Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tarimba Gulam Abbas (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, maana nilishakata tamaa, nilijua leo sipati nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu Subhana-huwataala kwa kutuwezesha kuwepo hapa. Nakishukuru chama changu kwa kunipeleka mbele ya wananchi wa Kinondoni na hatimaye wakanichagua kwa kura nyingi sana. Nawaambia wananchi wa Kinondoni niko imara, nina nguvu, nina akili ya kuwatumikia kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru familia yangu ikiongozwa na mke wangu Latifa Hasnal Faizal na dada yangu kipenzi Zera Abbas Muhammad Ali ambao kwa kipindi chote wamekuwa ni silaha kubwa katika kuniwezesha kusimama nikawa imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati akizindua Bunge hili la Kumi na Mbili, yenyewe inatosha kuwa ni dira ya vipaumbele kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu hili kwa kipindi cha miaka mitano inayokuja. Hata wataalam wa mipango wanaweza wakafyonza humo ndani na wakapata vitu ambavyo Watanzania wengine watavipokea kwa mikono miwili. Siyo rahisi kuandika hotuba kama ile, Rais lazima atakuwa ni mtu mwadilifu, ambaye amemweka Mungu mbele kuangalia Watanzania wanahitaji nini, awafanyie nini na nchi yake iko wapi na anataka aione iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu ni mtu ambaye anaongozwa na hofu ya Mungu. Hii inanifanya niseme kwamba viongozi wa Serikali wawe ni wateuliwa Mikoani au Wilayani, Serikali Kuu wawe na hofu ya Mwenyezi Mungu katika kufanya kazi zao. Hapo tutafanikiwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu nisome maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo ameyasema. Aliwauliza binadamu lakini akajibu mwenyewe; iko katika Surat Azuma aya ya 9, nitaisoma kama ilivyo, anasema: “Hal astawi? (Anauliza, wanafanana?) Aladhina yaalamuna waladhina laayaalamuna. (Yule anayeijua na yule ambaye hajui, hawa watu wamoja wanafanana hawa?) Akajibu, Mwenyezi Mungu hakusubiri watu wamjibu, akasema, balaa (hapana).” Maana yake imekusudiwa mtu mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu ni mtu ambaye amepata daraja kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Tushukuru kwamba tuna Rais ambaye ana hofu ya Mwenyezi Mungu na ndiyo maana mipangoyake inakubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, sisi Wabunge wote humu tumekuja hapa kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, tunapozungumza humu ndani hatuzungumzi kwa utashi wetu, ni utashi wa wananchi waliotutuma. Wananchi wakitueleza kwamba nendeni Bungeni kazungumzieni suala fulani, kaiambieni Serikali yetu suala fulani, Serikali ni ya wananchi na Bunge ni la wananchi, wapi tunakinzana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kila Mbunge akisimama anaongelea kuhusu TARURA; Spika anazungumzia TARURA, kila mtu anazungumzia TARURA, jamani sasa ifike wakati Serikali msikie hili. Huo ndiyo uadilifu ninaouzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi humu ndani tukizungumza, maana yake ni kauli ya Mungu, ni kauli ya wananchi na hapo ndipo tutapata mafanikio. Kuna options nyingi tu ambazo zimewahi kujadiliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama TANROADS hatuwezi tukapunguza fedha zake, iunganisheni na TARURA iwe ni kama division ya TARURA, wawe na mfuko mmoja mkubwa, wafanye kazi pamoja. Siyo lazima tuwe na utitiri wa vyombo, hapana, vyombo vinaweza vikawa vichache, kazi zikawa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli is alone, anasaidiwa na watu wachache lakini anafanya kazi kubwa, it is possible! Kwa nini hatumuigi Mheshimiwa Rais? Mbona kaitembelea Tanzania nzima? Wote humu ndani tumepata fadhila zake, tumetumia jina la Mheshimiwa Magufuli katika kupita. Aljazaul-ihisani ilal-ihisani (Anayekufanyia wema, mrudishie wema). Mheshimiwa Dkt. Magufuli katufanyia wema mkubwa katika Taifa hili. Tumrudishieni basi wema kwa kuwatumikia wananchi wake. (Makofi)

(Hapa kengele iligonga kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nisije siku nyingine nikaomba habari za Kinondoni Waheshimiwa mkanikatalia, lakini nataka…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele imeshagonga. Ahsante sana.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Basi nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ni mmoja kati ya Wajumbe wa Kamati ya Bajeti. Nimepata nafasi nzuri sana ya kuupitia Mpango huu. Nimeuona, tumeujadili, nasema ni Mpango mzuri ambao Serikali imekuja nao, lakini naiomba Serikali iweke room for improvement. Haya maoni ambayo yanatolewa yote ni maoni mazuri, wayachukue, isiwe kama ni taratibu zile nyingine kwamba tunazungumza lakini bado wanakuja na Mpango ule ule, mapendekezo yale yale, hilo haitakuwa jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najikita zaidi katika private sector. Ningependa sana huu Mpango uje waziwazi kwenye private sector, tuwe na vibrant private sector, hakuna uchumi unaoweza ukaendelea bila ya kuwa na private sector ambayo ina nguvu, inayochochea exports, lakini vile vile inachochea domestic spending, bila mambo haya tutakuwa tunajidanganya. Tutakuwa tunazungumza lakini tunajifanya kama tunasahau kama private sector ni mbia mkubwa sana wa maendeleo katika nchi yetu. Tumeangalia na figure zimetolewa na Wizara. Tuchukue tu mfano wa ule Mpango ambao umemalizika 2021. Contribution ya private sector ilikuwa inatarajiwa trilioni 48 karibu asilimia 45 ya kile kinachotarajiwa. Huyu si mtu wa kawaida. Huyu ni mbia ambaye lazima tuhakikishe tunakuwa nae na tunamuamini, private sector lazima iaminiwe. Tusitengeneze private sector ambayo hatma yake tunapeleka wrong waives, wrong information or wrong message kwa investors nje kwamba kufanya kazi au biashara Tanzania ni jambo gumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni wazi, hebu angalia hawa wataalam wa World Bank, kuna huyu mtaalam anaitwa Simeon Diankov na Gerald Paul, Wachumi wa World Bank hawa walivyotengeneza ile ease of doing business index, Tanzania katika kuangaliwa, tuko watu wa 141, tumewekwa kama medium. Sasa jamani tunashindwa, Rwanda is very easy to do business, Rwanda jamani? Kitu gani kinatufanya Rwanda wao iwe ni easy to do business, sisi iwe ni medium, basi hata Zambia? Zambia nao wanafanya vizuri, wako easy, Kenya wako easy, sisi tunafunga wapi kiasi kwamba kwetu sisi ionekane tuko katikati, tunachotafuta ni nini? Tunatafuta industry ya private iwe inapewa nafasi zake. Sasa hivi iko suffocated, it is a fact, nimepata bahati ya kufanya kazi Serikalini, nimefanya kazi katika Private Sector, sasa hivi na mimi eti nami ni mwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sikiliza, kampuni moja inazungukwa na regulators si chini ya sita au saba. Huyu anamuuliza hiki, yule anamuuliza hiki, yule anamuuliza hiki. Hajui aende wapi, who is the core regulator, aende wapi. Akipata matatizo, akiwa aggrieved huyu mtu anapata shida kubwa sana. Kampuni zinapata shida kubwa sana na haya ambayo yalikuwa yakizungumzwa kwamba business zinafungwa, naomba Serikali iangalie. Haiwezekani kampuni moja itaangaliwa na TRA, BOT, TCRA, OSHA, Fair Competition and Filling Company, hiyo ni mfano wa kwenye betting, huko usifikiri kuna Gaming Board of Tanzania peke yake, hawa ninaowatajia wako nyuma kila siku wanagonga milango. How can you do business?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachohitaji ni kuona kwamba mtu ambaye anafanya business Tanzania asababishe mwingine aliye nje avutike kuja Tanzania. Kwa kufanya hivyo tutapata kodi nyingi, tutaajiri watu wengi, lakini vile vile tutaondoa manung’uniko. Leo hii mtu akiwa aggrieved anakwenda wapi? Kwa nini tusiwe na regulatory ombudsman? Wafanyabiashara hawataki kwenda Mahakamani kushindana na Serikali. Katika vitu ambavyo wafanyabiashara hataki ni ugomvi na Serikali, lakini angekuwepo mtu hapo kama vile wa tax ombudsman hata regulatory ombudsman amekuwa aggrieved na chombo fulani cha Serikali huyu bwana anakwenda kwa ombudsman, anakwenda pale anazungumza mambo yake yanawekwa sawa, mambo yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaendelea na utaratibu tulionao sasa hivi, tuna suffocate private sector na private sector kama nilivyosema awali ni eneo moja ambalo ni mbia mkubwa sana wa biashara, mbia mkubwa wa maendeleo na ni maeneo ambayo tunahitaji kuyaangalia kwa nguvu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. Mungu atubariki. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ili niweze kuchangia hoja ambayo Yanga mwenzangu ameileta ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka mitano hadi mwaka 2025/ 2026.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kuunga mkono hoja hii na nina sababu kadhaa za kuunga mkono na wakati huohuo kuleta mapendekezo ambayo naamini kabisa kwa namna moja au nyingine yataweza kuboresha Mpango huu ambao leo tunaujadili. Nitaanza na hii dhana ya Serikali Sikivu. Mpango wowote ambao Serikali inaubuni ni lazima isikilize maoni kutoka kwa wachangiaji, hasa kutoka kwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, Serikali Sikivi imeoneshwa vizuri sana na Mheshimiwa Rais Samia naamini kwa kusikiliza mchango tuliokuwa tunautoa mwezi wa pili. Tulizungumza kuhusu ufanyaji kazi wa TRA na jinsi gani TRA inavyotukosesha mapato pale ambapo taratibu za ukusanyaji wa mapato zinavyokuwa sio sahihi. Vilevile tukazungumza suala la baadhi ya biashara kufungwa kutokana na ugumu wa ufanyaji kazi, Mheshimiwa Rais alichukua hatua za haraka sana. Naomba tumpongeze Mheshimiwa Samia kwa kusikiliza, hii ndiyo maana thabiti kabisa unapozungumzia Serikali Sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeonesha mwelekeo mpya huko nje business community imekuwa na imani kubwa sana na Serikali. Nina imani kabisa kutokana na imani ambayo inajengwa sasa wasaidizi wa Mheshimiwa Rais akiwemo ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Mchemba atasikiliza vizuri hoja zetu ambazo tunazileta uzichuje, zisaidie huu Mpango ili uwe bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala zima la maendeleo, nataka nimuangalie Mheshimiwa Hayati Julius Nyerere ambaye aliwahi kuzungumza na akatoa kauli ni nini maana ya maendeleo. Hili limekuwa likizungumzwa pia na Waheshimiwa Wabunge katika Mabunge mengi yaliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hayati Nyerere anasema: “Maendeleo hayawezi yakawa maendeleo kama sio people centred.” Maendeleo lazima yaguse watu ndipo yatakuwa ni maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haina maana vitu sio sehemu ya maendeleo, hapana, vitu ni sehemu ya maendeleo, lakini lazima i-translate na ishuke chini kwa mwananchi mmoja- mmoja. Hapo ndipo panapotuletea maelezo ama swali, je, Mpango huu unamgusa vipi mwananchi wa kawaida? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tuangalie hapo kwamba, Mpango huu lazima uwe na vielelezo vinavyopelekea mwananchi wa kawaida kusema naam, Serikali inakuja na mpango ambao utanigusa mimi, yule na mwisho jumuiya nzima ya Watanzania watafaidika na mpango huu. Yote haya ambayo tunayasema yanaelekea katika maeneo mazima ya uhuru wa watu kuweza kufanya biashara zao, kufanya kilimo chao katika nchi yao, kupata mazao ambayo wanaweza wakayapeleka nje wakaenda kuyauza. Hata utawala wa kisheria kwa sababu, kuna wakati tulilalamika sana hapa yale ambayo yanapangwa katika sheria nayo hayatekelezwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwepo na mjadala mkubwa sana, sitaki nirudie huko, mjadala ambao ndugu yangu msemaji wa mwisho alizungumzia wa korosho ule uliumiza watu wengi sana. Turudi katika utawala ule ambao tumejiwekea sheria zetu na zile sheria tuzifuate. Naamini kwa muelekeo ambao umeoneshwa na Mheshimiwa Rais ni dhahiri kabisa haya sasa yanakwenda kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Serikali imezungumza mambo mengi sana humu ndani, lakini Mpango huu lazima uwe ni unaotekelezeka. Tunataka Serikali itakavyokuja kufanya majumuisho itueleze ni namna gani imejitayarisha kuhakikisha kwamba inaitumia sekta binafsi ambayo ndiyo itakuwa ni moja kati ya wabia wakubwa katika Mpango huu. Ukiangalia numbers zinaonesha shilingi trilioni 40.6 zitatoka katika mchango wa sekta binafsi, lakini hata ule mchango wa Serikali wa shilingi trilioni 74.2 mchango ule utatetegemea vilevile sekta binafsi, Serikali haifanyi biashara. Ili 74.2 trillion shillings ziweze kukusanywa lazima business community hapa sasa iweze kuangaliwa na kuwa natured vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo, napenda nione kwamba, mchango wa Serikali katika kuhakikisha kwamba business community inalelewa vizuri uweze kuelekeza vizuri zaidi na Mheshimiwa Waziri aje kutuambia maana kuna kitu kimoja mimi kimenitia moyo, lakini kimenisononesha. Tuna watu wazuri sana katika nchi hii katika mawazo mema ya kufanya biashara na hapa nimpongeze Mpinzani wangu Mohamed Dewji ambaye tumesikia ameteuliwa na Rais wa South Africa kuwa ni mmoja kati ya watu ambao watamshauri. Sasa kama tuna mtu kama yule ndani ya Tanzania ambaye wenzetu wanamuona, sisi tunawatumiaje watu kama hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndipo sasa naiomba Serikali na napendekeza kwamba ni wakati umefika sasa Serikali ikaunda angalau timu ya wataalamu pamoja na wafanyabiashara mashuhuri, wakiwemo watu kama Mohamed Dewji, watueleze tufanyeje ili tuweze kufanikiwa zaidi katika suala zima la uwekezaji katika nchi yetu. Tuangalie tu, tusemeni kweli, Kamati ya Bajeti inazungumzia kwamba haijaridhika kuona kwamba Tanzania ni nchi ambayo si nyepesi ya kufanya biashara na wakatoa numbers wakasema tuko nafasi ya 141. Hata Mpango ule unaomalizika sasa ulikuwa unajitahidi kuifanya Tanzania iwe ndani ya nchi 100 katika wepesi wa kufanya biashara, lakini hatukufika huko. Ni vikwazo gani vilivyosababisha Tanzania isiweze kuingia katika zile nchi 100 zenye wepesi wa kufanya biashara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Serikali itakapokuja Mheshimiwa Dkt. Mwigulu atueleze ni vitu gani ambavyo watavifanya kuhakikisha Tanzania inakuwa ni moja kati ya nchi ambazo ni easy to do business, ili wawekezaji waweze kuvutika na wakaja. Kwa sababu bila wawekezaji ukweli ni kwamba tutapata maendeleo, lakini yatachelewa na tusingependa kuchelewa. Mkumbuke Rais wetu aliyepita, Hayati Mheshimiwa Magufuli, aliisababisha Tanzania kwa haraka zaidi kuingia katika Uchumi wa Chini wa Kati, miaka mitano kabla. Naamini kabisa Mheshimiwa Suluhu Hassan atatusogeza mbele zaidi ya pale ambapo Mheshimiwa Hayati Magufuli ameacha, kama mipango hii mizuri ambayo imewekwa itaweza kutekelezwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho napenda nizungumzie kuhusu ahadi za viongozi wetu wakuu. Wananchi wana imani sana na Serikali, wana imani sana na viongozi wao wakuu. Leo hii Wabunge tumekuwa tukilalamika sana tunazungumzia barabara za miaka mitatu, minne, mitano ambazo Mheshimiwa Rais alitoa ahadi. Sasa tusiende mahali tukafikia kwamba viongozi wetu wakitoa ahadi wananchi wa kawaida waseme, aah, haya ni kama yale yaliyopita, lazima tuyaangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu nampenda sana, kwa hiyo, napenda nione safari hii tunabadilisha mwelekeo, viongozi wakuu wakitoa ahadi zao wasaidizi wake wawe ni hodari wa kuzipokea na kuzifanyia kazi. Hatutataka tuje tukumbushie miaka mitatu iliyopita. Mheshimiwa Rais kama anayasikia haya nitaomba awape support ya kutosha Mawaziri wake katika suala kama hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemaliza na nilisema naunga mkono hoja hii, ahsante sana. (Makofi)