Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Neema Kichiki Lugangira (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyo mezani ya hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Napenda kujielekeza katika sekta ya kilimo na hivyo nitaendelea kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake na naomba nifanye rejea kwenye ukurasa wa 25 alisema kwamba: “kwenye miaka mitano iliyopita tumefuta tozo 168 ambapo 114 zilihusu kilimo, mifugo na uvuvi na 54 za biashara. Tutaendelea na hatua hizo.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufanikisha hili ambapo lengo kuu naamini ni kuimarisha uwekezaji na hivyo hivyo punguzo hizi zinaweza kuimarisha na kunufaisha wakulima wadogo. Hivyo napenda kuishauri Serikali kuwa ni muhimu sasa kufanya tathmini ili tuweze kujiridhisha punguzo za tozo hizi zote kama zinanufaisha wakulima wadogo kama ambavyo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali iagize wadau wote kufanya impact assessment ya tozo zote ambazo tumetoa, maana kwa uzoefu wangu inaonekana kwamba saa nyingine tozo hizi kunakuwa hakuna trickle- down effect ya kufika kwa wakulima wadogo ipasavyo. Mimi naamini kwamba uimarishaji wa mazingira ya ufanyaji biashara unatakiwa uende sambamba na unufaikaji wa wananchi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake kwenye ukurasa 26 naomba kunukuu, alisema: “Kwa msingi huo kwenye kilimo mathalani tunakusudia kuongeza tija na kufanya kilimo chetu kuwa cha kibiashara. Lengo ni kujihakikishia usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwandani na pia kupata ziada ya kuuza nje. Ili kufanikisha hayo, tutahakikisha pembejeo na zana bora za kilimo ikiwemo mbegu, mbolea, viuatilifu/ dawa na matrekta vinapatikana kwa uhakika na gharama nafuu.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena napenda kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya kwa miaka mitano iliyopita. Hotuba ya Mheshimiwa Rais imesisitiza yale ambayo yameandikwa kwenye Ilani ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi kwenye kifungu 35 – 46. Hivyo ili tuweze kufanikisha haya kwa kasi ambayo inatakiwa ningependa kushauri yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, ni lazima sasa tujikite katika uzalishaji wa aina mbalimbali za mbegu maana hivi sasa ukienda kwenye duka la mbegu utakuta 80% ya mbegu hizo zimetoka nje ya nchi na hivyo Tanzania tunakosa soko kubwa la uzalishaji wa mbegu. Aidha, naishauri Serikali iweke kipaumbele cha kujengea uwezo taasisi zetu za ndani na za binafsi za ithibati (Local Certification Boardies). Kwa kufanya hivi, tutaweza kufanikisha mbegu ambazo tunazizalisha ndani ya Tanzania nazo ziweze pia kuuzwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo jambo langu la tatu, nakubaliana na mapendekezo yaliyo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuhusu Wizara ya Kilimo kuwa na bodi za mazao na taasisi ambazo zinahitaji kupitiwa upya kimuundo ili ikiwezekana kuwe na taasisi chache zitakazoongeza ufanisi na kuimarisha usimamizi wa sekta hii. Nimesema hivi kwa sababu kwa jinsi ilivyo sasa wingi wa hizi bodi za mazao na taasisi unaleta mkanganyiko mkubwa kwenye sekta hivyo unakinzana na dhana nzima ya kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, mwisho niapenda kutoa wito kwa wadau wa sekta ya kilimo kuwa mstari wa mbele kuhamasisha uzalishaji na ulaji wa vyakula vyenye viini lishe vingi ili kuungana na jitihada za Serikali za kutokomeza udumavu na utapiamlo kwa ujumla. Kama ambavyo tunafahamu Waheshimiwa Wabunge Tanzania 32% ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa, kwa maana hiyo katika kila watoto 100 watoto 32 wamedumaa. Cha kushangaza zaidi mikoa inayoongoza kwa udumavu ni mikoa ambavyo inaongoza kwa uzalishaji wa chakula (food basket). Ndiyo maana nimesema tutoe wito kwa wadau hawa pamoja na kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya kibiashara pia wahamasishe uzalishaji na ulaji wa mazao yenye viini lishe vingi ambayo imo kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru tena kwa fursa hii ya kuchangia hoja iliyo mezani na naunga mkono hoja ya hotuba ya Mheshimiwa Rais, ahsante. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa fursa hii. Naomba nianze kwa kusema naunga mkono Maazimio yote mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Sekta ya Asasi za Kiraia ambazo mimi ni mwakilishi wao hapa Bungeni kupitia nafasi ya Viti Maalum Chama cha Mapinduzi, napenda kuwasilisha pole za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha Hayati Rais Magufuli. Vilevile napenda kuwasilisha salamu za pongezi kwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki hii zaidi ya asasi za kiraia 200 kutoka Bara na Zanzibar zimewasilisha tamko la pamoja la pongezi na pole kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Vivyo hivyo, Jukwaa la Wanawake Wakurugenzi wa Asasi za Kiraia kwa maana ya CSO’s and NGO’s na wao pia wametoa tamko la pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Bunge lako Tukufu kuwa Sekta ya Asasi za Kiraia zina imani kubwa sana na yeye kwa sababu ana uzoefu mkubwa sana wa uongozi. Nitumie fursa hii kutaja maeneo machache. La kwanza, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alianza ajira yake kwenye mwamvuli wa mashirika yasiyo ya Kiserikali linaloitwa ANGOZA (Association For Non- Governmental Organizations in Zanzibar) na kwa mantiki hiyo Mheshimiwa Rais ni mwana Azaki mwenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ana uzoefu mkubwa katika masuala ya uwezeshaji kiuchumi. Kupitia uzoefu huu mwaka 2016 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bani Ki Moon alimteua Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais kuwa Mjumbe wa Jopo la Dunia kama mwakilishi wa Afrika lililopewa jukumu la kumshauri kwenye masuala ya uwezeshaji wanawake kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, miaka 25 iliyopita Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa anatokea Sekta ya NGO’s alishiriki katika Mkutano wa Beijing uliokuwa unalenga kuleta ukombozi wa usawa wa kijinsia ikiwemo wanawake kwenye nafasi za uongozi na maamuzi. Hivyo kupitia yeye kuwa Rais wetu wa kwanza mwanamke, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameiwezesha Tanzania kuweka historia ya kuwa sehemu ya utekelezaji wa Maazimio ya Beijing. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, nikiwa kama mdau wa lishe, sisi wadau wa lishe tunatambua juhudi kubwa ambazo Mheshimiwa Makamu wa Rais mteule ameweka katika kuhakikisha nchi yetu inaboresha hali ya lishe. Vivyo hivyo, tunatambua pia jitihada kubwa ambazo Makamu wa Rais mteule, Mheshimiwa Dkt. Phillip Mpango ambazo pia ameweka katika eneo hilo la kuboresha hali ya lishe kwa kuhakikisha kwamba Halmashauri zote nchini zinatenga bajeti ya lishe kwa kulingana na idadi ya watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Sekta ya Asasi za Kiraia itampa ushirikiano mkubwa katika kutekeleza dira yake ya maendeleo ya Taifa letu la Tanzania. Naomba nitumie fursa hii kipekee kuomba kuwasilisha ombi rasmi la kukutana naye kama Sekta ya Asasi za Kiraia ili nasi pia tuwe sehemu ya mafanikio yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki na kumlinda Rais wetu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika, ahsante. (Makofi)