Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Omari Mohamed Kigua

Supplementary Questions
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni takribani miaka 13 toka Wilaya hii ya Kilindi imeanzishwa. Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba, pana umbali mkubwa sana kati ya Wilaya ya Handeni iliko ofisi ya Mamlaka ya Mapato na Kata mbalimbali za Jimbo la Kilindi hususani katika Kata ya Pagwi. Je, ni lini sasa utafiti huu utakamilika ili wananchi wa Kilindi waweze kunufaika na huduma hii? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vimetajwa vigezo vingi sana hapa, lakini vigezo hivyo inaweza ikawa ni sababu ya kutoleta maendeleo katika maeneo husuka. Je, Serikali haioni umuhimu kwamba kigezo cha jiografia tu kinaweza kutosha kugawanya Jimbo? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza kama ifuatavyo. Serikali imekuwa ikitoa pesa nyingi sana kwa ajili ya miradi ya maji, lakini kumekuwa na tatizo kwamba miradi hii imekuwa inakosa ufuatiliaji; kwa maana kwamba miradi ile, hasa ya maji imekuwa katika kiwango cha chini sana. Je, Serikali iko tayari kuwa na kitengo maalum kwa ajili ya kufuatilia kuhakikisha kwamba fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji zinakidhi mahitaji, kwa maana miradi itengenezwe katika viwango vinavyotakiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na nia na dhamira nzuri ya Serikali juu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo lakini imeonekana kwamba masharti haya hayawasaidii hawa wachimbaji wadogo na tunajua kwamba sasa hivi wimbi kubwa la watu wanaokosa kazi ni vijana. Sasa, je, Serikali iko tayari kupunguza vigezo vile ili watu wengi waweze kunufaika na mpango huu?
Swali langu la pili, je, Naibu Waziri yupo tayari kuambatana nami kwenda Jimboni ili tuweze kuzungumza na wachimbaji wadogo ili wajue dhamira ya Serikali ya kuwasaidia hususan wachimbaji wadogo? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa uharibifu wa mazingira umekuwa ni tatizo sugu sana hususan katika Jimbo langu la Kilindi katika Kata za Negero, Mkindi, Kilindi Asilia pamoja na Msanja kutokana na shughuli za kibinadamu; je, Waziri yuko tayari kwa kushirikiana na Wataalamu wetu wa Chuo Kikuu cha SUA, kwa mfano, tuna Watalamu wazuri, akina Profesa Dhahabu na Mariondo kwa ajili ya kupeleka timu kule kuweza kufanya tathmini kubwa? (Makofi)
Swali la pili, suala hili la mazingira limekuwa ni sugu sana; je, Serikali iko tayari sasa kwa kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha kwamba inapeleaka wataalamu wa kutosha wa mazingira kulinda maeneo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni ukweli usiopingika kwamba swala la changamoto ya maji ni tatizo kubwa nchini.
Je Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuchukua ushauri kwamba ili kutatua tatizo hili tuweke utaratibu wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi kwa mpango wa PPP ili kuondoa suala la changamoto ya maji nchi?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuchukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu sasa umefika ili kupata thamani ya fedha katika miradi yetu ya maendeleo ya maji kuhakikisha kwamba mnaanzisha kitengo cha ufuatiliaji pale Wizarani ili msitoe tu fedha lakini fedha zile ziwe zinamaana katika miradi yetu mbalimbali katika Halmashauri zetu? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Ujenzi, napenda kuuliza swali moja la ziada kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba barabara hii ni muhimu sana kiuchumi na ukizingatia kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kilindi kwa maana ya Songe hadi Gairo ni kilometa hizo alizotaja. Barabara hii nyakati za mvua ina changamoto kubwa sana na ni juzi tu Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya alipokuwa anakuja Makao Makuu ya Wilaya, alikwama maeneo ya Chanungu pale kwa takribani saa mbili.
Swali langu linakuja, je, ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atahakikisha kwamba watu wa TANROADS Mkoa wa Tanga wanasimamia kwa dhati matengenezo maeneo yafuatayo, kwa maana katika Bonde la Chanungu, Kijiji cha Mafulila pamoja na eneo la Kikunde, karibu kabisa na Kijiji cha Gairo hapa kuhakikisha kwamba barabara hii inapitika kwa msimu mzima wa mwaka? Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mawasiliano katika Kisiwa cha Pemba ni sawa kabisa na Wilaya ya Kilindi, baadhi ya maeneo hayana mawasiliano kabisa. Nini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu wananchi wa Kata ya Saunyi, Kata ya Loane na baadhi ya maeneo ya Kata ya Kimbya ambao hawana mawasiliano kabisa katika Wilaya yangu ya Kilindi? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kilindi ina takribani miaka 20 toka imeanzishwa lakini hali ya kusikitisha ni kwamba kituo kinachotumika ni kama post wakati ikiwa ni Wilaya ya Handeni zamani. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri yuko tayari kutembelea Jimbo la Kilindi ili kujionea hali halisi ya jinsi ambavyo hata OCD anakaa guest house mpaka leo? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali moja au mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba dhamira ya Serikali ni kuwahudumia wananchi na kuwapelekea huduma iliyo imara, lakini swali la msingi ilikuwa ni kueleza changamoto ya miradi hii.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kufanya ziara kupitia miradi yote ambayo nimeitaja hapo juu? Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, natambua jitihada za Wizara ya Elimu za kuanzisha Shule za Sekondari za Kata lakini ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wengi baadhi ya maeneo wanashindwa kupeleka watoto wao maeneo ya mbali, mfano Jimbo la Kilindi ambako wazazi hawana uwezo wa kupeleka watoto wao kidato cha tano na cha sita. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kushirikiana na halmashauri yetu ambapo tumeshafanya jitihada kubwa kutembelea Shule za Sekondari za Kilindi Girls, Kikunde na Mafisa ambazo tayari zina miundombinu kwa ajili ya kupata sifa ya kuwa na kidato cha tano na sita? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nampongeza na niwapongeze TAMISEMI kwa kutupatia kiasi kilichotajwa kwa ajili ya shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Halmashauri zetu nyingi hazina uwezo wa mapato, lakini natambua dhamira ya Serikali ya kutoa elimu bure. Nina maswali mawili ya nyongeza:-

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kukarabati shule kongwe ambazo ni za muda mrefu? Kwa mfano, Shule ya Msingi Masagali ya mwaka 1940 na Shule ya Msingi Songwe 1952? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutembelea hizi ili ajionee hali halisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, changamoto ya hosteli ambayo imejitokeza katika Jimbo la Mufundi Kusini haitofautiani sana na hali iliyopo katika Jimbo la Wilaya ya Kilindi. Ni ukweli usiopingika kwamba suala la hosteli ni kitu muhimu sana kwa sababu linachangia katika ufaulu wa watoto wetu. Je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kwamba shule zote za vijijini ambazo watoto wanatembea kwa umbali mrefu zinakuwa na hosteli?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba katika Jimbo la Kilindi ipo Shule ya Kwamkalakala ambayo ni miongoni mwa shule kumi za mwisho ambazo zimefanya vibaya kutokana na kutokuwa na hosteli. Je, Serikali ipo tayari kutoa msaada maalum kuhakikisha kwamba shule ile inajengewa hoteli? Ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Ahsante Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kabisa nami naungana na Serikali kwamba kuna umuhimu wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuwaletea Watanzania huduma. Pamoja na hali hiyo, zimejitokeza changamoto nyingi sana sana katika Hospitali hii ya KKKT mojawapo ni suala la utawala.

Swali: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kuangalia utaratibu ulio mzuri ili dhana hasa ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi iweze kufikiwa?

Swali la pili, kwa kuwa Kilindi haina Hospitali ya Wilaya: Je, Serikali iko tayari sasa kuitengea fedha Wilaya ya Kilindi ili iweze kupata Hospitali ya Wilaya? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, binafsi namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yenye ufasaha wa hali ya juu sana. Ni majibu ambayo yanatoa matumaini makubwa siyo kwa Wilaya ya Kilindi tu, lakini maeneo mengine ya Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, pamoja na shukurani hizo, nina swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Mahakama hizi ni chakavu na Mahakana zinazofanya kazi ni tatu tu.

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuanzisha hata Mahakama za Mwanzo I Mean kuanzisha hata ofisi ndogo ili huduma hii ipatikane kwa muda mfupi wakati tukisubiria ujenzi wa Mahakama hizi za Mwanzo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga daraja la muda la Nderema ambalo linaunganisha Wilaya ya Kilindi na Handeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuipongeza Serikali, naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mvua hizi hazikutegemewa na zimeharibu sana barabara kuanzia Handeni – Kibirashi - Songe – Gairo. Je, Serikali iko tayari kutuma wataalamu kwenda kuangalia hali ya uharibifu ili kuweza kurejesha mawasiliano katika eneo hili? Ahsante.
MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Handeni- Kibirashi hadi Kiteto imekwisha na hatua zote za mwisho zimeshakamilika; na kwa kuwa barabara hii ni barabara ya kimkakati inaunganisha mikoa minne kwa maana ya Mkoa wa Tanga, Manyara, Singida na Dodoma. Je, Serikali sasa haioni umuhimu kuanza kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami ili kuondokana na kero hii ya mara kwa mara? Hivi ninavyosema muda huu barabara hii haipitiki kwa wiki sasa.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi namba 358 limetaja barabara hii ambayo inaunganisha Wilaya ya Gairo na Kilindi, swali langu la nyongeza ni kama ifuatavyo; mwaka 2010 Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga barabara hii kw akiwnago cha lami. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi hii? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri juu ya tatizo hili, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la migogoro ya ardhi imekuwa ni changamoto kila eneo katika nchi hii na kama swali la msingi linavyosema kwamba katika Jimbo la Wilaya ya Handeni kuna changamoto ya migogoro ya ardhi. Je, nini mpango mkakati wa Serikali hususan kwa kupima maeneo haya ya ardhi kwa kuainisha maeneo ya wakulima na wafugaji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, changamoto hii ya migogoro ya ardhi iliyopo Handeni inafanana sana na changamoto iliyopo kuna mgogoro baina ya Wilaya ya Kilindi na Wilaya ya Kiteto ambayo imedumu muda mrefu sana. Je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba inatatua mgogoro huu? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na maelezo ya Naibu Waziri juu ya swali langu Namba 24, napenda kuuliza maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ni uchumi, barabara ndiyo kila kitu. Swali hili naliuliza kwa mara ya pili katika Bunge lako tukufu lakini majibu ni yale yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza: kwa kuwa barabara hii kipindi cha mvua imekuwa hapitiki na ndiyo maana nimekuwa naomba muda mrefu kwamba barabara hii itengenezwe kwa kiwango cha lami, ni kwa sababu ni barabara ambayo ina uchumi wa hali ya juu sana; barabara hii ina ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete; kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba bajeti haitoshi, fedha hakuna.

Je, wananchi wa maeneo haya ya Gairo na Kilindi ni liniwatarajie barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: barabara hii ambayo ina magari mengi na shughuli nyingi za kiuchumi, ina madaraja au mito ya Chakwale, Nguyami na Matale; kipidi cha mvua haipitiki na Serikali kwa kweli imejitahidi mara kadhaa kujenga madaraja.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kutuma timu yake kwenda kukagua kuona hali halisi, kwa sababu barabara hii kwa sasa hivi haipitiki na wananchi wanapata adha kubwa? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri wake wa maji kwa kututengea kiasi cha shilingi bilioni 2,146,000,000 kwa ajili ya huduma kwa watu wa Kilindi, baada ya shukrani hiyo ningependa tu nimuulize swali moja tu Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo mazuri ya kwamba wanafanya tafiti na tafiti hiyo itatoa majibu ndani ya mwezi ujao, sasa nataka tu kupata commitment ya Mheshimiwa Naibu Waziri je, wananchi wa Wilaya ya Kilindi wategemee nini kuhusiana na uhakika wa mradi wa huu ambao utahudumia zaidi ya vijiji 12? Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu haya ya kusema kwamba huu wa fedha unaoanza keshokutwa hapo tumetengewa shilingi milioni 182 kwa ajili ya kutengeneza kalavati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi lilikuwa linazungumzia kwamba ni lini Serikali itatengeneza daraja, kama katika maelezo yake alivyosema kwamba eneo hili lina kilometa 38 zinazounganisha Wilaya ya Kiteto na Wilaya ya Kilindi. Eneo hili lina changamoto kubwa kwa sababu daraja ni kubwa sana, kiasi hiki kilichotengwa hakitoshi hata kidogo kwa ajili ya kujenga daraja.

Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakwenda yeye au wataalam wake kwenda kuangalia upana wa daraja hili ili Serikali iweze kutenga fedha za kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; miaka ya nyuma Serikali ilishatenga pesa kwa ajili ya daraja hili, lakini nina uhakika thamani ya fedha kwenye daraja hili haikufanyika.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kutuma timu kuona kama fedha hizi zilitumika ipasavyo? Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Binafsi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa uamuzi wa busara sana sana wa kununua magari katika halmashauri zote za Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; ni ukweli usiopingika kwamba huduma ya ambulance ni muhimu sana katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania. Hata hivyo, huko nyuma imejitokeza changamoto kwamba huduma ya magari haya ya ambulance yanapelekwa sehemu moja mawili, matatu wakati sehemu nyingine hakuna magari kabisa. Sasa nini mpango wa Serikali katika kuepuka hili siku za usoni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali imefanya jambo jema sana, inaenda kujenga vituo vya afya kwenye tarafa takribani nchi nzima. Je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tarafa zote hizo pia zinapata magari ya wagonjwa kwa maana ya ambulance? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, binafsi naomba kwanza kuipongeza Serikali kwa kuamua kuanza kujenga hata hizo kilometa 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, inaunganisha mikoa minne, kwa maana ya Mkoa wa Tanga, Manyara, Dodoma na Singida. Kama hiyo haitoshi, ni kwamba barabara hii ni barabara ambayo Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanga ndiko linakopita. Sasa nataka kuuliza swali.

Je, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa haraka na kuhakikisha kwamba kilometa zote 461 zinakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara ya kupita barabara hii mwaka 2021; na kipindi hiki mvua zinanyesha.

Je, yuko tayari kumwagiza Meneja Barabara Mkoa wa Tanga aweze kufanya marekebisho katika maeneo ambayo yameharibika?Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri tu lakini nina maswali madogo mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la Bondo katika Kata ya Mswaki ni eneo muhimu sana kwa ajili ya mvua, halikadhalika kwa ajili ya mazingira. Lakini eneo hili ni la Serikali na lina GN 341 toka 1960. Swali langu je, nini mpango madhubuti na endelevu wa Serikali wa kulinda maeneo haya ili yasiweze kuvamiwa na wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; moja ya ahadi ya wenzetu wa TFS juu ya eneo hili walikuwa wajenge Kituo cha Afya lakini naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwamba tayari tumekuwa tukipata Milioni 500 Kituo cha Afya kwenye kijiji cha Mswaki kimejengwa. Je, nini kauli ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba wako tayari sasa kutujengea bwawa kwa ajili ya kitu kinaitwa CSR? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Nataka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, barabara ambayo inaanzia Dumila kupita Turiani kupita Kata ya Negelo hadi Vibaoni Handeni, ni barabara muhimu sana. Kwa upande wa Morogoro imeshakamilika kwa kiwango cha lami: Je, ni lini kilometa 120 kwa kiwango cha lami itakamilishwa?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nimshukuru pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kwa majibu yenye kutia matumaini kiasi, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Wazari kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imetenga eneo kwa ajili ya Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa sababu eneo hilo limetengwa takribani miaka ishirini iliyopita je, ni utaratibu upi au mipango ipi au ni parameter zipi ambazo zinatumika kuhakikisha kwamba mnajenga Vituo vya Polisi kwa kuangalia uhalisia wa mahitaji ya eneo husika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye sasa hivi ni Waziri wa Mambo ya Ndani alikwishatembelea Wilaya ya Kilindi na kujionea uhalisia wa changamoto ya Kituo cha Polisi jinsi kilivyo.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari kutoa commitment kwa wananchi wa Wilaya ya Kilindi kwamba mwakani watajenga Kituo cha Polisi? Ahsante.
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, ina vijiji 102, vitongoji 611, kata 21 na tarafa nne.

Je, ni lini Serikali italigawa Jimbo hili la Kilindi? Ahsante.
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanatia moyo kwa wana Kilindi na Watanzania kwa ujumla. Ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa Jimbo la Kilindi lina eneo kubwa la utawala; lina vijiji 102, tarafa nne, kata 21 na vitongoji 611, na gari ambalo linatumika sasa hivi ni gari bovu sana. Je, Serikali iko tayari kutuongezea gari lingine baada ya utaratibu huu ambao upo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa utaratibu huu ambao kila Mbunge anaujua hapa kwamba kila halmashauri itapata magari ya wagonjwa kwa mpango wa COVID-19. Je, ni lini utaratibu huo utakamilika ili wananchi wa Tanzania waweze kupata magari hayo? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, barabara ya Handeni – Kiberashi – Singida ni barabara muhimu sana na barabara hii nashukuru mkandarasi alikwisha ripoti site lakini kinachoendelea sasahivi ni kwamba kama vile kazi aiendelei Je, tatizo liko wapi? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wilaya ya Kilindi ina Tarafa Nne, Tarafa Tatu zina vituo vya afya. Je, ni lini Serikali itajenga kituo afya Tarafa ya Kimbe, Kijiji cha Ndegerwa? Ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, barabara inayotoka Handeni kwenda Songe na Kiteto ni siku ya pili sasa hivi haipitiki kutokana na na mvua zinazonyesha, na shughuli zote za uchumi zimesimama. Je, nini kauli ya Serikali juu ya barabara hiyo? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ni lini kata ya Mkindi, Kata za Masagaru, Kwekivu na Kimbe vijiji hivi vitapitiwa na minara kwa ajili ya masiliano kwa ajili ya wanachi wa maeneo hayo?
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri tu. Lakini pia nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti, hakika uko vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali madogo mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba maeneo madogo ya utawala ni tofauti na maeneo makubwa ya utawala. Sasa je, nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba maeneo madogo hayapewi rasilimali nyingi na watumishi wengi kuliko maeneo makubwa ya utawala? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; nini mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba maeneo yote makubwa ambayo yako sawa na Kilindi ambayo yanahitaji kugawanywa yanafanyiwa mkakati wa haraka ili yaweze kugawanywa? Ahsante sana. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi wa Wilaya ya Kilindi wanatambua jitihada za Serikali za kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya. Lakini tunazo kata tatu kwenye vituo vya afya vitatu kwenye Kata ya Jaila, Masagalu na kata ya Maswaki tunahitaji at least milioni mia, mia ili kuweza kumalziia vituo vya afya. Je, ni lini Serikali italeta fedha katika maeneo hayo? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nitoe shukrani za dhati sana kwa Serikali yetu kwa kutujengea daraja hili ambalo lilikuwa linaleta usumbufu mkubwa sana kipindi cha mvua. Baada ya shukrani hizo, sasa nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata hizi mbili za Songwe na Bokwa kuna ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami; je, Serikali iko tayari kuweka taa katika eneo hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna Madaraja mawili ya Chakwale na Nguyami ambayo yanunganisha Wilaya za Kilindi na Gairo. Je, ni lini Serikali itajenga madaraja hayo?
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mwaka 2015 nilikuwa nikiomba tujengewe Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi. Naomba commitment ya Serikali juu ya ujenzi wa kituo hicho cha Polisi. Ahsante sana.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, miaka mitatu iliyopita Serikali katika mpango wake wa maendeleo ilijielekeza kwamba itajenga SGR kwa reli hii ya kuanzia Tanga – Moshi - Arusha hadi Musoma. Je, mpango huo bado upo? Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza niipongeze Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kutujengea Vituo vya Afya kwenye tarafa tatu. Tuna tarafa nne Wilaya ya Kilindi lakini tuna Tarafa moja ya Kimbe haina kituo cha afya na umbali kutoka tarafa hiyo hadi Makao Makuu ya Wilaya ni takribani kilomita 120;

Je, nini mpango wa Serikali wa kujenga kituo cha afya kwenye tarafa hiyo? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri tu. Nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sababu barabara hii inaunganisha Kata tatu. Kata ya Msanja, Kata ya Kilindi Asilia na Kata ya Kimbe, ni Kata ambazo zina uzalishaji mkubwa sana wa mahindi na kipindi cha mvua inakuwa ni shughuli kubwa magari kupita. Sasa kwa sababu suala hili liko Serikalini; Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuelekeza Mkoa sasa kufanya tathmini hiyo na iweze kupandishwa hadhi barabara hiyo?

Swali la pili ni kwamba barabara hii ina madaraja mengi na ina vivuko vingi sana na kipindi cha mvua haipitiki. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kutoa maelekezo kwa TARURA ili maeneo haya yaweze kurekebishwa na Wananchi wa Wilaya ya Kilindi waweze kupata huduma ya Serikali? Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 inatarajia kutenga au itatenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia Kitua cha Afya cha Kilindi asilia na shilingi milioni 40 kwa ajili ya hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Spika, sasa, nataka tu nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, hizi taarifa za kwamba tumetenga shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Zahanati ya Masagalu amezipata wapi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuhamasisha wananchi kujenga majengo na wao kutenga milioni 50. Je, Serikali haioni iko sababu ya kutenga milioni 50 na kuwapelekea wananchi wa Masagalu na kumalizia majengo haya? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni Septemba niliuliza swali Na. 76 juu ya wananchi ambao wamevamia Msitu wa Bono uliopo Kijiji cha Mswaki kwenye Kata ya Msanja na Serikali ilisema itawaondoa itakapofika Desemba 30, kwa maana ya mwaka 2022. Nataka kujua: Ni nani ambaye anazuia kuondoa wananchi wale ambao wanafanya uharibifu mkubwa na msitu huo tunaoutegemea kwa ajili ya mvua? Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwenye Kata ya Kilindi Asilia na Kata ya Luhande kwenye Vijiji vya Misufini kuna changamoto kubwa ya minara, kwa maana ya mawasiliano yanakatika mara kwa mara.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kutuma timu yako kuangalia namna ambavyo mawasiliano yanavyopatikana muda wote?

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's