Parliament of Tanzania

SPIKA aunda kamati maalumu ya ushauri kuhusu shughuli za uchimbaji almasi nchini

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tazania Mhe Job Ndugai ameunda Kamati maalum ya Wabunge tisa itakayoshauri juu ya mfumo bora wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya Madini ya Almasi hapa Nchini.

Kamati hiyo, itakuwa na wajumbe tisa watakaoongozwa na Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Mussa Zungu na itafanya kazi kwa siku 30.

Akizungumza kabla ya kuhitimisha shughuli za Bunge la Bajeti, Mheshimiwa Spika alisema ameunda kamati hiyo kupitia Waraka wa Spika namba 3 wa mwaka huu.

“Kamati hii itatathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini kisha kuandaa mapendekezo mahsusi kwa ajili ya kuishauri Serikali kuhusiana na uendeshaji bora wa biashara ya madini hayo nchini,” alisema


Aliwataja wajumbe wa Kamati hiyo kuwa ni Mbunge wa Viti maalum(chadema) Dk. Immaculate Sware Semesi,Mbunge wa Viti maalum (CCM)Shally Raymond, Mbunge wa Tumbe Rashid Ali Abdallah(CUF),Mbunge wa Iramba Mashariki Allan Kiula(CCM), Mbunge wa Viti maalum(CCM) Restituta Mbogo, Mbunge wa Wawi Ahmed Juma Ngwali(CUF).

Wengine ni Mbunge wa Sumve Richard Ndassa(CCM), Mbunge wa Tabora mjini Emmanuel Mwakasaka(CCM) na Mbunge wa Ilala Mussa Zungu (CCM)ambaye atakuwa Mwenyekiti.

Alisema wajumbe hao wameteuliwa kwa kuzingatia vigezo vya taaluma, uzoefu, pande za Muungano, jinsia na uwakilishi wa Vyama vya Siasa Bungeni.

“Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda wa siku thelathini kuanzia Julai 10, na Kituo Kikuu cha kazi kitakuwa katika Ofisi ya Bunge hapa Dodoma,”alisema

Aidha, alisema hadidu za rejea za kamati hiyo ni Kuchambua Taarifa za Tume na Kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa na Serikali kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini na kuona Mapendekezo yake na namna yalivyotekelezwa na Serikali.

Nyingine ni Kutathmini mfumo uliopo wa Uchimbaji, Usimamizi na Udhibiti wa biashara ya madini ya almasi nchini na kubainisha manufaa ambayo Serikali inapata kutokana na uwekezaji uliopo katika madini hayo na kubainisha na kushauri kuhusu utaratibu bora unaoweza kutumika katika kusimamia uwekezaji, uchimbaji na biashara ya madini ya almasi nchini,”alisema Spika Ndugai

“Hadidu nyingine ni kushughulikia jambo jingine lolote linalohusiana na mfumo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa madini ya almasi nchini,” alisema

Alisema kuundwa kwa Kamati hiyo kumetokana na pendekezo la Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli la kuunda Tume ya kuchunguza na kufuatilia madini ya alamasi alilolitoa Juni 12 mwaka huu alipohudhuria mkutano wa kupokea Taarifa ya Kamati yake ya Pili ya Kuchunguza Masuala ya Kiuchumi na Kisheria kuhusu Usafirishaji wa Makinikia, Kamati ya Prof. Nehemia Osoro).


Alisema Bunge liliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa kadri itakavyohitajika katika kuhakikisha kwamba juhudi, uthubutu na uzalendo aliouonesha Rais katika kulinda rasilimali za madini haupotei bure.

Hata hivyo alisema kuundwa kwa Kamati hiyo ni hatua mojawapo ya utekelezaji wa Azimio la Bunge la kumpongeza Rais Magufuli katika jitihada za kulinda rasilimali za Taifa.

“Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini ya almasi duniani, Madini haya yana thamani na umaarufu mkubwa katika biashara ya vito,kama ilivyo kwa dhahabu na madini mengine ya thamani, yapo malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali nchini kwamba hatujaweza kunufaika ipasavyo kutokana na wingi na thamani ya madini ya almasi,”alisema Mheshimiwa Spika


Kamati hii itakayofuatilia kuhusu mfumo wa uchimbaji wa Madini ya Almasi hapa nchini ni ya pili kuudwa na Mhe Spika baada ya Kamati ile itayofuatilia suala la uchimbaji wa Madini ya Tanzanite hapa nchini ambayo pia aliuunda wakati wa mkutano wa Saba wa Bunge.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's