Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Sagini Jumanne Abdallah (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nianze kwakumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa na kwangu mimi ni mara ya kwanza kuzungumza katika Bunge lako Tukufu. Niwashukuru pia wana CCM na hasa Wajumbe wa Butiama kwa kuniwezesha kupita kwenye kura za maoni na baadaye vikao vya chama vikaleta jina na baadaye nikapita bila kupingwa. Watu wa Butiama nawaahidi mtumishi bora uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru familia yangu kwa kunipa moyo wakati wote wa harakati na wanaponipa moyo ninapohudumia wananchi wa Butiama kupitia Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hotuba za Mheshimiwa Rais zote mbili, napenda nianze kusema naunga mkono hoja hiyo, lakini nianze kwa kusema moja kwa moja zinapaswa kuwa rejea kwetu sote hususani wasaidizi wa karibu sana wa Mheshimiwa Rais kwa maana ya Mawaziri wetu na watendaji wote wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hotuba hizi hakuna jambo aliloliacha kwenye sekta ya kilimo, kwa mfano imezungumzwa kwa kirefu kuanzia ukurasa wa 13 mpaka wa 15 lakini imekwenda kutaja mifugo mpaka ukurasa wa 17 ambapo Mheshimiwa Rais amesisitiza umuhimu wa kuongeza tija katika mazao ya ukulima, ufugaji na uvuvi. Sasa ushauri wangu kwenye hili baada ya Rais kulizungumza kitaifa,ni jambo jema sasa wasaidizi wake warudi kwenye ngazi za utekelezaji ili kweli kilimo hiki kiweze kuleta tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Wabunge wamezungumza hapa kiwango cha chini cha uzalishaji kwa heka, nimehudumu pale Simiyu, wastani kwa hekari moja ya pamba wananchi wa kawaida wanapata kilo mia sabini, lakini pale pale Simiyu Wilaya ya Maswa wapo wakulima bora wanaweza kupata kilo 1,200 kwa hekari moja. Sasa kumbe upo uwekezano wa kuongeza productivitykwa heka badala ya kufikiria kuongeza ukubwa wa mashamba ni muhimu wataalamu wetu wajikite kuwaelekeza wananchi hasa wakulima namna ya kuongeza uzalishaji kwa hekari moja, mbili kuliko kuongeza ukubwa wa mashamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye mifugo, nilikuwa naongea na wananchi wajimbo langu nilifanya ziara baada ya vikao vilivyopita, unakuta ukubwa wa ng’ombe kwa maana ya uzito ng’ombe anaweza akawa na kilo 90, tukawa tunatania baadhi ya wananchi wanakilo 150, 120 kwa uzito, ina maana mtu anamzidi ng’ombe uzito, jambo ambalo halikubaliki. Sasa Wizara ya Mifugo na Wizara ya Kilimo tunaona wameanza vizuri na kasi nzuri, nampongeza Waziri na Wasaidizi wake, lakini zaidi na Katibu Mkuu kwa kazi ambayo wameanza kwa kasi kwenye sekta ya kilimo, ambapo wameshakutana na wataamu lakini wamesogeza huduma za ugani karibu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Simiyu kwenye viwanja vya 88 Nyakabindi utaalam wote wa sekta ya mazaoupo pale, kwa hiyo wananchi wetu wa mikoa ya jirani wamekuwa wakienda pale kupata elimu ya namna ya kuongeza tija kwenye mazao yao. Vile vile nimeona kwenye sekta ya mifugo Waziri na wataalam wanajitahidi kuhamilisha mifugo (artificial insemination)ili tuweze kupata koo bora na hivyo tuweze kupata uzalishaji wa mifugo iliyokuwa bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amezungumzia miundombinu na mimi kwenye hili namuunga mkono sana na naomba Watanzania wengine tuendelee kumuunga mkono kwenye hili. Nakumbuka kabla ya Rais wetu hajaingia kwenye sekta ya ujenzi watu wa Kanda ya Ziwa wakitaka kwenda Dar es Salaam ilikuwa inalazimika wapite Bukoba, waende Kampala, waende Nairobi ndiyo wafike Dar es Salaam, unaenda kwenye nchi yako unapita kwenye nchi nyingine mbili, lakini leo mtu anatoka Bukoba anaingia sehemu yoyote ya Tanzania kwa lami, hivi ni vitu vya kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Jiji la Dar es Salaam tafiti za World Bank, nakumbuka niliwahi kutoa taarifa iliyokuwa inaonesha kwambakwa ile foleni tuliyokuwa nayo, tulikuwa tunapata hasara, tunapoteza karibu shilingi bilioni 40 kwa siku kwa ile foleni tu, leo Rais amesaidia kufungua hizo barabara, kuweka hizo flyover, kupanua ukubwa wa barabara,efficient ya usafiri umeanza kuiona, frustration ambazo wananchi walikuwa nazo, wawe wanafunzi kuchelewa shule, wawe wagonjwa wanaopelekwa hospitali, wawe wasafiri wanaoenda airport walikuwa wanakumbwa na msongo wa mawazo kwenye foleni za barabarani, lakini leo tunaona Dar es Salaam inavyopitika, tunataka mikoa yote iwe hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Rais wetu aendelee, nina imani hata nchi jirani wanatuonea gere kwa namna tulivyopambana kuboresha miundombinu yetu. Ushauri wangu kwenye sekta hii ya usafiri na usafirishaji ni kushuka kule chini, Waheshimiwa Wabunge wamesema karibu wote kwamba kiwango cha fedha wanazopewa TARURA hakitoshelezi sekta ya TARURA kuboresha barabara za halmashauri na za vijijini. Nafahamu sababu, wakati wanaweka hivi viwango vya asilimia 30 kwa 70 kiwango cha barabara za halmashauri kilikuwa ni kilometa 58, leo tunazungumza zaidi ya kilometa 120,000 za barabara za vijijini, sasa kuendelea kuwapa kiwango cha asilimia 30 kwa kweli ni kuwatweza wataalam wetu wa TARURA na kufanya walaumiwe pasipo na sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunazungumzia hizi barabara kuu, naomba pia barabara za wilaya zetu zizingatiwe. Nafahamu tunayo barabara kutoka Ziroziro kwenda Bukabwa, Bwiregi, Nyamimange, Silolisimba hadi Serengeti, ushauri wetu hizo barabara zisaidiwe. Naona sekta ya ujenzi wanajenga kilomita mbili mbili kila mwaka,kwa kasi hii itachukuwa miaka makumi kabla hatujafika mwisho. Piai ipo barabara ya kutoka Mazami kupitia Butiama kwenda Nata, hii nayo ikamilike, maana ni ya muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya nishati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA:Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. JUMANNE A. SAGINI:Mheshimiwa Naibu Spika, basi nashukuruna naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda wa dakika tano, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye kuchangia. Mpango ulioandaliwa na Serikali kwa ujumla wake ni mzuri hasa huu wa miaka mitano. Kwanza niwapongeze Wizara ya Fedha kwa namna walivyochambua zile changamoto, maana yake wameainisha ni vitu gani vilisababisha Mipango miwili iliyopita na hususan Mpango wa Pili kushindwa kutekelezeka kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ninayoiona tu ni ile mikakati inayowekwa ya kushughulikia hizo changamoto ili mpango wa III uweze kutekelezwa kwa ufanisi. Ushauri kwenye eneo hilo waichambue vizuri ile mikakati ya utekelezaji katika ku-deal na zile changamoto kwa kuwa kuainisha nani anafanya nini, wakati gani, kinahitaji rasilimali kiasi gani ili changamoto kama hizo zisije zikajitokeza kwenye utekelezaji wa Mpango wa Tatu, kinyume chake tunaweza tukaingiza statement tutafanya hivi ukajikuta hizo statement hazijachambuliwa vizuri, changamoto hizo zikaendelea kuathiri utekelezaji wa Mpango unaofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza ni juu ya ile mikakati ya utekelezaji wa Mpango. Changamoto kubwa ninayoiona hapa ni kuainisha Mipango ya Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi na Serikali za Mitaa, Mikoa na kadhalika. Serikali ni pana kweli, ukizungumza kwa ujumla tu kuainisha mipango ya MDAs na Mpango Mkuu wa Serikali, kumbukumbu zangu wakati niko Serikalini kuna tendency ya ku-cut na paste, mtu atakwambia Mpango huu umezingatia MKUKUTA, Vision 2020 – 2025, sijui SP ya Wizara, lakini ukienda kuangalia mambo yaliyozungumzwa huoni moja kwa moja kama yana-linkage zozote na hiyo mikakati mikubwa ya kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ushauri wangu kwamba Wizara ya yenye dhamana na fedha ifanye kama ilivyowahi kufanya huko nyuma, kutaka hizi MDAs zichambue unaposema umezingatia MKUKUTA, Vision 2020 – 2025, Mpango wa Miaka Mitano, awamu ya tatu, aoneshe kindakindaki nini kiko wapi na eneo gani. Kwa kufanya hivyo Mpango unaweza ukajikuta unatekelezwa, lakini vinginevyo inaweza kuwa ni wishful statements ambazo utekelezaji wake unaweza kuwa na changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa takwimu; imetajwa kama ilikuwa changamoto. Ningetamani waainishe sababu zilizosababisha kuwe na changamoto ya upatikanaji wa hizi takwimu na sasa tumejipangaje hizi takwimu ziweze kupatikana hasa kutoka kwenye private sector. Kama pamekuwa na changamoto na hatujaijua itakuwa ngumu awamu ijayo pia kuzipata hizo takwimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye muundo wa utekelezaji ambapo Wizara, Tawala za Mikoa na Halmashauri na private sector zinaingizwa, tuonyeshe details kama nilivyosema mwanzo kwani wakati mwingine unaweza kukuta hakuna link kati ya vinavyotokea kwenye Serikali za Mitaa na hivi vinavyokuja kuzungumzwa ngazi ya Serikali Kuu. Ili mpango uwe jumuishi ni vizuri hizo linkage zionekane bayana, badala ya kuwa na jedwali tunaloonesha local government lakini huioni vizuri kama ina match na yale matakwa ya kisekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sekta ya Kilimo, nataka nishauri jambo; kwenye vijiji, kwenye kata ndiko shughuli za kilimo zinakofanyika, lakini Maafisa Ugani, wataalam wa kilimo kule ni wachache sana. Kuna kata moja Mheshimiwa mmoja alizungumza hapa ina barabara ya umbali zaidi ya kilomita 250, kata moja ina vijiji 16, hivi kweli kama una Afisa Ugani mmoja anawezaje kuwa effective kutekeleza shughuli za ugani kwenye kata kubwa kama hii? Ni ushauri wetu kweli kama tunataka kilimo kilete tija tuwe na vijana wanaojua eneo lao la kilimo, lakini tuwapeleke kule kilimo kinakotekelezwa hasa vijijini vinginevyo tutakuwa bado tuna changamoto tukidhani tutaongeza tija kwenye kilimo, lakini kisifanye hivyo kwa sababu ya uhaba wa wataalam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ugharamiaji wa Mpango, nadhani wadau wanaotajwa na Serikali ni wengi sana, lakini utaona kuna future tutafanya hivi, litatokea hivi, nilidhani kwa vile Mpango unaanza 2021/2022 mpaka 2025/ 2026 hizi engagement zote zimeshafika, vinginevyo itafika Julai tutatumia muda mrefu sana ku-engage hawa wadau wote, halafu utekelezaji sijui utakuja kuanza lini. Kwa vile kuna dalili za kuchelewa, ni ushauri kwamba sasa Serikali ifanye haraka ku-engage na hizi Taasisi za Serikali, Taasisi Zisizo za Kiserikali, Wadau wa Maendeleo na kadhalika na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye kuianisha mifumo ya Serikali na ya sekta binafsi; unajua kwenye Serikali kuna urasimu, kuna junior officer anaandaa dokezo senior officer analipokea, Mkurugenzi Msaidizi anaweka comments, Mkurugenzi halafu liende kwa Katibu Mkuu, wakati mwingine inaweza ikachukua hata mwezi kufikia uamuzi, lakini kwenye sekta binafsi vitu vinaenda haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni maoni yangu kwamba pengine katika usimamizi wa Mpango huu kuwe na mfumo wa tofauti, tukifuata huu mfumo wa Serikali wa madokezo kupita kwa watu saba kabla ya uamuzi, tunaweza tukajikuta tumechelewa kutekeleza Mpango wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, kengele imeshagonga.

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)