifuatwi. Naomba Wizara ifanye tathmini ya kuhusu jambo hili. Tafuteni udhibiti wa namna mikopo ya mabenki katika eneo la walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya wanafunzi iwe kwa wanachuo toka Diploma hadi Chuo Kikuu na mikopo iwe kwa ngazi zote au mwaka wa kwanza hadi wa tatu bila kujali hakuna mwaka wa kwanza au wa pili au wa tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunashuhudia Wizara hii kwa muda mrefu, lakini kwangu nilichokiona muhimu sana katika hii Wizara ni uadilifu wa Wizara. Uadilifu wa Wizara ya Elimu sasa hivi umekuwa mkubwa sana kwa sababu fedha zote zinazotoka kwenye Wizara zinakwenda chini zinafika salama na zinafanya kazi salama. Zamani ilikuwa fedha zikija huku zinarudi tena Wizarani huko huko lakini siku hizi zinafanya kazi vizuri sana. Kwa hiyo, nisifu uadilifu wa Wizara hii umekuwa mkubwa, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima, Katibu, Naibu na wote wanafanya kazi vizuri sana, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako malalamiko machache ambayo naona pale vijijini kwa sababu vitabu vile vya wanafunzi wa darasa la nne wanafanya mitihani havijaenda, lakini nimepiga simu kule wameniambia ndio vimeanza kwenda. Kama vinaenda kweli naomba vifike salama kwa sababu wanafunzi wanavihitaji vifike kwa wakati lakini tunafikiri kwamba Serikali imefanya vizuri kupeleka hivyo vitabu mapema na vinaendelea kusambazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Jimbo langu la Bunda na hili nimelisema muda mrefu. Wizara ya Elimu imetupa majengo mazuri sana kwenye Shule ya Makongoro ambayo ina wanafunzi wa high school na wale wa kidato cha nne lakini jengo la Bwalo la Makongoro
limejengwa mpaka kwenye lenta limeshindwa kumalizika na fedha yake ilikuwa imepungua. Tunaiomba Wizara itusaidie kwenye hilo jengo ili liweze kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekondari ya Nyamang’unta na Sekondari ya Salama kuna majengo ya maabara yameshindwa kukamilika. Tunaomba mtusaidie ili yaweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Msingi Salawe na Shule ya Msingi Stephen Wassira, majengo yalianguka na watoto wawili walifariki na taarifa zilitolewa kwenye vyombo vya habari na tukatoa taarifa Wizarani, TAMISEMI inajua na Wizara ya Elimu inajua. Mliahidi kutusaidia tunaomba mtusaidie hizo shule mbili ziweze kupata majengo yake kwa sababu watoto walipotea na wananchi walipata mateso ya kuhangaika muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule za Chamriho Sekondari na Mihingo Sekondari watoto wake wanatoka kilometa 17 kutoka eneo la kijiji wanachokaa na wasichana wale wakianza 50 wanamaliza 12 au watano. Kwa hiyo, tunahitaji shule hizi mbili zipate mabweni ili watoto wa kike waweze kusoma katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala muhimu sana ambalo mimi sijui kama mnaliona lakini lina-affect sana hii industry ya elimu kwa maana ya kiwanda cha elimu hiki ambalo ni masuala ya mikopo. Kama hatutaweza kudhibiti mikopo ya mabenki kwa walimu; mwalimu anapokea mshahara wa shilingi 2,000,000 lakini anaenda kupokea mshahara wa shilingi 150,000 na siyo walimu tu na watumishi wengine wote wa Serikali hii, kama hizi sheria za mikopo za mabenki kwa watumishi wa Serikali hatuwezi kuzidhibiti vizuri maana yake ni kwamba hakuna uaminifu utakaokuwepo. Ni lazima tuone mshahara unabaki kama sheria inavyosema. Mtu anapokea mshahara shilingi 300,000 anapokea shilingi 50,000 wengine wanapokea shilingi sifuri. Kwa hiyo, tufanye tathmini ya kujua hii mishahara ya watumishi na hasa walimu ambao wakati fulani hawana hela za akiba tuone tutadhibiti vipi ili walimu waweze kutumika vizuri kwenye shule zetu.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni kiwanda na tatizo liko hapa elimu yetu nzuri au mbaya? Ili kutambua elimu nzuri au mbaya ni namna gani tunazalisha? Je, tunazalisha watu wenye ubora kulingana na soko lilivyo au ni watu wasio na ubora kulingana na soko? Kwa sababu unaweza kuzalisha jambo, kwa mfano sasa hivi tunazungumza habari ya viwanda na kama tunazalisha watu wa historia, tunazungumzia watu ambao hawako kwenye mambo ya ustawi wa jamii na kwenye mambo ya ufundi kama walivyosema wenzangu, shule za ufundi hazipo, hivi tunalenga nini hasa?

Kwa hiyo, kwenye soko letu tunakokwenda huku mbele halitakuwepo, hatutapata watumishi wanaoweza kwenda kwenye viwanda. Elimu inataka unazalisha nini, ni suala la demand and supply. Kwa hiyo, tuweze kujua kwamba elimu yetu hii tunayozalisha watoto wakoje, ndiyo hilo wanasema quality education na quality in education, ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, tuangalie michango yetu inakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la matangazo la Baraza la Mitihani. Mimi huwa mara kwa mara najiuliza sana, mtu anakaa pale kwenye tv anatangaza, mitihani kidato cha kwanza au mitihani primary shule bora, St. Mary, St. Augustine, sasa unalinganisha na nini? Shule yangu ya Mihingo ina mwalimu mmoja toka inaanza. Shule yangu ya msingi watoto wanasoma nje, wana matatizo mbalimbali, unakuja kusema imekuwa ya mwisho kwa kulinganisha na nini, unalinganisha nani sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwamba mambo haya tuweze kuweka categories ili tulinganishe maana sasa hii mitihani tunalinganisha na nani? Huyu amekuwa bora kwa kulinganisha na nani? Hivi kweli leo unaweza kuleta hapa Barcelona ukasema inacheza sijui na Yanga halafu useme imekuwa ya kwanza eti kwa sababu tu ni sheria inaruhusu?

Kwa hiyo, nafikiri hata mitaala hii nayo tuiangalie upya wakati fulani haileti maana sana kwenye mambo haya ambayo yanakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule nyingi tumezungumza kwenye mambo ya sera. Mimi nafikiri huo mfumo unaouzungumza kwamba kuwepo na kongamano zito, alizungumza Mzee Mkapa, akazungumza Mzee Jakaya na hata Mheshimiwa Magufuli akitoka mtasema Mheshimiwa Magufuli alizungumza. Kwa hiyo, nafikiri kwamba hii mijadala hii iendelee kuwepo na hakuna mtu anazuia mjadala, nami nawaomba Wizara ya Elimu pale watu wanapotaka kufanya mijadala ya elimu basi tuwaunge mkono ili tuweze kuona kitu bora tutakachokuja kufanya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia jioni ya leo katika bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchangia Wizara hii ya Maji kwangu mimi naomba Mungu anisaidie nipate akili ya kusema vizuri kwa sababu ninaweza nikaruka humu Bungeni. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu aliwahi kusema ni bora kuongoza maskini mwenye matumaini kuliko kuongoza maskini asiye na matumaini na maskini mwenye matumaini ni yule aliyelima mihogo au ana shamba anaweza kumkopa mwenzake fedha kwa kumuomba kwamba mahindi yake yakifika atauza atamlipa lakini yule ambaye hana kitu kabisa huyo ni maskini asiye na matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge hili mimi naona ni maskini nisiye na matumaini maana kila bajeti inayokuja sioni kwenye Jimbo langu la Bunda kuna chochote mle ndani. Kwa hiyo, inavyofika wakati huu naona kwamba hivi Bungeni humu nafanya biashara gani humu ndani? Si bora tu nitoke nikachunge ng’ombe huko? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Bunda na Bunda kwa ujumla kuna miradi mbalimbali na mimi nashangaa watu wanasema hamna fedha, nadhani fedha zipo ila usimamizi wake ni kidogo sana au tuna ugonjwa unaoitwa D by D, hii ambayo wataalam wametupatia. Wizara ya Maji inatoa fedha kwenda kwenye Halmashauri, mamilioni ya fedha yanaenda, watekelezaji wa miradi ile ni watu wa TAMISEMI, wahandisi wako TAMISEMI na pengine hata Waziri wa TAMISEMI au Naibu wake, watumishi wake hawajui fedha ngapi imeenda huko, inajulikana kwa Wizara ya Maji tu peke yake. Waziri wa Maji anapokwenda kukagua maji anakuta fedha zimeliwa. Ukimuuliza Waziri sasa huyu achukuliwe hatua gani anakwambia mimi hao siyo wangu mpaka niende kushauriana na Mheshimiwa Jafo, hii biashara hatuiwezi hii, hii biashara itakuwa ngumu sana.

Kwa hiyo, ni vizuri tukaangalia huu ugonjwa wa D by D tunaufanyaje katika hizi Wizara mbili, vinginevyo tutapata shida sana na ndiyo maana tumeshauri hapa mara kwa mara kwamba Wakala wa Maji Vijijini uwepo ili Waziri apewe vitu vyote, fedha na watu wake aweze kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie miradi ya Wilaya ya Bunda kwa ujumla, tuna Mradi wa Kibara shilingi milioni 400, zimetumika pale kama shilingi milioni 300 na zaidi maji hayatoki, lakini kwenye taarifa utaonesha maji yanatoka. Kuna Mradi wa Buramba, shilingi milioni 353, maji hayatoki, kuna Mradi wa Kinyambwiga shilingi milioni 395, maji hayatoki, kuna Mradi wa Kwing’ombe shilingi milioni 700, mradi umeisha na Mwenge ukafungua, maji hayatoki, kuna Mradi wa Nyamswa Salamakati, shilingi milioni 252 zimetumika, maji hayatoki, kuna Mradi wa ufadhili wa Bomamaji, walikuja wafadhili pale Bomamaji wakatoa shilingi milioni 987 zimeliwa, ripoti ikatolewa haifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mkubwa wa maji wa Bunda ambao bomba lake linatoka Nyabeho nao unasuasua. Mbaya zaidi kuna mradi wa Mgeta, Nyang’aranga zikatolewa shilingi milioni 495 zimefika shilingi milioni 910 maji hayatoki na Waziri ameshafika pale akiwa Naibu Waziri. Sasa hili linakuwa ni tatizo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi ni kwamba ukimuuliza Waziri hapa nimezungumza habari ya malambo kule kwetu sisi Bunda malambo hayo ndiyo visima tunaita, ndiyo ng’ombe na binadamu wanakunywa. Tukamwambie atutengenezee malambo ambayo yalitengenezwa na Chifu Makongoro yatatusaidia huko tunapokwenda, akakubali hapa Bungeni kwamba atatengeneza hayo malambo akasema leteni mpango. Tumepeleka mpango tukamkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara, kuidhinisha huo mpango uende kujengwa ukija kumuuliza Waziri anakwambia malambo sichimbi mimi, anachimba Wizara ya Kilimo lakini Wizara hii ya Maji ndiyo yenye malambo. Sasa najiuliza hii ni kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba kiasi cha shilingi bilioni moja bajeti ya 2016/2017 hatukuitumia, Halmashauri ya Bunda haikupata taarifa. Bajeti ya mwaka 2017/2018 tumewekewa shilingi bilioni moja tumeleta mpango wa maji wa malambo sita hayachimbwi wala hamna kibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Bunda una mradi mkubwa wa maji na kuna kitu kinaitwa chujio. Mimi nimwombe Waziri, pale wanasema kuna shilingi bilioni 12, wanasema ni nyingi labda hizi ni za wizi. Sasa kama ni za wizi ngapi zinatosha sasa kwa sababu katika kuchimba, mimi siyo mtaalamu lakini katika mambo ya kuchimba hilo chujio kuna vitu vinaitwa clarifier, flocculant, rapid stand, refilter, mitambo na kuna vitu vingi mle ndani. Wataalam wa Wizara si waende waangalie kwamba ni fedha ngapi zinatosha kuweka hiyo chujio. Kwa sababu maji ya Bunda kila siku yanaletwa maji machafu, kila Waziri anayekuja mnanywesha maji machafu kwa nini sasa msipeleke wataalam watuambie hili chujio badala ya shilingi bilioni 16 ni bilioni ngapi? Wakati fulani tunaweza tukawa tunawalaumu watu tu kwamba mkandarasi amekula, amefanyaje, twendeni tukajiridhishe na mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze habari ya fedha, tumezungumza mwaka jana kwenye bajeti Sh.50 kuongezeka kwenye mafuta kwa ajili ya kupata fedha za kuhudumia maji lakini imekuwa wimbo. Sasa Wabunge tukubaliane, wakati fulani mimi nasema na tutaendelea kusema, humu ndani tukifa wote watasema Wabunge wa Tanzania wamekufa, hawatasema CCM wala CHADEMA. Ifike muda tukubaliane kwamba kwenye mambo yale ambayo tunakubali ni halali tuache UCCM wala UCHADEMA tukubaliane hoja. Kwa nini tunaweka shilingi 50 kwenye mafuta iende kwenye maji halafu haiwekwi, nani anaizuia na sisi ndiyo wawekaji wa fedha? Kwa hiyo, nafikiri Waziri anapokuja hapa atuambie anafanyaje kuhakikisha kwamba hiyo fedha kwa kipindi hiki itakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri, najua wakati fulani tukisema haya mambo yanamgusa Waziri, Naibu na watendaji wake, lakini watu hawa nao ni wapya. Hebu tuweke mtazamo mzuri, hivi Waziri anaposema shilingi bilioni moja imekwenda Bunda, lakini haikutumika, anatulaumu sisi Wabunge, hivi nani ana utaratibu wa kuwaambia Halmashauri fulani kwamba jamani kuna fedha zenu hapa mbona hatujaona proposal yenu ya kuanzisha miradi? Kwani wataalam wa Wizara ya Maji wana kazi gani? Kwani nani anaweza kujua mradi Bunda iko miradi mitano wanaandika imekamilika lakini haitoi maji, nani anaweza kujua? Ina maana Wizara ya Maji haina watu wa IT ambao wanaoweza kujua vitu hivi? Siku hizi watu wanafanya vitu kwenye computer kwa nini haya mambo hayafanyiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua bajeti tutampitishia Mheshimiwa Waziri najua na wewe una bidii sana ya kufanya kazi lakini mimi kwangu uadilifu si hoja. Kwangu mimi mtu awe mwadilifu na awe mbunifu. Unaweza kuwa na mwadilifu anakaa na hela tu kwenye droo hapo watu wanakufa bila maji. Kwa hiyo, tunajua Waziri wewe ni mwadilifu jitahidi kufanya innovative na creative kwenye ofisi yako ili watu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe ile proposal yangu ya Bunda ya malambo, sisi malambo ndiyo visima, atupitishie ili watu wakapate maji. Toka mwaka 2008 hii miradi imeanza kuzungumzwa humu ndani na bajeti zinakuwepo, lakini haitekelezeki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza niwashukuru tu watendaji wa Wizara tukianza na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, watendaji wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii kasoro wale tu wanaodhulumu ng’ombe hao siwezi kuwashukuru hao ambao wanadhulumu ng’ombe.

Mheshimiwa Spika, naliona jambo moja muhimu sana ambalo unaweza ukalifanya wewe kwa ujasiri wako. Wizara tulipokuja hapa Bunge hili tulikuwa tunataka kushughulikia masuala ya wafugaji na ardhi ya migogoro ya mipaka. Zikawekwa Wizara tano kushughulika matatizo hayo, zimeshindwa, zimeshindwa kushughulika matatizo ya wananchi katika mipaka na mapori. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nakuomba wewe sasa ama uunde Kamati Maalum ya Bunge kushughulikia migogoro hiyo au ukiona hilo ni gumu utuachie Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii washughulikie hiyo migogoro. Kwa maana sasa watendaji wa Maliasili wanaoshughulika na mapori ya akiba na hifadhi wanachokifanya ni kile ambacho umekizungumza sasa hizi hapa wanakwenda na ramani, hata kama hiyo ramani mipaka yake ya asili ilikuwa Bahi, lakini ramani yao inaonesha wamekuja vigingi UDOM, watafika UDOM halafu wanamwambia mwanakijiji vigingi vyetu vipo hapa kwa hiyo tuamue hapa. Haliwezi kuisha, hauwezi kuachia mgogoro wa mtu aliyeweka mwenye mali halafu aamue mgogoro wake, haiwezekani.

Kwa hiyo, tukubali sasa ile Wizara ya Ardhi na zile Tume zilizounda zimefeli. Sasa ni jukumu lako uunde Tume au uwaambie watu wa Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii waendelee ku-solve hiyo migogoro uwape mamlaka hayo, nilikuwa nafikiri kwamba hilo ni la maana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la Stiegler’s Gorge nilikuwa naliona kwangu kwa mawazo yangu, kwa sababu wafadhili hawawezi kujenga ule mradi, kama Serikali yetu ina uwezo wa kujenga huo mradi na wana fedha za kujenga huo Mradi wajenge na kama fedha hizo za mradi huo zitahujumu maeneo mengine ya miradi kwa mfano kwenye kilimo, ardhi, viwanda kama fedha zetu hazitoshi kujenga Stiegler’s Gorge kwa maana kwamba tuna mambo mengine yanagusa wananchi tuangalie upya juu ya mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake isije ikawa tukachukua fedha zote kama hatuna ufadhili tukazipeleka kwenye Stiegler’s Gorge halafu maeneo mengine ya nchi yakaathirika na mradi huo. Lakini kama ni mazingira, mimi mwenyewe nimesoma mazingira, mazingira yapo kwa ajili ya binadamu na binadamu yupo kwa ajili ya mazingira. Habari ya kukata miti milioni ngapi hiyo sawa, lakini miti mingapi tunakata kwenye nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuangalie kama tuna fedha ya kujenga hiyo ndo muhimu ili maeneo mengine haya tusije tukamalizia fedha. Kwa sababu wafadhili hawapo tayari kufanya ule mradi, nimeusoma muda mrefu wafadhili wamekuwa wakitukataza mambo mengi tu hata barabara ya Loliondo, hata maeneo ya kujenga viwanja vya ndege hata nini hawajengi viwanja hivyo. Kwa hiyo, suala ni moja tu tukubali tu Wabunge watuambie na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ituambie ina fedha za kujenga? Je, fedha hizi hazitaathiri maeneo mengine ya uchumi wetu? Basi hilo ndiyo jambo muhimu la kufanya kwenye mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumza kwenye maeneo yangu ya Bunda kwamba niwashukuru Wizara wamekuwa wanafanya maendeleo kwenye maeneo yanayozunguka vijiji vinavyozunguka mbuga za wanyama, niwashukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kunijengea Kituo cha Afya Kunyali, wanafanya maendeleo, niwashukuru Wizara kwa kuleta barabara zile za kuvuka vijiji 15 vya kwangu havina uwezo wa kwenda porini kwenye eneo la Serengeti wamesema watafungua barabara ya kutoka Mgeta kwenda kule. Nimshukuru Mtu wa TANAPA, ndugu yangu Kijazi kwa kuona hili kwamba sasa mnaenda kufanya maendeleo kwenye maeneovijiji vinavyozunguka maeneo yanayotuzunguka hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru kwa mpango wenu wa kupima vijiji vinavyozunguka maeneo haya ili vipate hati waweze kufanya biashara na mambo mengine na vijiji vyangu 15 mmsema vitakuwemo katika vijiji hivyo Unyali, Mgeta, Maliwanda, Kihumbu na maeneo mengine ambayo amezunguka maeneo haya. Niwashukuru sana kwa mpango huo ambao mtaufanya kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna zile vitu vya buffer zone, sasa buffer zone nashangaa buffer zone za National Park au Hifadhi ya Taifa kwa maana Mapori ya Akiba, TAWA na TANAPA zinakwenda kuweka kwenye maeneo ya vijiji mpaka ambao siyo wao, wao wanaweka mipaka kwa nini sasa? Kwa nini buffer zone isiende kwenye upande wako wewe? Nadhani kwa kuunda hiyo Kamati ambayo tumeisema tutashughulikia matatizo kama haya nadhani yanaenda kuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla niseme jamani timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga vizuri. Kigangwalla wanaweza wakakutafsiri kwa maana umekaa kimya upo hivi, lakini una uwezo wa kufanya kazi, Naibu wako anauwezo wa kufanya kazi, Makatibu wana uwezo wa kufanya kazi kwa hiyo tuwashukuru waendelee kufanya kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza shukrani zangu za dhati kwa Wizara hii, kwa kazi nzuri inayofanywa na watumishi wa Wizara hii kuanzia Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, AGP na watumishi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iwe inakumbuka ahadi zake Budget 2015/2016, 2016/2017, niliomba fedha za ujenzi wa vituo vya polisi, Nyamuswa na Mugeta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya makazi ya nyumba za askari polisi ni mbaya sana, tunaomba suala hili Serikali ilione na kulifanyia kazi haraka. Jimbo la Bunda ni wakulima wa pamba, naomba Kituo cha Polisi, Kata ya Haonyori, ambayo wakazi wake ni wakulima wazuri wa pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba askari watumie weledi wao wakati wa kufanya operation. Tarehe 12 Novemba, 2018, kulitokea mauaji ya watu wawili katika mapigano ya vijiji viwili, Remung’orori na Mekomariro lakini askari waliokuja kufanya operation katika tukio hili, walichukua bidhaa zote madukani, walikunywa bia zote katika baa na kupekua masanduku na kuchukua fedha clip zipo na tukio hili siyo zuri, askari watumie weledi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea. Ni dakika ngapi Mheshimiwa?

SPIKA: Dakika kumi.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa hizo dakika kumi.

Mheshimiwa Spika, nchi zetu za Afrika zilikuwa zinatawaliwa na wakoloni kwa miaka mingi tu ikiwemo Tanzania nayo ilitawaliwa na Waingereza lakini kwa sasa wakoloni hawawezi kutawala nchi za Kiafrika, kilichobaki ni kuwatawala katika fikra zao yaani fikra za Waafrika wengi viongozi wengi na hasa wasio kwenye chama tawala wamekuwa colonized na Wazungu. Ndiyo maana utawakuta wapo maeneo mbalimbali wanazungumza mambo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu gani? Nilikuwa naangalia hapa kwenye takwimu mbalimbali wanasema top ten best performing President in Africa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli yumo. Ana miaka mitatu tu toka ametawala nchi hii lakini ameingia ni wa nane, amemzidi mpaka wa Rwanda miaka mingapi ametawala? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa natazama mtu anazungumza mambo ya Stiergler’s Gorge namshangaa. Nataka ni-declare interest kwamba mimi nimesoma diploma, certificate na degree ya mazingira. Sheria ya Mazingira inasema hivi utawale mazingira na mazingira yakutawale. Ukiangalia nchi zote duniani zilizoendelea zina mabwawa ya hydroelectric power; Marekani, China, Uingereza zote wanayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja tu, China sasa ina mahali panaitwa Gorges Dam capacity yake ni MW 22,500. China imechukua mito kama mitatu imekusanya yote, ina watu bilioni sijui 3 leo tunazungumza Tanzania MW 2,400 watu ng’e, ng’e, ng’e, hivi wamekuwaje? (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, Marekani wana bwawa linaitwa Grand Coulee Dam, capacity yake ni 6,809. Sasa Marekani wametengeneza mto unaitwa Colombia, ule China unaitwa Yangtze, leo wale waliokuwa-colonized kwenye akili they are talking about mambo ya wazungu, sasa akili gani hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe tu angalizo, nampenda sana rafiki yangu Msigwa na tupo Kamati moja, mimi Mungu alinisaidia kuwa mkweli, ni vizuri tuwe wakweli. Kwanza amezungumza kwamba kwenye Kamati yetu hakuna taarifa lakini taarifa hiyo imo. Kamati imempongeza Rais kwa kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi nchini. Wewe ulitaka tuseme kwamba wamenyang’anya mashamba ya Sumaye? Rais anapofanya kazi nzuri ni kumpongeza. Naishukuru Kamati yangu ya Ardhi imefanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, tumempongeza Rais kwa kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Rais hanyang’anyi watu mashamba na Rais yeye hafuti umiliki. Nataka nitoe mfano, Bunge lako ndiyo linatunga sheria, leo mwanafunzi wa darasa la kwanza, la pili au la tano akiulizwa nani anatunga sheria za Tanzania watasema Bunge la Tanzania lakini hizo sheria haziwezi kwenda kufanya kazi bila Rais kupitisha. Kwa hiyo, Rais akipitisha ndiyo inakuwa sheria. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, matatizo ya hawa jamaa ndiyo hayo hayo, yaani wao ni kukuza maneno, Mwenyekiti wetu sisi anafanya kazi nzuri, kama amejiuzulu, amejiuzulu kwa utaratibu wa kawaida wa watu kujiuzulu. Mimi nampongeza Mwenyekiti kama amejiuzulu kwa utaratibu wa kawaida basi sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee, hakuna siku kwenye Kamati yetu na Mwenyekiti wangu yupo hapa tumewahi kuita watu wenye mashamba walionyang’anywa wakalalamika, tumeita watu wa porini, tourism na watu wa kila mahali, Kamati tuna majina.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, tuna orodha ya mashamba mengi nchi hii yanayotegemea kufutwa na mengine yamefutwa na sheria iko wazi…

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nadhani huyu ana jambo analo kichwani ndiyo linalomsumbua, kwa hiyo, tuendelee na utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuja na orodha ya mashamba yanayopendekezwa kunyang’anywa au kufuta miliki siyo kuleta wadau waliolalamika. Ni kweli kwamba Kamati ilikuja na mashamba mengi tu ya wakulima wadogo na wakulima wakubwa. Sheria ya Ardhi iko wazi inakutaka ukipewa uwekezaji miaka mitatu uwe umeendeleza.

MBUNGE FULANI: Ndiyo.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Sheria hiyo inasema tukitaka kunyang’anya shamba tutakupa siku 90 za kujitetea. Nani aliwahi kuleta hiyo barua wewe ukaiona? (Makofi)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, niombe nchi yetu tufanye kazi moja kuwaelimisha Watanzania waelewe nini maana ya kuwa mzalendo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nianze kwanza kwa kuzishukuru Kamati zote mbili, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo. Vilevile niwapongeze Wajumbe wa Kamati hizo na Mawaziri walioshughulika na Kamati hizo kusaidia kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natazama vitu katika Kamati hizi na nimeona kuna jambo nataka nilizungumze la Kamati Ndogo kuhusu kile kipengele cha Kodi ya Majengo. Kipengele hiki cha kodi ya majengo wakati kinatekelezwa katika maeneo yetu kimekuwa na vitisho vingi sana. Kwa hiyo, naomba wakati wanafanya ufuatiliaji wa kipengele waangalie kwa sababu huko vijijini kuna nyumba za nyasi na nyumba za bati, ilifika wakati ukijenga nyumba ya bati unadaiwa kodi, ikaonekana kama ni Kodi ya Kichwa hivi. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie vizuri kwenye kodi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Taifa ni letu wote na kama kuna watu wana ndoto kwamba nchi hii ni ya Rais John Pombe Magufuli na chama chake na wako tayari kuiharibu kwa wakati wowote wanavyotaka kwa maslahi yao watakuwa wamekosea sana. Hotuba nyingi zinazokuja hapa hata ya ndugu yangu hapa Mheshimiwa Kubenea anauliza habari ya ma-DED kwamba ni makada wa CCM, lakini hapa tuna Wabunge zaidi ya 100 kwenye uchaguzi uliopita na wametangazwa na ma--DED hao wanaosema ma-DED wa CCM. Sasa DED amemtangaza kuwa ameshinda, amekuja Bungeni halafu anamsema ni mbaya, sielewi kinachoendelea huko mbele katika mambo kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi yanazungumzwa hapa. Nilikuwa natazama sana wakati Rais wa United State, Trump, alivyo-tweet juu ya White House, kuhusu ya Wazungu wale weupe wa South Africa kwamba anataka kuwalinda wale Wazungu kwa maana ya ardhi ya South Africa. Nikamtazama Julius Malema, nikamtazama Ramaphosa ambaye ni Rais, wote walikusanyika pamoja kutetea ardhi ya South Africa bila kujali upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimuona Malema alienda mbali zaidi anawaandaa wanachama wake anawaambia tuko tayari kufa kwa ajili ya ardhi yetu, hatuko tayari kutoa ardhi yetu kwa sababu ya umasikini wetu au kwa sababu hatuna uwezo wa kufanya jambo hili. Huyu ni mpinzani wa South Africa lakini nchi yetu leo hata tungezungumzia habari ya kugeuzwa kuwa wanawake tayari watu wanatetea. Mimi sielewi kama katika nchi hii hali ya hewa inavyoenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanazungumza democracy lakini wanashindwa kutofautisha democracy and futures of democracy…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa heshima ya Paroko nafuta hilo neno, tunaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine wakati fulani unaweza ukaongea hata ukachanganyikiwa kwa sababu leo kama tuna watu ambao ni Watanzania wanaodhani kwamba Rais au utawala wa nchi hii ambao tuliupata bila kumwaga damu na kuna watu walihangaika kuupata kwa kuzunguka tukapata uhuru, leo ni mwaka wa 48, wanadhani kwamba nchi za Ulaya, za Mabeberu wanaweza kuamrisha Watanzania wakampa mtu Urais kwa kupitia nchi za Ulaya, haya ni mambo ya ajabu na ya aibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais aliyekuwa maarufu sana hapa duniani na Afrika, Nelson Mandela, alifungwa miaka 27. Alipotoka jela wala hakwenda Ulaya kutafuta Urais, alikaa kule kwake na wala alipotoka jela wala hakutafuta nani alimweka jela. Alikaa kwenye nchi yake akawaambia uhuru tunautafuta na uhuru akapewa na Wazungu waliomweka ndani miaka 27 akaishi nao, ni historia kubwa sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mtu akikosewa dakika mbili, dakika tatu, imekuwa matatizo. Leo tuna Rais bora kabisa katika nchi za Afrika, ameandikwa humu ndani ukisoma, ana miaka mitatu lakini ameandikwa anafanya vizuri. Leo nchi yetu ni ya 10 kwenda kwenye uchumi bora katika nchi za Kiafrika. Sasa leo wanapita tu wanachafua nchi yetu ambayo ni yai letu la kulea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wale wote ambao wana mawazo hayo warudi tufanye kazi ya ndani wasichanganye demokrasia na utekelezaji wa demokrasia. Kama kuna utekelezaji mtu anazungumza ni watu wanafungwa na kesi zinacheleweshwa, mmeona juzi Mheshimiwa Rais ameteua Majaji na anaendelea kuteua ili mambo ya kesi yaende vizuri na mambo mengine pia tunaendelea kuyatendea haki, mfano, uchaguzi tumechagua vizuri na tunaendelea kuchagua. Tunapozungumzia demokrasia maana yake nchi yetu inatekeleza demokrasia. Tumechagua Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani, Wabunge na Rais hiyo yote ni demokrasia, sasa demokrasia inayozungumzwa ni ipi, mimi sielewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wasilete hofu kwamba utendaji mzuri wa Mhesimiwa Dkt. Magufuli watakosa vyeo, ukikosa cheo ni Mungu ameamua, siyo wewe sasa. Mungu akisema wewe huwezi kuwa Mbunge huwezi kuwa Mbunge. Kwa hiyo, tukubali kwamba nchi ni yetu tumsaidie Rais afanye kazi vizuri ili tuendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, chama ni chenu na Ilani ya Uchaguzi inayotekelezwa ni yenu, tufanye kila namna tumsaidie Rais afanye kazi yake vizuri. Pale ambapo tunahitaji kumshauri, tumshauri vizuri, pale tunapotakiwa kutenda, tutende vizuri. Tukianza kuwa tofauti maana yake ni kwamba chama chetu kinakwenda kufa, kwa sababu aliye na dhamana ya kusimamia Chama cha Mapinduzi kwa sasa ni Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Huyo ndiye mchezaji wetu wa Chama cha Mapinduzi, tukimyumbisha wakamkanyaga mguu ukavunjika maana yake chama chetu kinaenda kupata matatizo, kwa hiyo, lazima tumlinde kwa heshima zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru tumeupata, nchi yetu ipo, ina miaka 48 na ina sifa, ni nchi pekee duniani yenye Muungano. Nataka niwakumbushe watu, tusipokuwa watetezi wa mambo mazuri tuliyoyafanya, kama mwaka 1995 Muungano wetu ulivyotaka kuyumba, asingesimama imara Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere, akaita Bunge na Halmashauri Kuu ya CCM na tukakubali kuendelea na Muungano leo Muungano usingekuwepo. Kama hatuwezi kuungana kutetea nchi yetu maana yake wote tunaweza kwenda kwenye matatizo. Nchi yetu ni ya amani na watu wetu hawakuzoea mabomu na timbwilitibwili nyingi, kwa hiyo, tunaomba watu wawe na amani na tuombeane amani ili tuweze kuishi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kusema kwamba suala la kum-support na kumpa nguvu za kutosha Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Pombe Magufuli sio la majadiliano tena, ni suala la kumuunga mkono kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kila kitu. Na yale anayoyafanya hayawezi kutufaidisha sisi tuliopo, yatawafaidisha wanaokuja na huku mbele kama wenzetu wa upande wa pili wa Gaza kama watakuja kupata nafasi watafaidi haya matunda ambayo Rais anayafanya kwa sasa, kwenye miaka milioni 200 inayokuja huko mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze mambo matatu leo, la kwanza nataka nizungumze habari ya TANAPA. Shirika hili linatunza hifadhi 16 lakini hifadhi zenye faida ni tano tu, na juzi tumeongeza hifadhi nyingine za BBK, Burigi, Kimisi na hifadhi nyingine zimeongezeka nyingi, hifadhi tano ndiyo zenye faida. Na sasa shirika hili lina michango na kodi ambayo inalipwa kodi ndani ya kodi, likitoa mchango wa kujenga Kituo cha Afya Hunyari, Bunda kodi inakatwa, likilipa cooperative tax ndani ya kadi inakatwa, na tumezungumza sana na Kamati ya Bajeti nadhani imepewa hiyo taarifa. Ninafikiri Serikali ione namna gani ya kulipunguzia hili shirika hizi kodi ndani ya kodi ili liweze kujiendesha lenyewe kwa sababu lina mzigo mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote mashirika kama haya huwa yanapewa ruzuku lakini TANAPA inajitegemea, kwa hiyo naomba waipe nafasi ili iweze kuleta namna ya kujenga miundombinu kwenye maeneo mbalimbali ili tuvutie wawekezaji na kuleta watalii wengi kama inavyoonesha kwenye hotuba ya Waziri Mkuu kwamba wameongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 67 fursa za ajira, lakini nikasoma Mpango wa Maendeleo wa Taifa ukurasa wa 23 unasema; upatikanaji wa pembejeo, hatua iliyofikiwa ni kununuliwa kwa lita elfu mbili mia mbili sitini na tisa elfu na kilo elfu tatu vya viatilifu zenye thamani ya shilingi bilioni tisa na hivyo viatilifu vya bilioni tisa vinaua panya, nzige, wadudu viwavijeshi, sasa mimi leo nataka nizungumze fursa ya viwavijeshi na fursa ya vipepeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya leo kuna soko la mende, kuna soko la panya, kuna soko la mbwa, kuna soko la kwerea kwerea ambalo tunatumia bilioni tisa kuwaua, kuna soko la senene, kuna soko la kila kitu. Nchi yetu tumegawana katika maeneo mawili, eneo moja lina asilimia 36 ambayo ina mambo ya mapori haya, Mapori ya Akiba, TANAPA, maeneo tengefu na maeneo yote yaliyoko hapa. Eneo 64 ni letu sisi tunaotumia Watanzania, sasa kama tunalitumia tuna vitu vinaitwa mende, nyoka, mbwa, vinatakiwa kupata masoko ya nje, tutafute namna ya kufungua masoko hayo vinginevyo tunaua ajira, wamezungumza hapa ukurasa wa 67 fursa ya ajira tunatafuta fursa ya ajira katika mende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mende leo ni zao kubwa sana Brazil, ukifuga mende wewe ni bilionea, kwa mfano mkate mmoja Brazili ni laki moja ambayo ni dola 44,000.4 ya Brazil ambayo ni sawasawa na laki moja na watu wanafuga mende sasa hivi wameanza kufuga Njombe. Leo tunapozungumza nyoka tunazungumza soko kubwa sana na viwanda vikubwa sana China. Kwa hiyo, tunafikiri kwamba kuanza leo watu wafuge nyoka kupeleka huko. Tunapozungumza kipepeo leo ni nafasi kubwa sana Malaysia na maeneo mengine.

Kwa hiyo tunapozungumza Kwelea kwelea, mmoja ni dola mia mbili hamsini ambayo ni pesa nyingi sana. Sisi tunasema tunatumia bilioni tisa kuua wadudu na kibaiologia na mimi ni mtu wa environment, unavyotumia ndege kuua wale wadudu maana yake unaua vyura vinavyohitajika, unaua nyoka wanaohitajika kule chini, unaua nzige wanaohitajika huko juu. Kwa hiyo, tunataka kujua ni namna gani eneo la uwekezaji litatumia viumbe hai hivi vilivyopo hapa kutengeneza njia kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wakenya wanashirika la KWS ambao wanatumia vibali hivi, kwa hiyo wenzetu wanatumia leo wanyama wetu hai, wanatumia mbwa, nyoka na membe kufunga katika maboksi kwenda nje. Kwa hiyo, tunaomba sasa Serikali najua Mheshimiwa Rais aliwahi kusema katika mambo, wakati huo tunafanya mambo ya ovyo, nasema yalikuwa mambo ya ovyo kupeleka twiga nje na wanyama wengine, lakini mzee alivyokuwa anakemea nchi sasa nchi imetulia, arudi aangalie ni fursa gani sasa ipo ambayo watu wanaweza kuitumia bila kuangalia mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumza hilo ili ieleweke kwamba kuna kuna soko kubwa sana la Afrika la wanyama hao. Pia kuna kitu kinaitwa konokono, Ghana ni chakula kibwa sana konokono na konokono kama mnavyomjua tunaita ni double entry anajizalisha mwenyewe, female and male yaani ukimfuga konokono mmoja akila majani mazuri hahitaji mume wala mke anajizalisha mwenyewe, anapata soko na ni dola elfu 25. Kwa hiyo ukienda Ghana ni soko kubwa sana kwenye maeneo hayo. Hivyo, naomba hili tatizo tusiogope kutafuta fursa ya mambo ambayo yapo wazi, tulizungumze wazi na vijana wapate ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia habari ya jimboni kwangu. Sisi kule jimboni tumejenga maboma tisa ya maabara za sekondari hayajamalizika kwa sababu nguvu za wananchi zimekuwa kubwa kwenye maeneo haya, tunaomba sasa maeneo yanayohusika waweze ku-support wananchi wa Jimbo la Bunda kwenye mambo ya maabara waweze kupata nafasi ya watoto wao kusoma sayansi ambapo kwa sasa sayansi inakuwa ngumu sana kuisoma kwa sababu maabara hazipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la barabara, ambapo barabara ya kutoka Nyamswa kwenda Bunda haijatangazwa na ni muda mrefu sasa tumekuwa tukisema barabara hii itatangazwa itapata mkandarasi tunaomba Wizara inayohusika na wamesikia na Rais amekuja pale akasema itatangazwa hivi karibuni, lakini haijatangazwa. Vile vile barabara ya kutoka Sanzati-Mugumu - Nata haijatangazwa na Rais amefika pale akasema itatangazwa hivi karibuni. Kwa hiyo, tunaomba kwa wanaohusika urekebishaji wa mambo hayo uweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja la Silolisimba Mgeta limekatika na Meneja wa TARURA Bunda amelifunga na sasa ni wiki moja. Tunaomba wanaohusika sasa waone namna ya kufungua ile barabara ili wananchi waweze kupeleka ng’ombe zao mnadani na watoto waende shule kwa sababu hali siyo nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilitaka kusema hayo tu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, nimpongeze Abbas alivyokuwa anachangia hapa vizuri zaidi amenikumbusha uwezo wa kawaida wa binadamu wa kufikiri ule unaitwa argue ni 100 na inaenda mpaka 150. Lakini wale wataalam wenye akili nyingi zaidi kama Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli wanaanza 170 mpaka 220 argue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti yetu tulio wengi hapa Bungeni na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ni moja tu yeye IQ yake kwa kuwa ni kubwa anawaza Tanzania ya 2050 itakuwaje wakati huo huo sisi tunawaza lini tunakuja Bungeni kuendelea na maisha yetu ndiyo tofauti yetu. Kama unawaza kurudi Bungeni unaweza ukazungumza vitu rahisi rahisi vya kufurahisha watu ili uje Bungeni hapa kama unawaza nchi itakavyokuwa huko mbele maana yake ni kwamba unawaza mambo makubwa bila kujali itakuwaje, waanguke au usianguke, ndiyo Mheshimiw Rais Dkt. John Pombe Magufuli anafanya mambo kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshangaa kuna vitu vingine hapa vinakuwa kama mtu anakuja vibaya, au anakuja vizuri sasa tunaambiwa bwana nyie wa CCM sijui Wabunge tunawapa ushauri hamfuati, ushauri siyo agizo, ushauri kuna ushauri mzuri kuna good advice na kuna bad advice. Kwa hiyo, ushauri unaweza ukaufuata kama unaona kama unakufaa au haukufai, ndiyo maana unaitwa ushauri. Tungefuata ushauri huo basi kulikuwa na lugha hapa mnajenga ndege za nini mnajenga reli za nini bandari sijui yameenda, lakini leo tunashauriwa leo nimeona hapa Mheshimiwa Silinde anashauri juu ya kuendeleza mapato ya ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ina maana amekubali ndege ni sahihi kuletwa hapa nchini. Kwa hiyo, tunakubaliana, leo tumeona watu wanashauri kujenga bandari kavu, ambayo bandari kavu kuijenga ni miezi mitatu, lakini kujenga reli ni zaidi ya mwaka mmoja miaka miwili. Kwa hiyo, tumeanza kile kikubwa tunakuja kwenye kile kidogo ili tuweze kwenda vizuri kwenye mambo yetu tunayoenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye barabara za Jimbo la Bunda na kwenye barabara za Mkoa wa Mara. Kuna barabara ya kutoka Nyamswa kwenda Bunda, Bunda kwenda Buramba, Buramba kwenda Kisolia, kuna barabara hiyo ipo toka mwaka 2000 mpaka leo haijajengwa amekuja Mheshimiwa Rais tarehe 4 alikuwa Kibara mwezi wa 9 tarehe 6 alikuwa kwenye Jimbo la Bunda ameagiza amefungua ujenzi wa hiyo barabara akaagiza nikitoka hapa kasi ya barabara hii iendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa ni miezi 9 sasa barabara hii haiendi, barabara ya Buramba kwenda Kisolia haiendi, barabara ya Nyamswa kuja Bunda haijatangwaza hata mkandarasi hajapitiaka, barabara ya makutano kule Sanzati bado inasuasua haiku vizuri, barabara ya kutoka Sangati kwenda Natamgumu bado iko vibaya. Sasa najiuliza sasa Wizara hii ya ujenzi na miundombinu kama kuna mtu alioa Mara halafu mke akamkimbia aje tumrudishie sasa shida iko wapi? Mbona sisi tunapata shida? Ukienda kwenye uwanja wa ndege tumeahidiwa mpaka leo haupo ukienda kwenye bandari haipo sasa ni nini kinatokea sasa kwenye Mkoa wa Mara kitu gani kinakuwepo? Tuna hasira sasa na mambo kama haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa Wizara ianze kuona Mheshimiwa Rais ametoa agizo la kujenga barabara hizo na kutangaza wakandarasi shida yetu iko wapi. Kweli tukafikiri kwamba watu waweze kujenga ili tuweze kuona kazi inaenda. Lakini vinginevyo uwanja wa ndege wa Musoma umepewa bilioni 10 na hautatolewa mpaka leo haujatolewa, Wizara hii ya Ujenzi kusema kweli nchi ni kubwa na wanafanya kazi nzuri niwapongeze kusema kweli, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe naomba sasa naomba sasa ujitahidi ufanye kazi vizuri, Mheshimiwa Engineer Nditiye umsaidie Mheshimiwa Kwandika nawe umsaidie na watendaji wote wa Wizara hii msaidiane nchi ni kubwa tusipoangalia sasa namna ya kupanga hivi vipande vyetu na keki yetu maeneo mengine yatakufa, yataendelea kupata shida sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuangalie kuangalia Mkoa wa Mara muuangalie, Mheshimiwa Rais ameusemea sana alipokuwa kule ndani na mwaka huu tuna maazimisho ya Mwalimu mwezi wa 10 tunataka zile barabara zipitike ili wageni watakavyokuja pale kutoka South Africa wawepo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeesha Mheshimiwa, kengele imeshagonga, ahsante sana.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika tatu hamna? (Vicheko)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community SADC – Protocol on Environmental Management for Sustainable Development)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nakubaliana na niishukuru Serikali kwa kuleta haya maazimio, maazimio yote matatu mimi nayaunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanazungumza viingereza virefu sana hapa, lakini ukweli ni kwamba dunia hapo inapokwenda sasa ni hatari zaidi. Na nchi yetu, ukiangalia katika zile nchi 10 za Afrika ambazo ziko, wanasema most likely to be destroyed by climate change, Tanzania ni nchi ya 10. Na kila nchi imepewa sababu zake za kutoweka; sisi tumepewa sababu za kutoweka kwa mambo ya mafuriko na ukame, floods and drought.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa kama hivyo ndivyo ilivyo, sisi tumeshaambiwa kwamba climate change ni jambo la kidunia, na ozone layer 0.003% imeshaharibika na uwezo wa kuirudisha ni mgumu sana kwa sababu nchi za Ulaya ambazo zinatumia viwanda vingi vinavyosababisha mambo ya greenhouse gases zinakuwepo; carbon dioxide, nitrus, methane chlorophene zinakuepo. Sasa kama sisi hatuna uwezo wa kuzuia hizo maana yake wametupa sababu za nchi yetu kutoweka na nchi yetu kutoweka ni mafuriko na ukame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sisi hatuna uwezo wa kuzuia hizo, maana yake wametupa sababu za sisi nchi yetu kutoweka na mafuriko na ukame. Kama ndivyo ilivyo, basi, sisi hatuna namna yoyote ya mpango wowote makusudi zaidi ya kupanda miti, kwa sababu miti ni carbon sinker, inachukua carbon dioxide. Kwa hiyo, lazima tufanye kila namna, kwa kila eneo, kwa kila mkoa, kwa kila sehemu kupanda miti ili kuepuka janga ambalo wametupa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia hizo dakika ambazo nimepewa. Mimi nimshukuru Waziri wa Ulinzi, Waziri mwenye TBS ambaye amekaa Serikalini muda mrefu, lakini anafanya kazi iliyotukuka kwa kweli anapaswa kupongezwa. (Makofi)

Niwashukuru Wakuu wa Majeshi, Mkuu wa Majeshi aliyepo CDF na wenzake wote wanafanya kazi nzuri. Duniani tunaposema nchi, maana yake ni Jeshi hakuna kitu kingine ambacho kinakuwepo zaidi ya hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nizungumze mambo tu kwamba ukiangalia kwenye maeneo mengi sasa kwenye hizi ukaguzi wa CAG, kuna suala la SUMA JKT. Mimi nilikuwa nataka kusema kitu kimoja, Jeshi ni jambo, ni kitendo, ni tukio, ni kitengo ambacho kinatakiwa kuwa kitakatifu cha kutosha, hasa ukija kwenye Jeshi ukakuta kuna vitu vidogo vidogo hivi vinazungumzwa SUMA JKT nimeona hapa ukurasa wa 34/35 kwamba wamekusanya madeni milioni 330, bilioni 1.545, wamekusanya madeni lakini kutoka kwenye deni kubwa lipi? Hapa ni madeni wamekusanya, kutokea deni kubwa lipi sasa? Maana yake tuseme kulikuwa na madeni labda bilioni mbili, wamekusanya bilioni moja tukasema labda wako afadhali. Lakini kitendo ukiangalia kwenye kitabu cha CAG kinaleta kasoro, kwa hiyo, tunaomba SUMA JKT wafanye kazi iliyotukuka kukusanya madeni na waone yale matrekta yanasaidia nini wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo hapo lipo Kilimo Kwanza, nilenda pale nikafikiri labda kuna matrekta kama yanauzwa. Nikaambiwa kumbe matrekta yale yalisharudishwa Serikalini, yako pale Kilimo Kwanza, yamekusanywa yalikuwa yamerudishwa ili yaweze kulipwa wale wenyewe waweze kurudisha madeni yao. Sasa yamekaa pale, ni ya Serikali, hayajaenda kwa wananchi, hayalimi, hayauzwi yapo tu. Sasa nikasema hii maana gani hii, mambo gani haya tunafanya haya. Kwa hiyo, nasema kwamba Mheshimiwa Waziri naomba mkitoka hapa bajeti ikipita najua mnapitishwa, mkaangalie utaratibu, yale matrekta chukueni. Kama hamuwezi kuyauza yana bei ndogo, warudishieni wakulima waliokopa wakafanya kazi watakuwa wanalipa kidogo kidogo ili waweze kupata hiyo ajira yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo muhimu sana katika nchi yetu, kama JKT na kama Jeshi la Tanzania ambalo lina maeneo makubwa sana katika nchi hii, litatumia vijana wa JKT katika mambo ya kilimo na kuajiriwa tutafanya kazi kubwa sana. Nimeenda kwenye eneo moja linaitwa Chita kama unaenda Ifakara, Morogoro, eneo kubwa, bonde kubwa kuna matrekta lakini hakuna kazi inayofanyika. Nenda maeneo yote ya makubwa ya JKT, kuna maeneo mazuri, makubwa tunaomba JKT na Jeshi kwa ujumla watumie vijana wetu wale wa JKT kuwapa ajira kwenye maeneo hayo, mbona inawezekana, shida iko wapi? Kwa sababu uwezo wa kuwapa matrekta tunao, uwezo wa kuwahimili tunao, ....kuwapa tunao, shida iko wapi.

Kwa hiyo, naomba Waziri mwenye TBS uhakikishe kwamba vijana wetu wanapata ajira kutokana na maeneo makubwa ya JKT, tunaomba utusaidie namna ya kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze tu kwa ujumla, hatuna namna yoyote ya kulaumu mambo ya Jeshi. Mtu anayezungumza Jeshi labda ana kichaa, kwa sababu hawa ndiyo wanafanya nchi inakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, nianze tu na hoja iliyomalizika. Mimi ni mwanamazingira kwa kweli kama wenzetu hawa hoja za toka jana na leo wataendelea kuwa hivyo wa upande wa kushoto wanafanya kazi nzuri sana. Mheshimiwa ametoa mwelekeo mzuri sana wa mambo ya mazingira na kweli mimi nakupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kusema ukweli hili tatizo lipo isipokuwa kwamba sumu ya zebaki ipo kila mahali, hata chakula chochote unachokula kuna kasumu ndani yake.Tatizo la binadamu ni kiasi gani cha sumu kinachoweza kuathiri, lakini sumu kama sumu zipo tu kila siku zipo kila mahali, nikupongeze kwa kweli umefanya vizuri na mimi nadhani sina mjadala kwenye hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapokuja kwenye hoja ya pili, tunapokuwa tunapandisha haya Mapori ya Ugalla na Kigosi. Mapori haya tunachotaka kufanya ni kutengeneza circuit. Nataka nikukumbushe circuit maana yake nini, ukisema uende kutembelea Mikoa ya Kanda ya Ziwa maana yake unaenda kwenye Mikoa ya Mara, Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga, hapo umetengeneza circuit ya kutemebelea maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tourism industry kuna kitu tunaita circuit, kwa hiyo tukienda kwa mfano mgeni anataka kuja Kilimanjaro anatakiwa atoke Kilimanjaro aende KIA, akitoka KIA aende Lake Manyara, akitoka Lake Manyara aende Ngorongoro, akitoka Ngorongoro aende Serengeti; hapo umetengeneza circuit ya Serengeti na mafungu yake yanaweza kuwa yanaongezeka kutokana na hiyo circuit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa tunapandisha Mapori ya Kigosi na Ugalla tuna maana kwamba kuna Burigi, Kigosi, Ugalla na Katavi, lakini katikati yake kuna Mapori ya Akiba Muyowosi, Ugalla na Kigosi. Kwa hiyo, tunatengeneza circuit ya Kusini ambayo mtu akitembea; mtu/mgeni ukimwambia atoke Dar es Salaam aende Katavi, atembee Mbuga ya Katavi arudi Dar es Salaam hawezi kwenda anaona kama hajatengeneza kitu. Kwa hiyo, tunataka atembee Katavi aende Ugalla, aende Kigosi na aende Burigi, kwa hiyo tunakuwa tumetengeneza hiyo circuit ya upande wa Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, hali iko sawa na maendeleo yanakuja kwa njia hiyo. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hizi Kamati mbili na niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati. Nianze kwa kutazama tu jambo la mazingira na niishauri sasa Serikali yetu huko tunakokwenda sasa kuwa na Wizara maalum ya Mazingira ambapo nchi zilizoendelea sasa zina Wizara hii ya mazingira na ndiyo Wizara maarufu katika nchi zote za Ulaya na nchi zingine, kwa mfano Brazil ndiyo Wizara maarufu sana; ukienda Kenya ndiyo Wizara maarufu sana ya mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu hili tunaloliona leo ambapo tunazungumza habari ya mafuriko au habari ya kiangazi ni matokeo ya climatic change, ni climatic crisis ambazo tunaziona sasa hivi hapa na kwa bahati mbaya kitengo hiki cha mazingira hakiko kwenye viwanda, kinazungumziwa kama kitengo tu. Hata ukitazama hapa results zake ni kama vile watu wa ushauri, lakini huko kwenye maeneo ya nchi zote duniani hata Tanzania hapa kilitakiwa kuwa kitengo cha kuamua nini kifanyike katika nchi yetu kwa sababu nchi yetu sasa tunakokwenda suala la mazingira ni muhimu sana kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia katika maeneo kama ya Bunda kwenye Jimbo langu barabara ya Maliwanda, Stephen Wasira yote imekatika, barabara ya Kandege Tingilima haipo, barabara ya Sarawe, Kambubu haipo, Sarawe Bukama, barabara ya Kambubu Sarawe nayo haipo, barabara ya Nyangere Unyali haipo, barabara ya Nyabuzume Kiloleli haipo, barabara ya Tingirima na Tiling‟ati na Nyamso haipo, zote zimekatika; na hii yote ni kutokana na kwamba maeneo maalum ya hizo barabara, aidha watu wamelima mpaka kwenye barabara au watu wameng‟oa viti yote milimani au mabonde yote yameziba kwa hiyo hakuna mahali ambapo watu wanaweza kupita kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa nafikiri kwamba ni vizuri sasa tunakokwenda hii Wizara ya Mazingira tukaipa kipaumbele sana kwenye mambo kama haya ili yaweze kutusaidia huku tunakokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie uwanja wa Musoma, uwanja wa ndege Musoma Mkoa wa Mara; Mheshimiwa Rais alifanya ziara toka wa tarehe 4, mpaka tarehe 8 Septemba, 2018 na akazungumza sana juu ya ujenzi wa uwanja wamusoma, lakini mpaka leo hatua hazijaenda vizuri na uwanja haujajengwa tunasikia tu ten million imetolewa uthamini yakinifu umefanyika lakini hakuna kitu kinachoendelea pale. Tunazungumza habari ya reli ya kutoka Tanga, Moshi Arusha, Musoma kila mwaka tunaiona kwenye bajeti hapa lakini mpaka leo toka Mwalimu Nyerere amekuwepo mpaka leo sisi hatujawahi gari moshi linafika kwenye Mkoa wa Mara. Kwa hiyo, nafiri kwamba ni wakati muafaka sasa wakati tunashughulika na maendeleo haya yaende kwenye Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kusoma taarifa hapa nimeona kuna taarifa ya matrekta yaliyokuwa yananunulia na Serikali kupitia shirika letu la Suma JKT na Kampuni ya US, Russi ya Poland ambayo inaonekana asilimia 65 hela zimetolewa kwenda kununua matrekta, na matrekta 825 ndiyo yamefika kati ya 2,400 yaliyokuwa yanatakiwa kufika hapo. Sasa najiuliza katika haya matrekta yaliyokuja ni asilimia 34 point je, matrekta yaliyobaki hela zake zimelipwa au hazikulipwa? Na hiyo asilimia 65 ya hela zilizotoka zimekidhi vigezo matrekta yaliyokuja au kuna mengine hayajaja, na mbaya zaidi wanasema katika shirika hilo ambalo tumefanya makubaliano nalo linaelekea kufilisika sasa najiuliza hizi hela za wakulima ambazo tunatakiwa kuleta matrekta kuwasaidia wakulima zitapotelea humo au hatua gani itachukuliwa. kwa hiyo nilikuwa nashauri Serikali katika hili uweze kifanya vitu vya haraka zaidi kwenda kuona kinachoweza kutokea katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Bunda kuna barabara ya inatoka Makutano Butiama, Sanzati barabara sasa ina miaka nane toka inatengenezwa na kila mwaka wanapewa muda wa kumaliza lakini wameshindwa kumaliza naomba Wizara inayohuka Wizara ya Miundombinu ichuke hatua kwenye barabara ya Makutano Sanzati ambayo inatengenezwa kwa miaka 6 sasa, kuna barabara ya kutoka Nyamswa kwenda Bunda barabara ya lami, Mheshimiwa Rais amefika pale tarehe 6 akasema Mkandarasi aanze mara moja hatujamuona mpaka leo, kuna barabara ya kutoka Sanzati kwenda Nata Mgumu, tumetangaziwa kuwa Mkandarasi yuko barabarani hajafika mpaka leo. Kwa hiyo, tunaomba Wizara inayohusika ili iweze kuchukua hatua hizo za kuweka Wakandarasi kwenye barabara ambazo zinaweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nizungumze hayo kwenye Jimbo langu, lakini nilishukuru Bunge kwa ujumla kwa hatua ambayo ilikuwa inazungumziwa asubuhi, kwamba katika maisha yetu ya kitanzania na katika watanzania wote mambo muhimu ya kuzingatia ni usalama wa nchi yetu na maendeleo ya nchi yetu. Kwa yoyote yule ambaye anayumbisha nchi yetu na ikiuletea giza kwenye mambo yake ya kule anakotaka yeye hatua kali zichukuliwe dhidi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sakata linaendelea huku Marekani la impeachment trial, watu wenginine wanafikiri kwamba pengine hilo linatokana na sijui Ukraine au kuzungumza jambo fulani lakini ukweli ni kwamba kwa mara ya kwanza katika Marekani uchaguzi wao 2016 uliingiliwa na Urusi, na wanajiuliza mara mbili mbili waliingiaje mpaka leo, nani aliwaruhusu kuingia lakini leo Marekani wanazungumza kuingiliwa uchaguzi wao, lakini wao toka mwaka 1948 wamekuwa wakiingia nchini zingine uchaguzi kwa mfano uchaguzi wa Italia wa mwaka 1948 wameingia na kuweka na mgombea wao, uchaguzi wa Israel, mwaka 1996 Criton amekwenda pale ameweka mtu wake kuwa Waziri wa Israel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba huko tunakokwenda nchi yetu ijue kwamba wakoloni hawatakuja hapa, lakini mipango Marais wanaowataka vibeberu wao itakuwepo. Kwa hiyo tuchukue hatua za kutosha kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Awali ya yote nawapongeza Kamati zote mbili na Kamati shirikishi zilizokuwemo humu ndani na hasa Kamati yangu ya Ardhi Maliasili na Utalii. Kusema kweli katika miaka hii iliyokwisha, Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii imefanya kazi kubwa sana na ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nilikuwa namwangalia msemaji mmoja ambaye ni Mjumbe wa Kamati, Mheshimiwa Mch. Msigwa akiwa anazungumza habari nyingi inayomhusu Waziri wa Maliasili na Utalii, nikakumbuka kwamba huko nyuma tulikuwa tunafanya summit kubwa sana, wakati tunafanya mambo ya utalii, tumetangaza muda mrefu sana; na tulikuwa na summit moja tumekwenda mpaka kule Sunderland kwenye ule uwanja wa Stadium of Light tukafanya matangazo ya kutosha na Sunderland wakaja hapa kwetu wakajenga Kituo cha Kindergarten hapa ambayo iko kwenye udongo mwekundu; tumefanya matangazo Wachina wakaja hapa kwenye nchi yetu karibu 1,000; matangazo ya kutosha ya Israel, wamekuja hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilipomwona mwanaume mwenzangu anapiga piga yote hapa nikakumbuka ile misafara waliyokuwa wanabebana na Waziri mwenzake Nyalandu kwenda Uganda na kwenda Marekani ndiyo hiyo inayomsumbua saa hizi hapa. Kwa sababu sasa Waziri wetu hana mkataba wa kwenda Ulaya naye, sasa amekuwa chongo kwenye mambo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu lazima tuwe na utalii wa ndani. Kuwachukua vijana wetu wa kwenda kufanya kuhamasisha utalii wa ndani, siyo kosa. Je, ikitokea katika nchi yetu watalii hao wa nje wasipokuja kwenye nchi yetu tunafanyaje? Tunakuwa na mapori ya aina gani?

Kwa hiyo, nafikiri kwamba vitu vingine lazima tufanye mambo ya ndani na mambo ya nje. Kwa hiyo, nampongeza sana Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kazi yake nzuri sana anayoifanya.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka nizungumzie habari ya uvuvi na Waziri wa Uvuvi anisikilize vizuri. Huwa najiuliza sana, hivi makokoro yanaisha lini? Kama nchi yetu ilikuwa na mifuko ya nylon, tukapiga marufuku ikaisha, hivi makokoro ni mtaji wa nani? Ni mradi wa nani? Kwa sababu makokoro haya sasa hayaishi.

Mheshimiwa Spika, ni lini sasa upande wa Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi atakaa na wavuvi sasa watengeneze logistic za kutosha za kuamua nyavu na milimita sita za sangara ziweje? Nyavu za furu ziweje? Nyavu za gogogo ziweje? Nyavu za nembe ziweje? Kwa hiyo, tutakaa tutengeneze formula ambayo itatuwezesha sasa kwenda kuvua, tukasema mwaka huu tumeepukana na haya mambo ya uvuvi haramu?

Mheshimiwa Spika, sasa uvuvi haramu umekuwa ni kama chanzo cha mapato cha watu. Wakati fulani tuna watu wa samaki, tuna Maafisa Uvuvi wako kule kwenye ziwa. Sasa inatoka hapa timu inaenda kufanya operesheni. Kama hawa wako barabarani, unajua vitu hivi mimi huwa sivielewi!

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, matrafiki wa kutoka Dodoma mpaka Arusha wako barabarani, lakini leo inatokea wanasema leo tumefanya operesheni ya kukamata mabasi. Sasa hao matrafiki walioko barabarani wamewaondoa au wamewafukuza kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hao Maafisa Wavuvi walioko kwenye maeneo, leo mnaenda kufanya operesheni na wenyewe wapo, unamaliza kufanya operesheni unawaacha pale pale, kitu gani kitatokea? Tunaomba sasa tupate muafaka kwamba ni lini shughuli za makokoro zitaisha kwenye shughuli hizi za uvuvi?

Mheshimiwa Spika, kuna jambo la pamba na bahati nzuri watu wa pamba wako vizuri sana. Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ameteua vijana wazuri sana kwenye pamba. Naomba sasa watumie akili zao kuelewa haya mambo. Hivi ushirika wa sasa unatusaidia au unatugandamiza? Ushirika uliopo sasa hivi unatusaidia nini?

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ushirika ule ile Kamati ya Ushirika ni Mawakala wa Makampuni, lakini ushirika wa sasa unazuia makampuni kushindana, kwa sababu ushirika wa sasa inabidi wewe kama unataka kununua pamba uende kwao. Kama ni Kituo A, kama ni Maliwanda, uende Maliwanda wewe Kampuni ya S & C, Kampuni ya Olam, Kampuni ya Kingu, Kampuni ya Bon wote mwende kwenye ushirika huo. Halafu wanawapangia muda wa kununua pamba; wewe leo utanunua mpaka hapa, wewe utanunua hapa. Ushindani wa pamba utatoka wapi?

Mheshimiwa Spika, sasa wale washirika wa zamani walikuwa na pesa. Ushirika wa sasa ulikuwa na pesa ya kununua pamba, unashindana na makampuni binafsi. Ushirika wa sasa ni mawakala.

Mheshimiwa Spika, sasa huwa najiuliza, pamba ikitoka kwa mkulima ikienda kwenye ushirika anafika pale kwenye ushirika hana hela ya kununua pamba; amekopa tayari. Huo ushirika ukichukua pamba kutoka kwenye ghala kupeleka kwenye kiwanda hawana hela. Sasa najiuliza, hivi pamba inayochukuliwa kwenye ushirika kwenda kwenye kiwanda ikianguka au ikiungua moto humo ndani analipa nani? na je tunapeleka pamba kwenye ghala halafu lile ghala likaungua analipa nani?

Mheshimiwa Spika, mimi naona, ni kweli tunataka ushirika, lakini basi tuimarishe tukubaliane ushirika wa zamani urudi, tutafute fedha tuwape ushirika wanunue pamba washindane na makampuni, vinginevyo sasa utakuwa ni wakala tu; wako pale wanakula hela na watu hawataki, wananchi hawawataki tunang‟ang‟ana nao tu wanakula hela. Nishukuru tu kwamba Mheshimiwa Waziri amesema kwamba angalau kipindi hiki basi tunaweza tukafanya mambo ya watu walipe kutokana na benki, inaweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie habari ya TANAPA, TANAPA ni shirika letu tumewapa mzigo wa hifadhi 22 kutoka 16, lakini hifadhi zenye faida ni tano; hata hivyo zenye faida zaidi ni mbili tu, ni Serengeti na Kilimanjaro; sasa wanamzigo wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, hili takriban ni Bunge la Nne wameomba kupunguziwa kodi. Hawaombi hela, wanaomba kupunguziwa kodi. Hivi inakuwaje leo TANAPA wakienda kunijengea mimi madarasa ya watoto shule, wanajenga Sekondari na wanalipizwa VAT? Wanalipa VAT kujenga mradi wa kijamii? Shida nini?

Mheshimiwa Spika, tumeomba hapa, wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika umesema, tumesema, sasa tufanyeje ili TANAPA wapunguziwe kodi ili waweze kujiendesha? Kwahiyo mimi naomba hili jambo lizungumzwe na liweze kufanya mafanikio kwenye jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, tuna TAWA, TAWA sasa inaonekana ni mamlaka ndogo ambayo sasa kila wakati tumekuwa tunainyanganya uchumi fulani kwa manufaa yetu sisi binafsi badala ya manufaa ya nchi kwa kweli. Kwa mfano suala la umeme wa Selous linaendelea kwa yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini mapato yao wamepandisha nadhani kutoka 33.8 bilion wamepandisha mpaka 48.8 bilion; lakini sasa uendeshaji wa TAWA kwenye shughuli zao za kawaida ni bilioni 150. Sasa kama hatuwezi kuwasaidia hawa TAWA na wanalinda mapori yetu, mapori ya akiba, mapori Tengefu, maeneo oevu, kama hatuwezi kuipa fedha za kutosha watafanyaje ili wajiendeshe?

Mheshimiwa Spika, muhimu ni mishahara ya watu wa TAWA, lazima sasa Serikali sasa kama hatuna uwezo kuipa TAWA fedha za kutosha tusaidie mishahara ya watu wa TAWA ifanane na watu wa TANAPA; maana haiwezekani! Watu wanaolinda ndio walio kwenye ukingo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana ahsante naunga mkono hoja.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naungo mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia jioni ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizishukuru Kamati zote mbili ambazo zimewasilisha hapa taarifa zao, zimefanya kazi vizuri, zimetuonesha Wabunge kwamba kitu gani kinafanyika kwenye Kamati zao lakini kipekee nimshukuru Waziri wa Nishati Dkt. Kalemani ambaye kwa kweli ni mtambo wa bidii, kijana anayetembea kijiji kwa kijiji, hatua kwa hatua, transfoma kwa transfoma, nguzo kwa nguzo, nyaya kwa nyaya, anafanya kazi nzuri sana tunapaswa hata tulete pongezi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwapongeze kwa kazi pamoja na Naibu wake na watumishi wake wote kwa kazi nyingine zinazofanywa na Mawaziri hapa iko siku tufanye kama mlivyofanya juzi kwenye Maspika waliokuja hapa tuanze kuwapa tunzo Mawaziri wanaofanya kazi vizuri humu ndani kwani sisi tuna kosa gani. Mawaziri wanaofanya kazi vizuri kwa mwaka kama huu tunaomalizia tunawapa vyeti au tunawapa zawadi maalum hata tukisema siku moja wachukue posho yetu ya siku moja sio mbaya, wanaofanya kazi vizuri. Kwa hiyo Waziri wa Nishati anafanya kazi nzuri sana na Naibu wake na watendaji wake wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri wa Ulinzi kwa kweli sijui tunasemaje, katika watu ambao nimewahi kuwaona wanashinda vishawishi vya binadamu hapa duniani wakiwa hai ni Waziri Mwinyi, anafanya kazi vizuri sana. Ameshinda vishawishi vya binadamu na tama za binadamu anafanya kazi vizuri sana. Nimpongeze Mheshimiwa Doto kijana huyu kama tunamtunza vizuri na tunampa moyo atakuwa kiongozi bora katika nchi hii, ana nidhamu ya kutosha, anafanyakazi vizuri, lakini pia nimpongeze pacha mwenzangu Waziri Lugola ambaye ajali imempata kazini, amefanya kazi vizuri huku nyuma, ametufanya sisi Wabunge leo tukitembea barabarani trafiki wanapisha uongo au kweli?

WABUNGE FULANI: Kweli.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Kwa hiyo, amefanya kazi, kwa ajali iliyompata ni ajali tu, aendelee kuhangaika na ajali yake lakini alifanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri mwenzake aliyekuja alinde yale maslahi ambayo tunaona yapo kwa Wabunge. Pale ambapo tunakamatwa tunafanyaje tukipiga simu apokee haraka. Kwa hiyo niwapongeze wote kwa kazi nzuri waliyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Bunge hili katika orodha ya Mabunge, maana yake watu huwa wanasahau, Bunge hili katika orodha ya Mabunge yaliyopita, hili Bunge ni la mfano. Limemsaidia Mheshimiwa Rais kufanya kazi kubwa sana za Kitaifa na lazima tuandikwe kwenye historia.

Mheshimiwa Spika, Bunge hili ndiyo limeleta Bwawa la Nyerere, limetengeneza barabara za flyover, limesaidia Rais kuleta Hospitali za Mikoa, Hospitali za Wilaya na limetoa elimu bure. Kwa hiyo, Wabunge walioko hapa wote kwa ujumla hata wanaopiga kelele hapa na wenyewe wanaandikwa tu. Maana kelele hapa ni za Bungeni tu, wakienda mitaani kule wanasema nimeleta umeme, nimeleta hospitali, nimeleta hiki. Hawa hawa ndio wanapiga kelele humu ndani. Wakiambiwa wapige kura hapa, wanapiga hapana. Wakienda huko wanajivunia maendeleo ya Chama cha Mapinduzi. Hawana kingine wanachoweza kujivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Machi, 2017, Rais wa Marekani anaitwa Donald John Trump alimpongeza Rais wa Tanzania. What is so special? Kwa sababu ni Rais bora wa Afrika, alimpongeza Trump. Watu wajue sera zetu za Chama cha Mapinduzi za nchi yetu ya kutofungamana na upande wowote ziko pale pale. Hii habari ya kusema sijui nini kimefanyika huko, sijui Pakistani twende, sijui jambo limetokea tukio mahali twende, sijui nani amesema hivi; hatuendi huko! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi ni nchi ambayo inajitegemea, ambayo haifungamani na upande wowote. Watu waje, Marekani ni marafiki zetu. Wakija na upande wa ushoga, hatutaki ushoga. Tutakataa! Maana nawashangaa watu, tunakuwa kama vile mazoba fulani hivi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amekataa hadharani. Sasa kama kweli hoja yetu ni kukubali ushoga ili tuwe na maadili bora ya nchi hii, hatuwezi sisi mambo ya namna hiyo! Kama ni ushoga, waende kwa wanaoutaka ushoga uko! Sisi hatuwezi kuwa na ushoga. Wanaoutaka ushoga waushabikie. CCM na viongozi wake na Wabunge wake, hatutaki ushoga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa nije kwa ndugu yangu Dkt. Kalemani. Naomba Dkt. Kalemani sasa tuelewane na hapa sasa nitaongea pole pole. TANESCO umetembea sana kwenye vijiji, lakini bado uzalishaji wa accessories wanaita viunganishi ni tatizo kwenye nchi yetu. Bado mita ni tatizo kwenye maeneo yetu, bado nguzo kwenye viwanda, Wakandarasi wanaenda kulipa fedha, hawapati nguzo kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, bado TANESCO hawajawa vizuri bado, isipokuwa TANESCO Mara kwangu wamekuwa vizuri. TANESCO hawajawa vizuri, hawawezi ku-react haraka kwa watu. Kwa hiyo, tunaomba sasa, kwa kuwa umefanya kazi kubwa sana ya kutembea ardhini, sasa rudi ofisini uwashughulikie wale ambao hawafanyi kazi vizuri ili tuweze kufanya kazi vizuri kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi Mheshimiwa Rais amesema soko lile liitwe Ndugai, lakini najiuliza, tuna jengo la Utawala hapa linaitwa Annex, liko hapo, lina jina gani? Kwa nini Mheshimiwa Rais akuone huko akupe, sisi Wabunge hatuwezi kusema Annex ya Utawala apewe Ndugai? Kuna utata gani hapa? Mimi mbona sioni shida hapa!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi natoa pendekezo, Annex iliyoko hapo iitwe Ndugai, kwani kuna ubaya gani? Amefanya kazi kubwa sana ya Serikali hapa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii nzuri.

Mheshimiwa Spika, kimsingi ukiangalia alipowakilisha Mwenyekiti wa Kamati na Kambi Rasmi ya Upinzani ni kama wamekubaliana. Rafiki yangu Mchungaji amezungumza mambo mengi lakini ametoa na majibu. Mchungaji anapoizungumzia UNESCO ni kama vile kuna kachombo fulani hivi ka nchi kanapodhibiti mambo fulani hivi ya nchi fulani. UNESCO imeanzishwa mwaka 1945 inaitwa United Nation Education, Scientific and Cultural Organization. Mwaka 2014, UNESCO ilikuja kwenye Pori la Selous kuweka tahadhari ya Pori la Selous kwa ajili ya mauaji ya tembo. UNESCO ilikuja kuangalia mauaji ya tembo yanayofanyika kwenye Pori la Selous. UNESCO kazi yake ni kuangalia usalama wa maeneo maalum katika nchi mbalimbali kwa vizazi vilivyopo na vijavyo kama alivyosema Mheshimiwa Msigwa hapa sustainable development.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho UNESCO wanafanya kwa sasa ni kumpa kumzawadia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutunza mazingira ambayo sasa wameiondoa Selous kwenye hatari wameiweka kwenye usalama. Sasa leo nashangaa unaposema UNESCO kwamba itaondoa miradi, yaani umeitengenezea miradi ambayo unaitunza kwa vizazi vya sasa na vijavyo halafu waondoe mradi, sijawahi kuona. Kwa hiyo, UNESCO ipo pale kuangalia usalama wa maisha ya maeneo mbalimbali kwa vizazi vya sasa na vinavyokuja.

Mheshimiwa Spika, nafikiri wote waliotoa ripoti hapa, Kambi ya Upinzani waliposoma, Mwenyekiti wa Kamati alivyosoma wamefanya sawa. Mheshimiwa Msigwa amesema sasa kwa kuwa Pori la Akiba Selous lilikuwa linasaidia TAWA kwenye mapato na sasa limekwenda TANAPA, kwa hiyo, Serikali ifanye jitihada kwa sababu TAWA na TANAPA ni mali ya Serikali, hakuna nchi zinazojitegemea hapa, hakuna kusema TAWA ina hela zake na TANAPA ina hela zake, ni mali za Serikali. Kwa hiyo, sasa kwa sababu TANAPA inapungukiwa mapato mengine ya kusaidia maeneo mengine kwa hiyo Serikali isaidie TAWA kwa kuwapa hela za kuisaidia kwenye maeneo mengine. Tuna mapori ya akiba 23 yanatosha kuifanya TAWA ipate fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilichokiona hapa na ambacho kwa kweli tunatakiwa kukifanya ni kwamba katika Pori la Selous kuna wafanyakazi 700 wa TAWA na wafanyakazi wa TAWA na TANAPA wanalipwa tofauti. Wafanyakazi wa TAWA wanalipwa mshahara wa laki nne na zaidi wakati wafanyakazi wa TANAPA wanalipwa shilingi milioni moja na laki tano. Sasa inakuja hoja, wafanyakazi wa TAWA ambao wametunza hilo pori toka likiwa bovu, wameliwekea miundombinu, wengine wamezeeka wamebakiza miaka 3, 4 kustaafu, sasa leo kwa mujibu wa sheria zilizopo mtawaondoa wote waende TAWA halafu wataajiriwa wa TANAPA kufanya kazi ile.

Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge wafanyakazi 700 walio kwenye Pori la Selous wabaki pale pale na wenyewe wafaidi hizo hela za TANAPA ambazo zitawekwa mule ndani na wenyewe wapate hiyo mishahara. Naomba tusiwaondoe mule ndani ili mishahara itakayokuja iwakute mle ndani na wenyewe wafaidi. Wamefanya kazi kwa muda mrefu wa kutunza lile pori tusiwaondoe wakaenda kusononeka huko, ni kama vile umetengeneza kitu halafu wewe unanyang’anywa. Kwa hiyo, niombe Serikali na niombe tuliunge mkono ili wafanyakazi 700 wa Selous waliopo pale wabaki kwenye maeneo yao wapandishwe vyeo, wahamishwe waende TANAPA ili na wenyewe wapate kilichoko mule ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine kilichopo ni kwamba TAWA nayo imetumika sana kutengeneza yale maeneo, imeweka miundombinu na vitu vingi. Kwa hiyo, kama kuna uwezekano kama tulivyosema wengine basi Serikali sasa kupitia TANAPA ione namna gani kwenye mapori ya akiba yaliyobaki kuimarisha namna ya kutengeneza kitega uchumi ambacho kitawasaidia kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, kusema kweli hakuna jipya, mambo yote yameenda vizuri. Namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii amehangaika sana na habari ya kusema wadau, habari ya kusema nani, lile ni pori la akiba, wadau walishasikilizwa muda mrefu na ni mali ya Serikali. Kwa hiyo, Serikali imefanya uhifadhi kwa kulitoa kwenye pori la akiba na kupeleka kwenye national park.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi sioni kama kuna tatizo ambalo liko hapa. Mimi naipongeza Serikali, nampongeza Mheshimiwa Rais ametuwekea ule mradi pale na watu wengine wajue jamani kuweka Pori la Akiba Selous kuwa hifadhi maana yake ni kama tunatunza kiota chetu, tuna mradi wa Stiegler’s Gorge mkubwa, Mradi wa Nyerere ambao umeanzishwa pale, tunatakiwa tuuwekee mazingira mazuri na waliosema eneo lote liwe hifadhi mimi nakubaliananao ili eneo lile lilindwe vizuri ili tuweze kuutunza ule mradi wetu vizuri kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, lakini naona hoja hii imeisha, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hii hoja ya maliasili. Kwanza niwashukuru ndugu zangu wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii; kimsingi ni kwamba Wizara hii sasa imetulia, na tumewapa sifa nyingi Kigwangala, mwenzako Kanyasu, Katibu Mkuu na wengine wote wa TANAPA na mambo ya misitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hofu yangu ni kwamba tumewasifia sana sasa msije mkafanana na timu fulani iliyofanya mambo yake jana tukayaona; kwamba mkishasifiwa halafu mnarudi nyuma halafu mnapigwa magoli huko mbele mnakokwenda. Kwahiyo naomba tu-maintaine hiyo ambayo tumewasifia muendelee kuwa nayo tu msifanane na mambo ya Simba ya jana ili muendelee kufanya vizuri huko mnakoenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tofauti kubwa sana ya kuhifadhi mazingira au kuhifadhi kwa jumla ya mbuga zetu na kufanya biashara ndani ya mbuga zetu, tofauti ni kubwa sana. Tukisema kuhifadhi tunaweza kuweza askari kwenye mbuga zetu zote, national parks na game reserves; wakazunguka, hakuna mtu anaingia na sisi tunaendelea kuhifadhi kilichopo mle ndani. Tukisema kufanya biashara katika mbuga zetu tunahitaji tuboreshe miundombinu katika national parks zetu na game reserves zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapo ndipo kuna shida. Tunataka hela ndani ya game reserve, tunataka hela ndani ya national park lakini miundombinu yetu yote katika maeneo yote ni mibovu; na national parks tunazozitaka zote ni kama tano ndizo zinazofanya biashara vizuri. Kwahiyo tunaomba sasa Serikali yale makato na TANAPA, tumezungumza na Waziri wa Fedha, tumezungumza kwenye Kamati, Spika alizungumza hapa, Bunge linazungumza, shida ni nini? Sisi tunataka mapato yaje ninyi mnazuia. Kwahiyo naomba sasa kwenye kipindi hiki Serikali na hasa Waziri wa Fedha aweke jambo hili, wapunguze tozo kwa kwenye national parts TANAPA ili ipate nafasi ya kuweka miundombinu kwenye maeneo yetu ili wafanye biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo limezungumzwa Stiegler’s Gorge hapa, mwenzangu Dkt. Mollel amelizungumza vizuri lakini na mi niliweke vizuri. Duniani kote tunapozungumza mazingira tunazungumza climate change, tunazungumza ozone layer; na leo tunapozungumza ozone layer 0.0% ya ozone layer inaenda kumomonyoka. Marekani tangu imeundwa imeshindwa kuleta sheria za kurekebisha ozone layer, kwa maana ya climate change in house. Kupunguza hewa ukaa ambayo ni carbondioxide, tangu dunia imeundwa Marekani haijapunguza kwa sababu ya interest ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Uingereza wanataka kujitoa kwenye muungano kwasababu wanataka kulinda paundi; wanataka kulinda fedha yao. Sisi leo tunazungumza habari ya kujenga Stieglers Gorge kuna mtu anasema oo hatutapata umeme, hatupata wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusema kitu kimoja, kwamba hao wenzetu wakati fulani nawashangaa, tukisema tunapitisha bajeti hawataki, tukijenga vituo vya afya wanatangaza wao, tukijenga barabara wanatangaza wao, wanasema umeme hawautaki lakini ukija wanatumia wao; sasa shida ni nini? Tufike wakati tukubaliane; kwamba sasa umeme wa Stiegler’s Gorge ukitoka kwenye maeneo ya hao ambao hawataki Stieglers Gorge wapelekewe umeme wa gharama kubwa na umeme wa bei nafuu uende kwenye maeneo yetu. Tunashangaa sana hili suala la Stieglers Gorge lilishaisha jamani; Mheshimiwa Msigwa wewe ndiyo uko hapa tulishamaliza hilo jamani wewe ni mjumbe, tulishamaliza, tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kuhusu hifadhi ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Makumbusho ya Mwalimu Nyerere tunaomba …

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere naomba ukae, Mheshimiwa Msigwa kanuni iliyovunjwa.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Kanuni ya 64 Mbunge hatasema uongo ndani ya Bunge. Hakuna mahali ambapo sisi kama Wabunge wa Kambi ya Upinzani tumesema hatuutaki umeme, Bunge ni mahali ambapo tunatoa maoni tofautitofauti na hatimaye tunakuja na hitimisho lililo bora. Maneno anayoyazungumza ni ya kuligawa Taifa kwamba watu wengine wasipate umeme umeme huu siyo mali ya CCM, kodi ni mali ya wananchi. Kwa hiyo ningeomba tuongoze kwasababu anasema uongo sisi hatujasema hivyo kama Wabunge.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mmemsikia Mheshimiwa Msigwa kuhusu uchangiaji wa Mheshimiwa Mwita Getere kuhusu mradi wa umeme na maneno aliyoyasema kwamba pengine kuna watu hawahitaji umeme ama kwa namna moja wanataka kuzuia umeme usipatikane.
Kwa mujibu wa taarifa anayoitoa Mheshimiwa Msigwa ni kwamba hakuna taarifa hiyo kwenye kitabu cha Kambi ya Upinzani lakini pia wachangiaji wa upande wa Kambi ya Upinzani hakuna aliyesema hataki umeme.

Kwa hiyo Mheshimiwa Mwita Getere katika mchango wako changia kwa namna ambayo haioneshi kama kambi ya upinzani imekataa umeme.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea; nilikuwa nazungumzia kuhusu Makumbusho ya Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo naomba; Mheshimiwa Kigwangwala kwa kweli pale ndiyo mahali ambapo kuna barabara inayotoka Kilawila inapita Mgeta kwenda Makumbusho ya Mwalimu Nyerere; ni muhimu sana kwenye hiyo barabara kwasababu tunataka tuunganishe pori la Serengeti na Makumbusho ya Mwalimu Nyerere. Jambo hili tumelizungumza kwenye Kamati na nafikiri kwamba tulizingatie; kwa sababu makumbusho ya mwaka huu ya Mwalimu Nyerere nafikiri barabara hii ndiyo itatumika; tumezungumza sana kwenye jambo la namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilikuwa nataka nizungumze jambo moja tu ambalo linaweza kuwa lina maana sana katika mambo haya. Haya mambo ya hifadhi ya wanyama pori yanahitaji ushirikiano kati ya viongozi wa wanyama pori au viongozi wa Wizara na wananchi wanaozunguka maeneo hayo. Tumekuwa na tatizo la kulipa fidia bilions of money kila mwaka; lakini tumeona kuna nchi zingine wenzetu wanaweka ukuta wa kutumia nyaya za umeme; tumeona kwenye maeneo mengi. Tumeona Botswana, nimekwenda South Africa nimeona baadhi ya maeneo; wanaweza kulinda wanyamapori wanaoingia kwenye watu. Haya mamilioni tunayotumia kulipa fidia kwanini isitumike kujenga huo ukuta wa umeme? Kwanini tunang’ang’ania vitu ambavyo kila siku vinafanya kazi ambayo inaleta hela ambazo hazipo sana?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana, niwashukuru wote wa Wizara, niwapongeze, na Waheshimiwa Wabunge wote tuwaombe hii Wizara iko vizuri tupitishe bila matatizo yoyote; ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nawashukuru wapiga kura wa Jimbo la Bunda kwa kunipa nafasi hii. Naishukuru Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kufanya kazi nzuri sana kwa Awamu hii ya Tano iliyopita na kusema kweli wamefanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumshukuru Mheshimiwa Rais, amefanya kazi kubwa, lakini moyo wake wa kutufanya sisi tuwe humu ndani kwa kuwa na kauli moja tu ya kusema corona ipo na itaendelea kuwepo lakini sisi tutaendelea kufanya kazi. Kwa heshima yake na kwa Mwenyezi Mungu, tutafika huko tunakokwenda. Niwaambie, hili suala la corona halitaisha, litaendelea kuwepo, kwa hiyo, mkiendelea kuogopa, mtaogopa mpaka mnaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze habari ya viwanda. Nimesikia wenzangu wengi wanazungumza kuhusu viwanda. Katika karne hii ya viwanda na teknolojia kubwa hatutegemei huko tunakokwenda kuwa na viwanda ambavyo vitaajiri watu wengi. Kwa sababu duniani kote kuna aina mbili za viwanda ukiacha mambo ya cherehani na vitu vingine. Kuna capital intensive industry na kuna labour intensive industry. (Makofi)

Mhshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, viwanda hivyo viwili, capital intensive ni kiwanda chenye kutumia mitaji mikubwa, lakini wafanyakazi wachache; na labour intensive iliyokuwa inatumika kwenye karne ya 19 kurudi nyuma inatumia mtaji mdogo lakini wafanyakazi wengi. Huko tunakokwenda hatutakuwa na viwanda vya labour intensive, kwa sababu teknolojia yenyewe inakataza kuwa na viwanda vingi kwa eneo moja kwa maana ya climatic change. Greenhouse gases inakuwa kubwa na watu wanaleta matatizo mengine ya mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukubali huko tunakokwenda, kwenye nchi yetu tuwe na viwanda hata vya kanda tano vikubwa ambavyo vinaweza kufanya kazi nzuri. Mtu mmoja aliniambia ukileta kiwanda cha nyanya hapa ukawa unasaga tani 500 kwa siku, hakuna nyanya hapa Tanzania. Hakuna sehemu wanalima nyanya za kutosha kwa kiwanda hicho. Kwa hiyo, labour intensive ni kiwanda kikubwa kinachojengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuna Kiwanda cha Ngozi cha Arusha, tunataka kiwe kikubwa, lakini stores zake zijengwe Mara, Shinyanga na Mwanza. Stores zile ziwe za kutunza ngozi na kusafirisha kupeleka kiwandani. Hivyo ndivyo viwanda tunavyovitaka sasa hivi. Viwanda ambavyo ajira yake ni Watanzania ambapo watoto wetu wanaotoka mashuleni wawe wanaajiriwa kufanya kazi ya kukusanya ngozi, kuwa agents wa ngozi na mazao. Kwa hiyo, hivyo ndiyo viwanda. Tunataka kuwa na kiwanda kikubwa cha capital intensive, tunaweza kukiweka hata Singida au Mwanza Kiwanda cha Alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna yale mambo ya kilimo tuliyazungumza sana, lakini nashangaa sijui kuna giza gani limetokea Tanzania. Tunazungumza mazao ya mafuta Tanzania, lakini alizeti inalimwa kila mahali. Yaani tumeshindwa kutamka tu kwamba tunataka tani ngapi za alizeti na soko liwepo tuweze kufanya kazi hiyo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunasema viwanda vya sasa kusema kwamba vitaajiri watu wengi, itakuwa ndoto. Kwa hiyo, tutengeneze mazingira ya viwanda vinavyofanya kazi, lakini ajira yake iwe wajasiriamali, siyo kwenda maofisini kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze habari ya maji; na hili Waziri wa Maji anielewe na Waheshimiwa Wabunge wanielewe vizuri. Itakuwa ni ndoto kusema kwamba tutapeleka maji vijijini kwa style tuliyonayo. Lazima maji tuyafanye kama REA. Lazima twende tukajifunze REA ilifanyaje ikapeleka umeme? Tunaposema Kijiji A kina umeme, inawezekana kuna kaya 200 ndiyo zina umeme, kaya 600 hazina umeme, lakini tunasema kijiji kina umeme. Mtu anaweza kwenda kwenye friji akapata umeme pale; kufanya welding akapata umeme; tufanye maji kama umeme, yapite mabomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natoa mfano mmoja pale kwangu Bunda. Kutoka Bunda kwenda Nyamuswa kwangu ni kilometa 25. Hesabu iliyopigwa kwa force account inakuwa ni shilingi milioni 800 badala ya shilingi bilioni mbili. Ukinunua mabomba mita 112, ukinunua yale matenki, ukiweka DP; tunataka mabomba yapitie barabarani, ukifika kwenye kijiji waweze DP tatu au nne au sita, yanaendelea hivyo hivyo. Kama yanakwenda Dar es Salaam kutoka Dodoma, kila kijiji barabarani kinapata umeme. Mabomba yaende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya mabomba ni ndogo sana, lakini ukipeleka kwa sasa tulivyo tunavyotumia manunuzi hatuwezi kupeleka maji vjijijini, lazima maji tubadilishe. Hata hiyo tunayoita RUWASA, muundo wake ni shida. Kwa sababu gani? Mkoani mtu aende kupata fedha kutoka wilayani, lazima DP tenda yake ifanyike mkoani. Kuipata hiyo hela kutoka mkoani ni ndoto. Kwanza ukiongeza hela, hakuna kitu kinachoendelea hapa ndani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima niishauri Serikali, Waziri wa Maji anafanya vizuri sana…

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri Mheshimiwa Rais anamteua kijana mzuri sana, anafanya kazi nzuri, nawapongeza wote. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, mnielewe, marafiki zetu humu ndani ni Mawaziri, huko nje ni kesi. Waziri akikupindisha, umeshaanguka huko pembeni pembeni huko. (Makofi/ Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango wangu. Kwanza nikushukuru wewe binafsi mama wa kazi, mama mzito, software and hardware, ambaye unafanya kazi kwa akili kubwa sana, mtu anaweza kukuona simple lakini uwezo wako ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru Waziri Mkuu, huyu ni mtu mwema, Waziri Mkuu wetu niliwahi kumfananisha humu Bungeni kama Rashid Kawawa (Simba wa Nyika), ukimtuma kazi anafanya. Kufanya kazi na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli miaka yote hiyo, Mungu akubariki Mzee. Maana yake lile lilikuwa burudoza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Mawaziri wote, maana nimeona hapa Mawaziri wengine wameanza kuyumba, wana hofu mara baraza litakufa au litafanyaje. Fanya kazi kwa uwezo wako mambo ya Uwaziri ni dhamana, ikitoka unakuwa Mbunge kama sisi kuna kosa gani? Kwa hiyo fanya kazi kwa uwezo wako. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie jambo moja muhimu, tutofautishe kati ya utendaji au utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi au ilani anayoitekeleza Rais aliyeko madarakani na nidhamu ya diplomasia ya utendaji wa kazi, hivi ni vitu viwili tofauti. Leo Rais wetu Mheshimiwa Samia, akisema anakwenda Marekani hatuwezi kumzuia tukasema Rais Magufuli hakwenda, hiyo ni diplomasia ya utendaji, lakini leo Rais aliyeko madarakani akishindwa kutekeleza reli, akishindwa kujenga Bwawa la Nyerere, akishindwa kujenga shule zilizoko kwenye ilani, wananchi watatuhukumu kwenye Chama cha Mapinduzi, lazima atafanya tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Rais, Mheshimiwa Samia akisema Tundu Lissu njoo, usiwe kibaraka wa Nchi za Ulaya, njoo tukupe cheo hapa. Atakuja na atafanya, hatuwezi kuuliza. Kwa sababu kuna watu wa namna hiyo, wamefanya hivi na wakapewa na wakaishi. Hiyo ni diplomasia ya utendaji, lakini utekelezaji wa ilani upo pale pale, kwa hiyo, tutofautishe hayo mambo ndugu zangu ili twende vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, linalofuata sasa hivi ni la Waziri Mkuu, naomba anisikilize. Mheshimiwa Lukuvi amwache Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize. (Kicheko/ Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere hata kama yeye anazungumza wewe unaongea na mimi huongei na Waziri Mkuu.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo linamhusu.

NAIBU SPIKA: Unaongea na mimi siyo na yeye. Hata hivyo Mawaziri wake wako hapa wanakusikiliza usiwe na wasiwasi, Mheshimiwa Waziri Mkuu ana mikono mingi, masikio mengi na macho mengi, usiwe na wasiwasi.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo linaitwa kodi ya majengo. Kodi ya majengo haina tofauti na kodi ya kichwa, leo vijijini mama bibi kizee anaenda kuorodhesha nyumba yake ya vyumba viwili na sebule anaambiwa kwa sababu ana bati alipe kodi ya majengo, hii hapana. Hatuwezi kwenda kuwalipisha watu kodi ya majengo watu wa vijijini, tunawa-encourage watu wasijenge majengo ya mabati, tunataka watu wabaki kwenye nyasi, haiwezekani. Hili naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu alichukuwe na alitendee kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ripoti ya CAG tumeonyesha kwamba kuna trilioni 360 ambazo zinakaa pale kila mwaka kwa sababu mauzo hayapo. Ukichukua trilioni 360 ukazigawa kwa bajeti ya trilioni 32, ni miaka 11 ya bajeti ya Bunge hili, ziko pale! Naomba tuunde Tume...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ngoja tuweke takwimu vizuri, trilioni 360?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Ndiyo, trilioni 360.

NAIBU SPIKA: Ukurasa gani huo uliosoma wa trilioni 360?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, madeni yaliyo pending ya TRA ni trilioni 360…

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jerry Slaa.

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali ni kweli kwamba TRA ina mashauri ya kesi yaliyoko kwenye Mamlaka, Bodi na Mahakama mbalimbali yenye thamani ya shilingi trilioni 360. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Mwita Getere endelea na mchango wako.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana mtaalam, huyu ni mtaalam namjua, ni mtaalam mwenzangu huyu. Namshukuru sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ndiyo kosa la watu kutochungulia mambo. Kuna bilioni 52.5 ambazo ziko kwa DPP. Sasa hizo fedha naomba tuunde tume ya kwenda kuchunguza trilioni 360 na bilioni 52.5. Hizo bilioni 52.5 ziko kwa DPP tuzichukue ziende kutengeneza madawati ya watoto, hizo fedha zipo wazi pale, kwa hiyo tuzichukue zikatengeneze madawati ya watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi niende pole pole. Bandari ya Bagamoyo. Tunaambiwa kwamba itakuwa bandari kubwa kuliko zote Afrika, sawa na vema; tunaambiwa kwamba meli kubwa zitatia nanga hapo kwenye hiyo bandari, sawa na vema; tunaambiwa kodi kubwa itakusanywa, sawa na vema; tunaambiwa viwanda karibu 3,000 sijui na 100 vingine, sawa vema. Swali la msingi, nini Serikali yetu inapata kutokana na hiyo bandari? Nani atafuta maelezo ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwamba bandari hiyo ni mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza TRA ikishakuwa pale haikanyagi pale; pili ardhi yote hiyo ya bandari inachukuliwa, hatupati chochote; tatu maili 250 magharibi, maili 250 mashariki itakwenda kwao na jamani tukisema maili wale ambao mnajuwa hesabu ni kwamba, maili 250 ni kilomita 400, kilomita 400 inaenda. Nani atafanya maelezo hayo kwa wananchi, umma kwa Tanzania ujue kwamba faida ya bandari hiyo au maelezo hayo siyo halali. Naomba hiyo mikataba ya Bandari ya Bagamoyo iletwe Bungeni ili tuthibitishe kwamba haya wanayosema ni ya kweli au siyo ya kweli…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imegonga.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Mimi nijielekeze tu kwenye suala la NEMC. Kwanza niwapongeze Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Jafo na mwenzake Chande na maafisa wake wote, wanafanyakazi nzuri na tunatumaini kwamba kazi yao itakuwa nzuri zaidi mbele tuendako. Mheshimiwa Jafo ni mzoefu, tuna uhakika ataendesha Wizara hii vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, sisi Watanzania wa Bara na Visiwani ni wamoja. Toka tumeunda Muungano wetu mwaka 1964 hatujaona kwamba tunabaguliwa. Isipokuwa kuna wanasiasa wenye uchochezi kwa matakwa yao lakini sisi ni wamoja. Kwa umoja wetu tuendelee kupendana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna haja ya kushukuru sana Serikali ya Uingereza na huko tunakoenda tuendelee kuwashukuru. Nasema hivyo kwa sababu gani? Kumbukumbu zinaonyesha mwaka Januari, 1964 wakati wa maasi ya lile Jeshi la Tanganyika King’s Rifles tulizidiwa kabisa kwenye nchi yetu na pengine kipindi hicho Mwalimu angeondoka lakini kwa sababu wenzetu walitupa uhuru bila kinyongo alipoomba msaada walikuja wakatukomboa.

SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere nadhani unge-pick topic nyingine.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naendelea na agenda nyingine.

SPIKA: Ahsante.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nizungumzie mambo ya NEMC. NEMC wanafanya Environment Impact Assessment ambayo ni Tathmini ya Mazingira lakini katika nchi yetu NEMC imekuwa kikwazo kikubwa sana cha maendeleo.

Mheshimiwa Spika, historia ya NEMC ilitoka Marekani mwaka 1969, wao walianzisha mambo haya baadaye wenyewe hata mikataba ya NEMC na mambo mengine ya mazingira hawaweki, lakini kwetu sisi NEMC imekuwa kikwazo kikubwa sana. Naishauri Wizara na hasa watu wa NEMC tuangalie namna gani tuta-handle hii Tathimini za Mazingira kwenye mambo ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, nataka kutoa mfano mmoja, leo ukitaka kuchimba kisima kijijini ni kazi ngumu sana. Kazi ngumu kuliko kawaida! Hata hivyo, vijijini huko tunapokwenda, mapipa ya mafuta ya ma-petrol yamejaa kwenye majumba. Sasa sijui kipi tunataka kusaidia! Sijui tunachokisaidia ni kipi? Mabipa ya mafuta ya petrol na chupa zimejaa kwenye nyumba za watu na nyumba zinaungua, lakini leo mtu akitaka kujenga kisima hata pump moja ni kesi kubwa sana kuliko kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Wizara, mimi ni Mjumbe wa Kamati, tumezungumza kwenye Kamati kwamba tutungeneze utaratibu wa kuangalia tathmini ya mazingira kwenye miradi ambayo wananchi wana uwezo mdogo na wanaweza kuifanyia maendeleo. Tunacho-encourage hapa ni watu wapate maendeleo. Tunawasukuma watu wajenge wapate miradi ya kimaendeleo, lakini NEMC yenyewe inavunja haya maendeleo. Haileti hayo maendeleo.

Mheshimiwa Spika, tuna stage za NEMC, wana hatua nyingi za kufuata kwenye tathmini ya mazingira; kuna suala la scoping, kuna screening. Screening ndiyo ya kwanza, waangalie kama mazingira unayoyaona yanaweza kuathiri watu, wanyama na kadhalika?

Mheshimiwa Spika, leo hatua zote zinafuatwa. Ili upate kuchimba kisima cha mafuta, uwe na shilingi milioni tatu, shilingi milioni nne mpaka shilingi milioni 10. Unachimba saa ngapi? Mradi mdogo unahitaji kupata fedha; na fedha zenyewe wameelekeza kwa watu ambao ni wataalamu, waliopewa kufanya kazi hiyo. Wale wataalamu siyo kama Waingereza, siyo kama Wamarekani ni watu wengine wa nje; ukiwapa hela, hawana kitu cha upendo. Wanachohitaji ni hela. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mradi wowote wa Tanzania ukifanyiwa tathmini ya kimazingira (Environmental Impact Assessment) hawaendi kufanya review. Hakuna monitoring and review. Wakishaandika kama wameuza, mkimalizana, wanaenda jumla, hawarudi tena. Watarudi kuja kusema oh, tunakufungia kwa sababu hujafanya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaomba Wizara ambayo ni ya Kamati ambayo nami nimo, kwamba waangalie hili jambo sana. Tumezungumza sana kwenye Kamati, waangalie namna ya kufanya, miradi midogo inayohitaji screening, inayoinahitaji tathmini ya mazingira ipunguziwe hiyo haja ili watu wapate mazingira ya kufanya kwenye jambo lao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la kufanya ni sheria za mazingira. Kuna sheria inasema mita 200, kuna sheria ya maji mita 200, kuna sheria ya mita 60; sasa tueleweke kwamba tuna sheria gani tunatumia kwenye vyanzo vya maji? Ni mita
200 au ni mita 60? Sheria hizi za mazingira ziende kwenye kata, vijiji, vitongoji na kwenye halmashauri ili wananchi waweze kuona kwamba sheria hizi zinatumikaje kwenye jambo kama hili ambalo ni nzuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka kutoa hiyo historia ambayo ilikuwa imeipunguza, lakini nimeongea haya ambayo nimeeleweka.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hii Wizara. Kwanza tu nimpongeze dada yetu, ndugu yetu Mheshimiwa Prof. Ndalichako, anafanya kazi kubwa sana kwa kweli. Hii ni pongezi bila unafiki, anafanya kazi kubwa sana. Wizara hii toka ameishika tumekuwa na mabadiliko makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo shule zilikuwa zinaitwa za vipaji au shule maalum; ukienda pale Mara kuna Alliance, kuna Tabora, kuna Msalato, kuna Nganza na maeneo mengi. Amefanya kazi kubwa ku-renovate zile shule zimekuwa nzuri sana. Shule zile zinavyojengwa, hata kama imejengwa Bukoba, Tabora na kadhalika, watoto wetu wote wa Kitanzania wanaenda kusoma pale. Kwa hiyo, amefanya kazi nzuri sana, mama tunatakiwa kukupongeza kwa kazi nzuri, kuwapongeza na watumishi wako wote waliofanya kazi hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumza jambo la corruption of mind; na katika hili namshukuru sana Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wetu. Alikataa jambo la corruption of mind. Hivi kweli asingekuwa yeye, hili suala la corona huku kwetu leo ingekuwaje? Tungevaa mabarakoa mpaka yakavunja kila kitu. Kwa hiyo, akakataa corruption of mind kwa maana ya kwamba siyo kila kitu unachokiona ukifanye wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza Wabunge wengi hapa leo, hivi kuna haja gani watoto wanaokaa kwenye ardhi ya udongo mwekundu ukaambiwa wavae uniform nyeupe kila siku? Kuna haja gani? Kuna vitu vingine Mheshimiwa Prof. Ndalichako unatakiwa uvitazame, kwamba jamani hivi kweli hili tunaenda nalo mpaka lini? Nasema hiyo ni corruption of mind. Juzi tu kuna mtoto ameniuliza swali, ni mwanangu mdogo tu, kwamba hivi baba, Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanzania ni nani? Nami nimekaririshwa huko primary nikasema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Akanicheka, nikasema huyu mtoto amekuwaje? Akaniambia hapana baba, Mwalimu Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, kwa sababu Tanganyika iliishia 1962 na Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanzania alianza 1964. Ni nani sasa? Rashid Kawawa, si nikakaa kimya. Corruption of mind! Yaani tunakaa, tunakariri vitu, hatuna uwezo wa kubadilisha kwamba hili liendeje na lifanye kazi gani? Mama nakushukuru umefanya kazi nzuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kuhusu kile kituo changu cha VETA. Chuo cha VETA mama nimekutembelea sana na nimekuja kwako sana. Kuna shule inaitwa Mgeta Primary ina Chuo cha Ufundi, inafundisha ufundi pale, imesajiliwa kwenye ufundi, inafanya mitihani miwili; ya kawaida na ufundi. Mama naomba ukumbuke kwenye hicho Chuo cha VETA, kipindi hiki kwa kweli, utakuja nayo tu, kwa sababu uliniahidi kwamba mwaka huu utaondoka nayo, nami nakubali kwamba ukija uje vizuri kwenye hiyo VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule nane katika Jimbo langu la Bunda; kuna Shule ya Hunyali, haina Walimu wa Sayansi; Shule ya Chamuriho, haina Walimu wa Sayansi; Shule ya Salama, haina Walimu wa Sayansi; Shule ya Milingo, haina walimu wa sayansi; Shule ya Mtomalilo haina walimu wa sayansi, Shule ya Nyamanguta, haina walimu wa sayansi; Shule ya Makongoro, haina Walimu Sayansi; na Makongoro High School, haina Walimu wa Sayansi. Kama katika shule wanahitajika Walimu 24 wako watano au sita. Naomba tafadhali kwenye huo mgao wa Walimu uweze kupata nafasi ya kunisaidia kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere, mimi huwa nasema na huwa tunaimba hivi bila Mwalimu mambo yangekuwaje? Hivi inakuwaje yule Mwalimu ametutumikia miaka 24 na yeye hakujenga chuo wala hakujenga barabara, leo mkienda kujenga chuo nyumbani kwake, chuo kinakaa pale kama maganda fulani, hivi hivi anajisikiaje pale kwenye kaburi lake, hivi kama hakukuwa na haja ya kwenda kujenga pale kwa nini waende kujenga? Wametoa Walimu, wametoa kila kitu na kila jambo liko pale, lakini chuo hakipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Mwalimu pale kwenye kaburi lake anajisikiaje? Kama Wizara haijawa na mpango maalum jamani wa kwenda Butiama, isiende, ili yule mzee akae vizuri kule, hivi anaonaje wameenda kumjengea chuo wanaliita jina lake na chuo hakipo miaka 14; majengo tumewapa bure, kila kitu tumewapa bure, hivi inakuwje? Hii nayo inaleta tatizo sana kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nilitaka tu nimkumbushe mama VETA ni muhimu sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nakupongeza kwa kukalia hicho kiti. Nilikuwa natafutatafuta hapa historia kwamba kuna mtu aliwahi kuwa mdogo zaidi wa kukalia hapo, nikajua ni wewe tu peke yako ambaye ni mdogo zaidi uliyewahi kukalia kiti hicho hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo ambayo wanasema nafasi inapata mtu au mtu kupata nafasi. Nadhani Wabunge wamejua kwamba, sasa hiyo nafasi imepata mtu. Kwa hiyo, ataishughulikia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii, sasa mimi huwa naangalia, yaani ukimwangalia Waziri wake aah, super, yuko vizuri sana yaani jamani. Ukimwangalia Naibu wake yuko vizuri sana, Katibu wake ndiyo usiseme, Mheshimiwa Kijazi. Wakae sasa ili tusiwabughudhi; maana inaonekana kama miaka yote tunawabughudhi. Ili tusiwabughudhi, waamue Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili, wako pamoja kwenye Kamati moja, wajiulize ni wapi ambapo sasa kuna shida ya Watanzania kwenye ardhi hii, waende watatue hayo matatizo ya Watanzania. Kwa sababu hatuwezi kuwa humu miaka nenda rudi, mwishoni Wabunge tutachokwa sasa. Nenda rudi, tunapigia akili kwamba Watanzania wananyanyaswa kwenye maeneo mengi. Watafute maeneo ambayo yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ardhi Na. 4 inaruhusu, kwa sababu ardhi yote ni ya Rais. Kwa hiyo, waangalie. Mimi huwa najiuliza, hivi ni kwa sababu hatukuandika land reserve, tumeandika game reserve? Ukisema land reserve, ni ardhi yote ya Watanzania; general land, the village land, yote hiyo na ya game reserve ni ya Rais. Kwa hiyo, tuangalie, ni wapi tunakosea jamani? Wapi tunakosea kila siku Wabunge tuko humu tunapiga kelele? Tuamue tulete migogoro yote. Marehemu Rais Magufuli aliunde Kamati, imeenda huko imefanya kazi, walete hiyo ripoti basi tuone wamebakiza wapi ili tumalize? Kwa nini tunapiga kelele kila siku humu ndani haiishi? Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naipongeza Serikali kwa maana ya kuweka hali nzuri ya mambo ya mapori yalivyokaa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ila naomba Mheshimiwa Rais aingilie kati migogoro yote ambayo wananchi wanakerwa nayo na pia tumwombe Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu na wote, wale ng’ombe wote waliochukuliwa kwenda porini wakashinda kesi, warudishwe.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere ahasante.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Jamani warudishwe ng’ombe wa wananchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Kilimo. Nikupongeze wewe mwenyewe kwa jinsi unavyoendesha Bunge hili toka mimi nimeingia humu hii term ya pili, unaendesha Bunge vizuri sana mimi kwa kweli naku- mind yaani unafanya kazi vizuri sana. Kuna hospitali inajengwa kule kwangu Unyali ambako ulikuwa unaishi inaitwa Ndugai, ikikamilika nadhani tutakupeleka ufungue sasa hapo ndiyo utaona maisha yanaendaje huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru Wizara ya Kilimo viongozi wake wako vizuri sana, Waziri, Naibu Waziri, viongozi wote wako vizuri, kinachozungumzwa hapa ni matatizo ya kilimo ya muda mrefu. Wabunge wakiwa wakali hapa Mheshimiwa Profesa Mkenda na Mheshimiwa Bashe msiseme wanawasema nyie, tunazungumza matukio ya kilimo toka uhuru yanaendaje, tatizo letu liko hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea, naomba unipe nafasi kidogo niseme jambo moja. Kwa nini tusiunde kamati hata kama ni ya watu watano professional ambao watakuwa wanaangalia hizi Wizara? Waangalie katika bajeti hii 2020/2021 tumesema nini, bajeti ya 2022/2023 waje watuambie hapa tulichokisema wakati uliopita ili watakapokuwa wanazungumza kwenye bajeti mpya tuwe tunaona wametenda nini na wamepatia wapi? Haiwezekani kuzungumza habari ya kilimo cha pamba, korosho, alizeti miaka nenda rudi hakuna kinachotatuliwa. Lazima tujifunze jambo moja tujue ni wapi tumekamilisha jambo limeenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana ulikuwa unasema mambo ya tija, tunapozungumzia tija ni jambo kubwa sana. Tija ya mazao yote kwa mfano tija ya pamba, wenzetu wa Misri, Sudan, India heka moja ya pamba wanazalisha kilo 1,000 mpaka 1,200, Tanzania heka moja ni kilo 250 mpaka 300. Sasa fikiria tija ilivyo, ukizalisha 300 kwa heka moja ukauza kwa Sh.2,000/= ni Sh.600,000/=, ukizalisha 1,000 kwa heka moja ukiuza Sh.1,000/= ni Sh.1,000,000. Kwa hiyo, suala la tija hapa ni muhimu sana katika uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, sasa watu watuambie jamani mliyozungumza msimu uliopita sasa tumetekeleza. Kwa mfano Jimbo langu la Bunda, Tarafa ya Chamriho ndiyo wazalishaji wakubwa wa pamba Mkoa wa Mara, waje waseme pamba tumefikia kiwango hiki lakini sasa hivi kazi ni ile ile. Ukizungumza pamba, alizeti na ufuta tija hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi sasa mkulima anaanza kutayarisha shamba mwenyewe, kulima na kupanda mwenyewe, anatafuta mbegu mwenyewe, analinda usiku wanyama wa pori wakali mwenyewe, ikifika kwenye kuuza Serikali imefika, akitaka kuuza kila mahali anazuiliwa, mambo ya ajabu haya duniani hapa. Kwa hiyo, nafikiri sasa ifike muda tumsaidie mkulima kwenye kuzalisha apate tija kubwa na sisi twende kuingia.

Mheshimiwa Spika, zao la pamba lilivyo kwa mikoa yote inayouza pamba, mkulima analima na kupanda mwenyewe, akienda kuuza anaenda kwenye ghala anakopwa. Siku ya kwanza anapeleka pamba AMCOS amekopwa, AMCOS wanachukua pamba wanapeleka kiwandani wamekopwa, kiwanda kinachukua fedha kinapeleka benki mkulima hajapata fedha, ni shida. Watafiti watuambie kwa nini mkulima wa pamba akipeleka pamba ghalani asipewe pesa pale pale, kuna hoja gani? Pamba ya mtu inakopwa kwa sababu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa huwa najiuliza maswali ya kiakili tu, hivi pamba imeenda ghalani, AMCOS haina hela, amekopa mkulima, hivi ghala likiungua analipa nani? Pamba imechukuliwa kwenye gari inapelekwa kiwandani sio ya kiwanda ni ya AMCOS hivi gari ikiungua atalipa nani? Kwa nini kama watu wana fedha wasiende kununua pamba kwenye maghala ili wakulima wapate fedha zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, AMCOS hawana hela, hivi kuna haja gani ya kuwa na AMCOS? Kama kweli Serikali inataka AMCOS iwepo, iwape fedha kama ilivyokuwa zamani, Ushirika zamani walikuwa wanapewa fedha wanaenda kununua pamba. Sasa tuna AMCOS haina fedha, ni mawakala tu, wanasubiri mkulima alete pamba waanze kumdhulumu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, kilo moja mara 100, 200 …

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja lakini ndugu zangu rekebisheni yale mambo tunayozungumza humu ndani. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nianze kwa kumpongeza Waziri ambaye ametuletea mpango. Mpango wake ni mzuri sana na unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ambao tunaujadili sasa hivi hapa ni kamnofu/kakipande kamoja ka miaka mitano tuliopitisha kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilipopitisha ulikuja mpango mrefu wa miaka mitano. Sasa hapa tunajadili kakipande tu kale ka miaka mitano ndio maana tunaona miradi mingi iliyoko humu ni ile ile ambayo inakuwepo, miradi ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema miradi mingi tuliyonayo, tuna Bwawa la Nyerere, tuna reli ya umeme, tuna bandari zinajengwa na tuna miradi mingi ya kimkakati inajengwa. Kama kweli tuko tayari, nchi hii watu walihangaika sana kutafuta uhuru na bahati nzuri viongozi wetu watangulizi wa nchi hii walianza kwa kutengeneza utaifa na sio kutengeneza uchumi. Nchi nyingine zilianza kutengeneza uchumi bila kutengeneza utaifa. Sisi tumetengeneza utaifa upo na leo tunafahamiana vizuri sana. Kwa hiyo, kutengeneza uchumi na kupanga mipango sisi sio shida kwa nchi hii ya Tanzania, shida yetu ni kusimamia mipango, ndio shida tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi najiuliza, kama miaka mitano iliyopita tumepanga mipango ya miradi ya kimkakati ,hatukuimaliza na leo ni mpango wa tatu tunaenda unaisha mwaka 2025. Bwawa la Nyerere litakuwepo, labda reli itakuwepo, labda bandari kwenye mkakati itakuwepo, hivi hii mipango itakwisha lini? Kwa hiyo, nafikiri kwamba Mawaziri wote na hasa Waziri mwenye mpango mwenyewe tuhakikishe kwamba miradi mikubwa tuliyopanga inaisha kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema jambo moja tu, hii nchi hata tungepata Rais ananuka mafuta, hakuna. Kwa sababu watu wetu tunaowategemea huko chini hawapo. Sasa nchi hii imebaki kila Rais anayekuja Rais anafanya nini? Je, ninyi mmefanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna chama kikubwa cha CCM, tuna viongozi mahiri, tuna vijana tumewafundisha, ni makada na wazalendo, kwa nini hawafanyi mambo Rais amewaagiza? Leo kuna miradi inaliwa tu sasa tunasema tunatafuta hela, ipi sasa? Maana miradi yote ninayoiona ni ile ile na kusema kweli ndiyo tulivyopanga na huwezi kuleta mpango mpya. Cha msingi ni kukusanya fedha ili miradi iende kutengenezwa. Hicho ndicho cha msingi tulicho nacho. Tukusanye fedha miradi itengenezwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani nilikuwa nasikia jambo wanasema, bwana Bwawa la Nyerere lina hela ambayo imekuwa ringfence. Sasa sijui Kiswahili cha ringfence ni nini? Kwamba kuna fedha ipo kiasi kwamba hatuhitaji fedha nyingine kutengeneza hilo bwawa. Tutakuwa tunatoa humu tunajenga. Kuna hela za ringfence ya SGR zinakuwepo na mimi najiuliza kama ipo au haipo kwa nini tusikope sasa hiyo fedha tukaifungia, tukasema hiyo fedha imalize huu mradi? Kwa nini tusifanye hivyo? Mara tunaambiwa fedha tunakusanya tunalipa, mara tunaambiwa fedha tunakopa, tuambiwe wazi sasa fedha za mradi wa Bwawa la Nyerere ziko wapi? Ziko tayari au tunazikusanya? Fedha za bwawa, reli na miradi mingine ya kimkakati. Mimi nafikiri hili ndilo jambo la msingi tulifanye.

Kwa hiyo, naishauri Serikali tuhakikishe tunakusanya mapato na tuyatumie ipasavyo, vinginevyo itakuwa ni mchezo wa kuigiza. Nchi yetu iko salama kabisa, tatizo ni namna ya kusimamia miradi yetu iende, tatizo ni namna ya kusimamia fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza jambo moja, jana nimesikia wanasema Mto Ruaha hakuna hata tone la maji. Mimi nimewahi kutembelea ule mto, sehemu kubwa ya ule mto hakuna kina kirefu. Sasa najiuliza hivi tukipeleka pale tukawa kila mita 500 au kilometa 15 tunachimba kina kirefu kwenye huo huo mto tunachimba mpaka tukaumaliza, hivi maji yakiisha si yatabaki mle ndani? Tumekuwa na mvua zinanyesha kila siku kwenye nchi hii, lakini maji yote yanatoroka yanaenda ziwani. Sasa najiuliza hivi tunafanyaje? kama hatuna uwezo wa kukinga maji kukabiliana na suala la climatic change tutafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia habari ya Bunda, Mheshimiwa Mwigulu mpango huu ni msingi wa bajeti ijayo. Sasa najiuliza hivi Mheshimiwa Waziri wa Fedha wewe ungekuwa Mbunge wa Jimbo la Bunda ungefanyaje? Kama leo ndoo ya maji ni shilingi 1,000 mpaka 2,500 wakati kutoka ziwani ni kilometa 25. Leo maji yanakuja mpaka Dar es Salaam, mnasema maji yaje Dodoma, yaende Tabora, Shinyanga sijui yaende wapi, lakini Bunda kilometa 25 hatuna maji. Wanachi wangu, wananchi wa Mama Samia wanachota maji kwa ndoo shilingi 1,000 hadi 2500. Hivi wewe ungekuwa Mbunge wa Bunda ungefanyaje? Hivi wakikwambia hauwatetei hawana maji unafanyaje? Kwa hiyo, nakuomba kwenye mpango ujao wa bajeti uhakikishe kwamba maji yanaenda kwa babu zako, usiwaache kwenye hii hali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya TAMISEMI. Awali ya yote tumshukuru Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Rais ambaye anafanya kazi nzuri sana katika Tanzania hii, nami namwombea kwa Mungu aendelee kumtunza. Watanzania wamwache Rais afanye kazi yake kadri anavyoona yeye, kwa sababu ni muda wake wa kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru Wizara hii kwa sababu inafanya kazi vizuri. Wapo Mawaziri vijana kabisa hapa. Yupo Katibu Mkuu, tunamfahamu Profesa, amefanya kazi mpaka kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri mbalimbali, ana uwezo huo. Makatibu wake wapo vizuri sana na wanafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la TAMISEMI ni coordination. Bahati nzuri ukurasa wa 90 mpaka 93 wameongelea ubadhirifu wa mali ya Umma TAMISEMI. Watumishi wazembe; mahusiano yao na Halmashauri ni kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kimenishangaza sana juzi hapa. Tarehe 07 Aprili, 2022 Mheshimiwa Rais alikuja Bunda, tukaongea, Mheshimiwa Bashungwa alikuwepo. Kukawepo na fedha ya Sekondari kati ya Tingirima na Kyandege, bahati nzuri Mheshimiwa akazungumza, hela ikaletwa. Hela ya sekondari imekuja toka tarehe 07, vifungu vya kufungua hiyo hela itumike vimefunguliwa tarehe 12 mwezi wa Nne, halafu nimeona hapa wanasema tuna call center, tuna maeneo maalum. Tatizo la TAMISEMI ni coordination. Mahusiano yake na watu wa chini ni shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, viongozi tuliowaweka hapo; Waziri ni kiongozi mzuri sana, bajeti yake tutapitisha, nami naunga mkono hata kabla sijamaliza. Yupo vizuri, tatizo, ashughulike na walaji wa Halmashauri. Halmashauri ya Bunda ni mbaya na imepata hati mbaya. Siyo chafu, ni mbaya. Amekuja Rais amesema, lakini mpaka leo hakuna mtu ametoka kwenye ofisi ya Mheshimiwa Waziri kwenda pale kushughulika na ile Halmashauri. Juzi Mkurugenzi ameulizwa mtu aliyekula hela za Afya; DMO amekula hela za Afya, anaulizwa Mkurugenzi, anakimbia na mafaili. Sasa ni vurugu zinatokea. Kwa hiyo, coordination ni mbaya sana katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo, naomba kwenye hilo, mshughulike nalo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo limezungumzwa hapa la Utawala Bora na nyie mmelizungumza vizuri hapa. Utawala Bora maana yake Wizara hii ndiyo inatafsiri D by D. Wao ndio wanatakiwa wapeleke maelekezo ya Utawala Bora kwenye Kata, Tarafa, Vijiji na kwenye Vitongoji. Shida iliyopo hapa naona tunazungumzia sana Madiwani, hivi Wenyeviti wa Vijiji wanaishije? Wenyeviti wa Vitongoji wanaishije? Wenyeviti wa Mitaa wanaishije?

Mheshimiwa Spika, hivi kweli leo kijiji kina mnada, kina madini, kina mifugo na kila rasilimali zilizopo hapa, Halmashauri inakusanya zote, inapeleka Halmashauri, Mwenyekiti wa Serikali, Serikali yenyewe haina chochote inachopata. Hata kuwalipa mishahara basi, achieni mapato yao yale ya kisheria ya Na. 7 mpaka Na. 8 wayapate wao. Kama kuna mnada mahali, kijiji kilicho na mnada kipate mapato. Kama kuna mawe wanakusanya, wapewe. Sasa... (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Getere kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe.

T A A R I F A

MHE. ALLY A.J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Getere kwamba hata sasa kwenye zoezi linaloendelea la anuani za makazi, watendaji ndio wanaofanya kazi, lakini Wenyeviti na wale Wenyeviti wa Vitongoji wameachwa pembeni.

SPIKA: Mheshimiwa Getere, unapokea taarifa hiyo?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naipokea sana, kwa sababu ni mwelewa, naye anayajua haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako, kama inawezekana, siyo lazima, kama ulivyosema kwa Viti Maalumu wakae, nasi siku moja tukae basi na hii TAMISEMI hata kama ni katika ukumbi wa Pius Msekwa, tulizungumze hili jambo la Utawala Bora. Uchaguzi upo karibu, 2024 nadhani tunaanza uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unakwenda kusimamia watu, unatumia billions of money kusimamia watu; wanapatikana Wenyeviti wa Vijiji, zinapatikana Serikali, wanapatikana Wenyeviti wa Vitongoji, halafu unawa-dump. Hakuna semina, hakuna mafunzo, hakuna vitabu vya kujifunza, hakuna chochote. Haiwezekani! Sasa tunakuwaje na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huku juu sisi tunatembelea magari, wao hata kuwasimamia basi wapate chochote. Halmashauri inakusanya chochote; mchanga inakusanya, mawe inakusanya, minada ni yao, kila kitu inabeba. Inawaacha wamekaa pale bure. Sasa Utawala Bora huu utakuwaje jamani? Haiwezekani. Kwa hiyo, nafikiri kwamba hili nalo tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona Wizara imetenga fedha nyingi sana za sekondari; na sera zetu zinasema tujenge Sekondari kwenye Kata, tujenge sijui vituo vya afya kwenye Tarafa, sioni shida. Naomba twende mbali zaidi, tujenge sekondari kwenye maeneo maalum. Inawezekana tukawa na Kata tatu zina sekondari moja. Umbali wa kutoka Kata hiyo mpaka sekondari ni kilomita tatu. Inawezekana kwa mfano Bunda, ukitoka Vijiji vya Mahanga na Machimero kwenda Sekondari ya Mihingo ni kilomita 17, halafu leo unasema huwapi sekondari. Watoto wanaokwenda kujiunga kutoka hivyo vijiji wanaweza kuwa 60, wanamaliza 20.

Mheshimiwa Spika, umbali wa kutoka pale ni mrefu, mvua ikinyesha hakuna mahali pa kujikinga, ni porini. Kwa hiyo, tuwe na dhana ya kujenga sekondari kwenye Kata na kwenye maeneo maalum ili tusiwe na fedha na lengo tu kwamba tunajenga kwenye Kata, hapana, ni maeneo maalum.

Mheshimiwa Spika, leo Sekondari ya Sanzate ambayo wanaiita Mama Samia, inajengwa na hapa tunapozungumza wananchi wanachimba msingi. Naomba Serikali itambue hiyo Sekondari. Wananchi wamechoka, Sekondari ya Mahanga na Machimero wanachimba msingi, Sekondari ya Nyaburundu wanachimba msingi, Sekondari Maliwanda na Kisarakwe wanachimba msingi. Wananchi wamechoka, wanataka kujenga sekondari kwenye maeneo maalum. Umbali wa kutoka kwenye maeneo hayo kwenda hapo, ni suala kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tumezungumza vituo vya afya, kuna vitu vinashangaza sana. Nami nimekuwa Bungeni hapa wakati fulani najiuliza maswali mengi sana. Tuliomba vituo vya afya vikajengwa 2016, tukaambiwa vituo vya afya vinajengwa kwa shilingi milioni 700. Kwa mfano, Kituo cha Afya Mgeta, shilingi milioni 700, tukaambiwa tutakupa shilingi milioni 400, halafu shilingi milioni 300 itapelekwa MSD kuleta vifaa tiba. Tumepewa shilingi milioni 400 tumejenga Kituo cha Afya Mgeta, kipo mpaka leo, vifaa hakuna. Wameleta vifaa vya shilingi milioni 161, wame-dump hapo ndani. Hata majokofu ya kufanyia mortuary hamna.

Mheshimiwa Spika, nauliza, tuliambiwa hapa zile fedha siyo kwamba zilikuwa za makusanyo, tulikuwa tumepata msaada sijui wa Canada sijui wapi, shilingi milioni 700 kila kituo. Waliopewa shilingi milioni 500, watapewa shilingi milioni 200; waliopewa shilingi milioni 400, watapewa shilingi milioni 300, hizo fedha ziko wapi? Ziko wapi? Tuliambiwa kwamba zimekwenda MSD, ziko wapi? Kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Waziri akija hapa aje na tafasiri ya kwamba hizi fedha zinapatikana wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kwamba katika ile haja ya kujenga TAMISEMI, nyie vijana msimwangushe Rais, amewaamini sana. Jamani mimi niseme, Rais Samia amewapa mamlaka yote Mawaziri. Kwa hiyo, kama Waziri anazingua, ni yeye; nasi humu Bungeni tutamzingua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatuwezi kusema kwamba mnakosa nini, mnapewa msaada. Juzi Mheshimiwa Bashungwa nimeona Mheshimiwa Rais anakwambia, Inno! Anakuita Inno, take care. Sasa nasi tunakwambia, umepewa hiyo kazi, Rais amekuamini sana. Tutekelezee yale ambayo yanayoitajika.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, tujengewe Sekondari Jimbo la Bunda. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. BONIPHACE M. GETERE. Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza nizishukuru Kamati zote mbili. Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nina mambo kama matatu ya kuchangia. Ningeomba nianze na jambo la NIDA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Serikali ni kuwaibika kwa wananchi wake, sielewi ni kitu gani kinafanyika kwenye jambo la NIDA mimi sielewi mpaka leo. Tangu mwaka 2012 mpaka leo, miaka 11, vitambulisho vya Taifa (NIDA) ni asilimia 30.08 tu ambayo imekamlilika. Kwa mujibu wa taarifa zilizoko hapa za Kamati, watu waliotegemewa kuandikishwa ni milioni 34,080,610 na walioandikishwa na kupewa vitambulisho vya namba yaani kwa maana ya kupewa namba ni milioni 19,634,720 maana yake ni kwamba watu milioni 14,445,000 mpaka leo haijulikana wana namba au wana nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo waliopata vitambulisho ni 10,230,710 na milioni 9,400,004 hawajapata, hiyo ni asilimia 30 kwa hesabu zilizoko hapa. Sasa mimi najiuliza; vitambulisho vya NIDA ndiyo maisha ya Watanzania sasa hivi. Yaani kila kitu leo ni NIDA. Uende benki, uende kila mahali. Sasa najiuliza, hivi sustainability ya Vitambulisho vya Taifa ni ipi sasa? Kama milioni 34 imeshindikana, je, tukisema watu umri wa miaka 18 mpaka 85 pengine milioni 50 vitatengenezwa vitambulisho vya Taifa kwa miaka mingapi?

Sasa nashindwa kuelewa hivi kitambulisho kimoja cha taifa ni bei gani? Ambayo inaweza kutosha tukasema tunatoa Bilioni 3 au Trilioni 3 tukamaliza tatizo lote la vitambulisho vya taifa kwa hawa watu 34?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata zangu kwenye Kata ya Mgeta, Kata ya Zalama, Kata ya Mihigo, Kata ya Mihunyali, Kata ya Uhunyali na Kata ya Mang’uta, Nyamuswa hivyo vyote ni asilimia 25 tu wamepata vitambulisho. Kuna kata moja asilimia sijui tatu, hamna vitambulisho vya Taifa na wimbo umekuwepo, wimbo, wimbo, tutauimba mpaka lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanadai vitambulisho vya Taifa mpaka lini na taasisi zipo na fedha wanasema walishatoa zipo? Nataka kutoa ushauri kwa wale ambao tumeandikisha vitambulisho vya Taifa kwenye wilaya zetu na kwenye majimbo yetu…

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natoa ushauri kwenye majimbo yetu kwamba Serikali sasa iangalie kila jimbo kwa kila halmashauri ambazo zimeandikisha vitambulisho vya Taifa, idadi kiasi gani, wajue kwamba ni kiasi gani cha vitambulisho vya Taifa ambavyo havijatoka, waende watoe huko huko vijulikane na bajeti ijayo au Bunge linalokuja tuambiwe sasa, hili suala la vitambulisho vya Taifa lina mwisho wake, ni lini litaisha sasa? Kwa sababu sasa imekuwa kesi hii? Hatuwezi kuwa na nchi ambayo ina vitu vidogo vidogo vinaathiri maisha ya watu, wanahangaika huko, tukubaliane sasa hii kazi inaisha lini? Nadhani maazimio yaje hapo watuambie hii kazi inaisha lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo lingine la mfumko wa bei. Sijui kama tunadanganyana au tunaangalia Taifa. Kutokana na covid 19, nchi zote duniani uchumi wao ulishuka kuanzia asilimia mbili mpaka asilimia saba na mfumko wa bei Nchi yetu ya Tanzania uko nafuu kidogo, sijui kama tunaangalia hili au tuna matatizo. Mfumko wa bei kwa Tanzania unalinganishwa na nani unaposema ni mkubwa? Kwa sababu uchumi ukishuka lazima kuwe na mambo kama hayo. Niseme tu kwwenye uchumi wa sasa kwa mfumko wa bei nchi yetu ni nafuu ukilinganisha na nchi zingine. Tunatazama leo hakuna mtu anadanganywa, lipo wazi hilo, hakuna haja ya kudanganyana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwa hilo kwamba mfumko wa bei kwa nchi yetu mara nyingi tunasema ni vyakula, najua hali ikienda vizuri kama ninavyoiona kwenye maeneo mbalimbali kwenye halmashauri, vyakula vitakuwepo na bei ya vyakula itashuka, lakini kuna kitu nakiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Mchumi lakini Wachumi wako humu wataniambia hivi kama tuna ujenzi wa miradi mikubwa kama Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mradi wa Reli, Bandari, Vituo vya Afya, Hospitali na Barabara na miradi mingine mingi mikubwa. Kama tunayo miradi mikubwa inayochukua sementi kwa wingi sana, inayochukua nondo kwa wingi sana, inayochukua mabati kwa wingi sana, inayochukua misumari kwa wingi sana, hivi tunategemea mfumko wa bei kwa vifaa vya ujenzi utashuka? Hauwezi kushuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoona ni kwamba lazima sasa Serikali itengeneze mpango maalum wa viwanda ambavyo vinazalisha sementi kwa ajili ya miradi mikubwa na viwanda ambavyo vitabaki kwa wananchi vinginevyo kama ni hivyo, hivyo viwanda vitakufa vyote kwa sababu vina bei, hata miradi mikubwa ina bei kubwa au nafuu kuchukua kwa haraka zaidi watauzia kwenye miradi mikubwa, wananchi wataendelea kuhangaika na bei kubwa. Kwa hiyo, tuangalie ni viwanda gani vinazalisha kwa wingi na vizalishe kwenye kiwango kinachotakiwa ili wananchi wabaki na sementi na miradi mikubwa ibaki na sementi. Kwa hiyo nafikiria kwamba kwa hilo naomba niishauri Serikali namna ya kufanya kwenye jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilizungumzie ni deni la Taifa. Ni kweli deni hili ni himilivu kama tunavyoambiwa, lakini ni himilivu mpaka lini? Ni nani atakuja kupata burden ya deni, ni lazima tujifunge mikanda kuona kama deni hilo linakua kwa kasi tuone namna ya kulipunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Mchumi pia ila nataka nishauri kwenye eneo hilo, kwa mfano kama leo tunalipa madeni kwa bilioni tisa, halafu tukakopa deni la masharti nafuu, tukawa tunalipa kwa bilioni nne. Halafu ile hela tuliyokopa kwa masharti nafuu tukalipa lile ambalo lina masharti magumu halafu tukabaki na salio, labda kwa mwezi tukawa tunalipa bilioni nne badala ya kulipa bilioni tisa, kwani hapo Mheshimiwa Mwigulu wewe unaonaje hapo. Kwa nini tuwe na madeni makubwa kiasi hiki? Tuone madeni makubwa yenye masharti magumu, tukope madeni yenye masharti nafuu tulipe, yaani tulipe lile deni lenye masharti magumu tubaki na lenye masharti nafuu, ili tubaki na akiba ambayo tutafanya kazi nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia. Kwanza, namshukuru Waziri wa Elimu na wote wanaotumikia Wizara hiyo wanafanyakazi vizuri sana, kimsingi Profesa Mkenda tunakuamini sana katika mambo yote unayoyafanya na kwa uwezo wako kwa hiyo tunategemea utaitendea haki hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi sana yamezungumzwa humu ndani, ombi langu la kwanza kwa Profesa ni kwamba Bunge hili katika suala la elimu wamezungumza mambo makubwa ya kutosha. Kiandikwe kitabu maalum ambacho sisi kabla ya bajeti itakayokuja, tuanze kukisoma tuliyosema humu ndani yametekelezwa yapi? Mambo yaliyozungumzwa humu ni makubwa sana na kila Mbunge aliyeongea humu, maneno yake yasomeke Hansard zote zisomwe hilo ndilo ombi langu la kwanza kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu la pili kwako Profesa ni VETA Bunda Vijijini. VETA ukiniambia kipaumbele cha kwanza VETA, kipaumbele cha Pili VETA, kipaumbele cha Tatu ni VETA, kipaumbele cha Sita VETA leo nimemaliza, kwa hiyo tutakutana huko kwenye VETA najua utaiwekea mpango maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza niongee kwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, kazi inayofanywa na Mama Samia siyo ya mchezo ni kazi kubwa sana, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, popote anapozungumzwa Mama Samia mjue inazungumza CCM. Kwa hiyo, lazima tukae chonjo, kuangalia siasa za kwetu zinaendaje. Mama anafanya kazi ametuletea fedha tumejenga madarasa, anahangaika huku na huku kwa ajili ya matumizi ya nchi yetu. Kwa hiyo, lazima tumlinde Mama afanye kazi kwa muda wote anaoutaka yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine Mheshimiwa Profesa nakuomba ufanye tathmini ya elimu bure, tunatoa Shilingi Bilioni 24-point hivi kweli tumefuatilia kwamba, Shilingi Bilioni 24 hizo zimegawanywa? Kuna asilimia 30 kukarabati, asilimia 30 huduma za shule, asilimia 20 sijui michezo, zinafanyakazi au tunapeleka Shilingi Bilioni 24 ambazo pengine tungezibadili tukajenga nyumba za Walimu tunapeleka hazina kazi ya kufanya? Tufanye review tuna miaka Sita sasa, kwamba hii elimu bure Shilingi Bilioni 24 tunazopeleka karibu Shilingi Bilioni 25 zinakazi gani sasa hivi zinafanyakazi iliyokusudiwa au zinaliwa? Kwa hiyo na hilo tulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho mimi nimekiona baada ya kupitia hotuba yako ni suala la watahiniwa. Kwa mfano, Darasa la Nne mwaka 2021, waliotarajiwa kutahiniwa ni 1,678,209 waliokuja kutahiniwa ni 1,561,599 wanafunzi 116,610 hawakujitokeza wanakwenda wapi? Hawakuja, ni watoro wanakwenda wapi? Shule ya Msingi 2021, waliotarajiwa ni 1,132,084 waliokuja ni 1,108,023 ambao hawakufika ni 24,000 wamekwenda wapi, wanafanyakazi gani? Kidato cha Pili ni wanafunzi 652,611 waliotajariwa, waliokuja ni 602,955 wanafunzi 49,656 hawakuja, wamekwenda wapi, wanafanyakazi gani? Kidato cha Nne Wanafunzi 538,024 waliokuja ni 521,351 wanafunzi 16,673 hawakuja kufanya mtihani.

Mheshimiwa Naibu Spika, amekuja Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Bashungwa juzi tulikuwa naye Bunda ametuambia Halmashauri ya Bunda peke yake wanafunzi 7,000 hawakufanya mitihani kwa mujibu wa ripoti ya CAG, hawakufanya! Ndiyo maana nikipiga kelele humu ndani kwamba Bunda kunahitaji kujengwa sekondari kutokana na umbali wa wanafunzi mniunge mkono kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi 7,000 nchi nzima ni Bunda kwa umbali wa sekondari zilivyo, kwa hiyo hilo nalo utalifanyia kazi. Kwa hiyo, sekondari zile ambazo zinajengwa na wananchi mziunge mkono ili tupunguze hao wanafunzi ambao hawaendi kufanya mtihani.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilikuwa nalizungumza hapa ni suala la kukopa, yaani mikopo ya wanafunzi wa Chuo Kikuu. Mimi naomba kama inawezekana kwa mwaka mmoja tu au kwa bajeti moja tu, tukubaliane kwamba wanafunzi wote wanaotaka kusoma tuwalipie karo, wote wenye kuhitaji kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwalipia karo mahitaji mengine wanayofanya tutachangiana. Hebu mwaka mmoja bajeti moja tukubaliane, wanafunzi wote waliokwenda vyuo vikuu tuwalipie karo ili tuone kwamba itakuwaje, si kila kitu ni kujaribu tuone, kwa sababu shida kubwa ya wanafunzi ni karo, hata kama tunalipia karo kila mtoto atakuwa na uwezo wa kusoma. Hili nalo tuliangalie tuone linakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la mwisho nililokuwa nataka kulizungumza leo ni elimu bure. Tumekubaliana Chama Cha Mapinduzi, Sera ya Chama Cha Mapinduzi tumekubaliana tunatoa elimu bure shule ya msingi mpaka sekondari lakini katikati hapo kuna kidato cha tano na sita; ukiangalia kidato cha tano na sita ni sekondari sasa kwa nini hatuwapi elimu bure? Umefika wakati sasa tuangalie kidato cha tano na sita tutoe elimu bure ili tukamilishe kile tunachosema elimu bure kwa shule ya msingi na sekondari. Kwa hiyo, tukubaliane kwamba mwaka ujao tupange mikakati ya kutoa elimu bure kwa kidato cha sita na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Wizara ya TAMISEMI.

Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Manaibu wake wawili, Katibu Mkuu na Viongozi wote wa TAMISEMI wanafanya kazi nzuri, tunajua kwamba wengi wao ni wageni kwenye Wizara hiyo na ninaamini kwamba wanatafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa utekelezaji wa bajeti kwa kutupa hela nyingi Wabunge wengi likiwemo Jimbo la Bunda ambapo tumepata bilioni 1.650 kwa miradi mbalimbali ya barabara ya Nyamswa – Bunda, barabara ya Sanzati – Nata, barabara ya Makutano – Sanzati na miradi ya afya na miradi ya zahanati. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu ukienda pale mitaani au ukiwa nje ya Bunge wanakuuliza mbona Wabunge, masaa yote mnampongeza Rais? Nadhani elimu iende kwa wananchi, tuwaambie kwamba Wabunge kazi yetu ni kupitisha bajeti, anayetekeleza bajeti na kuamua akusanye fedha ziende kwenye Majimbo yetu ni Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, yeye ndiye ana tekeleza bajeti, kwa hiyo tunamshukuru kwa sababu anatekeleza bajeti vizuri, anakusanya fedha na zinakuja kwenye Majimbo yetu. Kwa hiyo, lazima tufike hapa tuseme huyu tumekupa kazi ya kufanya na hiyo kazi unaifanya vizuri lazima tumpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kazi anayoifanya nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba sasa tuna Wizara ya TAMISEM) ina Viongozi wengi wapya lakini nawaomba watazame Jimbo la Bunda. Halmashauri ya
Wilaya ya Bunda inajengwa hospitali ya Halmashauri ya Bunda – Nyamswa – Ikizu pale Bukama, tumepewa Bilioni Tatu na Milioni Mia Sita Hamsini toka 2018 mpaka leo hospitali ile ni gofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza maswali mengi sana, huwa nasema hivi Rais anapochaguliwa na wananchi, Rais anaetokana na Chama cha Mapinduzi na Wabunge wa CCM ndiyo wengi humu ndani, halafu akateua Mawaziri ni wa kwake, akateua Wakuu wa Mikoa ni wa kwake, akateua Wakuu wa Wilaya ni wa kwake, Wakurugenzi na Idara mbalimbali ni wa kwake, sasa anapowateuwa wanakwenda na analeta hela kwenye Halmashauri zetu na hela azisimamiwi hivi wanamjengea kura au wana mharibia kura? Najiuliza maswali mengi sana, nasema kama mtu amemteuwa kwenda kusimamia Idara fulani maana yake aliyeniteua anataka nijenge, nifanye kazi nzuri ya ufanisi ili kazi yake na yeye mwisho wa kuomba kura watu wampe kura vizuri. Niwaombe Mawaziri, niwaombe Wateule wa Rais, watekeleze kile walichopewa na Mheshimiwa Rais, kuwateuwa kwa madhumuni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi yanayolalamikiwa na wananchi ni maeneo yanayotekelezwa na Serikali. Chama cha Mapinduzi kipo vizuri sana na tunaamini kipo vizuri masaa yote na muda wowote na miaka yote, lakini utekelezaji wa CCM kwenye upande wa Serikali kuna matatizo yake 3,650,000,000 zipo pale zimelala, amekwenda pale Waziri Ndugange nakushukuru ulikuja pale, umeyatazama pale ilivyo, hali ni mbaya. Juzi wananchi wa Nyamswa – Ikizu, vifaa vimeletwa vimefungwa na Halmashauri wenyewe wamefunga usiku, baada ya siku tatu vimeibiwa! Aliyekuja kufunga ni mwenyewe, aliyetoa taarifa ya wizi ni mwenyewe. Hizo taarifa tumewapa najua mtazifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe sana, Jimbo la Bunda Kituo cha Afya Mgeta, Kituo cha Afya Onyari, Sekondari ya Vilina na Halmashauri ya Bunda Hospitali naomba mtazame sana. Mheshimiwa Angellah Kairuki wewe unafanya kazi vizuri naomba uende utazame, lakini najiuliza swali moja hivi amezungumza hapa Mheshimiwa Kishimba, anasema tuunde Wizara ya Kero, mi najiuliza kwani Mheshimiwa Waziri na ofisi yako ukisema ukaleta hapa tathimini ukaleta karatasi humu ndani fomu, ukasema Wabunge wote wenye kero jazeni fomu halafu ukatukutanisha kama ulivyofanya Mkoa wa Mara juzi juzi hapa, kwani kuna ubaya gani? Si Waziri wa Kero ni wewe huyo huyo unataka nini sasa? Ni wewe huyo huyo Waziri wa Kero. Kwa hiyo, nikuombe kwamba sasa hili nalo ulitazame vizuri ili uweze kulitazama.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maombi haya sasa naingia kwenye maombi maana naweza nikaanza nikasahau haya yaliyotokea hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba Halmashauri ya Wilaya Bunda. Mheshimiwa Waziri na Mawaziri wengi wamepita pale sana, Wabunge nataka niwaeleze Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ni kama vile mtu anakaa Mkoa wa Morogoro halafu katika hapa Mkoa wa Dodoma halafu mbele yake ni Mkoa wa Singida, Halmashauri ya Bunda iko Jimbo la Mwibara iko Singida, Bunda wako Morogoro, wakitoka Morogoro wafike Dodoma wafike wachukue nauli waende Singida warudi tena Morogoro. Mazingira machafu sana, kelele nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko nchi zimeundwa kutokana na Jiografia yao. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, iliundwa kutokana na Jiografia yake, tunaomba Halmashauri ya Bunda majengo tunayo iliyokuwa Halmashauri ya Bunda ya zamani ya Mzee Wasira, iko pale ina majengo yale tumeyaacha yanateketea, majengo mazuri sana tusaidieni sisi hatuhitaji majengo tunahitaji Halmashauri na Mkurugenzi awepo pale tuweze kupata Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi mengine niliyonayo ni Zahanati ya Kijiji cha Bigegu sasa naomba haya viongozi wote mnao husika msilikilize vizuri. Hali ya hewa hapo ni mbaya sana, Zahanati ya Kijiji cha Bigegu, Zahanati ya Salakwa, Zahanati ya Mawanga, Zahanati ya Nyaguzume haya ni maeneo hatarashi sana wananchi wa pale watoto wanakufa na malaria umbali wa kituo ni mrefu sana, naomba hilo nalo mlichukue. Naomba Kituo cha Afya Mihingo, Kituo cha Afya Nyamang’uta, Kituo cha Afya Kitale na Salama. Hali ya hewa hapo siyo nzuri kwa upande wa Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba barabara ya Kambugu – Nyabuzume – Vigutu – Butiama tumeishaiomba sana na Mheshimiwa Sagini, tuunganishe hizo barabara iweze kupita wananchi wa maeneo hayo ambayo wanafanya kilimo cha alizeti. Barabara ya Mikomarilo – Mirwa – Buhemba kule soko la Butiama barabara hiyo inahitajika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia barabara ya Mavunga – Mtaro kwenda Jimbo la Bunda Mjini, barabara ya Mgeta – Salakwa – Maliwanda – Kilawila. Sisi tunazungukwa na Hifadhi ya Serengeti, Grumeti imetuzunguka pale lakini wananchi hawana uwezo wa kwenda kuuza mazao yao kwenye hoteli zile mle ndani, kwa hiyo tunaomba hiyo barabara tuipate ili wananchi waweze kufanya biashara kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije suala nyeti sana, Waheshimiwa Wabunge wenzangu tusijifanye vichaa, tunaomba tuelewane hali ya madawati kwenye shule zetu za msingi ni mbaya sana, Bunda peke yake madawati 11,840 hayapo! Jimbo la Bunda la kwangu 4,815 hayapo, hata ningetengeneza madawati kwa Mfuko wa Jimbo Milioni 51 nitakaa miaka 11 ambayo wananchi hawawezi kusema kwamba wanakubali au hawakubali, kwa hiyo hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya madawati kwenye nchi yetu siyo kwamba imeanza leo, Awamu ya Tatu ilikuwepo, Waziri Sumaye alitangaza kila mwananchi alitengeneza, wananchi waliungana wakatengeza dawati moja, 2018, 2019 nadhani humu humu Bungeni hata Bunge letu lilichanga tukatengeneza madawati mengi sana kwenye shule, haiwezekani watoto wakakaa chini, haiwezekani watoto wa nchi hii huru wanakaa chini haiwezekana! Tunaomba Serikali mtuunganishe mnaweza mkafanya mambo mawili:

Jambo la kwanza tangazeni kwamba wananchi watengeneze madawati tushirikiane nao tutengeneze; Pili tutumie Taasisi zetu na maeneo ya Serikali kutengeneza madawati. Naomba sana Waziri haiwezekani tukawa Wabunge, humu ndani watoto wa maskini wanakaa chini, haiwezekani! Kwa hiyo, tuangalie hali ya madawati siyo nzuri sana kwenye maeneo yetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere ahsante sana muda wako umeisha, nakushukuru sana.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Madini. Namshukuru Waziri wa Madini, Naibu Waziri, Katibu na Viongozi wote wa Wizara ya Madini, wanafanya vizuri sana kwenye Wizara hii, wameitoa mbali na sasa hivi inakua ilipotoka asilimia 4.7 mpaka hiyo asilimia Tisa sasa inaenda ni jambo la kupongeza sana. Ahsanteni sana kwa kuifanya Wizara ionekane ni Wizara ya maana sana kwa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa haya ma-“b” anayoweza kuweka kwenye Wizara ya Madini tumeona mikataba ya ma–“bi” na ma–“bi” inaongezeka maana yake yote ni maono yake katika nchi hii ya kuona madini yetu yatumike vizuri kutoka ardhini yaingie kwa wananchi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri ambayo anafanya Mheshimiwa Waziri Dotto, kusema kweli wachimbaji wadogo amewatoa mbali sana hawakuwa hapo, ametoa maeneo mengi sana amesaidia migodi mingi sana kwenye mazingira lakini nimuombe Mheshimiwa Dotto atazame maeneo kama matatu ya wachimbaji wadogo, wakiwemo wachimbaji wadogo wa Jimbo langu wanaitwa Nyabuzume na Nyaburundu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni PL hizi leseni kubwa za utafiti zinachukuliwa na wachimbaji wakubwa wanakaa nazo miaka, hata kama hawachimbi wachimbaji wadogo wanazunguka hapo pembeni hakuna kupewa, wanakaa nazo miaka mingi, utafiti miaka mia, kwa hiyo nadhani hilo nalo uliangalie ili wachimbaji wadogo wanaozunguka migodi mikubwa au maeneo ya wachimbaji wakubwa waachie maeneo mengine kwa wachimbaji wadogo, hilo ni jambo kubwa sana kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni PML hizi nazo ni leseni ndogo zinazokatwa wachimbaji wadogo, nao wamekuwa kama mafisadi na wenyewe. Wengine ana PML tano, 10, 40, 50 zinakaa kwa muda mrefu wenzao wanazunguka humu ndani hamna kitu, hata wale wengine viongozi wao nao wana ma-PL ya kutosha, hilo nalo uende ulitazame viongozi wachimbaji wadogo wapewe maeneo yanayotosha kwa ajili ya uchimbaji

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni mitaji. Wamezungumza Wabunge wengi hapa, nikamsikiliza mwingine anasema twende tukamwambie Mheshimiwa Mwigulu Wizara ya Fedha itupe fedha, hizo ni ndoto! Kuomba Wizara ya Fedha ikupe mikopo ya wachimbaji wadogo hizo ni ndoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dotto nikuombe, mimi najiuliza hivi watu wa mbolea wanafanyaje amezungumza hapa Mheshimiwa Nyongo hapa, tunakopesha tunaleta mbolea tunagawa kwa wakulima tunaipa ruzuku mbolea maana yake hiyo ruzuku inaenda kutusaidia kwenye maeneo yetu inaleta chakula humu ndani. Sasa kwa nini hatutoi ruzuku kwa wachimbaji wadogo, ambao ndiyo wanaleta fedha kwenye nchi hii, wachimbaji wadogo ndio wanaoleta fedha hatuwapi ruzuku kwa nini sasa? Na hii kazi inatakiwa kufanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa dotto nikuambie kitu kioja nenda NMB benki, nenda CRDB benki nenda Benki ya Exim, nenda benki zote unazoona zinafaa uweke nao mkatabawa kukopesha wachimbaji wadogo. Mchimbaji mdogo asiende benki mwenyewe, umpeleke wewe ufanye kitengo humu kwenye Wizara yako, uende uongee nao wako tayari kuwakopesha wachimbaji lakini ukisubiri Wizara ya Fedha ikupe fedha na miradi mikubwa tuliyonayo ya mikakati hizo ndoto, hizo ndoto kama jina lako ni ndoto tu! nendeni CRDB, NMB kaa nao panga nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa mfano, wanapoenda wachimbaji wadogo wanaambiwa kwamba vifaa unavyotaka ni Milioni 100, Milioni 100 wanataka asilimia 20, asilimia 20 hapa unazungumza milioni 200 au milioni 50 wanapata wapi hiyo Milioni 50? Unawaambia ulete nyumba, ulete kila kitu watapata wapi hizo nyumba zinatoka wapi? Hawakopeshwi! Kwa hiyo, wewe chukua hicho kitengo chukua wachimbaji wadogo walete maandiko yao, proposal zao uzione, nenda kwenye mabenki ongea nao, mabenki wawakopeshe ninyi mtakuwa ni dhamana ya hawa wachimbaji wadogo, kwa hiyo naomba hili nalo ulichukue uweze kuliweka sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo lipo Mheshimiwa Dotto nakushukuru sana kwanza kwa kufungulia wale watu wa Kinyambwiga, wachimbaji wadogo wanapokuwa na migogoro mnawafungia kwa muda mrefu sana, mimi huwa najiuliza maswali mengi sana hivi ulishaona Wabunge tunaoshindwa kwenye uchaguzi? Ulishamuona Mbunge mzuri aliyeshindwa kwenye uchaguzi? Unajua anawakimbia hata watu hataki kuwaona, sasa kama kazi yako wewe inayokupa chakula au inayokuweka uwe na heshima ukishindwa unasononeka, kwa nini umfungie mchimbaji mdogo miezi sita, mwaka, anakula wapi? Kuna mamantilie wako hapo, kuna watu wa maji wanapeleka, kuna watu wa maziwa wanapeleka mnafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa madini unakua kwa asilimia 9.7 mpaka asilimia 10 inaenda, kama uchumi unakua na wachimbaji wadogo wanakuwa maskini maana yake nini? Maana yake haufunganishwi sasa na uchumi wa wachimbaji wadogo. Nikumombe Mheshimiwa Doto kwamba wachimbaji wadogo sasa umewapeleka mahali pazuri, uwasimamie wakue. Kadri uchumi wa madini unavyokua na wenyewe wakue sasa waweze kuendelea kwenye shughuli za kuleta maendeleo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna vitu vingi vya kujiuliza hapa wachimbaji wadogo wakipata madini mahali mkubwa naye anakata leseni anakaa nayo wanawakimbiza mnaenda kuwafungia, yaani wao wamekuwa kama vibarua, wakipata hapa madini wanahama wakipata madini wanahama hivi haitokei siku moja wakapata madini mkawapa? Mkasema sasa tunawapa eneo hili lote, kwa hiyo sisi wachimbaji wadogo tukiwa tunapata madini maeneo mengine mnawagawia watu wengine wakubwa sisi tunakuwa kama vibarua tu. Ninakuomba kwenye hilo nalo ulitazame vizuri ili wachimbaji wadogo hawa wapate mitaji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la vifaa, kama ni mabenki basi kama ni Wizara ya Madini kwa nini isikope sasa, kopeni hivyo vifaa vya wachimbaji wadogo halafu ninyi muwape kwa sababu ninyi ndiyo mnawajua, kwa nini muwambie benki ziwape na hazina dhamana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri kwamba ninyi kopeni hivyo vifaa vitafuteni, kwa mfano watu sasa wanataka kupima kufanya utafiti wa kutosha kujua hapa kuna madini wasihamehame, madini kama vifaa vile vya utafiti mita moja ni rola 130 ukifanya utafiti. Kwa hiyo unapotoboa matundu matatu ni dola kama 390, sasa dola kama 300 maana yake ni kwa hela ya kitanzania mchimbaji mdogo hawezi kufanya utafiti. Kwanini kama walivyosema STAMICO, GST msiwape fedha wakawasaidia wachimbaji wadogo kuwapimia maeneo ambayo wanajua kwamba kuna dhahabu, hapa sasa wamekuwa wanatoboa hapa wanahama wanatoboa hapa wanahama sasa nchi nzima itakuwa matobo tu! Tutafute vifaa vya kutosha vya kuonesha kwamba hapa jamani kuna dhahabu muweze kutulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dotto ninakuomba baada ya bajeti yako kupitishwa hapa naomba uende Nyabuzume Jimbo la Bunda uende Nyaburundu Jimbo la Bunda, uwasaidie wale wachimbaji wadogo wapate mikopo kuna dhahabu pale mabilioni na mabilioni ya matani ya dhahabu iko pale tuwasaidie wapate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Wizara hii ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara. Nipende kwanza kumshukuru Mheshimiwa Waziri, najua, nimefanya naye kazi katika Wizara hii ya Viwanda, mimi nikiwa mjumbe wa Kamati yake. Ni Waziri mahiri sana, anajiweza katika vitu vingi. Namshukuru kwa kufanya kazi vizuri na Naibu wake.

Mheshimiwa Spika, lakini nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa mapambano yake haya ambayo anaendanayo katika viwanda. Nilikuwa naona katika shughuli hizi alizokuwa anazungumzia Mheshimiwa Mgaya hapa, juu ya Liganga na Mchuchuma. Sasa kutokana na hayo mimi nikaona nije na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, nianzenayo kabisa, Ukurasa wa 58; inasema, kuendeleza na kujenga viwanda mama ikiwemo viwanda vya chuma, Miradi ya Mchuchuma na Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa, wazo limekuwepo tangu uhuru, ilani imeandikwa zaidi ya miaka 40. Sasa mimi nataka kujiuliza, Liganga na Mchuchuma sasa ni wimbo au ni mradi? Maana sasa tujue, Liganga na Mchuchuma ni wimbo au ni mradi? Maana tumesema Liganga na Mchuchuma hadi tumezeeka na tunaenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Liganga na Mchuchuma tunaenda kufa, Liganga na Mchuchuma tunaenda kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe hakuna jambo lisilowezekana duniani. Hakuna jambo…

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Getere kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Katani.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naye ameanza mapema huyu. (Kicheko)

SPIKA: Aah, ngoja, samahani, sijamsikia. Umesemaje Mheshimiwa Getere?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ameanza mapema. (Kicheko)

SPIKA: Nadhani katika watoa taarifa humu ndani unaongoza kwa hiyo, uvumilie tu. (Makofi)

Mheshimiwa Katani Katani.

TAARIFA

MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, nilitaka nimpe taarifa Mheshimiwa Getere kwa alichokisema. Tangu mimi nakuwa Mbunge mwaka 2015 mpaka leo, habari ya Liganga na Mchuchuma imekuwa ni maandishi ya kwenye makaratasi. Kwa hiyo, naunga mkono hoja yake tuone jambo hili linakaaje.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nakuunga mkono kamanda. Na ninapokea Taarifa yako…

SPIKA: Mheshimiwa Getere unasubiri uitwe kwanza.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa yake kwa sababu, ana uchungu na huo mradi. (Kicheko)

SPIKA: Subiri kwanza Mheshimiwa Getere, usiwe na haraka sana.

Mheshimiwa Getere, unapokea taarifa ya Mheshimiwa Katani?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naipokea.

Mheshimiwa Spika, nataka kuzungumza kwamba hakuna jambo ambalo haliwezekani duniani. Tumekuwa na wazo la kuja Dodoma toka mwaka 1972, lakini limewezekana. Nami nilikuwa kwenye Kamati, naona juhudi za mama katika huu mradi inawezekana. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Rais kwamba hii jitihada aliyonayo ya Liganga na Mchuchuma iwezekane kwenye hii miaka inayokuja. Kwa hiyo ikifika 2030 wakati Rais anaanza labda anataka kuacha au kama anataka kuendelea, basi mradi utakuwa umekamilika. Nimwombe sana kwa jitihada yake hii, ili Liganga na Mchuchuma sasa zisifutike kwenye mawazo ya Watanzania, uwe mradi ambao unatuletea faida.

Mheshimiwa Spika, nizungumze habari ya viwanda vilivyotaifishwa na viwanda vilivyobinafsishwa. Wamezungumza wengi hapa. Hii nataka nitoe mfano na Wabunge wengine msikilize humu ndani, maana yake kuna watu wengine wakizungumza kwenye mikoa mingine tunakuwa tunagunaguna, mikoa mingine mna-support.

Mheshimiwa Spika, wamezungumza jana hapa Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Rukwa habari ya Ziwa Tanganyika, Wabunge tumewa-support na Serikali imewasikia, imekwenda kuwasikiliza. Tulizungumza sisi wafugaji ambao tulikuwa watu wanaofuga ng’ombe kuhusu mambo ya hereni, tumezungumza sana, Serikali ikasikia ikasimamisha mradi. Hivyo, wanapozungumza watu wa Tanga kuhusu eneo la Kiwanda cha Tanga Cement tuwasikilize. Kwa nini tusiwasikilize? Kwa sababu mikoa yote tumewasikiliza. Tuwasikiliza tujue nia yao ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa natazama haya maneno yaliyokuwa yanaendelea hapa, kilichokuwa kinazungumzwa. Ukiangalia kwenye mitandao yote hili jambo limeandikwa, ukiangalia kila mahali hili jambo limeandikwa na ukilitazama vizuri liko kisheria. Kuna mahakama, kuna taasisi zetu, Tume ya Biashara na kuna Tume ya Mahakama, wamezungumza vizuri, wametoa maamuzi yao yanafuatwa. Kwa nini Serikali haitaki kuchunguza haya maamuzi?

Mheshimiwa Spika, kingine, amezungumza Mheshimiwa Shabiby hapa, inawezekana kabisa na siyo kuwezekana, ndivyo ilivyo, Kiwanda cha Tanga ndicho kina deposits nyingi miaka milioni karibu 30 na Kiwanda cha Twiga kina mitambo mizuri sana hapa Tanzania. Sasa hapo upime uone; je, kitu gani kitahama, kama Twiga Cement itachukua kile kiwanda itachukua clinker na malighafi kutoka Tanga kuja Dar es Salaam au itapeleka mitambo mizuri ya Dar es Salaam kwenda Tanga? Waliangalie hili sana, waliangalie.

Mheshimiwa Spika, walipozungumza Wabunge wa Tanga maana yake tuna imani kwamba inawezekana wakaweka maboksi pale kikawa ni godown pale. Clinkers zote zikaja Dar es Salaam, cement ikazalishwa biashara ikaendelea, lakini itakuwaje kwa wafanyakazi?

Mheshimiwa Spika, katika viwanda, tuna aina mbili ya viwanda; kuna labour intensive na capital intensive. Kiwanda cha Tanga ni capital intensive, kiwanda chenye mtaji wa kati ambapo wafanyakazi wengi ni Watanzania, ndiyo wanaweza kutengeneza thamani ya mnyororo. Sasa leo tunaona kuuza ni sahihi, cement inaweza kutengenezwa hata katika maeneo yote ya Tanzania, lakini kwa sababu tumetawanya kwenye mikoa mbalimbali kila mkoa tunataka upate faida yake.

Mheshimiwa Spika, lazima Serikali iangalie watu wa Tanga, wananung’unika nini. naomba hili jambo Mheshimiwa Waziri asilichukulie kama kawaida. Maana yake nasikia mtu anasema ni kiwanda cha mtu binafsi, anauza, anafanyaje, hapana, viwanda vyote vilivyobinafsishwa vya Serikali ni lazima tukae na kuviangalia vinafanyaje kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba, Mheshimiwa Waziri namwamini sana, utawasikiliza Watanzania wanaonung’unika na utafanya maamuzi ili kiwanda kile kifanye kazi. Ni kweli mtu anayemiliki kile kiwanda hana uwezo, lakini ni kweli kama kuna wazawa wanataka kumiliki kile kiwanda tuwaruhusu wamiliki hicho kiwanda kama wana uwezo wa kufanya hivyo. Kwa hiyo naomba tuendelee kuangalia hili jambo linafanyikaje.

Mheshimiwa Spika, wakati niko kwenye Kamati ya Viwanda, mara nyingi sana wamesema tunajenga industrial park Bunda. Wilaya ya Bunda na Mkoa wa Mara kwa ujumla viwanda vya samaki vimekufa, viwanda vya pamba vimekufa, viwanda vya maziwa vimekufa, yaani ule mkoa sasa umebaki ni hewa tu. Tunaomba sasa Serikali iangalie Mkoa wa Mara kwa maana ya viwanda vya samaki, maziwa na pamba. Vinginevyo ule mkoa umebaki hewa, hakuna namna. Kwa hiyo naomba Waziri ufikirie jambo hili la kutufufulia viwanda ili watu wapate fedha katika Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Afya. Cha kwanza niwashukuru tu Waziri wa Wizara ya Afya, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wataalam wote wa Wizara ya afya. Kimsingi kwenye upande wetu wa afya kwa ngazi za juu wanajitahidi sana kufanya vizuri, wanafanya kazi nzuri na Mheshimiwa Ummy kwa kweli, ni zawadi tu ya kukupa mfanyakazi bora wa kufanya kazi za umma hatujakupa, lakini anafanya kazi vizuri sana. Hana mbambamba, yuko straight kwenye jambo hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo yananitatiza hapa naomba niyaseme tu. Hivi kweli toka tumepata uhuru tunashughulika na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza. Hivi kweli toka tumepata uhuru wakati wa Nyerere, zahanati zilikuwa chache sana na vituo vya afya vichache sana na kwenye Wilaya tunapata hospitali chache, lakini huduma zilikuwa zinapatikana. Hivi kweli nchi yetu leo tunapeleka mabilioni ya hela kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya na mikoa, lakini hakuna huduma, hakuna huduma kwenye zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli nchi yetu leo tunapeleka mabilioni ya hela kujenga zahanati, kujenga vituo vya afya, kujenga hospitali za Wilaya na Mikoa, hakuna huduma. Hakuna huduma kwenye zahanati, hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda pale Bunda, juzi nilikuwa natembelea hospitali moja ya Bukama mpya tumejenga ina Nesi mmoja. Huyo ndiyo alete dawa, atibu, afanye nini. Ni mwanadamu yule, anaweza kupata tatizo. Ukienda zahanati ya Matimero, kamejengwa kabanda watu wanazalia, wanazaa nje, ukienga Kambubu ni hivyo hivyo. Zahanati za Tanzania – sijui kuhusu maeneo mengine – lakini kwenye Jimbo langu hali ni mbaya kuliko kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunafanyaje, tunajenga majengo mpaka lini, yaani tunafanyaje kwa mfano? Kwa nini tusiamue hizi tulizonazo tukubaliane kupeleka wahudumu wa afya na wataalamu wa afya kwenye maeneo haya. Kwa nini tunajenga majengo makubwa? Nenda Hospitali ya Wilaya ya Bunda, jengo la kwangu, bilioni 35 iko pale, sijawahi kuona hospitali ya Wilaya rufaa inaenda kituo cha afya, sijawahi kuona ndiyo Bunda hiyo tunaiona.

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani mtu akienda hospitali ya Wilaya hapati dawa anakwenda kituo cha afya Ikizu ndiyo anapata dawa. Ikizu hiyo ni hospitali ya zamani ya mwaka 1959, imechoka. Kwa nini tusikubali, kwani sisi ni wafungwa wa mfumo wa D by D? Devolution by Decentralization sisi ni wafungwa? kwamba lazima tufanye hivi? Hivi kweli TAMISEMI kweli, ishughulike na ajira tunalia hapa, ishughulike na majengo tunalia hapa, ishughulike na TARURA tunalia hapa, ishughulike na kila kitu TAMISEMI?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusikubali tusijaribu maisha ya Watanzania hiyo Wizara ya Afya ichukue mfumo wote kutoka juu mpaka chini, kwa nini? Kwa nini tunajaribu maisha ya Watanzania, kwa nini watu wanakufa tunaona hadharani. Kwa nini watoto wetu wanakufa mtaani? Tuwaache Watanzania tuwatibu wapate akili, waweze kujigharamia wenyewe kwenye umaskini wao na ujinga wao waweze kusoma vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naomba kwa vyovyote vile itakavyokuwa Wabunge tukubali tuombe inavyowezekana, mbona tumeomba maji imewezekana, tumeomba kilimo imewezekana, kwa nini leo tunashindwa kuomba afya zetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunataka kutibu watu wetu kwa bima ya afya kwa wote, hivi kweli tutaipeleka bima ya afya kwa hali hiyo? Yaani Waziri anayeiamuri MSD atoe dawa ni mwingine na Waziri anayepokea dawa ni mwingine, haiwezekani. Madaktari wa zahanati, vituo vya afya na Wilaya wametuma hela kuja MSD kununua dawa, hela zinakuja MSD kununua dawa, dawa hazitoki, ni maneno tu. Nani atasema sasa huyu MSD atoe dawa? Tukubaliane kwamba jamani afya za Watanzania tusichezee, kama tumejenga zahanati zimefika mwisho tuongeze watumishi, hospitali na dawa watu watibiwe, shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna sera ya Taifa inalinda watoto, miaka mitano utakwenda utoe 54,000 utatibiwa, iko wapi? Watoto wanakufa nani anapokea? Hakuna kitu. Kwa hiyo, niombe kwenye hili jambo kwamba sasa tuna hali mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Mgeta cha kwangu pale tumejenga karibu milioni 500 lakini sasa nenda mortuary imejengwa 2018 haina jokofu mpaka leo, vifaa kuna ultrasound hakuna wataalam, tulijenga tulisema vile vituo vya afya vya zamani cha kwangu kilipewa milioni 400, tukaambiwa kwamba kuna milioni 700. Milioni 400 ya majengo, milioni 300 ya vifaatiba hakuna. Ni shida. Nani aamuru? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukubali kwamba sasa Wizara hii tusiweke afya za Watanzania kwenye mashaka, tuiweke iwe moja. Haya mambo ya D by D tuyaache, kwani nani anakufa, si dini tu, mradi ukubali mambo ya dini utaishi maisha yako marefu. Uwe Muislam utaishi, uwe Mkristo utaishi, hata ukiwa Mlokole, mradi tu uache dhambi. Sasa kwa nini tusikubali ili hospitali hizi zitoe matibabu, afya zetu ziende hii Wizara ichukue Wizara yote, ikope mikopo ya kutosha ilete kwetu hapa tufanye kazi. Kwa hiyo naomba hiyo inaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ummy, juzi nilikuwa India nikawa naongea na watu wa Apollo. Apollo ziko nyingi India. Sasa nikawauliza hivi ninyi mnafanyaje? Wakasema huku kwetu Waziri yeyote wa Serikali, hizi Apollo unazoziona ni za Serikali lakini ana uwezo wa kuja hapa akaangalia kinachofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri wakati tumekaa pale tunasubiri Waziri anafika pale. Dawa ni cheap, bei ndogo sana India dawa. Sisi kwetu hapa kila mtu ana bei yake, wala Waziri husogei, wala husemi. Tuna bei elekezi ya maji, bei elekezi ya mafuta, bei elekezi ya dawa hakuna, wewe kunywa tu ufe, hakuna! Hakuna bei elekezi! Tuna bei elekezi ya kila kitu lakini siyo dawa. Wewe nenda unavyotaka fanya unavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakaniambia bwana ninyi Watanzania afya zenu mnaweka siasa. Tusifiane hapa humu ndani lakini kwenye afya watu wanakufa, tusifiane nenda kwenye mstari utaendaje, utasemaje? Unakwenda kituo cha afya mtu mmoja utasema nini sasa, haiwezekani. Kwa hiyo ombi langu ni kwamba Wizara hii iwe moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ummy nilipokuwa India niliuliza hivi mashine hizi za saratani ninyi mnafanyaje, wakatuambia iko mashine inaitwa PET-CT Scanner, ninyi watalaam akina Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla mnaijua, ambayo imefungwa Ocean Road toka 2021 mpaka leo haijafanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ndiyo ukiiweka ikikamilika maana yake ukimwingiza mgonjwa yeyote mwenye saratani na magonjwa yoyote ya moyo inasoma moja kwa moja bila kuleta ujanja. Kwenye nchi zetu nasikia hapa Afrika Mashariki ni sisi tu tumenunua hapa ni bilioni 14. Sasa nikajiuliza bilioni 14 ndiyo nini? Kwa nini tusinunue ile mashine ikawepo Benjamin Mkapa, Wabunge tuko hapa ndiyo Bunge linaishi, ndiyo Mji Mkuu wa Serikali, ukimpeleka Mbunge pale mpaka umpeleke aende kupiga mionzi Dar es Salaam. Kwa nini tusinunue bilioni
14 ikakaa hapa, tukanunua Mwanza, tukanunua kwenye kanda, bilioni 14 PET- CT Scanner zikakaa pale zikatusaidia. Mionzi yenyewe mpaka uende kupigwa Ocean Road, hakuna Mwanza, tuna Hospitali ya Mkoa Mara imekaa pale Mheshimiwa Ummy, si uende uitembelee uione ina hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unatibu tu wagonjwa, jamani hivi hospitali ya Mkoa wa Mara imekuwa tena kama clinic? Maneno gani haya, imekuwa kama zahanati! Sasa Mkoa wa Baba wa Taifa mmeufanyaje? Jamani, mbona hali mbaya. Mama Maria badala ya kutibiwa pale Mkoani analetwa mpaka Dar es Salaam, mambo gani haya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi niombe hii PET- CT Scanner ifanye kazi lakini muilete Benjamin Mkapa, iende Mwanza, Mara, kila mahali iweze kufanya kazi, vinginevyo ndugu zangu mimi niwaombe hata ningeongea nini kama hii Waziri hatuwezi kuiunganisha tunapoteza muda. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Wizara ya Kilimo. Kwanza niishukuru Wizara kwa kupitia Waziri wake Mheshimiwa Bashe na wenzake wote na Mavunde wanafanyakazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni moja tu, jana nimesikiliza Ufaransa, wanasema Waziri Mkuu waliyopewa Ufaransa baada ya Emmanuel Macron kushinda ni mwanamke. Kwa hiyo, wenzetu nao wanaanza kuiga nchi za kiafrika kama Tanzania, kwamba akina mama wanafaa kushika uongozi wa ngazi ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini dhana yangu hapa nataka kuzunguza ni kitu kimoja tu kwamba, kilichompa uongozi wa uwaziri mkuu ni kwamba alipokuwa Waziri wa Kazi aliongeza ajira za kutosha Ufaransa. Sasa kwa nini, kwa sababu nchi za wenzetu ukimpa Waziri kazi unamuamini na unampa full mandate ya kufanya kazi hiyo. Mama Samia amekuja kwenye nchi yetu amewapa mawaziri wetu madaraka yote wafanye. Leo nchi yetu ikifeli kwenye kilimo; na ni wazo tu, kuna Waziri mmoja alikuwa anazungumza hapa juzi, akasema “akili ya afya”; alikuwa anazungumza Mbunge mmoja, sahani siyo Waziri; Mbunge mmoja, Balozi, anasema akili ya afya Watanzania inafanya tunakuwa masikini. Waheshimiwa Wabunge tumuachie Mheshimiwa Bashe na watu wake na Mheshimiwa Mavunde na watu wake. Kwa sababu wana uwezo wa kuonesha wana uwezo wa kufanya kazi tuwaachie madaraka yote wafanye tuone. Tumuulize Bashe wizara kwenye bajeti ijayo kitu gani kitafanyika?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, taarifa yangu ni fupi tu, kaka yangu Mwita pale anachangia anasema “akili ya afya” ni “afya ya akili” siyo “akili ya afya”. (Makofi/Vicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni dada yangu ni Kiswahili na mimi Kiswahili sikijui, namshukuru tuendelee. Kwa hiyo, niombe tuwape mandate ya kutosha. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuzungumza jambo moja kubwa sana. Waziri Bashe atuambie atakapokuja hapa, ni mikakati gani ataweka ili kuokoa ushirika nchini? Ushirika wetu umeyumba kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya kuwepo kwa ushirika nchini ni nzuri sana, lakini ushirika wenyewe umekuwa na uwezo wa kutosha. Ni kitu gani anafanya, ni sheria gani atatumia, ni kanuni gani atatumia, kama ni kanuni ndogo au kanuni kubwa, ni utaratibu gani atatumia kupunguza wezi wa mali za ushirika nchini? Atuambie mikakati yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru Mheshimiwa Bashe Mheshimiwa Rais wameleta Pikipiki 7,000. Niwaombe sasa, hizo pikipiki 7,000 basi akazifungie GPS. Pikipiki ukipeleka huko mtu anaishi Bunda, pikipiki inakaa Bariadi; mtu anaishi Tanga pikipiki inakaa Pwani. Pikipiki zetu zimekuwa za kutembeza kama bodaboda zifungieni GPS ili watu wajulikane wapo wapi, wanafanya kazi gani, wanafuatilia nini nadhani hili litakuwa jambo zuri sana kuwadhibiti wale maafisa ugani ambao umewapa nafasi ya kuhudumia wakulima…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kwa mchango mzuri.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, kwanza nimshukuru waziri mwenyewe na Naibu Waziri wake na watendaji wake wote wanaofanya kazi wanafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba Mashimba wewe ni ndugu yangu na unafanya kazi na unatembea kila mahali tunakuona unafanya kazi na Ulega lakini kiukweli wizara ambayo siielewe ni hii hapa. Siielewi kwa sababu gani najiuliza hivi sisi watanzania kwa nini tunakariri maneno tumekariri maneno kwa nini? Zero grazing kwa nini tunakariri? Wafugaji wanaangaika kila nchi kila mahali wanaangaika tuna pori mapori ya NARCO ambayo yana uwezo wa kuchukua ng’ombe 61,000 waliopo sasa hivi ni 19 zero grazing kwa nini tunaangaika wenzetu hawana maeneo? Nchi yetu bado nzima ukienda singida ukienda maeneo ya mapori yapo ya kutosha tuna Hifadhi za Taifa ziko 22 zinazofanya kazi na kutoa hela ni tano tu 17 zimelala.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna game reserve uwa najiuliza hivi maana ya game reserve ni ni hivi neno reserve maana yake nini? Maana yake sijui ukipata shida usaidiwe ziko 27 zinafanya kazi 5 tu, tuna open area tuna maeneo ya wazi mengi tu tuna misitu, wafugaji wanauwa ng’ombe eti Wizara ya Mifugo na Uvuvi kazi ya kufanya ni kupeleka hereni yani wananchi wale wanateseke wewe wanaenda tena na hereni wananchi wanateseka uwapi malambo, hivi hii wizara ikoje? Hivi tukifanya zero grazing watanzani hivi minada ya watanzania si ndio study tour yao hivi leo mbuzi unaweza kwenda mnadani ukanunua mbuzi mmoja laki moja utaweza?

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi mbona Wabunge wote kila mnada mnaenda na watu wanaishi pale kwa starehe kwa nini tusitafute solution ya wafugaji tukawapa maeneo. Sikubaliani leo kwamba pori fulani tuwape wafugaji tukiwapa pori tuwapangie vitalu, na walipe kodi leo ukienda Misenyi ng’ombe wale walioko NARCO misenyi ile inahitaji ng’ombe 15 wako ng’ombe 900 kila mahali mashamba ya Serikali yapo hayana ng’ombe wafugaji wanateseka kila mahali na ng’ombe tunakula nyama tunakunywa maziwa kuashia koo imeisha ipo tu why.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe waziri najua unafanya kazi na wenzako sasa mkae kwa kweli hii bajeti tutawapitishia lakini bajeti ijayo mtatuambia hivi kazi kweli humu ndani ikoje? Hivi kuna nini kwa nini watu wanateseka? Amezungumza Mbunge mmoja hapa ukianza kuzungumza habari ya mfugaji umezungumza mwananchi, watu wanateseka mali zao zinaisha, nenda umasaini ng’ombe zinaisha kila mahali nenda Mara juzi nimekwenda pale Mto Mara mtu wangu amenywesha ng’ombe mkasema mavi yamekuja ng’ombe wahame, mavi yanauwa samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jamani ehe! tukubaliane kwamba hawa wafugaji mnataka tuweje? Tuna nchi yetu ina mifugo mingi, tunakula nyama mnadani, tunatosheka na nyama, halafu tunafilisi watu tuteseke, kwanini tuteseke? Kwa nini wananchi wateseke na nchi yao ipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani nendeni Hispania, mimi nimekwenda Hispania pale, wana eneo kama Mkoa mzima, wanazo block za kutosha, wana ng’ombe wa kutosha. Hiyo haitoshi, Mheshimiwa Waziri Mashimba hebu nikuulize swali, hivi leo una ng’ombe wapo hapo NACRO – Kongwa, hivi ukichukua madume kwa sababu dume moja linazalisha majike 25, hivi ukichukua madume yale ukawagawa hata kwenye Kata madume 40 ni ng’ombe 1,000 tukaanza kubadilisha ufugaji wetu kwa kutumia madume yetu, hivi shida iko wapi? Shida ni nini?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani Mwalimu Nyerere alipeleka ng’ombe kila mahali kila kijijji, leo hakuna kitu, mnaacha wafugaji wanaisha lakini mnadani mmekaa na vitabu mnakusanya ushuru, mnakusanya wapi? Mnada wa kwenda Kenya badala ya kwenda Tarime mpakani alivyozungumza Mbunge hapa mnaweka kirumi, maana yake ndiyo nini kirumi mimi sielewi sasa, yaani mnapokwenda kuweka mpakani kirumi ukienda Misenyi tunapambana na Uganda kwa malisho, mnasema Uganda wanakuja kulisha huku ndani, hivi pori limejaa na majani yapo, kwa nini watu wasilishe, shida nini? Mkae mpange! Wizara hii nami naanza kuitilia mashaka, hivi kweli mnapigania ng’ombe au mnampigania nani? mnapigania samaki au mnampigania nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi naomba mkae…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere hebu subiri kidogo hapo, Mheshimiwa Lucy uko salama hapo? Upo salama, kama upo salama kaa pembeni, maana yake! Haya Mheshimiwa Getere endelea. (Kicheko)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipunguza, maana yake jazba ni kubwa sana kwa sababu mimi kuna vitu naviangalia miaka nenda rudi, miaka nenda rudi, watu wanahama wanafilisika, mtu alikuwa na ng’ombe 1,000 zinakuwa mia mbili, zinakuwa mia, zinakuwa sifuri, kila mwaka watu wanahama, ardhi ipo imejaa Tanzania, hamuweki!

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mashimba sasa nikuulize swali, juzi nilikuja ofisini kwako na Diwani na Kata ya Salama na Kata ya Kiloleli mkatuambia mnatupa majosho yale mawili, Kiloleli na Salama Kati, mkatuonesha bajeti je, hizo fedha ziko wapi? Mpaka leo hatuzioni, eti Wizara ya Kilimo fedha zake Milioni 18 za kwenda kuchimba majosho mpaka sitolewe kwenye Wizara! Eti yenyewe haitoi Wizara, yaani humo ndani kuna matatizo humo ndani! Hii Wizara muitengeneze, ninawaomba Watendaji wenu muwatengeneze ninyi ni viongozi wazuri, nawashukuru sana muendelee kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Wizara ya Michezo; mimi leo yangu ni ya ushauri tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuwateua watendaji wazuri katika Wizara hii Mheshimiwa Mchengerwa na mwenzake Naibu, Katibu Mkuu na watendaji wote wanafanya kazi nzuri kwa kweli, kwa mara ya kwanza na mara nyingi tumeona sasa michezo hii inaenda na watu wanahangaika kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nimshukuru kwakweli Mheshimiwa Rais kwa sababu Wizara nyingi amechagua watu sasa wenye mtazamo mpana, vijana walikuwa wanalia mara nyingi kwamba tunaambiwa sisi ni vijana Taifa la kesho, kumbe wanasema Taifa la leo, wamepata nafasi tunataka waitendee haki Wizara zote walizochaguliwa vijana, Mheshimiwa Mchengerwa nakushukuru sana kwa uchapakazi wako.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kushauri mambo machache tu; ushauri wa kwanza alikuja hapa Mfalme wa Morocco tukaoneshwa uwanja hapa Dodoma na magreda yakaenda pale yakatengeneza uwanja ule na tukaahidiwa kwamba uwanja huu utakuwa upo tayari sijajua ni mwaka gani lakini maana yake ulikuwa upo busy kwenye huo uwanja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka kujua tu kwamba je, hilo wazo la kujenga uwanja wa Dodoma pale limekufa au linaendelea? Maana sasa sioni kwa mfano kwa Tanzania kama kweli tunapata msaada hivi hata kuweka uzio ni kiasi gani hicho, kuonesha kwamba sisi tuna uwanja na tumeuwekea uzio. Uwanja huu wa Dodoma ambao ndio uwanja wa kitaifa tungeweza kuwa nao kwa sababu tulipata msaada na tungeendelea kuona uwanja kwamba uwanja huu unapendeza kwa Jiji la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri mwingine ninaotaka kutoa, sasa tukubaliane Wizara hii ya Michezo na Serikali kwa ujumla watupe shortlist hivi tuna mikoa 26, mikoa mingine ina viwanja hivi kuweka nyasi za bandia kwenye hivyo viwanja kuna shida gani? Ni fedha kiasi gani zinahitajika kwenye hivyo viwanja?

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Wizara kwenye bajeti ijayo mtuambie kwamba katika viwanja tulivyonavyo 26 vya mikoa ni vingapi vimewekwa nyasi bandia. Lakini hili niseme mimi niombe TFF kama sio TFF Wizara ya Michezo nendeni mkatoe tuzo maalum kwa Bakhresa (Azam Tv) muwape tuzo maalum wapeni tuzo maalum Bakhresa (Azam Tv) wametufanyia kazi nzuri sana kwenye nchi hii vijana wetu wengi walikuwa sasa wamelewa Ulaya wanatazama ligi za Ulaya, leo kila mtu yupo kwenye tv ya Azam wapeni tuzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Mheshimiwa Waziri wewe ni kijana, angalia na Serikali yako mkae vizuri na Mawaziri na wetu wengine na Waziri Mkuu nendeni mkamwite Bakhresa na timu yake na makampuni yake yote, kampuni ya Bakhresa inafanya kazi nchi karibu 55 karibu 60 mwambieni tutengenezee nyasi za bandia, mpunguzieni bei zote za vifaa vya michezo, viwanja vyetu vyote vitakuwa na nyasi za bandia kwa kupitia Bakhresa kwa sababu biashara hii anaiweza. Kwa hiyo niwaombe kwamba sisi tusihangike mambo mengi, tuna mtu ambaye ni msamaria na mzalendo wa kweli kweli katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpeni viwanja vyote 26 vya mikoa na vile vya Zanzibar vilivyopo Zanzibar atengeneze mpunguzieni bei ya baadhi ya vifaa vinavyohusika mimi nadhani hilo linaweza kuwa wazo zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine michezo ni ajira, nilikuwa naomba sasa kwanza demokrasia TFF, kila tukifanya uchaguzi wa TFF wa Rais kila mara kunakuwepo na watu mara wanakamatwa, mara karatasi zimepungua, mara watu wamefungiwa, mara sijui kuna nini, kuna nini TTF, kuna nini humo ndani kila uchaguzi ukija wa TFF hadi watu wafungwe, wengine waende lock up wengine wafanywe nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri uchungulie humo ndani hii ni kazi ya utendaji; wekeni demokrasia ndani ya TFF, anayegombea kama anastahili apewe fomu, ajaze fomu vizuri na ashinde, kwa hiyo nafikiri kwamba hili nalo tulitazame na tuone linavyokwenda kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini academy, tujitahidi sasa tuna kanda sijui ngapi ikiwemo Kanda ya Ziwa, lakini kanda zipo nyingi kuna Kaskazini, kuna Kusini, kuna Kanda ya Ziwa tukajenga academy kwa hizo kanda tukubaliane kwamba sasa academy ziwepo kwenye hizo kanda, lakini tuhakikishe kwamba kwa kila timu ya ligi kuu inakuwa na timu ndogo inakuwepo academy zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuhakikishe kwamba hilo linakuwepo, tupate wachezaji bora kwenye maeneo yote, lakini pamoja na hayo niwapongeze sana Tembo Warriors ambao walikuwepo, ile timu ambayo inakwenda kuchezo Kombe la Dunia, mimi naomba hata Wabunge tuwachangie, kwani kuna shida gani mbona watu wengine tunawachangia. Hebu kaeni vizuri tuangalie hayo mambo, tuangalie hawa watu ndio neema tunaipata hivi mtu anahangaika kwenyewe na fimbo yake na nini hadi anashinda anakwenda Ulaya tunashindwa nini kuwachangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali ikae vizuri wachange na sisi Wabunge tuwachangie, mimi nafikiri kwamba hili ni jambo zuri na timu zote zinazoshiriki tuone nafasi gani tunawachangia ili na wenyewe waweze kucheza vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimefurahi waliokuwa wanazungumzia wanamuziki, jamani wanamuziki wetu wa Tanzania wanahangaika sana, nilikuwa nasoma historia ya Diamond alivyoshinda kwenda kuwa mtu maarufu, wanahangaika wanakwenda kwenye ukumbi wanafukuzwa, wanahangaika sana hakuna chombo cha kuwashika, wakipata wenyewe wakishakuwa maarufu ndio tunaanza kuimba, wamezunguza watu wengi hapa tutafute namna ya kuwashika mkono, vijana wapo wengi hata Jimbo la Bunda tunao vijana wengi sana wanaimba vizuri, lakini namna ya kufika huku inakuwa shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutafute mfuko maalum ambao utakuwepo wa kuwasaidia wasanii, tuweke mfuko maalum uwe chini ya Waziri Mkuu ambao utawasaidia wasanii wetu waweze kufanya vizuri kwa sababu ni ajira. Lakini mfuko huo pia uwepo wa kusaidia timu za Taifa. Sasa timu kama ya Biashara ya Mara leo wamenyong’onyea inafanya vibaya watu wanaiona kama timu imefanya vibaya, lakini ile timu imeshindwa kwenda kucheza michezo ya nje, imekosa nauli ya kwenda huko, sasa leo wanacheza kwenda wapi, wanasikitika Mungu wangu, sasa wanajiuliza tukicheza tukishinda tunakwenda wapi, hakuna fedha ya kutupeleka kucheza michezo ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuundeni mfuko wa kusaidia vilabu ili viweze kufanya vizuri tunakokwenda nakushukuru kwa yote hayo. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, cha kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa utulivu wa nchi yetu, lakini pia kwa kutupa nafasi ya kujadili masuala yanayohusu nchi yetu kwa uwazi na bila woga. Sasa kazi iliyobaki ni sisi Wabunge kuwasimamia wananchi ambao wametutuma kuja hapa kusema haki na kuwasemea katika mambo yale ambayo ni maovu.

Mheshimiwa Spika, hii document ya CAG iko wazi, ni public document kwa hiyo kila mtu anaiona. Hata hapa mtu akisema ataonekana kwamba labda huyu akisema hivi amesema vibaya tutakuwa tunajidanganya tu, kwa sababu hii document iko wazi na hata mataifa mengine wameshaisoma. Kwa hiyo, ni kazi yetu sisi Wabunge kuwasemea wananchi ambao wametutuma kuja hapa kusema yale ambayo yanawafaa. Maana yake itakuwa ngumu sana kutosema ambapo unaangalia kila kurasa tatu za majedwali, kila majedwali kumi, matano, manne, matano, sita, saba Halmashauri ya Bunda imo.

Mheshimiwa Spika, kila ukizungumza wizi wa vifaa vya tiba Halmashauri ya Bunda imo, kila ukiuliza sijui hela za POS hazikuja Halmashauri ya Bunda imo. Wakati fulani inaniwia vigumu sana kusema hii ripoti kila wakati inaangalia Bunda na Bunda ndiyo jimbo langu na Halmashauri ndiyo Halmashauri yangu, mnaohusika mmeiona hiyo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa najiuliza maswali mengi na Bunge lililopita tulisema hivi haya maazimio tunayoweka humu ndani yanaenda wapi, yaani nani anayatekeleze? Sasa nikajiuliza wewe Spika na Bunge lako katika Katiba Ibara ya 143 umepewa mamlaka, Ibara ya 96(1) imelipa mamlaka Bunge hili kuunda Kamati mbalimbali na tumeweka PAC, tumeweka LAAC na tumeweka PIC.

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza tuunde Kamati nyingine ambayo itakuwa inafuatilia maazimio ya Ripoti ya CAG. Najiuliza tarehe 2 Novemba, 2022 tulizungumza juu ya KADCO na tukaamua katika azimio kwamba sasa Serikali iende ikachukue uwanja wa KIA yaani Kampuni ya KADCO itoke uwanja wa KIA ikabidhiwe Serikali kwa Mamlaka ya Ndege Tanzania.

Mheshimiwa Spika, azimio tumeweka na mbaya zaidi nimesoma hapa mpaka Baraza la Mawaziri wameweka wamezungumza hili jambo, mpaka leo tunazungumza hamna kitu. Sasa hayo maazimio tunampa nani, yaani hii kelele tunampigia nani kwa mfano, maana yake mimi naona wezi wote tunaowazungumza humu ndani wengi wameteuliwa na Mawaziri, wengi wameteuliwa na Rais na wengi tunao sisi Chama Cha Mapinduzi ambao ndiyo waamuzi.

Mheshimiwa Spika, yaani Rais wa Chama Cha Mapinduzi, Mawaziri wa Chama Cha Mapinduzi, wezi wanaiba, chama kinawataka wawafukuze wezi hawawatoi. Maazimio ya Bunge tunataka, maazimio ya Bunge hili, mwizi na mtetea mwizi wote waende lock up wote mazianyati, tumechoka sasa, tunamtetea nani? Kwa mfano, sasa lile azimio limesema, ninajiuliza hiyo KADCO ni mtu au ni nani, yaani KADCO ni chombo fulani au nini sasa?

Mheshimiwa Spika, kama azimio la Bunge limesema, Mawaziri wamesema na jambo halitekelezeki na siyo kwamba hiyo KADCO inaleta faida, imetengeneza hasara karibu ya shilingi bilioni sijui tano. Hivi ni nini sasa tunasema, tunazungumza kufanya nini? Mheshimiwa nafikiri kwamba tuunde Kamati nyingine ambayo itashughulika na jambo hilo ili itusaidie.

Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa nasikia Wabunge wanazungumza wizi wizi, wizi, nimesoma ripoti hii nimegundua kumbe wizi siyo peke yake tu, yaani hapa tunapokwenda kunadalili ya mauaji ya Watanzania wasio na hatia. Hivi kama vituo vya afya na zahanati 16 na kama hospitali za mkoa na hospitali za rufaa 17 zinakuwa na madawa yaliyoisha muda wake zaidi ya miezi mitatu mpaka miaka kumi ikiwemo Benjamin Mkapa ambapo tunatibia Wabunge.

Mheshimiwa Spika, dawa zimeisha muda wake zenye thamani ya shilingi bilioni 3.5 zimeisha muda wake, sasa hapa tunasema nini, tunazungumza kupata nini? Yaani leo Tanzania ambayo tuna wasomi, tuna mifumo ambayo inaangalia expire date iko wapi kwneye dawa, leo tuna dawa, vituo vya afya, zahanati, bohari kuu zimeisha muda wake na zipo. CAG anasema miezi mitatu mpaka miaka kumi, zipo.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni dalili moja wapo ya kwamba huko tunakokwenda tutaua Watanzania wasio na hatia na wataalam tunao. Mimi nafikiri kwamba nalo hilo tuliangalie maazimio haya tunampa nani? Lazima tukubali sasa kwamba Bunge lijalo kama kuna Ripoti ya CAG tupate kwanza maazimio yetu tuliyoyaweka Bunge hili kama yametekelezwa, kama hayakutekelezwa hakuna haja ya kujadili, tunajadili nini sasa. Nafikiri kwamba tuangalie kwamba inakuwaje.

Mheshimiwa Spika, nimeangalia kitu kinaitwa GPSA, taasisi mbalimbali zimeagiza magari shilingi bilioni 35 point, mpaka ripoti hii inatengenezwa hayajaja, labda sasa sijui kama tutajibiwa au itakuwa muda mwingine. Shilingi bilioni 35 magari yameagizwa hayaji, watu wanadai magari, hayaji, hela zimetolewa. Sasa tunamwambia nani? Tuunde Kamati ya kufuatilia maazimio hayo ili tuweze kuwa na uhakika wa jambo hili.

Mheshimiwa Spika, kuna mikataba yaani tunaajiri wakandarasi, tunatengeneza mikataba, tuna wanasheria na tuna kila kitu, riba shilingi bilioni 418; yaani tunalipa watu hewa, mtu umemtengenezea mikataba riba shilingi bilioni 418, ukigawa kwa shilingi 500 kituo cha afya ni vituo karibu 387. Tunagawa, yaani unawapa watu bure tu, shilingi bilioni 418. Watoto wanakaa chini, hali ni mbaya zahanati hazijafikia, tunagawa. Kwa hiyo, nafikiri kwamba tuunde kamati ya ufuatiliaji wa jamnbo hili.
Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho, Wabunge wamesema mambo mengi hapa ukisema ni kumalizia tu, mambo mengi yamezungumzwa humu ndani. Amezungumza mtu mmoja hapa jana Mbunge na Wabunge wengi wamesema hili Bunge letu sasa linatazamwa, lina Spika wa Mabunge ya Dunia. Kwa hiyo, sasa lazima tuangalie na nimekusikia kwenye kauli yako wakati unahitimisha baada ya kupata zilke kura nyingi ukasema kwambva IPU fedha zao mali yao itakaa salama. Naomba sasa usalama wa Watanzania wa mali za umma ukae salama kwenye Bunge hili waanzie hapa. Nikuombe waanzie hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Mkurugenzi hivi tukizungumza hapa tunamzungumza Rais, hivi Rais amemteua Mkuu wa Mkoa amemteua Mkurugenzi kwenda kuiba?

MJUMBE FULANI: Hapana.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, Rais amemteua Mkurugenzi kwenda kuiba? Tunamsaidia Rais wezi wote walioiba huko dani tuwatoe. Siku moja niliwahi kusema hapa na narudia…(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Getere malizia sekunde 30 muda wako umeshaisha.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, niliwahi kusema hapa, nikibahatika kupata Uwaziri au Unaibu Waziri baada ya siku tano mtakuwa mmenifukuza, kwa sababu ziara yoyote nitakayoenda kila nitakaemkuta ameharibu ni lock up, lock up, lock up, nikirudi mtasema nimekiuka demokrasia, mtanifukuza kazi, ahsante sana. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi hii nami nitoe mchango wangu. Kwanza, nampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutuletea hii miswada mizuri sana; inaonekana wamefanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikutie moyo na wewe Mama Mchapakazi; inavyoonekana ni kwamba kuna watu hawaelewi. Kuna mambo mawili duniani yanapatikana tu kwa kufanya kazi, kwamba busara na umaarufu, hakuna chuo cha busara wala umaarufu. Kwa hiyo, umaarufu wako na busara yako ni kushinda matatizo. Kwa hiyo, nawe unaelekea kushinda matatizo, tunakupongeza kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, nilikuwa naangalia hizi sheria, sasa najiuliza, kwanza nimeangalia mambo hapa. Kuna watu tunazunguza mambo hapa bila kujali tunapoelekea. Nchi yetu hii tuna watoto wa mitaani au watoto kwa mfano tunaita mayaya sijui, wale wanaofanya kazi nyumbani wanaitwaje? Wamejaa hata kwenye nyumba za Wabunge humu ndani, lakini sasa tunaangalia tu jambo hili, jambo hili; la pili hatuangalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukiangalia hapa ni kitu kimoja, ninachoomba ni Serikali itafute vipimo vya DNA, vitapakae kwa kila Halmashauri na kila vituo vya afya ili tuweze kujua nani kampa mtoto huyu mimba? Maana watoto wa mitaani hata tunaowaona Dar es Salaam, wengine ni wa watu wakubwa tu. Tumeona kesi kubwa kabisa inaendeshwa na watu, viongozi wakubwa tu wana watoto. Sasa nataka tujue, Mwanasheria aniambie, hivi vipimo vya DNA vinapima muda gani? Kabla au baada? Tujue maana yake! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mimi nimempa mtu mimba halafu kwa ushahidi wa mazingira, ukanifunga miaka 30. Waziri wa Sheria uko hapa, nikapigwa miaka 30, nikarudi baada ya miaka 30, nikafanya utafiti mtoto aliyezaliwa DNA ikaonesha siyo wangu na wamenipiga miaka 30 inakuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri kwamba hivi vitu tuviangalie inavyokuwa. Vile vile sheria hii ukiisoma vizuri hapa kwa Mwanasheria alivyotuletea hapa, inamzungumzia mwanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari, ndiyo inavyozungumza. Sheria kuu inasema, anayepewa mimba ni mtoto wa chini ya miaka 18. Sasa kwa elimu yetu kuna watoto wanasoma kwa mfano Sekondari, kuna mwanafunzi ana miaka 18, akipigwa mimba inakuaje? Anahukumiwa kwa uanafunzi au kwa umri wake? Maana nataka kuliona hili nalo limekaaje hapa ili tuweze kujua wanahukumu kwa umri au utoto? Kwa sababu inaonekana hapa tunazungumzia wanafunzi wa Primary na Sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ninachokiona ni ile adhabu tunayotaka kuitoa. Tunatoa adhabu ya miaka 30, sasa najiuliza, hii adhabu tunamwadhibu mhalifu au tunaiadhibu Serikali? Kwa mfano, unamfunga mtoto wa Chuo Kikuu, inawezekana akampa mtoto wa Primary au wa Sekondari mimba, tukampiga miaka 30, lakini miaka 30 hiyo Serikali inatoa chakula, inamhudumia Gerezani. Sasa tunaimpa adhabu Serikali au mhalifu? Kwa sababu mhalifu atakwenda atasoma, atafanya ufundi na kadhalika. Tuangalie na hii miaka ambayo tunaitoa.
Mheshimiwa naibu Spika, kingine ambacho nataka kukizungumza hapa ni wale wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi; na wakati fulani sasa tunamwacha mzazi miaka 18. Halafu tumesema kwamba atakayesaidia mtoto kupata mimba huyu naye tumshitaki. Sasa tunajiuliza, ni nani anayesaidia? Kwa mfano, chini ya miaka 18, wale wanaomaliza Darasa la Saba wako wa miaka 7, 8, au 9; Je, akitoroka yeye amekwenda mjini, wako wanaokwenda kusalimia mjini, sijui wanaenda kusalimia shangazi wapi, wakitoroka huko, halafu unamkamata mzazi wake? Una maana gani? Unamwonea. Wanaosaidia ni akina nani hawa? Pengine nafikiri wanaosaidia ni wale ambao kwa mfano, Serikalini wamekwenda wamefanya mkataba wa mtoto kuolewa. Amepita kwa Mwenyekiti wa Kitongoji amekubali, amepita kwa Mtendaji wa Kijiji amekubali au Mzazi wake amechukua mahari, hapo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, kama mtoto ametoroka, halafu unasema mzazi wake amemwoza Dar es Salaam, anajuaje? Tutaonea watu hapa. Lazima tuangalie ni namna gani tunafanya katika kutetea haya mambo. Vinginevyo kikubwa ninachokiona mimi ni DNA. Serikali ilete DNA itapakae kila mahali, tuipeleke kwenye Vituo vya Afya ikae pale halafu tulete wataalam ili mtu ahukumiwa kwa ukweli. Kama amempa mtu mimba, ioneshe kwamba hii mimba ni ya mtoto kabla hajazaliwa ili mtu akahukumiwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. BONIFACE M GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nipate kuchangia katika miswada hii miwili. I declare interest kwamba ni member wa Kamati hii sasa kwa bahati mbaya unasema Kiswahili lakini lugha yenyewe ya chemistry na yenyewe inahusu Kiingereza sana. Sasa ndio maana…
NAIBU SPIKA: Kwa mfano neno member ni mjumbe huna haja ya kusema member unasema mimi ni Mjumbe wa Kamati, sio? (Kicheko)
MHE. BONIFACE M GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa kuleta miswada hii mzuri sana. Waziri na Naibu Waziri wake tunawashukuru sana, Kamati na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kwa ujumla sisi tumepitia sana hii miswada yote miwili lakini kwangu leo mimi nitajikita kwenye Muswada huu wa Government Laboratory Authority Act 2016 ambao ukija hapa utachukua page namba 16 mpaka 35.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka tu nizungumze mambo yanayohusu Wabunge kwa ujumla, mjue hali halisi ilivyo kwenye maisha yetu Watanzania. Kunazungumzwa mambo ya sample au sampuli. Kuna sampuli za aina mbili, kuna zile signal ambazo zinachukuliwa na polisi wakati mtu akihisiwa kwamba amekunywa sumu au ameuawa kwa sumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo sasa hapa ni namna gani hiyo sample au hivyo vipimo vya mtu aliyefariki inachukuliwa na polisi kutoka kijiji A mpaka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Kuna matatizo makubwa sana ya kufanya hiyo postmoterm anapokwenda kuchukua daktari, anapokwenda polisi. Polisi mwenyewe kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali mpaka alipwe na analipwa na mtu ambaye amefiwa. Sasa imagine kwa mfano mtu huyu ni maskini anafanyaje, inakuwa ni shida na Mkemia Mkuu wa Serikali ukipeleka lazima uwalipe. Sasa hii naishauri Serikali kwamba katika hivi vipimo ruzuku zitolewe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali katika maabara hii ili pale ambapo watu hawana uwezo wa kupima vipimo hivyo waweze kupimiwa bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna zile sample zinapochukuliwa kutoka kwenye viwanda, environmental pollution, yale maji machafu yanatoka kwenye viwanda wanakwenda kupima, mathalani ni kijiji A kimepata athari, wamepiga kelele amekuja mtaalam wa NEMC amechukua vipimo amepeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Mkemia Mkuu wa Serikali anataka hela, mtu wa NEMC wa kupeleka hiyo sample anataka hela na vipimo kutoka kwenye viwanda kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali unalipa milioni tatu mpaka milioni saba.
Sasa ni lini wanakijiji watapata haki hiyo? na anayelipa hizo hela milioni tatu, milioni saba ni mwenye kiwanda. Ambaye anatuhumiwa ndiye mlipaji wa hizo hela. Kwa hiyo, hapa tunafikiri kwamba Serikali iweze kutoa hela nyingi kwenye maabara hii ili tuweze kupimiwa, kwa mfano wanavijiji ambao hawana uwezo waweze kupimiwa bure ili waweze kupata haki yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho mimi nakizungumzia hapa ni suala la DNA. Nimezungumza kwenye kipindi kilichopita kwamba wakati fulani hiki kitu usipopima vizuri watu wataozea magerezani. Mathalani unapelekwa kufungwa kwa hisia tu kwamba mimi nimempa mtoto mimba, mtoto wa shule miaka 10, 20, unaenda unafungwa miaka 20 au 30. Siku unatoka kwa sababu kipimo chenyewe kinasema mpaka mtoto apatikane, sasa miezi tisa imepita, mtoto amepatikana amekwenda kufanya utaalam wakasema mimi siye niliyeweka hiyo mimba na mimi nimeshaozea magerezani, sasa haya ni maneno gani haya? (Makofi)
Kwa hiyo nafikiri kwamba wataalam nao wajikite zaidi kujua vipimo hivi kabla mtoto hajazaliwa ili mtu aweze kuokoka kwa kujua kama mtoto si wake. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vingine katika hii DNA ni suala la kuangalia, wamezungumza wengi, Kambi ya Upinzani imezungumza sisi kamati tumezungumza. Hivi hawa watu wakemia hawa! Kwa mfano mimi nahisi mtoto si wangu, nimekwenda kusoma Marekani nimerudi, sura nikiangalia mpaka kidole sio changu sasa naanza kujihisi, hapa kuna nini? Sasa napeleka kutafuta DNA, sasa huyu mtu ana nafasi kubwa sana ya kusema mtoto huyu ni wako. Wakienda wakakubaliana na mke wangu kwenye mambo fulani hivi akasema ni wako sasa halafu mimi nikagundua si wangu namfungia wapi? Tunawapa nafasi kubwa sana hawa, tutafute vifungu vya kuwabana ili waweze kuona kwamba namna gani itaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vinginevyo ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge mimi nimefurahi sana jana. Jana tumepitisha muswada mzuri hapa, nimshukuru Mheshimiwa Halima Mdee na Mheshimiwa Mama Profesa pale, wametuletea vifungu, huu ni muswada unahitaji vifungu, sasa maneno ya kebehi ya nini hayana maana humu ndani. Kwa hiyo, nafikiri kwamba muswada wa jana ulikuwa mzuri sana na huu unaokuja tukubaliane kwamba hali ndivyo ilivyo. Kwa mfano leo tunasema Waziri asiteue, lakini Mawaziri wote wanateua. Sasa kama tunataka Waziri asiteue Baraza basi tulete sasa muswada humu ndani au maombi rasmi ya kuondoa Mawaziri wote wasiteue Mabaraza. Sasa huyu Mheshimiwa Ummy Mwalimu tutakuwa tunamuonea sisi hapa. Kwa hiyo, tumruhusu kwamba hii kazi ni ya kwake lakini naye aweze kukaa na management yake huko tunakokwenda mbele tufanye mabadiliko kama alivyosema Mheshimiwa Dkt. Ndugulile.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vinginevyo niishukuru Serikali, niwashukuru na Wabunge wote, tufanye mambo kama ya jana, tuonekane Bunge liko vizuri tusizomeane, sisi sote ni ndugu, unanizomea mimi ndugu yako!
Mheshimiwa Katekista Selasini, unanizomea wakati tunasali wote? Mimi ndugu yako! Sasa unanizomeaje? Kusema kweli mimi nilifikiri kwamba iko siku kama haya mambo yataendelea mturuhusu tuingie humu na rungu basi tupigane halafu tuendelee kushindana humu ndani. Naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2019
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamati za pande zote, wamefanya kazi nzuri. Niwashukuru Wabunge wote waliozungumza mambo ya kisheria na yasiyo ya kisheria. Niseme wazi tu kwamba kutunga na kubadilisha sheria siyo rigid kama walivyosema wengine, siyo Biblia, inaweza kubadilika wakati wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka kwamba unaweza ukafanya jambo baya leo kesho ukalifanya kuwa zuri. Miaka michache iliyopita tulishuhudia hapa mkwarema wetu hapa Mheshimiwa Zitto akifukuzwa na CHADEMA kwa nguvu zote lakini leo CHADEMA wamemkodi kuwasemea mambo hayo wanayotaka wao. Kwa hiyo, kwa lugha rahisi ni kwamba leo CHADEMA imefyata mkia kwa Mheshimiwa Zitto, amekuwa mtu wao kwa lugha hiyo ambayo anazungumza nayo.

T A A R I F A

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kwa kusema kwamba mashirika haya yaliyopo sasa hivi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere, kuna taarifa.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji, CHADEMA hatujamkodi Mheshimiwa Zitto, ana haki ya kuzungumza kama Mbunge yeyote kwenye Bunge hili, achangie sheria zilizopo Mezani asitafute umaarufu kupitia kwa watu wengine.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere, endelea na mchango wako.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, huyu ameshachoka na akili yake, tuendelee na mambo mengine hapa. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu wazi…

MHE. TUNZA I. MALAPO: Umechoka wewe, mtu mzima hovyo! [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, no, hii lugha si sahihi, naomba afute hii lugha.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zitto, nafurahi kwamba umesimama wakati wamezungumza wote wawili, ungenyoosha huku ukanyoosha na huku, kwa nini unaonesha upande mmoja? Nyoosha mikono pande zote mbili ili uonekane unatenda haki, siyo unaona upande mmoja halafu jicho lako moja halitaki kuona.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere, akili yake haijachoka lakini pia Mheshimiwa Getere siyo hovyo kwa hiyo maneno hayo yote yanaondoka kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Kicheko)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme tu kutoka kwenye roho yangu, kwanza kuna sheria nyingi sana zimetungwa hapa, kuna mtu amehoji kuhusu Miswada au sheria tisa kuzungumzwa hapa sijui ni Kanuni gani imevunjwa, kama hakuna Kanuni inayovunjwa hata tungezungumza Miswada au sheria 18 au 30 hakuna kosa kwa sababu vitabu vyote viwili vimeeleza vizuri, cha Upinzani na kitabu cha Mwanasheria na cha CCM kwenye upande wa Kambi ya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana …

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kwamba Mheshimiwa Zitto Kabwe alifukuzwa CHADEMA na aliyekuwa amepewa jukumu la kumshughulikia ni Mheshimiwa John Heche na ndiyo maana alivyoshinda Uenyekiti wa Vijana Kafulila aliondolewa akapewa Mheshimiwa Heche na leo bahati nzuri ndiyo anamtetea Mheshimiwa Zitto, kwa hiyo hiyo ndiyo siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ilikuwa ni taarifa tu Waheshimiwa Wabunge. (Kicheko)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshemiwa Getere, endelea na mchango wako.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa nimeipokea, mimi nasema kwamba haya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana faida kubwa sana katika nchi yetu na yanafanya kazi nzuri lakini Bunge hili na hasa Bunge la Awamu ya Nne na baadhi ya Wabunge wamekuwa mawakala wa kutetea mambo ya hovyo katika nchi yetu. Haiwezekani tukawa na mashirika yalitoka nje, kwa mfano, shirika limekuja hapa limesajiliwa labda kwenye Mkoa wa Mwanza, ni mkoa mzima, lakini shirika linajikita kwenye eneo moja tu, linafanya kazi zilezile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya hata Wabunge hawaelewi hapa, hata sisi Wabunge tunaibiwa na mashirika hapa. Yanakuja mashirika hapa yanafundisha mambo ya good governance, utawala bora, wanakuja kufundisha Bunge zima wanakuja na fedha wanaita Wabunge 20 wanawafundisha wanakula hela wanaondoka, hata Wabunge sisi tunaibiwa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumetengeneza sheria ambayo itatufanya sisi hapa tuishi na mashirika ambayo yanafuata sheria, yanakuja na matumizi bora na miradi inayoeleweka. Siyo mtu anakuja na shirika lake, na mradi wake anaoujua yeye, mashirika mengine yamekuja hapa badala ya kufanya shughuli zilizowaleta hapa wanafanya mambo ya kisiasa.

T A A R I F A MHE. JOHN W. HECHE: Taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Kwa hiyo, tuache Rais Dkt. John Pombe Magufuli atunyooshe nchi ilikuwa imeoza.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere, kuna taarifa, Mheshimiwa Heche.

MBUNGE FULANI: Na mimi ninayo.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Getere na kwa sababu kuna watu wamechangia hapo kwenye taarifa yake…

NAIBU SPIKA: Mpe anayechangia, usianze watu wamechangia kwenye taarifa yake.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo. Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Getere kwamba siku hiyo ya Kikao ambacho kimezungumzwa hapa cha Kamati Kuu ya kwetu tunamuondoa Mheshimiwa Zitto, kuna mtu aliyehusika kuandika mkakati wa mabadiliko ambaye alikuwa anaitwa M1 na yeye siku ile alikuwa anatetemeka mpaka kidogo ajikojolee kwa sababu alijua Mheshimiwa Zitto atamtaja. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mimi nashindwa kuelewa, tena Mheshimiwa Heche unapenda sana kutumia maneno double standard, sijui kama huwa unasoma Kanuni. Sasa hivi jirani yako hapo hicho ulichosema anachekelea wakati sasa hivi kuna mtu kaitwa neno ambalo yeye mwenyewe alikuwa amekasirika. Sasa wewe utasemaje mtu amekasirika anatetemeka anataka kujikojolea, wewe unaona unaweza kuzungumza hizo habari Bungeni? Mheshimiwa Heche, tumieni maneno yenye heshima na staha, hata wewe ungeambiwa hapa unataka kujikojolea usingefurahi.

HOJA YA KUTENGUA KANUNI

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa mujibu wa Kanuni ya 28, nakusudia kuongeza muda ili Bunge likamilishe shughuli zake. Sasa nitawahoji.

(Hoja ilitolewa iamuliwe) (Hoja Iliamuliwa na Kuafikiwa)

NAIBU SPIKA: Hoja ya kuongeza muda imekubaliwa, tunaendelea na uchangiaji, Mheshimiwa Getere, endelea.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fulani mimi niliombe Bunge lako hapa, ile sheria iliyokuwa inaruhusu kuangalia vyeti feki na vyeti safi walete humu Bungeni ili tujue wa Darasa la Saba ni yupi na aliyesoma ni yupi.

MHE. SAED A. KUBENEA: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Naambiwa hapa ameshapewa taarifa tatu Mheshimiwa Getere. Mheshimiwa Getere.

MHE.BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yasiogope kufanya kazi sahihi ndani ya Tanzania, waje wafanyekazi sahihi ndani ya Tanzania, wasiogope maneno na kama ni wezi, hatuwataki kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naunga mkono.
Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wa Mwaka 2022
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie Bima ya Afya kwa Wote. Cha kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais kwa utulivu wa nchi yetu kafanya kazi nzuri heshima tunayo baraka na neema ya nchi tunayo kila kitu kinawezekana hata jana nimeona nchi nyingi zinafika kwenye nchi yetu zinapongeza demokrasia ya nchi yetu. Kwa hiyo, haya yote anafanya vizuri Mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme neno moja tu kabla sijaendelea. Huu Mfuko kwa akili yangu na matamanio yangu napenda uwe Mfuko wa heshima kwenye nchi yetu na Mfuko wenye heshima kwa Mama. Usiwe mfuko wa majanga kwa Mama narudia usiwe Mfuko wa majanga kwa Mama, uwe Mfuko wenye heshima kwa Mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme neno kidogo tu maneno machache tu ambayo Wabunge wengi wamechangia. Leo nchi yetu ina miundombinu mingi sana ina Vituo vya Afya siyo vingi lakini asilimia 90 au 85 ina Zahanati hata siyo nyingi lakini zipo. Ina Hospitali za Wilaya lakini leo ukienda Bunda Hospitali ya Wilaya ya Bunda ina majengo mazuri sana, ina Madaktari wawili tu hakuna tiba, kuna Kituo cha Afya Mgeta kimejengwa 2017 kina ultrasound na majengo mengine ya mortuary, mortuary tu jokofu halijawahi kuwekwa mpaka leo. Nimetembea TAMISEMI, nimetembelea Wizara ya Afya hakuna majokofu kituo kipo kina daktari mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najiuliza, Mheshimiwa Ummy nakupenda, najua unachapa kazi, huu Muswada ukija nao utajiandaa, utawaamrishaje Mganga Mkuu wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya, utaamrishaje Daktari Mfawidhi wa Zahati wakati yuko Tamisemi? Wewe uko Wizara ya Afya? Leo nchi yetu katika tiba imegawinyika kwenye maeneo mawili, eneo zuri zaidi ni eneo la Hospitali za Rufaa, eneo la Hospitali za Kanda na Hospitali za Mikoa ziko vizuri sana kwa sababu ziko Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Hospitali za Wilaya Vituo vya Afya, Zahanati Mganga mmoja, uwajibikaji mdogo, madawa kidogo. Sasa niombe kwenye hili kama kweli tunataka kwenda kwenye Mfuko wa Afya kwa wote tujiandae. Nimuombe Mheshimiwa Rais, Wizara ya TAMISEMI ibaki na majengo, Watumishi wote wa Wizara ya Afya kutoka Zahanati mpaka juu waende kwenye Wizara ya Afya tuondoe hii D by D katika suala la uzima ambao siyo lazima sana. Watumishi wote wa chini wa Zahanati wa Vituo vya Afya wa Wilaya waende Wizara ya Afya, TAMISEMI ibaki na majengo. Tutafaulu kwa eneo kubwa kujenga hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wakati fulani hili jambo siyo hela ni uwajibikaji, uwajibikaji ni mdogo sana kwenye jambo hili chini Zahanati na Vituo vya Afya. Kwa hiyo, hilo niseme kwamba, hilo tulichukue tulifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa na mambo ya kushauri la kwanza tunaenda kuchambua maskini ambayo ni asilimia 20 milioni kumi na tano ama nyingine milioni nane, tunaenda kuwatambua ni utaratibu gani utatumika kuwatambua hawa masikini? Lazima tutengeneze utaratibu mzuri wa kuwachambua hawa masikini ili kuwalipia na kiwango cha kuwalipia kiwe affordable kiwe kiasi ambacho masikini wa Tanzania anaweza kulipa lazima hilo nalo tuwaelimishe Watanzania wajue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumesema tukiingia Mfuko wa Afya Watanzania watapata huduma bora ya afya na anauwezo wa kupata huduma maeneo yote. Ni kweli kwa Bima ya Afya ya sasa hivi iliyopo inawezekana asipate huduma kwenye Wilaya ya Ukerewe na Wilaya nyingine. Lakini hilo ni jambo moja kwamba atapata huduma je, Bima ya Afya kwa Wote inatoa huduma kwa vigezo vyote? Au huduma ya afya mtakuja mtuambie ukiwa na bima hii utapata huduma hii. Ili wazo la kuleta generally kwamba Bima ya Afya ikitokea yote mtu atapata huduma bila vikwazo vya fedha nayo tuiondoe. Lazima tuonyeshe Watanzania kwamba huduma ipi anapata kwa Bima ya Afya aliyonayo? na siyo kwamba, kila mahali atapata Bima ya Afya yeyote. Kwa hiyo, nalo tulitazame vizuri Mheshimiwa Ummy ulieleze vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilikuwa nalisema ni Watanzania kwa ujumla. Hata sisi Wabunge tumekuwa mafundi wa kukodi ndege kwenda vilioni, tumekuwa mafundi wakukodi magari kwenda vilioni lakini hatukuwa mafundi wa kulipia watu Bima ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wamekuwa mafundi wa kuzika watu siyo kuwahudumia, sasa tujiondoe kwenye hilo tuwe mafundi wa kulipa Bima ya Afya tuokoe watu kabla ya kwenda vilioni lazima tuwe na hali hiyo. Mtu akisikia fulani amefariki anakodi ndege, anakodi magari, maturubai, vitu gani anaonekana fundi kuzika mtu lakini siyo fundi kumuhudumia na hilo nalo tuliangalie sana tuone namna gani tunaenda kuokoa hiyo hali ambayo siyo nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Ummy nimesikia unazungumza Mkoa wa Mara ambao ni Mkoa wenye watu wengi sana milioni mbili na ushee una CT scan ambazo zimekaa pale mieze sita hazijafungwa na hilo nalo ndiyo tumetoka kuzungmza vifaa tunanunua lakini kufunga hatufungi. Sasa itakuaje? Niombe Mkoa wa Mara tuone muazibike nataka kutokupata tamko kutoka leo kwamba hiyo CT scan itafungwa lini? au ndiyo watu waendelee kufa na Mfuko wa Afya unakuja na watu wanaenda kufa na vifaa tunavyo. Kwa hiyo, nalo tulizungumze na wewe kwa sababu umelisema wewe hapa ndiyo maana kwamba linafanyikaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho nikuombe Majokofu ya Zahanati ya Kituo cha Afya Mgeta lakini upeleke kwa Waganga wa Hospitali ya Wilaya Halmashauri ya Bunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)