Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Shally Josepha Raymond (44 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, namshukuru Mungu kwa neema za kutujalia sote uhai. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Profesa Sospeter Mwijarubi Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Mheshimiwa Dkt. Merdad Matogolo Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kero yangu kubwa ni kuhusu gharama kubwa ya biogas kwa kuwa maeneo ya vijijini ni wafugaji hususan wanawake wa Kilimanjaro. Naomba iwepo namna ya kupunguza gharama ya kujenga na kuunganisha nishati na madini ya biogas majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, michango mikubwa watumiaji wanayotozwa kwa ajili ya EWURA hainiingii akilini na wala haipendezi kwa watumiaji wa maji na umeme wanavyotozwa na EWURA katika ankara tofauti, bahati mbaya EWURA yenyewe hairejeshi chochote kwa wananchi kama CSR, natumaini kuona wakitoa mchango wa kuwaelimisha wanawake kwenye ujasiriamali na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumiaji wengi wa umeme vijijini ni kwa ajili ya taa na baadhi luninga na kuchaji simu. Namwomba Mheshimiwa Waziri awaagize Mameneja wa Mikoa wateremshe tozo za vijijini ili familia nyingi zinufaike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tozo la umeme kwenye shule na vyuo; kumekuwepo na malalamiko makubwa sana kwa wamiliki wa wa maeneo tajwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kurekebisha tatizo hili, mfano, Kibosho School of Nursing, Chuo hiki kiko Moshi Vijijini katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo. naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa pongezi kwako na Waheshimiwa wote kwa kuchaguliwa kuingia kwenye Bunge la Kumi na Moja. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaliwa kuwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa nami nampongeza sana. Nimeisoma hotuba yake nzuri na nimekubaliana naye, lakini naomba ufafanuzi kwa mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezeshaji wananchi kiuchumi. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, ukurasa wa 14 na 15, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi imeelezwa vizuri sana, naomba kunukuu:-
“Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuwadhamini wajasiriamali wenye miradi inayokidhi vigezo kwenye taasisi za fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba ufafanuzi wa kina kwani Tanzania ni kubwa na wajasiriamali ni wengi sana na hivyo si rahisi kama maandiko yalivyokaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rahisi kusema kuliko kutenda, hivi Waziri Mkuu anavyosema Serikali itaendelea kuwadhamini wajasiriamali anaweza kuwaeleza Watanzania ni lini dhamana hiyo ilitolewa na ni akina nani walifaidika? Endapo anazungumzia mabilioni ya JK, naomba kutofautiana naye kabisa kwani fedha zile zimetoweka na mzunguko sasa umekwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia nzuri ya Serikali, naomba wananchi wapatiwe miradi zaidi ya fedha. Katika Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwawezesha wajasiriamali na wakulima wa Kilimanjaro mradi wa kopa ng’ombe ambao uliweza kuwapatia lishe bora, nyumba za kisasa, ada za watoto shuleni na hatimaye maisha bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aya ya 23 inasema, nanukuu:-
“Serikali imehamasisha uanzishaji na usajili wa vikundi vya kiuchumi kama vile Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na Benki za Jamii Vijijini (VICOBA).
Serikali pia imesimamia uanzishwaji wa Taasisi mwamvuli ya kusimamia VICOBA inayoitwa VICOBA FETA. Takwimu zilizotolewa Februari, 2016 na Taasisi hiyo zinaonesha kuwa, kuna vikundi 100,000 vya VICOBA vyenye wanachama milioni 2.2 na mtaji wa shilingi trilioni 1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya wanachama wa VICOBA ni wanawake”. Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na taarifa njema alizotupa Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu ushirika wa SACCOS na VICOBA, naomba atufafanulie ni jinsi gani wanawake hao watapatiwa mafunzo ya ushirika. Mpaka ninavyozungumza, jukumu kubwa limekuwa kwa Wabunge. Naomba nichukue nafasi hii nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu atufafanulie jinsi ya kuwapatia mafunzo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ule ukurasa wa 16, aya ya 24, hotuba imeonesha wazi hali ya Vyama vya Ushirika, SACCOS zinazokidhi vigezo vya usajili nchini imepungua kutoka 5,559 mwaka 2013 hadi 3,856 mwaka 2015. Huu ni upungufu wa asilimia 30.6 sawasawa na 31%. Huu ni upungufu mkubwa na tatizo ni kwamba, Serikali haitoi kipaumbele kwa ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba kufafanua, Novemba 2006, Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Magufuli alitangaza Baraza la Mawaziri na ndipo umma wa Tanzania ulipozisikia Wizara zilizopo. Wengi mpaka sasa wanajiuliza hivi Wizara ya Ushirika iko wapi? Endapo ni idara, je, iko kwenye Wizara gani? Pendekezo ni kwamba, ipelekwe kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwenye Awamu ya Nne, Wizara hiyo ilikuwa kwenye Kilimo na ilijulikana kama Wizara ya Kilimo na Ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kipekee namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai kwetu sote tulio hapa, ambao tunaweza kushiriki katika mjadala huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imetupa dira ya nchi yetu inakoelekea kwa kazi zilizofanyika pia mwaka mmoja katika awamu hii ya uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt.John Joseph Pombe Magufuli. Natoa pongezi kwa uongozi mzima na namshukuru Mungu kwamba nchi yetu iko salama na tuko tayari sasa katika kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze mchango wangu kwa kuzungumzia suala zima la ajira. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ametueleza kwamba vijana wapo wengi na wamepelekwa mafunzo lakini katika hao vijana aliotueleza wamepelekwa kwenye mafunzo hatukuambiwa lengo lilikuwa ni kiasi gani. Tumeweza kupewa takwimu pale kwamba vijana waliopelekwa mafunzo katika kipindi hiki walikuwa wawe vijana ambao watarudi ili waweze kuwa wameandaliwa vizuri, lakini je, lengo lilikuwa ni vijana wangapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata hofu kwa kasi ya maendeleo. Naona kwamba kwa speed tunayoenda siamini kama endapo hatutaongeza kasi tutaweza kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Nasema hivyo nikiwa na maana kwamba, pamoja na kuwa na rasilimali nyingi katika
nchi yetu, rasilimali kubwa sana ni rasilimali watu lakini watu hawa lazima waandaliwe na waandaliwe vizuri ili wanapohitajika watumike vizuri. Kwa hiyo, naomba au nashauri Halmashauri zote ziweze kujua hawa vijana walio katika umri wa kufanya kazi wameandaliwa kiasi gani?
Nikifika hapo nataka nisisitize tu kwamba tuwe na takwimu sahihi za kuweza kujua ni wangapi na wanapelekwa vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni bei kupanda hasa za vyakula. Muhimu zaidi nikienda kwenye ukurasa wa 21 inapozungumziwa kilimo, sikuona walipozungumzia kilimo au upatikanaji wa sukari katika nchi yetu. Sukari ni bidhaa ambayo imekuwa
ikipanda bei kila mwaka. Sukari ni bidhaa ambayo inatumika kila siku kwenye nyumba na kwenye familia. Sukari ni kitu ambacho tunaita ni kifungua kinywa, maeneo mengine kama ninakotoka ukitaka baraka, basi unampelekea bibi au babu sukari na anakubariki. Sukari imekuwa ni tatizo inapopanda bei na hasa tunapoelekea kwenye kipindi cha mfungo wa Ramadhani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kama huu mwaka jana sukari ilianza kuadimika na mpaka sasa sijui kama Serikali imeshapata ufumbuzi kwamba mwaka huu sasa ifikapo mwezi Mei wakati wenzetu watakuwa wanafunga, sukari hiyo itabakia na bei ileile ili kila mtu afuturu kwa raha. Mara nyingi unakuta familia ambazo ni duni, wanafuturu kwa uji wa chumvi. Kwa kweli, katika nchi kama Tanzania haipendezi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, kipindi kama hiki, kabla hatujafikia ule wakati ambapo, nadhani sasa hivi viwanda vimefungwa tayari lakini Serikali iwe imefanya mpango mahsusi wa kuona kwamba, akiba ipo, wamewakutanisha wenye viwanda, waagizaji na wale wafanyabiashara wakubwa. Jukumu la kuagiza sukari litolewe kwa wale wenye viwanda. Hii inayokuja ghafla, sukari inaagizwa na watu ambao wapo tu, wafanyabiashara wamekaa tu wanangojea ili watupige bei siyo jambo zuri kabisa. Naomba hilo liangaliwe kwa sababu kila mtu ana haki ya kupata kifungua kinywa katika nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mbegu za mazao mbalimbali kwa wakulima wadogo. Hapa ndani ukizungumzia mbegu zinazozungumziwa sana ni korosho, kahawa, mahindi na mtama yaani zile cereals. Hata hivyo, sasa hivi tunazungumzia pia kilimo cha mihogo na viazi, sijasikia wala sikuona katika hotuba ya Waziri Mkuu akizungumzia tutapataje sasa mbegu ya viazi vitamu na mbegu nzuri ya mihogo katika Halmashauri zetu. Kwa sababu haya ni mazao mbadala na yote ni ya wanga lakini ikipatikana mbegu nzuri basi tutakuwa katika hali nzuri sana ya kuweza kuwa na mazao mengi ya kutosha na tutaweza kusahau hayo mambo mengine ya njaa. (Makofi)
Naomba nizungumzie jambo lingine kuhusu wanawake wetu na inavyozungumzwa katika Ilani ya CCM kwenye ule ukurasa wa 117, ibara ya 61, 62 na 63(a),(b), (c), (d) na (e), kuwawezesha wanawake kiuchumi. Imewekwa vizuri sana katika Ilani na imezungumzwa jinsi gani watasaidiwa au wataelekezwa kuwa na vikundi kama VICOBA na SACCOS lakini inapokuja kuwapa elimu wanaachiwa. Unakuta wanawake wako kwenye VICOBA lakini mwanamke mmoja anakuwa kwenye VICOBA zaidi ya kimoja akiamini kwamba nikivunja mzunguko hapa
nitapokea mwingine na mwingine, hiyo ni dhana potofu. Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwasiliane na vyuo au watu wanaotoa elimu ili wanawake wetu waweze kupatiwa elimu ya ujasiliamali na uwekezaji. Ukimuelimisha mwanamke umeelimisha familia nzima. Mwanamke akiwa na elimu ya kufanya ujasiriamali ambao unaeleweka, akiwa na elimu ya kuwekeza na hivi leo umetueleza hapa kwamba tutapata semina ya hisa na mwanamke huyo huyo akiwa na elimu ya hisa basi atakuwa amefungua milango ya kupata kipato ambacho kitakuwepo siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu na Tukufu itoe fursa kwa wanawake kupatiwa elimu na wasimamiwe na Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum. Wabunge hawa wa Viti Maalum wana muda wa kuzunguka mikoani na kwenye Taifa zima kuona kwamba wanawake hawa wanapata elimu. Tunaomba Serikali iweze kuzungumza na taasisi na vyuo mbalimbali, wanawake hawa wapatiwe elimu ambayo ina muendelezo, elimu ambayo kila leo watajua nikiwekeza hivi ni benki au kwenye hisa naweza nikasimama na nikawa nimeimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba niseme kwamba jambo hili la elimu bila malipo limeleta faraja kwa wazazi wengi. Kuna wazazi ambao walikuwa hawawezi kupeleka watoto wao shule lakini sasa mtoto akiandikishwa akienda shule ana uhakika wa kusoma kutoka darasa la kwanza mpaka darasa la 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ninayoiona hapa wadau wengine wa elimu wamerudi nyuma, hilo neno bure limeleta shida. Maana yake ni kwamba mpeleke mtoto wako shule atapatiwa elimu bila malipo lakini haikutoi wewe mzazi kutokununua uniform, kumlisha mtoto wako na
kutokuangalia uhakika wa vitabu vya mtoto wako, madaftari na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni jinsi gani tutaelimisha wananchi wetu waondoe hiyo dhana potofu kwamba elimu ni bure basi mtoto akishaandikishwa wewe mzazi usiangalie tena, hivi kweli? Hata mbwa anazaa mtoto wake anamtunza, anamtafutia maziwa, anajua saa za
kunyonyesha sembuse mwanadamu mwenye utashi, akili na anayetawala vyote, anashindwaje kujua kuwa mwanangu anatakiwa kula? Hii ni dhana potofu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba itolewe elimu kumwambia mtu sawa Serikali itakupa mwalimu, itatoa vitabu vya kufundishia na itahakikisha mwanafunzi anafika shuleni na anasimamiwa lakini wewe ukiwa kama mdau unatakiwa uchangie mambo yafuatayo na usikwepe majukumu. Hakuna mzazi anayezaa mtoto wake amuache hivi hivi. Naomba sana nyie Waheshimiwa Wabunge tushirikiane pamoja kutoa elimu hiyo lakini pia na Serikali iendelee kuelimisha kila wakati ili wajue kwamba wanawajibika na wanatakiwa kuendelea kutoa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nizungumzie suala la ajira. Vijana wengi wanamaliza vyuo na kuhitimu lakini wanatarajia kupata white collar jobs na kweli siyo wote wanaweza kwenda kulima. Pia wale wanaotaka kulima kama wanatokea eneo ninalotokea mimi Kilimanjaro wala hakuna ardhi ya kilimo. Niombe kama Serikali imejipanga vizuri iko tayari sasa kufungua maeneo mapya kwa vijana ambao wanamaliza vyuo waweze kupatiwa ekari za kwenda kufungua mashamba darasa ambapo pia yatakuwa ndiyo maeneo yao ya kuishi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya kugawa vihamba yamekwisha, vihamba havipo tena na vijana ni wengi, nchi hii ilikuwa na watu wachache sasa hivi tupo karibu milioni 50. Nashauri na napenda sana watu wapate baraka wazae watoto wengi tu lakini na nchi yetu ihakikishe kwamba watoto hao wanapatiwa mahali pa kukaa na mahali pa kujiendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema ni mwisho lakini sitaitendea nafsi yangu haki kama sitazungumzia suala hili la tabia nchi na jinsi ya kuboresha mazingira. Naomba sana wote tuwe tayari sasa kuotesha miti.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na nafasi tuliyopata sisi Wabunge kuzungumzia mambo ya maendeleo ya nchi yetu katika jengo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyekiti wangu, amewasilisha ripoti ambayo ni nzuri kabisa, ripoti ambayo tuliijadili na ripoti ambayo inazungumzia mambo mengi. Nimesimama kuweka msisitizo katika mambo machache tu ambayo labda naona ni vyema kama wote, tukayafahamu na tukaweza kuyafafanua zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze sana Amiri Mkuu ambaye ni Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuvisimamia vyombo hivi na kuviimarisha na hata tukawa na amani katika nchi yetu, amani inayotuwezesha sisi tukae hapa, tuweze kuzungumza kwa nafasi bila wasiwasi,. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ina amani kwa vile Wizara ya Ulinzi na Usalama na Wizara zote nyingine zinazohusu mambo hayo ziko vizuri, Wizara ya Mambo ya Ndani, ikisimamiwa na Waziri wetu Kangi Lugola na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ikisimamiwa na Waziri wetu, Mwinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati hatukuona tatizo sana, kwa hela za matumizi kutoka kwa wakati, hela ambazo zilikuwa zina shida ni hela za maendeleo. Inapokuwa kwamba hela za maendeleo haziendi kwa wakati kama ilivyoandikwa kwenye ripoti yetu, inakwamisha mambo mengi na hapa nitaanza sasa na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, haikuweza kupata hela za maendeleo kwa wakati muafaka na hivyo kufanya majengo yetu yaliyo katika Balozi kuwa katika hali ambayo siyo nzuri. Wakati Balozi zetu haziko kwenye hali nzuri, inaonesha taswira mbovu kwa nchi, majengo yale yanaonekana yamekaa tu na kwa hivyo basi, kwa vile hatukupata pia nafasi sisi Wabunge, kwenda kutembelea yote nitakayozungumza hapa ni kwa nadharia kwa yale tuliyoelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kwamba kwa kuwa ni ngumu sana kuendelea kulipia kodi ya pango katika maeneo mengi kwenye Balozi zetu, ni vyema sasa, Balozi zetu zikawezeshwa, zikajenga majengo yake, zikaweza kupangisha zikanufaika kwa kodi na pia ikaonesha jinsi ambavyo sisi tunajali heshima ya kuwa na Balozi katika maeneo husika. Sioni sababu ya kutaja yote lakini, niseme ni mengi, imekuwa hivyo, kwa hiyo naweka msisitizo kuwe na mortgage finance ambayo itasaidia Balozi hizo, kwa sasa na kwa muda ujao wakaweza kupata kipato lakini pia wakawa katika hali nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hayo tu, hata magari yaliyoko kule, naamini nitatoa ushuhuda kwa magari yaliyo India kwa sababu niliwahi kwenda matibabu New Delhi nikaliona gari la Balozi na zile fujo za uendeshaji India, gari hilo limegongwa kila upande huku na huku, lakini sio rahisi sana, pia wakawa na magari kwa wakati muafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali ione umuhimu wa kuonekana kwa sababu wanasema ni vyema muonekano ukawa mzuri, yaani halo effect, mara moja na mtu akaku-judge kwa muonekano mpaka akaja kukuangalia ndani inakuwa ni jambo la baadaye sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuhusu Wizara hii ya Mambo ya Nje, ni ile (APRM) African Peer Review Mechanism haijaweza kupata nafasi yake katika nchi yetu. African Peer Review Mechanism inaiweka nchi katika mizani na nchi nyingine na sisi tunaamini Tanzania tuna utawala bora, tunaamini Tanzania tuna uongozi mzuri, tunaamini Tanzania sasa hivi, tuko vyema. Ni kwa nini basi, African Peer Review Mechanism isiwezeweshwe ili tukapimwa, tukalinganishwa na nchi nyingine za Afrika wakaweza kweli, kutupa tathmini, wale eminent persons wanaofanya tathmini hiyo, imeshafanyika mara moja, miaka ya nyuma, lakini wakati muafaka, eneo hilo limepauka, ofisi hiyo imebidi wamrejeshe, Bibi Rehema Twalibu aendelee kukaa kaa pale tu lakini sio kwa hali ambayo inakubalika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua huku Bungeni kuna mwakilishi ambaye anatuwakilisha kule, lakini hela wanazopata zinapitia Wizara ya Mambo ya Nje, wangeweza wenyewe kupata fungu lao na wao wakaweza kupangilia na hivyo basi tukaweza kufanyiwa tathmini vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa, kwenye uwakilishi wetu, katika Balozi katika kutafuta biashara. Hivi majuzi yamekuweko mazungumzo na pia hali halisi kwamba kuna mizigo iliyokuwa inakwenda Congo, lakini imekwama kwa sababu au ni ya mahusiano, au ni jinsi ambavyo hatujaweza au Wizara yetu haijaweza kusimamia vizuri, naomba kupitia Bunge hili, sasa Wizara ya Mambo ya Nje, ifanye mkakati maalum ili hata ile mizigo iliyokwamba Tunduma itoke mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba sisi, misimu yetu ya kilimo inafahamika wazi, ni wakati gani tunalima, wakati wa masika, ni wakati gani tunavuna, ni wakati gani tunauza, mara nyingi na imekuweko hata juzi, hata jana, tumezungumza kwamba bidhaa zetu, yakiwemo mahindi hayana soko, lakini kama Wizara hii, ingezungumza na Wizara nyingine za Mambo ya Nje, mahindi haya yangetoka yakapitia Zambia, yakaenda kuuzwa, sioni kwa nini tuna Wizara ambayo inahusika na bado mambo hayo hayatekelezeki kwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wakati wa kupitisha maazimio ya hii ripoti yetu ya Kamati, jambo hilo likafikiriwa na likazungumziwa sana ili tupate masoko mengi, kote, ili bidhaa zetu, ziweze kuuzwa kwa haraka na wakati muafaka, hela hiyo iweze kurejeshwa kwa wananchi wetu na sisi wenyewe tuendee kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Majeshi yetu yameendelea kuimarika kila wakati na niseme tu, kuna mambo machache ambayo yakiwekwa vizuri, hata majeshi haya yatakuwa hayalalamikiwi na mambo haya sijui kama yanahusu sana haya majeshi moja kwa moja au yanahusu Wizara ya Fedha kwa sababu ni madeni ya nyuma ya majeshi yetu kulipa katika vyombo vinavyotoa huduma, vikiwemo vyombo vinavyotoa huduma ya maji na vyombo vinatoa huduma ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu tumeingia Bunge hili tumekuwa tukiomba sana madeni ya maji yalipwe kwenye mamlaka za maji. Kuna maeneo ambayo ni nyeti, huwezi kwenda kukata maji; na hapa eneo la uhakika na la karibu sana ni Chuo cha Polisi Moshi. Kuruta wanapoingia pale wanaingia wengi kwa mara moja, maji yale yana madeni ya siku za nyuma ambayo ni makubwa yanakwenda kwenye takriban bilioni mbili. Kwenda kukata maji kwa kuruta haiwezekani na wala haieleweki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba, kwa sasa wanakwenda vizuri kulipa current bills lakini basi Wizara ya Mambo ya Ndani izungumze na ione kwamba italipaje madeni ya nyuma ili ile Mamlaka ya Maji kule Moshi (MUWASA) isifunge shughuli nyingine na wala watu wasichukie watakapoona kwamba wamepeleka pendekezo la kupandisha maji, watadhani kwamba ni kwa ajili ya ile bili kubwa ya CCP ndiyo maana wananchi wanapandishiwa maji. Hapa naweka msisitizo tunaomba sana madeni ya nyuma yalipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme pia walizungumzia, lakini niseme kwamba ni vyema basi vyote hivyo vikafanyika kwa pamoja ili tuweze kujua kwamba kama tunavyoamini majeshi na msemo unaosema hilo jeshi mambo yake na vitendo vyake sawasawa, viwe sawa hata kwenye ulipaji madeni ili wote waweze kuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba napongeza ile hali ya vyombo vetu vya majeshi kuweza kuwa na kandarasi zao; ujenzi wa nyumba za polisi wanajenga wenyewe sasa. Hata hivyo, naomba basi pamoja na kwamba wanajenga wenyewe, wajenge nyumba za kwenda juu; na hizi nyumba za kupanga bungalows zinachukua nafasi kubwa. Ni wazi kwamba kwa sasa Mungu haumbi tena nchi, alishaumba, ni sisi wenyewe tutumie vizuri. Kwa hiyo nitoe rai yangu kwamba majengo yanayojengwa sasa polisi na kwingineko yaende juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nipongeze vyombo hivyo vyote na niwaombee kwa Mungu tuendelee kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia Mapendekezo haya ya Mpango. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai kwa sababu wote tulio hapa tumebarikiwa kuweza kuzungumzia maendeleo ya nchi hii na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutamka rasmi kwa kweli kwamba Mpango huu ni mzuri na umeandaliwa kitaalam na kwenye Kamati tulipata fursa ya kuelimishwa. Sambamba na hilo, niseme mambo mengine yametekelezeka siku za nyuma ni bahati tu kwamba jambo likishatekelezeka haliwi tena motisha. Nasema hivyo kwa sababu hata guru mmoja wa management Maslow alisema: “once a need is satisfied is no longer motivation”. Hapo alikuwa anazungumzia mahitaji maalum ya mwanadamu katika maisha, ikiwemo chakula, mavazi, malazi yaani nyumba na pia labda esteem hierarchy of needs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Tumekuwa na kipindi kizuri japo kwa kupambana lakini tumefuta maradhi. Kwenye Mpango wa kwanza kabisa walikuwa wamedhamiria kuondoa ujinga, umaskini na maradhi. Ujinga umeondolewa kwa jumla na sasa hivi Watanzania wanaweza wakaongea kama watu wanaoelewa. Siyo hayo tu, maradhi yaliyokuweko wakati tumepata uhuru hayapo tena. Hata awamu hii tumeona hospitali zimeboreshwa, madawa yamekuwepo, tunaona ni jambo la kawaida ambavyo siyo kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo. Niseme tusibweteke bali tuzidi kupambana na hapo ndiyo nasema kwamba kuna haja ya kila mmoja wetu hapa ndani kuleta mapendekezo ili kuboresha Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunapanga? Tunapanga ili kutengeneza taswira ya siku za baadaye tunataka nini na iweje. Pia tunapanga kwa sababu rasilimali ni kidogo hatuwezi kwenda na vyote kwa mkupuo lazima tupange ili twende na vichache tupangue kila kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu nilitamani kuona jinsi gani mwananchi wa kawaida anapata fursa nzuri kufikia benki na ninaposema benki nina maana mabenki yaliyopo nchini. Mpaka sasa hivi tuna commercial banks zinazozidi 50 na zinakaribia 60 tuseme zaidi ya 57 lakini mabenki hayo pamoja na watu kupenda kuweka hela zao benki kwa usalama, kuweka katika amana ili waweze kuzifaidi siku za baadaye na ili ziweze kuongezewa, ukiweka kwenye amana unapata interest rate yaani unapata faida imekuwa ngumu kwa sababu gharama ambazo benki inatumia kuweka hela zile imezidi ile asilimia 3 ya amana inayolipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza mwananchi huyu wa kawaida ambaye hataki kulalia hela yake kama mto, hataki kuificha ikaja kuliwa na mende na panya au siafu, anafanyaje ili aweze kupata raha ya kuweka hela yake benki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo mwananchi huyu huyu anapopeleka hela yake benki kuna mwingine ambaye yuko tayari mwenye uelewa zaidi anakwenda kukopa. Hapa kwenye ukopaji wako wa aina mbili, wako wakopaji ambao ni wa biashara, wakopaji wakubwa wakubwa au hata kama hakopi lakini wafanyabiashara wakubwa kama aliyekaa kushoto kwangu, lakini wako wakopaji wadogo kama mimi ambao tunakopa katika mishahara yetu na wafanyakazi wote wa nchi hii. Ukija kuangalia riba zao zinalingana anayekopa kwenda kufanya biashara ni asimilia 16 au 17 na anayekopa kutoka kwenye mshahara ni asilimia 16 au 17. Sasa najiuliza uhalali uko wapi? Natamani kuona Mpango huu wakati unaandaliwa mabenki hayo yanakaa chini na Serikali na kuona namna ya kuteremsha riba hii ya kukopa. Unakuta Benki Kuu iko vizuri, discount rate sasa hivi imefika 7 ambapo ndiyo gharama ya commercial banks kuchukua hela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka nadhani ni mwanzoni mwa mwaka huu au mwishoni mwa mwaka jana Serikali imeamua kuwa Treasury Single Account. Kwa hiyo, sasa hivi mabenki hayapati hela kiholela kutoka Serikali lakini hela hiyo pia haipatikana kwa gharama kubwa sana inapatikana kwa asilimia 7 tu, nilitaraji kuona anapokopa mtu wa kawaida ambaye ni mfanyakazi, Mbunge au mtu ambaye kulipa wakati wa re-payment hakuna gharama kubwa akopeshwe labda asilimia 3 juu ya ile ya Benki Kuu ya 7, kwa hiyo, iwe kwenye single digit kama asilimia 9. Katika Mpango huu ningetamani kuona hizo riba zinarekebishwa mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nikirudi kwenye watu wa kawaida kuwa na account, nakwenda sasa kwenye mkulima wa korosho kwa sababu mwaka huu tumeelimishwa sana kwenye korosho anayefungua account katika benki wakati wa mauzo ya korosho. Mauzo ya korosho au kahawa yako kwa msimu, msimu ukiisha kashachukua hela yake amekwenda kujenga, amekwenda kufanya nini mpaka msimu mwingine tena wakati analipwa na lazima alipwe kwenye benki, anakuta ile account imeshakuwa dormant anaanza kuhangaika. Mzee huyu ametoka kijijini ametumia gari, amelala kule ili aweze ku-activate account, ni jinsi gani Serikali itaelekeza au itaongea na mabenki haya hizi account za hawa wakulima ziweze kuwa wazi bila gharama wala usumbufu leta barua kwa Mwenyekiti, leta kitambulisho hiki watu hawa account hizo ziwe wazi kila wanapokuja kuingiza hela yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupendekeza jambo lingine ambalo ni kuhusu kujenga taifa lenye afya. Taifa zuri lenye afya ni taifa la leo na kesho. Wote hapa tuna afya nzuri kwa sababu wazazi wetu walitulea vizuri kati ya siku moja mpaka miaka mitatu. Sasa hivi unakuta utapiamlo bado uko katika maeneo yetu, hata maeneo ambayo unaweza ukafikiria labda wana vyakula sana na ambayo unaweza ukafikiria labda lishe ni bora ikiweko Kilimanjaro bado kuna utapiamlo, Mbeya bado kuna utapiamlo, hiyo ni Mikoa ambayo nina uhakika utapiamlo uko kati ya asilimia 29 mpaka 30. Sasa Mpango huu unatusaidiaje kuhakikisha kwamba tunafuta kabisa utapiamlo katika nchi hii kama tulivyodhamiria kufuta kabisa watu kutembea bila viatu, tumeweza tukafuta watu hao hao wakaweza kuwa na afya bora, tukawa tunatoa dawa za minyoo shuleni, tunakwenda tunatoa vaccination shuleni, nakadhalika na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiitumia Wizara ya Mifugo na Wizara ya Kilimo tunaweza tukafuta utapiamlo. Wananchi wakielimishwa kuwalisha watoto wao vizuri na sasa hivi Waziri wa Afya anasema kabisa mtoto wako asile chochote mpaka miezi sita na kila binti anayejifungua sasa anatamani kunyonyesha kwa sababu pia binti ukionekana hunyonyeshi tayari unaonekana una yale maradhi, kwa hiyo, siku hizi wananyonyesha. Baada ya muda wa kunyonyeshwa mtoto huyu aendelee kupata chakula kizuri hata ule uji unaopikwa mashuleni uwe mzuri, uwe na maziwa, yagawanywe shuleni watoto wale wadogo wanywe uji wa maziwa mazuri na mayai yagaiwe shuleni, yai moja moja kila mtoto, watoto wetu wale vyakula vizuri waondokane na utapiamlo. Mama mjamzito ale vizuri kwa sababu mtoto anaanza kupata virutubisho akiwa ndani ya mama na siyo nje. Mama akila vizuri anachokula kinaenda kwa mtoto na baada ya kujifungua hicho hicho ndiyo mtoto anaendelea kunyonya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo niombe kabisa Mpango huu uonyeshe jinsi gani mama atatuliwa ndoo ya maji ifikapo 2020/2021. Tumelipigia kelele huku Bungeni hata tumeomba iongweze shilingi 50 lakini bado kuna maeneo hayajawezekana. Kuna maeneo ambayo yamefika asilimia 90 nayo ni mjini lakini vijijini maji safi na salama hakuna kiasi hicho. Naomba tunapoelekea kumaliza Bunge hili turudi tukisema angalau tulizungumzia maji na sasa Tanzania nzima ina maji safi na salama na hakuna mwanamke anayejitwisha ndoo umbali mrefu, muda ule wa kwenda kubeba maji anautumia kulea familia na kwa kazi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu mazingira. Natamani kuona ifikapo mwisho wa Mpango huu hakuna mwanamke anayepikia kuni, wala mkaa ila wote tunatumia NLG (gas) na tupewe mafundisho ya kutumia gesi ili zisije kuleta madhara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tuko hapa tunatamani kusaidika na sisi tukasaidie watu wetu, naomba sana chondechonde viingie kwenye Mpango. Ahsante kwa nafasi hii nashukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote walio kwenye ofisi yake pamoja na ya Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu; mafunzo kwa wanawake wajasiriamali. Tunashukuru kwa vitambulisho. Kipekee tunaomba wawezeshwe kielimu na hasa kwenye utunzaji wa fedha ili wakuze vicoba vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kwa fursa hii na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na watendani wote.

Mheshimiwa Spika, swali langu linahusu zao la kahawa Mkoa wa Kilimanjaro. Serikali ina mpango gani kushirikiana na wakulima wakubwa ili watoe msaada wa pembejeo, elimu na hata kuwatafutia soko wakulima wadogo? Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii; na jina langu ni Shally Josepha Raymond, lakini kwa vile baba yangu alikuwa anaitwa Joseph, mkiita hivyo naitika na nakubali pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu sana kwamba ametuweka wote hapa tuweze kuzungumzia mambo ya maendeleo ya nchi yetu. Kipekee naomba shukrani hizi ziwafikie wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao ndio walionipigia kura nikaingia hapa kupitia Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia Wizara ambayo ni nzito na Wizara ambayo kwa kweli Ilani ya CCM inazungumza wazi kwamba sasa twende kwenye uchumi wa viwanda kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Iko kwenye ilani! Mwasilishaji wa hotuba hii, Waziri wetu yuko makini na ni mzungumzaji mzuri, ameongea kwa makini, wataalam wameandaa hotuba vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla yangu amezungumza Mwenyekiti wa Kamati hii, na mimi niseme kwamba naungana naye na yote aliyosema, lakini na mimi nataka nihoji kupitia kwako Mwenyekiti, Kamati ilipokaa ilikuwa na nia nzuri na imetuambia, ila kuna mambo magumu nimeyaona kwenye taarifa ya Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna shida ya uwasilishwaji wa fedha za maendeleo. Hadi kufikia mwezi huu wa tatu walikuwa wamepewa shilingi bilioni moja tu. Sasa shilingi bilioni 1.6 kwa viwanda vya Tanzania nzima, itafanya nini? Nirudi pia kwa Waziri wangu, yeye leo hapa amekuja na kitabu chake hiki, anatuomba hapa tumpitishie shilingi bilioni 81.8, Tanzania nzima! Hivi kweli fedha hiyo ndiyo italeta mabadiliko ya viwanda? Haifiki hata trilioni moja! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipitia hiki kitabu cha Mpango wa Maendeleo, nikidhani kwamba labda hiyo ndiyo Wizara iliyopewa fedha nyingi kutokana na mabadiliko tunayotarajia, lakini nikakuta hapana, kuna Wizara ambazo zimepewa mpaka shilingi trilioni tatu. Sasa hii Wizara ya Viwanda na Biashara inashindikana nini kuipa hata shilingi trilioni mbili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuwaombea fedha ili hii mipango mizuri iliyoainishwa kwenye kitabu hiki iweze kutekelezeka. Niseme wazi kuna jambo ambalo linanikera. Wakati sisi huku tunawaombea fedha au tunaona kwamba fedha hii haitoshi, Mawaziri wetu wanatuambia hiyo hiyo, tutaenda kigumu kigumu! Hii siyo kazi ya mtu! Ni kazi ya nchi hii, sisi tumeona, na ninyi mnatakiwa mwone! Fedha hii haitoshi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miaka ya 1980, SIDO ilikuwa inafanya vizuri sana nchini. SIDO zikuwepo katika Mikoa yote na sasa hivi SIDO zimebaki mfumfu tu, haziko vizuri. Sasa najua tunapoongelea viwanda, kuna viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Mimi kwa ajili ya ajira ya vijana wetu, naomba nibaki kwenye viwanda vya kati au vidogo kiasi ili nianzie hapo SIDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mkoa una eneo la SIDO limetengwa na wapo sasa watu wanafanya shughuli kule ndani ya SIDO, lakini Serikali kiasi imetoa mkono wake. Mimi nilikuwa naomba maeneo haya ya SIDO na viwanda hivi vilivyokuwa vimeanzishwa kwenye SIDO, sasa vifanyiwe kazi maalum ya kivifufua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shughulil za viwanda, wengi tunazungumzia tu mashine, lakini nguvu kubwa ya kiwanda ni rasilimali watu, na sisi watu tunao. Tunao vijana wetu ambao wanatafuta ajira. Ndiyo maana unakuta hata zile nchi zinazoendelea, zinatafuta nchi ambayo ina labor, yaani cheap labor inakwenda kufanya huko viwanda vyao. Sisi iko hapa hapa, tunataka kufanya viwanda hapa. Kwa hiyo, tuna hao vijana watakaopata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumbukumbu zangu sahihi kabisa, kila kitu kilikuwa kinapatikana SIDO, vijiko vizuri vya SIDO, makufuli mazuri ya SIDO, vitasa vizuri vya SIDO, makarai, mabeseni, leo imekuwaje? Kwa nini hatuvipati vitu hivyo? Eti tunaagiza, tunataka vitu imported, vitusaidie nini? Matokeo yake ndio hata vitu vingine tunaishia kwenye mitumba, wenzetu wamechoka wametupa, sisi tunaletewa huku, hapana!
Naomba kupitia kwako, Wizara hii isimamie SIDO, vijana wetu wapate ajira na ndiyo hiyo sasa tuanze kuona tunafufua viwanda kwa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vikubwa ambavyo vilikuwa nchini na bado baadhi vipo. Wakati huo nitoe mfano wa Kiwanda cha Kuzalisha Sukari (TPC), kiwanda cha kuzalisha sukari. Ajira yake ni watu 5,000, lakini haikuishia tu ajira, kiwanda hicho kilikuwa pia kina training school. Wale vijana wanakuwa trained pale, wanakuwa na shule ya kuwafundisha, wanaweza kuchonga vyuma, wanaweza kukarabati vyuma hivyo, wanaweza kuvitumia. (Makofi)
Sasa nilikuwa naomba kila mwekezaji anayekuja akaweka kiwanda, awe pia na nafasi ya ku-train vijana wetu ili wawe ni watu ambao wana ujuzi katika jambo lile linalofanyika. Hili linaweza kufanyika pia kwenye viwanda vya sementi, bia labda na viwanda vingine. Pia kwenye hicho kiwanda cha TPC ningependa pia wafufue ile training school.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi nyumbani. Naelewa kwamba charity starts at home. Mimi nitokako ni Kilimanjaro, viwanda vyetu vyote vimekufa, sasa hivi tunacho hicho kiwanda kimoja cha TPC na labda kile cha Bonite ambacho ni private na kiwanda kingine ambacho kipo ni kiwanda kidogo tu cha kutengeneza bia. Tena ni bia ya Serengeti maana ile Kibo imeshakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anapita katika kampeni zake za kuomba kura za Urais, alisema haitachukua muda mrefu viwanda vyote vitafufuliwa. Kwa haraka haraka naomba nivitaje tu; najua haviwezi kufufuliwa mwaka huu au mwaka ujao, lakini ianze sasa basi process ya kifufua. Tuna Kilimanjaro Machine Tools, tuna Kiwanda kile cha Magunia na hiki ni kiwanda muhimu kwa sababu pale Kilimanjaro ni wakulima wa kahawa na hii kahawa haiwekwi kwenye gunia lingine labda kama la sulfate, hapana, unyevu utabakia. kwenye kahawa. Gunia moja tu linalofaa kuweka kahawa ni lile la jute. Kwa hiyo, bado kuna soko la magunia hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wangu ajue kwamba sasa kuna kazi kufufua kile Kiwanda cha Magunia. Haiishii hapo, pia kuna Kiwanda cha Ngozi. Kwenye kiwanda cha ngozi, kuna private sector ambayo kuna muhindi, ni Shaha Industries, anatengeneza vifaa vya ngozi ila umeme unakuwa ni shida na pia kodi zimemuwia ngumu amefunga, aweze pia kuzungumza naye ili kiwanda hicho kifunguliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tuna shauku kubwa, tuna hamu ya kuona kwamba tunapiga hatua. Naomba nimtakie kila la heri na ninaunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kipekee namshukuru Mungu na nakiri kwamba Mungu ni mwema kila wakati ndiyo maana tuko hapa wote kama ilivyompendeza yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme wazi kwamba nitazungumzia maeneo matatu tu na nitajikita katika hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Nashukuru kwamba kitabu hiki ni kizuri, kimeeleweka na sasa basi nataka kuzungumzia machache ili niendelee kuboresha maeneo aliyotuletea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na ule ukurasa wa 38 pale alipozungumzia Mfuko wa Afya ya Jamii (Community Health Fund). Mfuko huu ulianzishwa siku nyingi na ulianza pia wakati inaanza NHIF lakini hauko katika mfumo rasmi kama NHIF ambao uko kwa watu ambao wana ajira na wanapata mishahara yao kila leo. Kwa hiyo, NHIF utakatwa kwenye mshahara lakini hii CHF ni ya hiari. Inapokuwa hiari leo ukiwa nacho utatoa kesho huna hutoi. Bahati nzuri sana Serikali inajazilia mkitoa kumi Serikali inajazia kumi, mijini au manispaa inaitwa tele kwa tele huku kwingine inaitwa kujazilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nia nzuri ya Serikali mfuko huu umedumaa. Pamoja na takwimu tulizopewa hapa kwamba wanachama wameongezeka lakini kwa Tanzania nzima figure ni kidogo. Sasa nini kifanyike? Serikali ina nia nzuri kuwa na wananchi wenye afya nzuri kwa sababu Taifa lenye wananchi wenye afya nzuri ni Taifa zuri. Watu wanafanya kazi, watu hawaumwiumwi, hakuna wengi waliolazwa hospitalini na pale anapopata rufaa anakwenda kutibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shida ya CHF unakatwa au unakuwa na hiyo kadi unatibiwa katika eneo linalokuzunguka, pale pale katika kata labda sanasana wilaya, huwezi kwenda mbali. Inapokuja rufaa ile kadi haitumiki wakati NHIF unaweza ukatibiwa Tanzania nzima. Ombi langu la msisitizo Serikali ione sasa kuna kila sababu kuuongezea mfuko huo ili mtu akishakuwa na ile kadi ya CHF atibiwe kutoka wilayani mpaka mkoani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wetu hawajiwezi sana, mara nyingine kama mtu hana watoto basi inakuwa uwezo wake ni mdogo. Naomba hili lifikiriwe kwa mapana, Serikali haiwezi kupungukiwa kwa kiasi hicho. Siku za nyuma watu hawa walikuwa wanatibiwa bure leo imekuja lazima tuchangie na sasa tuko kwenye wakati wa mpito Serikali inataka iwe na ule mfuko wa jinsi ya kutibu kwa ujumla, naomba sana hili jambo lisimamiwe na liwezekane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema kilio changu cha CHF, kwa sababu naumia sana kwani wanawake wa Kilimanjaro wengi wangependa kujiunga lakini wamejiunga wachache kutokana labda na hali duni, wakati mwingine mazao hayatoshi au kipato ni kidogo na ninaamini hata huko kwa Wabunge wengine hali ni hiyo. Niseme wazi Wabunge tulio hapa ni wadau wakubwa wa mfuko huo kwa ajili ya watu wetu na hasa wale Wabunge wa Viti Maalum tunaweza kutumiwa kutoa hiyo elimu na siku zote tuungane kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naomba sasa nizungumzie jambo lingine ambalo ni ajira kwa vijana. Jambo hili limezungumzwa kwa muda mrefu, ajira kwa vijana, mimi najiuliza vijana wa wapi? Najiuliza mwenyewe vijana wa Tanzania walio wapi? Ni kina nani hao?
Wana ujuzi gani? Je, hii ajira mnayomfikiria anaitaka? Sasa leo ilivyokuja TAMISEMI nikajua hapa hapa jungu kuu, kwa sababu hakuna zaidi ya TAMISEMI. Halmashauri zetu ndizo zenye watu wote na vijana wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ufanyike utaratibu rasmi wa kutambua vijana ambao hawana ajira. Vijana hawa wakishatambuliwa tuwajue wako eneo fulani kama ni kata, kama ni wilaya wako vijana wangapi na wanataka ajira za aina gani? Suala hili linaweza likaonekana gumu lakini tuna vijana wetu wengi wanafanya research zao lakini hazifanyiwi kazi. Kuna vijana wengi ambao wako kwenye shule au kwenye vyuo lakini nao pia hawatumiki. Naomba sasa halmashauri ziwajue vijana ambao hawana kazi na watambulike rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano kidogo tu. Hivi tulivyo hapa kuna vijana wanaandikishwa kwenda JKT unakuta wilaya nyingine wamepeleka maombi vijana 5,000 na wanatakiwa vijana 200 tu. Je, wale 4,800 wanakwenda wapi? Tuwatumie sasa wale vijana tuwajue hawa ndiyo kundi linalohitaji ajira na tuwaelekeze namna ambavyo watasaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ambayo hayatumiki mfululizo, mojawapo ni eneo la Nane Nane unakuta nyumba zipo, watu ambao wanakuweko pale au mashirika wakishatumia ile wiki ya Nane Nane nyumba zile zinafungwa sana sana zinakuwa ni maeneo matupu. Kwa nini sasa vijana kama wale tukishirikiana na hawa wadau ambao wana majengo huko Nane Nane, tusiwatumie kama majeshi yetu, kama ni wale wakulima, vijana wale wakafundishwa pale kwa muda hata wa mwaka mzima mpaka tena itakapofika Nane Nane na baadaye Serikali ikasaidia kuwapa kianzio? Mtu kusimama na kuweza kujitegemea au kusimama mwenyewe ni kitu kigumu. Ndiyo maana unakuta hata mstaafu anapofika wakati wa kustaafu anaomba kuongezewa muda kwa sababu hajasimama sembuse vijana wetu hawa wadogo? Naomba Serikali na sisi wenyewe tuwasaidie vijana hao wasimame wapate ajira na waweze kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo nataka kulizungumzia ni hili eneo la biashara ndogo ndogo. Ni kweli tamko limetolewa kila mahali watambue maeneo ya kufanyia biashara na yapimwe. Hili ni jambo zuri na ningeomba kabisa hata hizo Halmashauri hivi sasa zilinganishwe au zipimwe kwa kigezo hicho kwamba ni Halmashauri gani zimeweza kutambua maeneo hayo au Halmashauri ngapi zimeweza kuweka hayo maeneo katika hali nzuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niseme jambo moja. Kuna zile biashara ndogo ndogo zaidi, biashara za babalishe, mamalishe, nataka niufahamishe umma huu kwamba sasa hivi watu wengi wanapenda kula kwa mama lishe kwa sababu chakula ni kitamu, kinapikwa kidogo na kilichoungwa vizuri na nazi na kila kitu. Mtu anapiga kona tu anachota anakula kwa mama lishe. Shida ya maeneo haya yamekaa hovyo hovyo, takataka zinatupwa hovyo, mitaro inaziba, huwezi kumchukulia mtu hatua matokeo yake ni kipindupindu na magonjwa ambayo hatukuwa tumetarajia. Hii yote ni kwa sababu wale ni watu ambao wanatembea na jiko na vitu vyake vya kulia, dakika yuko hapa, dakika yuko pale, wanahamahama. Athari nyingine Serikali inaingia gharama kubwa sana kusafisha miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika ule ukurasa wa 37, Mheshimiwa Waziri ameongelea shughuli za usimamizi wa usafi kwamba sasa baada ya tamko la Rais tufanye miji yetu safi kila mwisho wa mwezi kila mtu akafanye usafi, itadumu kwa muda gani? Is this sustainable? Inatakiwa sasa tujue kwamba watu wote wanatakiwa waweke maeneo yao safi hususani hao akina mamalishe na babalishe. Mwarubaini wake ni nini? Ni Halmashauri zetu kutenga maeneo sasa ya kina mamalishe wawaambie hapa ndiyo mtakapokuwa mnafanyia biashara zenu na msionekane kwingine. Siyo tu kwa akina mamalishe ni pamoja pia na wale vijana wetu ambao wanaitwa matching guys.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, ninamshukuru Mungu kwa kuwezesha kujadili mada za kuiletea nchi yetu ya Tanzania maendeleo.
Pili, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri, Injinia Edwin Ngonyani na Injinia Joseph Nyamhanga, Katibu Mkuu Ujenzi, Dkt. Leonard Chamuriho, Katibu Mkuu Uchukuzi, Profesa Faustine Kamuzora, Katibu Mkuu Mawasiliano, Injinia Dkt. Maria Sasabo, Naibu Katibu Mkuu Mawasiliano na watendaji wote wa Wizara husika na bodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni kuhusu mawasilianio ya simu. Utakubaliana na mimi kwamba simu za mkononi zimeshamiri kila kona ya nchi hii, lakini kila leo gharama za simu zinapanda.
Swali, hivi Mtanzania wa kawaida anafaidikaje na wawekezaji hao wa mitandao mbalimbali wakiwemo Airtel, Vodacom, Tigo, Zantel, Halotel na wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atoe mwongozo kwa makampuni hayo yatoe elimu ya ujasiriamali kwa wanawake kama mgao wa CSR. Niko tayari kuungana nao kule Kilimanjaro ili elimu hiyo iwafikie wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi naungana na wenzangu kuendelea kumpongeza Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache lakini sitaweza kumaliza ila nianze tu na yale ambayo ni muhimu zaidi. Kwenye ukurasa wa 43 kwenye kile kifungu cha 58 kazi mojawapo au shughuli aliyotuambia ni pamoja na programu ya Taifa ya kurasimisha na kuzuia ujenzi holela mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sizungumzii hayo anayokwenda kufanya nazungumzia miji ilivyo sasa hivi. Ni kweli miji yetu ilikuwa imepangwa hasa ili miji ya awali kwamba kuna maeneo ya residential, industrial areas, miji na kadhalika. Kilio changu ni hali tuliyofikia sasa, eneo kama Oysterbay ni residential area lakini sasa unakuta Oysterbay kumekuwa ndiyo kwenye pubs, vilabu, ndiyo kwenye kelele usiku na mchana, Oysterbay. Leo Mwalimu angefufuka angesema nini? Sasa sijui jinsi gani yeye Waziri ambaye anashughulikia makazi analizungumzia hili na anafanya nini ili Halmashauri zisiruhusu kujenga hivyo? Sasa hivi Oysterbay hakukaliki, ni fujo tupu. Namuomba Waziri huyu mhusika aweze kuona ni jinsi gani sasa watu watalala usiku na kuamka mapema wakafanye kazi zao. Oysterbay na kwingineko kumeharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu huu Mji wa Dodoma, ni mji mtarajiwa kuwa Mji Mkuu au Jiji la Taifa, lakini kuko hovyo, Dodoma haijakaa namna hiyo na Dodoma ndiyo yenyewe yenye Capital Development. Iweje watu wa Nigeria walivyokuja huku, walichukua zile ramani zetu wakati wakitaka kuhamisha Lagos kwenda Abuja, wameweza kutekeleza, mji ule umehama na ni kuzuri tu. Si kweli kwamba hawa Mawaziri wetu hawajasafiri, kabla hujatua nchi yoyote ndege ikianza kutua unaona miji ilivyopangika, kwa nini wanakwenda tu wanang‟azang‟aza macho hawatuletei huo ujumbe. Sasa hivi Lagos imeshahamia Abuja na kumepangika, kwa nini siyo Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kuzungumza ni makazi ya watu wa kawaida. Ni miaka mingapi sasa, hamsini na ya uhuru bado watu wanaishi kwenye tembe, zile nyumba ambazo tukiwa tunakuja Dodoma tunaziona, bado watu wanaishi kwenye makuti, bado watu wanaishi kwenye nyumba ambazo hata huwezi kujua kama bado tuko Tanzania. Mabati yameshushwa bei watu wajenge nyumba nzuri, haiwezekani, Waziri mhusika anasemaje, anatoa semina lini kwa watu walio vijijini wajue maana ya kuishi katika nyumba bora? Tunataka kuona anatoa semina, watu waishi kwenye nyumba zenye mabati, zenye kuta nzuri na wasaidike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua muda ni mfupi sana na nakosa amani kabisa kwa vile hakika ni mambo mazuri ningetaka kuongea lakini nizungumzie mkoa wangu. Mkoa wa Kilimajaro sasa hivi hatuna tena mahali pa kuishi vihamba vimegawiwa limebakia eneo la makaburi tu. Naomba huyu Waziri wetu kila inapowezekana tuonyeshwe eneo jipya ili vijana wetu wahamie huko sasa wakaweke makazi mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuhusu Dodoma, tulikuja lile Bunge la Tisa tukakuta viwanja vimepangwa ukutani tukajichagulia viwanja, tumepelekwa Itega, mpaka leo kule Itega hawajapeleka maendeleo. Mimi ni mmojawapo ambaye nimeathirika, nilinunua kiwanja shilingi milioni nne lakini nakwendaje kujenga Itega, hakuna juhudi zozote za kuwezesha watu kujenga makazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nizungumzie National Housing. Ni Shirika ambalo limefungua watu macho na hata hapa Dodoma wakaone ghorofa za Medeli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwamba, ametuweka tena hapa kuzungumzia maendeleo ya nchi yetu, hii ni fursa ya pekee kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeze sana Waziri wetu wa Fedha na Mipango. Bajeti hii ni nzuri na imeweka mazingira ambayo yataweza kuwavutia wawekezaji wa nje na ndani, lakini kuna maeneo ambayo yanatakiwa tuyaangalie kwa undani zaidi, nitaongelea kwa hawa wawekezaji wetu wa ndani ambao ni wakulima, wavuvi, wafugaji na wachimbaji wadogo wadogo, kwa sababu hao ndiyo walio karibu zaidi na wale wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu lazima iweke mazingira rafiki kwa watu hawa kuweza kufanya shughuli zao, hawa wakifanya biashara zao vizuri au wakifanya mafanikio katika biashara zao watawezesha wale wananchi wa kawaida ambao wanatumia bidhaa zao wapate chochote ili waweze kukitumia na hivyo basi kwa kutumia vile ambavyo hawa wanazalisha kodi itapatikana na itachangia katika bajeti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ina maeneo mawili, kuna ukusanyaji wa mapato na matumizi ya mapato. Ni muhimu kabisa wote tulio hapa na walio nje waone jinsi gani makusanyo yanafanyika na yanafanikiwa. Mara nyingi makusanyo yakishakuwa kidogo hata matumizi hayapatikani kabisa. Bajeti ya mwaka uliopita, mwaka 2015/2016 tuliona jinsi gani makusanyo yalisuasua na haya yalipelekea matumizi kutokufanyika kwa wakati. Suala hili la wakati ni suala ambalo linafanya mambo yote yanakuwa hayatekelezeki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kabisa ambavyo watu wamekuja kupewa hela miezi miwili kabla au wanapewa hela kipindi ambacho hawawezi kuzitumia tena. Hii inawapelekea wale watu kutumia vibaya kwa ubadhirifu au inaleta mambo mengine ambayo siyo mazuri. Naomba kuanzia sasa tusimamie makusanyo na hapa nipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, tumeona makusanyo ambavyo ni mazuri, tunaambiwa kwa mwezi ni trilioni moja na zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuyasimamie makusanyo hayo na yaende sasa na jinsi bajeti ilivyopangiliwa, makusanyo yaende kama yalivyopangiliwa kwenye matumizi. Wale ambao wanapewa kutumia wasimamiwe, kwa sababu kama hujampa huna cha kumsimamia na wewe sasa huwezi kumuuliza chochote, unamuulizaje na hukumpatia? Naomba hilo liwe angalizo na wote tushirikiane kuona inaendaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia hapa ni kuhusu vijana na wanawake, nikisema vijana ile dhana kwamba kijana ni mtoto wa kiume tu hapana hata mabinti zetu ni vijana, vijana ni ‗ke‘ na ‗me‘ sasa inapokuja kwamba wanafanya shughuli zao mathalani wengi wa vijana wetu wanafanya mambo ya saluni za kike na kiume, lakini pia wana ujasiriamali wa lishe, kuna hawa ambao wanapika na kuna wengine ambao wanatengeneza vitu ambavyo vimekaushwa, kama ndizi za kukausha, popcorn na vitu vingine, yote hiyo ni vitu vya ujasiriamali mdogomdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wanatakiwa wawezeshwe kwenye vifungashio ili wafanye vitu vyao kwa usafi. Nani atakayewawezesha? Ni Serikali iweke mazingira rafiki ya wale ambao wanawapatia vifungashio hivyo vipatikane kwa wingi na kwa urahisi. SIDO ndiyo mahali ambapo vifungashio hivyo vingetoka kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona maeneo ambayo SIDO imetamkwa kwamba itasaidika au itafunguliwa zaidi. Nimeona Mkoa wa Mbeya, nimeona Mkoa wa Pwani lakini sikusikia Kilimanjaro ikitajwa, naomba kwa vile ile SIDO ya Kilimanjaro iko vizuri na vitu hivi vinafanyika, Mheshimiwa Waziri wetu wa Viwanda na Biashara aweke jicho lake kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mengi ya kutaka tushirikiane lakini sasa muda siyo rafiki kwangu; naomba nirudi kwenye jambo moja ambalo naona nisipolisema leo nitaweza nikakosa usingizi, kuhusu Serikali kulipa madeni yake ya ndani. Tulizungumza hapa na wakatueleza ambavyo taasisi zake zinadaiwa na mojawapo ikiwa ni taasisi ya maji inayoitwa MUWSA kule katika Mkoa wa Kilimanjaro. Mamlaka ya maji ile imefinywa sana, wametoa maji katika Chuo cha Polisi (CCP) na maeneo mengine ya Serikali kama Magereza lakini maji yale hayalipiwi. Itamkwe wazi kama Serikali inaona taasisi hizo zitumie maji bure ijulikane!
Mheshimiwa Naibu Spika, napata uchungu, inabidi sasa maji yapandishwe bei na anayeumia kwenye maji zaidi ni mwanamke, mwanamke yule atasaidiwaje! Inawezekanaje taasisi za Serikali zitumie maji bure na zile mamlaka zinajilipa mishahara zenyewe hazitegemei Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena naomba Serikali ilipe madeni yake mapema iwezekenavyo, taasisi zile zifufuke ziweze kununua vitendea kazi kama magari. Tumeambiwa kwamba, kuanzia sasa madeni ya taasisi yatalipwa centrally, naomba Hazina ilipe haya madeni mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu hizi milioni 50 za kila Kijiji. Nauliza, inapozungumziwa hapa kama ndiyo kwanza imeanza inakuwaje? Tulikuwa na hela za uwezeshaji kwa wanawake kuanzia enzi za Mwalimu Nyerere, zikaja mabilioni ya Kikwete, lakini zikishatolewa hivyo hakuna ufatiliaji, nendeni kule kwenye zile benki, achene kuziachia benki zinateseka na pesa ambazo zinawekwa kwenye suspense. Naomba Serikali ikadai kupitia Wizara ya Fedha, hatuanzi kwenye clean plate.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo najua kwamba zile zikipatikana na hizi milioni 50 zitakuwa zimekuwa nyingi tutakuwa tumefungua wigo wa kuwawezesha wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru nisingependa kengele ya pili inigongee. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba kumpongeza sana Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe na Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer Ramo Makani, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na watendaji wote wa Wizara, Wakuu wa Mashirika na Taasisi zote zinazohusiana na Wizara hii. Baada ya pongezi hizo, naomba sasa kueleza yangu machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ni kati ya hifadhi chache zinazoingizia nchi yetu Tanzania pato kubwa sana la fedha za kigeni. Mlima huu unayo theluji kileleni ambayo inapungua siku hadi siku. Haya ni matokeo ya tabia nchi, lakini ukame unachangia sana. Hakuna mashaka kabisa kuwa ukame unaweza kupunguzwa kwa kuotesha miti maeneo yanayozunguka mlima. Jambo hili linawezekana kabisa endapo wanakijiji watapatiwa miche.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali ni lini Serikali itaagiza miche kwa wanavijiji hawa ili waoteshe kwa nguvu zote? Nitapenda kupata majibu wakati Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mgao wa asilimia 25 wa mapato ya mlima kwa Halmashauri zinazozunguka mlima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Rejea ukurasa wa 148 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Barabara ya Marangu – Tarakea, Rongai, Kamwanga - Bomang’ombe – Sanya Juu (kilomita 171); kwenye kila kifungu 259, mwisho wa paragraph; kuhusu kazi nyingine za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kiboriloni – Tsuduni – Kidia (kilomita 10. 8).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua kipaumbele hicho kimetengewa shilingi ngapi na ni lini Ujenzi huo utaanza? Wananchi wanasubiri kwa hamu sana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yaliyo kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kuwa barabara ambazo Mheshimiwa Rais alipokuwa Njombe, alitoa ahadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Moshi Vijijini, barabara ya RAU –Shimbwe juu kilometa 10; Vunjo – Barabara ya Himo – Mandaka, Kilema Maua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukumbushia ahadi hizo naomba pia kukumbushia madeni ya Contractor wa Kichina aliyejenga Barabara ya Dumila – Kilosa ambaye alitulilia sana Kamati ya PAC tulipawatembelea. Kwa umoja wetu tuliona kuwa kusitishwa kwa Ujenzi ni gharama kubwa kwa Serikali. Ref. (Interest accumulation). Ushauri wangu kwa siku za baadaye, tujenge miradi michache na tuimalize kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini si kwa umuhimu, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa Hotuba nzuri na kazi nzuri pia, keep it up engineers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mpango wa uzazi. Rejea hotuba ya Mheshimiwa Waziri Ibara ya 43, ukurasa wa 16, nitanukuu mwisho wa Ibara hiyo: “Wizara kwa kushirikiana na wadau, imetoa mafunzo kwa watoa huduma 3,233 ili kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za aina mbalimbali za uzazi wa mpango. Hadi sasa kiwango cha kutumia uzazi wa mpango kimepanda kutoka asilimia 27 mwaka 2010 hadi asilimia 32 mwaka 2015/2016. Lengo ni kufikia asilimia 45 mwaka 2020.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kasi ni ndogo sana. Ajenda ya mpango wa uzazi inahitaji kupewa kipaumbele kama mkakati sahihi wa kukabiliana na changamoto zetu za maendeleo. Tanzania ina kasi ya asilimia 2.9 ya ongezeko la watu, kasi ambayo ni kubwa. Akinamama wengi huzaa
wastani wa watoto watano. Idadi ya watu inakadiriwa kufikia milioni 65 ifikapo mwaka 2025, miaka nane kutoka sasa. Idadi kubwa ya watu ina matokeo hasi kwa maendeleo, ukuaji wa Miji na maisha ya watu (socio- economic growth); inagusa malengo yetu ya maendeleo endelevu katika sekta karibu zote; elimu, afya, uchumi, kilimo, mazingira na Miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kasi ya kuzaliana ikipungua tutakuwa na rasilimali za kutosha kuboresha elimu na kilimo chetu. Elimu na kilimo ni sekta muhimu kwa nchi yetu, idadi ikipungua, Serikali itaweza kuweka akiba na kuongeza uwekezaji kukuza uchumi wetu, ujenzi wa reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege na kadhalika, zikiwemo shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Wizara hii ipatiwe bajeti ya kutosha kuwezesha Halmashauri kutekeleza mipango ya uzazi (family planning) yenye matokeo. Programme za afya ya mama na mtoto zipewe uzito stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Ummy kwa kuwa na Wizara ambayo ni ya muhimu sana kwa maisha yetu na pia kwa afya zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee katika ule ukurasa wa 16, ibara ya 43 katika hotuba yake, hapa anazungumzia uzazi wa mpango. Ukizungumzia uzazi wa mpango watu wanakimbilia labda kufikiria ni vidonge, ni njiti, ni sindano, sio lazima, kuna uzazi wa mpango wa kuhesabu. Naomba watu waandaliwe katika kuhesabu namna ya kutenganisha watoto miaka mitatu, mitatu ili wawe na watoto ambao wana afya bora toka utotoni wawe watu wazima ambao wana afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalizungumza hili kwa sababu kasi ya kuongezeka Watanzania ni kubwa, ni kubwa zaidi ya maendeleo yetu. Tunapozungumzia watu na maendeleo watu ndiyo wanaotawala na kuendeleza maendeleo. Unakuta kwamba idadi ile inaongezeka kwa kasi kuliko maendeleo yanayopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo sahihi, ninaomba Wizara hii sasa iangalie jinsi gani itaelimisha watu ili tuende tukiongezeka taratibu na hapo nina maana, familia ikiwa na mtoto mmoja, wawili au sana wale waliotangulia kama sisi watatu, inatosha. Yale mambo ya familia kuwa na watoto sita, kumi yamepitwa na wakati. Najua maandiko yanasema zaeni mkaongezeke, lakini tukiongezeka holela pia tunakufa kiholela, ifikapo mwaka 2025 ongezeko hili litakuwa limepitwa kabisa na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde, nimuombe Mheshimiwa Ummy atakapopita mashuleni aende akatoe elimu na pia wale wanaohusika watoe elimu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda watoto na sasa hivi natarajia wajukuu, nawapenda sana wawe wengi, lakini siyo hovyo hovyo tu, nataka vitoto vyenye afya, vitoto vitakavyoweza kukidhi nchi yetu hapo tunapoenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani hao ninaotarajia waelimishwe, ni ile ofisi ya maendeleo ya jamii. Ile ofisi imekaa choka mbaya, ina wasomi wazuri wana degree, wana masters, wengine wana postgraduate, wengine nilikutana nao mashuleni, lakini hawana vitendea kazi kabisa. Ofisi ya maendeleo ya jamii popote ilipo labda kwingine huko miji mikubwa lakini kule kwenye miji midogo midogo hata gari lenyewe la kuwafuata ile jamii wakatoe elimu halipo. Naomba sana Mheshimiwa Ummy, imezungumzwa jana na mimi nasisitiza, ofisi hiyo ipatiwe vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taasisi zetu, likiwemo Kanisa Katoliki, lina Vyuo vya Nursing lakini vyuo hivyo vimekosa walimu wa kutosha na hivyo naomba atakapokuwa anazungumza Mheshimiwa atauangalie ni jinsi gani atatoa pia walimu katika Chuo cha Nursing kule Kibosho, chuo ni kizuri katika Hospitali ya Kibosho, ni chuo ambacho najua nae ana ndoto ya kwenda kukiona, lakini viko vyuo vingi tu na hospitali nyingi tu ambazo hazina Madaktari wa kutosha ikiwemo Bambo kule Same na vituo vingi vya afya. Hata kile kituo cha afya ambacho alikijenga Lucy Lameck, Moshi Vijijini miaka hiyo kiko Shimbwe, kiko mbali sana hakuna hata usafiri wa kufika mjini, bado watu wanabebwa na chekecheke kuletwa mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kukumbushia Hospitali ya KCMC, hospitali hii sasa inataka kusaidiana na Ocean Road, hospitali hii sasa inakwenda kutoa huduma Kaskazini na Mikoa yote inayozunguka katika kutibu kansa. Hili ni eneo ambalo linahitaji gharama kubwa, wadau wamechangia vya kutosha, tunaiomba Serikali iweze kuangalia eneo hilo ili tupunguze ule msongamano pale Ocean Road ili huduma hii ya kansa ya mionzi na nyingineyo ya chemotherapy itolewe vizuri pale KCMC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kila mmoja wetu anapojifikiria anafikiria afya yake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wakurugenzi wote na watendaji wote wanaohusika katika Wizara hii na sekta zote husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri/Naibu Waziri watakapokuja kutoa ufafanuzi, wanijulishe:-

(i) Wananchi wanaozunguka Mlima Kilimanjaro wanafaidikaje na mlima huo?

(ii) Ni lini elimu ya utunzaji wa mazingira itatolewa kwa wananchi hao, hususani wanawake na vijana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tembo wanaogopa sana nyuki, je, Serikali iko tayari kuwagawia mizinga ya nyuki wananchi wanaoishi maeneo yanayovamiwa na tembo ili kuwazuia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza zijengwe hosteli za bei nafuu kwenye mbuga za wanyama ili wananchi wa kawaida na wanafunzi wapate fursa ya kutembelea vivutio hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Zaidi kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na sote tuko hapa tunazungumzia maendeleo ya nchi yetu. Sina budi pia kumpongeza Waziri wa Wizara hii, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa hotuba nzuri waliyotupatia. Shukurani zangu ziende kwa Mheshimiwa Rais kwa kuondoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa ni kero kwa wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilimo kuna mambo manne ambayo ni muhimu, ardhi, unyevu, pembejeo na pia inabidi sasa nguvu kazi iwepo na nguvu kazi ni sisi. Nguvu kazi hiyo ipo katika matabaka mengi lakini nitazungumzia lile la chini ambalo ni wakulima wadogo wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wadogo wadogo nchi hii wanajitahidi sana sana na wengi hapa ni watoto wa wakulima. Tumeona na tumekuwa kwenye kilimo lakini kuna kero ambayo haijawahi kupata ufumbuzi, ni kero ya masoko ya bidhaa zao na nitatoa mfano wa zao moja tu zao la mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu analima mahindi yake ili auze apate hela akafanye shughuli ambayo anataka yeye kulipa ada au kujenga nyumba na mengineyo, lakini siyo wakati wote ndiyo anataka hayo mahindi yafikie mpaka yakomae yakauke. Kwa mfano, mtu anategemea mvua mbili ikimpendeza Mungu, kuna vuli na masika. Wakati wa vuli anaweza akalima mahindi akaamua kuuza mahindi mabichi na mahindi mabichi haya ni mazuri. Katika hekari moja yanapatikana mahindi mabichi kama 45,000 mahindi haya akiuza hindi moja moja Sh.100 anapata Sh.4,500,000 lakini akilingoja hindi hili likakauka akaja kuuza anaweza akapata magunia 15 na labda akawa tu amepata Sh.700,500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililo hapa ni jinsi gani mtu huyu anakereka anapozuiwa kuuza mahindi mabichi. Wengi wenu hapa Waheshimiwa ni wateja au ni watu ambao wanafurahia mahindi wakati wanaelekea Dar es Salaam pale Dumila, Morogoro. Naiomba hii Wizara iwaache wakulima wauze mahindi yao pale ambapo wako tayari. Kwa nini nasema hivi? Wanaambiwa wasiuze, wanawekewa doria na mageti mengi sana halafu unamnyima nguvu kwa sababu yeye anafanya kazi ili aweze kupata kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo kwenye masoko baada ya ombi hilo ambalo najua watalifikiria Mheshimiwa Dkt. Tizeba yeye ni mtu mwenye uelewa mkubwa anaweza akaliwekea mikakati, naomba sasa nirudi pale kwenye kitabu chake kwenye ule ukurasa wake wa 14 na ule wa 110 anapozungumzia mitamba. Watu wengi ni wafugaji na baadhi ni zero grazing. Mifugo ninayoisikia inazungumziwa humu ndani ni yale makundi makubwa ya ng’ombe ya kuswaga. Mimi natoka eneo ambalo halina eneo kubwa, tunafuga ng’ombe mmoja, wawili lakini tunafuga kisayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri hii mitamba sasa tupatiwe kule Kilimanjaro tuweze kufuga kisasa. Mitamba hii ikishakuwepo ndani ya nyumba inatupatia mbolea, mbolea hii ndiyo inakuwa kwa ajili ya migomba na kahawa. Hiyo inakuwa kama mgonjwa na uji, migomba mizuri isipopata samadi haiendi. Kwa hiyo, naomba awamu hiyo inayokuja au popote anapoweza kunisaidia niweze kuwapelekea wale wanawake wangu wa Kilimanjaro wafuge kisasa na pia tupate maziwa tutakayopeleka kwenye viwanda, maziwa toshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nienda haraka haraka kwenye ufugaji wa nyuki. Mimi mpaka sasa hivi ukiniuliza nyuki ziko kwenye Misitu au Kilimo sijui lakini naomba leo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai na leo hii tunaweza kujadili bajeti hii ya mwaka 2017/2018. Pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuonesha azma yake ya kuwa muumini mzuri wa elimu na kupata Ph.D yake akiwa kwenye lile Bunge la Tisa kama Waziri. Pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio changu ni tumrudishie mwalimu heshima yake. Madeni ya walimu yalipwe, walimu wapewe motisha, walimu wapatiwe vifaa vya kufundishia, walimu wapatiwe/wajengewe nyumba za kuishi hasa vijijini, walimu wapandishwe madaraja kwa wakati, walimu waruhusiwe kujiendeleza na kadhalika. Kwa kuwa walimu ndio wanaofundisha fani zote, mishahara yao iboreshwe. Ualimu ni wito utunukiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya kufundishia iwe kiingereza kuanzia shule ya msingi ili tuweze kuingia kwenye soko la ajira la Afrika ya Mashariki (East Africa) na kwingineko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni mazingira duni ya kujifunzia yanayosababishwa na miundombinu katika maeneo husika kama maji, umeme, vyoo pamoja maabara. Ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kumaliza zoezi la madawati, lakini nalo limezaa tatizo la madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali Kuu isiziachie Halmashauri tatizo hili kwani si sahihi sana hasa ukizingatia kuwa uwezo wao ni mdogo na mambo ya kutekeleza ni mengi sana kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu bila malipo, juhudi za Serikali kutoa elimu bila malipo kwa watoto wote zinaendelea na mimi ninaziunga mkono na kuzipongeza sana. Wadau wa elimu na jamii wanazo hoja kuhusu ubora wa elimu wanayopata watoto, mjadala huu ni wetu sote. Ni jambo jema hasa tunapoelekea awamu ya nne ya mapinduzi ya viwanda inayoitwa exponential age.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha elimu hii inabidi wadau wote washiriki kikamilifu na kwa uaminifu mkubwa. Aidha, ninaomba Serikali itoe hela za kutosha kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mpango, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo kwa hakika naona hata hii siku moja mliyotupa haitoshi kabisa, ingefaa kila mtu hapa akapata muda wa kuchangia kwa sababu ni fupi na inaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye ukurasa ule wa 47 unaozungumzia huduma za kibenki, naanzia pale kwenye ukurasa wa 44 na nitakwenda moja kwa moja kwenye mikopo. Kuna riba inayotozwa kwa anayekopa lakini kuna riba anayopewa yule anayeweka. Wanakwenda kuwekeza kwenye savings au kwenye FDR na hizo hela zinakopeshwa sasa ile riba imetofautiana sana, anaekopeshwa analipa asilimia 17, huyu ambaye ameweka analipwa asilimia mbili mpaka tatu ndiyo inafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kuna haja gani mtu apeleke hela yake benki akaweke kama analipwa kidogo hivyo? Mbaya zaidi kuna yale makato ya service charges. Ukienda kwa mwaka kama mtu ameweka laki moja yake na hakuweza kuongezea unakuta yote imekatwa kwenye service na hakuna kitu anachopata, maana yake ni nini? Namuomba Waziri wetu aangalie jambo hili, akae na hizo benki husika ili waweze kuona tatizo hili kwamba limekuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile mikopo kuna ile mikopo ya wafanyabiashara na kuna mikopo ya wafanyakazi. Hii mikopo ya wafanyakazi haina matatizo kufuatilia, yeye anafanya kazi pale au hata kama ni Mbunge upo hapa mkopo wako utalipika tu na hata nikiondoka leo bado yale mapato yangu yatalipa ule mkopo. Kwa nini tunatozwa kiwango kinacholingana na wale wafanyabiashara? Mfanyakazi anatakiwa atozwe kidogo zaidi na isipishane zaidi na ile ya kuwekeza, ningeomba kufahamu jambo hili siyo haki kabisa. Mikopo hiyo ina bima, ufuatiliaji ni mdogo kwa kweli naona wakati sasa ufike, Waziri akae mezani na haya mabenki waone ni jinsi gani wanarekebisha jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo la mabenki, niende katika ukurasa wa 17 ule utaratibu au mikakati ya kupunguza umaskini. Napongeza hatua ya Wizara hii kutoa mafunzo kwa wataalam, lakini katika kutoa mafunzo kwa wataalam sikuona Wizara imejipanga kutoa mafunzo kwa wale ambao ndiyo wanaonufaika na elimu hii inakuaje? Mnatuelimishia wataalam, lakini hamkupanga fungu la kuelimisha wale ambao ni wanufaika, sioni kama hapo tutapiga hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri sasa aangalie wataalam hao wakishaelimika pia aweke fungu ambalo wataelimishwa wajasiriamali wadogo wadogo, wale wa VICOBA, watu wote ambao wanataka kuingia kwenye biashara ili waweze kunufaika na hii elimu ambayo wamepatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 34 naomba nizungumzie kidogo kuhusu ukaguzi wa hesabu za Serikali. CAG anakwenda kwenye ukaguzi lakini tumeona kabisa na tumeelezwa hela ya kumuwezesha CAG ni kidogo japo kwa kipindi kilichotajwa ameweza kupatiwa, lakini tunaomba CAG afikiriwe, tumemuombea bajeti iliyopita na sasa tena tunamuombea kwa sababu tulienda tukaona kuwa hakuweza kutembelea maeneo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 35, kuhusu usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma. Naona hapa wameeleza vizuri usimamizi unavyokuwa lakini nauliza kwamba, Serikali ilikuwa na hisa kwenye mashirika mengi tu lakini hatukuorodheshewa hadi sasa imekidhi asilimia ngapi kwenye mashirika kadhaa na ufuatiliaji wake ukoje. Mashirika mengi yalikuwa mikononi mwa Serikali, mengine sasa yamekwenda private, mengine hayapo tena kabisa na Serikali. Je, Serikali imefuatilia hisa zake kwa yale mashirika yote? Hapa tunapata wasiwasi. Mimi nipo kwenye Kamati ya PAC na tuliona kwamba kuna maeneo ambayo Serikali imesahau hata hisa zake. Nilikuwa naomba sana Wizara ifuatilie ili iweze kujua imewekeza wapi na inalipwa kwa jinsi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika currency yetu, hela yetu hizi noti. Coins hazina tatizo japo zote zinaitwa noti nacoins, naomba Wizara izungumze na Benki Kuu itoe elimu ya kufanya utunzaji wa noti.Kamati yangu ilipata nafasi ya kwenda kutembelea Benki Kuu tukaona jinsi ambavyonoti hizo sasa inafikia mahali wana-thread, wanaondoa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni gharama sana ku-thread ni bora tungekuwa na notiambayo ingeweza kudumu, amezungumza mzungumzaji mmoja kabla yangu lakini mimi nataka niende mbali zaidi. Utunzaji wa notie unatakiwa uwe kwenye akili ya mtu it is a mindset.Mtu anaichukua noti yake vizuri, anaweka kwenye wallet, lakini Watanzania wengi anachukuanoti yake anafunga kwenye kitambaa, anasokomeza anakosokomeza. Hiyo noti hata ingekuwa ya gharama namna gani lazima itachakaa. Naomba Serikali ione umuhimu wa kuelimisha watoto toka wakiwa wadogo namna ya kutunza hela, namna ya kuthamini noti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda nchi za nje unakuta dola siku zote imenyooshwa wanashangaa wakija Tanzania dola inakunjwa, wakija Tanzania pound inakunjwa, hela haikunjwi ndugu zangu, ukitunza hela inakutembelea. Weka notiyako kwenye wallet, hela ipendeze na hiyo hela itadumu na mfukoni itaenea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie umuhimu wa kuona kwamba imefikia wakati yeyote anayetaka kujaribu biashara kabla hajaingia kwenye biashara aingie katika elimu au ataelimishwa na wale wanaomhusu au atakwenda kupata mafunzo. Tuna vyuo vyetu vingi tu kimojawapo ninachokifahamu kwa undani sana ni Chuo cha Ushirika (Moshi Cooperative University).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna wakati wanafunga shule, wakifunga chuo nilikuwa naomba Waziri akiweza kutukutanisha akatupa semina kama Wabunge wake na tukianza kwenda kukutana na wale tunaowasimamia wapate elimu katika vyuo hivyo na sisi wenyewe pia tutachangia gharama za kuelimisha watu hawa. Tukielimika kutakuwa hamna tatizo, tutakuwa na Waziri wetu mzuri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri mzuri na wote tutazungumzia maendeleo, sioni kwamba saa zote tukikaa tulaumu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, makusanyo yanatosha kutuambia tupongeze, naomba nichukue nafasi hii kupongeza sana Wizara hii kwa makusanyo yaliyopatikana na pia nipongeze Wizara hii kwa jinsi ambavyo imejitahidi kulipa deni la Serikali, hatuwezi kudaiwa kila siku, dawa ya deni ni kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kipekee kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai aliyotupa sisi sote hapa. Nawashukuru sana wanawake wa Kilimanjaro walionituma kuwawakilisha huku Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Niseme hakika wote katika Wizara yake akiwepo Waziri wetu wa Nchi, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Makatibu Wakuu na Naibu Waziri wote wametutendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie kwenye ule ukurasa wa 14, uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Imerodheshwa pale takribaini Mifuko mitano lakini tunaambiwa jumla programu na Mifuko mingine iko 31 ambayo inawezesha wananchi kwa kutoa mikopo. Hoja yangu ni kwamba, wananchi hao wanaopewa mikopo wakiwemo vijana, wanawake, wajasiriamali hawana elimu ya kukopa. Japo wanapewa hizi hela kwa mkopo lakini elimu yao ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana niliomba elimu kwa wananchi hawa wakiwemo wanawake wa Kilimanjaro na bahati zuri sana tuna Chuo Kikuu cha Ushirika, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ione sasa ni wakati wa kuzungumza na chuo au na vyuo vinginevyo wakatoa elimu ya kukopa kwa wanawake au wajasiriamali wale wakati vijana wale wa chuo wanakwenda field. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna sababu mikopo inatolewa halafu hairejeshwi. Kuna mifuko ambayo mpaka sasa ikiwemo mfuko uliotoa mabilioni ya JK, hela zile hazikurudi na zile ni revolving funds, zimefika mahali zimekwama, hakuna ufuatiliaji. Niombe Kiti chako na nimuombe Mheshimiwa Spika imefika wakati sasa huku ndani iundwe Tume kufuatilia zile hela za revolving zimefia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nizungumzie usalama wa chakula. Bahati nzuri sana mvua zilizonyesha mwaka uliopita zilikuwa nzuri, chakula kimekuwepo, lakini uhifadhi wa chakula hiki siyo mzuri, wananchi wetu hawana maghala ya kuhifadhi chakula. Tunaambiwa kwamba ifikapo 2025 tutakuwa takribani Watanzania milioni 70 lakini tumejiandaa vipi kuzalisha chakula ambacho tunaweza kutumia na kingine tukahifadhi ili kulisha wananchi wetu? Niombe Wizara ya Kilimo iliangalie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye mifugo. Wananchi wengi wa Tanzania ni wafugaji lakini mifugo mingi ni ile ya kiasili (indigenous) hakuna kuboreshwa kwa mifugo hiyo. Mwaka jana tuliambiwa kwamba Serikali itasaidia mitamba bora na mitamba hii inaweza ikasambazwa kwa wafugaji wa hali ya chini. Naomba kujua mpaka leo tokea mwaka jana ni mitamba mingapi imetolewa kwa wafugaji hao ili tujue imeboreshwa kwa kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo ni mizuri lakini inapozagaa hovyo siyo mizuri kwa sababu inaharibu mazingira. Niipongeze pia Wizara ya Mifugo, Waziri aliyepo madarakani ameweza kudhibiti hilo na mpaka sasa hivi tumesikia migogoro kidogo sana kuhusu wafugaji. Naomba nimpongeze Waziri na Naibu Waziri wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie ujenzi wa viwanda. Kwa kweli tumepewa taarifa kwamba viwanda ni vingi na vinaendelea kuwepo lakini niseme kwamba tunapokwenda kwenye viwanda tuangalie pia teknolojia inayotumika. Sasa hivi imekuwa ngumu kufufua vile viwanda kama Machine Tools, Kiwanda cha Tanzania Bag kule Moshi kwa sababu ya teknolojia iliyokuwa imetumika huko nyuma haikuweza sasa kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana vile viwanda vya Kilimanjaro vifufuliwe na pia vinapokwenda kufufuliwa na kujengwa vipya tutumie sasa teknolojia ambayo ni ya kisasa zaidi. Ni wazi kwamba viwanda vile vinatoa ajira, Kilimanjaro wengi sana walikuwa wanategemea ajira hizo, vijana wetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ninawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote. Nitazungumzia maeneo mawili tu, kwanza utunzaji wa vyanzo vya maji na uvunaji wa maji ya mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasisitiza Serikali izidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, narejea kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji ukurasa wa 16, Ibara ya 34 naomba kunukuu; “Wizara imeendelea kuvitambua, kuviwekea mipaka na kuvitangaza vyanzo vya maji kuwa maeneo tengefu ili kuvilinda na kuvihifadhi kwa ajili ya kuzuia uharibifu na uchafuzi wa vyanzo hivyo.” Ombi langu ni kwamba hata vile vyanzo vya maji vya mamlaka mbalimbali vipatiwe hati miliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kasi ya uvunaji wa maji ya mvua bado iko chini kabisa, kwa masikitio makubwa sikuona kabisa msisitizo wa jambo hili kwenye hotuba. Ninaomba kujua Serikali ina mpango gani wa kunufaika na maji yanayotiririka hovyo na kupotelea baharini wakati wa mvua. Mfano, barabara ya Dar es Salaam - Dodoma eneo la Kibaigwa pande zote mbili maji yanatua na wakati mwingine yaliua, lakini hakuna juhudi za kuyatumia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninakukumbusha mradi wa maji wa Nyumba ya Mungu - Mwanga, Same, Mombo, ni lini hasa utamalizika?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa kuwepo sisi hapa salama na tuko katika mambo haya ya maendeleo. Nawashukuru wale wanawake wa Kilimanjaro walioniwezesha kufika hapa na leo nazungumzia jambo la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu haina mwisho naamini hata Wabunge walioko hapa bado wanajisomesha, bado wanajiendeleza, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Profesa Ndalichako na wote ambao wameshiriki katika kuandaa hotuba hii ya bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja katika ule ukurasa wetu wa 62 mpaka ukurasa wa 64 wanapozungumzia EP4R. Nimeona wanafanya maandiko tofauti wanapata hela za kutosha wanakarabati majengo, wafadhili wanaenzi shughuli zao. Ombi langu na naomba hata ninyi Wabunge ikiwapendeza iletwe hapa tuazimie hela hizo zisimamiwe na Wizara hii ya Elimu zisiende tena kule TAMISEMI, kwa sababu kama zinapatika na zimekuja na sasa zinafanya jambo la elimu na wengi mmekwenda kutembea mmeona ukarabati hata wa zile shule za zamani kwa nini sasa zinakwenda TAMISEMI, hapo bado inanikanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa ombi hilo na pongezi hizo kwa Mheshimiwa ninampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la awali mpaka kufikia form four hili ni jambo jema na wazazi wengi wamependa, sasa hakuna sababu ya mtoto yoyote asiende shule. Baada ya elimu hiyo nini kinachoendelea, mwanafunzi akishafunguliwa mlango wa kusoma nawaomba na nawapongeza wanafunzi wote walio mashuleni leo na hata siku za baadae nawapongeza sana kwa kupiga vita ujinga, nawapongeza sana na nawaambia elimu yenyewe ni vita.

Niwaombe tu sasa ukishamaliza form four usibweteke kwamba wewe ni graduate ukae tu, endelea kujiendeleza. Nasema hivyo kwa sababu hata yule graduate aliyemaliza Chuo Kikuu ajira zimekuwa ni shida, kila siku Wabunge wanapigiwa simu wanaombwa wawatafutie kazi, kazi hazipo! Tatizo tu siyo kazi kutokuwepo nadhani hata Walimu na wazazi tunakosea mahali pa kumjenga mwanafunzi au mtoto achukue taaluma gani ambayo mbeleni itamfungua zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani tunasema sayansi, je wewe mzazi unamsisitizia mtoto wako hata kujifunza kuhesabu, kwa sababu msingi wa sayansi ni hesabu. Nawaomba wazazi wote sasa wawe wanapitia vitabu vya wanafunzi wao au watoto wao wajue kwamba wanafunzi hawa wanasoma wanavyotakiwa. Huko mbele tunaona wazi kuna ajira ambazo hazitahitaji tena wafanyakazi, kuna ajira ambazo zinajifuta kwa sababu sayansi sasa imeshafunguka. Kuna fani ambazo sasa hivi zinafanywa na roboti, zinafanywa na mashine, mtu mmoja anakaa anaendesha kiwanda kikubwa, hatuhitaji tena wale mashine operator wengi ni kwa nini sasa wazazi, walimu, wasimwambie mtoto achana kiasi na haya masomo ya sanaa nenda kwenye masomo ya sayansi ambako baadae unaweza kuwa na ajira unayotaka wewe kuingia kwenye payroll.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kabisa kwamba tulianza kujenga maabara lakini imefika mahali inasuasua, naomba ule mpango wa kujenga maabara uendelezwe. Pia kuwa na maabara bila walimu wa kufundisha sayansi haisaidii, kuna wakati ambapo wazazi tulikuwa tunachangia wale walimu wa sayansi kwa kipindi, ikafika mahali likatoka Toleo la 16 la mwaka 2015 michango isifanyike tena, sasa wale walimu temporary wa kufundisha sayansi mashuleni hawapo tena, nataka ufafanuzi kutoka Serikalini endapo wale walimu hawatakuwepo wale wanafunzi waliopo shuleni sasa hivi watafundishwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona kabisa kwenye maabara tunazungumza kupata walimu wa sayansi, naomba pamoja na walimu wa sayansi tuna wale lab. technician ambao wanafanya maandalizi ya vifaa vya experiment. Naomba wafikiriwe ajira zao ziongezwe tunahitaji lab. technicians ambao wana uzoefu au hata kama ni wageni, lakini wawepo kila lab inalojengwa lipate lab. technicians wawili, kama ni la sayansi labda la physics, chemistry au biology tupate angalau wawili kwa shule moja. Haielezeki tuwe na labs lakini hazina technicians unamtarajia mwalimu huyo aandae vifaa vya experiment mwalimu huyo aje sasa awafanyie vijana hao experiment. Kwa hiyo, hii ajira ya lab. technians naomba sana ifunguke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa kwenye suala tunalosema kwamba Walimu wetu hawapati stahiki wanazostahili. Tumeona Serikali imejitahidi, lakini kuna wale walimu ambao kwa kweli wanafanya masomo ambayo yanasababisha wao wakae vipindi zaidi pale shuleni. Naomba hawa walipwe hardship allowance. Mwalimu siku zote alikuwa mtu wa maana sana, mwalimu alikuwa akipita anaheshimika, anasalimiwa kwa heshima, nyumba yenye heshima ni nyumba ya mwalimu, lakini sasa hivi walimu wengi wamedhalilika ile heshima imekwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeona labda irudishe walimu wengine wa sekondari kwenda primary wenzangu wamezungumza, tunaomba wale walimu wa sekondari wanaokwenda primary waandaliwe pia, kwa sababu mwanafunzi akishapata msingi mzuri kama tunavyosema tu nyumba nzuri ni msingi, mwanafunzi akianza hapa chini basi akienda huko juu ameshajiimarisha na ameshajitambua. Naomba sana tuwaanzishie wanafunzi hawa msingi mzuri ili huko wanakoenda sasa waweze kwenda kufanyakazi wakiwa wanajua wanafanya nini. Siku zote elimu haina mwisho, hata wale ambao wameshamaliza Masters wanakwenda kwenye ajira lakini pia wananyanyasika labda kwa vile hawana uzoefu. Naomba ule muda wa kwenda kufanya field iweze kuandikwa kwenye vyeti vyao kwamba amefanya field mahali fulani na amekuwa na ufaulu wa kiasi fulani. Kwa sababu mwanafunzi anapokuja kua-apply kazi kwa mara ya kwanza, swali linakuja ana uzoefu ama experience gani?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kipekee namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai ambapo sasa wote tuko hapa tukizungumzia Jeshi letu, lakini zaidi sana nawaombea na naliombea Jeshi hilo lizidi kupata nguvu na kutulinda kama linavyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa na chombo makini kama Jeshi hili. Nampongeza CDF na pia nawapongeza wale wote waliomuunga mkono ambao ni wastaafu akiwemo Major General Mboma, Major General Waitara na Major General Mwamunyange. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri leo ametuletea hapa hotuba ambayo ni fupi, inaeleweka na inakubalika, naomba nimpongeze sana Waziri wetu, nimpongeze Katibu Mkuu na timu yake yote walioandaa kitabu hiki, nimeshakisoma kama mara tatu, pamoja na ile ya Kamati. Niseme wazi kwamba mimi niko kwenye Kamati hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumepata elimu siyo tu kwamba wametoa kuomba fedha lakini tumepata pia kama semina. Sasa ninachoomba hapa, kama walivyosema pia wa upande mwingine hela hizi wapewe zote na hata kama nyingine waliogopa basi waongezewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la kwanza; Serikali iwalipie wanajeshi hawa bili yao ya umeme na maji wanayodaiwa kwenye vyombo vingine kama vile taasisi za maji na umeme, TANESCO. Inakuwa fedheha Jeshi linapodaiwa vitu vidogovidogo ya nini? Kule hawathubutu kuwakatia, ile lugha haitembei pale kwa sababu wao wakitugeuzia kipande raia hatuna hamu. Naomba namna gani ya kulipa hayo madeni ifikiriwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukrani zangu kwa Jeshi hili kuwa wakarimu kwa ile Hospitali ya Lugalo. Kwa kweli hawatibiwi wenyewe tu hata sisi wananchi ikizidi sana wanatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo halinipi amani ni ajira za Jeshi kwa Jinsia ya Kike ni pungufu. Leo tumewaona walivyopendeza huko nje, walivyo nadhifu, na imara, lakini ukiangalia wanawake ni wangapi, sikuona, nimemwona tu raia mmoja wa Jeshi kule. Naomba wanavyotoa ajira mpya wanawake wafikiriwe, inapendeza. Mbona nchi nyingine zina Wanajeshi wa ngazi ya juu wanawake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT inalitoa Jeshi kimasomaso. Waliwahi kupewa tenda ya kutengeneza madawati, walitengeneza kwa wakati na madawati yakapatikana kwa ile hela iliyokuwa imerejeshwa. Wamepewa kutengeneza ule ukuta wa Mererani, wamefanya kwa wakati. Naomba taasisi zote zitoe kazi kwa JKT, ikianzia Bunge kwa hivi viti tunavyokalia. Wanatumia mbao nzuri, wanatumia mninga na pia wanatumia soft. Pia na ninyi ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, naomba zile furniture zenu mnazoagiza za kuishi Dodoma muwape JKT wawatengenezee na watawaletea kwenye milango yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tunapowafikiria mafao yao wanapata kwa wakati, lakini zile pensheni haziji kwa wakati na pensheni ni kitu ambacho mtu anatakiwa akipate baada ya jasho jingi na kazi ngumu na kukung’uta saluti nyingi sana nao wafurahie sasa. Naomba wafikiriwe sana wale viongozi wapatiwe zile pesheni zao waweze kuzifaidi kabla hawajazeeka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba pia Wanajeshi ambao ni wanamichezo waweze kupatiwa ruhusa kwenda kwenye michezo au kwenda kwenye mashindano kama yale ya Kili Marathon, tumeona mara nyingi wanakuja Wakenya wanachukua zawadi nyingi Kili Marathon ni International Marathon ikikaribia Kili Marathoni ule Mji wa Moshi unakuwa Wazungu tu, watu kutoka nje. Yanapofika yale mashindano hakuna Mtanzania anayesogea hata nafasi ya tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Jeshini tuna vijana ambao wana uwezo, naomba ikiwepo Kilimanjaro Marathon, ikiwepo Tulia Marathon, ikiwepo KIA Marathon Wanajeshi wetu wajiandae kuja kushiriki kwenye marathon hizo wachukue hizo zawadi, sioni kama kuna tatizo, wanajeshi wana uwezo mkubwa sana wamekuwa wakishinda sana wanajeshi kwenye netball najua kabisa kuwa hata hiyo wataweza na watashinda na watachukua zawadi nyingi ambazo zitatupa heshima kila mahali na pia watatutangaza nchi yetu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Jeshi kwa kutoa demo wakati wa sherehe za Uhuru, wakati wa sherehe za Muungano, tumeona tukioneshwa vyombo vyetu vifaru, tumeona tukioneshwa vyombo vyetu vya vita, tumeona tukionesha makomandoo walivyo na uwezo. Kwa kweli vijana wanasema hakuna Jeshi kama hili, siyo vijana wa nchi hii tu hata nje ya nchi hii tunajua Jeshi hili lina nguvu. Tunaomba waendee na pia waendelee kuwa kivutio kwa vijana kujiunga na Jeshi, vijana wetu wengi wanapenda kuwa Wanajeshi lakini wanakuwa na hofu ila wakiwaona katika kufanya vile vitu vyao vile vizuri zuri vile, wanasema na mimi siku moja nitakuwa Mwanajeshi na nina hakika watafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wanapofanya miradi yao waombe na hela za kukarabati miradi hiyo. Nitatoa mfano wa mradi mmoja, juzi wamejenga ukuta wa Mererani, ukuta ule japo umekabidhiwa lakini watatakiwa wauone kwamba ukuta ule unabakia kuwa imara siku zote. Sioni bajeti yoyote ya kusema kwamba hii ni ya ukarabati wa ukuta wa Mererani hakuna kitu kinachoishi maisha kama hakitunzwi. Kwa hiyo, naomba watakapoleta bajeti yao ya mwakani waombe na hilo fungu la kukarabati lile eneo la Mererani ili sifa zao ziweze kubakia na uimara wake uweze kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabla sijamalizia nisije nikasahau kuunga hii hoja mkono, hii kwangu ni hoja muhimu sana. Niliwahi kupitia huko Jeshini kwa mujibu na nilikuwa kwenye ile operesheni aliyokuwa Almasi, operesheni Kagera na namba yangu ni K7078 mimi Mwanajeshi tukiitwa leo ni vita imetokea mimi Frontier Soldier hata kwa umri huu. Tulikuwa na wimbo mmoja unasema “hilo Jeshi mambo yake, vitendo vyake sawasawa” na leo mmeona nadhani kila mmoja leo alikuwa na amani kuwa na Jeshi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe tu ndugu zangu huo mshahara wa Waziri yoyote akayesisima nadhani atakuwa yeye anasumbuka sana. Tunaomba tuwapatie na iwe ni ya mfano kwamba hakuna usumbufu. Niishie kwa kuwaomba sana wao Wanajeshi wetu waendelee kutulinda tunawapenda, tunawaheshimu, tunawafurahia na kila wakati tunawaombea kwa Mungu na kila wakati tunaamini kwamba wakiwepo hakuna mtu anayethubutu kuleta usumbufu wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa kutupa sisi sote zawadi ya uhai, tupo hapa tunazungumza mambo ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupongeza tena na niungane na mwenzangu aliyetangulia kwa wewe jana kupokea ripoti zile mbili na kuzikabidhi Serikalini, Ripoti ya Natural Gas na ile Ripoti ya Uvuvi. Tumeona kazi yako na nia yako njema katika kudhibiti mianya yote ambayo inatupotezea mapato katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na niipongeze hotuba yake ambayo kwa kweli imeandikwa vizuri na tumeielewa na ndiyo maana unaona mijadala yote iko moto.

Mheshimiwa Spika, kabla sijasimama nilipokuwa najiandaa ilinilazimu kwenda kule Library nikachukua Hansard ya mwaka 2017 ambayo pia wenzetu walikuwa wamechangia. Niseme wazi kwamba nimei-miss michango yao na sijui kwa nini mpaka leo hatupati michango ya upande wa pili? Kwa nini nimevutiwa kwenda kuchukua michango yao? Nilitaka kuona mambo waliyoyazungumzia mwaka 2017 leo yameendaje? Mengi waliyokuwa wamelalamikiwa yametekelezeka na lazima niseme wazi kwamba Mheshimiwa Waziri Mpango mambo yako yako vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha ni moyo wa uchumi na ndiyo maana wote wanaozungumza wanaipiga mawe, lakini tunasahau kwamba kuna mambo mazuri yamefanyika hapa katikati. Mwaka 2017 kipindi kama hiki kila mtu alikuwa analalamika bei juu, walio kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani vyakula viko juu, sukari hakuna, mahindi hakuna, mchele ghali; lakini leo kila mtu amekaa raha mustarehe. Kila kitu kinapatikana, Mwenyezi Mungu amesikia kilio chetu, uji upo, mchele upo na sukari ipo. Mambo hayo yote wanadamu tumezoea kila siku kulalamika; hata mambo mazuri hamwoni sasa? Hata mvua zilizokuja hamzioni? Hata watu wanafuturu vizuri, wakiwepo na Waheshimiwa Wabunge wanafuturishwa kila leo, hawaoni? Bado wanalalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu akiwa na hulka ya kulalamika, hakuna namna unavyoweza kumbadilisha, lakini namshukuru Mungu mfungo huu umekuwa mzuri. Niseme kwamba na hiyo iweze kumpa pia, ahueni huyu Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niende katika ule ukurasa wa 87 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri unaozungumzia uratibu wa mikakati ya kupunguza umasikini. Nilipokwenda Library nilichukua pia kitabu cha Wizara hiyo cha mwaka 2017, kama hiki na nikaenda ukurasa huo huo katika uratibu wa mikakati ya kupunguza umaskini. Kilichozungumzwa mwaka 2017, mwaka jana ilikuwa ukurasa wa 76 mwaka huu ni 87, hayapishani sana. Ni mambo mazuri ndiyo, lakini yote ni kwenye makaratasi.

Mheshimiwa Spika, mwananchi wa kawaida ukimwambia unapunguziwa umaskini kwa kuzidi kuboresha au kuandika maandiko ya SDGs, maandiko ya Poverty Monitoring System, tunazidi kuboresha mifumo, tunazidi kuboresha, haimuingii akilini. Nami pia niliyetumwa hapa na wanawake wa Kilimanjaro wanaonisubiri waone tumepiga hatua kwenye kupunguza umaskini, naomba kutamka kwamba sielewi. Ni kwa nini sasa sielewi?

Mheshimiwa Spika, nilitaraji sasa baada ya wasomi kuangalia hizo SDGs waje na pendekezo au waje na maagizo kwa Serikali; jamani, tumeamua kupunguza umaskini, tunaomba au tunaagiza sasa tupeleke projects ambazo wananchi watazisimamia na wanawake walio hapa wengi ni Viti Maalum, wanajua ambavyo wanaombwa kule kwenye maeneo yao semina ya kujifunza ujasiriamali, semina za kuboresha maeneo, za mazingira, semina za ufugaji, l akini wanafuga nini? Hakuna mifugo iliyoboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri wangu wa Fedha akatuzungumzie kunakopatikana mitamba bora, wanawake wakopeshwe. Miaka ya nyuma Mwalimu Nyerere peke yake katika awamu zote aliweza kutoa projects ambazo zinafanya kazi watu wakarejesha. Ilikuwa inaitwa kopa ng’ombe lipa ndama; na mpaka leo ndiyo iliyowatoa watu. Watu waliweza kuboresha maisha yao, wanapata maziwa, wanapata samadi, wanapata nyama nzuri na ngozi.

Mheshimiwa Spika, ni Mwalimu tu katika awamu zote tano, yeye alitoa projects na zikalipa mpaka leo. Ndiyo akaweza kuchanganya wale ng’ombe wa kiasilia na ng’ombe wa kisasa. Maeneo mengi yaliyoboresha kipato ni yale ambayo yaliweza kufaidi mradi huo. Namwomba Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango aangalie ni projects zipi zitaweza kwenda kuboresha kipato cha akinamama?

Mheshimiwa Spika, tumeona wanawake wanaingia kwenye VICOBA, Serikali inasema kwamba inakwenda kusimamia VICOBA, mnasimamiaje VICOBA ambavyo hamjui vimeanzishwaje? VICOBA hivyo ni vya kudunduliza, amechangia mmoja akasema na ile hela ya VICOBA sasa inakwenda kwenye kucheza kamari. Tunafanyaje? Tunatokaje hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba wanawake hawa wapewe elimu ya VICOBA kila mara. Hapa wenyewe sisi, wengi wa Wabunge wako ni wasomi, lakini kila leo umejitahidi kutuletea semina za mambo mbalimbali ili tuweze kuendana na wakati. Sasa wanawake wale tunawapelekeaje semina hizo? Haitoshi kabisa kuzungumzia vitu vyao walivyoanza halafu tukasema tunasimamia SACCOS. Unasikia Serikali inaingia kwenye SACCOS. SACCOS ni uanzishaji wa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba Serikali imeweza kwenda kuangalia wasiuze zile mali za SACCOS, lakini uanzishwaji wa SACCOS ni wa hiari. Wenyewe wanakaa wanakubaliana. Maeneo ambayo SACCOS zimeshamiri ni kule ambako hazijaingiliwa. Leo Serikali ukienda ukaingilia, umeharibu.

Mheshimiwa Spika, nakuomba, dakika chache zilizopita umesimama umetoa amri. Najua, amri yako au your wish ni kutekelezwa na ikitekelezwa kwenye hili jumba lako Tukufu wewe ndio umesema. Naomba siku moja ikupendeze, zile hela zinazotolewa au zilizowahi kutolewa na Marais siku za nyuma zikaenda kwa wanawake, zikaenda kukopeshwa, halafu zikaishia ziliko, mimi najua ziko kwenye benki kwenye suspense accounts. Tuma Tume yako fedha hizo zikakaguliwe, iwe ni NMB, iwe ni NBC, iwe ni CRDB, zile hela zirudi kwenye mzunguko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zile hela ni revolving funds, zirudi. Hazina inajua ni kiasi gani kilitoka. Mara ya mwisho tulipata mabilioni ya JK, mpaka leo yako wapi? Waliojifurahisha wameyafungia, zime-lock mahali. Utashangaa hata viongozi wakubwa au wake wa viongozi walienda na wao wakakopeshwa. Hivi walikuwa wanastahili hizo hela? Nakuomba, siku itakapokupendeza zile hela zirudi kwenye mzunguko, wanawake wakopeshwe, vijana wakopeshwe hela hiyo ikombolewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye ripoti tumeelezwa wazi ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, hili ni jambo jema. Naomba ubia huu usimamiwe na Serikali sasa iwe makini kuangalia ni jinsi gani ubia huu unaendeshwa. Tuna bahati moja nzuri sana ya kupata Wakaguzi wa Serikali ambao ni makini, ambapo tulikuwa huko nyuma na Uttoh, sasa hivi tuna Profesa Assad. Ukiona ripoti zake, ziko wazi, hakuna anapoficha. Pamoja na madaraka yake hayo makubwa, nafasi yake amepewa; tukitaka sasa kujua value for money kwenye projects inashindikana maana naona wataalam hawa hawapo.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi ameagizwa, lakini amepewa majukumu na amefungwa mikono, hana namna ya kuajiri watu ambao wana uelewa kwenye eneo hilo. Sasa inamwia ngumu. Tunamhoji tunasema, aah, umemaliza ukaguzi sasa tunataka tuwe tena na ukaguzi ule mahususi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hii nafasi na naungana na waliozungumza asubuhi na maombi aliyotoa jirani yangu Mheshimiwa Mchungaji Getrude Rwakatare kumwombea ndugu Reginald Mengi apumzike mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa jioni ya leo na ndio mchango wangu wa kwanza kwenye bajeti na nilikuwa naisubiri sana hii Wizara ya Maji kwa sababu nikiwa kama mwakilishi wa wanawake maji ni kila kitu kwa mwanamke yeyote. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Makame Mbarawa, Naibu Waziri mwanangu Mheshimiwa Aweso, timu yote ya wanamaji maana yake wao wanafamilia ya maji kutoka wizarani mpaka mikoani, niwapongeze kwa juhudi zao kwa kipindi chote kuhakikisha kwamba maji yanapatikana. Kipekee niwapongeze wanawake wote, wanawake wa Tanzania wasiochoka kuhakikisha maji yanapatikana, kulea familia zao, kutunza familia zao, wakiwemo wa mjini na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika Mungu ni mwema naye leo ametupa uhai tukaweza kuzungumza haya mambo hapa nami nimrudishie sifa na utukufu Mwenyezi Mungu nikiamini kwamba atatupatia maji mengi zaidi Tanzania. Niseme kwamba ni vyema basi kama tunaamini hivyo na tumeipokea hii ripoti nzuri maana yake hii ripoti kwa kweli inatiririka kama kitabu cha hadithi, niseme kwamba hakuna litakaloshindikana kwenye ripoti hii ila tu Serikali nayo isikie na ili nisikose muda wa kukamilisha azma yangu naomba kuunga mkono hotuba hii kwa aslimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani ni mwaka wa nne sasa toka nimeingia kwenye Bunge hili la Kumi na Moja, nimewakuta Wabunge waliokuwa wametangulia wanazungumzia Sh.50 nyingine ya maji ambazo zimekuwa ring fence ambazo zimefanya kazi kubwa na leo kwa hiari yao wenyewe wanaomba tena Sh.50 ziongezwe, labda chanzo cha mafuta ni kigumu sana kwamba vitu vitapanda bei, lakini Wabunge sisi ndio wawakilishi tumekuja na chanzo kingine tumesema kwamba basi ikatwe kwenye bundle za simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiari yashinda utumwa, kwa hiari yao na watajua namna ya kuongea na wawakilishi ili kila mtu apate maji safi na salama ambayo ni haki yake. Mungu alitupa maji tunafurahi kabisa. Nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri toka ule ukurasa wa 12 mpaka wa 22 ambapo ukurasa huo wa 12 anazungumzia usimamizi na uendeshaji wa rasilimali za maji, akizungumzia mabonde ya maji, vyanzo mbalimbali na management ya maji, lakini sikuona msisitizo kwenye maji yanayotoka angani. Tanzania inaelekea kupata athari kubwa kwa ajili ya tabia nchi na zikianza mvua zinaanza kwa kasi kama zile za juzi zilizoharibu miundombinu ya barabara au watu walishindwa kupita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize tu wasomi wetu wako wapi? Hayo maji yanayotiririka na kupotea ardhini na kurudi tena baharini wamejipanga vipi kuhakikisha tunayakinga. Hivi majuzi Wabunge wote walikwenda kule kwenye mji mpya Ihumwa, sijui yale majengo kama yana makinga maji, mimi nilibahatika pia kwenda na Kamati ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama na tukahoji hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaalamu wa ku-reserve rain water ni mdogo sana. Miaka hiyo nikisoma Kifungilo tulikuwa na rain water na ndio maji safi na salama. Sasa wamejipanga vipi pale Ihumwa kuwa na maji mengi maana yake zikija mvua za Dodoma ni nyingi sana kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia sasa eneo ambalo mimi nashiriki kama Diwani ambapo ni kule Siha. Siha kuna shida ya maji, pia tambarare yote ya Kilimanjaro, wengi waliniambia wewe unachangia nini na Kilimanjaro maji bwerere. Nataka niwaambie hivi kuna maeneo ambayo hayajaona maji safi na salama ikiwepo Same, Mwanga, Rombo na huko Siha, maji safi na salama ni shida. Alipokuja Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye namshukuru sana aliona wote walikuwa wanamwomba maji safi na salama naye alisema jambo hili ataliwekea mkazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi Mamlaka za Maji zina mafanikio makubwa na best practice zinaonekana, successful cases zimeonekana ikiwemo Mamlaka ya Maji MUWSA inayoongozwa na Joyce Msiru binti aliyekubuhu kabisa katika nyanja ya maji na anaipeleka vizuri. Sio hayo tu Dodoma yenyewe hatuna shida ya maji na Dar es Salaam pia niwapongeze sana Wakurugenzi hao na wale wengine. Siha kuna shida moja tu MUWSA ilipopelekwa kwenda kusimamia sasa management maana yake shida ni management na mpaka sasa hivi kwa kipindi kifupi sana tumepata Siha bilioni 4.3, naishukuru Serikali. Hata hivyo, ile bilioni ya kwanza bilioni 1.8 ya mwaka 2016 iliyojenga yale matenki ni kama imepotea maana yake yale matenki sasa hayatoi maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu ambaye nimempongeza sana awali katika ile timu, waone sasa kwamba hawa wenzetu wa MUWSA watakapofika kule Hai wasisikilize hiyo ya kwamba haitawezekana, maana yake zimetokea tuhuma nyingi, hapa sio mahali pake lakini waendelee kusimamia ili maji hayo yaweze sasa kutumika kwa wingi na kusambazwa katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiomba fomu ya kuomba maji kule Siha ni Sh.345,000 ambapo MUWSA ni Sh.20,000 tu. Sasa nashindwa kuelewa kwa nini wale wananchi wanashindwa kukubali, labda hapa pamepungua elimu. Nawaomba sana MUWSA itoe elimu na Katibu Mkuu asimamie jambo hili kwa sababu wanaoteseka ni wale wanawake wa kule mbali. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kipekee namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai kutuweka wote hapa tuweze kuisemea nchi yetu mambo ya maendeleo na pia tuweze kuishauri Serikali. Awali ya yote naomba niwapongeze sana wenyeviti wote wawili kwa wasilisho lao na pia naomba nichukue nafasi hii rasmi kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji ambao ni wachumi waliobobea na mnaona mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Katibu Mkuu Dotto James kwa kubana matumizi, mengine yamesemwa kwenye ripoti na sasa niende tu moja kwa moja kuzungumzia ile sekta ya benki. Kwenye kamati tumekesha na hawa watu, kamati ya bajeti tunatoka saa nne hawali, hawanywi hawachoki, Mheshimiwa Waziri anakuwa Dar es Salaam asubuhi jioni yuko na sisi na tumezungumza mambo mengi. Kuna mambo ambayo tumemshauri na naomba nichukue tena nafasi hii kuweka msisitizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya benki imekaa kibiashara na kweli ni biashara huria lakini Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kila leo anataka kumtetea mtu wa chini. Watu wa chini hawa wanaokota fedha zao kidogo kidogo, wanakuwa kwenye vikoba, wanataka kwenda kuweka fedha salama wanapeleka benki na benki wanaweka kwenye savings account wanapata asilimia moja tu (1 percent). 1 percent ikikatwa service fee inakata mpaka ile fedha yao waliyowekeza matokeo yake vikoba wameamua kufanya nini! Wameamua kuvunja vikoba ndani na kugawanya ule mtaji halafu wanaanza upya. Hapa nasimama nazungumzia wale wanawake walionituma hapa Bungeni, wanawake wa Kilimanjaro. Nawashukuru sana kunileta hapa na sitawaangusha nitalizungumzia jambo hili kila siku mpaka benki ziweze kulihuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiingii akilini, haiingii akili fedha zinavyokusanywa na benki zinakwenda kuwekwa kwenye treasury bonds lakini kwa miaka miwili ni asilimia 8.17, miaka mitano asilimia 10.22, miaka kumi wanalipwa wao asilimia 13, miaka 15 asilimia 15.19 na miaka 20 asilimia 16.71. Shida inatoka wapi! Kweli kuweka ni gharama na pia wanapokuja kulipa hujui yule aliyeweka fedha yake benki ataichukua saa ngapi atetemeshe, lakini kuna wale wazee ambao wanaweka fedha benki na wanaweka tu mpaka itakaposomwa siku ya mauti, fedha ile unakuta imekwisha. Hivi inakuwaje, tunakubalianaje na jambo hilo, nazidi kumuomba Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa vile alivyo msikivu hili jambo alizungumzie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba niwazungumzie watumishi wanaokopa benki. Mtumishi anakwenda kukopa benki, yeye amekaa ofisini mshahara ukija unakatwa deni linalipwa lakini asilimia yake ya kulipia lile deni (interest rate) inalingana na asilimia ya mtu ambaye anafanya biashara. Kuna risk gani hapo? Kuna rate ya ku-default ni ndogo sana mshahara tu ukiingia tu tayari imelipwa hata hapa Bungeni kwa wale tuliochukua mkopo mshahara ukiingia hujauona umeshalipa deni. Kwa nini sasa hayo mabenki yasione kwamba wale wanaokuja kukopa ambao ni wafanyakazi hao ndio wale wanaolipa pay as you earn kubwa na yenyewe pia inakatwa bila kusumbua, wakashushiwa interest rate kutoka kwenye two digits kwenda kwenye single digit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana jambo hili lizidi kuangaliwa na linazungumzika. Mimi hainingii akilini tuna mabenki yetu mazuri kama CRDB, tuna mabenki yetu ya hapa nyumbani kama Posta, tuna benki kama NMB lakini mabenki ya nje yaje hapa yafanye rough ya kutafuta hela halafu na sisi tunajirusha tunataka kulingana nayo mnamsaidiaje huyu mwananchi wa chini anayezungumziwa siku zote na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili jambo likakae kitaalamu zaidi hata kama hiyo hela wanakopeshana wenyewe kwa wenyewe waangalie basi jinsi gani interest rate itashuka na huyu mfanyakazi anayekesha ofisini anakopa kagari kake mnaziita sijui Vitz aone raha ya kufanya kazi ametulia ajue kwamba analipa kwa ustahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi kwamba tumelizungumza na narudia tena na ninaamini linafikirika na linazungumzika. Lakini niiombe pia hii Wizara ya Fedha iweze kuangalia jinsi gani wale watu wa SACCOS watalipwa asilimia moja zaidi ya interest isilipwe moja kwa sababu wao wanakusanya kule nje wanaleta hela huku benki. Hiyo nayo wangetosha wapewe elimu na hayo mabenki na pia wapewe asilimia moja zaidi na iliwahi kutokea huko nyuma sijui inashindikana wapi ili waweze ku-run ofisi zao vizuri. Matokeo yake tutakuwa tu tunalaumu SACCOS hawafanyi lakini SACCOS pia hawapati elimu ya kutosha, SACCOS hawana motisha, SACCOS hizo ndio maana wanaanza kula wanakuwa mchwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya yalifanyika na yakawezekana naamini kwamba bado yatawezekana, tukiweza kuwapa motisha hawa wanaokwenda kutuokotea hela na nitawakumbusha tu. Mwaka jana Serikali ilichukua hela zake ambayo ilikuwa inawaachia mashirika yakae nazo waweke kwenye benki zao za commercial wamepeleka kwenye akaunti BOT lakini mashirika yale Benki zile zinaenda kutafuta hela na sasa hivi kuna benki ambazo zilikuwa na deposit kidogo zime-trip na benki hizo zinaendelea kumbe bado huku nje kuna hela, watu waliamua kuzishikilia lakini wale wakandarasi wanaolipwa pia na BOT zikisharejeshwa hela kwenye akaunti za wale makandarasi kwenye commercial banks wameenda kwenye zile benki ambazo zinaaminika na mnazijua benki zinazoaminika na sisi pia tuna-save huko kama CRDB. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niwaombe sana watu sasa waende wanunue hisa, hisa zipo chini unaambiwa kwenye hisa buy low, sell high huu ndio wakati wote na mimi nawaambia wanunue hisa na wananchi wetu wapewe elimu ya hisa. Lakini nimwombe Mheshimiwa Dkt. Mpango leo tumezikia lugha ngumu sana huku ndani kwamba uchumi umeendaje wape hawa Wabunge wako semina, kuna mataasisi mengi tunatakiwa kuelimishwa tukuone tujue, Wabunge wanataka elimu ili waweze kufikiri sharp kama wewe. Dkt, please PHD yako ni ya ukweli sio Honarally umesoma vitabu mpaka vikasema enough wape watu semina hapa ndani tuongee lugha zinazofanana. Bahati nzuri nao wamekiri ni makanjanja lakini sio mmoja wengi hapa uchumi hatuujui. Tunaomba utupe semina kila Bunge likianza tupe semina tuonge lugha ambazo zinafanana na wewe baada ya kuzungumzia bajeti nakushukuru kwa yote uliyotufanyia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niipongeze sana Kamati ya PIC Kamati hii imefanya kazi kubwa na ya weledi chini ya Mheshimiwa Dkt Raphael Chegeni na niseme kwa mara ya kwanza tumeona dividend zikilipwa hadharani, kuna ambao walikuwa wana hisa lakini walikuwa hawalipwi hivi imekuaje overnight wakajua ni baada ya nyie Kamati kufanya na kwenda kuwaelimisha walipe. Wanapolipa inakuwaje, hela hizo zinaingia kwenye mfuko mkubwa wa Serikali tunapata vifaa ambavyo tunastahili kupata, tunapata dawa, tunapata hela za kununuliwa vitu ambavyo visingenunulika kama hizo hela zisingeokotwa. Kwa hiyo, nawapongeza sana hii Kamati ya PIC na nasema kwa kweli uzi ni huo huo Spika hakukosea, nampongeza sana Spika kwa sababu ni Kamati mpya ilikuwa haipo na naona tukienda tukirudi mambo yatafanyika makubwa zaidi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana sana kwa nafasi hii ya leo, ambayo kwangu ni muhimu sana, hata nimeahirisha kwenda kufanya checkup ya afya yangu. Kipekee namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, kwetu sote tuliokaa hapa tuweze kuzungumzia mambo ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha nawashukuru wote waliotupatia sadaka zao, akiwemo Mbunge mwenzetu, lakini pia wako wale watu wa maziwa jana, tumepata maziwa ya ASAS, tumepata maziwa ya Tanga Freshi, asiyejua kushukuru hata hatabarikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Leo nimesimama hapa nizungumzie eneo moja tu la mifugo, na ni eneo la kuku na kuku siyo kuku wote, najikita kwenye kuku wa kienyeji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msanii aliyeimba supu ya kuku wa kienyeji ni tamu sana, hakukosea ni kweli kabisa, toka tunakua, ukimuheshimu mgeni nyumbani, unamchinjia angalau kuku wa kienyeji ili apate kukarimika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni takribani mwaka wa nne sasa toka nimeingia Bunge hili na kila siku namfuata Waziri wangu wa Mifugo na Uvuvi nikiulizia vifaranga wa kuku wa kienyeji wanapatikana vipi? Niseme kwamba nimekuwa nikijibiwa, napewa namba za simu na kila ninapopiga, ambako amenielekeza sipati simu, lakini hilo haliniondoi kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri huyu kwa kazi zake nzuri ambazo zimeonekana kitaifa yeye pamoja na Manaibu Waziri wake wote, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara mpaka Madereva wao wanaowaendesha kwa usalama Wizara hii itaweza kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ni muhimu sana kwa wanawake, na hata dakika hii ukichukua sensa ya walio huku Bungeni, ukiondoa wale waliomsindikiza Mheshimiwa Mbunge aliyeapishwa, wengi ni wanawake. Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni muhimu kwetu sisi kwa sababu bila Wizara hii hatuna kitoweo na sisi wanawake bila kitoweo nyumbani, hakuna chochote kinachokwenda mdomoni. Ukitaja maziwa, ni kitoweo, ukitaja samaki ni kitoweo, ukitaja kuku ni kitoweo, ukitaja ng’ombe ni kitoweo, ukitaja nguruwe ni kitoweo! Ukitaja yule mkuu wa meza ni kiweo, nitaje kipi ambacho siyo kitoweo, ambacho ni muhimu kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwetu wanawake, siyo tu tunataka kile kitoweo, tunataka kitoweo na ziada ya kutuingizia kipato. Ingekuwa wameweka mkazo kwenye kuku wa kienyeji, na kila mwanamke mtanzania au kila familia ikafuga kuku, na wale vijana wanaomaliza shule ambao hawajapata ajira wakafuga kuku, leo tungekuwa hatuna uhaba kabisa wa mayai, ambayo ni protein, tungekuwa hatuna uhaba kabisa white meat, kwa wale ambao hawataki kuongeza uzito, na pia tungekuwa hatuna upungufu wa protein popote pale.

Mheshimiwa Spika, lakini kundi hilo limeachwa na kuku hawa hawana kazi kubwa sana kuwalea, hawa ni scavengers, wanacharukacharuka tu, mtu akitaka kukuonyesha kwamba una harakati nyingine anakwambia wewe acha mambo ya kuku wa kienyeji. Yeye anachakurachakura huku na huku, lakini kuku hao sasa hivi wanafunikwa, wanafutika, utaambiwa kuna guchi, sijui kuna kuroiler sijui kuna crossbreed, ni lini sasa gene hii itatafutiwa utalaam wa kuikuza ili watu wengi zaidi wafuge kuku wa kienyeji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni takribani miaka 58 sasa toka tumepata uhuru, lakini tatizo la ugonjwa wa mdondo bado ni usumbufu mkubwa, bila ya ugonjwa wa mdondo, ule wa new castle kwa lugha nyingine, kuku wa kienyeji wangezagaa huku. Niwasifu sana wenzetu wa Singida, ambao kwa kweli ukiuliza kuku hii imetoka wapi, Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza, niko hapa natamani wanawake wangu wote wa Kilimanjaro wafuge, kila mmoja awe na kuku wake wa kienyeji hata kama atamfugia chini ya uvungu, lakini mbegu haipatikani, napataje mbegu ya kuku wa kienyeji ili nikasambaze Kilimanjaro, kila mwanamke afuge, kila mwanafunzi afuge nikae kwenye geti la shule niwape vifaranga viwili viwili, wafuge kila mtu na shida ya kitoweo iondoke.

Mheshimiwa Spika, utanishangaa na wengine watanishangaa, kwa nini anang’ang’ana kuku wa kienyeji, gharama za kule kuku wa kienyeji ni kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana atakapokuja kujibu Mheshimiwa Waziri, anieleze, kwa nini wanaruhusu hii kutoa chanjo kwa kuku hawa ikawa ni mtu kutaka na isiwe ni mass vaccination ili sasa tufute na tutokomeze kabisa, kwenye mambo yake yake ya kipaumbele nimeyasoma, amesema kwamba natarajia kupunguza na hiyo iko kwenye ule ukurasa wa 13, kudhibiti, lakini naomba atokomeze kabisa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumzia sana hao kuku wa kienyeji na kila mtu kunielewa shida yangu, na wale wanawake wangu wa Kilimanjaro na kokote wanawake wapo, naomba sasa nije kwenye kuwapa miradi vikundi vya akina mama popote walipo.

Mheshimiwa Spika, tukisema mitamba, mtamba mmoja mzuri anakwedna mpaka shilingi milioni moja, hatuwezi wanawake sisi. Nakwenda kwenye ng’ombe sasa, ili ng’ombe tumpate, tumfuge, tupate maziwa, tupate samadi ya kwenye mashamba yetu na kila mahali. Nilikuwa naomba Serikali, kwa vile Serikali yetu ya Awamu ya Tano ni sikivu na inapenda sana pia kutekeleza mambo ya Mwalimu Nyerere, irudi upya, kusambaza mitamba kama Mwalimu Nyerere alivyosambaza mitamba kwenye ile awamu ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, endapo tutafuga vizuri, tukakopeshwa mitamba, kopeshwa ng’ombe lipa ndama, tutaweza tena kuibua mbegu mpya ya mitamba mizuri yenye maziwa mengi, kuliko hii tunayofanya sasa hivi, wamesha crossbreed mara nyingi sana wenywe kwa wenyewe, na pia unakuta maziwa yanayopatikana sasa ni kidogo.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo, nimeona, kwenye kitabu tumeelezwa kwamba idadi kubwa imeongezeka kwenye artificial insemination, lakini basi ningeomba, hiyo artificial insemination ifanyike bure, tuwazalishie watu bure. Mwingine ng’ombe anapata joto anakuta hana hela ya kwenda kulipa, sasa hiyo inapoteza tena, anapoteza muhula mmoja wa kuendeleza au wa kuzalisha ng’ombe. Nilikuwa naomba sana, kama Mheshimiwa Waziri atanielewa ninalowaombea watu wangu wenye uwezo mdogo, tupate…

SPIKA: Malizia Mheshimiwa Shally.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga hoja mkono asilimia 100, ahsante sana Spika wangu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono kwa asilimia mia moja. Baada ya hayo, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara na taasisi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ni rasilimali muhimu kwa kilimo, ufugaji, viwanda, misitu, hifadhi na kadhalika, hatimaye kwa kutuhifadhi sote tutakapokufa. Bahati mbaya sana, Mungu alishamaliza kuumba ardhi. Kwa namna hii lazima usimamizi wa ardhi ufanyike kwa uangalifu mkubwa sana. Mpango wa matumizi bora ya ardhi unahitajika sana na Serikali ina wajibu wa kuziwezesha na kusimamia Halmashauri zote nchini, vijiji vyote na mpango wa matumizi bora ya Ardhi ya Vijiji chini ya Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto, yako mashamba makubwa katika maeneo mbalimbali ambayo hayaendelezwi vizuri na baadhi kuwa mashamba pori. Kwa kuwa baadhi ya mashamba haya; umiliki umebatilishwa na Hati kufutiwa, ni lini sasa mipango ya matumizi ya mashamba hayo itafanyika? Ushauri wangu ni kwamba, hayo mashamba yagawiwe vyama vya ushirika na vijiji, badala ya kugawa kwa watu binafsi. Kwani ni wengi na itasababisha migogoro zaidi, mbaya zaidi wananchi wengine huuza maeneo waliyogawiwa. Katika mashamba hayo yatengwe pia maeneo ya uwekezaji wa viwanda, ujasirimali wa vijana, shule, vituo vya afya na mahitaji mengine ya shughuli za Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi yaliyofanywa mwaka 1973 kumilikisha mashamba makubwa ya kahawa kwa Vyama vya Msingi vya Ushirika huko Kilimanjaro, tunaona faida zake hadi sasa. Baadhi ya wawekezaji wanalipa kodi ya pango kwa Vyama vya Ushirika, lakini pia wanatoa maeneo kwa shughuli za jamii. Muhimu zaidi ni kwamba bado wanaendeleza zao la kahawa. Ombi, wawekezaji hawa washauriwe kuelimisha jamii inayowazunguka jinsi ya kuendeleza zao la kahawa kupitia CSR –Corporate Social Responsibility.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naunga hoja mkono na ninakupongeza Waziri, Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, na timu yote ya Wizarani kwa kazi nzuri ya kuwapatia wananchi wa Tanzania maji safi na salama. Changamoto ni kuwa Tanzania imezungukwa na maziwa (lakes) kadhaa, lakini hatujaweza kunufaika nayo. Nini kifanyike ili vyanzo hivyo vya maji vinufaishe wengi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uvunaji wa maji ya mvua, msimu wa mvua maji yanatiririka hovyo kila mahali na mvua zikiisha shida iko pale pale. Kwenye kitabu imesemwa kidogo sana, swali, ni lini sasa Serikali italeta Muswada hapa Bungeni wa kutunga sheria ya kuokoa kila tone la maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, haingii akilini kwamba Serikali inaingia gharama kubwa sana kutibu maji machafu hadi yawe safi na salama wakati ambapo yale ya mvua yaliyo safi naturaly yanapotea ardhini. Maji ya mvua yanayotiririka barabarani na kuharibu miundombinu yajengewe mabwawa. Mfano, maji yanayotiririka Kibaigwa, njia ya Dodoma – Dar es Salaam ni lini sasa maji hayo yatakingwa kama ilivyo Morogoro (Mindu Dam)?

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza sana mamlaka zote za maji nchini, ombi, Wizara izisaidie kudai madeni ili zifanikiwe kuendesha shughuli zake kwa amani na utulivu. Taasisi za Serikali zinadaiwa hela nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi mabovu ya maji safi na salama viwandani, shambani/bustani, car wash na kwingineko; ombi, Serikali itujulishe mkakati wake wa kukomesha jambo hilo kwani maji safi na salama ni ghali sana; vifaa/taps za maji zinamwaga maji hovyo, Serikali itoe tamko kuhusu jambo hili. Kwenye taasisi, mashuleni na majumbani zitumike zile bomba za kuhisi (sensor).

Mheshimiwa Naibu Spika, usimamizi wa uchimbaji visima vijijini unaposimamiwa na wataalam Wizarani si mzuri kwani gharama zinakuwa mara mbili. Wengi wanaona ni vyema Halmashauri zikasimamia. Wizara isiingilie maji yanayosimamiwa na wafadhili, mfano Hai - Himo – Njia Panda; mradi unaosimamiwa na Kilema Kusini Water Users Association uwe huru kujiendesha kama ulivyo Mradi wa Uroki. Nashukuru kwa Mradi wa Mwanga/Same – Korogwe kutengewa hela. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai kwetu sote. Nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona umuhimu wa Wizara hii na kumteua Waziri na Naibu Waziri walio waelewa na makini sana kwenye kazi zao.

Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe na Mheshimiwa Juliana Shonza, Katibu Mkuu Ndugu Susan Mlawa, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Nicholaus B. William, Mkurugenzi wa Habari Dkt. Ryoba na Viongozi wote Wakuu kwenye Idara nyingine ikiwemo Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Spika, nakubali kabisa kwamba kuna mambo ambayo yanatendeka, yanabadilisha utamaduni wetu bila hiari yetu Watanzania, kutokana na uwepo wa mitandao kama luninga, simu na kadhalika. Baadhi ya mambo hayo ni mavazi yasiyo ya heshima, maigizo ya filamu za nje na mengineyo. Je, Serikali ina mpango gani kukomesha vituko hivyo katika hatua za awali kama kwenye Shule za Msingi?

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Idara ya Habari. Tatizo langu ni mtiririko wa taarifa ya habari asubuhi. Je, ni lini TBC itatangaza habari mfululizo bila kuingiliwa na majadiliano yoyote ili tuwahi kazini?

Mheshimiwa Spika, kuhusu michezo. Inaumiza sana kuona jinsi ambavyo hatujaweza kuingia kwenye kiwango cha juu cha Kimataifa kwenye soka. Nataka ieleweke kuwa, maandalizi yetu ya zimamoto hayatatufikisha mbali. Kila Wizara iwe na dawati la michezo mahali pa kazi.

Mheshimiwa Spika, napendekeza wachezaji waandaliwe toka utotoni kwa lishe bora, elimu na mazoezi. Makuzi ya wanamichezo yasimamiwe toka awali na wazazi na waalimu.

Mheshimiwa Spika, mwisho, naunga mkono hoja na ninaomba kwenye miaka ijayo waongezewe fedha zaidi bila ukomo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa ya kuchangia na uongozi mzuri huku Bungeni. Pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, IGP na Wakuu wote wa Majeshi yote, Zimamoto na Uokoaji, Magereza na Idara ya Uhamiaji kwa ufanisi mzuri.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo wizi wa magari umepungua sana, ajali barabarani zimepungua na hata wizi wa kuvunjiwa nyumba. Hizi zote ni juhudi za Jeshi la Polisi, pongezi sana sana.

Mheshimiwa Spika, ombi, uongozi wa Jeshi la Polisi uone umuhimu wa kulipa deni kubwa la maji, linalodaiwa na Mamlaka ya Maji safi na Salama na Uondoaji wa Majitaka Moshi (MUWSA) Ref. Deni la CCP-MSH. Deni hili limeshahakikiwa lakini ni zaidi ya miaka saba halilipwi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anajibu hoja alitolee maamuzi, la sivyo nitalazimika kushika shilingi kwenye mshahara wake japo sipendelei kabisa kufanya hivyo kwa Waziri makini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kwa kuwa Mtanzania, mwakilishi wa wanawake wa Kilimanjaro Bungeni. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yote ya viongozi wa Idara, Vyuo na Shule zote Nchini kwa juhudi za kutoa elimu bora. Nawapongeza wazazi wote wenye wanafunzi mashuleni na kwenye vyuo ndani na nje ya nchi, pia nawapongeza wanafunzi hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwezesha elimu bila malipo na kuendelea kuteua maprofesa kwenye nafasi mbalimbali jambo hili limewafanya vijana wengi sasa waheshimu elimu na ufaulu mzuri, vilaza sasa wameshastuka kuisha elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni ufunguo wa maisha, wananchi wakiwa na elimu nzuri, Tanzania ya viwanda itawezekana, maradhi ya kuambukiza yatakwisha, rushwa itapungua au kwisha kabisa, ujambazi utakwisha na mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu, Serikali imejiandaa vipi kuwapatia mtaji vijana wanaofuzu vyuo ambao hawajapata ajira ili waanze shughuli za ujasiriamali? Serikali ina mpango gani wa kuwapatia ardhi au maeneo ili vijana kununua viwanja vilivyopimwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya watu wazima, naomba kuisikia Serikali ina mpango gani kuhusu kuendeleza elimu ya watu wazima, yakiwepo mafunzo ya IT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, naungana na wote waliotangulia kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mimi ni shahidi wa kazi inayoendelea barabara ya Sanya Juu - Kamwanga.

Mheshimiwa Spika, naomba baada ya mkataba wa Ujenzi wa barabara ya Kiboriloni –Kikarara, Tsuduni – Kidia kusainiwa, tunaomba sasa ujenzi uanze kwa kasi kabisa baada ya subira ya miaka zaidi ya saba.

Mheshimiwa Spika, vile vile tunaomba sehemu ya barabara ya kutoka Chuo cha Wanyamapori – Mweka hadi lango la Mlima Kilimanjaro ijengwe kwa kiwango cha lami ili kuondoa kero kwa watalii, kwani ni ya charangawe na ni nyembamba sana. Bahati nzuri mvua nazo katika eneo hilo ni nyingi, hivyo kupelekea watalii kusukuma magari badala ya ku-enjoy safari.

Mheshimiwa Spika, pongezi kwa kazi nzuri iliyofanywa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Marangu na Machame kuelekea Mlima Kilimanjaro, imesaidia kuboresha mazingira ya utalii.

Mheshimiwa Spika, ushirikishwaji wa wanawake katika kazi za barabara ni jambo kubwa na zuri. Ni vizuri ushirikishwaji huu ufanyike kwenye Wilaya zote nchini. Kuna kazi za ujenzi wa barabara katika wilaya zetu zinazoweza kutekelezwa na wanawake. Nashauri mwongozo wa Wizara kuhusu suala hili uelekeze kila Wilaya kutoa mafunzo kwa wanawake na kuweka asilimia ya kazi ambazo lazima zifanywe na wanawake.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha agusie mafunzo ya utunzaji barabara kwa jamii. TANROAD na TARURA watoe mafunzo hayo.

Mheshimiwa Spika, kero kwa wale waliopita barabara ya Arusha - Moshi siku za karibuni watakubaliana nami kuwa hii ni moja ya barabara yenye msongamano mkubwa wa magari. Inachukua muda wa saa tatu kusafiri umbali wa kilometa 85 Tengeru - Himo.

Mheshimiwa Spika, tunaomba mazungumzo kati ya Serikali na JICA yakamilike mapema ili hatimaye upanuzi wa barabara kutoka Tengeru hadi Himo ufanyike kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kipekee kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa muda huu kunipa tena pumzi ya kuweza kuchangia mambo ya maendeleo katika nchi yangu, nchi yenye amani, huru na ambayo inaheshimu raia wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue muda huu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kutuletea bajeti nzuri tofauti na bajeti zote na hata huko nje wanasema walizoea kusikia nyongeza kwenye pipi, karanga, kilevi, mafuta, leo mambo ni tofauti kabisa. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wangu huyo, Dkt. Philipo Mpango, Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Ashatu Kijaji na mimi nasema kwa kweli hizo PhD zao ni za uhakika. Nampongeza Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu na timu yao yote. Zaidi sana nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliosimama na kuchangia bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijaitendea haki nafasi yangu kama sitakishukuru chama changu cha CCM kilichopitisha jina langu mara kilipopokea jina hilo kutoka kwa wanawake wa Kilimanjaro. Nawashukuru sana wanawake hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumzia keki ya Serikali. Keki hii sasa iko kwenye mgawanyo lakini inapatikanaje? Bajeti ya Serikali au bajeti yoyote ile ina pande mbili, ina makadirio ya mapato na matumizi, kwenye mapato tuna kodi, mikopo, misaada na pia kwenye bajeti ya Tanzania tunayo pia nafasi ya kupata gawio kule Serikali ilipowekeza. Hapa niwapongeza sana CRDB kwa kutoa gawio la shilingi bilioni 9.9 zikiweko shilingi bilioni 6.7 za Serikali na zile nyingine kwenye taasisi. Pia NMB walitoa na nadhani mashirika mengine machache yametoa. Naomba huo uwe ni mwendelezo. Upande mwingine wa bajeti una matumizi yanayotumika kwenye social services, vichocheo vya maendeleo ikiweko mindombinu kama barabara lakini yote hayo ni kwa ajili ya maendeleo na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walipa kodi ni wananchi wote tukiwemo sisi na wale wa chini na ili kodi iongezeke inabidi wale wafanyabiashara wadogo wasaidiwe ili waweze ku-graduate wawe wafanyabiashara wakubwa. Tumeona Serikali yetu imetoa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo ili ikifika mahali sasa na wao watakuwa wakubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kutoa vitambulisho ni moja lakini waendelee kutoa elimu kwa watu hawa ili waweze kuja kuwa wafanyabiashara wakubwa. Hata hivyo, niiombe Serikali yangu sikivu, katika kuwalea hawa wafanyabiashara wadogo na kati wawalipe pia wazabuni, hao ni wafanyabiashara wa kati wanaoenda kuomba mikopo benki, wanatoa huduma Serikalini lakini wakati wa kulipwa inachukua muda sana na watu wale wengine wanakata tamaa au wanaondoka kabisa kwenye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, niiombe Serikali yangu sikivu ilipe pia madeni ya wale wanaotumia utility, wanaotumia huduma za maji na umeme, walipe yale mashirika yanayotoa huduma hizo. Hapa nawaombea sana Mamlaka za Maji ikiwemo Mamlaka ya Maji ya Moshi (MUWSA), deni lake sasa ni takribani shilingi bilioni 2, limeshahakikiwa lakini bado hawajalipwa; DAWASCO imelipwa na pia Arusha imelipwa. Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Fedha ametenga fedha, naomba katika ile awamu ya kwanza ya kulipa watu hawa waweze kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme wazi kwamba naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri ili nisije nikasahau. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nina mambo mawili ambayo ni maombi sasa. Naomba ili wafanyabiashara hao katika kuwafanyia mambo yawe rahisi kibiashara, wa kati na wakubwa, ile Blue Print tuliyoambiwa hapa sana chonde chonde iletwe na tufanyiwe semina na wananchi waeleweshwe ili wajue jinsi gani watarahisisha mambo yao kwenye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo linasumbua sasa hivi, mwaka jana tuliliona ni zuri tukasherehekea ni kuhusu sanitary pads za wanafunzi au wahitaji ambao ni mabinti. Kweli hakuna jambo ambalo ni bure na sisi kila tukisimama hapa tumeona ambavyo Wizara hiyo imepata shida na ilipo-test imeona kwamba jambo hilo halikuwa kwa manufaa ya wahusika. Basi nami nije pia na pendekezo langu, naomba kuwepo na vocha, tunasema kuwe na tozo kama tulivyofanya kwenye chandarua (hati punguzo), ikiwezekana taulo hizi za kike kwa wanafunzi wetu zipatiwe hati punguzo. Tuliona jinsi ambavyo awamu iliyotangulia ilishughulikia malaria ikatoa hati punguzo kwenye chandarua, kiwanda kikaweza kupata msamaha kiasi lakini pia mhitaji anakwenda na hati punguzo kununua. Hawa ni wanafunzi, wapatiwe vocha waende wakapatiwe hati punguzo hiyo waweze kununua pungufu ya bei, kwa ujumla wake tutakuwa tumechangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda mtauliza kwa nini haswa? Mimi ni jinsi ya (K), ni mwanamke, najua shida tunazozipitia toka utoto mpaka kufikia hapa. Kuanzia miaka 15 mpaka kufikia miaka 55, hilo jambo halikwepeki lakini hatuangalii kwa wote tunaangalia kwa wanafunzi na hasa wanafunzi wale ambao wanatoka katika mazingira duni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wanafunzi ambao kwa siku tano hawaendi darasani kwa vile ila hali inakuja na mambo mengi, kichwa kitauma, maumivu ya tumbo, kichefuchefu, lakini sio hiyo tu hata ile kutoka ni shida. Kwa hiyo, ili nisifafanue zaidi kwa sababu wote wanaelewa, naiomba Serikali yangu sikivu iangalie itakachoweza kufanya ili watu hao wanufaike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuhusu bajeti hii ni kwenye kilimo. Kweli kila aliye humu ndani amepitia eneo la kilimo. Mimi nimetokea eneo ambalo kahawa ndiyo zao la biashara lakini pia kuna ndizi na mazao mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini kuhusu kahawa? Wako waoteshaji kahawa wenye mashamba makubwa pembeni yake yuko mtu wa kawaida ambapo shamba lake dogo lakini shamba la mtu yule ni choka mbaya yaani limekata tamaa, shamba na mwenyewe wamekata tamaa. Naiomba Serikali yangu iweze kuzungumza na hawa wakulima wakubwa kama wataweza kuungana sasa na wale ambao wanawazunguka kama inavyofanyika Kilombero kwa out growers wa miwa ifanyike hivyo Kilimanjaro kwa wale wakulima wa kahawa ili tuweze kuwa na kahawa nzuri na tuongeze pato la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye utalii, nataka nizungumzie tu kwamba kuna kodi ambazo wamepunguziwa lakini pia kuna kodi ambazo bado zipo lakini wale waliokuja kama wadau kwenye Kamati ya Bajeti shida yao siyo ile tozo ya kodi. Juzi Mheshimiwa Waziri amepunguza ule ukiritimba wa kwenda kulipa tozo nyingi. Namwomba ikiwezekana kwenye utalii aangalie ili kuwaweka kwenye one stop center wakifika walipe ili watalii hawa wapate tena hamu ya kurudi Tanzania na kuja kutembea bila kufikiria shida zilizopo za kuanza mahangaiko hapa na pale. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kipekee namshukuru Mungu sana kutuweka hapa ili tuongee masuala muhimu haya kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, amani, amani, amani, nikiuliza hapa mna amani? Wote mtasema ndiyo na ndiyo maana mko chini ya jengo hili mkisikiliza na mkitafakari na mkifanya kazi nzuri hizi kwa wananchi wenu. Amani ni kitu muhimu sana kwa mtu mwenyewe kwenye nafsi yake na kwa mtu na watu wake na Taifa na viongozi wa juu na wananchi wao.

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa kuzungumza machache. Mimi ni mjumbe wa Kamati hii na mashahidi ninaowazungumzia ni wajumbe wenzangu. Kwa heshima na taadhima, naomba niseme kwamba matamko yaliyotoka kutoka kwa wenzetu hawa yalileta mtafaruku kwenye nchi yetu. Naanzia na Mheshimiwa Josephat Mathias Gwajima, yeye ni Mbunge mwenzetu, ni mtu tunayemsikiliza, ni mtu tunayeishi naye lakini pia alituambia yeye ni Mchungaji au ni kile cheo kingine hapa nchini na kwa mataifa mengine.

Mheshimiwa Spika, aliposema mataifa mengine na akaleta ushahidi pale kwetu akisema kwamba anapozungumzia chanjo anazungumzia hapa na anaikataza hapa, nikajiuliza na bado najiuliza kama waumini wake wako nchini hapa na nchi nyingine haya mambo yalivyoanza nchi nyingine kwa nini hakuzungumzia nchi hizo? Kwa nini linakuja kuzungumziwa hapa leo? Kweli yeye Kanisa lake ni kubwa lakini chanjo zimeanzia nje ndiyo zikaja hapa, kwa nini hakukataza kule kwa nini anakuja kukataza hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili la chanjo katika nchi yetu ni hiari mtu uamue uchanje au usichanje lakini anapolitamka yeye na analitamka kwenye nyumba yake ya ibada au kwingineko anakataza, anapokataza anakwaza, anapokwaza ni kwamba anamnyima mtu uhuru wake. Unaposema imani ni kitu very sensitive, imani yako ndiyo inakupa wewe ujisikie unajiamini na unakuwa huru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kujadili jambo hili kwenye Kamati mengi yamezungumzwa na Mwenyekiti wangu na mimi ni sehemu ya yale yaliyozungumzwa. Jambo gani limenifanya nisimame na kuomba kuchangia ni kwamba mtu mmoja au watu wachache wasiingilie uhuru wa mtu. Wahenga walisema hiari yashinda utumwa ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipotuambia tuchanje alisema hiyo ni hiari yenu hatukulazimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa inatia uchungu, inakera na unajua kwamba mimi nimesimama hapa kama kiongozi wa wanawake nikijua jinsi gani wanawake wanaimani na wanapenda kusikiliza viongozi wao, tutakavyobweteka tukasema ameongea kiongozi yule tusijilinde, tusilinde wengine tunakwenda kuhatarisha familia zetu. Naunga mkono adhabu zilizotolewa kuhusu shahidi huyu kwa sababu yeye alitukwaza alipokuwa akisema kwamba anazungumza kwa kuoteshwa au kwa kufuata Roho Mtakatifu. Mimi ni Mkristo Roho Mtakatifu ndiyo tunavyobatizwa, tunabatizwa kwa maji na Roho Mtakatibu. Huyu Roho Mtakatifu asiyetaka utakatifu anataka vitu basi huyu siyo Roho Mtakatifu bali Roho Mtakavitu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni suala la Shahidi Mheshimiwa Jerry Silaa, haihitaji rocket science kuzungumza na kusema kwamba mshahara unakatwa kodi. Kodi ni kitu ambacho kiko kwa mujibu wa sheria na kuna kodi nyingi sana katika nchi hii na hii kodi ya mshahara ipo. Wabunge wanalipwa mshahara kama public servants na Pay As You Earn inakatwa, sasa sioni ni kwa jinsi gani mtu mwelewa kama Mbunge anakwenda kwenye mikutano yake ya hadhara anapigiwa makofi, anapata mihemko na anazungumza zaidi ambavyo angetakiwa.

Mheshimiwa Spika, nasikitika sana kwamba Mheshimiwa mwanangu huyu alisema hatukatwi kodi na aliulizwa, je, wewe ulikuwa unakatwa kodi ulipokuwa Mstahiki Meya? Akasema yeye alikuwa anapata posho na alikuwa hakatwi kodi. Sasa kama hivyo ndivyo kwa nini wakati ule hakuliona ni tatizo amekuja kuona ni tatizo leo hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu unakaa unajiuliza Bunge hili lilianzishwa miaka mingi nyuma toka enzi za mkoloni na yanayofanyika hapa yalikuwa yanafanyika, kwa nini hao wote waliopita miaka hiyo hawakuona, inakuja kuonekana leo, unajiuliza hapa kuna jambo gani? Kwa nini limeleta simanzi na taharuki? Unajiuliza hivi hii ni sawa, tunyamaze? Hatukuweza kunyamaza, naunga mkono adhabu zilizotolewa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai kwetu sote na utashi wa kujadili maendeleo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa juhudi nyingi za kuendeleza sekta hii, Naibu Waziri, Katibu Mkuu Mifugo, Katibu Mkuu Uvuvi na wakuu wote wa Idara na vyuo husika kwa kazi nzuri. Natoa shukrani kwa kampuni ya Asas, Iringa na Tanga Fresh, Tanga kwa ukarimu wa kutunywesha maziwa yao leo.

Mheshimiwa Spika, leo nitazungumzia ufugaji wa kuku wa kienyeji. Awali ya yote naomba ufafanuzi wa takwimu za mifugo ya nchi hii, iliyotolewa ukurasa wa nne aya ya 10. Hivi takwimu hizi zinapatikana vipi au ni za kwenye mashamba ya Serikali tu? Mimi ni mfugaji mdogo lakini sijawahi kutembelewa na afisa yeyote anayefanya sensa ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, kwenye ukurasa wa sita mwanzo tunaelezwa kuwa kuku wa asili wameongezeka kutoka milioni 38.2 hadi milioni 38.5, hii ina maana kwa mwaka mzima ni kuku 300,000 tu wameongezeka. Tatizo ongezeko ni asilimia ndogo sana na ukizingatia kuwa kuku hawa wa asili ni rahisi sana kufuga kwani wao wana scavenge in their own na ni msaada kwa akinamama wa vijijini na vijana wetu wanaomaliza shule ambao hawana ajira. Mfano hai tumeona kwenye mradi wa TASAF. Swali, Serikali ina mpango gani kuwa na local chicken gene bank?

Mheshimiwa Spika, toka nimeingia Bunge hili la 11, kila mara namsumbua Waziri na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, jinsi ya kupata vifaranga hao wa kienyeji kwa ajili ya wanawake wa Kilimanjaro, lakini wananipa namba za simu ambazo hziajibiwi, ni lini sasa nitapatiwa vifaranga hao?

Mheshimiwa Spika, tatizo uchanjaji wa mifugo; ni takriban miaka 58 tangu tupate uhuru, lakini ugonjwa wa mdondo ukurasa wa sita, aya ya 16 inayosomeka mpaka ukurasa wa saba imeelezwa vizuri sana. Ni kwa nini Serikali haifanyi mass vaccination? Naona kwamba ni vyema chanjo hiyo na chanjo nyingine zote zikatolewa bure.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya vipaumbele katika mpango na bajeti 2018/2019 ni pamoja na kudhibiti magonjwa ya mlipuko na magonjwa ya kipaumbele (page 13:iii) ni kwa nini isiwe kuondoa kabisa magonjwa hayo ili watu wa hali ya chini wafuge kuku wa kienyeji bila hofu?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kutukutanisha tena hapa tuzungumzie Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2021/2022-2025/2026, uliobeba dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wetu sisi wote tumeletwa na watu humu ndani, na sisi wenyewe ni watu na mahitaji watu waliotutumia waliyonayo ni sawa na tuliyonayo. Naipongeza Serikali kwamba hatukuwa tumesimama tukipiga mark time bali toka ule mpango wa miaka mitano mitano ulipoanza mambo mengi yamefanyika; barabara zimejengwa, maji yameboreshwa, elimu imekwenda mbele, lakini kiubinadamu tu jambo likishatekelezeka halina motisha tena. Alisema guru wa management, once a need is satisfied it’s no longer a motivation. Na hilo ndiyo linatufanya kila siku tuone kwamba kuna jambo la kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naanzia pale kwenye viwanda, na ninazungumzia kwenye viwanda katika mpango wamepanga kuzuia au kulinda viwanda ambavyo vinaagiza vitu kutoka nje ili vile vya kwetu vinavyotengenezwa viweze kupata soko na pia viboreshwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nitakwenda moja kwa moja kwenye viwanda vya sukari. Sukari ni bidhaa ambayo inahitajika na kila mtu, na sasa hivi ninavyozungumza ni siku chache tu wenzetu Waislam watakwenda kwenye Mfungo Mtukufu wa Ramadhani, na sukari ni bidhaa ambayo inahitajika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na sukari siku zote imekuwa mfungo huu unatokea wakati ambapo viwanda viko kwenye maintenance na vitafungwa au vimeshafungwa kwa ajili pia ya mvua. Lakini sukari hiyo mpaka mwaka jana ikifika wakati huu sukari inaadimika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi tumezungumza hapa; Serikali inafanyaje sasa kuhakikisha kwamba sukari haiadimiki tena. Kumbukumbu zangu zinanikumbusha kwamba Waziri wa Kilimo alisema mwaka huu shida hiyo haitakuwepo. Na namuomba Mungu shida hiyo isiwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kama haitakuwepo ninachotaka kusema kuhusu viwanda vya sukari ni nini; kwa kuwa shida kubwa inayotokea ni kwamba wale wanaoagiza sukari wanasema wanaagiza sukari ya viwandani, ile sukari nyeupe nyembamba ile na siyo sukari ya kula watu, wao waagiza industrial sugar. Lakini unakuta kwamba wanachanganya humohumo na kuja kufanya repacking.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoomba, Serikali sasa ione kwenye mpango huu inaboresha au inawasukuma hao wenye viwanda vya sukari hiyo sukari ya viwanda itengenezewe hapa hapa nchini. Tuna viwanda vingi vya sukari vikiwemo TPC, Kilombero, Mtibwa Sugar, vingine wamesema vinakuja Bagamoyo, vingi tu. Sasa naomba kabisa kwenye mpango huu tuelezwe ni viwanda vingapi vya industrial sugar vinakwenda kufunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu nimeona mambo yanayohusu utawala bora lakini sikuona utawala bora kwenye ngazi ya chini; tuna watendaji wa vijiji, tuna watendaji wa kata. Watendaji hao ni watu muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku, watendaji hao ndio wanaoishi na wananchi wetu, watendaji hao ningetaka iandikwe watapewa elimu. Na wanapewa elimu gani; elimu sasa ya kuweza kujenga kanzidata kuhusu mambo yanayofanyika kwenye maeneo husika yakiwemo yale ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila aliyesimama hapa amezungumzia kilimo, nitazungumzia kilimo kivingine, ya kwamba tuwe sasa na database ya kujua ni mazao gani yanayolimwa kwenye eneo fulani na ni ukubwa wa eka ngapi yanalimwa? Na ni wakulima wangapi wanalima mazao hayo, na yanavunwa kiasi gani. Wakati huo tukiwa na rekodi hiyo, Serikali inakuwa tayari ina rekodi ya kutafuta masoko. Wanatafuta masoko na tukishapata haya mazao wanakwenda sasa kuuza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna changamoto moja; kijijini wakishavuna wanakwenda likizo. Wamevuna wanafanya sherehe, kwingine wanaweka kidogo akiba, hakuna kuunganisha sasa nini kinafanyika, wanakaa hivyo mpaka msimu mwingine. Na ukizingatia kwamba sisi kilimo chetu kinategemea zaidi mvua za msimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali yangu sikivu iangalie sasa baada ya kilimo – na sasa hivi kuna vijana wengi ambao wako vijijini; wako waliomaliza form six, wako waliomaliza chuo kikuu na pia wazazi wao – watu hao wanawekwa katika zoezi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda tu nitoe mfano kidogo wa kule Libya alipokuwa, Hayati sasa, Muammar Gaddafi. Yeye alikuwa vijana wakifikia rika fulani kama anakwenda kupata mwenza basi anamzawadia dola 5,000. Sisi Tanzania hatuna hizo petrol dollars lakini Mungu ametubariki kuwa na eneo kubwa, tuna ardhi kubwa na vijana hawa wangeweza kabisa wakafunguliwa maeneo wakapewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo lazima kama umezaliwa kule ulikotoka hakuna maeneo, basi watoke kule waende kwenye maeneo mazuri. Hata kama watakuja Mbeya, kule Rungwe kuna maeneo mazuri tu, au Sumbawanga, wakagawiwa maeneo mazuri wakafungua mashamba ikajulikana ni batch gani, ni mashamba yapi wakaenda wakalima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana hawa wakishalima mashamba hayo wanafungua sasa ukurasa mpya wa kilimo cha wasomi. Ninaomba sana mpango huu uweze kufikiria namna ya kuwafungulia au kuwatawanya vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliposimama kuzungumza yalikuwa yanazungumziwa mambo ya michezo. Naomba niliendee vingine, naona huku ndani Waheshimiwa wanazungumza timu zile kubwa tu za watani wale wawili. Sasa hao wachezaji mnaowajua wakishaondoka - sitaki kuwataja majina maana yake mnaweza mkacheka, japo nina timu yangu fulani – ni lini sasa sisi tulio hapa ndani na Serikali kwa ujumla, Wizara ya Habari na Utamaduni, itashuka chini kule kwenye kata tuwe na timu za kata? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na isiwe kazi ya Mbunge tu, Serikali ipeleke wataalam, tuwe na timu za wilaya, tushindanishe watu. Hapa ni mtu mmoja tu anayefahamika ikitajwa inajulikana ndiyo kule kwake, inaitwa Namungo eeh? Eeh, Namungo tu ndiyo inayofahamika hapa, labda kwa vile kiongozi huyo alikuwa refa. Sijasikia, naskia wananitajia Singida na nini lakini sijasikia Nkasi, sijasikia Mbeya. Ila nikupongeze, umewatoa Mbeya kimasomaso kuna Tulia Marathon. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nawaomba, Waheshimiwa kila wakati wanachukua jezi kupelekea wachezaji wao, lakini hatujazisikia timu zao. Mpango huu kwa kuwa michezo ni ajira basi ishuke chini, tuandae vijana wetu toka utotoni wakue wakijua michezo na waendelee kuboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kumekuwa kuna shida na ugomvi mkubwa kuhusu TARURA, na kilio, TARURA, TARURA. Lakini kwenye mpango sikusikia Mfuko wa Barabara. TARURA inajenga barabara, ikishajenga inaacha, kuna Mfuko wa Barabara ambao ndiyo unaotunza barabara, ulikuja hapa Bungeni mkautungia sheria. Tutagombana hapa na TARURA lakini tunamgusa ambaye siye. Hebu tutafute chanzo cha ugonjwa kiko wapi. Naomba mpango huu utueleze kuhusu Mfuko wa Barabara, hela zile zimegawanywa vipi au zinakwenda kwa jinsi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Mfuko wa Maji; tumesikia ujenzi miundombinu ya maji lakini hatujui ule Mfuko wa Maji unakwenda vipi. Mtandao wa maji safi na salama unakwenda kasi, lakini mtandao wa maji taka hatuusikii ukitajwa. Itakuja siku, na sasa hivi hizi mvua zikituvuruga kidogo tu ukipita kule Jiji kama Dar vinyesi vinaelea juu kwenye zile barabara za halmshauri/jiji, wanachomekea kule ile mipira inatokea. Ninaomba mpango huu uelekeze sasa mnapotaja maji mtaje maji safi/ salama na usafi wa mazingira… kengele ya ngapi?

NAIBU SPIKA: Ya pili.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kipekee namshukuru Mungu wote kuwa hapa na pia nakupongeza kwa kuwa wa matokeo Result Oriented Speaker. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona kuna kila sababu ya wote tulio hapa tumshukuru Mungu kuzaliwa Tanzania, nchi ambayo imezungukwa na vyanzo vya maji kila upande, tuna Lake Victoria, Lake Nyasa, Lake Tanganyika, kuna Bahari ya Hindi lakini katikati ya Tanzania yetu kuna mabwawa mengi ya maji, kuna maeneo mengi ya milima. Vyote hivyo ni vyanzo vya maji na sioni kwa nini Watanzania miaka nenda rudi tunalalamika hatuna maji hatuna maji. Niseme tu kwa kifupi maji tunayozungumzia hapa ni maji safi na salama na usafi wa mazingira kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, miaka ya nyuma kwa wale ambao wana umri wangu au zaidi watoto walikuwa wanazaliwa wakikuwa wana meno ya brown, lakini sasa hivi kila mtanzania akikuchekea ana meno meupe kwa sababu maji hayo yametibiwa na Serikali yetu iliona ni vyema basi kupunguza ile fluoride ili watu wote wanywe maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna shida, wataalam wetu wako wapi pamoja na vyanzo vyote hivyo vya maji? Jangwani kwenyewe, mfano ukienda Dubai maji yapo, sasa Egypt maji yapo, sisi urafiki wetu na nchi hizo uko wapi? Kwa nini tulalamike maji, maji na tutenge Mifuko ya Maji kila wakati tuje, hapa tu-ring fence hela. Naiomba Wizara hii akiwemo Mheshimiwa Awesu, kijana anayependa kumtua mama ndoo kichwani na anayezungumza sana nchi hii haina ukame, tuone sasa tumefikia muafaka.

Mheshimiwa Spika, nianze kushukuru kwa ule Mradi wa Maji wa Mwanga, Same mpaka Korogwe ambao sasa ikifika Desemba kila mahali patakuwa na maji. Hata hivyo, niseme wazi, nimetokea Kilimanjaro ambako tuna mlima mzuri unaotiririsha maji, wengi wanapenda kuolewa Kilimanjaro au kuoa Kilimanjaro kwa ajili ya yale maji. Tatizo ni tambarare ya Kilimanjaro hatuna maji, ukienda Rundugai hakuna maji, tambarare yote hiyo. Tunaomba sasa Waziri wetu aje atembelee maeneo hayo ili pia naye atupe solution. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo success stories za Mamlaka ya Maji Safi na Salama, wewe ni shahidi ulikuwepo hapa miaka hiyo, mkipitisha Sheria za Mamlaka za Maji, tumeona kuna ushindani na tumeona mafanikio katika miji, maji ni salama, miji mingi tu ikiwemo Dar es Salaam, Moshi, Musoma kule Mara. Huko kote nilikozungumza hao Wakurugenzi walipita Moshi wakajifunza, wakaenda sasa kupeleka huo utaalam kwingine na unakunywa yale maji yakitoka kwenye bomba moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba umefika wakati, baada ya kupunguza kiwango kikubwa cha yale magonjwa ya maji ikiwemo cholera (kipindupindu), sasa tuone kwamba ni haki na siyo ombi tena Wizara hii ya Maji ijue kwamba mwanamke anatakiwa afungue bomba la maji ndani ya nyumba yake na siyo kumtua tu ndoo na kuanza kubeba kwa mkono, hapana kila nyumba iwe na maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba Wizara hii inapata hela nyingi sana na pia ina wakandarasi wazuri na kelele zinapigwa, lakini wewe ni shahidi kila anayesimama hapa anasema maji hayatoshi. Nataka atakapokuja kuhitimisha Waziri aseme, tumefikia kiwango gani siyo hiyo 95 kwa miji na 75 kwa vijiji tu, kwa sababu maji yote yanaanzia vijijini, hakuna maji yanayoanzia mjini kwa nini kule vijijini asiagize RUWASA kila kijiji yanapoanzia maji lile bomba litoe kwanza maji vijijini halafu ndiyo litoe mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hainiingiii akilini maji yanaanzia kwangu halafu wanaofaidi ni mjini, ina maana wale watu wa mjini ndiyo wanayajua maji na ijulikane kwamba maji hayana mbadala, huwezi kuchukua soda, ukachukua K-Vant au ukachukua kinywaji chochote ukafulia nguo wala kuoga, maji hayana mbadala kabisa, kiu ya maji ni ya maji na matumizi ya maji ni ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme pia Serikali itoe elimu; maji haya safi na salama yanatibiwa kwa hela nyingi sana, lakini maji hayo hayo utayakuta ndiyo yanayoosha magari, maji hayo hayo ndiyo yanafanya kazi za hovyo zile inamwagilia bustani na kadhalika. Kwa nini tusipige hatua maji ya kunywa na kupika yawe ni tofauti na maji ya matumizi mengine yawe ni tofauti. Wengi mmetoka nje kuna mabomba mawili bomba moja ni la kunywa tu lingine ni ya kuoga na mambo mengine yale yale yanazunguka na yanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linguine, naona wasomi wetu pia hawachangamshi akili vizuri. Kuna lile Mindu Dam Morogoro, limekuweko siku nyingi na lime-solve matatizo mengi, lakini ukija katika hii barabara kabla hujafika Kongwa pale Kibaigwa maji yanakata mpaka yanavunja barabara, kwa nini kusiwepo na Dam lingine likakinga maji hayo yanayotoka huku Simanjiro yakatengeneza Dam linguine, ina maana wazee wale wa zamani walikuwa na akili kuliko sisi? Wasomi hawa walikuwepo, kwa nini maji yaharibu barabara tu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kipekee namshukuru Mungu kwa siku ya leo na zaidi sana niseme nafurahi na ninawashukuru wageni kutoka Kilimanjaro kwenye Jimbo la Mheshimiwa Profesa ambao wale kwa kweli ni mabosi wangu kazini. Na leo wataniona nikichangia live mubashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze sana Profesa kwa hotuba ya kurasa 143 ambayo imesheheni kila jambo la kilimo. Na niseme kwamba, yote ni mazuri, lakini sasa sisi tunafanya nyongeza na maombi. Naona kabla sijasahau nianze na maombi, wametaja vitu vizuri, mbegu za maparachichi, wametaja mbegu za alizeti, wametaja mbegu za maharage, yote hayo yametajwa hapa ndani, lakini hayajatufikia hata kule Rombo hayajafika.

Mheshimiwa Spika, sasa niombe kupitia kwako tuweze kupatiwa mbegu hizo. Maparachichi yale nikayasambaze haraka sana na mbegu zote ambazo ni nzuri, lakini zaidi sana watupatie mbegu ya kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TACRI iko Kilimanjaro unaifahamu, lakini tunaambiwa kwenye hotuba waliosambaziwa mbegu za bure ni wakulima 220 tu; ni wachache ni tone tu la maji kwenye bahari. Naomba sasa ikiwapendeza watusambazie mbegu hizo, wamekua wakiitisha sana semina hapa za wakulima, lakini wakulima wa Kaskazini wa kahawa hatujafikiwa. Kwa hiyo, tunaomba elimu hiyo, ili tuweze kwendanayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwamba, sisi Tanzania tumekuwa na baraka miaka mitano iliyopita hatukuwa na njaa na mpaka tumegawa chakula na tulizalisha zaidi asilimia 126, hiyo ni neema pekee. Kwa hiyo, tulipata shida ya mafuta na kama tulipata shida ya mafuta mwanamke hawezi kutofautishwa na mafuta ya kupika, pale ambapo huna chochote cha kupika unatupa kitunguu kwenye mafuta unafunga mlango, watoto wanasikia kikiungua wanadhani unapika pilau kumbe hamna kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ninawaomba hii mbegu ya alizeti waliyoizungumzia isambazwe kote kwenye kaya zote Tanzania, kila mwanamke akizalisha debe moja la alizeti tumejikomboa, hatutangoja mafuta kutoka bandarini yanayoshushwa ambayo ni ya kiwango cha chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ametueleza katika vipaumbele vyake, ameeleza Mheshimiwa Waziri kwamba, anatamani kuona alizeti inazalishwa kwa wingi na hapa Dodoma kutakuwepo na mashamba ya mfano. Na nawaombea Wabunge wote wapate eka mbili-mbili hapa Dodoma, hapa kwako, ipitishwe kwenye halmashauri yako tukalime hiyo alizeti yawe mfano. kila Mbunge awe na shamba, asiwe tu Mbunge wa kuongea kwenye karatasi, haitusaidii sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa vile wewe ni diwani wa huku nakuomba sana utufikirie Wabunge wenzio tuweze kwenda kulima. Kwa sababu, amesema mbegu hiyo nzuri ya RECORD ya alizeti mpaka sasa imesambazwa kwenye mikoa mitano tu ikiwepo Mbeya na hiyo iko kwenye ule ukurasa wa 31, Kigoma, Dodoma mpo, Morogoro na Singida, huko kwingine je?

Mheshimiwa Spika, natamani kuona kila kaya. Na haya mafuta yaitwe, ikimpendeza sana Mheshimiwa Waziri, amuombe mama Rais Samia Suluhu Hassan, Jemadari wa nchi hii, aweze kuitwa mafuta yake yaitwe Samia. Tumechoka kula mafuta ya Korie na ya nini hayana viwango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninalotaka kumuomba tu Waziri wetu wa Kilimo, Profesa Mkenda, ni kuhusu kilimo hai (Organic Agriculture). Organic agriculture au mazao yanayozalishwa kwa kilimo hai yamekuwa na bei kubwa sana nchi za nje. Kahawa inayozalishwa katika viwango hivyo inafika hata kilo moja shilingi 10,000 ambapo bei ya kawaida Arabika Coffee ambayo ni nzuri kabisa ni shilingi 4,000. Na ninazungumzia Arabika Coffee kwa sababu, Kahawa ya Arabika Kilimanjaro sisi tunalima Arabika na tunalima katika tambarare ya Mlima Kilimanjaro ambayo ardhi yake imepata volcano kidogo. Ndio kahawa ambayo ina-blend kahawa zote duniani ili kuipa aroma nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sasa kahawa hii watu baada ya kuona ni shida sana kulima wameamua kung’oa ile kahawa na sasahivi watu wanalima ndizi badala ya kahawa. Nimuombe sana Profesa atusaidie na ana Katibu mzuri tu, Katibu Mkuu mzuri ambaye anayajua hayo maeneo, tuweze kurudisha tena hili zao la kahawa katika njia yake nzuri kwa sababu, wengi wa miaka hiyo wamesomeshwa na zao la kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bahati ya kahawa ya arabika unaweza kuotesha mazao mengine, ni inter- cropping. Kwa hiyo, haizuwii ndizi kuoteshwa, haizuwii maharage kuoteshwa, haizuwii mahindi kuoteshwa. Kwa hiyo, kwenye kahawa hizo unaweza ukalima mazao mengi na ikawa ni faida kwa familia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nazungumzia hivyo kwa sababu, natoka eneo ambalo watu mashamba yao ni kidogo na yanaitwa vihamba. Kihamba kikubwa kabisa tena cha tajiri ni eka saba, sasa wengine wote ni eka tatu, mbili na moja na nusu na wote wanategemea hayohayo. Nimewaona wadau wa kilimo hapa, nimemsikia Jaqueline yupo, tunaomba basi afike na watusaidie tulime kahawa hizo pamoja na haya mazao ya horticulture. Zao mojawapo ambalo naliomba sana ni zao la parachichi, lakini pia tunaomba hata hii migomba yetu iweze kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakubaliana na mimi kwamba, zao la mgomba linavunwa mwaka wote mzima, yani vijana wanakwambia 24/7 annually. Kila siku ndizi inakatwa na ndizi itaota, lakini unakuta sasa wasipopelekwa vizuri katika kulea migomba hii inatoa mikungu midogo sana ambayo haina tija. Nilikuwa naomba sasa ili kilimo hiki kiweze kuwa cha tija, tuweze kupatiwa mbegu ambazo zinatoa mikungu mikubwa, lakini pia tuweze kupatiwa maafisa ugani ambao watakuwa kama wale wa zamani; maafisa ugani wa zamani walikuwa wanajua kaya fulani ina migomba mingapi, kaya fulani ina kahawa ngapi, kaya fulani inazalisha kiasi gani na kwa pamoja sasa ndio inaweza kuleta summation, yaani junla ya mavuno yote ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kuna mazao ambayo yapo tu siku zote, ni kama mazao ya mtama yanalimwa kidogo sana kwenye tambarare, lakini muhogo umekuja na sisi wachaga tunaogopa mihogo kwa sababu, mihogo tunaogopa ina sumu, lakini nasikia kuna mihogo mizuri imekuja ambayo ni salama.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ah sante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kipekee namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai. Niunge hoja mkono nisije nikasahau kwa sababu hii Wizara ni muhimu sana kwangu japo siku zote naishia kuomba kuomba, lakini wananchi wangu hawafikishiwi maombi yangu wala hawajibiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo ni Wizara ambayo kwa kweli kila mtu anastahili kuwa karibu kwa sababu, sisi kina mama tukishajifungua siku hizi unaambiwa miezi sita wasinyonyeshe, lakini baada ya hapo mtoto anaweza akapewa maziwa mengine kidogo; na kama wewe ni Mtanzania mzuri, basi utamchanganyia maziwa ya ng’ombe au kama kuna wale wenye mbuzi wazuri, maziwa ya mbuzi kidogo, mtoto anaendelea kunyonyeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara chache sana utakuta mama wa Kitanzania anapenda maziwa ya unga. Sasa naomba kuiambia Wizara hii kwamba, hiyo mifugo tunayohesabiwa kwamba iko ranchi, ng’ombe milioni 33, lakini sasa tunaambiwa ng’ombe wa maziwa ambao ni mitamba itasambazwa milioni moja na ushee. Sasa naangalia, hivi hiyo milioni moja na ushee itakayosambazwa Tanzania kwa ruzuku, itawafikia wafugaji wangapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hiyo figure iangaliwe vizuri, kwa sababu Kilimanjaro, wakati amekuja kuzindua kampeni, Waziri Mkuu aliombwa; tunaomba mitamba ya ng’ombe, tunaomba mbuzi wa maziwa na pia aliombwa, vifaranga wa kuku wa kienyeji kwa kila mwanamama. Huko Kaskazini Kilimanjaro sisi hatujui kusweka ng’ombe, wanafuga kwenye zero grazing. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwombea sana Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mungu amlaze mahali pemba Mbinguni kwa sababu peke yake ndiye aliwafanyia wale watu wakafuga kwa faida kwenye miaka ya 85 mpaka 87. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alitoa mitamba bora na leo nimemsikia hapa ametajwa Mheshimiwa Kimiti, alikuwepo kwenye Bunge hilo. Mitamba ile ikasambazwa ndiyo wakabadili kutoka kwenye ile indigenous breed wakaja kwenye hybrid. Kuanzia wakati huo, wakaweza kukamua maziwa lita 20 kwa ng’ombe mmoja kutoka lita mbili kwa ng’ombe. Sasa, ni kipindi kirefu na mpaka sasa wameshapoteza ile mbegu. Kwa hiyo, uzalishaji umeshuka, namuomba sana Waziri wa Mifugo ambaye amezoea ng’ombe wengi lakini sijui wanakamua kiasi gani atufikirie tena Kaskazini tupate hiyo mitamba mizuri. Kopa ng’ombe, lipa ndama! Na hapo ndiyo tutaweza kuboresha tena mifugo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kama zoezi hilo litafanikiwa basi hata uchumi wa wananchi kule utabadilika. Lakini sio hiyo tu kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa. Hata hawa ng’ombe wanaofugwa nje, nadhani hali sio nzuri. Ng’ombe ana kilo 100 hadi 120. Ng’ombe mzuri anatakiwa awe na kilo 300, mzungumzaji aliyezungumza kabla yangu ameeleza vizuri sana na mimi nasisitiza kwamba ni bora sasa tukaingia katika ufugaji wa tija kuliko ufugaji huu wa kuangaliangalia tu kubahatisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii nihame sasa kwenye ng’ombe lakini nimalizie kwa kusema ng’ombe wakiwepo nyumbani tunapata samadi ambayo inaboresha mashamba yetu ikiwemo kahawa. Ni juzi tu kimefunguliwa kiwanda cha viatu vya Ngozi pale Karanga. Tunategemea ng’ombe hawa hawa wa Tanzania watupe Ngozi nzuri na sio tukaagize ngozi kuja kutengeneza viatu hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie sasa kwenye eneo ambalo nina passion nalo. Kuku wa kienyeji. Niwapongeze sana ALVI wameweza kuja na mbegu ya Horace, katika ule ukurasa wa 11 tumeelezwa ambayo itaweza sasa kutengeneza kuku wa asili ambao ni wazito na ambao wanaweza wakatoa kilo nyingi na mayai mengi.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Ninachoomba tu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shally subiri taarifa ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO; Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri anaotoa mama yangu Mheshimiwa Mbunge pale. Kama ilivyo na ndizi Moshi, Bukoba, mchele wa Kyela na Shinyanga kuku wote wale anaowasema wa kienyeji ni kuku wa Singida na Dodoma, hiyo ni Fahari ya Makao Makuu. Akisema wa asili inaanza kuonekana kama dawa ya kienyeji hivi. Kwa hiyo, aseme kuku wa Singida na Dodoma. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Shally.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea Taarifa, lakini nataka tu nimwambie kwamba kisayansi hilo jina la mkoa alioutaja bado halijaingia na nachangia kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri na haya majina ninayoyatamka ndiyo yaliyoandikwa. Lakini, Tanzania tunajua. Hata ukifika Chako ni Chako unauliza kuku wa Singida wapo, lakini kwenye vitabu bado kuku wa Singida hamna. Kwa hiyo nishukuru sana kwa hilo na atakapopelekewa maombi kwamba anigawie kidogo ili wafike kule Kilimanjaro basi asiwe mchoyo kwa vile yeye ndiyo mwenye fungu lote lile la fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pia pongezi kwa ugunduzi wa chanjo mpya inayoitwa tatu moja. Chanjo hii iko kwenye ule ukurasa wa 37 ni ya kuzuia magonjwa matatu, mdondo wa kuku, ndui ya kuku, mafua ya kuku na hiyo dose kichupa kimoja cha shilingi 6,800 kinatibu kuku 200. Kwa hiyo, mtu wa kawaida akinunua kichupa kimoja amemaliza kazi. Kwa hiyo, naomba sana kwa kweli niwapongeze watafiti hawa walioweza kuleta chanjo hiyo na hivyo basi niseme nmtakaopatiwa vifaranga hao kwa wale wanawake wa Kilimanjaro hata hatutakuwa na uoga wa maradhi ya kuua hao kuku. Pia tutapata samadi ya kuku au inaitwa kinyesi cha kuku lakini mbolea ya kuku kwa ajili ya mashamba yetu na bustani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme wazi, hakuna bajeti iliyopita hapa, huu ni muongo wangu wa tano bila kuomba vifaranga hivyo. Swali nimeuliza nikaambiwa nikanunue hivyo vifaranga kwa shilingi 2,500 bei ya ruzuku. Sasa sitaki wa kwangu, nataka Wizara ifanye pilot scheme mkoani Kilimanjari akina mama wale wafuge kwenye nyumba zao na pia iweze kufanana katika hali ya ufugaji wa kawaida. Nimechoka kusikia tunahesabiwa mifugo iliyo kwenye mashamba darasa, iliyo kwenye ranch, sasa inafanya nini huko? Yaani tutaje figures za nini? Niseme wazi kwamba kwa kweli…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, oh! Basi niulize tu swali moja. Nilikuwa na swali moja ili nisije kusema nashika shilingi nikakosa hata haya mambo ninayoomba. Bodi ya Wizara kwa umoja wao mwaka huu walitoa gawio la shilingi 348,940,989 ukilinganisha na trilioni 1.5 iliyotolewa mwaka wa 2019 ambayo ni anguko la asilimia 77. Ni nini kilichosababisha hiyo? Nilidhani sasa wangetoa gawio kubwa lakini wameshuka. Naomba watakapokuja kujibu nijibiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono tena. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kutujaalia uzima na ninawashukuru sana wanawake wa Kilimanjaro walionipa hii nafasi ya kuja kuwasemea Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa moyo wa dhati kabisa niipongeze hii Wizara ya Maliasili na Utalii. Kipekee nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro; nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Mary Masanja; Katibu Mkuu, Dkt. Allan Kijazi na pia niwapongeze watendaji wote na vile vile niwashukuru wale wa Kamati iliyowasilisha hoja mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa sababu nilitaka tu kusema hii Sekta ya Utalii iko mahututi hospitali. Iko mahututi kwa sababu kwa kweli walipigwa na mambo mengi, lakini zaidi sana na UVIKO 19. Wote waliokuwa na biashara za utalii wanalia, maduka au ofisi zao zimefungwa na hata wale wanyama waliokuwa wanachangamka wakiona magari yanazunguka kule, wamenyong’onyea sana. Naomba Wabunge wote kwa pamoja na wananchi wote tuungane tuhakikishe tunairudisha hii sekta katika hali ambayo italeta faida tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Utalii inatuingizia nchi hii mapato (GDP) ya asilimia 21, lakini sasa unakuta yameshuka ghafla bila hata ile graph kwenda iki-dwindle, yaani imeshuka chup! Kwa sababu hali siyo nzuri. Hata hivyo ilianza kushuka, kama msemaji aliyenitangulia alivyosema baada pia ya mapato haya kwenda kwenye kapu kuu. Sasa jambo kubwa ambalo linatakiwa tukubali ni kwamba kuna mambo yanayofanyika hata kwenye hesabu, unafanya trial and error halafu kama haitekelezeki, yaani if it doesn’t work mnaamua sasa kusimamia njia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu uharibifu mkubwa wa barabara za kwenye hifadhi hauwezi kuja kuwapeleka watalii katika hali salama. Mtalii anapotoka kwao anataka hata akija kutembea au hata kama ni mtalii wa ndani, amalize route yake kwa siku. Barabara zile zimeharibika, kwa sababu hakuna namna ambavyo wanapata hela kwa haraka kwenda kuzitengeneza. Hii inakuwa siyo rafiki na haina afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za Serengeti zimeharibika, Manyara zimeharibika na hata zile barabara za kupanda mlima Kilimanjaro zimeharibika. Sasa hivi route ile, ule muda uliokuwa unatumika kupanda mlima umeongezeka. Bahati tu ni kwamba mvua imenyesha sana, hawapandi mlima sasa hivi kwa wingi, kwa sababu kila saa ni mvua na ukungu. Kwa hiyo, naomba tu, mvua zikisita, hela ipatikane kutoka Serikali Kuu, barabara zikatengezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata kile kibanda cha Mandare ambacho ni maarufu wanapotulia wale watalii wakifika kule juu, kiliungua na mpaka leo hakijakarabatiwa kwa sababu hela haijapatikana kwa urahisi. Hili siyo jambo zuri kabisa. Ukienda Afrika Kusini, ukiwa unataka kwenda Table Mountain, kile kifaa cha kukupeleka Table Mountain kinashughulikiwa kama vile ni jicho, kwa sababu ni utalii unaotangazika. Sasa sisi hata hii ya kupanda tu mlima inashindikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi mlima Kilimanjaro kunakuwa kuna ile rescue route; kuna wakati ambapo baada ya mvua kunakauka, mtu akiwasha kiberiti au sijui ni watu wale wabaya tu waharibifu wanawasha tu bila kujijua, basi inabidi waende waka-rescue. Barabara zile hazionekani tena na hakuna njia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata vyoo vile vya kwenye route haviko katika hali nzuri. Hivi Watanzania tuko serious kweli! Hii tumeipa Wizara na bado hawana hela na tunasema kwamba hii Wizara inatuingizia mapato. Mimi naleta hiki kilio hapa Bungeni, Waheshimiwa Wabunge, naomba mniunge mkono kila atakayesimama asemee hali ya kurudisha hii Wizara katika hali nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wao walikuwa wanatuingizia mapato ya nje asilimia 25 na hiyo iko katika utalii, lakini pia unakuta kwenye huduma za jamii wanatuingizia asilimia 60. Zimekwenda wapi? Ajira milioni 5.6 ni pamoja na wale porters, nachanganya wote; wale wanaobeba, wale waongozaji, wako huko huko. Sasa hivi nimesema nawasemea wale akina mama kwa sababu vijana wao wako nyumbani na wao, wanangoja mahindi yakomae wachome na mama zao. Vijana walikuwa hawakai ndani, wote wako njiani wanawasindikiza watalii. Naomba sana, hili jambo lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu, ni bahati mbaya sana kwamba sio Wabunge wote wamepata fursa ya kwenda kutembelea Mbuga za Wanyama au Hifadhi. Naomba ikikupendeza, wakati ambapo mnafikiria huko kwenye Kamati ya Uongozi, mtenge fungu kidogo tu, nasi Wabunge tutaongezea wenyewe, tuwe kama group la Wabunge, watalii wa ndani. Wenzetu huko nje wanafanya, kwa nini hapa nje ishindikane? Haina haja tuko hapa tunazungumza jambo ambalo hatulielewi wala hatuzungumzi pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walitutembelea Kilimanjaro, Wabunge walemavu. Walikuja, walihamasisha, waliwaleta ma-pilot, walikuwa wanaongozwa na Mheshimiwa Riziki Lulida, tulipanda nao mlima. Wale ni walemavu na tukaweza kupanda mlima na leo wanatutangaza huko nje. Leo asubuhi umetuambia Mabalozi wa Utalii wametutembelea wengi, sasa wataenda kutangaza halafu wakifika tutatembeaje? Naomba jambo hilo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu misitu yetu. Nimeona kwamba waliomba kifunguliwe chuo kingine cha misitu, lakini nakumbuka kulikuwa kuna Chuo cha Olmotonyi. Sasa naomba wanapokuja kujibu waseme kile Chuo cha Olmotonyi kiliendaje? Au hakiendi vizuri ndiyo maana kinatakiwa kufunguliwa chuo kingine? Maana iliombwa katika ile report ya Kamati ya Kisekta.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchangiaji wa kwanza alileta ugomvi wa mifugo na Mbuga za Wanyama. Nataka niseme hivi, Mungu alipoumba, aliumba kila kitu viwili viwili. Wanadamu waliumbwa wawili, simba wakaumbwa wawili; yaani wanyama, ndege na kila kitu na akasema enendeni mkazaane mwongezeke. Pia akampa mwanadamu utashi akatawale wanyama wote hao. Sasa leo tunawajua ng’ombe wetu walivyo na Tanzania wengi wanafuga ng’ombe wa kuswaga. Yuko Rais wetu mstaafu alisema mnaposwaga ng’ombe, mswagaji anakonda na ng’ombe wanakonda. Hivi kwa nini tusifuge hawa ng’ombe?

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba kama nchi yetu na Serikali za Mitaa zitoe maeneo ambayo yanatosheleza kufuga ng’ombe wakanenepeshwa tukawa ni wafugaji wazuri, tukawa na maziwa mazuri kuliko kuhesabu tu kwa idadi, kuliko kwenda kuingilia wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Naomba tuwapatie hizo hela wakarejeshe. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwanza kwa kumshukuru Mungu kwa kutupa uhai tuwepo hapa kuzungumzia suala la walimu na hii Bodi ya Kitaaluma ya Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu ni mtu muhimu sana katika maisha. Naamini kwamba ukitoka kwa mama mtu mwingine ambaye anakulea zaidi katika maisha ni mwalimu. Uwe ni mwanaume au mwanamke, mwalimu ni mtu ambaye anaheshimika na ndiye ametufanya hivi tulivyo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya ukiwauliza watu au wazazi mtoto wako unataka awe nani? Watakuambia zile kazi ambazo zinaingiza fedha nyingi. Ukimuuliza engineer atakuambia nataka mwanangu awe engineer, ukimuuliza daktari atakuambia nataka mwanangu awe daktari, ukimuuliza mfanyabiashara atakuambia nataka mwanangu awe Mkurugenzi na awe CEO. Ukimuuliza mwalimu, kwa vile anajua dhana halisi ya mwalimu atasema, natamani mwanangu awe mwalimu lakini hii fani siyo nzuri kifedha. Mwalimu anayeifahamu kazi yake, mwalimu aliyefundishwa somo la malezi, angetamani mwanae awe mwalimu kwa sababu hata katika wanawake bora nasikia ni walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi sasa kwenye Muswada na niende kwenye Sehemu ya Tatu inayozungumzia kuhusu registration. Kuna vipengele vingi vimeainishwa pale lakini naomba kusema kwamba kutokana na shule nyingi zilizopo nchini, shule za Serikali, shule za private na shule ambazo ni za kujitegemea tu tuseme, kwa kuwa na hii Bodi itasaidia sasa hata wale ambao wanakuja kutoka nje kuanzisha shule zao wajue wanapata walimu ambao wanakidhi vigezo na Serikali yenyewe ijue inapata walimu ambao wanakidhi vigezo. Kwa hiyo basi, kuwa na hii Bodi itasaidia ku-register walimu kutokana na qualification, aina zao za ualimu na ngazi zao na hata atakapokwenda kusoma naamini atakachoongezea kitamsaidia yeye kuongeza hata kipato chake atakachokuja kulipwa baada ya kusoma mafunzo anayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na aliyesema awali kwamba hii Bodi isishughulikie tu walimu wa shule za primary na secondary bali iende hata kwa walimu wa vyuo. Tunaelewa kwamba ili mwalimu wa chuo abakie pale chuoni kuwa Assistant Lecturer lazima awe ame-perform vizuri. Atakuwa amefaulu vizuri sana lakini atakuwa bado hana yale madili ya kiualimu na ndiyo maana yake wakishakuwa Assistant Lecturers ili ukawe lecturer lazima upitie kozi mbalimbali. Kwa hiyo, napendekeza kwamba walimu wa vyuo nao wafikiriwe kuingia katika Bodi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuangalia taaluma tu kwa mwalimu haitoshi na hapa katika Muswada wote haikuzungumziwa namna ambavyo mwalimu anaweza akatulia sasa akajifua, akaboresha ile taaluma yake. Hapa nina maana kwamba unakuta mwalimu yuko vizuri kitaaluma, lakini ana shida fulani fulani kutoka kwenye familia na anapoamka ili akafundishe mwanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nazungumzia katika zile Maslow Hierarchy of Needs, tuseme mojawapo shelter. Unakuta mwalimu ameamka kwenye nyumba duni sana anakwenda kufundisha wanafunzi ambao wengi wao wameamka kwenye nyumba bora, unadhani mwalimu huyu atatulia kweli ajiendeshe kitaaluma wakati ameweka mkono kwenye tama anafikiria akirudi nyumbani anaingiaje pale. Mwanafunzi anamsaidia mwalimu vitabu akifika pale hakuna hata mahali mwalimu anaviweka vile vitabu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Muswada huu ukipita ifikiriwe tena njia nyingine ya kuboresha maslahi ya walimu na kuwafanya wawe na settled minds. Nyumba za walimu ziboreshwe, mafao ya walimu yafikiriwe, mwalimu apewe mshahara ambao unalingana na kazi anayofanya. Mwalimu anaamka alfajiri kabla ya mtu yeyote kuwahi shule, kengele igongwe, apange watoto aingie darasani. Mwalimu atarudi wa mwisho, akipitia lessons lakini mwalimu huyo huyo ni yeye anafua watu kama hawa waliokaa hapa ndani, wote mmepitia kwa walimu lakini kipato chake ni kidogo kuliko wengine. Naomba sana Wizara ya Elimu iangalie hilo ili walimu waishi kwa raha, watembee vifua mbele na wakifikiria kugawa akili na uwezo wao ili tuweze kuwa na Taifa zuri ambalo linaweza kufikiri kimaendeleo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na madai ya walimu muda mrefu na hapa naichomeka hiyo pia wakati tunapowafikiria kuwatengenezea Bodi lakini tuitengeneze hii Bodi wakati madai yao yameshatekelezwa, wamelipwa mishahara yao, wana amani na nchi yao, wanaweza sasa kwenda kufanya vizuri. Tuna bahati kipindi tunachozungumzia sasa Kiongozi wetu aliyepo madarakani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa Mwalimu na pia mkewe Janeth ni Mwalimu, kwa hiyo, huu Muswada umekuja wakati muafaka kabisa, wakati ambapo watu waliopitia dhiki hizo wako katika madaraka na watawafikiria wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, pia naomba walimu wafikiriwe katika incentives, waongezewe au wawe wanapewa hardship allowance. Naamini kabisa mwalimu akipewa vitu vya kumpa motisha, hata wengine wanaokuja nyuma wasiopenda kazi ya ualimu wataikimbilia na Bodi kama hii itakuwa na maana, hakuna sababu kuizungumzia
Bodi ambayo inaenda kuzungumzia watu ambao bado wana malalamiko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda tena pale kwenye madhumuni ya Muswada huu ile Sehemu ya Tano inaweka masharti kuhusu malalamiko ya walimu. Malalamiko haya yamekuwepo miaka yote, siyo malalamiko ya kubuniwa na kwa vile sasa yanaenda kufika mwisho kwa kuwa na hii Bodi tunataraji basi tukiunga mkono wote Muswada huu ukapita basi kuanzia mwaka 2020 hivi wala hatutafika huko malalamiko ya walimu yatakuwa hayapo tena katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile Sehemu ya Saba inayozungumzia makosa na adhabu, makosa mbalimbali yaliyozungumziwa hapa yakiwepo ya kufundisha bila kusajiliwa na mengineyo, naomba nipendekeze kwamba siku za nyuma walimu hao walikuwa wanafundisha wakiwa na ma-inspector wanawapitia shuleni mara kwa mara, wanafunzi na walimu walijua ma-inspector wanakuja. Kwa hiyo, naomba katika kuboresha japo halitaingia kwenye huu Muswada, lakini ifikiriwe pia walimu hao wawe na watu wa kuwazungukia mara kwa mara, badala ya kuwafikisha kwenye adhabu wawe wameshajirekebisha kabla hilo jambo halijafikia wakati wa kupeana adhabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikuwa na mengi zaidi ya hayo, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namshukuru Mungu pia kwamba tupo hapa, tunajadili mambo haya mazuri. Ni muda mrefu sasa takribani mwezi wa tatu tupo kwenye jambo hili la bajeti, lakini jana imepita vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache ambayo nataka kuchangia. Ni wazi kwamba tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa mambo mazuri ambayo ameona yafanyike kipindi hiki kwa wananchi wake. Nianze na hili la kutokuwepo kodi kwa waajiriwa ambao wanapata Sh.270,000 kwa mwezi au Sh. 3,240,000 isiyozidi hapo kwa mwaka. Watu hawa ni wengi Tanzania hii, lakini watu hao kwa sasa au waajiriwa hao hawatadaiwa kodi hata kidogo. Kwa hiyo fedha hiyo itakwenda sasa kutumika vizuri katika shughuli zao na kipato chao kitakuwa kimetulia. Niwaombe waipokee hii kama tunu kwa sababu wote wanapodaiwa wa juu na chini inakuwa kwamba ile kodi sasa inawapunguzia kipato hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya CCM ni Serikali sikivu na ilipoona kwamba watu wamepanga sasa kufungua viwanda vya dawa imeondoa kodi kwenye vifungashio vya dawa. Sasa niwahamasishe wote ambao wanataka kwenda kufungua viwanda vya dawa, wakafungue viwanda vingi vya dawa ili matibabu yawe rahisi na kila mtu apate matibabu. Taifa lolote linalokwenda vizuri ni taifa ambalo watu wake wana afya nzuri na watu wenye afya nzuri ni watu ambao wanapata matibabu kwa gharama nafuu. Endapo hiyo kodi sasa imeondolewa, ina maana dawa hizo zikishapatikana vile vifungashio havichajiwi kodi, kwa hiyo watu wataweza kupata matibabu kwa gharama ambayo wanaweza wakaipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sio hayo tu, niseme wazi kwamba Waziri wa Fedha pamoja na timu yake akiwepo Naibu Waziri na Katibu Mkuu walikuwa na Kamati ya Bajeti kila siku wakihakikisha kwamba vifungu hivi vinapitiwa na vikija hapa vinakuwa salama. Hilo limekuwa hivyo na nichukue nafasi hii kuwapongeza sana kwa sababu bajeti hii ni bajeti iliyokubalika ndani ya nchi hii dunia nzima imeisikia na Afrika Mashariki imeisikia, tumwombe Mungu wote tuwe salama tuweze kuja kushuhudia matokeo yake kipindi kama hiki mwakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe jambo moja tu, wakati tukijadili bajeti hii, tulikuwa tumefikiria sana jinsi gani wanafunzi wetu watapata chakula kwa urahisi mashuleni. Hapa naona kwamba endapo sasa ile kodi itaondolewa kule kwenye mahindi yale, basi wazazi wengi wataweza kuchangia mahindi, maharage ili wanafunzi mashuleni waweze kupata chakula chao kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hainiingii akilini mwanafunzi anashinda kutwa nzima hajala chakula lakini naambiwa kwamba mahindi ni ghali kumbe mahindi yamejaa tele kwenye godauni. Kwa hiyo, niseme kwamba alivyozungumza Waziri leo kwamba jambo hilo amelifikiria na itakuwa salama kwenye kilimo, nimpongeze kabisa kwa sababu sasa mahindi hayo yanaenda kutoka katika bei ambayo inakubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, lakini pia tuliona kiwanda kikubwa cha kukamua mafuta ya alizeti kama ilivyo Singida ‘C’ kimepunguziwa kodi ili mafuta yale yaweze kupatikana kwa urahisi. Naamini kwamba hata vile viwanda vidogo vidogo, atakapohitimisha Mheshimiwa Waziri, atavifikiria viwanda vyote vile vidogo vidogo vinavyokamua mafuta ya alizeti ambayo tunayakuta barabarani wakati tumnasafiri na yenyewe yanaenda kuondolewa kodi na mafuta hayo sasa yanaenda kupatikana kwa bei inayokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo mafuta hayo yatapatikana kwa bei nafuu, hatutakuwa hapa tunasubiri mafuta yaliyo bandarini, mafuta ya majina ambayo ni ya kigeni sana na wote tutakwenda sasa kulima alizeti yetu tukijua kwamba tunakwenda kupata mafuta kwa bei ambayo inakubalika kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba kuna kesi nyingi ambazo zinakuwa zinasubiri mahakama, lakini Waziri ametueleza kwamba Kamishna wa TRA sasa ameweza kupata nafasi na kukaa na wafanyabishara wale wakubwa nje ya mahakama waweze kufanya mashauriano na kesi hizo ziweze kufanyika na kumalizika. Hili ni jambo jema, jambo hili halitakiwi kumsubiri Rais anavyotembelea mahali apokelewe na mabango au aweze kuitisha wafanyabiashara. Kama Waziri wa Fedha ameshatamka kwamba Kamshna wa TRA anaweza kuongea na watu hao nje ya mahakama, najua kwamba inaenda kupunguza kesi nyingi sana ambazo zimerundikana na watu hao watakuwa sasa hawana tena tatizo.

Sambamba na hilo hata wale wafanyabiashara wadogo ambao walikuwa wanafunga maduka yao kwa hofu ya kufuatwa fuatwa na TRA, sasa wanaweza kwenda kuongea na Kamishna na maduka yale hawatafunga wala hawatafunga biashara zao tena.

Kwa hiyo, nina uhakika Kariakoo inaenda kushamiri, wanakwenda sasa kufanya biashara zao vizuri, kwa sababu jinsi ambavyo alilielezea vizuri Waziri wa Fedha ni wazi kwamba watu hawa wamesikia ahueni, wanaenda kufanya kazi kwa nafuu na wanaenda kufurahia biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ambayo ambayo yalikuwa yanahusu Muswada leo, nilete habari njema kwenu wote. Niseme kwa uhakika kabisa Benki ya CRDB ina takribani bilioni tisa na ushee zimekaa hazijadaiwa na hizo ni gawio la miaka mingi kwa watu ambao walinunua hisa CRDB lakini hawajui kama walinunua hisa wala wababa wengine hawakuwaambia wake zao na wengine wameshatangulia mbele ya haki. Ninapozungumza bilioni tisa, bilioni tisa ukiweka katika denomination ya elfu elfu inajaza chumba kizima. Ni fedha nyingi sana ambazo zinaweza zikabadili uchumi wa eneo la Tanzania kwa mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fedha hizo zikishakaa kwa muda mrefu huko kwenye benki ya biashara kama CRDB basi muda ukifika BOT inaziita ina call kwa sababu ni unclaimed form yaani hazina mdai. Sasa zikienda zikirudi kule tunakuwa tumepoteza. Natoa rai na nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, wananchi wenu ambaye anajua kuna mtu alinunua hisa za awali CRDB wakati ule ndiyo hisa zinauzwa, awashauri wakachukue gawio lao kwenye benki yao walionunua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo nawaomba sana na namuomba sana Mkurugenzi Mkuu Majid atoe kurasa kwenye magazeti ya nchi hii yaandikwe watu wote walionunua hisa, inaniuma kuona kwamba hela zinakwenda kufungiwa zinaitwa unclaimed for wakati watu wanashida na hela. (Makofi)