Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ally Anyigulile Jumbe (9 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia naomba nami niungane na wenzangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia tumepata nafasi ya kuwatumikia Watanzania tukiwa wamoja katika Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru pia Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. Huyu Rais amejidhihirisha hasa kuanzia kwenye uchaguzi wetu ambapo alihakikisha hata sisi wanyonge tunapata nafasi ya kufika hapa kupitia Chama Cha Mapinduzi ambacho anakiongoza kama Mwenyekiti wa Chama.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nidhahiri maneno mengi yanaweza yakasemwa juu ya huyu Rais, lakini nataka niwaambie Watanzania wote na Bunge hili Tukufu kuna wakati na mimi sitaki tufike huko tutakuja tujilaumu na kusema tunge, haya yasingetokea. Naomba tusifike huko tukafikia kwenye maneno ambayo Wanyakyusa wanasema pride comes after a fall. Naomba Watanzania na Bunge hili lifike wakati lijitathmini juu ya huyu Rais na ikiwezekana Wabunge tuungane, tufikie wakati tutoe tamko. Sio kwamba Rwanda ni wajinga walipofikia pale, sio kwamba Wachina ni wajinga walipofikia pale. Niwaombe Bunge hili, najua maneno haya wengi hawayapendi, lakini naomba tusifikie wakati wa kujilaumu tukasema tungelifanya hivi kwa huyu Rais basi Tanzania ingefika hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015 imemfanya Rais wetuna Chama Cha Mapinduzi kufikisha asilimia 84.4. Ilani bora ya sasahivi ya Chama Cha Mapinduzi, naomba sasa ifikishe Rais huyu kuzidi miaka mitano ijayo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hotuba hii na kuunga mkono kwenye maeneo machache. Naomba nifike kwenye eneo la kilimo ambapo zao la cocoa ambapo ukiitaja cocoa unaisema Kyela moja kwa moja, ni zao ambalo limetufikisha hatua ya kujiona na sisi tuna dhahabu. Hata hivyo, zao hili kwa sasahivi halimnufaishi mkulima kupitia kitu kinachoitwa stakabadhi ghalani. Wataalam wetu hawajatufikirisha vizuri, wamelichukua desa lao kama lilivyo wamelihamisha. Wamedesa mfumo unaotumika kwenye mazao ya msimu wameleta kwenye mazao ya muda wote.Cocoa sio zao la msimu ni zao ambalo lipo muda wote wa mwaka na zao hili sio zao ambalo linalimwa kwenye mashamba makubwa, ni vivuli kwenye nyumba za watu. Watu wanaokota kilo moja moja, kilo tano tano. Sasa huyu mtu ukidesa mfumo wa korosho au kahawa ukauleta kwenye mfumo wa zao kama hili, unafeli nahapo ndiyo unapofeli mfumo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye zao la cocoa sasahivi mtu anashindwa kusubiri siku nane za kuvundika cocoa ndipo akauze anaamua kuuza kwa Sh.2,500, wakati yule anayenunua mtu wa kati anapata zaidi ya Sh.5,000. Kwa kweli hili suala naomba kusema halijatusaidia wana Kyela na ni lazima tukae chini wataalam waishauri Serikali vizuri tuweze kutatua hili tatizo ili mnufaika awe ni yule aliyelengwa na ushirika ili suala la kumfanya apate faida yeye sio mtu wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kyela pia tunalima mpunga. Ni bahati mbaya sana, sasahivi kuna maneno yanaenea kwamba mchele wa Kyela umepungua ladha! Sio kweli. Ladha ya mchele wa Kyela ni ile ile ilakuna watu wanauza mchele wao kwa kutumia jina hilo. Naomba Wabunge na Watanzania wote waelewe mchele wa Kyela ni ule ule. Tunachoomba kwa Serikali sasa ni kwamba tuna mito minne mikubwa, sasa tunahitaji skimu za umwagiliaji ili tuwaoneshe mpunga wetu ulivyo bora ukiwa mwingi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji ni tatizo kubwa sana, lakini naomba hebu tujikite pia kwenye sera zetu. Sera ya Maji inasema mtu asitembee zaidi ya mita 400, lakini kwenye kituo kimojawachote watu 250. Maana yake ninini? Maana yake nikwamba kwenye saa 12 ina maana wanatakiwa kuchoka watu 20 kila saa moja na kila dakika tatu achote mtu mmoja na hapo ni kwamba maji yachuruzike muda wote. Sasa naomba hili suala liangaliwe na wataalam ili kuweza kuweka vizuri na takwimu zetu zikae vizuri tofauti na zilivyo kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zetu sasahivi zinatia aibu. Mheshimiwa Rais anajitahidi kujenga barabara nzuri, lakini ndani ya muda mchache zinaharibika na tatizo lingine linaloharibu barabara ni kwamba viwango vyetu bado hatujaviweka vizuri, lakini bado tuna matatizo ya matuta barabarani. Hebu tujiulize, je mpaka sasa tunaingia kwenye uchumi wa kati tunahitaji matuta kudhibiti spidi? Matuta haya yanaharibu barabara lakini kwa uchumi wetu sio mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Rais kwa kusema Wabunge tujitathmini, sisi ndiyo walinzi wa Rais wetu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Dunia na Afrika nzima inashangaa na kustaajabu ukuu wa Mungu ambao amebariki Taifa hili mpaka sasa hatujaingia kwenye lockdown na tunakaa kwenye Bunge hili. Naomba tuendelee kumshukuru Mungu na sifa na utukufu vimwendee yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Watanzania na Wabunge wote tusijisahau, haya yanayotokea ni kwa sababu ya mtu mmoja tu, Mungu huwa anamwangalia mzawa wa kwanza wa familia, matendo yake ndiyo yanayoshuka chini. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alimwamini Mungu, alisema Watanzania hatuna haja ya kuingia kwenye lockdown hata kama Mataifa mengine yanaingia twende tumuamini Mungu na yale maneno naomba tuendelee kuyaishi ndiyo yaliyotufikisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu haya yote pia Rais Dkt. John Pombe Magufuli hakufanya yeye peke yake, alikuwa na msaidizi wake ambaye alikuwa pia anamuonesha na kushauriana naye, naye si mwingine, ni mama yetu kipenzi, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan. Huyu mama ndiye yule ambaye aliahidiwa kwamba atampokea kijiti Mussa, sasa Mussa amebaki yeye anaendelea na ndiyo maana naomba leo niwasalimie kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

WABUNGE FULANI: Kazi iendelee.

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waziri Mkuu anafanya kazi kubwa sana na anachapa kazi usiku na mchana. Ndiyo maana katika yote niseme naunga mkono hoja hii ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, nilipenda niongelee mambo mengi sana lakini nimejikuta nipo kwenye masikitiko makubwa sana. Kata kumi za Wilaya ya Kyela leo ni siku ya tatu wananchi wako kwenye maji, wako kwenye mafuriko. Naomba nichukue nafasi hii kuwapa pole, lakini naomba sasa hata kama taarifa hazijafika basi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa kiiangalie Wilaya ya Kyela kwa jicho la huruma. Wilaya ya Kyela Kata kumi za Katumbasongwe, Bujonde, Kajunjumele, Matema, Isaki, Mwaya, Ikama, Ipinda na Makwale. Kata hizi zote wananchi wametoka kwenye nyumba zao, hawana chakula wala mahali pa kulala wako nje na mpaka barabara zote hata barabara yetu ya lami ipo kwenye maji sasa hivi na kuna sehemu imeanza kubomoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu kuna haja ya kuipendelea Wilaya ya Kyela kwa namna moja au nyingine kwa sababu moja tu. Wilaya ya Kyela ndiyo iko chini kabisa kwenye uwanda, iko mita 450; mvua zote zinazonyesha Ileje, Songwe, Rungwe na Busokelo matokeo yote mabaya yanaelekea Kyela. Hata barabara zilizoko Kyela sasa hivi zimegeuka kuwa mito.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kyela bado haijapata pesa za development kwenye barabara zake. Miaka mitano iliyopita mpaka mwaka huu hakuna pesa hiyo. Naomba sasa Serikali iiangalie Kyela tofauti na sehemu zingine kwani yenyewe iko tofauti na sehemu zingine, iko chini mno. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala dogo tu ambalo ni la Kimungu. Kuna watu wanashangaa kwa nini Tanzania hiko hivi? Viongozi wote wanafanya vizuri. Nataka niseme, ndugu zangu, kila Rais aliyetokea Tanzania alikuja kwa mkono wa Mungu na kwa kazi yake maalum. Hakuna Rais aliyekuja kivyake vyake kwa sababu nchi hii imebarikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wa Kwanza alikuja kwa ajili ya Uhuru na kutuunganisha Watanzania wote ili tuwe kitu kimoja. Akafuata Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi; baada ya kuungana Watanzania wote, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi aliona Watanzania mmoja mmoja, hawana uchumi wa kutosha, akatufungua wote, tukapata fedha, tukajifunza kutumia fedha. Nakumbuka kwetu ndiyo wakati ambao watu walianza kujifunza kuvaa viatu, tulikuwa tunaviita Ahsante Salim.

Mheshimiwa Naibu Spika, alipokuja Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa, akaona kwamba nchi haina fedha, lazima nchi ijikamilishe, Serikali iwe tajiri. Akaifanya Serikali ya Tanzania ikaanza kuwa na uchumi wake na kulipa madeni. Akaja Rais Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete akaifanya Tanzania ijulikane nje. Hiyo ni kazi ya Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu walikuwa hawajui hata kwamba Mlima Kilimanjaro uko Tanzania. Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alitufanya watu wa nje wajue Mlima Kilimanjaro uko Tanzania. Likaja Bulldozer ambalo kazi yake ilikuwa ni kuifanya Tanzania ijitegemee na hapa ndipo tulipofika. Haya hayajafika kwa kudra tu, ni Mungu aliyapanga kwamba yatakuwa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nataka kukishukuru sana Chama cha Mapinduzi. Chama hiki ni chama ambacho Mungu alikibariki, kwa sababu ni chama pekee ambacho kinafuata mifumo ya vitabu vya Mungu. Nimesoma kwenye Biblia; Kutoka 18:21-23 ndiko zilikoanzia nyumba kumi kumi. Maana alisema watu waongozwe na nyumba kumi kumi, elfu elfu na hamsini hamsini.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kwa utangulizi nikushukuru sana wewe mwenyewe, Naibu Waziri wa Maji na Mheshimiwa Suma Fyandomo na Bahati kwa kwenda kuwaona wahanga wa mafuriko kule Ipinda. Wanawashukuru sana. Mlichokifanya ni kitendo cha utu Mungu aendelee kuwabariki. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nikushukuru kwa utangulizi ulioanza nao na ninaomba hata katika hotuba yangu basi haya mambo yaingizwe moja kwa moja kwamba nami nayasema kama ulivyoyasema. Kitendo cha ugawanyaji rasilimali yetu, kufuatana na umuhimu wa sehemu ambapo barabara na sehemu za uchukuzi unaenda ni kitendo ambacho kinatakiwa kizingatiwe sana na Wizara yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejipanga nizungumzie mambo machache. La kwanza, ni suala la Serikali yetu kutimiza wajibu wake. Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi nataka nikiri inatimiza wajibu wake ipasavyo. Hata hivyo: Je, watendaji wetu wanafanya kazi zinazotakiwa? Hapana. Maana Serikali yetu inatoa fedha za matengenezo ya barabara kupitia Mfuko wa Barabara na kwa kweli zinatoka vizuri, lakini wenzetu wanaoenda kuzitumia hizi fedha wanafanya kazi ambayo kwa kweli wanaiaibisha taaluma ya Uhandisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo barabara nyingi, lakini nitatolea mfano barabara chache tu. Haiingii akilini, barabara inafanyiwa matengenezo, hapa kiraka kinachimbwa, wanatengeneza, lakini ukikaa siku mbili, ukirudi tena hapo hapo unakuta shimo. Naomba tujiulize, tatizo liko wapi? Haya yanapoteza rasilimali zetu sehemu moja kutengenezwa mara mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, utakuta sehemu iliyotengenezwa ni hiyo hiyo, sehemu inayofuata nayo inaharibika hakuna hata mita moja, sentimita mbili hapo hapo shimo linatokea. Hii barabara tunayoipita ya kutoka Dodoma kuelekea Iringa, kwa kweli wakati mwingine hatutakiwi kuwasimulia hata watoto wadogo, watatushangaa kabisa. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Chamuriho, Waziri wetu haya matatizo myaangalie yasiendelee tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni suala la ubora wa barabara zetu ambazo zinajengwa. Unashangaa kuna barabara zimejengwa hazina hata miaka kumi, lakini wameshaanza kuweka viraka. Tatizo liko wapi ndugu zangu? Tunapofeli ni wapi? Hivi ma-engineer wetu wako wapi? Tatizo kubwa tunaanza kusingizia eti Mkandarasi ndiye anafanya hivyo. Siyo kweli. Naomba hapa Bunge hili tuelewane vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, anayefanya barabara yetu idumu na iwe nzuri ijengwe kwa viwango siyo mkandarasi, ni msimamizi (consultant). Hao wanaajiriwa na Serikali yetu na wanasimama upande wa Serikali. Sasa nani alaumiwe hapa? Naomba sana, kuanzia sasa nashauri tuwe na standard za ujenzi wa barabara za Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunashindwa kuweka standards zetu basi tudese. Tufanye tutengeneze desa, nami hilo desa ninalo Mheshimiwa Waziri. Desa lenyewe ni barabara ya kutoka Uyole kwenda Kasumuru. Kwa nini tusichukue kama mfano? Kwa nini tusichukue nyaraka zao tukazitumia kama standard ya ujenzi wa barabara za Tanzania? Barabara ile ndugu zangu imejengwa mimi nina ndevu moja; ipo. Mpaka nimefikisha ndevu nne, naiona, miaka zaidi ya thelathini ipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya kutoka Iringa kwenda Igawa sasa hivi ina vipara na haitadumu zaidi hata ya miaka kumi ijayo. Naomba tutengeneze standard zetu. Barabara ile ndugu zangu ya Uyole Kasumulu, ikitengenezwa vizuri, ikisimamiwa vizuri ina uwezo wa kuishi miaka mingine kumi. Walijenga SOGEA nina uhakika nyaraka za barabara ile zipo, twendeni tuzichukue, tutengeneze, tuziweke vizuri, iwe ni reference ya ujenzi wa barabara zetu, kila nchi duniani ina reference ya ujenzi wa barabara zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee masuala ambayo yanaharibu barabara, mojawapo ni matuta, matuta barabarani yanaharibu barabara zetu. Ndio maana hata ukiangalia matuta yenyewe hayana hata standard, mengine yamekaa kama vichuguu, mengine yamekaa utafikiri ni matuta ya mbatata sasa, tuelewe lipi na ndio maana nataka niseme barabara zetu matuta yanaziharibu. Kwa nini tusifanye utaratibu mwingine? Matuta yana athari nyingi sana kwa uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, linapokuwepo tuta ni lazima mtu akamate breki, vipuri vile vya breki hatutengenezi hapa nchini vinatoka nje tunatumia pesa zetu kununua vitu nje ya nchi. Uchumi wetu unapungua. Kila unaposimama ukikanyaga breki unapoanza kuendesha gari, gari linakula mafuta mara ishirini ya lilivyokuwa linatembea. Mafuta hatuna hapa, lakini kitaalam ile lami haiwezi ikastahimili mzigo unaosimama, inastahimili mzigo unaodundadunda. Kwa hiyo, naomba hebu tuachane na haya tutafute njia nyingine ya kuweka hata box cover tu watu wapite chini barabara ipite juu haitasumbua hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba nisemee kidogo barabara moja ambayo inatoka Ibanda kwenda Itungi Port. Meli zimejengwa tunaishukuru Serikali, lakini mpaka sasa meli zinashindwa kupata hata mafuta. Tarehe 13 -17 Aprili, gari la kupeleka mafuta kwenye meli limeshindwa kupita, kwa sababu barabara ni mbovu na barabara hii tangu mwezi wa Disemba, 2019 iko mezani kwa Mtendaji Mkuu atoe kibali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sasa hivi inaenda kutengenezwa, naomba niishukuru Serikali, lakini zaidi ya yote naomba pia Serikali itusaidie watu wanaotembea na vimulimuli wameweka kwenye magari mbele pale kama vile na wao ni rider, jamani tunashindwa kutembea vizuri barabarani, tunaomba Serikali itoe tamko katika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni ume-set standards na sisi ni wanafunzi wako na hata tunapochangia tunajua tuko na mlinzi wetu ambaye ni wewe na sisi tutakulinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sitachangia kwa hasira kama alivyofanya Mheshimiwa Mlugo na Mheshimiwa Tabasamu na wengine kwa sababu ninataka leo liwe ni fundisho tujifunze tusome tujue vizuri maeneo yetu tunakotoka.

Mheshimiwa Spika, nitaongelea mfumo wa pili aliousema mchangiaji wa kwanza Mheshimiwa Mhagama mfumo wa Stakabadhi Ghalani na nitahusianisha mfumo huu na zao lililoko Kyela zao la kokoa ambalo ni zao kati ya mazao muhimu yaliyowekwa katika mfumo wetu wa mazao saba Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfumo huu pia hata ulivyoingizwa Wilayani Kyela uliingizwa kwa ubabe hakuna aliyefanya utafiti hakuna aliyezungumza na mkulima kilichofanyika ni kwamba leo tunazungumza kesho makampuni yote yasinunue kokoa. Ilikuwa ni kitendo cha ukatili na kuna makampuni yalipoteza pesa zao. Ukiuliza wanakwambia Serikali imesema Serikali ni nani kama siyo sisi wananchi? Ndugu zangu hili lilifikia hatua ya kutuparang’anya wana Kyela tulifikia hatua ya kuanza kuichukia Serikali lakini ilikuwa ni kwa sababu ya watu wachache.

Mheshimiwa Spika, cocoa ni zao ambalo ni tofauti na mazao mengine yaliyoko Mtwara kama korosho ambayo yanalimwa kwa msimu. Kokoa inalimwa kwenye vivuli sisi Wanyakyusa zao la cocoa ni zao la heshima kuwepo nyumbani kwako. Zao lile hatulimi porini maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba huwezi ukachukua mfumo unaotumika kwenye zao la korosho ambalo ni la msimu ukaja kwenye mfumo huo ukauleta kwenye cocoa ambayo inachumwa kila siku kwa msimu na kila mtu anaokota kidogo kidogo.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea mfumo wa korosho ukahamishiwa kwenye mfumo wa cocoa matokeo yake ni kwamba wale wote waliokuwa wananunua cocoa makampuni yote yalipoteza pesa zao na hata walipokubali kilichofuata ni kwamba wale wote ambao walikuwa wananunua cocoa hizo walishindwa kuendelea na biashara kwasababu wengi pia walifikia kufilisika na kampuni mojawapo ni Baoland ambao mpaka sasa hivi hawanunui kokoa Kyela.

Mheshimiwa Spika, hili zao kwetu huwezi ukamfanya mtu asubiri kila mtu anachuma siyo zaidi ya kilo tano kwa wiki ukisema huyu mtu anayechuma kilo moja asubiri aziandae cocoa ndani ya siku tano kama kuna jua lakini apeleke mnadani akishapeleka mnadani anatakiwa kusubiri mwezi mzima ndipo apate pesa sasa wewe elfu 30 unaisubiri mwezi mzima kwa kweli haiingii akilini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kinachotokea hawa watu wanashindwa kusubiri tumetengeneza tabaka la wanunuzi wa kati ambalo limejitengeneza automatically kwenye mfumo badala ya kununua kuuza hizo cocoa kwa shilingi elfu nne watu wanauza cocoa hizo kwa shilingi elfu tatu, na ni kwanini kwa sababu cocoa yao siyo cocoa kwa ajili ya kupata utajiri cocoa ya Kyela ni kwa ajili ya matumizi ya kila siku mtu anataka auze cocoa akamtibu mtoto, mtu anataka kuuza cocoa apeleke school fees kwa mtoto, anataka auze cocoa abadilishe mboga halafu auze cocoa angalau jioni akakae na wenzie anywe bia ndiyo kazi ya cocoa sasa leo unapomwambia mtu asubiri inashindikana.

Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba niseme mambo machache ambayo ninaomba sana Serikali inisikilize hili zao katika dunia hii kokoa iliyopo Kyela ndiyo hamira ya cocoa inayotoka Ivory Coast, cocoa inayotoka Ghana kwa ubora kokoa yetu inaongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kuna fununu…

SPIKA: Dakika moja ya kumalizia

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 30 machi, nilimuandikia message ndugu yangu Mwigulu Nchemba nikimuombea kwamba ikitokea baada ya kuchukuliwa Mheshimwa Mpango kuwa Makamu Rais basi nikasema naomba Mheshimiwa Rais ikimpendeza uwe Waziri wa Fedha; na bahati nzuri yale maombi yalitokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya hivyo kumuombea kwa sababu nilijua uwezo wake na nilijua uzalendo wake alionao kwa nchi hii ya Tanzania. Sasa tumeshakupata Mwigulu Nchemba na baada ya kukupata tumeshaanza kuona matunda yako pamoja na ya Naibu Waziri wako. Matunda haya hayajajificha, tumeanza kuyapata kwa kuyashika mkononi. Katika hili naomba nimshukuru sana Mama yetu, Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Ingekuwa tupo mtaani ningesema ameupiga mwingi kukupata wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaona matunda ya kupata shilingi milioni 500. Kwa jimbo langu mimi Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa pesa hiyo tunakwenda kujenga kilometa 2.5 za lami mjini. Hii itakuwa ni alama kubwa sana ya kazi kubwa uliyoanza nayo kuifanya. Maana yake ni nini? Kama naweza kujenga kwa milioni 500 kilometa 2.5 kwa kujiongeza ninaomba niiongezee shilingi zingine milioni 500 niende vijijini nikapige kazi ya mara mbili ya hiyo pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninaomba niseme, sifa zangu zitakuwa nyingi sana baada ya kuona matunda mengine yajayo, hasa kwenye eneo la jinsi utakavyogawanya hizi pesa zilizopo kwenye bajeti. Huko nyuma tumekuwa tukiona wakati mwingine sehemu nyingine hazifikiwi ilhali ni sehemu muhimu.

Ninaomba kama ni ma-flyover basi hata Tunduru kule, hata Iringa wayaone, siyo Dar es Salaam tu. Kama ni flyover pale Mbeya napo nani amewaambia hai-fit? Inakaa vizuri, tena inapendeza; ninaomba twende huko. Lakini hebu tupeleke akili sehemu zote za Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapozungumza watu ambao wanastahili kupata hata ile reli ya SGR TAZARA inastahili ifike hapo, tusirudi tu huku kwenye mpya, tukitengeza TAZARA, nataka nikuhakikishie, uchumi wetu utapanda zaidi ya ulivyo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunapotoa hizi rasilimali Mheshimiwa Mwigulu, wakati mwingine inasikitisha. Kyela ni sehemu ambayo inapata magonjwa mengi kwa sababu ya jiografia yake. Hata hivyo tangu mwaka jana hospitali imeungua wodi zimeungua pesa leo ndiyo zinapelekwa milioni 500 tu ilhali tuliomba na kwenye bajeti ilitengwa 1.3 billion, lakini sehemu zingine utakuta pesa zimeenda na wala hawakuunguliwa. Mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri, hebu iangalieni Kyela kwa jicho tofauti na sehemu zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ile ndiyo inayopokea masalia yote ya maji yanayotoka milimani, Ileje, Rungwe na Busekelo. Sasa miundombinu yake yote imeharibika kiasi kwamba hata kupeleka wagonjwa hospitalini ni ngumu, watu wanakufa vijijini kwa sababu hawawezi kufika haraka sehemu za kutolea huduma za afya. Kwa hiyo ningeomba hili tuliangalie si kwa Kyela tu lakini kwa Tanzania nzima. Twende tuangalie maeneo ambayo yapo prone namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala la takwimu. Katika kitu muhimu kuliko vyote kwenye uchumi ni takwimu sahihi. Leo kwenye bajeti tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya sensa ya wananchi wa Tanzania, lakini hivi tunahitaji kutenga hizo fedha? Mimi kwa mawazo yangu, nilitaka nishauri kwamba inawezekana hatukuwa na haja hiyo iwapo tungetumia vizuri sana rasilimali watu tulionayo; na nina uhakika wala tusingekuwa tunakisia idadi ya Watanzania, tungekuwa tunasema kwa uhuru tena kwa uhakika; kwamba leo hii tumeamka asubuhi tupo na watu kiasi fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusiwatumie hata mabalozi kwamba watoe taarifa za kila siku watu wapo wangapi hapo kwake Inawezekana ikaenda kwa mwenyekiti wa kitongoji tukatengeneza system nzuri ya mtandao. Tunaweza tukawa na computer zikaa pale kila siku au hata kwa wiki zikawa zinatolewa taarifa za idadi ya watu waliopo hapo. Mimi nafikiri kiasi hiki kisingefikiwa tungefanyia kazi nyingine. Ninaomba sana hebu twende tuangalie takwimu zetu za kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za Ulaya zimefanikiwa sana. Hakuna mtu anayelala nchini au kwenye nyumba ya mtu asijulikane yupo hapo na ameingia lini na anaondoka lini; na hata kwa usalama wa nchi itatusaidia sana. Zamani ilifanikiwa sana, hata kwa mabalozi, balozi alikuwa anajua ni nani ameingia kwenye eneo hilo na anatoa taarifa kwa nini haya tumeyaacha. Hivi, vyama vingi ndivyo vinatakiwa kuondoa hayo? Mimi ningeomba turudi huko tufanye mambo makubwa nchi yetu ipo kwenye eneo zuri na inaenda kuzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kwenye mapato ya simu. Tumesema sana na Serikali inategemea kupata kama 1.2 trillion kutoka kweney simu. Mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri, hebu kaa na watoa huduma wa simu wakuhakikishie uwezekano wa kupata kiasi hiki. Kwa sababu kuna sehemu kuna kuwa kama inaonekana haiwezekani ikapatikana hii. Sasa ili kuweka vizuri mimi nikuombe hebu fanya utafiti zaidi ili pesa hiyo ipatikane. Maana katika utafiti wangu nimegundua kwenye GSM na kwenye M-Pesa au Tigo Pesa pato lote la wao ni takriban bilioni 700. Sasa je, sisi tunaendaje hapo juu? Mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri lifuatilie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la polisi. Tunahitaji kuwatunza sana polisi. Kuna sehemu tunasahau kuwasemea, na bahati nzuri Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Masauni wote mmepita huko. Ninawaomba nendeni mkawaboreshee mafao hawa, hawa jamaa ndugu zetu wanalala nje kila siku na tunawategemea sana.

Naomba sana polisi tuwaangalie kwa jicho linguine. Lakini pia ningeomba nikutafutie chanzo kingine ambacho kinaweza kikawa ni privilege, lakini pia inaweza ikaonyesha uzalendo hata kwa Wabunge hapa hapa. Hebu tengeneza plate number za Wabunge halafu wawe wanalipia kidogo kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, plate number za Wabunge tu zinaweza zikalipa. Hebu angalia hata huko kwenye Serikali sehemu ambazo tunaweza tukatafuta, zikawa na Karangi kazuri kabendera yetu, tukawa tunalipia kwa mwezi au kwa mwaka itakwa vizuri zaidi na tutaongeza mapato. Unapokuwa Dodoma huwezi kupeperusha bendera, lakini ili ujulikane huyu ni Mbunge usijifiche ile plate number inaweza ikakusaidia, lakini iende kwa uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba kusema nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ninawaombe tu viongozi wetu wote wa Tanzania waendelee kumuenzi Mungu na waendelee kumkumbuka Mungu, kwamba tupo hapa kwa sababu Mungu ameichagua Tanzania kuwa Paradiso yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 30 Septemba, 2020, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikwenda kuomba kura pale Mbeya; na alisema maneno makuu matatu ambayo Wanambeya wanayakumbuka. Jambo la kwanza alisema naomba wanambeya mnichagulie Wabunge wote wa Mkoa wa Mbeya waingie Bungeni, Wanambeya wakafanya, ahsante Wanambeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili alisema, naomba Wanambeya nichagulieni Tulia, roho yangu itulie. Sasa kama huko alipo anatusikia tunamwambia roho yake itulie sana, Tulia alichaguliwa na sasa ndiyo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia tunataka tumwambie aliyemuachia kazi Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kazi yake anaiendeleza na anaupiga mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu alilolisema, alisema nataka niifanye Mbeya iwe ni kitovu cha biashara kwa Nchi za Kusini mwa Afrika na SADC kwa ujumla. Ili mambo haya yatimie, kuna mambo muhimu ni lazima yawepo hasa ya miundombinu; na jambo la kwanza ni uwanja wa Mbeya ambao tayari unaendelea vizuri. tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni barabara; barabara ya TANZAM, barabara muhimu kuliko zote na nataka niseme katika barabara ambazo kwa sasa zimesuswa ni hii barabara. Sasa naiomba Serikali kama kweli lengo lipo vilevile halijabadilika, ni lazima sasa Serikali yetu ihakikishe inakwenda kuijenga barabara hii kwa viwango sahihi. Sasa hivi ajali za magari zinatokea kila sehemu, ukitoka Mbeya kilomita 70 ni kila siku kuna ajali, barabara imeharibika na hii barabara ndiyo inayounganisha SADC, ndiyo inayounganisha magari yote na mizigo yote inayokwenda Malawi, Zambia, Congo mpaka Zimbambwe. Kuisusia barabara hii ni kuisusa Tanzania kiuchumi na kuharibu bandari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapofika Mbeya, ukifika pale katikati hapapitiki, barabara haipitiki, pamejaa vibajaji, daladala na kadhalika. Tunaomba Serikali sasa ichukue hatua za haraka ijenge barabara ile kwa njia mbili nina uhakika itatusaidia wakati huo tunafikiria kujenga bypass. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ili kuhakikisha ile ndogo ya Mheshimiwa Rais inatimia ni lazima TAZARA ifanye kazi. Naomba katika jambo la TAZARA Bunge hili livae meno ya chuma, tuache kuvaa meno ya plastiki kwa sasa. Naomba hili suala siyo la mchezo, safari hii tumekubaliana na Zambia tubadilishe mikataba, mkataba uwe mzuri, lakini tutunge sheria ya maana. Upande wa Tanzania mambo yamekwenda vizuri, leo naambiwa eti Zambia hawana Bodi ya Wakurugenzi mpaka watakapounda Bodi ya Wakurugenzi ndipo hizo Kanuni na Sheria zipitishwe, tunakwenda wapi? Ni lazima sasa tutoe tamko lenye maana. Naiomba Serikali; katika hili Serikali tuwe wakali, mkataba huu unaiangusha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, ili lengo hili litimie ni lazima Mbeya kuwe na Bandari ya Nchi kavu pale Inyala. Vyombo vyote vya usafiri vikiishia pale Inyala na nchi za SADC kule Kusini zikachukua mizigo pale uchumi huu utakwenda na Serikali itaona bandari yetu itakavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tazama ramani utaona nchi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nzuri kuliko zote duniani ni Tanzania; na si kwamba, ni Tanzania tu ambayo imejaliwa, Tanzania hiyo ni Tanzania ambayo inatoa mwanamke bora sana duniani anaitwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu...

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Nani, Mheshimiwa Jumbe kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hamisi Taletale.

T A A R I F A

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, alipoimba nilikuwa nataka kuingia chini ya meza. Kwa hiyo, nimuombe asirudie tena kuimba nyimbo nzuri akiwa anatutisha, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa…

MHE. ALLY J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa hiyo kwa sababu yeye ni talented sina haja ya kumbishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka tu kusisitiza kwamba, Tanzania hii ni nchi ambayo imebarikiwa sana. Inatoa mwanamke bora kabisa ambaye anaitwa Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Rais wa nchi hii. Ni nchi hii duniani ambayo inatoa Spika bora kabisa, a super woman, anaitwa Tulia Ackson. Ni nchi hii inatoa Mawaziri bora kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka tu niseme katika hali ya nchi kama hii ni lazima tufike wakati tujue kwamba, sisi tunaangaliwa na dunia nzima. Na tunapoangaliwa na dunia nzima ni lazima tuwe tunakubaliana kwamba, tumekuja hapa Bungeni kwa ajili ya hoja na si kutakiana ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hili kwa masikitiko makubwa. Jana mchangiaji Mheshimiwa Festo Sanga amechangia vizuri sana kuhusu suala la kuwatetea wananchi juu ya mambo ambayo yanaendelea Mbarali lakini matokeo yake imeonekana yeye hayupo kwa ajili ya kutetea wananchi bali ana maslahi yake. Sisi hapa tumekuja kwa ajili ya kuwatetea wananchi, hatujaja kwa ajili ya kufurahisha watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ameongea hapa Mheshimiwa Saashisha kuhusiana na suala la kutokutumia wataalam vizuri, tunatafutiana ajira. Nina mfano mmoja mzuri naomba niuweke hapa. Pale Bandari ya Tanga tulipokuwa tunasomewa taarifa hapa kulionekana kulikuwa kuna baadhi ya vitu ambavyo hazikuwa sawa. Aliyeibua mambo hayo nataka nikwambie, yupo mfanyakazi aliibua mambo hayo mpaka sasahivi hayupo kazini, alifukuzwa na hakuna mtu anayetaka kumjadili wala kuona kwamba anafaa kuendeleza bandari n ani mtaalam. Kuna jamaa mmoja anaitwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kumtaja jina kwa sababu, namfahamu na yeye ndiye aliyeibua uozo, walipoona anaibua uozo huo wamemfukuza kazi. Ninaomba wanaohusika wawatafute hao watu watatusaidia kwa mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongelea mambo ya kuanzisha Bandari ya Bagamoyo. Hivi bandari tulizonazo tumezitumia kwa uhakika?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA
UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ally Mlagila Jumbe kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali yetu inathamini sana misingi ya utawala bora, na kwa kuwa Serikali yetu imejipambanua kuhakikisha wkamba, inapambana na rushwa na inasimamia haki kwa watumishi wote wa umma ambao wamekuwa ni chanzo cha utendaji kazi bora, matumizi bora ya fedha na suala zima la maadili katika utendaji wa kila siku wa wawatumishi; kwa hiyo, kwa kuwa Serikali imejipambanua hivyo ninaomba tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge tuko tayari kumfahamu mtumishi huyo na kufuatilia kama iko misingi ya utawala bora imevunjwa kwa uadilifu na utendaji kazi uliotukuka kwa mtumishi huyo, Serikali itachukua hatua zaidi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe unapokea Taarifa hiyo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri?

MHE. ALLY J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Bagamoyo tunaisema sana hapa. Je, hivi Bandari ya Tanga tayari tumeshamaliza kazi zote zilizotakiwa pale, ili iweze kupokea mzigo? Ni kweli Bandari ya Dar es Salaam inafika wakati inaelemewa. Je, Bandari ya Mtwara ambayo ina kina ambacho ni natural, ambayo iko vizuri, Je, tumeitumia ipasavyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeomba Bandari ya Bagamoyo tusiiseme kama bandari. Tukisema industrial park itakuwa ni nzuri zaidi, lakini tukisema juu ya bandari ninaomba bandari tulizonazo tuweze kuzitumia ipasavyo, ili...

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jumbe inaonekana watu wameupenda sana uchangiaji wako. Kuna Taarifa kutika kwa Mheshimiwa Soud.

T A A R I F A

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba tu kumpa Taarifa mchangiaji kwamba, wakati tukiongelea kuhusu networking ya bandari, basi pia tuiweke pia Bandari ya Zanzibar umuhimu wake kwa sababu nayo pia ni sehemu ya nchi ya Tanzania. Na huduma itakapotoa itatoa kwa ajili ya nchi nzima. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Sawa. Mchangiaji anaweza akaweka huo mchango, lakini tusije tukachanganya mambo, tukaanza mambo ya muungano hapa halafu tukawa tumezalisha jambo lingine zito.

Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe.

MHE. ALLY J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bandari ninaomba likae hivyo, lakini naomba nijielekeze pia kwenye barabara na mchango ambao tunachukua kwenye mafuta wa road toll. Tunakoelekea sasahivi ni kwamba tunaenda kwenye magari nyanayotumia gesi; na hapa yupo Dangote anatumia gesi. Tunakoelekea itatokea wakati huo mfuko ambayo tunatoa kwenye mafuta tutashindwa kuufikisha na utashindwa kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wataalamu watusaidie, nchi zote sasa hivi zimeacha ku-charge kwenye mafuta, tutumie teknolojia, tuangalie ni namna ambavyo tunaweza tukapata hiyo kodi kwenye magari baada ya kwenye mafuta. Kwa mfano, kuna Road Toll; tunao uwezo wa kutumia teknolojia, Wajerumani wame- advance sana, wana kitu kinaitwa MOT, gari linahesabika kwa jinsi linavyotembea barabarani ndivyo linavyolipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mkulima ambaye analima kwa trekta, anatembea shambani, diesel anayonunua analipa Road Toll, mchenjuaji ambaye yuko kule porini anatumia diesel kuendesha mtambo wake, analipa Road Toll kwa kununua mafuta. Hii siyo haki. Hebu tutafute njia sahihi ambayo itahakikisha kila mmoja analipa kwa haki. Gari lililobeba mafuta, limelipa Road Toll, halafu mtu anayeenda kutumia shambani, analipa Road Toll. Hata kuendeleza kilimo inakuwa ni shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, hebu tukae na wataalam wanaotakiwa, ambao wanaweza wakafanya haya mambo vizuri, watuhakikishie na watuongoze. Sasa hivi zipo taxi pale mjini, zote zimehamia kwenye gesi, hazilipi. Hakuna anayelipa tena mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba hebu tunapozungumza mipango hii twende kwenye irrigation. Tuna irrigation ambazo ni muhimu sana; kuna irrigation ambayo iko sehemu ya pale Malawi na Tanzania ambayo inasisitizwa lakini leo sioni Mpango ukiongelea hiyo, ambayo ni Songwe River Basin.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Haya, ahsante sana.

MHE. ALLY J. MLAGHILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ili na mimi niweze kuchangia machache kwenye Muswada huu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Mheshimiwa Spika, naomba tu niseme kama kuna kipindi ambacho Tanzania inaenda kujijengea heshima Kimataifa pamoja na mambo yote ambayo yamefanyika, basi kwa kupitisha sheria hii tunaenda kuingia kwenye hanga za juu sana na tutakuwa tumejitengenezea heshima kubwa Duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge lako linaenda kuingia kwenye vitabu vya kutunga sheria ambayo kila mtu alikuwa anaisubiri. Wananchi wengi na wadau wameipongeza sana Serikali. Wamekupongeza sana kwa kukubali kuleta Muswada wa Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, sina haja ya kuelezea manufaa ya Sheria hii kwa sababau kila mmoja ameeleza na kila mmoja anajua, ninachotaka kusisistiza ni kwamba taarifa zetu binafsi ni biashara, huko Duniani na huko kwenye hanga taarifa zetu ni biashara, zitaenda kutumika kibiashara. Katika kutumika kibiashara ni lazima tuhakikishe taarifa zetu ni sahihi na zinalindwa, kulindwa kwake kunakuja na sheria hii. Ndiyo maana katika kulinda haya maslahi kuna kitu tumekisema kwa juu juu sana, ni kwenye jina la Sheria hii, tunaposema tu Ulinzi wa Taarifa Binafsi mimi nafikiri kuna kitu kinapungua.

Mheshimiwa Spika, hii sheria ikiongezewa faragha mbele, ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha italeta uzito sana, kuna nchi tayari wameishafanya hivyo New Zealand wanasema Data Protections and Privacy na hapa jirani Uganda wanataja hivyohivyo, Tanzania tunapata wapi kigugumizi kuweka hiyo privacy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme machache kwenye privacy. Tukiacha Sheria ikawa hivi, kuna mtu mwingine atakuja hadharani ataanza kukuuliza wewe unaitwa nani? Ulizaliwa lini? Jina la Baba yako ni lipi? Kwa sababu hatujaweka privacy, privacy ni jinsi pia ya kuchukua hizo data, mkakae pembeni kwa siri na huyo mchukua data, mchukua taarifa, sasa tusipoilinda hiyo nafikiri tutakuwa bado hatujajenga msingi ambao utakuwa imara sana.

Mheshimiwa Spika, kule Wanyakyusa mtoto wa kike hawezi kutaja jina la Baba Mkwe. Sasa ukilifanya hili liwe peupe kuna mtu atahukumiwa kwa kutaja jina la Baba Mkwe wake, usije ukafikiri kwa mfano sisi ng’ombe kama mkwe hawezi kusema kusema ng’ombe atasema hata linaloelekeana atasema ngwafi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi ninaomba hebu hili neno la faragha liingizwe ili taarifa zetu tunapozitoa pia ziwe ni siri. Mtu unaumwa magonjwa makubwa ambayo hutaki watu wengine wajue, huwezi ukasema na mwingine anasikia ni lazima kuwe na utaratibu wa privacy, utaratibu wa faragha kama neno faragha siyo zuri kwa Kiswahili tutafute neno lingine kuweka uzito, naomba sana hili neno liongezwe.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna vitu pamoja na uzuri wa sheria hii, kuna mtu ambae tumemsahau, wakati wote sisi ni marehemu watarajiwa ukifa taarifa zako zinabaki kwenye vyombo. Je, kuna sehemu gani ambapo huyo marehemu ataenda kulindwa na taarifa hizo? Ninaomba tuweke taarifa za marehemu ni jinsi gani zitakavyolindwa na ni nani atayezisimamia? Kuacha hivi hivi, mimi Baba yangu alifariki, wengine hapa Baba zao wamefariki data zao tuna uhakika gani kwamba zitalindwa na sheria hii? Ninaomba hilo kama siyo sasa basi kwenye Kanuni liangaliwe vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho Sheria yeyote inayotungwa ili iwe nzuri, inatakiwa ilete manufaa na isiwe mzigo kwa wananchi, isiwe mzigo. Tumetunga sheria hii vizuri sana, sheria hii inaenda kusimamiwa na Tume lakini Tume itasimamiwa na Bodi, hawa ni watu wengi sana na hawa watu wengi watahitaji rasilimali fedha, woga wangu na baridi ninayoipata nikwamba mbona vyanzo vya pesa bado hatujaviweka vizuri. Sheria yetu haijawa wazi, inasema tu Bunge litapitisha, Bunge litapitisha kwa Bajeti ipi? Kwa nini wasitengeneze na wao vyanzo vyao? Ninaomba tunapoelekea huko mbele tuangalie jinsi ya kupata vyanzo ambavyo vitaelezwa EWURA, walipokuwa wanatunga Sheria walisema watatoa wapi pesa. Sisi kwenye sheria hii tumesema kiujumla mno, ningeomba tuweke vizuri kwenye Muswada huu, tujue ni jinsi gani tunaenda kupata pesa.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya yote sidhani kama kuna Mtanzania ambaye anaipenda Tanzania hatatupongeza kwa kupitisha Sheria hii, na mimi ninasema tuungane wote Wabunge hapa, tuipitishe Sheria hii kwa manufaa na mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga hoja mkono, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ili na mimi niweze kuchangia machache kwenye Muswada huu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Mheshimiwa Spika, naomba tu niseme kama kuna kipindi ambacho Tanzania inaenda kujijengea heshima Kimataifa pamoja na mambo yote ambayo yamefanyika, basi kwa kupitisha sheria hii tunaenda kuingia kwenye hanga za juu sana na tutakuwa tumejitengenezea heshima kubwa Duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge lako linaenda kuingia kwenye vitabu vya kutunga sheria ambayo kila mtu alikuwa anaisubiri. Wananchi wengi na wadau wameipongeza sana Serikali. Wamekupongeza sana kwa kukubali kuleta Muswada wa Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, sina haja ya kuelezea manufaa ya Sheria hii kwa sababau kila mmoja ameeleza na kila mmoja anajua, ninachotaka kusisistiza ni kwamba taarifa zetu binafsi ni biashara, huko Duniani na huko kwenye hanga taarifa zetu ni biashara, zitaenda kutumika kibiashara. Katika kutumika kibiashara ni lazima tuhakikishe taarifa zetu ni sahihi na zinalindwa, kulindwa kwake kunakuja na sheria hii. Ndiyo maana katika kulinda haya maslahi kuna kitu tumekisema kwa juu juu sana, ni kwenye jina la Sheria hii, tunaposema tu Ulinzi wa Taarifa Binafsi mimi nafikiri kuna kitu kinapungua.

Mheshimiwa Spika, hii sheria ikiongezewa faragha mbele, ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha italeta uzito sana, kuna nchi tayari wameishafanya hivyo New Zealand wanasema Data Protections and Privacy na hapa jirani Uganda wanataja hivyohivyo, Tanzania tunapata wapi kigugumizi kuweka hiyo privacy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme machache kwenye privacy. Tukiacha Sheria ikawa hivi, kuna mtu mwingine atakuja hadharani ataanza kukuuliza wewe unaitwa nani? Ulizaliwa lini? Jina la Baba yako ni lipi? Kwa sababu hatujaweka privacy, privacy ni jinsi pia ya kuchukua hizo data, mkakae pembeni kwa siri na huyo mchukua data, mchukua taarifa, sasa tusipoilinda hiyo nafikiri tutakuwa bado hatujajenga msingi ambao utakuwa imara sana.

Mheshimiwa Spika, kule Wanyakyusa mtoto wa kike hawezi kutaja jina la Baba Mkwe. Sasa ukilifanya hili liwe peupe kuna mtu atahukumiwa kwa kutaja jina la Baba Mkwe wake, usije ukafikiri kwa mfano sisi ng’ombe kama mkwe hawezi kusema kusema ng’ombe atasema hata linaloelekeana atasema ngwafi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi ninaomba hebu hili neno la faragha liingizwe ili taarifa zetu tunapozitoa pia ziwe ni siri. Mtu unaumwa magonjwa makubwa ambayo hutaki watu wengine wajue, huwezi ukasema na mwingine anasikia ni lazima kuwe na utaratibu wa privacy, utaratibu wa faragha kama neno faragha siyo zuri kwa Kiswahili tutafute neno lingine kuweka uzito, naomba sana hili neno liongezwe.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna vitu pamoja na uzuri wa sheria hii, kuna mtu ambae tumemsahau, wakati wote sisi ni marehemu watarajiwa ukifa taarifa zako zinabaki kwenye vyombo. Je, kuna sehemu gani ambapo huyo marehemu ataenda kulindwa na taarifa hizo? Ninaomba tuweke taarifa za marehemu ni jinsi gani zitakavyolindwa na ni nani atayezisimamia? Kuacha hivi hivi, mimi Baba yangu alifariki, wengine hapa Baba zao wamefariki data zao tuna uhakika gani kwamba zitalindwa na sheria hii? Ninaomba hilo kama siyo sasa basi kwenye Kanuni liangaliwe vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho Sheria yeyote inayotungwa ili iwe nzuri, inatakiwa ilete manufaa na isiwe mzigo kwa wananchi, isiwe mzigo. Tumetunga sheria hii vizuri sana, sheria hii inaenda kusimamiwa na Tume lakini Tume itasimamiwa na Bodi, hawa ni watu wengi sana na hawa watu wengi watahitaji rasilimali fedha, woga wangu na baridi ninayoipata nikwamba mbona vyanzo vya pesa bado hatujaviweka vizuri. Sheria yetu haijawa wazi, inasema tu Bunge litapitisha, Bunge litapitisha kwa Bajeti ipi? Kwa nini wasitengeneze na wao vyanzo vyao? Ninaomba tunapoelekea huko mbele tuangalie jinsi ya kupata vyanzo ambavyo vitaelezwa EWURA, walipokuwa wanatunga Sheria walisema watatoa wapi pesa. Sisi kwenye sheria hii tumesema kiujumla mno, ningeomba tuweke vizuri kwenye Muswada huu, tujue ni jinsi gani tunaenda kupata pesa.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya yote sidhani kama kuna Mtanzania ambaye anaipenda Tanzania hatatupongeza kwa kupitisha Sheria hii, na mimi ninasema tuungane wote Wabunge hapa, tuipitishe Sheria hii kwa manufaa na mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga hoja mkono, ahsante sana. (Makofi)