Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Omar Ali Omar (1 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia na mimi fursa hii. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu wetu muumba wa mbingu na ardhi, aliyetuwezesha kusimama hapa na kukaa kitako huku tukiwa na hali ya afya njema wakati wenzetu wengine sasa hivi wako makaburini na wengine wako hoi bin taabani mahospitalini. Tuwaombee dua wote hao wapate nafuu ili tuungane nao katika kujenga Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kwanza kutoa shukrani zangu za dhati…

SPIKA: Mheshimiwa Khatib, vipi walioko mahospitalini wana nafuu?

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, vizuri sana.

SPIKA: Aah, basi. Haya endelea Mheshimiwa Omar. (Kicheko)

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana..

Naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa wapiga kura wangu wa Jimbo la Wete, Pemba. Wengi wamezoea kule tuseme kwamba Wazanzibar walio wengi hasa wakiingia kwenye Kisiwa cha Pemba wanasema waja leo warudi leo? Kwa maana ya kwamba hiyo ni jumla ya question mark. Usiende ukarudi, ukienda ubakie.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakishukuru chama change cha ACT - Wazalendo. Kwanza namshukuru sana kiongozi wangu wa chama, Ndugu Zuberi Kabwe pamoja na Mwenyekiti wangu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Ndugu Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

SPIKA: Mheshimiwa Omar, samahani kidogo. Kwani hicho chama bado kipo?(Kicheko/Makofi)

MHE. OMAR ALI OMAR:Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, naenda moja kwa moja kwenye hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwenye ukurasa wake wa 14 ambapo alitamka bayana katika hotuba yake ile kwa kusema kwamba katika kipindi hiki cha awamu yake ya tano ya miaka mitano inayofuata atatoa ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa nia ya kuleta maendeleo kwa pande zote za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Rais kwa hatua hiyo na kwa nia yake safi na tayari matunda yake tumeanza kuyaona, kwa sababu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, tayari amepanga safu nzuri sana ya kuhakikisha kwamba sasa Zanzibar inafikia uchumi wa kati, kwa sababu ameanza kutumbua majipu. Nafikiri labda yeye kafuata kichogo cha mlezi wake, naukifuata kichogo cha mlezi wako, basi inawezekana wewe ukafanya vizuri zaidi kuliko hata mlezi wako huko nyuma kwa sababu kazi yako itakuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, naomba sasa niende moja kwa moja kuchangia katika hoja hizo, kuangalia zaidi ya changamoto za Muungano. Zamani tulikuwa tunaziita kero, lakini siku moja nilikutana na Mheshimiwa Waziri akasema sasa tusiziite tena kero, tuziite changamoto. Na mimi nakubaliana naye kwamba changamoto hizo, kwa sababu tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Serikali ya Zanzibar, kero zile zinazofika nadhani 21 kama sikosei, tayari kero 11 zimeanza kupatiwa ufumbuzi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa Mheshimiwa Waziri anayehusika na Muungano akae chini na kutafakari na kutumia juhudi na maarifa na uwezo wake wote kuhakikisha kwamba zile changamoto ambazo zimebakia basi zimeondolewa kabisa. Ili kwamba sasa Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano tusizungumze tena kero, tuzungumze maendeleo. Baadhi ya kero hizo, ni wafanyabiashara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KHATIB SAID HAJI: Endelea.

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wa Zanzibar wanapochukua bidhaa zao kutoka Zanzibar na kuzileta Tanzania Bara, wanatozwa kodi mara mbili. Hilo ni tatizo kubwa ambalo ni moja katika vitu ambavyo vinatakiwa vipatiwe ufumbuzi.

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Omar, nakushukuru sana.

MFUNGE FULANI: Aunge mkono hoja. (Kicheko)

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ila ungeniongezea kidogo kwa sababu ulichukua muda wangu kidogo.

SPIKA: Unataka kuunga mkono hoja?

MHE. OMAR ALI OMAR: Mheshimiwa Spika, nilitaka uniongezee japo dakika moja.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Omar. (Kicheko)

Wiki ijayo tutakuwa na muda mwingi zaidi wa dakika kumi kwenye kujadili Mipango, kwa hiyo, utamalizia.