Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Supplementary Questions
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya Jimbo la Kavuu yanafanana kabisa na matatizo ya Jimbo la Magu na hivi karibuni kupitia mpango wa REA wameweza kuweka umeme katika Kata yangu ya Usevya katika Jimbo la Kavuu. Hivi karibuni umeme umeanza kuwaka takribani wiki tatu baada ya REA kukamilisha ujenzi wake pale lakini mpaka sasa hivi wananchi hao hawana umeme ikiwemo pamoja na mimi. Je, kwa kuwa wananchi wale walikuwa na hamu na umeme huo ambao haupatikani, Serikali inasema nini kuhakikisha kuanzia sasa umeme unapatikana?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nasikitika kwamba, pesa hizi ni za bajeti ambayo tunakwenda kumalizia, naomba nijue ni lini pesa hizi zitatoka ziende zikafanye kazi hiyo kwa wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili, kwa uzoefu unavyojionesha pesa hizi zinaweza zikatoka mwisho wa bajeti yaani Juni 30. Je, pesa hizi zinapotoka zinakwenda wapi?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza napenda kuishukuru Serikali kwa kutambua uwezo wa wajasiriamali wa Mkoa wa Katavi ambao bado wana viwanda vidogovidogo, lakini kwa kuwa, Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inalenga uchumi wa kati, je, Serikali inasema nini kuwekeza sasa katika viwanda vikubwa kutokana na malighafi zinazopatikana Mkoa wa Katavi ili tuweze kufikia malengo ya uchumi wa kati?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili; kwa kuwa, Mkoa wa Katavi una wanyama wengi wafugwao hususan ng‟ombe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwekeza kiwanda cha kusindika mazao ya ng‟ombe, hasa katika Jimbo la Kavuu?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la msingi napenda kwanza kumshukuru ameweza kueleza kwamba kuna fedha ilitengwa kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 ambayo bajeti yake inakwisha mwezi wa Sita tarehe 30; na hizi fedha amesema Serikali imepanga kufanya matengenezo ya kilometa 42 kwa kiwango cha changarawe ambapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo ni shilingi milioni 246. Swali langu, je, fedha hizo zitatoka kabla ya Juni 30 mwaka huu? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na kufahamu changamoto za barabara zilizoko katika Majimbo yetu hasa katika mikoa yetu hiyo ya pembezoni, tatizo siyo barabara anayoniambia ambayo imetengewa fedha ya kutoka Kibaoni kupitia Majimoto mpaka Kasansa na kwenda Inyonga.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la barabara nilizokuwa nikisema ni ambazo ziko chini ya Halmashauri na concern yangu na ya wananchi ni kwamba Halmashauri hizi mpya zikiwemo na mikoa mingine mipya ya Simiyu, Geita pamoja na Katavi kwamba hazina bado uwezo wa kuwa na hizo barabara. Swali langu la msingi hapa ni kwamba Serikali iangalie sasa namna ya kutafuta fungu la dharura kwenye barabara zilizoko ndani ya Halmashauri. Kwa mfano, kwangu, barabara ya kutoka Mamba…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kikwembe, naomba ufupishe tafadhali.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Kwa mfano, kule kwangu, barabara ya kutoka Mamba kwenda Kabunde, barabara ya kwenda mpaka Maimba, barabara ya kutoka Lunguya mpaka Majimoto; barabara hizi hazipo kabisa. Naomba Serikali iangalie namna ya kupata fungu la ziada kuweza kutoa hiyo kwa ajili ya kutengeneza. Naomba kupata majibu ya maswali hayo, lini fedha hizo zitapatikana na ningependa zitakapopatikana tupewe taarifa.
MHE.DKT. PUNDECIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali yetu ina lengo jema la kuunganisha barabara za mikoa ili kuharakisha maendeleo katika nchi yetu yote; na kwa kuwa ujenzi wa barabara nyingi umekuwa ukikumba nyumba nyingi zinazokuwa pembezoni mwa barabara ambazo zinawekewa „X’ kwa mfano, kutokea Ilalangulu kwangu kule mpaka Kasansa na fidia mara nyingi wanatathmini pale ambapo pesa zinakuwa hazijapatikana lakini pindi zinapopatikana wanakuja kuwalipa wananchi fidia ile ya mwanzo:-
Je, Serikali inasema nini kufikiria namna ya kutathimini upya fidia za wananchi mara ujenzi unapoanza?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa, suala hili ni nyeti na linagubikwa na mambo mbalimbali ndani ya jamii ikiwemo imani mbalimbali za kidini, mila na desturi. Je, ni lini sasa White Paper hiyo itapitishwa katika makundi mbalimbali ya jamii, ili iweze kupata maoni yake mbalimbali na kuweza kutungwa Sheria inayoweza kumlinda mtoto?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili; chini ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kuwa, mpaka sasa hivi elimu yetu ya mpaka sekondari ni bure. Je, Serikali sasa haioni kuna umuhimu wa kuongeza elimu ya kidato cha bure ikawa mpaka form six ambayo ni elimu ya lazima, ili tuweze kuvuka ule umri wa miaka 18 ukizingatia sasa hivi watoto wameanza kusoma wakiwa chini ya miaka minne mpaka mitano? Je, Serikali inasema nini kuhusiana na hilo?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa napenda niishukuru Serikali kwa kukiri udhaifu mbalimbali ambao unaweza kuwa unasababishwa na ajali zinazoweza kuwa zinatokea ambazo zimeelekezwa kwenye swali la msingi ikiwemo ni pamoja na uzoefu na uchakavu wa miundombinu. Swali langu la nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba wote tunafahamu Tanzania na China ni nchi marafiki na bidhaa nyingi za biashara karibu asilimia 95 zikiwemo pikipiki za bodaboda zimekuwa zikitoka China.
Swali langu, je, ni kwa nini Serikali sasa isione namna ambayo inaweza ikafanya mazungumzo na Serikali ya China kwa kuangalia bidhaa ambazo zinaingizwa zikiwemo za bodaboda na vitu vinginevyo ili Serikali ya China ama kupitia makampuni yanayoagiza hizi pikipiki kuweza kuchangia katika zahanati zetu kama vile ambavyo wawekezaji wengine wanavyofanya katika kutoa huduma za jamii? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, pamoja na kuanzishwa na kuletwa hiyo Sheria ya Bima, je, Serikali haioni pamoja na hayo yote, kuiomba na kufanya mazungumzo na Serikali ya China pia katika kusaidia kuongeza vifaa tiba? Kwa sababu bima peke yake haimsaidii mwananchi aliyekatika miguu miwili ama mmoja kuweza kutibiwa na bima, bado atahitaji kununua mguu wa bandia na vitu vinginevyo na hospitali za Serikali yetu bado hazina uwezo katika wa kuwa na vifaa kama hivyo. Je, hawewezi wakafanya mazungumzo ili kuweza kupatiwa huduma hasa za afya ambazo zinaweza zikaenda moja kwa moja vijijini kwa wananchi wetu? Ahsante.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sitakuwa mbali sana na wanaohitaji miji ipandishwe hadhi. Kwa kuwa kata ya Majimoto sasa imekuwa kubwa kiasi ambacho inatakiwa kupandishwa hadhi na tumekwishaleta maombi katika Wizara inayohusika. Je, ni lini sasa maombi hayo yatashughulikiwa ili kata ya Majimoto iwe Mji Mdogo?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira yaliyopo Nsimbo yanafanana kabisa na mazingira yaliyopo katika katika Jimbo la Kavuu na kupitia initiative ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye ziara katika Jimbo la Kavuu alituomba tuanzishe Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe kufuatia kuwepo na kadi za CHF kwa sababu za NHIF hazitumiki kule.
Je, Serikali sasa haioni kuna umuhimu, kutokana na juhudi za wananchi wa Jimbo la Kavuu kuwapatia gari la wagonjwa ambao wamekuwa wakitumia umbali mrefu kutoka Mpimbwe kwenda Mpanda na sasa tutumie katika Jimbo la Kavuu?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa, napenda nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, suala hili ni la kikatiba kwa maana ya kwamba linahusisha Serikali ya wananchi kwa maana ya Serikali za Vijiji. Kwa kuwa wananchi wamekuwa wakichangia takribani 20% ya maendeleo katika maeneo yao ya vijiji. Je, Serikali sasa inafikiria nini kupeleka pesa za maendeleo kwa wakati ili wananchi hawa waweze kujua sasa ile miradi ni mali yao? (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, katika majibu yake ya msingi amesema kwamba watalipwa pale maeneo watakapoyahitaji, lakini tukiangalia kuna maendeleo yanayoenda kufanywa sasa hivi, kwa mfano katika barabara yangu ya Kibaoni, Usevya, Mbede, Majimoto, Mamba, Kasansa mpaka Mfinga ambako tutatekeleza REA III. Ni lini wananchi hawa wenye alama za ‘X’ za kijani mtawalipa pesa zao ili waweze kufaya marekebisho ya nyumba zao waweze kuweka umeme wa REA?
MHE. DKT. PUDENSIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kumweleza kwamba, pamoja na kwamba Serikali ina nia njema ya kuweka sekondari za wasichana kila tarafa na kwa sasa katika Jimbo langu ama Mkoa wa Katavi kila tarafa bado haijawa bado na Sekondari za form five na six.
Je, haoni sasa kuna umuhimu na ulazima wa hii Shule ya Sekondari ya Mpanda kuanza sasa kwa kidato cha kwanza mpaka cha sita ili tuweze kuzuia mimba za utotoni kama sera na Serikali inavyosema?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza. Wakati tunapitisha bajeti tuliongelea suala la kodi ya majengo kwamba nyumba za kawaida zitaanzia shilingi 10,000 na nyumba ambazo zinakuwa kwenye level ya maghorofa zitaanzia shilingi 50,000. Lakini cha kushangaza mpaka sasa hivi tunaona kodi hizi hazina uwiano, unakuta kati ya nyumba na nyumba mwingine anapelekewa kodi ya shilingi 10,000 mwingine shilingi 30,000, mwingine shilingi 40,000.
Je, nini kauli ya Serikali kuhusu hizi kodi na uwiano ambao si sawa kati ya Halmashauri ama Manispaa ndani ya Manispaa moja unakuta kata nyingine bei ni tofauti na kata nyingine bei ni tofauti, ama Halmashauri moja ni bei tofauti na Halmashauri nyingine ni bei tofauti.
Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na kodi ambayo tuliipitisha sisi wenyewe Wabunge wakati wa bajeti? (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na swali la Mheshimiwa Kapufi kuhusiana na hizi kodi za zimamoto, ninachojiuliza na wananchi wanachojiuliza hasa wa Jimbo la Kavuu wanataka kujua, kwa nini hizi tozo zimeanza kutozwa sasa, na watu gani wameshirikishwa? Kwa sababu zinaoneka zimeibuka, hata kama zilikuwepo kwa ujibu wa Sheria, zimeibuka kiasi kwamba hata wale wenye guest houses sasa hivi zimamoto wamekuwa wakiwavamia na kuwa-charge hizi kodi. Kwa hiyo, tunaomba ufafanuzi ni gazeti namba ngapi zilizoruhusu hizi kodi zianze kutumika?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyatoa kwa sababu mengi ni ya ukweli. Ni kweli nyumba nyingi hazijafanyiwa uthamini lakini zinatozwa hizo kodi na kodi zinazotozwa ni kwamba siyo zile tulizopitisha za shilingi 10,000 wala shilingi 50,000 ni zaidi ya shilingi 300,000 kwa nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini. Kwa hiyo, nashukuru kwa jibu lake ambalo amelisema ni la ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye swali langu, kwa kuwa nyumba nyingi za watu binafsi hazina BoQ kwa sababu wanajenga kwa kujidunduliza, leo mwananchi akipata shilingi 50,000 anasema ananunua cement, kesho kutwa akipata shilingi 100,000 atanunua bati, haweki kwenye kumbukumbu kwamba mwisho wa siku ametumia shilingi ngapi; na hiyo nyumba Serikali haifanyii uthamini, lakini kesho inampelekea bili ambayo wao uthamini wao aidha ni wa macho ama ni wa nini, bila kuangalia kumbukumbu za yule mtu binafsi.
Je, Serikali inasema nini na inatoa mwongozo gani thabiti kwa kutoa majawabu ili wananchi hawa ambao ni kama mimi binafsi, ambaye siweki kumbukumbu, nimejenga nyumba na leo nakuja kufanyiwa uthamini ambao ni zaidi ya pesa ambayo nakuwa nimeweka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali la pili, tangu utaratibu huu umeanza, je, Halmashauri zimefaidika kwa kiasi gani? Kwa sababu sehemu ya Halmashauri sasa hawakusanyi mapato, mapato yanakusanywa na TRA na pia majengo mengi, maboma yako kwenye Halmashauri huko ambayo ni zahanati na mashule. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu la Kavuu kuna maboma ya shule 69 hayana mabati mpaka kesho, Halmashauri zimefaidikaje na hizi pesa zinazokusanywa? (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilitaka kufahamu kutokana na maswali yaliyokuwa yanaulizwa, Mheshimiwa Mbunge aliyeketi muda siyo mrefu ameongea kuhusu Waheshimiwa Wabunge kutelekeza watoto. Sasa nilitaka kuuliza, Waheshimiwa Wabunge hawa wanatelekeza watoto kwa Waheshimiwa Wabunge wenzao ama nje ya Wabunge? (Kicheko)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwa kuwa benki hii ukiitazama na kwa namna ambavyo anaongea kwamba inaelekea kupata hasara ni kwamba benki hii inaweza ikafa na Serikali ilikwishaahidi kuinusuru kwa kuipatia mtaji. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ya kuipatia mtaji ili benki hiyo iweze kufanya kazi?
MHE.DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameongea kuhusu maeneo ya hifadhi ambayo yamekuwa yakihifadhiwa na Serikali lakini pia vyanzo vya maji. Kwa kuwa, wananchi wangu kwa kupitia Halmashauri ya Mpimbwe, Jimbo la Kavuu, wananchi wangu wa Kata ya Itobanilo; vijiji vya Senta Unyenye, Amani na Lunguya wamekuwa wakitumia maji ya Mto Kavuu ambao unapakana na mbuga ya Katavi na askari wa Katavi wamekuwa wakiwanyanyasa wananchi wakati vijiji hivyo hawana maji na tumekuwa na ujirani mwema wa kutumia.
Je, Serikali inasema nini kuhusu hawa watu wa National Park kupiga wananchi hovyo wakiwa wanaenda kutafuta huduma za msingi?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Kavuu na Mkoa mzima wa Katavi, kutokana na jiografia yake imekaa kama umbo la pweza. Je, Serikali inafikiria nini katika Jimbo la Kavuu, Halmashauri ya Mpingwe kuanzisha Mahakama yenye hadhi ya Wilaya kutoka kwenye hadhi ya Mahakama ya Mwanzo ili kuwanusuru wananchi kwenda katika makao makuu ya Nyonga ambayo wanapita katikati ya mbuga na kuhatarisha maisha yao?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nipate kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali ina nia njema ya kupeleka nishati mbadala katika maeneo mbalimbali ya Tanzania; na kwa kuwa, Jimbo la Kavuu lina idadi kubwa ya wafugaji na kinyesi cha wanyama kinapatikana kwa wingi hasa ng’ombe, nguruwe na mbuzi. Pia, kwa kuwa, bado hatuna mtandao mzuri wa majitaka katika miji mingi ya vijijini ikiwemo Jimbo langu la Kavuu. Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka kupitia taasisi za TADETO na UN Habitat katika kuanzisha miradi ya biolatrine ambayo inatumia kinyesi cha binadamu katika maeneo ya mashule, ili tuweze kupata gesi ya uhakika kutokana na kwamba sasa uharibifu wa mazingira katika Jimbo la Kavuu umekuwa mkubwa especially katika kukata miti hovyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, naomba niulize si kwa Serikali na Watanzania kwa ujumla, je, matumizi ya mkaa na gesi yapi ni bora zaidi?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa maswali ya Shule za Sekondari za Wasichana katika eneo la Masasi linafanana kabisa na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mpanda iliyoko Mpanda Mjini na tumeshaleta maoni kwa Waziri wa Elimu pamoja na Waziri wa TAMISEMI kwamba shule ile ilikuwa inachukua kuanzia Form One mpaka Form Four na ikabadilishwa ikawa Form Five mpaka Form Six. Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango wa kuhakikisha shule ile inachukua wasichana kuanzia Kidato cha Kwanza mpaka cha Sita kwa kuwa tuna shule moja tu Mkoa wa Katavi ya boarding? (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Kwa kuwa tatizo kwenye swali la msingi la 323 la usafiri wa patrol kwa vituo vya polisi lipo karibu nchi nzima. Je, Serikali sasa inajipangaje kwenda kutatua tatizo hili la usafiri wa patrol katika vituo vya polisi hasa katika Jimbo langu la Kavuu?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Kibaoni – Majimoto - Mamba – Kasansa – Mfinga – Muze – Kilyamatundu - Mbozi imekuwa ikiandikwa sana katika vitabu vya bajeti kwa takriban miaka 10 sasa. Ni lini barabara hii ya kutoka Kibaoni - Kilyamatundu - Mbozi itafanyiwa upembuzi yakinifu na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa sababu pia iko ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka 15 mfululizo? (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kurekebisha na kuvitibu visima viporo ambavyo mpaka leo havijatengenezwa.
Je, Serikali inasema nini sasa kuhusu visima vyangu virefu ambavyo vimetengenezwa miaka sita iliyopita mpaka leo havijarekebishwa, ambavyo ni, Kisima cha Tupindo, kilichopo Kata ya Mbede na Kisima cha Kibaoni ambavyo mashine zake zimedumbukia ndani na vimetumia kutengezwa takribani pesa za Serikali milioni 800?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwa kweli leo nimefurahi kidogo. Naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri amenijibu vizuri. Naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza:
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, sera hii inalenga kutatua changamoto inayowapata wananchi kuhusu mitazamo mbalimbali lakini umesema pia sera hii inalenga kuwakopesha wanavikundi na mtu mmoja mmoja, swali langu ni kwamba; ni kwa nini sasa Halmashauri nyingi zimekuwa zikiwalazimisha wananchi wakope wakiwa kwenye vikundi vya watu watano na kuendelea, jambo ambalo kimsingi linamnyima mkopaji mmoja mmoja mwenye uwezo wa kukopa ambaye anaweza akajidhamini ili aweze kujiendeleza katika maisha yake?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, naishukuru Serikali yangu kwa sababu imeweza kuondoa riba katika hii mikopo ambayo imekuwa ikitolewa na Halmashauri asilimia kumi, lakini, ni kwa nini sasa, bado tunasema kwamba, kwa mfano kwenye Mifuko ya Akinamama na Vijana, wazee na wanaume hawapati mikopo hii, jambo ambalo tunaweza tukawakopesha na wakaweza kuendeleza mifuko hiyo?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Jimbo la Serengeti yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Jimbo la Kavuu hasa katika Kata za Chamalendi, Mwamapuli, Majimoto na vitongoji vyake; kumekuwa na matatizo ambayo wananchi hasa wafugaji wamekuwa wakisukumizwa na askari wa wanyamapori ndani ya Mbuga ya Katavi na wamekuwa wakipotea na mara nyingi wakiwa wakitafutwa na ndugu zao ni nguo tu zinapatikana:-
Je, Serikali inasema nini sasa kwa ujumla kuhusu askari wote wa wanyamapori wanaofanya kazi katika mbuga zote za National Park katika kuhakikisha usalama wa wale wanaowaita majangili wakati sio majangili? Kwa sababu tu wanakuwa wameingia kwenye mbuga, kwa hiyo, wataitwa majangili.
Je, Serikali inasema nini kuhusu Askari hao ambao wamekuwa wakiwateka wananchi na kuwapora ng’ombe zao na mali…
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Kata ya Maji Moto wameanza kuwekeza kuitikia kauli mbiu ya viwanda; na kwa kuwa hawana umeme wa uhakika; na kwa kuwa, REA Awamu ya Tatu, round ya kwanza haijulikani itaanza kutekelezwa lini katika Jimbo la Kavuu, je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuharakisha hizi tafiti zao za geothermal kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa Maji Moto umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Kibaoni, Usevya, Ilalangulu na Manga vimefikiwa na umeme unaotoka Sumbawanga, lakini kumekuwa na tatizo kubwa la kukatika kwa umeme katika maeneo hayo na kufanya wananchi katika Kata ya Kibaoni kupata hasara sana kutokana na kukatikakatika kwa umeme. Je, Serikali inawaeleza nini wananchi waliopata umeme huu ambao ni wa Kata ya Kibaoni kupata umeme wa uhakika ambao hauwatii hasara? (Makofi)
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Waziri ametamka mradi ambao uko katika Bonde la Ziwa Rukwa lakini uko katika Jimbo langu mradi wa umwagiliaji wa Kirida ambao nilikwishaleta maombi pamoja na mradi wa Mwamapuli. Je, Serikali inakuja na kauli gani sasa kuhusiana na hii miradi ambayo tayari tulikwishawekeza pesa isipokuwa iliharibika kwa ajili ya mvua ili iweze kuendelezwa na kuleta tija kwa wananchi ambao tayari miundombinu ipo?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake yenye matumaini kwa sababu barabara ya kutoka majimoto Inyonga zabuni imeshatangazwa. Swali langu ni kwamba kwa kuwa barabara hii iko chini ya TANROADS na TANROADS wamesema kwamba wanatangaza zabuni ya kumpata mpembuzi na msanifu ili waweze kuianza barabara hiyo na kwa kuwa zoezi la kutangaza zabuni na mpaka kumpata mkandarasi ni la muda mrefu. Je, ni lini sasa katika maombi yangu maalum ya kilomita 2.0 katika Mji wa Usevya yatapatiwa majibu na barabara hiyo ianze kutengenezwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mkandarasi alipatikana ambaye ameweza kujenga kilomita
1.7 katika Mji wa Inyonga, lakini katika mwaka wa fedha 2018/2019 mkandarasi wa kujenga kilomita 2.5 amepatikana na yupo katika eneo la mradi. Je, ni eneo gani la mradi ambapo mkandarasi huyo yupo?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa napenda niishukuru na niipongeze Serikali yangu kwa namna ambavyo imekuwa ikiwajali wananchi hasa wanaoishi vijijini na pia kuangalia namna gani ya kutatua matatizo ya wananchi. Pamoja na pongezi hizo za kupongeza Serikali yangu, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza; ni kwa kiwango gani Taarifa ya Wizara hizi ambazo zilikaa kama Kamati ambazo zimeweza kuja na ushauri namna gani ya kutatua matatizo ambayo hasa katika vijiji mfano katika Jimbo langu la Kavuu, vijiji vyangu ambavyo ni vijiji vya Ikopa, Itura, Luchima, Sentaunyenye, Iziwasungu, Kabunde na kwingineko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa tuna migogoro mikubwa katika kijiji cha Luchima na mpaka wa TANAPA kwa ajili ya mto wa Kavuu na nilikwishaleta maombi mwaka jana na TANAPA walikwishaanza kujenga kisima kwa ajili ya kupunguza mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Kijiji cha Luchima pamoja na mpaka wao. Je, ni lini sasa hawa ndugu zangu wa TANAPA wataweza kumalizia kile kisima ili wananchi wangu wa kijiji cha Luchima waweze kuwa huru katika kufanya shughuli zao za kilimo na uvu vi bila kuingiliwa na askari wa TANAPA.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa barabara hii ya kutoka Kibaoni mpaka Mlowo imekuwa ikitajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na pia imekuwa ikitajwa kwenye kila bajeti inayopitishwa na Bunge hili. Je, kutokana na majibu aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, barabara imekwisha fanyiwa upembuzi yakinifu? Hivyo basi wanatafuta fedha ili kuja kuiwekea lami.

Je, Serikali haioni sasa kwamba ni hasara kuifanyia barabara upembuzi yakinifu na baadaye kuja kuitafutia fedha kwa ajili ya kuweka lami jambo ambalo utasababisha tena kuja kufanya upembuzi yakinifu mwingine?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi nzuri za Serikali kutaka kuhakikisha wananchi wanapata mazao yao pindi wanapokuwa wamelima vizuri lakini napenda kujua, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inafanya utafiti wa kutosha kuhusiana na aina ya mbegu na aina ya mbolea pamoja na aina ya udongo wa sehemu husika ili wananchi waweze kulima vizuri na wasiweze kupata hasara? Katika Mkoa wangu wa Katavi, Jimbo la Kavuu mahindi yameenda vizuri na mvua hizi lakini bado kuna mdudu ambaye amekuwa akishambulia mahindi na hivyo kusababisha hasara.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mkoa wa Katavi na Mikoa mingi ya Kusini Magharibi imekuwa ikitajwa kama ni mikoa ya uzalishaji wa mazao ya chakula yakiwemo mahindi, mpunga na maharagwe.

Je, Serikali ina mkakati gani hususan katika Mkoa wa Katavi kuhakikisha kwamba inafanya utafiti na ku-introduce zao la biashara kwa wakulima wa Mkoa wa Katavi ili waweze nao kutoka kwenye masuala ya mazao ya chakula waende sasa kufanya biashara katika mkoa huo? Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba watu wao wanapata mazao ya kibiashara?
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo yaliyopo Jimbo la Mlimba yanafanana na matatizo yaliyoko katika Jimbo la Kavuu na kwa kuwa nilikwisha omba maombi maalumu kwa ajili ya matengenezo ya daraja linalounganisha Kata ya Chamalemu D na Mwamwamapuli. Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kupeleka pesa kwa ajili ya kutengeneza daraja hilo hili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma za afya katika Kata ya Kibaoni badala ya kuzunguka Kata ya Mbede?

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's