Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mary Francis Masanja (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na leo tumekutana katika Bunge lako hili Tukufu. Kipee nikushukuru sana wewe binafsi, kwa kuendelea kulitumikia Bunge hili Tukufu, lakini pia kwa leo kuwa katika uamuzi au ujumuishi maalum wa Sekta yetu hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Wabunge wote waliochangia kwenye sekta yetu hii ya maliasili na utalii na niwapongeze sana kwa kuweza kutupa mawazo chanya ya kuweza kuijenga sekta hii ya maliasili na utalii. Mawazo yao, michango yao na ushauri tumeupokea. Niwaahidi kwamba tunaenda kuufanyia kazi kwa nguvu zote, nikishirikiana na Mheshimiwa Waziri na niwaahidi kwamba sisi tuko imara na tumejiandaa kuhakikisha kwamba tunachapa kazi ili tusiwaangushe wao pamoja na wananchi waliotupa dhamana ya kuwaongoza katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza kuelezea kwenye eneo la maliasili misitu. Jukumu la Sekta ya Maliasili na Utalii kwanza kabisa tunahifadhi maliasili zilizopo nchini, lakini pia tuna malikale, lakini baada ya kuhifadhi tunaendeleza utalii. Kwenye eneo hili la maliasili misitu nitapenda sana kuzungumzia upande wa matumizi ya mkaa na kuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa asilimia 95 ya Watanzania tunatumia nishati ya mkaa na kuni na naomba nilielezee hili kwa ufasaha kabisa kwa kuzingatia Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002, Sura 323 inasema kwamba mkaa ni moja ya mazao ya misitu yanayoruhusiwa kuvunwa kisheria. Naomba hili nilifafanue kwa ufasaha kwamba hakuna Waziri wala mtu yeyote ambaye amewahi kuzuia uvunaji wa mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naongea hivi kulingana na sheria hii, lakini nitapenda kufafanua kwa nini sisi Maliasili na Utalii tunasimamia eneo hili. Tunaomba sana na sheria hii tunaisimamia pale tu ambapo uvunaji wa mkaa unafanywa kiholela. Tunasimamia kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunahifadhi maliasili misitu ili iwe endelevu kwa vizazi na vizazi vijavyo. Kwa hiyo, kwa kuzingatia kwamba zao hili linachangia asilimia 3.5 ya GDP lakini pia kwa asilimia 43 ya GDP inachangia pato ghafi la sekta ya misitu ikiwemo mbao na mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili tunawahamasisha wavunaji wa mkaa na watengenezaji wa mkaa kwamba pale tu ambapo wanahitaji kwenda kuvuna mkaa, basi watapata vibali maalum ili kuonyesha maeneo stahiki ambayo yanapaswa kuvunwa, lakini pia kuendelea kusimamia maliasili misitu kwa ajili ya maendeleo ya baadaye.

Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba wiki moja iliyopita ambayo tulikuwa kwenye Wiki ya Mazingira Duniani ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia alitoa tamko juu ya tujiandae sasa kuanza kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati ya mkaa na kuni twende kwenye nishati mbadala ya gesi. Aliagiza taasisi mbalimbali vikiwemo vyuo, mashule, mahospitali na magereza kwamba tuendelee sasa kuhamasisha wananchi waanze kuhama kutoka kwenye matumizi ya mkaa na kuni, tuelekee sasa kwenye kutumia gesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kupunguza ukataji wa miti holela, lakini pia pale panapo umuhimu sana wa uvunaji wa mkaa, basi utoke kwa vibali, si kama ambavyo sasa hivi wananchi wamekuwa wakijichukulia kwa namna ambayo si stahiki sana na inasababisha sasa uvunaji unakuwa ni holela, miti inakatwa ovyo na mwisho wa siku itasababisha jangwa litokee hapa nchini na tutaonekana sasa sisi kwenye usimamizi wa maliasili misitu kwamba tumelegea kidogo. Kwa hiyo niwaombe sana na katika hili tuendelee kuwaelimisha wananchi, yeyote yule ambaye anahitaji kwenda kuvuna mkaa, basi apate kibali aelekezwa na eneo ambalo anapaswa kwenda kuvuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitapenda kuongelea kwenye eneo la utalii, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwenye eneo hili, wametupanua mawazo mengi na wametupa michango mingi sana ya kwenda kuboresha kwenye sekta ya utalii. Tumeyapokea mawazo yao, lakini nitapenda tu kuwakumbusha kwamba, sisi kama Watanzania, nitaomba sana uzalendo uanze na kwetu sisi. Nikisema hivyo, naamini kabisa utalii ukianza na sisi wenyewe, tutachangia pato kubwa sana hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, uzalendo uanze na sisi Wabunge tuliomo humu ndani na kwa ridhaa yako, nitaomba baada ya kumaliza Bunge lako hili Tukufu, tumeandaa safari, Wabunge tuwe mfano, Wabunge wazalendo naamini wote humu tuko ni Wabunge wazalendo tutembelee maeneo yetu ya vivutio na sisi tuwe mabalozi namba moja wa kutangaza utalii ndani na nje ya nchi. Naamini kabisa sisi wenyewe tukiwa wazalendo, utalii utakua kwa kasi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeandaa mikakati mingi ya ku-promote utalii na vivutio vilivyomo hapa nchini na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba baada ya Bunge hili nadhani wataanza kuona tu amshaamsha zitakazokuwa zinaendelea. Pia tulikuwa tumeshaandaa mipango mikakati ya kukutana na watu mbalimbali wakiwemo Waandishi wa Habari. Hata hivyo, tuna mkakati wa kusambaza vipeperushi mbalimbali hasa kwa wale ambao wanapokea wageni wetu wanapoingia hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza nikatolea mfano, kwa mfano, tunaweza tukaandaa hata vipeperushi kwa hawa vijana wetu au wananchi ambao wanapokea wageni wetu kutoka nje ya nchi, wakawa na vipeperushi maalum lakini pia wao wenyewe kwa uzalendo kama Watanzania, pale ambapo unambeba abiria yeyote yule aliyetoka nje ya nchi mueleze kwamba tuna Mlima Kilimanjaro, tuna hifadhi, tuna malikale, tuna kila aina ya vivutio hapa nchini. Kwa hiyo ile elimu wakati unampeleka kule anakoenda kupumzika, anakuwa tayari ameshaanza kujua kwamba Tanzania ina vivutio vya namna gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tutasambaza vipeperushi ambavyo vitasaidia pale ambapo abiria wa kutoka nje ya nchi anaingia ndani ya nchi, basi ataonyeshwa Ngorongoro crater iko wapi, kama ni Serengeti iko wapi, lakini pia ataonyeshwa vivutio mbalimbali vinavyotokana na malikale. Hii yote ni kuhakikisha kwamba mgeni yeyote anayeingia hapa nchini, basi aelezwe Tanzania ina mazao gani ya utalii ambayo yatamhamasisha yeye aende kwenye kutalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda pia kuongelea kwenye swahili tourism, hili nalo litakuwa ni eneo mojawapo la kuhamisha utalii, ambapo tutandaa vitu mbalimbali ikiwemo maonyesho ya mavazi, lakini pia tutaanda matamasha mbalimbali ya vyakula vya asili, ngoma na utalii wa utamaduni. Haya yote ni maeneo ambayo tumejipanga, sisi kama Wizara kuhakikisha kwamba sekta hii ya maliasili na utalii inakuwa kwa kasi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, pale ambapo tuna uhitaji wa kuonyesha ubalozi katika maeneo yetu, naweza nikaja kwenye wilaya mojawapo nikataka kucheza hata zile ngoma zetu ili kuhakikisha kwamba utalii wa utamaduni unakua, tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunauendeleza utalii wa Tanzania na vivutio vyake vilivyomo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda pia kuongelea eneo la miundombinu; niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba eneo hili tumezingatia bajeti hii mtakayoipitisha ninyi kuhakikisha kwamba maeneo yote yenye vivutio yanapitika kwa ufasaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeandaa bajeti ambayo itakidhi kulingana na maeneo yote ambayo yana changamoto ya miundombinu. Kwa hiyo hifadhi zote na maeneo yote ya malikale tumezingatia. Tutawaomba tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tunapopitisha bajeti hii basi muipitishe tu vizuri mkiamini kwamba tunakwenda kutekeleza na kuhakikisha kwamba miundombinu itapitika na watalii waweze kuingia hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuliongelea ni kuhusu mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wamependa kuyaongelea kuhusu ufunguzi wa mageti. Eneo hili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Nawashukuru sana. (Makofi)