Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. George Boniface Simbachawene (41 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kwanza kabisa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mizuri ambayo kusema ukweli imezidi kuongezea yale ambayo Mheshimiwa Rais aliyasema siku ya hotuba yake. Kwa hiyo, tumeendelea kupata mambo mengi zaidi ambayo yatatusaidia kuyafanyia kazi. Mmesema mengi katika sekta ya afya, kilimo, mambo ya utawala, utumishi, ukusanyaji wa mapato na mambo mengi sana mmeyasema ambayo yanaangukia katika Wizara yangu ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwahakikishia kwamba yote haya tunayafahamu. Tanzania mpya ya Magufuli inayokuja, ni ya watu kufanya kazi. Tunataka tuwahakikishie kwamba Mheshimiwa Rais anaendelea kuisuka Serikali na mtambue kwamba Serikali bado haijakamilika. Bado tunahitaji Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, lakini tutakwenda mbali zaidi; tunataka kusuka vizuri sana Wakurugenzi mpaka Wakuu wa Idara. Tunataka tuwachuje, wawe na vetting nzuri kabisa na siyo kuokotana tu. Tunataka Tanzania mpya, tukisema kuanzia juu Hapa Kazi Tu basi ni Hapa Kazi Tu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mengi yaliyosemwa hapa liko moja ambalo limejitokeza sana juu ya elimu bila malipo. Elimu bila malipo limesemwa na Wabunge wengi na ni kwa sababu halifahamiki. Serikali imeamua hata wakati bajeti haijafika, lakini kupitia kwenye wigo ule ule wa bajeti ya mwaka 2015/2016 kunyofoa katika utoaji wa huduma ya elimu, katika vote ya Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha kwamba tunapata shilingi bilioni 131.88 kwa ajili ya kuanza kutoa elimu bila malipo kwa watoto wetu wa kuanzia chekechea hadi kidato cha nne. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwezi tumepanga kupeleka shilingi bilioni 18.777 ambazo zimegawanyika katika maeneo manne. Kwanza ni fedha kwa ajili ya mitihani ya kidato cha nneambayo Serikali italipa moja kwa moja Baraza la Mitihani. Kwa hiyo, watoto wote kuanzia darasa la nne, form two, lakini kidato cha nnewenyewe watalipiwa na Serikali. Pili, ni fedha kwa ajili ya fidia ya ada, badala ya ile ada ya shilingi 20,000/= na shilingi 70,000/= Serikali inalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, fedha ya uendeshaji wa shule za msingi na sekondari, hizi zote Serikali italipa. Fedha kwa ajili ya chakula shilingi 1,500/= kwa kila mtoto wa shule maalum za msingi na kila mtoto wa shule za bweni za sekondari. Sasa kwa zile shule za bweni za sekondari, kwa zile shule za hostels ambazo zimejengwa na jamii hili limeleta mkanganganyiko kidogo, kwamba zile shule za bweni ambazo zimejengwa na jamii kupitia mipango yao wenyewe, kupitia wadau wengine wa maendeleo, hizi si hostels zinazotambulika na Serikali. Tunafahamu zipo, lakini siyo zile ambazo Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutambue kwamba shule hizo ni karibu shule 3,252 zenye watoto karibu 1,334,280, ni wengi sana. Kwa hiyo, huwezi ukakurupuka ukaja na mpango wa kuwalisha wale; tumeona tuanze na hawa wa bweni lakini baadaye kama itawezekana, tunaweza tukaenda huko, lakini siyo jambo ambalo sisi katika fungu hili la sasa, tumeliwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukue nafasi hii kuwaomba wadau, wazazi na Halmashauri husika maana ndiyo wadau muhimu katika mamlaka zile. Kama zilianzisha shule hizi za bweni, basi zijue utaratibu ziliokuwa zinautumia, ziendelee nao, lakini utaratibu huo sasa usiwe unatoka katika maagizo ya Wakuu wa Shule kuwaagiza wazazi wawalazimishe kuhakikisha kwamba watoto wao wana chakula, wanaleta bwenini. Sisi tumesema hizi shule siyo za bweni ni za kutwa. Kwa hiyo, tunaamini mtoto atakaa nyumbani na atakuja kusoma shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kumekuwa kuna jitihada ya kuwafanya wakae shuleni, ni jitihada ya nyongeza tu na hivyo jukumu lile linabakia bado kwa utaratibu ule ule wa wazazi na wadau na pengine mamlaka zao zilizoamua ziwepo hizo shule, lakini siyo jukumu la Serikali kwa sasa mpaka hapo baadaye.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nielezee hili kama sehemu ya jambo lililoletwa mkanganyiko mkubwa. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, kwanza kabisa kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana Naibu Waziri wangu Suleiman Said Jafo, ananipa ushirikiano mkubwa, ananiheshimu, tunafanya kazi vizuri na kwa raha sana.
Pili, namshukuru sana Katibu Mkuu Engineer Iyombe na Manaibu wake, Deo Mtasiwa anayeshughulikia masuala ya afya na Benard Makali ambaye anashughulikia masuala ya elimu pamoja na Wakurugenzi na Watumishi wote wa Wizara ya TAMISEMI; wanatupa ushirikiano mzuri na tunafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nipate fursa ya kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Kibakwe kwa kuniamini, lakini kwa kuendelea kunivumilia wakati naendelea kutekeleza majukumu ya Serikali. Nataka niwafahamishe kwamba nawapenda na baada ya Bajeti hii nitakwenda kuonana nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu imepata wachangiaji wengi sana. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote wa pande zote za Bunge kwa kutoa michango mingi yenye tija na maudhui mbalimbali katika kuboresha utekelezaji wa Serikali katika Wizara yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata wachangiaji na nikushukuru pia wewe na Wenyeviti wote mliosimamia Wizara yangu, kusimamia uchangiaji wa waliozungumza 140, si jambo dogo; na walioandika kwa maandishi 60 na wenyewe wamenipa michango yao, nawashukuru sana. Michango hii mingi pamoja na uzuri wake na aina na staili mbalimbali ambavyo imetolewa mimi kwangu nilikuwa nachukua yale muhimu yanayonisaidia katika kufanya maisha ya Watanzania yawe bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini hata ambao hawakusema, nao wangependa waseme, hata ambao hawakuandika nao wangependa waandike, lakini itoshe tu kwamba hawa wachache waliosema wametosha kuwakilisha wote na kwa hivyo, wote ndani ya Bunge hili mmesema juu ya Wizara yangu. Nawashukuruni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, siyo rahisi sana kujibu hoja zote kadri zilivyotolewa maana ni nyingi mno. Tutaandaa matrix maalum itakayokuwa inazungumza aliyesema na aliyeuliza jambo na ufafanuzi wake tulivyoutoa katika kabrasha maalum ambalo tutawapatia kabla hatujaondoka hapa Bungeni, ili kila mmoja ajue hoja atakazosema mtu mwingine ili aweze ku-refer katika hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zile chache nitakazobahatika kuzijibu, basi kama nitajaliwa kusema, nitazisema. Hata hivyo, ninazo nyingi sana hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu mwaka 2015 tukiwa kwenye uchaguzi, Watanzania wengi waliomba kwa dini zao mbalimbali, kwa ibada mbalimbali wakiiombea nchi hii ipate kiongozi atakayewapeleka mbele. Ni imani yangu kwamba Mwenyezi Mungu aliyapokea maombi ya Watanzania wengi na ndiyo maana tumempata Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye ameanza kutupeleka mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais Magufuli ni nani? Rais Magufuli ni mtu anayechukia rushwa, ufisadi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka, lakini anakusudia kukusanya kodi. Pia akishakusanya kodi anataka kubana matumizi. Dhamira yake ni ili kupunguza gap tuliloacha wanyonge na maskini wanaoishi maisha ya tabu katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo ya kisiasa katika dunia inatofautiana. Iko mifumo ya kijamaa na fikra na dhana za kijamaa, lakini iko mifumo ya kibepari na fikra na dhana za kibepari. Mtu anajitokeza na kujipambanua kama kiongozi wa watu; asipowazungumzia na kuwapenda maskini walioko chini, kuwanyanyua wakaribie walioko juu, huyu dhana yake na fikra yake ni ya kibepari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, misingi ya Taifa letu imejengwa katika fikra na mawazo ya Mwalimu Nyerere, ambaye aliheshimu usawa, haki na umoja. Usawa kwa kipato, usawa kwa hadhi. Kadri tunavyoacha gap kuwa kubwa kati ya maskini na wenyenacho, hatujengi Taifa sustainable. Taifa hili litakufa na mara moja litaondoka katika amani na utulivu, vitu ambavyo tumevijenga kwa muda mrefu sana wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maono haya anayoyafanya katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inarudi kwenye mstari sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Singapore, chini ya Waziri Mkuu Lee Kuan Yew, mwaka 1999 alipoichukua nchi ile ali-dedicate kuhakikisha kwamba anapunguza na kuondoa unyonge wa watu masikini. Matajiri hawa huwa wapo tu, lakini kazi ya kiongozi ni kuwachukua maskini, kuwasukuma, kuwaleta juu. Walikuwa na Sera kama zetu na wao walikuwa non-aligned movement, lakini leo wamefika mbali sana kwa sababu wamekubaliana wote na ni akili ya mtu huyu mmoja ndiyo imewafikisha hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, China, mwaka 1949 hadi 1980 chini ya Chama cha Kikomunisti, China imetoka ilipokuwa chini ya mawazo ya Mao Tse Tung na rafiki yake Biao ambao waliitoa China ilipo na walipewa fursa ya mawazo yao ku-prevail wakaifikisha China ilipofika. Nawaomba sana Watanzania, tumpe ruhusa Rais, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ana dhamira ya dhati, anatupeleka ambapo wote tunaona ni sahihi. Nami niseme pande zote mbili, dhana hiyo na sense hiyo inaonekana hata pamoja na msimamo ya Vyama vyetu, tukubaliane kwamba Rais wetu anaenda vizuri. Tuache afanye kazi, ashughulikie huu upungufu ambao upo?
Mheshimiwa Naibu Spika, wako watu kwa namna tunavyokuwa tunajenga Taifa linalopotea; utaona linaanza kuwa na madalali wengi na watu waacha kufanya kazi; Taifa linalopotea utaona watu wanakubaliana katika kupata fedha bila kufanya kazi; Taifa linalopotea utaona wenye nguvu wanaacha kufanya kazi, wanyonge na wasio na afya nzuri ndio wanaofanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoka leo kuanzia Dodoma mpaka kufika Dar es Salaam, miezi ya kilimo utakaowaona wanafanya kazi mashambani ni wazee na watoto. Vijana hawafanyi kazi. Ni lazima uamuzi wa dhati ufanyike na tukubaliane wote kama Taifa kwa sababu hata hizi siasa tunazozifanya leo, ni kwa sababu ya amani na utulivu na hiyo gap kati ya wenye nacho na wasio nacho imekuwa ikishughulikiwa kwa muda mrefu kwa miongo ya viongozi waliopita tangu tumepata uhuru mpaka sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunahitaji mawazo mapya, nami naamini mawazo sahihi ni ya Rais Magufuli. Rais wa namna hiyo anayetaka kuleta mabadiliko katika nchi yoyote ile duniani na hasa tulizoziona zikibadilika duniani, Rais wa namna hiyo huwa hataki urafiki na mtu, hataki aonekane kama ana kundi na ndivyo alivyo Mheshimiwa Rais Magufuli. Hana rafiki, hana swahiba, yeye ameipeleka nchi mbele; ukileta mchezo, anatuambia tunasonga mbele, wewe unabaki, tunasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wa pande zote, wale tunaomuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Magufuli tumfuate na tusonge mbele. Kura alizopigiwa Mheshimiwa Rais wala hazikutoka kwa misingi ya pande hizi mbili. Alizikuta kura za watu wanaonung‟unika na maumivu mengi hawajui cha kufanya; wakitusikiliza upande huu hawatuelewi, wakitusikiliza upande huu hawatuelewi. Tuwaache Watanzania wamfuate Mheshimiwa Dkt. Magufuli na sisi tuwaunge mkono na tusaidie Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa haya tunayoyafanya hapa ndani ya kupitisha Bajeti ili mambo yaweze kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, zimechangiwa hoja nyingi sana, lakini nianze kujibu baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge. Lilizungumzwa hapa suala la mgawanyo wa fedha ya Jimbo. Ni kweli nikiri kwamba tulifanya makosa katika mgawanyo wa fedha za kichocheo cha maendeleo ya Majimbo na kuzipeleka kwenye Halmashauri badala ya kuzipeleka kwenye Majimbo. Ndugu zangu, ndiyo tumetoka kwenye uchaguzi, tulikuwa tumewekana sawa, lakini basi imetokea kwa bahati mbaya, mtuwie radhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa waraka kwa Wakurugenzi wote nchini. Kwanza, tumewaambia wasimamishe na kama wamefanya, basi warudishe na kuhakikisha kwamba wanazigawa kwa misingi ya Majimbo, hizo hizo zilizokwenda kwa sababu hapa tuna changamoto tatu. Moja, ni kwamba kuna maeneo ambapo yamezaliwa Majimbo mapya, lakini fedha imepelekwa inataja Jimbo la zamani. Kwa hiyo, Jimbo lingine hili linapata shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili nalijua, kwa mfano, kule Bunda kuna rafiki yangu Boni halafu kuna Ester Bulaya. Kwa hiyo, unakuta pale sasa hawajui ni nani anachukua kipi? Tumetoa maelekezo mazuri, naamini watafanya masahihisho na vigezo vinavyotumika ni vile tulivyovisema hapa siku moja kwamba asilimia 25 ya fedha hiyo inayokuwa imepangwa kama ni fedha ya Mfuko wa Jimbo, huwa inagawanywa sawasawa (pro-rata). Asilimia 75 inayobakiwa inagawanywa kwa misingi ya ukubwa wa eneo, kiwango cha umaskini, lakini pia inagawanywa kwa kuzingatia kigezo cha idadi ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vigezo kwa mchumi aliyebobea ambao tunawaweka kwenye Halmashauri zetu, haviwasumbui katika kupiga hesabu. Hata hivyo, tunawasimamia kwa karibu ili tuweze kuona wanapiga hesabu vizuri na Majimbo yote yanagawanywa; kama ni ndogo, basi wote tupate kidogo kidogo, kama tutajipanga upya kwa mwaka unaokuja, tuje na hesabu nzuri zaidi ya bajeti ya kutosha kwa ajili ya Majimbo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala la Viti Maalum, kuwa Wajumbe wa Kamati za Mipango na Fedha kwenye Halmashauri. Jambo hili lina logic, lina sense, hakuna namna unaweza ukalipinga hivi na unaweza ukaonekana mtu wa ajabu ukilipinga bila kutoa sababu za maana. Maana hawa Wabunge wa Viti Maalum ni Wawakilishi wa wananchi. Kikao cha Kamati ya Fedha kinaalika Wajumbe mbalimbali na kikao kile wanachotoa pale ni mawazo, wala Mbunge hawi Mwenyekiti; wote ni Wajumbe tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuingia mle akatoa mawazo yake juu ya rasilimali zilizopelekwa kwenye Halmashauri, ubaya uko wapi? Mimi mwenzenu siuoni! Hata hivyo, masuala ya Kiserikali yanakwenda kwa mabadiliko ya kimaandishi. Kwa sababu jambo hili lilikuwepo, acha tulichukue tukalifanyie kazi na baadaye tutakuja na msimamo wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu kutopandishwa madaraja, wengi wamesema. Haya yamesemwa kwenye maoni ya Kamati lakini Wajumbe wengi wamesema. Mniwie radhi kwamba siyo rahisi kuwataja majina, maana vinginevyo nitachukua muda mrefu, lakini nitatambua kwenye majibu rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu kutopandishwa vyeo mwarobaini wake sasa umefika. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lililopita kwa kupitisha Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu. Hivi katika bajeti yangu hii, nimeleta bajeti ya kiasi zaidi ya Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya Tume hii kuanza na tunaendelea kuzungumza. Tunaamini Tume hii Makao Makuu yake itakuwa Dodoma ili waweze kuwahudumia Walimu kwa urahisi. Tume hii ikianza, ndiyo itakayomaliza matatizo yote haya ya Ualimu ikiwa ni pamoja na hili la kupandisha madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu wetu wameumia sana. Mtu anafanya kazi, maana kupanda madaraja ni kila baada ya miaka mitatu, mitatu. Mtu anafika miaka tisa hata kumi na mbili hajapandishwa daraja, halafu aliyeanza kazi, ame-lobby lobby amefanya ujanja, sijui ametoa rushwa, amepandishwa daraja mpaka anamzidi aliyefanya kazi miaka kumi. Hii haiwezi kukubalika na tutaliangalia. Tume hii siku nitakapokuwa naizindua, nitahakikisha first task ni hiyo na hata ikibidi tuweze kutengeneza upandaji wa madaraja wa mserereko ili waweze kukutana na wale waliopanda wakipitiliza, basi na wenyewe tutawashusha kwa sababu wapo pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo limechangiwa na wengi lakini pia na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya TAMISEMI, ni mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam, yaani DART. Ni kweli mradi huu ulikuwa na makando kando mengi sana. Kweli kabisa! Hakuna asiyejua, ni ukweli kabisa! Makando kando mengi ya DART kama DART, yamesababishwa na DART kumchukua mwendeshaji wa muda. Maana kulikuwa na mwendeshaji wa kudumu anayekuja kuendesha mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam, ambapo kulingana na miundombinu ilivyokuwa imekamilika, mchakato wa kumpata mwendeshaji wa kudumu unaweza ukachukua miaka miwili hadi mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yakatokea mawazo mema na mazuri tu kwamba jamani hivi hapa nchini kwetu hatuwezi kupata mwendeshaji wa muda kwa kipindi cha miaka miwili hadi hapo tutakapompata mwendeshaji wa kudumu? Jambo hili likaonekana ni jema kwa sababu shida tunayoipata Dar es Salaam tunaiona, miundombinu imekamilika, tunasubiri nini? Kwa nini tusianze? Ukiangalia kwa watu wenye uzoefu wa ku-operate mabasi mengi na wenye facilities, ikiwa ni pamoja na garage kubwa, maeneo makubwa ya kuweza kutunza magari na mass operation, a big flit ya mabasi kama 100 hadi 200, wenye uwezo huo ni UDA.
Kwa hiyo, UDA na wao wakaomba kama walivyoomba waombaji wengine. Katika ku-evaluate hao waliokuwepo huko wakati huo, wakaona kwamba UDA wanaweza wakatusaidia katika ku-operate mabasi haya kwa muda. Kilichotokea ni kwamba kumbe UDA nyuma yake ana makandokando mengi. UDA inamilikiwa sasa na kampuni inaitwa SGL. Kampuni ya SGL ikawa ime-assume kwamba imechukua the full control ya Shirika la UDA na ikaanzisha kampuni ya UDART iliyokuja kuomba kazi DART.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kilichotokea pale ni kwamba, sisi tulipoingia mwezi Desemba, tukaanza kazi, tukaangalia, tukawaambia hapana, uhalali wa UDA huku tunauona una mashaka. Kwa hiyo, hatuwezi kuendelea na huyu.
Kwa hiyo, mambo makubwa matatu tuliyo-achieve ni yafuatayo:-
Moja, tukawaambia sikiliza, wewe unasema una full control ya Shirika la UDA, umetoa wapi hiyo full control? Anasema nimenunua hisa kutoka Jiji. Lete vielelezo; akaleta. Tukamwambia lakini unadaiwa wewe! Huko Jiji la Dar es Salaam kwenyewe hujamaliza kulipa deni lote. Akasema ninachodaiwa nadaiwa tu, lakini hizi hisa nilikwishazinunua. Kwa hiyo, ushahidi wa hayo na kesi ya Jiji na UDA na SGL ilikuwepo Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya sana tulipofikiria kushughulikia jambo hilo, tukajikuta tunafungwa, maana yake waliingia mpaka Deed of Settlement kati ya Jiji na Simon Group. Deed of Settlement na wakasajili Mahakamani ya kwamba kweli amenunua, lakini tunamdai fedha hizi na kwamba akitulipa fedha hizi tunampa the full control ya shares zetu asilimia 51.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo tulimkuta SGL amemfungia sandukuni TR ambaye ana asilimia 49 shares. Tukaenda pale tukamwambia kama humfungulii huyu, sisi hatuzungumzi na wewe. Akaenda Mahakamani akasema nafuta hii kesi ya kumfungia huyu Mahakamani, akamfungulia. Tukamwambia TR wewe asilimia zako 49 zipo? Akasema asilimia zangu 49 mpaka nikazi-verify. Akaenda aka-verify, tukazikuta asilimia 49 zile, tukazikomboa, zipo. TR anazo asilimia 49 za hisa. Kwa hiyo, Serikali mle kwenye UDA ina asilimia 49, lakini tukamkuta UDA amechukua unissued shares au unallotted shares, amezichukua zote zilizokuwa zimebakia za wabia, wanahisa wawili kati ya Jiji la Dar es Salaam na Treasury Registrar, anasema zote zile za kwake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi 49 tumeshazikomboa lakini anasema hizi unallotted shares, hisa zisizogawiwa, anasema na hizi ni zangu, Bodi iliniuzia. Tukaenda tukamshinda, akasema nakubali bwana, sitaki kupoteza huu mradi, narudisha. Kwa hiyo, amekubali, amezirudisha zile hisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumekomboa unallotted shares, tumemrudisha TR kwenye nafasi yake ya share zile 49, tumebakia na kampuni ya SGL ambayo ni kampuni ya Mtanzania ambayo ina hisa 51 alizozinunua Jiji. Sasa kila kitu Jiji as an authority wamekifanya, Jiji as an authority wamepokea hizo pesa; Jiji as an authority wamekubali kuuza. Leo mkisema turudi tuka-nullify ile sera, kwa maslahi ya nani? Maana sasa mradi unasimama. Kutafuta mtu mwingine it will take us three or four years. Serikali hii kazi yake pia ni kuwezesha, lakini tunawezesha watu ambao wanafanya mambo kisheria. We have tried to prune him in every wrongs that he did; tumemtoa huko!
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tutakubaliana, naomba nisiendelee na hili maana ni refu mno. Tunakuja kutoa taarifa rasmi ya Serikali ndani ya Bunge na Wabunge tutaliangalia on merits tutakubaliana. Mkisema tusifanye, Serikali hatulazimishi. Mkisema tufanye, kwa sababu Dar es Salaam kuna foleni watu wa Dar es Salaam na sisi tunaumia, tutaangalia the option.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hatulazimishi kufanya, tumeyakuta madudu tumeya-clear. Sasa kwa nini tubebe sisi msalaba? Msije mkaniua, mkanishikia vifungu vyangu hapa! Nipeni bajeti yangu mimi niendelee, nina mambo mengi ya kufanya ya afya na kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Property Tax kwamba sasa ikusanywe na TRA; hivi nani hapa haiamini TRA? Mkusanyaji mkubwa wa kodi katika nchi hii, whatever kodi, popote pale, ni Waziri wa Fedha. Waziri wa Fedha ndiyo mwenye TRA! Sasa kama anasema ana njia na ana muscles za kukusanya zaidi kuliko sisi, kwani hivi bajeti za Halmashauri za Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinatoka wapi? Over 95 percent Halmashauri zetu hazina uwezo wa kujitegemea hata kwa asilimia tano. Hela zote zinatoka Serikali Kuu Hazina, anayekusanya ni TRA. Sasa akisema anataka kukusanya, sana sana unamwambia baba nakushukuru, ukikusanya niletee. Basi! Mimi sioni kama kuna tatizo hapa! (Makofi)
Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, sisi tutadai haya mafungu tunayopendekeza, Waziri wa Fedha atuletee. Akisema anataka kukusanya, hewala; akisema kusanyeni nyie hewala, lakini tumekubaliana kwamba sisi Mamlaka ya Serikali za Mitaa hasa kwa mfano kwa Dar es Salaam, tulikuwa tumejiandaa vizuri sana katika kukusanya kodi hii, naye akasema mimi sifanyi chochote, nitapokuja tutashirikiana kwa pamoja, lakini fedha hii itakusanywa. Ninyi kinachotakiwa kufanya, si tumepitisha bajeti, tumwombe Waziri wa Fedha atupe fedha zile tulizopitisha, that is it.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo naomba tuliangalie, lakini kimsingi sioni tatizo lake na wala sitaki kuingia kwenye matatizo na sioni tatizo kwa Waziri wa Fedha na wala sioni kwamba ana nia ya kutokuisaidia Wizara yangu kufanya kazi, mimi naiona dhamira yake ni njema. Kazi yangu mimi na nyie Wabunge ni kusimamia, mimi kuhakikisha kwamba napata fedha kutoka kwa Waziri wa Fedha ili tuweze kupeleka malengo na bajeti iweze kutekelezwa mbele zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, posho za Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Sheria namba saba (7) na nane (8), ukizisoma kwa pamoja na program mbalimbali tulizonazo tulikubaliana kwamba asilimia 20 ya mapato ya ndani yapelekwe kwenye vijiji na asilimia 20 ya mapato ya ndani haya ni vyanzo vya ndani, actual own source na ile ambayo huwa inapelekwa kutoka Hazina ya fidia ya vyanzo vya mapato vilivyofutwa, vilivyokuwa kero. Kwa hiyo, ukichukua ile, ndiyo inayoitwa own source kwenye Halmashauri, yaani vyanzo vile vinavyopatikana na vile ambavyo vilifutwa na Serikali Kuu inavifidia kwenye Halmashauri. Ukivijumlisha ndiyo unatakiwa uchukue 20 percent uipeleke kwenye vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hii kwa baadhi ya maeneo ya vijiji na kwenye Halmashauri zetu inawasaidia sana Wenyeviti wa Vijiji kwa mgawanyo ufuatao:-
13% ya fedha hiyo inakwenda kwenye vijiji; 4% inakwenda kwenye Ward C; na 3% inakwenda kwenye Vitongoji. Kwa hiyo, at least hata kama ni kadogo, kanaweza kufika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii fedha siyo ndogo kwa kila eneo; own source ya Dar es Salaam ni Shilingi bilioni 85. Hebu piga 20 percent halafu uipeleke kwenye Mitaa kwa own source ya Manispaa ya Ilala peke yake ni bilioni 85. Piga 20 percent of it, peleka kwenye Mitaa, it’s a big sum, inaweza kusaidia. Own source ya Mpwapwa inaweza ikawa ndogo, ukichanganya na ile ya ruzuku, inaweza ikasaidia kitu.
Waheshimiwa Wabunge, tuna mambo mengi ya kufanya, tuna shida nyingi kwa wananchi wetu. Hili ni jambo jema! Nami nasema naona kabisa umuhimu wa Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Vitongoji, ikiwa ni pamoja na Madiwani. Wanafanya kazi nzuri, lakini iko nature ya aina fulani za kazi if we exaggerate tutajikuta nchi hii kila mtu anastahili kulipwa hela inayotoka Hazina na hela hiyo haitoshi. Ziko kazi nyingine kwa nature yake ni kutaka heshima tu. Mashehe na Wachungaji, hawalipwi mishahara. Wanachongojea ni sadaka ikipelekwa, hewala; isipokuwepo, hewala.
Vile vile zipo nature za kazi nyingine ni za kujitolea, kwa mfano, Wenyeviti wa Vijiji. Kwanza unaheshimika, watu wanakuja pale kwako, lakini vijiji vyenyewe mle mle ndani vina makusanyo. Ndiyo maana vijiji huwa vinatakiwa kusoma mapato na matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kila kikao baada ya miezi mitatu, kijiji kinatakiwa kusoma mapato na matumizi. Hivi huwa wanasoma mapato na matumizi yapi? Kuna incomes mle ndani za minada, soko na nini. Naamini, Waheshimiwa Wabunge wote wa pande zote twendeni tukatafakari vizuri tukaangalie uhalisia, tukikutana hapa kwenye bajeti nyingine, tunaweza tukawa tumeboresha wazo hili, tukaona namna bora ya kulifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amehimiza usafi, lakini tunazo sheria mbalimbali. Usafi ni lazima uende pamoja na upangaji wa miji yetu. Lazima kila Halmashauri nchini iweke utaratibu wa kuwekeza katika upangaji wa miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, problem ya nchi yetu, shida yetu sisi Watanzania, kila mmoja anategemea program. Kila mmoja anategemea mpango utakaokuja na fedha, tena zisiwe za ndani tu, ziwe mpaka za nje, huyo mtu utakuta amechangamka kweli! Yako mambo wakati mwingine hayahitaji hata pengine program! Hata wakati mwingine hayahitaji fedha!
Mheshimiwa Naibu Spika, tuchukulie wewe una Maafisa Ardhi watatu, wanne kwenye Halmashauri yako, hebu niambie kama kila siku wanapima square meter labda ya 5,000, yaani kila siku wanachukua na vibarua wale wanaenda site wanapima; si wamefundishwa kupima na kupanga! Hivi kweli kama wangekuwa wanafanya hiyo kazi kila siku, baada ya miaka mitano, miji yetu itakuwa vile? Wamekaa pale wanangojea waletewe program na pesa wakati wameajiriwa kwa ajili ya kazi ya kupima na kupanga!
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, nyie ni Wajumbe, kwenye Vikao vya Baraza la Madiwani, twendeni tukawahimize watu wetu, pamoja na program zinazoandaliwa na Wizara ya Ardhi, pamoja na program zinazoandaliwa na Wizara yangu ya TAMISEMI, bado tuna haja ya kutumia ile human resource tuliyonayo kule hata kama ndogo kuhakikisha kwamba inafanya kazi ile kila siku ili kupunguza migongano na matatizo yanayotokana na miji yetu kutokupangwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika usafi wenyewe wa kawaida huu, tumetoa wito na Mheshimiwa Rais ametoa mfano. Nachukua nafasi hii kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameanzisha utaratibu mzuri wa kuwafanya vijana wachangamkie usafi na anasema usijifanye mstaarabu, kuwa mstaarabu na ili uwe mstaarabu ni lazima uonyeshe usafi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, usafi wa mazingira ya makazi yetu, usafi wa sehemu zetu za biashara ni muhimu sana. Tujitokeze Watanzania kutengeneza Taifa lenye usafi na kila mmoja awajibike, tusitupe uchafu hovyo. Pengine unakuta gari ya Mbunge au Waziri au Kiongozi anaenda Dar es Salaam, mnafuatana njiani, anatupa chupa ya maji barabarani. Sisi tuonyeshe mifano mizuri ya kufuata taratibu na kanuni za usafi.
Mengi niliyoyasema haya yalisemwa na upande wa Kamati ya TAMISEMI lakini na Waheshimiwa Wabunge wengi walichangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili ambalo limesemwa kwenye hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba Serikali Kuu inaingilia madaraka ya Serikali za Mitaa kwa kufanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala, Wakuu wa Wilaya na akadiriki kusema mpaka Wakurugenzi. Pia likazungumzwa hili jambo lingine kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanaingilia mamlaka na majukumu ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ngojeni niwakumbushe na sitaki kuchukua maneno mengi, ngoja niwasomee sheria. Mwingiliano huu tunaousema unaweza ukawa na tafsiri zinazolingana na mazingira yetu, lakini naomba niwakumbushe; na bahati mbaya hii citation iko kwa Kiingereza, sasa naomba niisome:
“In relation to the exercise of powers and performance of functions of the Local Government Authorities conferred by this Act.” Hii ni sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, urban authority lakini this provision reads the same as the one in the District Authority.” Anasema: “in relation to the exercise of powers and performance of the function of the Local Government Authorities conferred by this Act.” Kifungu cha 78(a), lakini kwenye JUTA, ile sheria rasmi ni kifungu cha 87.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasema: “The role of the Regional Commissioner and of the District Commissioner shall be to investigate the legality when questioned of actions and decisions of the Local Government Authorities within their areas of Jurisdiction and to inform the Minister (The Minister in respect of this law is the Minister responsible na TAMISEMI) or take other appropriate action as may be required. The legality of the actions, decision and the way of doing things kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, inaweza ikahojiwa, ikatazamwa na kuangaliwa na kuchukuliwa hatua na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya. Sio mimi, ni sheria. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, shida moja inayokuja siyo kwamba wanaingilia. Wao, why tunasema wanaingilia? Kama vitu vinaenda sawasawa, assume everything goes vizuri, vitu vinaenda sawasawa! Tukimkuta Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya anaingilia, tunamshangaa. Why unaingilia mamlaka halisi ya watu hawa ambao wanaweza kufanya mambo yao? Hao wamefanya kosa na watachukuliwa hatua, pindi tukiwakuta wanaingilia wakati mambo yanakwenda sawa. Pia hatuwezi kusema wasiingilie kama mambo hayaendi sawa. When things are not moving okay, hatuwezi tukasema sisi ni mamlaka ya Serikali, tumepanga, tumeamua! Mmepanga, mmezingatia sheria?
Mmezingatia kanuni? Mmezingatia taratibu? Kama mmezingatia hivyo, then there is no need of interference. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hakuzingatia, wanasema…
MHE. PAULINE P. GEKUL: (Aliongea nje ya microphone).
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gekul, mwache Mheshimiwa Waziri amalize kujibu hoja.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, wanasema the legality; kwa hiyo, the legality maana yake ni kwamba tuna-assume kwamba kuna kitu kimevunjwa na ndiyo maana lazima wafanye interference. Hiyo ndiyo tafsiri ya sheria na niwaombe sana, hakuna mwingiliano wowote unaofanyika na wale watakaokuwa wanaingilia, leteni taarifa tujue wameingiliaje, tutafsiri kwa mujibu wa majukumu yao tuone kama wameingilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema eneo lingine ni kwamba Wakurugenzi wapatikane kwa kufanya usaili. Ni mawazo, tunayachukua kama kweli tutaweza kupata watu bora, lakini kuna shida huko kubwa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine lililosemwa na watu wengi ni uanzishaji wa maeneo mengi ya utawala. Waheshimiwa Wabunge nchi yetu bado ni kubwa. Ukiangalia namna tunavyokwenda na kuigawagawa pengine the rationale kwenye hii hoja ni kwamba, mgawanyo ambao hauzingatii matatizo genuine kama alivyosema Mheshimiwa Keissy, kwamba unalikuta eneo lingine ni kubwa sana na hapa Kambi ya Upinzani mlisema pengine tuzuie mgawanyo tena wa nchi hii, imetosha; ili tuhakikishe tumefanya. Yako maeneo mengine bado wenzetu hawajaridhika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano. Mkoa wa Kilimanjaro, una square kilomita 14,000 plus or something; Wilaya ya Mpanda Vijijini ina square kilomita 19,000, unasemaje unazuia mgawanyo? Ukiichukua Kilimanjaro ukaijumlisha pamoja na Zanzibar, haiifikii Mpanda Vijijini. Watu wanaongezeka. Ndiyo maana sasa hivi wala hatukai kwa makabila, tunahitaji kufanya movement. Twendeni, ni lazima tutaendelea na hili, hatuwezi kufanya hivyo, lakini tutajaribu kuzingatia alichosema Mheshimiwa Keissy, tuangalie uwiano upya na vigezo vinavyotumika isije ikawa ni upendeleo unaofanyika na ambao utatuletea nchi yetu kuingia kwenye imbalance of peace. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine lililosemwa na Wabunge wengi pia kwamba barabara za Halmashauri zichukuliwe na TANROAD. Waheshimiwa Wabunge wa pande zote mbili, jambo hili haliwezi kutupeleka kwenye jibu. Ni vizuri nichukue maoni yaliyotolewa na mtu mmoja nilimsikia alisema tuanzishe Wakala wa Barabara za Vijijini, Barabara za Halmashauri. Hili amelichukua kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Naomba niisome. Katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi kifungu cha 39(a)(3) kimesema:
“Kuanzisha Wakala au Taasisi itakayosimamia kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za Miji na Majiji na Halmashauri ambazo ziko chini ya TAMISEMI.” Kwa hiyo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ililiona hili na sasa hivi wataalam wanafanyia kazi jambo hilo kutuletea namna bora ya kuweza kuanzisha huu Wakala. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni changamoto za elimu ya msingi bila malipo. Tumejitahidi sana. Serikali ilipoingia madarakani kuanzia mwezi Desemba hadi Juni kabla hatujapitisha hii bajeti, tulisema lazima tuanzishe elimu bila malipo. Msingi wa hili Waheshimiwa Wabunge, kusema ukweli ni hali ngumu waliyokuwanayo baadhi ya wazazi kutoka familia maskini katika kuwapeleka watoto wao shule. Ilikuwa siyo rahisi kwenda kumwandikisha mtoto darasa la kwanza. Mambo yaliyokuwa ni magumu! Mzazi alitakiwa kutoa hadi Sh. 20,000. (Makofi)
Kwa hiyo, dhana ya elimu ya msingi bila malipo, inazingatia uendeshaji wa shule bila ada, wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi wa wanafunzi. Vile vile hatukusema wadau hawawajibiki! Huku mbele tukazungumzia; na jana nilimsikia rafiki yangu, shemeji yangu Mheshimiwa Cecilia Paresso, shukuru Mungu mimi nimeoa kule kwenu, najua hili jambo limewasaidia wangapi kwenda shule! Watoto wa maskini walikuwa hawaendi! Katika uandikishaji wa darasa la kwanza mwaka huu, malengo yetu tumepita kwa karibu watoto 400,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, ina maana hawa 400,000 wasingekwenda shule! Rwanda watoto waliokwenda darasa la kwanza mwaka huu ni 150,000; Burundi ni 120,000. Sisi 400,000, hawa walikuwa ni sawasawa na watoto wa darasa la kwanza wa nchi mbili, wasingekuwa wanakwenda shule. Tungetengeneza bomu la namna gani? Leo wanakwenda shule kwa sababu Serikali imeamua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepanga mpango kwamba tulianza kuanzia Desemba mpaka Juni, 30 tupeleke Shilingi bilioni 18.77 kwenye shule zetu na zinaenda straight kwenye shule na hizi ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watoto hawa wanasoma, hakuna michango ya uendeshaji wa shule; hakuna michango ya ada; na tumefuta ada kwa ajili ya Sekondari na tumefuta gharama za kulipia mitihani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwezi wa Kwanza mpaka mwezi wa Sita mwaka huu tutapeleka Shilingi bilioni 131. Fedha hizi ni nyingi! Unasema hatukujipanga, hata takwimu zako ulizokuwa unazisoma jana zime-tally na hizi ninazozisema mimi. Kwa hiyo, information uliyotupa ni sahihi tumeitekeleza, lakini bado tuna changamoto, lazima tuzishughulikie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zenyewe tuliposema shule za bweni, tulimaanisha shule za bweni zile ambazo zinajulikana Kitaifa, lakini Shule za Kata na zenyewe zilijenga mabweni na kuna watoto wanaishi pale. Je, watakula wapi chakula? Haya ni mambo tushirikiane, tunajenga Taifa letu! Hatukuwa hivi tulipo leo. Tumefika hapa kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa na waliopita. Tusilaumiane, tushauriane. Tusikatishane tamaa, tusaidiane ili tuweze kutimiza matarajio ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubadili kanuni za Halmashauri ili kuruhusu uwepo wa Kamati za Uwekezaji, tumeanza. Halmashauri sita tunafanya pilot study kwenye Halmashauri sita na hili limesemwa na watu wengi. Zikifanikiwa hizi, tutaanzisha Kamati za Uwekezaji kwenye kila Halmashauri, kwa sababu wengi wanapenda kukopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la maslahi ya Madiwani nimelisema. Ufinyu wa bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya barabara, maji, afya, ni kweli hatuwezi kumaliza kila kitu kwa bajeti hii. Waliopata this time, next time watapata wengine. Kwa hiyo, sisi tunatunza record na tutajitahidi kugawa rasilimali hizi kwa uwiano na vigezo sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nisiache kuzungumzia masuala ya mgawanyo wa bajeti ya ruzuku. Ile ruzuku ugawanyaji wake na vigezo vilivyoweka ilikuwa ni only population; lakini katika data analysis za kisasa, ni lazima uangalie poverty margin, uangalie ukubwa wa eneo, uangalie population. It is not only population!
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mengi kama nilivyosema yamesemwa, lakini kusema ukweli siyo rahisi kuyajibu yote. Nakushukuru sana na nawaomba sana Wabunge wote wa pande zote muunge mkono bajeti hii. Hii bajeti ndiyo maisha ya Watanzania! Nawaomba sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Yule atakayepinga, ananikatisha tamaa. Tuache twende tukatekeleze yale ambayo tumewaahidi wananchi na niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wote wa pande zote mbili, muunge mkono bajeti ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza kabisa, niseme tu kwamba maoni mengi yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na kwa sababu Wizara ya TAMISEMI inafanya kazi kwa karibu na Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, tutashirikiana kuhakikisha kwamba yale yote yanayohusu TAMISEMI tunayashughulikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili eneo ambalo limeguswa sana ni tozo na ushuru kwenye Mamalaka za Serikali za Mitaa kupitia Sheria ya Fedha, Sura Na.290 ambayo imebainisha vyanzo mbalimbali ambavyo vinatoka kwenye kilimo na vingine kwenye biashara, lakini hapa nitazungumza kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli ni kweli kabisa na Mheshimiwa Rais amesisitiza sana kwamba tufanyie kazi eneo hili la kodi kwa maana ya ushuru na tozo mbalimbali kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kwamba haziendi kutozwa kwa watu maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya majukumu makubwa ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kwamba tunajenga uwezo na kujenga mazingira ya wananchi wetu ili kuweza kujitegemea na kuishi maisha bora. Watu hawa wanapojitegemea hivyo, kazi ya Serikali ni kujenga mazingira wezeshi, kuwafanya watu hawa waweze kumiliki lakini pia kuendesha biashara zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumegundua mambo yafuatayo katika utafiti na ndiyo maana baadaye nitasema nini tunafanya, kwamba kuna problem ya double taxation yaani kodi zinatolewa mara mbili katika jambo moja. Pia kuna kodi kufanana, kwa mfano, mahali ambapo unatozwa service levy haupaswi tena kutozwa produce cess, kwa hiyo, hizi unakuta kule zinakuwa zinatozwa zote kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumegundua kwamba kuna tozo hutozwa kwenye mitaji yaani tozo inatozwa kwa kupiga hesabu ya mtaji badala ya faida. Pia kuna tozo za ushuru usiozingatia mazingira ya uzalishaji, haya yote tumeyafanyia kazi na AG ataleta hapa mabadiliko ya sheria ambayo sisi kwa upande wa TAMISEMI tumeshamaliza tumepitia sheria zote, tumeangalia zile tozo zote, tunadhani nyingine zinahitaji kuletwa hapa ili tubadilishe sheria zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tulitunga hapa sheria ambayo inatoza service levy hata kwa non corporate entity, yaani mtu ana kibiashara cha saloon unamtoza service levy 0.3% ya turn over, huu ni unyonyaji, haiwezekani! Hii ilikuwa inatozwa kwa corporate entity tu, kampuni kubwa ndiyo inatozwa lakini sio mtu ana saloon ya mtaji wa shilingi milioni tano unamtoza service levy, hii siyo sawasawa. Kwa hiyo, marekebisho hayo yote tutayazingatia na maandalizi ya sheria yako tayari, tutaleta hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Waziri wa Elimu kwa kuwasilisha bajeti nzuri, lakini pia kwa kutekeleza majukumu yake vizuri pamoja na watendaji wote wa Wizara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachukua nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote wa pande zote mbili, kwa michango yao mizuri ambayo kwa hakika inalenga katika kusaidia Taifa hili kwenda vizuri katika suala zima la uhai wa Taifa kwa maana ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa mengi hapa na pengine niseme tu, yote haya sisi kama Wizara ya TAMISEMI ambao ndio wamiliki wa shule za Serikali, maana hapa kulikuwa kuna kuchanganya kidogo mambo na pengine nitumie nafasi hii kueleza kwa uwazi; kwa nini tuligatua shule zile za Serikali kutoka Wizara ya Elimu kuleta TAMISEMI? Msingi wake kwanza ni wa kikatiba, ugatuaji wa madaraka ni wa kikatiba. Ukisoma Ibara ya 145(1) na Ibara ya 146(2) zinaeleza juu ya uanzishwaji wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri lakini pia mamlaka hizo zinapewa majukumu ya huduma za jamii, afya, elimu barabara na mambo mengine yote yanayohusiana na jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kulikuwa kuna mjadala mkubwa na ninajua mjadala huu umekuwa ukiendelea hata kwenye ma-corridor ambapo kimsingi mjadala huu unataka kuturudisha tulikotoka; kwa maana ya kwamba Wizara ya Elimu isimamie shule zote, isimamie wanafunzi wote, itunge mitihani, itunge vitabu; yaani ishughulikie ithibati, imiliki shule za Serikali, iangalie shule za binafsi, iangalie vyuo, iangalie Vyuo Vikuu, vyote hivi vinarudisha Wizara ya Elimu. Tunarudi tulikotoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema tukaangalia kama TAMISEMI imeshindwa, imeshindwa kwa sababu gani? Kwanza nieleze, mgawanyo wa haya majukumu ni upi? Baada ya mafanikio ya MESS I na MESS II, katika elimu ya sekondari mwaka 2008 Serikali ya Awamu ya Nne iliamua kugatua shule hizi kuzipeleka kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa. Majukumu ya TAMISEMI ni yafuatayo katika elimu: kusimamia uendeshaji wa elimu msingi, yaani Elimu ya Awali, Elimu ya Msingi, Elimu ya Sekondari, Elimu Maalum na Elimu ya Watu Wazima.
Pili, kuratibu upelekaji wa rasilimali fedha na ruzuku za uendeshaji kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, lakini tatu kusimamia matumizi ya fedha na ruzuku shuleni, lakini nne, kuimarisha rasilimali watu kwenye ngazi za shule, Halmashauri na Mikoa na tano kusimamia uwajibikaji wa watendaji wote na viongozi wote wa elimu kwenye ngazi za shule na Halmashauri za Mikoa; sita, kusimamia uendeshaji wa michezo katika Shule za Msingi na Sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya ni majukumu ambayo yamekabidhiwa kwa TAMISEMI. Sasa TAMISEMI ni nani? Ni mamlaka za Mikoa, Wilaya na Halmashauri zetu kwamba leo hii Mkurugenzi yule ndio mwajiri wa Walimu wa Sekondari. Ni rahisi sana kwa mfano shule za kwenye Wilaya yako ya Kasulu kwa mfano kuhudumiwa na Mkurugenzi shughuli zao zote. Issue hapa: Je, Mkurugenzi anawahudumia? Kwanini hawahudumii? Ndiyo issue ya kujadili. Anashindwa nini? Hana nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kuhamisha! Mnakumbuka ilivyokuwa maandamano Wizara ya Elimu pale, palikuwa hakuna hata mahali pa kukanyaga, tulikuwa tume-centralize. Ukisoma hata democratic development za aspects mbalimbali za kimaendeleo ya kidunia decentralization ndiyo mfumo wa kidemokrasia. If you centralize, maana yake unataka mtu anayesoma shule ya Kasulu kule, yule Mwalimu Mkuu awe chini ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Dar es Salaam. Hizo allowance za kumlipa anaposafiri kwenda kucheki kule na kurudi, tutazitoa wapi? Tusirudi kule tulipotoka jamani, kama kuna makosa, tuyajadili hayo. Mimi sisemi kwa sababu nipo leo TAMISEMI, naweza nikatoka kesho, lakini tunataka kurudi kule kwa jazba. Wizara ya Elimu ina majukumu gani? Hebu tuyaangalie. (Makofi)
Kwanza huo udhibiti, hapa yanazungumzwa masuala ya vitabu; huo udhibiti tu peke yake, ni majukumu makubwa kweli kweli! Ithibati peke yake ni majukumu makubwa; Vyuo Vikuu peke yake ni majukumu makubwa; Vyuo vya Elimu hivi vya kati vya Diploma na Certificate ni majukumu makubwa; Vyuo vya VETA ni majukumu makubwa! Leo mnasema na shule turudishe kule. Tunataka kufanya kosa walilolifanya waliopita. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu wali-centralize na mambo haya yakashindikana na leo tumeongeza shule, tuna shule nyingi, tuna Walimu karibu laki mbili wa Shule za Msingi, tuna Walimu karibu laki moja wa Sekondari. Hawa wote tunataka waende Dar es Salaam. Tuna wanafunzi hawa; hivi inawezekanaje? Hebu tutafute jibu, kwaniini hatutoi huduma nzuri? Tatizo ni kwamba tuliokabidhiwa ambao ni sisi Wabunge, tupo kwenye Halmashauri, ndipo shule zilipo; tuna Wenyeviti wa Halmashauri, ndio wanaowa-controll kwa nidhamu na kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, wanasimamia, rasilimali, zinakwenda? Ndiyo maana Mheshimiwa Rais anasema kama kuna uozo, upo kwenye Halmashauri. Mimi sikatai, ni kweli. Hapa tusaidiane Waheshimiwa Wabunge, hili Taifa ni letu. Tunapofika hatua fulani, lazima tukubaliane wote; na ndio maana nataka nikubaliane na aliyesema hebu siku moja tufungiane kusiwe vyombo vya habari. Nafikiri alisema Mheshimiwa Mbatia, akasema, hebu tuzungumze mambo ambayo tuna maslahi wote ambayo yanafanana. Tukiwa tunazungumza tuna-criticize tu hapa hatuwezi kupata majibu. Kwa mfano, unazungumzia waliosimamia mitihani mwaka 2014/2015 kwamba hawajalipwa baadhi ya fedha zao. Unajua kilichotokea? TAMISEMI wameomba 17.7 billion, Wizara ya Fedha ikatoa 17.7 billion. TAMISEMI wanakwenda kupeleka kwenye Halmashauri zile pesa, wanasema hazitoshi. Wanarudi wanaomba 6.8 billion kwamba hizi hawa wamekosa. Unauliza 6.8, how? Wanasema, kwa sababu hii na hii; hebu leteni mchanganuo. Mchanganuo unakuja, 1.04 billion. Sasa hebu niambie, kwanini Waziri wa Fedha asikatae kutoa fedha, aseme ngoja kwanza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nasema uozo upo kwenye Halmashauri zetu. Ni lazima wote tujikute tuna majukumu na sisi Waheshimiwa lazima tuhakikishe tunahudhuria vikao vya Halmashauri kwa sababu tumepewa majukumu makubwa. Halmashauri zimepewa majukumu makubwa na ndiyo maana tunawajibika katika hata huu upungufu kwa sababu maamuzi yote tumepewa sisi kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili PAC na LAAC na Makamu Wenyeviti wao pamoja na Wajumbe wa Kamati hizi kwa kazi kubwa na nzuri wanazozifanya na kwa namna tunavyoshirikiana katika kufanya kazi ya maendeleo ya Watanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zimezungumzwa hoja nyingi sana, lakini kwa sababu ya muda pengine sio rahisi sana kuweza kuzijibu zote vizuri na nyingine ni mambo yanayoanza upya. Hata hivyo, nataka niseme jambo moja tu ili Bunge na sisi wote kwa faida ya maslahi ya Watanzania tuweze kuwa makini nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapojadili Taarifa za Kamati ni lazima mambo tuliyoyachukulia hatua na kuyamaliza kwenye Kamati kule hayapaswi tena kuja huku na yanapokuja huku yanataka mjadala mpana sana ambao haupo. Kwa hiyo, tunapata shida kwa sababu baadhi mambo hapa tulikuwa tumekwishayazungumza na pengine ilipaswa kuwekwa vizuri ili yasirudi nyuma tulikotoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukulie mfano tu suala la UDA. Suala la UDA ni la muda mrefu, lakini nizungumze kifupi tu sitaki kwenda kwenye historia, ikuwaje na ikawaje. Nina muda mrefu lakini nikumbushe tu kwamba tarehe 13 hadi 15 Januari, 2015 Kamati ya LAAC ilitembelea Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kupokea taarifa kuhusu uuzaji na wakati huo Jiji la Dar es Salaam lilikuwa na msimamo wa kutokuahirisha uuzaji wa hisa zile. Maoni haya yalitolewa na Kamati ya PAC iliyopita ilikuwa chini ya akina Zitto Kabwe, lakini Kamati ya LAAC ikaagiza kwamba Jiji liondoe shauri lililofunguliwa Mahakama Kuu kitengo cha biashara ili Simon Group Limited aweze kulipa hisa hizo.
La pili, Simon Group Limited iruhusiwe kulipia hisa hizo haraka na ya tatu Jiji litoe account ya Benki kwa Simon Group Limited ili Simon Group Limited alipie hisa hizo kupitia account hiyo. Hapa yanasemwa mambo kama vile mjadala huu unaanza leo na wakati Jiji lenyewe limekwisharidhia. Tarehe 21 na 22 Januari, 2015, Kamati ya Fedha ya Uongozi ya Jiji la Dar es Salaam iliridhia kutekelezwa kwa maagizo haya ya LAAC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najiuliza hapa, Serikali hii ni mpya, Waziri mimi ni mpya, mambo haya yalikwishapita, kinachosemwa hapa maana yake ni kwamba maamuzi yaliyofanywa na Baraza lililopita la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam yanataka kuvunjwa na Baraza hili lililokuja leo. Sina hakika kisheria inakaaje lakini naanza kuona tatizo na mgogoro kama Bunge hili linaweza likaanza kufuta maamuzi ya Bunge lililopita, kama Serikali inaweza ikafuta maamuzi ya Serikali iliyopita, naanza kuona tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nasema lakini tumekwenda vizuri na Kamati yako, tumekwenda hatua kwa hatua na mpaka sasa tuna maagizo ya Kamati ya LAAC juu ya jambo hilo na kuna taarifa wanazozihitaji zaidi ili tuweze kufahamu tunalimalizaje jambo hili. Kwa hiyo, Kamati hii tunafanya nayo kazi vizuri, Waheshimiwa Wabunge wasubiri tutakapomaliza na Kamati hii italeta mambo haya hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa suala la Madaraka ya Rais kuteua. Ukisoma Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 35(1), (2), (3) na (4) Rais anaweza ku-establish madaraka yoyote na anaweza kuteua mtu yoyote kushika nafasi yoyote kwa namna atakavyoona inafaa, hawezi kuhojiwa. Sisi wengine wote kama Mawaziri tunafanya kwa niaba yake kwa sababu ndio Mkuu wa Utumishi wa Umma. Kwa hiyo, haya mambo tunapoyazungumza tujue kwamba yana Misingi ya Kikatiba na Ikulu haiwezi ikakosea kwa sababu iko equipped. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikubaliane na Waheshimiwa Wabunge vizuri sana kwa asilimia mia moja kwamba wateule hawa ni vizuri wakafundishwa, wakapewa semina kama mlivyoshauri, ingawa tumefanya hivyo kwa kiasi kwa kanda, tumetoa semina kwa Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya, Ma-DAS, lakini tutaongeza jitihada ya kutoa semina zaidi ili wajue mamlaka yao na mipaka yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba Serikali inataka kuzivunja Mamlaka ya Serikali za Mitaa, hapana! Serikali nia yake ni kuziimarisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa sababu zipo Kikatiba. Sura ya Nane, Ibara ya 145 na 146 zinatamka uwepo wa Mamlaka hizi, kama zilivyo Serikali nyingine. Kwa hiyo Mamlaka hizi zinapaswa kuendelea kuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, sisi katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika Ibara ya 147, tumesema waziwazi kabisa kwamba tutajitahidi sana kuziboresha na kuzipa uwezo Mamlaka hizi. Tumesema hapa kuendelea kuzifanyia mapitio Sheria zote zinazohusiana na Serikali za Mitaa na Mamlaka za Tawala za Mikoa ili kuharakisha mchakato wa Kugatua madaraka na lengo la kuziwezesha kutoa huduma bora zaidi kutoka ngazi za Vitongoji, Vijiji hadi kwenye Kata.
Pia tumesema (b) kuendelea kuzijengea uwezo Serikali za Vijiji kwa kuzipatia rasilimali watu na fedha ili ziweze kupanga na kusimamia kwa ukamilifu miradi yao. Lakini pia tumesema kuendelea kuongeza kiwango cha ruzuku katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, pia tunasema kuimarisha ubora wa upatikanaji wa huduma za jamii katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Pia tumesema kuendelea kuchukua hatua kali za kinidhamu, za kisheria kwa watendaji wabovu na wanaofanya ubadhirifu katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Hii tumeisema katika Ilani yetu ya Uchaguzi na hatuwezi kwenda kinyume na Ilani hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, niseme tu, kwamba ingekuwa sasa unataka kuchukua hatua hizi tunazozichukua sasa kwa falsafa ya kutumbuana kwa maana ya kuchukua hatua za haraka kunapotokea ubadhirifu au matumzi mabaya ya madaraka, ukalinganisha kinachofanyika leo na kinachosemwa na Wabunge, ukafanya flashback, ukaangalia Bunge lililopita na kilichokuwa kinasemwa juu ya Serikali kutokuchukua hatua, unaiona contradiction. Kwa hiyo, utawala wa nchi yetu hii unaweza ukawa mgumu sana kuutengenezea ideology kwa sababu kila mtu anataka kutengeneza ideology yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tufike hatua tuamue, na watu wote waliopiga kura kwenye uchaguzi uliopita walipigia kura mabadiliko, nataka niwahakikishie Watanzania wanayataka mabadiliko kwa sababu walipigia kura mabadiliko, whether wao walipigia CHADEMA, whether walipigia CUF, whether walipigia CCM lakini wote wengine walifanya hivi, wengine walifanya hivi, lakini walikuwa wana lugha ya mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ina maana gani? Ina maana kwamba Watanzania wamechoka kuishi vile ilivyokuwa, wanataka kitu kipya na ndicho hiki ambacho Rais Magufuli anakileta, si kama tulivyozoea. Hapa hatuna uwezo wa kukubaliana na kila jambo, tunaweza tukakubaliana kwamba yanahitajika mabadiliko wote tunakubaliana. Yafanyikeje haliwezi likawa jambo la kukubaliana, kwa sababu yanaweza yakawa kwa namna moja hayo yanayotaka kufanyika yanakugusa, kwa hiyo, hatuwezi kukubaliana, tuache walioshinda na anayeiongoza nchi atupeleke kwa mwendo unaotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yamesemwa mengi lakini kama nilivyosema kwamba sisi tutaendelea kushirikiana na Kamati hizi lakini lilizungumzwa suala lingine la suala la Oysterbay Villa. Oysterbay Villa ulikuwa ni mradi wa kujenga nyumba kwa ajili ya kupangisha, mradi huu kusema ukweli ulikuwa ni mbovu, haufai na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameshawasilisha Mahakama ya Rufani maombi namba 299 ya mwaka 2016 kupinga uamuzi wa Jaji wa Mahakama ya Kitengo cha Biashara na Sheria uliofanyika ili ufanyiwe mapitio. Kwa hiyo, maana yake sisi Serikali haturidhiki na kinachofanyika pale katika lile, kwa sababu ya muda siwezi kwenda into details.
Mheshimiwa Naibu Spika, East Africa Meat Company zilitengwa fedha kiasi kikubwa tu, Dar es Salaam ilitoa Dola milioni moja, Ilala ikatoa Dola laki nne na themanini, Temeke Dola laki mbili na thelathini na mbili, Kinondoni Dola laki moja na themanini kampuni ya NICO ikatoa Dola laki moja na kumi na moja. Pia kulikuwepo na mwekezaji mwingine anaitwa Rheinhold and Mahla wa Malaysia ambaye alitakiwa kutoa mitambo yenye thamani kubwa tu kama sehemu yake ya umiliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ile bodi ya East African Meat Company ilipoanzishwa, ilipopata ile fedha ikaanza kuzitumia fedha zile kwenda kutafuta mitaji badala ya kutumia fedha zile kufanya uwekezaji. Serikali hii haifumbii macho ufisadi. Haturidhiki na hili tunaendelea kuchukua hatua na tumeshaanza kuchukua hatua, lakini tumewaomba wanahisa hawa wakutane waone wanaweza kufanya nini? Wakishindwa kukubaliana na wanahisa, basi waseme na ikibidi wa wind up ili wagawane kilichopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Jiji wasikae peke yao lazima wajue kwamba kuna Mamlaka hizi zinatakiwa na zenyewe kushiriki kuona kama wanakwenda mbele au wanakwenda wapi, wakishindwa Serikali itachukua hatua juu ya hao waliofanya hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile imezungumzwa asilimia 10 ya mikopo ya akinamama na vijana na hapo hapo ikazungumzwa asilimia 20 kwa ajili ya fedha kupelekwa kwenye mitaa na vijiji kama fidia ya vyanzo vilivyofutwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, own source inayozungumzwa hapa na kwa maana ya asilimia 10 iko huko huko Halmashauri ambako ninyi Wabunge mpo na ni Madiwani. Wakurugenzi ambao wanashindwa kupeleka fedha hizo mko nao huko na mnashiriki vikao. Mamlaka ya kuwawajibisha mnayo, kuwafukuza hata kuwasimamisha kazi Wakuu wa Idara mnayo, lakini hawapeleki pesa mnawangalia.
wa Kinondoni nafikiri, alichangia, rafiki yangu pale, amesema wao wamepeleka mpaka bilioni mbili, lakini pia kuna Mbunge wa Nyamagana amesema na wao wanapeleka kwa sababu wamemsimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge hayo mnatakiwa mkawasimamie nyie kuhakikisha kwamba fedha hizi zinakwenda kwa wapiga kura wetu. Ingawa kuna mgongano mkubwa sasa katika fedha hii ya gawio hili, hasa unapozungumza kuna maagizo ya Kamati hapa ambayo hayakupitishwa kama parliamentary resolution, yakaagizwa kwa Serikali kwamba 60 percent ya own source ifanyiwe development.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo inasemwa 20 percent ipelekwe kwenye vijiji, 10 percent igawiwe kwa vijana na akinamama mikopo, 20 percent ibakie utawala, 10 percent ipelekwe kwa ajili ya kukatia bima ya wazee. Yaani there is a contradiction. Nadhani kwa sababu Serikali ndiyo inayotengeneza sera na hili jambo ni jambo la kisera, acha tukakae tutashirikishana tuone namna gani mgawanyo huu unaweza. Kwa sababu formula hii ya 60 percent development ilifanywa wakati Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla akiwa Mwenyekiti wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, si Halmashauri zote zenye uwezo wa kuwa na fedha ya kutoa 60 percent na zikabaki zinaweza kufanya shughuli zake. Itabidi tuzifanyie cluster ili tuone zipi zinaweza zikatoa hiyo pesa kwa development na zikaweza kujiendesha na zipi ziko maskini ambazo zina hela kidogo, hizo hazitaweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili la fedha limezungumzwa na Waziri wa Fedha. Tatizo la Wakuu wa Idara kukaimu, tumefanya upembuzi, Wakuu wa Idara 802 wanakaimu, kati ya hao 583 hawana sifa. Hata hivyo, nani anayepandisha mtu kuwa Mkuu wa Idara? Ni Mkurugenzi, ambaye mnaye pale, moja ya majukumu ya Mkurugenzi ni kuwaambia, wewe kama unaona wanafaa mbona huwapandishi tuwathibitishe? Kazi yenyewe ni nyepesi tu, kuwaleta kwetu na tuwapeleke for vetting, wakirudi wanathibitishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakurugenzi hawafanyi hivyo muwahoji huko kwenye vikao na muwachukulie hatua endapo hawataki kuwathibitisha wenzao. Tusaidiane ingawa tunatafakari kwa sababu upungufu ni mkubwa tufanye mass promotion. Tufanye vetting kwa pamoja, tuwatafute watu wenye uwezo wenye sifa, halafu tufanye mass promotion tunadhani pengine inaweza ikasaidia kwa sababu hawa kila siku wanatoka na kuingia.
Mheshimiwa Naibu Spika, maagizo ya RC na DED yanayoharibu Mipango ya Halmashuri na kuvuruga bajeti, lakini mengine yanaingilia Mamlaka ya Halmashauri zenyewe. Nataka niungane na Waheshimiwa Wabunge, kwamba hii haikubaliki na kwa sababu jambo lenyewe limekaa kitaaluma unajua masuala ya utawala hayana principle yaani yana namna fulani hivi, masuala ya utawala huwezi kuyatengenezea kanuni kama hesabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani bado kupitia semina hizi tunahitaji kutoa elimu kwa wenzetu ambao wako huko, kuanzia Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Ma-DED, lakini pia na Ma-DAS. Nimeambiwa na najua kuna Wakuu wa Wilaya wengine hana raha mpaka aitishe Kamati ya Ulinzi na Usalama kila asubuhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiitishwa kila siku asubuhi watu watafanya kazi saa ngapi? Polisi, OCD anakuwepo pale, mwisho nchi itakuja kuvamiwa pale hawana hata habari wako kwenye Kamati ya Ulinzi na Usalama. Kwa hiyo hili halikubaliki na nachukua nafasi hii kusema waziwazi kawmba waache, Kamati za Ulinzi na Usalama ni vikao muhimu na vinatakiwa kufanyika kwa jambo mahususi au maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yako maamuzi mengine yanafanya interference. Kinachoruhusiwa na hawa Viongozi wa Serikali Kuu ni kufanya intervention pale ambapo mambo hayaendi sawa, kwa mfano sheria inavunjwa, kuna mipango na mikakati ya kupiga hela, hapo ndipo wanapoweza kufanya intervention, lakini haiwezi kuwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa imetoa maamuzi kwa kufuata sheria, utaratibu wote, halafu wewe unasema hii sikubaliani, hapana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo inaitwa interference, kwa hiyo haikubaliki, tutaendelea kuelezana, lakini wanajitahidi wanafanya kazi vizuri, tunahitaji kueleweshana, tunahitaji kuelimishana na hao walioteuliwa ndugu zangu ni Watanzania wenzetu. Tusiwe na sense ya kuwabagua, wana elimu, wana sifa, wamesoma hata sisi tulipokuwa Wabunge hapa hatukuja na uzoefu huu. Kwa hiyo, tukubaliane kwamba ni wenzetu, ni ndugu zetu, wanatakiwa kupata fursa na wao kujifunza. Ukisoma, Mheshimiwa Zitto alikuwa ameni-consult hapa nikamwambia viko vifungu ambavyo vinawapa Mamlaka lakini kwa sababu ya muda acha niliache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie vikao vya Mabaraza ya Madiwani na Kamati za Uongozi vinapoitishwa wakati Bunge linaendelea. Tumetoa maelekezo kwamba wasiitishe vikao hivyo wakati Bunge linaendelea. Tumetoa na kuelekeza ma-RAS, nadhani ujumbe labda haujakwenda, pengine tupeleke nguvu zaidi ya kuwaeleza wao wenyewe kwamba, lazima wahakikishe wanaitisha vikao hivyo wakati Bunge halipo kwenye session ili Wabunge wapate fursa ya kuhudhuria.
T A A R I F A...
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naikubali lakini itabidi tu-harmonize haya mawazo na yale mawazo mengine, tupate utaratibu fulani mzuri unaoweza ku-accommodate situations zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie. Kinachokosekana kwenye mamlaka zetu zilizoundwa na Serikali ya Awamu ya Tano ni ari na kasi ya watu kutaka kutekeleza majukumu yao. Niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge, ninyi ni Viongozi wale walio kule ma-DC, Wakurugenzi ni Viongozi wenzetu. Tukiwa na tabia ya ku-interact, unafika pale usisikilize Madiwani tu wamekwambia kitu, basi unabeba, huyu hafai, amefanya hivi, sikiliza na upande wa pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tufahamu kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama; na hivyo vyombo vya Ulinzi na Usalama viko chini yao wana taarifa ambazo wakati mwingine sisi hatuna. Kunaweza kukawa kuna mpango wa kufanya hujuma fulani na yeye anayo taarifa halisi, ya kweli, wewe huna.
Mheshimiwa Naibu Spika, Madiwani wanafika pale wanakukamata wanakwambia huyu hivi hivi na hivi na wewe unaamini. Unakwenda kuanza kusema, hapana, huyu anaingilia anafanya nini; tuwe na tabia ya ku-interact na hawa viongozi wenzetu itatusaidia. Itatusaidia sana kuyajua yaliyo ndani, kujua taarifa za siri, nani anafanya nini na wakati mwingine ningetamani kama ninavyoyajua mimi na nyie mngeyajua kwenye maeneo yenu yangesaidia kuondoa hii migongano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa inayoongozwa chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza na Makamu Mwenyekiti wake Dkt. Pudenciana Kikwembe pamoja na wajumbe wote kwa ujumla akiwepo Mzee wangu Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa na Mheshimiwa Mwanne Mchemba. Tunawashukuru sana kwa namna mnavyotupa ushirikiano na mara zote mmekuwa ni walezi wetu na kusema kweli Kamati hii tunafanya nayo kazi vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla kwa michango mizuri kupitia kazi hii ya Kamati iliyofanyika kwa muda wa miezi 12. Kazi hii ni kubwa na mambo mengi wameyasema. Nitangulize tu kusema kwamba yote tumeyapokea na tumeyachukua na tutayafanyia kazi yote kwa ufanisi na kwa ufasaha mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaliyosemwa ni mengi lakini siyo rahisi kwa muda niliopewa kuweza kuyajibu yote na kwa kuwa wajibu wangu na mimi ni kuchangia, basi nitumie nafasi hiyo kusema baadhi ya yale tu ambayo naona yamesemwa sana na watu wengi na mengine haya tutaendelea na mfumo ule wa Kanuni za Kudumu za Bunge kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili tuweze kuyamaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa na la kwanza ambalo limesemwa sana na wote ni namna ambavyo Wakuu wetu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanavyohusiana katika kufanya kazi ya umma na kuleta maslahi tunayoyatarajia wote. Imesemwa hapa kunakuwa na misuguano katika baadhi ya maeneo ya Wilaya na Mikoa kati ya viongozi hawa wa kiserikali na viongozi wawakilishi wa wananchi kwa maana ya viongozi wa kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa tofauti zao ukiondoa udhaifu wa baadhi ya wengine ambao ni hulka zao na hapa ndiyo maana inasemwa hata habari ya semina elekezi. Siku za nyuma mambo ya semina hizi yalilaumiwa sana na kupingwa kweli kweli kwamba semina elekezi, semina elekezi. Tukasema tutoke kwenye semina elekezi as long as mtu ana CV nzuri amesoma, akipewa vitabu vya kufanyia kazi lakini wakati anapoteuliwa akaelekezwa naamini atafanya kazi vizuri kama ana hekima na busara kwa sababu naamini suala la uongozi siyo tu kuwa na PhD, Masters au First Degree pia hekima ni kitu cha msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu hizi zinatusaidia tu kujua vitu lakini hekima inatusaidia kujua useme na ufanye nini kwa wakati gani. Kwa hiyo, nitoe rai na niwasihi sana baadhi ya wenzetu hawa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wajitahidi pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu lakini pia wawe na hekima na busara kwa sababu sasa wao ni viongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika hili wakati mwingine na wao kama binadamu wanakuwa tempted, anatokea kiongozi anasema mimi ni mwakilishi wa wananchi bwana, huwezi kuniambia kitu na unamwambia kiongozi mwenzio vile na yeye atakwambia anavyoweza kusema. Ndiyo maana yanatoka majibu kama yale na mimi ni mteule wa Rais, ni kwa sababu kulikuwa kuna reaction fulani iliyopelekea na yeye akawa excited akafikia hatua hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoe rai kwa sote, sisi kama viongozi wa kisiasa na viongozi wengine wote, tunapokwenda mbele ya jamii basi tusichukue nafasi hiyo ya kutambiana kwamba mimi ni nani, mimi ni nani, bali wote tujitahidi kuwa waadilifu na kujua kwamba nafasi zetu ni kubwa kwa jamii. Wakati mwingine ni mambo ya mahusiano tu, unamkuta Mbunge au Diwani, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya iko pale au ya Mkuu wa Mkoa iko pale hajawahi kwenda hata siku moja ku-pay courtesy call, wanakutana kwenye matukio. Hili si jambo jema kwa sababu pia viongozi hawa sheria imewapa madaraka na mamlaka makubwa tu na kwa sababu ya muda sina haja ya kuisema. Niwasihi na niwaombe viongozi wenzangu kwamba wale ni viongozi wenzetu tushirikiane nao, tufanye kazi nao pamoja kwa faida yetu sote lakini kwa maslahi mapana ya wananchi wetu na kwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la pili lililoguswa sana ni kwamba flow ya fedha kwenda kwenye shughuli za Mamlaka ya Serikali za Mitaa si nzuri sana. Takwimu za Kamati zinaonesha kwa utafiti walioufanya na ambao na sisi tunao ni kwamba 85% zimekwenda kwa ajili ya maendeleo, kwa hiyo utaona ni 15% ndiyo haijaenda na bado tuna miezi kadhaa hapa, nadhani tunaweza tukafikia hatua nzuri ya 100% kwenye fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye OC zimekwenda 46% kwa fedha iliyotoka Serikali Kuu lakini sehemu ya OC pia ni pamoja na own source. Makusanyo ya ndani ya Halmashauri na yenyewe ni sehemu ya OC. Kwa hiyo, niwasihi sana Waheshimiwa Wabunge tuyasimamie sana makusanyo ya ndani ili yaweze kutusaidia kutekeleza majukumu mengine ambayo yangeweza kutekelezwa na OC ile ambayo imepungua iliyotakiwa kuletwa na Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tufahamu kwamba mahusiano ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu huwezi kuyaachanisha kwa sababu kwa nature yake Serikali Kuu ndiyo imezaa Serikali za Mitaa na Serikali Kuu kazi yake ni kuzilea Mamlaka za Serikali Mitaa. Tunahitaji mishahara, tunahitaji fedha za maendeleo ambazo Serikali Kuu inatafuta na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni lazima zitimize wajibu wake kuhakikisha kwamba zinatunza fedha za makusanyo na kuhakikisha kwamba zinaenda kwenye maendeleo pia kwa maana ya sehemu ile ya usimamizi wa miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko Mamlaka za Serikali za Mitaa nyingine ambazo hata pamoja na kukusanya own source kubwa tu inayofikia kwa mwezi hata zaidi ya milioni 100 ambayo ni kiwango kidogo, ziko zinazokusanya mpaka bilioni moja kwa mwezi, zinashindwa kuwalipa hata posho za vikao halali Madiwani. Huku ni kugombanisha Serikali Kuu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa maana ya Madiwani. Kwa sababu haiwezekani wewe umekusanya fedha, kikao kile kwa mwezi kinatakiwa kifanyike kwa chini ya shilingi milioni 20, wewe unazipeleka kwenye matumizi mengine mnapeana likizo, mnapeana safari watumishi, Wakuu wa Idara wanapeana safari zinatumika zinakwisha halafu wanasema Serikali haileti OC ndiyo maana hatuwalipi posho za vikao. Kuanzia sasa Halmashauri ambayo itawakopa Madiwani huyo Mkurugenzi hana sifa ya kuendelea kuwa Mkurugenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine lililosemwa sana ni suala la mihuri ya Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji. Nilikwishalisema, Wenyeviti hawa wa Mitaa na Vijiji mbali ya masuala ya ulinzi na usalama lakini mihuri yao ile ndiyo inayowatambulisha kwa wananchi wao wanaowaongoza. Mihuri yao ile ndiyo inayowafanya watu wamalizane katika mahusiano ya mikataba midogo midogo katika maeneo yao. Ni lazima mamlaka za juu ziheshimu madaraka na majukumu waliyopewa hawa viongozi wa chini, Wenyeviti wa Mitaa na Wenyeviti wa Vijiji na hata Wenyeviti wa Mashina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kitendea kazi hicho ni muhimu kwao na vizuri wakaachiwa na ndiyo maana nilisema warejeshewe na hii niliisema siyo kwa Dar-es-Salaam ni kwa nchi nzima. Viongozi hawa nchi nzima warejeshewe kitendea kazi hiki ili wafanye kazi yao vizuri. Ndiyo wanaotambulisha mgeni anapoingia au kutoka kwenda sehemu nyingine lakini ndiyo wanaoandika vibali hata vya mifugo, mfugo ukauzwe hapa na ndiyo wanaosababisha kule chini kunakuwa na amani na utulivu, lazima tuwape nafasi yao hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ma-WEO na ma-VEO ambao hawajaajiriwa na Serikali Kuu haitatokea hata siku moja kwa idadi ya vijiji tulivyonavyo tukatimiza idadi yao kutokana na watumishi wa umma tulionao na changamoto tulizonazo za upungufu katika idara mbalimbali. Niendelee kusisitiza kwamba Mamlaka ya Serikali za Mitaa ni mamlaka kamili zinazoweza kuamua kutafuta watu wa kuwaajiri hata kwa mikataba na wakawalipa fedha hiyo kutoka kwenye own source. Hawa ndiyo watakaosababisha ufanisi na makusanyo hata kwenye Halmashauri zenyewe. Kwa hiyo, hili halijazuiwa lakini kadiri tutakapopata vibali vya ajira tutaendelea kuwaajiri kupitia Serikali Kuu. Mheshimiwa Kairuki akitoa vibali sisi tutaendelea kuajiri lakini kwa upungufu tulionao Halmashauri ziendelee kuwaajiri hawa watendaji watakaotusaidia wenye sifa zinazostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni miradi ya Halmashauri ambayo haijakamilika. Iko miradi ambayo haikuwa ya Serikali Kuu lakini ilipangwa na Halmashauri zenyewe na ikawa vipaumbele vyao na wakasema wataitekeleza miradi hiyo kwa kutumia own source zao. Nitoe rai na niagize Mamlaka ya Serikali za Mitaa pale ambapo wana mikataba na wakandarasi au na suppliers, wanawatesa wenzao wanahangaika, wao walishaanza kutekeleza upande wao wa mikataba, wametekeleza miradi hiyo, lakini hawawalipi kwa kisingizio cha kwamba Serikali Kuu haijatoa fedha. Mlikubaliana kwamba mtawalipa kutoka kwenye own source, muwalipe suppliers and contractors kwa sababu ni kuwaonea na wengi wamefilisika na wengi hata wamekufa kwa sababu ya madeni hayo, hii haikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nichukue nafasi hii kuzungumzia juu ya property rates…
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshamaliza maandalizi yote ya kukusanya kodi ya majengo katika Halmashauri 30 ambazo tulikubaliana hapa na tukapitisha sheria na kwa sasa wako tayari kuanzia mwisho wa mwezi huu kukusanya fedha hizo. Hata zikikusanywa na Waziri wa Fedha kwa sababu ndiye anayeshika Sera na Sheria ya Fedha, mwisho wa siku zitarudi huku kuja kutusaidia katika miradi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba kuunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 – Wizara ya Fedha na Mipango
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Fedha na Naibu Waziri wa Fedha kwa mipango na bajeti nzuri ya kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo kusema ukweli ni bajeti ambayo ni realistic.
Mimi nimesimama ili nizungumze pamoja na mambo mengi ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge, yanayohusu Wizara ya TAMISEMI ambayo ndiyo Wizara ya wananchi, lakini ndiyo Wizara inayokwenda kubadili maisha kwa maana ya huduma za Jamii ambazo wananchi wanazitarajia kutoka kwenye Serikali yao, pia waheshimiwa Wabunge mliahidi sana kule kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo megi ambayo mmesema juu yamaji, juu ya miundombinu, lakini mimi nimesimama hapa kwa sababu ya muda nizungumzie eneo moja ambalo limeonekana kuchangiwa na Wabunge wengi sana takribani Wabunge 27 wamezungumzia suala la huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitoe takwimu ya hali tuliyonayo kwa sasa kwenye zahanati na vituo vya afya. Tunavyo vijiji 12,545 na sera yetu inasema kila kijiji lazima kiwe na zahanati, zahanati tulizonazo ni 4,700 tu.
Kwa hiyo, tuna upungufu wa zahanati takribani 7,845 kwa sababu tulizonazo ni asilimia 38 tu, utauona upungufu huu ni mkubwa. Lakini sera yetu pia inasema tutakuwa na kituo cha afya kila kata, tunazo kata 3,963 na tuna vituo vya afya 497 tu ni asilimia 13 ya mahitaji. Kwa hiyo upungufu wetu ni vituo vya afya 3,466.
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka ya Serikali za Mitaa zimejitahidi sana, kuna ujenzi mbalimbali ya majengo ambayo sasa tunayaita maboma, tunayo jumla ya maboma ya zahanati 1,443; tunayo jumla ya maboma ya vituo vya afya 244 na tunayo jumla ya maboma ya hospitali za Wilaya 51, kazi hii imefanywa vizuri sana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini. Mpango wetu sasa wa kushirikiana kwa Serikali nzima tumejaribu kuongea na Waziri wa Fedha na Waziri wa Afya ambaye yeye anasimamia utoaji wa huduma na Wizara ya TAMISEMI ndiyo inayojenga, inamiliki na kuendesha utoaji huu wa huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejaribu kuzungumza, jambo la kwanza tulilokubaliana ni kwamba tupitie upya ramani ile ili iwe ramani ambayo inamudu kwa uchumi wetu lakini itatoa huduma zinazostahili zote. Kwa sababu ramani iliyopo Waheshimiwa Wabunge kama mnavyofahamu ni kubwa kiasi kwamba inakatisha tamaa kwa vituo vya afya kuwa na ramani kubwa kiasi kile. tulipoipunguza ramani ile tunahitaji kiasi kama cha bilioni 2.5 kwa kila kituo cha afya kilichokamilika na huduma zake zote kutolewa ikiwa ni pamoja na upasuaji, fedha hizi bilioni 2.5 Waziri wa Fedha ananiambia tunaweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa bajeti hii ya sasa niombe mambo mawili, la kwanza tuendelee na mpango wetu ule ule wa Halmashauri kuwa na mpango wa kuwa na zahanati kila kijiji waendelee na mpango wa wananchi na Halmashauri kuendelea, isipokuwa sisi Serikali kuu tuone namna ambavyo tutakuja na mpango wetu sasa wa ujenzi wa vituo vya afya, hapa tunaweza tukafanya vizuri kwa sababu kwa upungufu tulionayo, tukiwa tunajenga kila Halmashauri kituo cha afya kimoja kila mwaka wa fedha nina hakika kwa miaka mitatu iliyobakia tutakuwa tumejenga vituo vitatu vitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutakuwa na vituo vya afya vingi tu kuliko hata tulivyojenga toka tulivyopata uhuru. Kwa hiyo, mimi nasema kwa bajeti hii ambayo tunakwenda nayo yakwanza hii ambayo imetenga takribani bilioni 32 kwa ajili ya umaliziaji wa maboma haya niliyoyataja, itatufikisha mahali fulani. Lakini bado niwaombe na niombe sana kwamba tuhakikishe tunasimamia own source hii ambayo tulipanga kukusanya ili maboma haya ya vituo vya afya yakamilike kwa sababu ndiyo tuliyopitisha kwenye bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yakikamilika haya maboma tutakuwa tumekamilisha zahanati 1.443, vituo vya afya 244 itakuwa ni hatua moja mbele ili tukija kwenye bajeti inayokuja ya mwaka 2017/2018 tutakuja na mpango huu sasa ambao tutakuja na bajeti mahususi kwa ajili ya vituo vya afya kama nilivyosema ambayo kama tutakwenda hivyo kila mwaka, kila Halmashauri ikajenga kimoja ambacho kinakamilika nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tunaweza tukajenga vituo vya afya vingi kwa miaka mitano, na hata tukimaliza miaka yetu mitano tukaweza kusema tumefanya kitu gani kila mmoja kwenye jimbo lake.
Waheshimiwa Wabunge, niwasihi na niwaombe sana, muunge mkono bajeti hii ya Serikali ili iweze kutekelezwa kama ambayo tumepitisha kwa shilingi bilioni 32 katika sekta ya afya lakini tusimamie tu michango yetu kwa makusanya ya Halmashauri yaweze kukusanywa kwa sababu utoaji wa huduma siyo ujenzi tu wa haya majengo, pia kuna suala la watumishi kwa idadi inayotakiwa ya watumishi. Lakini pia ni jambo ambalo linahitaji katika ukamilifu wake ili iweze kutoa huduma ile tunayostahili, kwa hiyo lazima haya yote yaende yakiwa yanaandaliwa kwa pamoja, tusikurupuke tukawa na majengo lakini vitu vingine vikawa haviendi sawa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnafahamu tuna upungufu wa wataalamu wa afya, lazima tuwe na huo uwezo na wenyewe pia ujengwe sambamba na ujenzi wa haya maboma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilidhani haya ndio machache ambayo yamesemwa,na mimi nimeona nizungumzie kwenye jambo hili la afya, nirudie tena kutoa wito Waheshimiwa Wabunge tukashirikiane kule; tuhimize makusanyo ya Halmashauri ili mipango tuliyoipanga hii maana imepangwa na sisi iweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kusimama mbele kwa kazi ya kujumuisha mjadala wa bajeti ya mwaka 2017/2018 juu ya bajeti ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla wa pande zote mbili kwa michango yenu mizuri na muhimu ambayo ililenga kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wa pande zote mbili wametoa michango yao; walioweza kuchangia kwa maandishi ni 47 na waliochangia kwa kuongea ni 34. Michango yao yote tumeizingatia na tumeijibu hoja kwa hoja katika jedwali hili la majibu ya hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa michango ni mingi na waliozungumza ni wengi, pengine haitakuwa rahisi kuweza kutumia muda huu wa kuzungumza kumjibu kila mmoja alichokisema, lakini muamini tu kwamba kila mmoja alichokisema tumekizingatia na tutakizingatia wakati wa kutekeleza bajeti itakayopitishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwenu ni kwamba mtusaidie tuweze kupata fedha hizi tulizoziomba ili tuweze kutekeleza majukumu kama tulivyoainisha katika malengo ya Wizara, Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuanza kujibu hoja za Wabunge, nataka niseme maneno. Michango mingi imetolewa na Wabunge, pamoja na uzuri wa michango hiyo, iko baadhi ya michango ilileta hali ya kutokuelewana. Kutokuelewana huko kumetokana na lugha na pengine matamshi yanayotamkwa ambayo kimsingi, hata kama katika utaratibu unaambiwa tunakuja huku Bungeni kupewa ushauri kama Serikali, lakini unaona huo utayari wa kupewa ushauri haupo kwa sababu anayetoa ushauri tayari ana hukumu na kutumia lugha ambayo haiko sawa sawa kimaadili, lakini pia hata katika kanuni zetu za uendeshaji wa shughuli za Bunge. Ndiyo maana katika mjadala kulitokea kusimama kwingi na vurugu nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu, ukitaka kujua historia ya nchi yoyote lazima uangalie vipindi vyake vya utawala. Nchi hii toka tulivyopata uhuru Rais wetu wa kwanza alikuwa Mheshimiwa Julius Kambarage Nyerere ambaye naye katika wakati wake, hasa alipoamua kujenga Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea alipata shida kubwa. Walitokea wapinzani, walitokea waasi na mtakumbuka akina Oscar Kambona, akina Kasanga Tumbo; na mnakumbuka katika historia nini kilitokea kwa baadhi ya watu waliokuwa wapinzani wa misingi ya Ujamaa na Kujitegemea ambao leo hii hapa tunajivunia kwamba imeliweka Taifa hili salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha pili amekuja Mzee Mwinyi. Rais Mwinyi katika kipindi chake akafungua milango ya uchumi akaleta uchumi huria; na kwa maneno yake alisema unapofungua milango na madirisha basi nzi wataingia, matakataka yataingia, wadudu wataingia, hewa chafu itaingia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufungua milango ya uchumi akaonekana yeye ni mtu asiye na weledi wa uchumi, ni mtu ambaye amefungua kila kitu, mambo yanaenda holela, wakapatikana wa kulaumu na wakalaumu sana. Hata hivyo, kipindi hicho kikapita na leo hii tunakumbuka Awamu hizo zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuja Mkapa akaleta discipline ndani ya Serikali, akaboresha utumishi ndani ya Serikali, akaboresha heshima ya Serikali. Kwa kufanya hayo naye akaambiwa huyu ni Mkapa ameleta ugumu wa maisha na akalaumiwa sana. Kipindi hicho kikapita na chenyewe tunakikumbuka na tunakipongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuja Kikwete ambaye amemaliza Awamu ya Nne, Rais mpole, mjuzi wa Diplomasia ameijenga nchi yetu kujulikana sana Kimataifa, amejenga uchumi na miundombinu, amefanya mambo makubwa akaambiwa ni Rais dhaifu, tena ni mpole aliyepitiliza hafai kuwa Rais; hapa hapa humu ndani na bahati nzuri waliosema wamo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anapongezwa sana kwamba ni Rais mzuri hajapata kutokea, amefanya mambo makubwa, anakumbukwa kwa mema na makubwa aliyoyafanya na anakumbukwa na watu wa pande zote mbili na ushahidi ni namna alivyoshangiliwa juzi alipokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa stadi hii na mifano hii, leo hii kuweka mipango na mikakati ya baadhi ya wenzetu humu ndani ya kumdhalilisha na kumtukana Mheshimiwa Rais si jambo la kwanza; kumbe inawezekana akimaliza atapongezwa na kusifiwa. Kwa hiyo, ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Rais wangu, haya yanayosemwa ni utaratibu wa kawaida wa miongo yote ya utawala wa nchi yetu, yeye aendelee, tunasonga mbele na sasa nchi inakwenda mbele katika uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi majuzi IMF na World Bank wiki iliyopita imezindua taarifa ya hali ya uchumi ya Tanzania na imepongeza uchumi wa Tanzania kwamba ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na uko stable. Uchumi wa Tanzania kwa sasa uko very stable, unakua kwa asilimia saba nukta moja. Kwa Afrika inazidiwa na Côte d’Ivoire ambayo uchumi wake unakua kwa asilimia
saba nukta tisa. Kwa ukanda huu wa East Afrika hakuna nchi inayotukuta, sisi katika Afrika ni wa pili, katika sifa kama hii bado watu wanasema hawaoni kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo hii Rais huyu anazindua ujenzi wa reli ya treni ya standard gauge inayotaka kutupeleka sasa kwenye miundombinu ya usafirishaji pamoja na barabara zinazojengwa zilizounganisha mikoa yote na za lami sasa watu wanasafiri. Zamani ukisema unatoka hapa kwenda Moshi ni hadithi, leo hii kaka yangu Selasini akiwasha gari saa hizi, saa tatu yuko Moshi anakula nyumbani kwake chakula; haya ni maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Rais huyu ambaye sasa anajenga nchi na uchumi mkubwa unajengeka na unatupeleka kwenye viwanda, viwanda vingi vinafunguliwa bado wanasema hawaoni anachokifanya. Rais huyu anayesisitiza uwajibikaji, anaondoa rushwa, amesababisha Watanzania wanapata huduma nzuri wanapokelewa vizuri maana huko nyuma ilielezwa kwamba watumishi wa umma ni miungu watu, leo hii watumishi wa umma wamegeuka wanawahudumia Watanzania, wamegeuka wanawapokea vizuri. Ukienda hospitali unapokelewa na nesi vizuri unahudumiwa vizuri, wanasema Watanzania wamekuwa waoga, Watanzania ambao wamekuwa waadilifu na wanaona mambo yanavyokwenda vizuri, wanaambiwa wamekuwa waoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie watumishi wa umma wa nchi hii kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inafanya kazi nzuri na muiunge mkono; na sisi tunatambua changamoto mlizonazo watumishi wa nchi hii; kwa kuhakikisha kwamba mnafanya wajibu wenu bila kushinikizwa. Naamini kabisa matunda haya yanayopatikana yataivusha nchi yetu kutoka mahali ilipo na kufika mahali pazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zimezungumzwa hoja nyingi lakini nianze na moja ambayo inakera hivi. Huwezi ukasema kitu bila kuwa na takwimu na bahati mbaya sana takwimu tunazileta sana humu. Kibaya zaidi ni kwamba kumbe mtu akiamua kukupinga hawezi kukubali hata takwimu utakazomletea hawezi kukubali chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa elimu ya Tanzania inashuka, lakini kinachoweza kutusaidia kujua kwamba elimu inashuka au inapanda ni matokeo ya wanafunzi wanaofanya mtihani. Kama kipo kigezo kingine labda ni baadaye lakini cha kwanza ni matokeo. Sasa nifanye ulinganisho, katika sekta ya elimu matokeo ya darasa la nne mwaka 2014, ufaulu ulikuwa ni kwa asilimia 64, leo 2016 matokeo ni kwa asilimia 93, watoto wamefaulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, darasa la saba mwaka 2012 watoto walifeli sana, ilikuwa ni asilimia 33 ya ufaulu, leo hii ni asilimia 70. Matokeo ya kidato cha pili, mwaka 2012 ilikuwa asilimia 57, leo hii ni asilimia 91. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 ilikuwa ni asilimia 45, leo hii ni asilimia 70 ya ufaulu. Matokeo ya kidato cha sita yanatisha ni karibu wanafunzi wote wamefaulu. Mwaka 2012 ilikuwa asilimia 88 tu ndio waliofaulu, leo hii ni asilimia 99 ndio waliofaulu. Ahsanteni Walimu wa Tanzania, tunawashukuru sana Walimu wa Tanzania. Ninyi ni wazalendo wa nchi hii, Walimu wa Tanzania ni wapenda maendeleo ya elimu ya nchi hii, tekelezeni wajibu wenu na Serikali inatambua mchango wenu; na wala ninyi sio waoga. Msijazwe upepo wa kuambiwa ni waoga, sidhani kama kwa mwoga huenda kilio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini, Serikali tunatambua na ndiyo maana tumechukua hatua. Hadi sasa tumelipa madeni ya Walimu wote nchini bilioni thelathini na tatu, madeni yasiyo na mshahara. Kwa mwaka 2015/2016 – 2016/2017, tumelipa bilioni thelathini na tatu na tumelipa kwa takribani mikoa yote na madeni ambayo yamebaki yanadaiwa ni yale tu ambayo ni ya mshahara, lakini yale yasiyo ya mshahara yote tumeyalipa na tunahakikisha kwamba na madeni ya mshahara na yenyewe tutayalipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bila malipo imebezwa humu ndani sana na katika ubezwaji huo ni ubezwaji wa kupotosha. Serikali inatumia billioni ishirini na mbili nukta tano kila mwezi. Wakati fulani ili kumwandikisha mtoto darasa la kwanza ilikuwa ni lazima mzazi atoe kati ya Sh. 30,000/= mpaka Sh, 100,000/=, Serikali imesema marufuku, itagharamia gharama hizo za uandikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa ruzuku ya uendeshaji wa shule, wazazi hawachangishwi, Serikali inatoa chakula kwa shule za bweni, lakini Serikali inagharamia mitihani, ilikuwa wazazi wanalipia mitihani sasa hivi ni bure. Ilikuwa hakuna vitabu sasa hivi tunapeleka vitabu na tumegawa vitabu zaidi ya millioni sita, ukijumulisha vyote vya kuanzia elimu ya msingi na sekondari, vitabu vingi tumegawa na sasa uwiano wa mwanafunzi wa vitabu ni kitabu kimoja wanafunzi watatu. Kwa hiyo, tunakaribia kufika kwenye lengo la milenia lakini watu wanasema hakuna kinachofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwasihi Watanzania kwamba elimu yetu inaboreshwa na inatazamwa kwa ukaribu sana na Serikali na tutahakikisha kwamba pale ambapo Serikali ina wajibu wa kufanya mambo tutaendelea kuyafanya zaidi. Kwa sasa tunatumia billioni karibu ishirini na tano kwa kila mwezi kwa ajili ya kuondoa zile gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haimaanishi kwamba kwa kusema tu elimu bure na kuchukua gharama hizi zilizokuwa zinawaumiza wazazi na kusababisha udahili wa wanafunzi kupungua; leo hii kwa mwaka tumeandikisha wanafunzi wa chekechea na darasa la kwanza zaidi ya milioni moja na laki nne wakati lengo lilikuwa laki tisa. Haya ni mafanikio makubwa ambayo wazazi sasa wanawatoa watoto wao kwa sababu hakuna gharama za lazima wanazotakiwa kuzilipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio haya makubwa yanatokana na fedha hizi ambazo Serikali inagharamia, lakini mtu anasema uwepo wa elimu bure basi Mwalimu Serikali ilipie kila kitu, ihakikishe mtoto huyu amechukuliwa kutoka nyumbani kupelekwa shuleni, mtoto huyu amepewa kila kitu jamani, hii tafsiri ni ya upotoshaji ni tafsiri isiyowatakia mema Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasihi wazazi wa nchi hii kwamba watoto ni wa kwetu lazima tushiriki kusaidiana na Serikali kuhakikisha kwamba wanapata elimu kwa sababu mwisho wa siku haipati faida Serikali peke yake bali hata sisi wazazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa Sekta ya Afya. Sekta hii ina changamoto kadhaa na zimesemwa na Waheshimiwa Wabunge. Moja ni changamoto ya upatikanaji wa dawa. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017, hadi mwezi Machi tumepeleka kiasi cha Shilingi bilioni 79.7 za dawa. Tulipofanya ukaguzi tumekuta baadhi ya Hospitali za Wilaya zina fedha za dawa zipo kwenye akaunti hawataki hata kuzitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawataki kuzitumia ili zibakie baki mle baadaye wajue cha kufanya, huu ni wizi tu. Hizo fedha zimetolewa kwa ajili ya dawa, ni lazima zinunue dawa na watu wapate dawa, lakini wananchi wakienda kule wanaambiwa dawa hakuna. Niseme, Waheshimiwa Wabunge sisi ndio Madiwani, tuko kule, tufike hatua hata tukague akaunti za Halmashauri, si kosa kwa sababu Mbunge unashiriki kwenye Kamati ya Fedha na kule kwenye Kamati ya Fedha ndiko mnakohoji mpaka akaunti kwamba zina fedha au hazina pesa.

Waheshimiwa Wabunge, msije kulalamika huku, sisi tunakwenda kukagua kwenye akaunti ambazo ninyi mko kule, tunakuta kuna fedha zimebaki, unamuuliza Mganga Mkuu hizi fedha zimebaki za nini, anajiuma uma tu. Kwa hiyo, tunawasihi Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani kusimamia kuhakikisha kwamba dawa zinapatikana, Serikali inapeleka fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu wa fedha Serikali imepanga kutumia Shilingi billioni 96.433 kwa ajili ya dawa; tunahakika ni dawa nyingi, lakini bado hapo hujazungumzia CHF, hujazungumzia Mfuko wa Afya ya Jamii ambao na wenyewe unaingiza fedha nyingi sana. Mnapowauliza hizi zilizopelekwa na Serikali waulizeni hata yale makusanyo yao, ambapo katika yale makusanyo yao asilimia 33 ni kwa ajili ya motivation, inatakiwa ilipe hata on call allowances. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko Wilaya zinafanya hivyo na nyingine hazifanyi. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani tusimamie sana kuhakikisha kwamba rasilimali hizi zinatumika katika kuwahudumia wananchi wetu lakini tukibaki tunabishana na kuona ni sifa kusema hakuna dawa, Serikali hii imeshindwa, imefanya nini, tunapoteza maisha ya watu wetu bure kwa uzembe wa watu wachache ambao si waaminifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa upelekaji wa dawa sasa tunauboresha, tunataka sasa pesa hizi sasa zipelekwe mpaka kule kwenye vituo vya kutolea huduma kwenye zahanati, kwenye vituo vya afya, kwenye hospitali za wilaya na kwenye hospitali za mikoa. Hela zipelekwe kule, na tumeweka utaratibu ambao sasa kutakuwa kuna maafisa mahususi kwenye kila kituo cha afya na zahanati zinazozunguka kituo cha afya watakaosimamia ununuaji na upangaji wa dawa kuhakikisha kwamba zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa utaratibu tumeuboresha zaidi kwamba MSD watakapopelekewa ile quotation ya dawa na Halmashauri husika watakapokuwa out of stock hawana hizo dawa, lazima watoe hilo jibu mara moja ili sasa hao waende wakanunue kwenye maduka mengine kwa sababu na yenyewe hiyo haikatazwi tena sasa.

Kwa hiyo, nina hakika kwamba kama tutasimamia vizuri na Waheshimiwa Wabunge na Madiwani tutasimama vizuri nina hakika kwamba tatizo hili halitakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa watumishi. Ni kweli kwamba tuna upungufu wa wataalam wa kada mbalimbali, mahitaji ni tisini na sita elfu na ushehe hivi lakini waliopo ni arobaini na sita elfu na upungufu ni kama hamsini elfu. Changamoto hii ni kubwa, tuna shida ya ikama hiyo kwenye upande wa Walimu na kwenye upande wa Sekta ya Afya. Utaratibu wa Serikali ni kwamba tutaendelea kuboresha ikama hizi kadiri tutakavyokuwa tunapata uwezo wa uchumi kuweza kubeba ajira zinazotakiwa kuzitoa katika Sekta ya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunavyozungumza wage bill ya nchi yetu sasa is almost seventy percent ya GDP. Unapokuwa na wage bill kubwa kiasi hicho halafu bado una upungufu wa watumishi muhimu kama wa afya na elimu lazima kuna tatizo mahali. Ama tumeajiri katika kada nyingine watu wasiohitajika kuwepo, ama tumefanya over employment katika maeneo ambayo si muhimu kwa Taifa kwa sasa. Kwa hiyo, iko haja ya kuangalia ndio maana Serikali sasa tunaangalia masuala ya miundo, nafikiri atakuja kuzungumza Waziri wa Utumishi ili tuweze kuona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba kwa watumishi wa afya tumepata kibali cha hawa Watumishi madaktari 258 ambao nina hakika hawa tutawapanga kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma hospitali za wilaya na za halmashauri pamoja na vituo vya afya mara moja. Kuanzia siku ya Jumatatu hawa tutaanza kuwa-deploy na kuwapeleka huko na tunasubiri vibali zaidi vikitolewa ili tuweze kuwapeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa Walimu tumepata kibali cha ajira zaidi ya elfu nne na tumeweza kupeleka Walimu takribani elfu tatu na mia kadhaa hivi ambao tumewachukua wote wa masomo ya sayansi waliomaliza mwaka 2015. Hata hao tuliowachukua tumebaki na nafasi ya kibali ambapo hawajatosha. Tunaamini wengine waliokosa kwa sababu ya kukosekana kwa barua zao tumewaambia wazilete Wizara ya Elimu na zingine kama wakiweza hata TAMISEMI tutazipeleka kwa Waziri wa Elimu wazihakiki ili waweze kupata nafasi; wale waliokosa, ambao walimaliza mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilizungumzwa hapa habari ya ujenzi wa miradi ya afya na elimu, unazungumzia zahanati, madarasa, matundu ya vyoo na kadhalika na kadhalika. Mwaka uliopita tulipata hela ile ya maendeleo isiyo na masharti, inajulikana kama Local Government Development Grant. Tulipata fedha ingawa haikuletwa kwa kiwango kizuri tumepokea kiasi cha bilioni hamsini na nane. Waheshimiwa Wabunge, mkumbuke kwamba fedha hii kwa miaka mitatu mfululizo ilikuwa haijawahi kutolewa na ndiyo ilipelekea maboma mengi kubakia kwenye maeneo yetu bila kumaliziwa kwa sababu fedha hii ndiyo ambayo huwa inatumika kumalizia maboma haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kuwajulisha kwamba katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, kiwango hiki cha fedha kimeongezeka hadi kufikia billioni 256. Hizi shilingi billioni 256 zikisaidiana na utaratibu wetu wa kawaida wa nchi yetu ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambapo ni lazima wananchi washiriki katika shughuli za maendeleo yao, wakatoa nguvu zao, wakasogeza mchanga, wakasogeza mawe, wakanyanyua mabomba au hayo yaliyopo hizi fedha zina uwezo wa kutusaidia kumalizia kwa kiasi kikubwa na kwa hivyo tutaongeza zahanati, vituo vya afya, tutapunguza upungufu wa madarasa na nyumba za Walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa wananchi wa Tanzania kushirikiana na Mamlaka za Serikali zao za Mitaa kuhakikisha kwamba wanachangia nguvu zao ili kwa uchumi wetu ulivyo na kiwango hiki cha fedha kidogo kiweze kuwa na tija kwa kumaliza kero hii ya wananchi katika maeneo ya huduma za afya na elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilizungumzwa issue ya mapato ya ndani. Kama maombi mengi yalivyokuwa yanatolewa na niishukuru sana Kamati kwa kupitia Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Jasson Rweikiza, walishauri sana kwamba sasa ile fedha inayopelekwa kwa ajili ya maendeleo kuwa sera ile ya asilimia sitini na kwa arobaini, yaani sitini iende kwenye maendeleo na arobaini ibakie kwa uendeshaji ilikuwa inapelekea Halmashauri nyingine zisizokuwa na uwezo kushindwa kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imesikia na tumeibadilisha ile sera sasa tutazipanga hizi Halmashauri kutokana uwezo wake. Zile ambazo hazina uwezo zitapeleka asilimia arobaini tu kwenye maendeleo na asilimia sitini itatumika katika uendeshaji wa Halmashauri. Hapa itatusaidia sana kuhakikisha kwamba Madiwani sasa hawakopwi posho zao, lakini pia uendeshaji hata wa shughuli nyingine za kiutawala utawezekana ikiwa ni pamoja na usimamiaji wa miradi ukiondoa OC per se ambayo italetwa na Serikali Kuu, lakini pia hii own source ni sehemu ya OC. Kwa hiyo, hii nayo ikitumika vizuri, ikisimamiwa vizuri itatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwenye Halmashauri zetu huwa tunaambiwa tu OC haijaja, lakini OC ni pamoja na own source, ikijumlishwa ndipo unaipata own source unapoipata OC total. Hii OC ndiyo inayoweza ikatumika hata kupunguza baadhi ya changamoto ndogo ndogo. Unamkuta Mkurugenzi anadaiwa na Mwalimu Shilingi 45,000 ya matibabu. Hivi kama una own source kwa nini usimlipe Mwalimu huyo akaondoka akaenda kufanya kazi yake? Tumeona mfano mzuri uliofanywa na Mkurugenzi wa Arusha, ndugu Kiamia. Nafikiri Wakurugenzi wote waige mfano huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haki za watumishi. Waheshimwa Wabunge wamezungumzia haki za watumishi. Tunalo tatizo kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambako Waheshimiwa Wabunge mpo, Madiwani mpo. Wapo Maafisa Utumishi ambao wanawatesa wenzao, hawataki kuwahudumia wenzao, wanataka wahudumiwe wao.

Waheshimiwa Wabunge, ninyi ndio mamlaka za utawala. Mwalimu au mtumishi anasema mke wangu yuko mahali fulani nataka kuhamia kwa mke wangu anakwambia sitaki hata kama ni ndani ya Wilaya moja, hata kama ni ndani ya mkoa mmoja. Hii haiwezekani lazima Sheria za Utumishi zizingatiwe. Walimu hawa wanayo haki ya kutoka sehemu moja kwenda nyingine lakini pia na kuishi na wenza wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi anapoomba ahamishwe kwa sababu anamfuata mwenza wake utadhani it is a privilege, ni hiari, no, ni haki yake ya msingi. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge, tusimamie haki hizi za watumishi, na ninyi ndio mamlaka za utawala na nidhamu kwenye maeneo ya Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unyanyasaji wa wananchi katika dhana ya uchumi wa viwanda, ujasiriamali na biashara ndogo ndogo. Hii habari ya kuwasumbua wamachinga, Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo. Wafanyabiashara ndogo ndogo hawa wakirasimishwa; alisema Mheshimiwa Mabula Mbunge wa Mwanza; wanaweza kuchangia makusanyo makubwa sana ya Halmashauri. Wanaweza kuchangia uchumi wa Taifa. Hata hivyo, wako wengine wanaona kama wafanyabiashara ndogo ndogo ni mkosi, nuksi, balaa, washughulikiwe na waondoke, hapana!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosema sisi ni kwamba mamlaka hizi ndizo ziwapangie maeneo mahsusi ya kufanyia shughuli zao. Maeneo mengine kwenye miji mingine ukienda wanapangwa vizuri hata wakati wa masaa fulani wanafanya ile biashara yao, ikifika kwa mfano saa moja watu wanaondoka, wanapanga biashara zao vizuri, wako kwenye maeneo mazuri na asubuhi baada ya saa nne, au saa tano wanaondolewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeambiwa na yule Mbunge rafiki yangu Raza kwamba kule Dar es Salaam wanawafukuza. Mheshimiwa Raza nitalishughulikia, hii si sawa. Hatuwezi kuwa na nchi ambayo ina watu wote wanataka kuwa na uchumi rasmi. Duniani kote, watu wasio na uchumi rasmi ndio wengi kuliko wenye uchumi rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili tumelifahamu lakini Halmashauri zote nchini zitenge maeneo mahsusi kwa ajili ya uwekezaji wa watu hawa wadogo wadogo. Ukiwa na Wilaya yako, hata kama ni wilaya si mji, ukawapangia wale washonaji, wanaosindika mafuta, ukaandaa eneo mahsusi, ukapeleka umeme, ukapeleka maji, ukapeleka barabara ni dhahiri eneo hilo litakuwa eneo la kiutalii, hata mtu akienda kwenye wilaya hiyo ataenda kutembelea eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, tuko huko, rasilimali zile ni zetu. Tuwaelekeze Wakurugenzi kuhakikisha kwamba wanatenga maeneo haya na kuyapatia miundombinu ili wafanyabiashara wetu wadogo wadogo hawa tukawaweke kule kwenye maeneo mahsusi si kama wanavyokaa kwenye barabara, kwa sababu pia na wao lazima wafahamu kwamba wako wananchi wengine wenye haki pia za kutumia maeneo ambako wao wanataka kufanyia biashara ambapo pia si sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya mipaka. Migogoro iko ya aina nyingi, iko migogoro ya mipaka ya mikoa, vijiji, wilaya, iko migogoro mingi sana. Kwa ujumla tuna migogoro zaidi ya 288 inayohusiana na mipaka ya vijiji na Hifadhi za Serikali; za misitu au za Taifa za utalii. Migogoro hii ni 288, lakini tunayo migogoro mingine takriban 56 ya mipaka na tunayo migogoro mingine takriban 18 na migogoro inayohusiana na ujenzi wa Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, niwasihi, sisi ndio tuko kule. Sisi katika Serikali tumeamua kujipanga na Wizara ya Ardhi, tumetengeneza task force ambayo inaipitia migogoro hii yote na tumeihakiki migogoro hii yote, tunataka ifike hatua tuje tufanye maamuzi ya
pamoja. Kwa hiyo, niwasihi sana kwa sasa tushiriki katika kuhakikisha kwamba tunatuliza migogoro hasa ya wakulima na wafugaji. Waheshimiwa Wabunge na sisi wanasiasa kwa ujumla tusiwe chachu ya kuhakikisha kwamba migogoro hiyo inakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limezungumzwa hapa suala la Utawala Bora, kwamba iko migongano ya mamlaka kati ya ma-DC, ma-RC, ma-DED, na Madiwani kuna migongano. Waheshimiwa Wabunge, kwanza hawa wote wanaotajwa wapo kwa mujibu wa Sheria na uwepo wake hauwi choice ya mtu mwingine, they are all supposed to be there, kwa hivyo hakuna namna ni lazima waelewane. Sasa kuelewana msingi wake mkubwa ni sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya na mengine, najua tutapata fursa wakati wa mafungu. Naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na naomba kutoa hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake kwa bajeti nzuri ambayo kwa kiasi kikubwa imejikita kutatua matatizo ya afya kwa Watanzania. Pia niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri tumeisikia na kwa kuwa tuna shida ya muda pengine si rahisi sana kujibu kila hoja na hivyo nitajikita kwenye maeneo manne ambayo yamezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza lilikuwa ni mpango gani upo kwa ajili ya kumalizia maboma ya vituo vya afya na zahanati katika maeneo yetu. Napenda tu nichukue nafasi hii kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge, kwa kuwa ni wawakilishi lakini pia wanaishi katika maeneo hayo, kwamba vyanzo vikuu vya mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu na hasa katika sekta zote ikiwemo sekta ya afya kwenye mamlaka zetu za Serikali za Mitaa ni hivi vifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa ni nguvu kazi, nguvu ya wananchi. Lazima tutambue kwamba wananchi hawa nguvu yao ni rasilimali ya Taifa, kwa hiyo lazima itumike katika kutatua matatizo yanayogusa maisha yao. Tukumbuke tu kwamba nchi yetu ni nchi inayofuata misingi ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea na ndivyo Katiba yetu inavyosema. Bado tunaamini kwamba kwa nchi masikini kama yetu tunapaswa kutumia nguvu za wananchi wetu katika kutatua kero za wananchi na kujiletea maendeleo. Vile vile tabia hiyo inajenga umoja lakini pia inajenga ownership kwa wananchi juu ya miradi inayowahusu ya huduma za jamii kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini chanzo kingine cha pili ni vyanzo vya ndani vya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ambavyo, nilipowasilisha bajeti ya TAMISEMI, nilisema, asilimia 40 ya fedha za ndani zitakwenda kwenye maendeleo na maendeleo yenyewe ni pamoja na kuchangia ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti eneo la tatu ni Mfuko wa Maendeleo (Local Government Development Grant) ambayo kwa miaka mitatu nyuma ilikuwa haitoki lakini bajeti ya mwaka 2016/2017 tulitenga kiasi cha billioni 158 na hadi mwezi Desemba tumepeleka kiasi cha billioni 56 kwenye Halmashauri mbalimbali na wamezitumia katika kuhakikisha kwamba wanamalizia maboma yaliyojengwa ya kutolea huduma za afya pamoja na elimu. Zimetolewa fedha hizi na kwa hivyo ni mipango na vipaumbele tu vya halmashauri ndivyo vinavyotakiwa ili kuweza kutekeleza miradi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2017/ 2018 tumetenga kiasi cha shilingi billioni 251.184. Fedha hizi zikigawanywa vizuri kwenye Halmashauri zetu na zikatumika kwa mujibu wa mwongozo tulioutoa wa asilimia karibu themanini kwenda kwenye miradi ya Maendeleo nina hakika zitaweza kupunguza matatizo ya umaliziaji wa maboma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa ni mamlaka ya Serikali za Mitaa kuweka Mipango yake kwa kutambua vyanzo hivi; ndiyo itatupeleka kumaliza matatizo haya ya upungufu wa miundombinu ya utoaji wa huduma za afya. Wananchi watakaojitoa na kujituma Serikali itapeleka fedha za kutosha kupitia mfuko huu ili waweze kumalizia kuezeka na kufanya finishing ili huduma ziweze kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoelezwa juu ya kuwepo kwa zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata. Tunazo kata karibu 4,200 kwa nchi nzima na tathmini tulizozifanya kwa ramani iliyotolewa na Wizara ya Afya ni takribani shilingi billioni 2.4 zinahitajika katika kukamilisha kituo kimoja cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, pamoja na mipango mingine ambayo Serikali inayo lakini ni jukumu la Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwanza kuweka kwenye mipango yao lakini pia kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo ingawa tunayo mipango mingine ambayo tunaendelea nayo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba tunakwenda kidogo kidogo kwa vituo vichache vichache na hatimaye tuweze kumaliza kwa nchi nzima angalau kwa kila Halmashauri kuwa na kituo kimoja kipya ukiondoa vile vya zamani. Kwa kufanya hivi tutakuwa na vituo vingi sana kuliko vituo tulivyovijenga toka tulivyopata uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu hapa kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba, tujitahidi basi kuwahamasisha wananchi, kutenga yale maeneo kama tulivyosema na wale waliokwishatenga yale maeneo si kwamba tumewaacha, hapana, tunafahamu na tuko kwenye michakato mbalimbali wa kuhakikisha kwamba tunatafuta funds ili tuweze kuanza ujenzi wa vituo hivyo. Lakini mipango iwepo kwanza kwa wananchi wenyewe wa mamlaka husika na hicho kidogo kilichoko ikiwa ni ku-clear na kuanza hata kidogo kwa kutumia ramani iliyopo waanze halafu Serikali inakwenda ina-respond na ku-support pale ambapo wameanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine lililozungumzwa ni asilimia tano ya wanawake, zile ndizo tunazosemaga asilimia 10 kwa wanawake na vijana, lakini hapa nizungumzie tano ambayo ndiyo inayohusika na Sekta ya Wizara ya Afya. Kwa mwaka 2016/2017 hadi kufikia mwezi Desemba tumepeleka kiasi cha shilingi billioni 15.6 kwenye Halmashauri ikiwa ni kiasi cha asilimia hizo zilizotengwa kutokana na mapato ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti nilisema kwamba mapato ya ndani ni pamoja na OC inayotoka Hazina ukijumlisha na Own Source na makusanyo ya ndani ya Halmashauri, ukijumlisha ndipo unapata the total, ile total yake ndiyo unachukua asilimia 10 unapata ile inayotakiwa kupelekwa kwa wanawake na vijana. Kwa hivyo, naamini kabisa hadi sasa wanufaika 18,000 kwa nchi nzima 233 wakiwemo wanawake wamenufaika na fedha hizi billioni zaidi ya 15 zilizopelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, si jambo ambalo halifanyiki linafanyika, lakini nitoe rai kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba wanapeleka kiwango hiki cha fedha kadri wanavyokusanya ili wasiwe na audit query kwa sababu jambo hili sasa Waheshimiwa Wabunge tunalisimamia kwa karibu. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kusaidia kuzishauri Halmashauri lakini pia huko kwenye Halmashauri mliko ndiko zinakotolewa hizo fedha na ndiko zinakopatikana. Kwa hiyo, washauri wazuri na tuwaelekeze ili waweze kutekeleza agizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti dhana ya ugatuaji wa madaraka katika sekta ya afya. Wakati mwingine kunazungumzwa kwamba kuna mkanganyiko. Niseme tu kwamba hakuna mkanganyiko wowote katika utoaji wa huduma ya afya kwa maana ya ugatuaji madaraka. Wizara ya Afya kazi yake ni kusimamia Sera ya Afya ya Taifa na katika kusimamia Sera ya Afya ya Taifa jukumu lake kubwa ni kuseti miongozo na standards ya utoaji wa huduma ya afya nchini; ambapo kwa kufanya hivyo tunazingatia viwango vya kimataifa, mahitaji ya kimataifa lakini pia na mahitaji ya ndani; wao ndio wanaosimamia sisi TAMISEMI ni watekelezaji wa maelekezo hayo. Kwa hiyo, wala hakuna mkanganyiko na Serikali ni moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugatuaji huu duniani kote maeneo ambako utoaji wa huduma za afya na maendeleo ya watu yamekuwa realized imetokana na dhana ya upelekaji madaraka kwa umma. Unapopeleka madaraka kwa umma unawapa the ownership na kwa kusema hivi hata mara moja haiwi mkanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifahamike kwamba unaposema TAMISEMI imepewa jukumu unamaanisha nini? Waheshimiwa Wabunge unaposema TAMISEMI imepelekewa jukumu hili, unamaanisha uwepo wa Mkuu wa Mkoa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Mkoa akisimamia rasilimali zote zinazokwenda kwenye Mkoa wake. Unazungumzia na wataalam wote tuliowapeleka kwenye Mkoa, unazungumzia uwepo wa Mkuu wa Wilaya na watalaam alionao, lakini pia unazungumzia uwepo wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Mkurugenzi na wataalam waliopo na Madiwani wanaosimamia kwa niaba ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ownership hii ndiyo iliyofanywa kwa nchi zilizoendelea kama Uchina, ndiyo inayofanywa na Japan. Sisi hatuwezi kuanzisha mfumo wa peke yetu, tukaanzisha jambo ambalo hatuwezi kuwa na ownership ya wananchi, maendeleo lazima yawe yanaguswa kwa ownership ya wananchi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu TAMISEMI tuna uwezo wa kufanya kazi hii na tunapata support nzuri sana kutoka Wizara za Kisekta ikiwemo Wizara ya Afya katika Sekta ya Afya na tunakwenda vizuri na tunashirikiana vizuri sana, tuendelee na utaratibu huu utatusaidia kuivusha nchi yetu kwenye matatizo tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Naibu Spika, hongera sana kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu miradi ya vijiji kumi kila Wilaya imekwama karibu yote. Kijiji cha Kidenge mtiririko umekwama, kila siku maelezo ni yale yale tu na Kijiji cha Makose na Njiapanda nao umekwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba visima katika Vijiji vya Munguwi, Chipogoro, Ilamba na Lutalawe. Naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa na kwa niaba ya Kamati napenda niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamepata fursa ya kuchangia hoja ya Kamati ya Bajeti kutoka pande mbili zote za Bunge, nawashukuruni sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Aidha, pia napenda niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao pia kwa namna fulani wamechangia lakini kwa kujaribu kufafanua baadhi ya maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge walihoji au wali- criticize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe waliozungumzia na kugusa ripoti ya Kamati ya Bajeti ni 17 na kwa sababu ya muda naomba nisiwataje majina yao. Hata hivyo si rahisi sana kwa muda nilionao kuweza kujibu hoja moja baada ya nyingine na kwa sababu hiyo nitajaribu kuchukua yale ya jumla jumla tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa suala la ukuaji wa uchumi, lakini pia pongezi zimetolewa na wengine wame-criticize na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango amejaribu kufafanua kwamba hakuna ubishi kwamba uchumi wetu unakua kwa kasi nzuri na kwa Afrika sisi ni miongoni mwa nchi tano yaani tupo kati ya kumi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo tunaweza tukajidharau lakini tunapojidharau katika mambo ya msingi yanayotupa heshima ni kama vile hatuitaki heshima. Kwa hiyo ni vizuri mimi niwasihi Waheshimiwa Wabunge kwenye mambo ambayo kama Taifa tunafanya vizuri ni vizuri tukasema tunafanya vizuri, lakini tukaboresha kwa maneno mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa jambo la misaada na mikopo na msemaji aliyesema na wengine wamesema, lakini nimtaje Mheshimiwa Msigwa ambaye amesema bajeti yetu inategemea asilimia 40 kutoka kwenye misaada na mikopo, sijui hizi takwimu zinatoka wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikusihi Bunge lako liangalie matumizi ya takwimu ndani ya Bunge, kwa sababu sisi ni viongozi lakini Bunge hili limejaa wasomi watupu. Matumizi ya takwimu yaangaliwe, tusitajetaje tu na kuzungumza zaungumza tu. Ni vizuri tukazisema za kweli na
zilizopo kwa sababu takwimu ni tafiti na kama hujafanya utafiti huna haki ya kuzungumza. Sasa kama unatumia takwimu zisizo halali maana yake hukuwa na haki wala usahihi wa kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bajeti ya mwaka 2018/ 2019 mchango wa misaada na mikopo tulioutegemea kwa bajeti ya mwaka 2017/2018 fedha zenyewe tulizozihitaji ni trilioni 2.13 ambayo kwa bajeti yetu ya trilioni 32.475 kiwango hiki cha misaada na mikopo tulichokihitaji ni asilimia 6.55 tu. Kwa bajeti ya mwaka 2019/2020 ambayo tunaindaa sasa na tupo katika mchakato, kiwango tunachokihitaji kutoka kwenye misaada na mikopo its only 3.38 trilioni ambapo bajeti yake inatarajiwa kuwa trilioni 33.5; kiwango hiki ni sawasawa na asilimia 10.005. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake kama Taifa tumebadilika, hiyo asilimia 40 ilikuwa ni zamani sana, tunakwenda kwenye kujitegemea na kwa hiyo kuzungumzia suala la misaada na mikopo kama ndio mwarubaini wa kuondoka kwenye umaskini wa nchi yetu sio sahihi ni kujidhalilisha kwa sababu tumejenga uwezo wa kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa suala la kama vile nchi kama nchi tunadharau, hatuheshimu, hatuthamini private sector katika kujenga uchumi. Hakuna nchi duniani ambayo leo hii inaweza kujenga uchumi wake bila private sector na Tanzania tunaheshimu sana private sector na ndio maana Serikali imetengeneza blue print, tumeripoti kwenye taarifa yetu. Serikali imeleta hapa sheria ambayo tumeifanyia kazi na kwenye ripoti ya Kamati imeelezea kwenye ukurasa wa 9 na 10. Kwenye ripoti ya Kamati tumeelezea kwamba tumetengeneza Sheria ya PPP, PPP maana yake ni nini, ni Public Private Partnership.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumeelezea kwamba pia Serikali imeongeza diplomasia ya uchumi, mabalozi wote wameagizwa kwa ajili ya kuhamsisha wawekezaji mbalimbali kuingia nchini. Hata hivyo mafanikio yamejionesha na kwenye ripoti yetu tumesema kwenye ukurasa wa 10 kwamba hata kwa kipindi hiki kifupi cha mwaka huu tu viwanda vitano vya dawa vinajengwa, kwenye ripoti yetu tumeonesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inaposemekana kama Serikali au nchi yetu hatuthamini wawekezaji mimi nashangaa na hii taarifa mmeitoa wapi kwa sababu kwenye ripoti yangu niliyoleta nimesema na namna tulivyofanya na Serikali ambavyo inafanya. Mimi nadhani mambo mengine tuyaseme lakini tuwe na kiasi katika kuyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji mmoja mmoja wamesema na wamechangia mambo mengi ya msingi ambayo Serikali imeyachukua na sisi kamati tumeyasema kwenye taarifa yetu. yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wame-criticize ni vizuri Serikali nayo ikayachukua; lakini unapo-criticize kwa jambo ambalo si sahihi, kwa mfano nimpongeze Mheshimiwa Silinde mara ya pili aliposimama kutoa taarifa amefafanua vizuri sasa kwamba fedha ya maji aliyokuwa anaisema si ya Mfuko wa Maji peke yake, ya Mfuko wa Maji yote ilipelekwa kama ilivyo isipokuwa Serikali haijapeleka fedha ya maendeleo kutoka Hazina. Kwa hiyo Mheshimiwa Silinde umefanya vizuri lakini mwanzo ulizungumza kwa ujumla kwamba hakujapelekwa fedha ya maendeleo ya maji. Kwa hiyo, kwa taarifa yetu umetutendea haki maana tulianza kushangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ambayo yamechangiwa sana na mimi niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge ni juu ya Serikali kuwa makini na ahadi ilizoziahidi na utekelezaji wake. Yapo yale maeneo ambayo Serikali tunakubaliana kabisa kwenye kamati, rai yangu kwa Serikali ni kwamba muhakikishe kwamba mnayatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, eneo la maboma ambayo tulikubaliana kwenye afya mmepeleka fedha vizuri lakini kwenye eneo la elimu hamjapeleka fedha vizuri kama tulivyokubaliana. Kwa hiyo, kwenye hili na Waheshimiwa Wajumbe wengi niwapongeze mmelisemea na Serikali wamesikia.

MHE. HALIMA J. MDEE: (Hapa alizungumza bila kutumia kipaza sauti).

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Tatizo lenu mnajua ku-criticize ndio kusema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Msigwa amelinganisha ukuaji wa uchumi na hali ya utoaji wa huduma. Huduma hizi haziwezi kuimarika kama misingi muhimu kama ambavyo Mheshimiwa Dkt. Mpango amezungumza, lakini kama pia alivyozungumza mjumbe wangu wa Kamati, Balozi. Amesema kwamba ni lazima tuimarishe kujenga ukubwa wa uchumi. Tunaweza tukawa na uchumi unaokuwa lakini uchumi huo ukawa mdogo, we have to strengthen the economy, so how do we strengthen the economy ni kuhakikisha kwamba miundombinu muhimu inayojenga uchumi inashughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kunahitaji maamuzi ya makusudi kujenga reli, ukijenga reli uchumi wako lazima utaimarika. Tukiwa na umeme wa kutosha kama tunavyojenga Stiegler’s Gorge ni maamuzi ambayo unayafanya leo lakini yatautunza uchumi kwa muda mrefu. Kama tunavyojenga miundombinu ya barabara, kama tunavyojenga miundombinu na kuhakikisha kwamba watoto wetu wanasoma vizuri; una-invest kwa watu, huko ndiko kuimarisha uchumi utakaokuwa na uimara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali iangalie pia namna ya kuimarisha katika eneo la ICT. Duniani sasa na nchi matajiri duniani wame-invest zaidi kwenye ICT na makampuni matajiri sana duniani ni wale wanaofanya biashara ya ICT. Kama Taifa ni vizuri na sisi tukaona tu-invest zaidi katika eneo hili kwa sababu hili eneo nalo tukifanya masihara nalo lina connection kubwa na uchumi wa kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tuna Mkongo wa Taifa ambao Serikali imewekeza hela nyingi sana, lakini utasikia internet low, malipo yanachelewa, efficiency inapungua. Sasa kwa nini tuwekeze fedha nyingi halafu tusipate faida ya jambo hilo? (Makofi)

Kwa hiyo rai yangu kwa Serikali ni kwamba ICT area ni muhimu sana iwe kwenye perfection na iwe kwenye precision kwa sababu bila kuwa na uhalisi na usahihi hatuwezi kupata tija na payback ya uwekezaji tulioufanya. Sasa tatizo hapa tatizo ni nini ni watu, software ama ni hardware? Hapa kama taifa tujaribu kutoka na wale ambao wanajua katika eneo hili wasitubabaishe zaidi tusiojua. Mimi naamini kama Serikali ime-invest lazima itulipe na malipo yake ni sasa wakati dunia inaishi kwenye maisha ya ICT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu michango ilikuwa mingi lakini kwa sababu ya muda nipende kurudia tena kuwashukuru wote kabisa ambao mmechangia maoni ya kamati yetu. Sisi kama kamati tunapongeza sana aina ya michango iliyotolewa inaweza ikawa mingine ilikuwa inakwenda kinyume lakini ukinyume huo ndio unaohitajika ili kufanya tufikiri zaidi. Kwa hiyo kimsingi yote yanahitajika katika muktadha wa kuchambua unachokifanya hasa katika utekelezaji wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya kwa niaba ya Kamati ya Bajeti naomba kutoa hoja.

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Fedha na Naibu Waziri wa Fedha kwa mipango na bajeti nzuri ya kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano ambayo kusema ukweli ni bajeti ambayo ni realistic.
Mimi nimesimama ili nizungumze pamoja na mambo mengi ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge, yanayohusu Wizara ya TAMISEMI ambayo ndiyo Wizara ya wananchi, lakini ndiyo Wizara inayokwenda kubadili maisha kwa maana ya huduma za Jamii ambazo wananchi wanazitarajia kutoka kwenye Serikali yao, pia waheshimiwa Wabunge mliahidi sana kule kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo megi ambayo mmesema juu yamaji, juu ya miundombinu, lakini mimi nimesimama hapa kwa sababu ya muda nizungumzie eneo moja ambalo limeonekana kuchangiwa na Wabunge wengi sana takribani Wabunge 27 wamezungumzia suala la huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitoe takwimu ya hali tuliyonayo kwa sasa kwenye zahanati na vituo vya afya. Tunavyo vijiji 12,545 na sera yetu inasema kila kijiji lazima kiwe na zahanati, zahanati tulizonazo ni 4,700 tu.
Kwa hiyo, tuna upungufu wa zahanati takribani 7,845 kwa sababu tulizonazo ni asilimia 38 tu, utauona upungufu huu ni mkubwa. Lakini sera yetu pia inasema tutakuwa na kituo cha afya kila kata, tunazo kata 3,963 na tuna vituo vya afya 497 tu ni asilimia 13 ya mahitaji. Kwa hiyo upungufu wetu ni vituo vya afya 3,466.
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka ya Serikali za Mitaa zimejitahidi sana, kuna ujenzi mbalimbali ya majengo ambayo sasa tunayaita maboma, tunayo jumla ya maboma ya zahanati 1,443; tunayo jumla ya maboma ya vituo vya afya 244 na tunayo jumla ya maboma ya hospitali za Wilaya 51, kazi hii imefanywa vizuri sana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini. Mpango wetu sasa wa kushirikiana kwa Serikali nzima tumejaribu kuongea na Waziri wa Fedha na Waziri wa Afya ambaye yeye anasimamia utoaji wa huduma na Wizara ya TAMISEMI ndiyo inayojenga, inamiliki na kuendesha utoaji huu wa huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumejaribu kuzungumza, jambo la kwanza tulilokubaliana ni kwamba tupitie upya ramani ile ili iwe ramani ambayo inamudu kwa uchumi wetu lakini itatoa huduma zinazostahili zote. Kwa sababu ramani iliyopo Waheshimiwa Wabunge kama mnavyofahamu ni kubwa kiasi kwamba inakatisha tamaa kwa vituo vya afya kuwa na ramani kubwa kiasi kile. tulipoipunguza ramani ile tunahitaji kiasi kama cha bilioni 2.5 kwa kila kituo cha afya kilichokamilika na huduma zake zote kutolewa ikiwa ni pamoja na upasuaji, fedha hizi bilioni 2.5 Waziri wa Fedha ananiambia tunaweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa bajeti hii ya sasa niombe mambo mawili, la kwanza tuendelee na mpango wetu ule ule wa Halmashauri kuwa na mpango wa kuwa na zahanati kila kijiji waendelee na mpango wa wananchi na Halmashauri kuendelea, isipokuwa sisi Serikali kuu tuone namna ambavyo tutakuja na mpango wetu sasa wa ujenzi wa vituo vya afya, hapa tunaweza tukafanya vizuri kwa sababu kwa upungufu tulionayo, tukiwa tunajenga kila Halmashauri kituo cha afya kimoja kila mwaka wa fedha nina hakika kwa miaka mitatu iliyobakia tutakuwa tumejenga vituo vitatu vitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutakuwa na vituo vya afya vingi tu kuliko hata tulivyojenga toka tulivyopata uhuru. Kwa hiyo, mimi nasema kwa bajeti hii ambayo tunakwenda nayo yakwanza hii ambayo imetenga takribani bilioni 32 kwa ajili ya umaliziaji wa maboma haya niliyoyataja, itatufikisha mahali fulani. Lakini bado niwaombe na niombe sana kwamba tuhakikishe tunasimamia own source hii ambayo tulipanga kukusanya ili maboma haya ya vituo vya afya yakamilike kwa sababu ndiyo tuliyopitisha kwenye bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yakikamilika haya maboma tutakuwa tumekamilisha zahanati 1.443, vituo vya afya 244 itakuwa ni hatua moja mbele ili tukija kwenye bajeti inayokuja ya mwaka 2017/2018 tutakuja na mpango huu sasa ambao tutakuja na bajeti mahususi kwa ajili ya vituo vya afya kama nilivyosema ambayo kama tutakwenda hivyo kila mwaka, kila Halmashauri ikajenga kimoja ambacho kinakamilika nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tunaweza tukajenga vituo vya afya vingi kwa miaka mitano, na hata tukimaliza miaka yetu mitano tukaweza kusema tumefanya kitu gani kila mmoja kwenye jimbo lake.
Waheshimiwa Wabunge, niwasihi na niwaombe sana, muunge mkono bajeti hii ya Serikali ili iweze kutekelezwa kama ambayo tumepitisha kwa shilingi bilioni 32 katika sekta ya afya lakini tusimamie tu michango yetu kwa makusanya ya Halmashauri yaweze kukusanywa kwa sababu utoaji wa huduma siyo ujenzi tu wa haya majengo, pia kuna suala la watumishi kwa idadi inayotakiwa ya watumishi. Lakini pia ni jambo ambalo linahitaji katika ukamilifu wake ili iweze kutoa huduma ile tunayostahili, kwa hiyo lazima haya yote yaende yakiwa yanaandaliwa kwa pamoja, tusikurupuke tukawa na majengo lakini vitu vingine vikawa haviendi sawa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnafahamu tuna upungufu wa wataalamu wa afya, lazima tuwe na huo uwezo na wenyewe pia ujengwe sambamba na ujenzi wa haya maboma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilidhani haya ndio machache ambayo yamesemwa,na mimi nimeona nizungumzie kwenye jambo hili la afya, nirudie tena kutoa wito Waheshimiwa Wabunge tukashirikiane kule; tuhimize makusanyo ya Halmashauri ili mipango tuliyoipanga hii maana imepangwa na sisi iweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayofanya na hasa ya kupeleka umeme vijijini, wanafanya kazi nzuri wanazunguka na kufanya kazi ambayo Taifa hili ipo siku litapiga hatua kubwa kwa sababu umeme ndiyo uchumi.

Mheshimiwa Spika, rai yangu kwenye eneo hili ni kwamba umeme huu utakuwa na maana kijamii na kiuchumi endapo utakwenda kwenye huduma za jamii; uende kwenye shule, zahanati, vituo vya afya, visima vya maji na sehemu za uzalishaji vijijini ndipo tutakapoona namna umeme huu unavyokuwa na maana kwa kupelekwa vijijini. Vinginevyo, kama si hivyo basi umeme huu utakuja kutafsiriwa baadaye kwamba ni kitu ambacho tumewekeza sana lakini hakijaleta tija katika uchumi lakini ikifika katika maeneo hayo utatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na hotuba yangu ambayo niliiandaa lakini hapa ninaihairisha kwa sababu nataka nijaribu kuchangia kwenye line ambayo mdogo wangu Mheshimiwa Silinde amechangia na natambua kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na hivyo ana ufahamu mkubwa na anayajua mambo mengi na tunashirikiana katika mambo mengi na sina mashaka hata kidogo juu ya uwezo wake, lakini nilitaka tu nimuongezee ujuzi juu ya masuala ya uchumi wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sera ya Dunia kwa sasa katika masuala ya umeme ni energy mixing, kwa nini? Energy mixing kwa sababu hakuna chanzo sustainable kwa sasa, iwe gesi inaisha; hiyo gesi unayosema inaisha, yawe maji yameathiriwa na uharibifu wa mazingira na yenyewe yanaisha, upepo mara utakuwepo mara hautakuwepo, chochote kile sasa hakina sustainability na ndiyo maana falsafa ya sasa ni mchanganyiko wa uzalishaji wa umeme wa aina mbalimbali. Sasa ume-derive hoja nzito sana hapa kwamba Serikali haijaliangalia hili jambo economically badala ya kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme wa gesi, inawekeza kwenye umeme wa maji…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge kelele zipo nyingi tutulie Mheshimiwa Silinde anapelekwa shule, endelea Mheshimiwa Simbachawene. (Makofi)

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Silinde anajaribu kutushawishi tuione Serikali imekosea, sisi Wabunge wenzie, Watanzania na dunia kwa kuwekeza katika umeme wa maji megawatt 2100 kutoka kwenye maporomoko ya Mto Rufiji na badala yake tuendelee na gesi ambayo hoja ya kwanza kabisa inaisha, hiyo gesi unayosema inaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unasema size ya bomba… MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa. SPIKA: Hebu tuvumiliaje kidogo…
WABUNGE FULANI: Aaaah! Kaa chini.

SPIKA: Haya Mheshimiwa Ally Saleh. (Kicheko)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama anavyosema, kwa heshima unatakiwa ukae kitako.

Mheshimiwa Spika, ni kweli anachosema kwamba gesi inakwisha lakini jua haliishi, utafiti duniani unaonesha the cheapest ya kufanya umeme ni jua ambalo haliishi, lipo siku zote. (Makofi)

SPIKA: Kuna mawingu siku nyingine, jua halifiki.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Una store, sayansi ipo ya kutosha ya kuonesha utafiti wa jua au umeme wa jua unakutosha na una storage, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Hayo mabetri ya ku-store umeme usafirishe nchi nzima labda jumba hili dogo. Hoja yake kwamba kuna limitations kwa hiyo energy mixing ni muhimu, nafikiri katika kujenga hoja yake yupo sahihi tu. Endelea Mheshimiwa Simbachawene. (Makofi)

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Ally Saleh rafiki yangu kwa kusema anatukumbusha pia kwamba tuweke na umeme wa jua, nimezungumza energy mixing means all sources of energy; inaweza ikawa ya makaa ya mawe, vyovyote vile ambavyo vinatoa energy lakini lazima tuwe na mchanganyiko kwa sababu hakuna ambacho ni sustainable, hata hilo jua yako maeneo hayana jua ambayo huwezi ukazalisha umeme. Na ili uhitaji umeme wa jua unahitaji kilometa za mraba nyingi mno kuzalisha megawatt moja, sasa tukienda huko na ardhi yetu na tunahitaji kulima na shughuli zingine za ufugaji, mzee tutapotea hata huko siyo kwa kwenda sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, amenitoa kwenye mstari lakini nirudi. Unazungumzia ukubwa wa bomba la gesi. Essence ya ukubwa wa bomba la gesi kwanza ilikuwa ni ndoto za baadaye, tungeweza kujenga la kipenyo cha sentimita 18, tukaamua kujenga cha 36 kwa sababu tulijua ugunduzi unaendelea na bomba hilohilo litatumika na eneo potential katika uzalishaji/ugunduzi wa gesi ni huko huko kusini. Kwa hiyo, tulipojenga bomba siyo kwamba tuli-equate gesi tuliyonayo leo na tunachokisafirisha, hapana hiyo sio thinking. Kwa hiyo, equation na yenyewe kidogo ina walakini.

Mheshimiwa Spika, lingine ninalopongeza, na nipongeza Kambi ya Upinzani, this time kwenye hotuba yao wameeleza conspicuously kwenye Ibara yao ya 52, msimamo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Mradi wa Rufiji (Rufiji Hydropower Project). Wanasema pamoja na kukubaliana na dhana ya kuzalisha umeme wa megawati 2,100, wamekubali, kwa hiyo hawa ni wenzetu, hawa ni wazalendo ila wana mambo ambayo wanataka tuyatazame. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani Serikali huu ni mchango mzuri wa Kambi ya Upinzani kwamba somo tulilolipiga kwa muda mrefu sasa wamelielewa na tuko pamoja katika jambo hili na ni hotuba hii wamesema hivi, haya maneno mengine tuendee tu kuwaelewesha.

Mheshimiwa Spika, cost of production katika uzalishaji wetu sisi Tanzania iko juu. Tunaposema uchumi wa viwanda hatuwezi kufika huko kama hatuja-deal na hili suala basic la umeme. Na ndiyo maana katika mpango mkakati wa uzalishaji wa umeme nchini tunasema by 2025 tuwe tuna megawati 10,000, megawati 10,000 unazitoa wapi kama una maporomoko kama yale ya Rufiji halafu unayaacha?

Mheshimiwa Spika, hizi kelele za pressure groups duniani zipo tu, huwa zipo tu, tusibadilishe mwelekeo kwa sababu ya kelele za pressure groups, hizi huwa zipo tu. Lakini kuna nchi gani imejitokeza na kusema inaupinga huu mradi, nchi kama nchi; hakuna nchi, ni pressure groups. Kwa hiyo, nasema mmeelewa, ni jambo zuri na sasa tuko pamoja tunakuunga Serikali Waziri kanyaga mafuta twende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rai yangu sasa, TPDC mmewawekea mzigo ule wa gharama za ujenzi wa bomba. Ukishaweka gharama za ujenzi wa bomba hatutayaona manufaa ya mnyororo wa thamani wa gesi kwa sababu lile bomba linachukua sehemu kubwa sana ya bei na ndiyo maana negotiation hata ya uzalishaji wa mbolea, negotiation ya kupeleka umeme viwandani bado zinasumbua.

Mheshimiwa Spika, na sisi kwenye Kamati taarifa hizi tunazo. Majadiliano yanasumbua, yako hapohapo kwa sababu wanabiashania visenti, visenti, mwenye kisima aliyegundua gesi – kwa sababu Waheshimiwa Wabunge, gesi haiwezi kuchimbwa na Serikali kwa sababu ile biashara ni risk. Unaweza ukatumia hela za Watanzania wote ambao leo hii tunataka kujenga vituo vya afya, tuna tatizo la elimu, tuna tatizo la huduma za jamii kwa ujumla, ukaenda ukachimba uka-hit dry well na umetumia billions of money. Kwa hiyo kazi hii inafanywa na Private Sector lakini ikishagundua ndiyo mnakuwa na mkataba wa makubaliano ya uendeshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hii ndiyo trend ya dunia nzima. Kwa hiyo, negotiations hizo tukishaweka na bomba la gesi – majadiliano hayaendi ndiyo maana viwanda vya mbolea vimesimama, hakuna kinachoendelea. Tuondoe bomba la gesi tulibebe kama Taifa kwa sababu tunafanya mambo mengi yenye gharama kubwa kuliko hata bomba la gesi, mbona haijawa-pegged? Ina maana standard gauge leo na yenyewe tuiwe TRC, ina maana barabara hizi tuweke TANROADS; itakuaje, tutaendeshaje?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uchumi kwa sababu umeme ndiyo utakao-tickle uchumi mzima kuamka ninasihi Serikali ione umuhimu wa kuchukua hii gharama tuibebe kwa ujumla wake. Kwa sababu umeme huu ndiyo unaobeba uchumi pia, tukiongeza hizi megawati maana yake umeme ukisambaa kila mahali uzalishaji unakuwa na bei rahisi, uzalishaji wa bidhaa zetu zitashindana hata kwenye masoko mengine huko duniani. Kwa sasa wanachotushinda wenzetu walioendelea na wanaotuuzia bidhaa ni costal production ambayo number one ni power, sisi umeme wetu ni aghali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niliomba nitoe rai hii na nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipa, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali na nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa kazi nzuri wanayoifanyia taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapojenga uchumi wa nchi kama ya kwetu, ambayo zipo falsafa tofauti, wengine wanaona tunakimbia, wengine wanaona tunachelewa, wengine wanaona tunakosea na wengine wanaona tunapatia, ni lazima uwe na msimamo ili kuweza kufanya unayofikiria kufanya na hasa kama umepewa dhamana ya haki na halali ya kuongoza nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Chama cha Mapinduzi kimepewa dhamana hii kwa kushinda uchaguzi na Chama cha Mapinduzi ndicho kinachoshika historia ya nchi hii kwa sababu ndicho kilichoongoza nchi hii toka tulivyopata uhuru. Tunafahamu wapi tulipotembea tukaona mabonde, tunafahamu wapi tulioona kuna miteremko mikali na tunajua namna ya kushika brake au kuongeza mwendo. Niwasihi na niwaombe wenzetu waliopo humu na Watanzania kwa ujumla waunge mkono jitihada hizi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajaribu kutekeleza miradi ambayo ilikuwa haijaweza kutekelezwa tangu katika mipango ya kwanza kabisa tulipopata uhuru, leo inafanyika. Tunafanya miradi mikubwa ambayo inajenga msingi wa uchumi wa nchi kwa ajili ya vizazi vyetu vijavyo, siyo kwa ajili ya sisi. Ukijenga reli, haujengi kwa ajili ya sisi leo na kwa hiyo, hata ukikopa hatukopi kwa ajili yetu sisi, tunakopa kwa ajili ya watoto na wajukuu zetu na kukopa si dhambi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunajenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Stiegler’s Gorge ambao hata tukikopa si kwa ajili ya sisi tu tunaoishi leo, ni kwa ajili ya vizazi vijavyo. Ni muhimu katika kuangalia hii mikubwa ikiwemo ya ufufuaji wa Shirika la Ndege kwa sababu ipo miundombinu muhimu ikiwemo barabara, ujenzi na huduma za afya, haya yote yanafanyika kwa gharama kubwa lakini pia uwekezaji kwa watoto wetu katika kutoa elimu bure ni mambo makubwa ambayo yakifanyika leo yana maana sana kwa kizazi kijacho kuliko sisi tunaoishi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa hapa suala la kukopa na pengine nianze na hili ambalo Mheshimiwa Zitto amelisema juu ya masuala ya mamlaka ya fedha.

Mheshimiwa Zitto ukiisoma Katiba Ibara ya 99 unayaona mamlaka ya Rais katika masuala ya fedha pia. Sasa lazima usome zote mbili na kwa sisi wanasheria huwa tunazisoma ili tuweze kujua kama sheria hizi zinasomeka kwa pamoja au zinaenda mutatis mutandis au zinaenda kwa kupingana. Ninachokiona hapa ni kwamba hiyo uliyoisoma lazima uisome pia na Ibara ya 99. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 99 inasema hivi; “Bunge litashughulikia jambo lolote kati ya mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na Waziri. Na mambo yanayohusika na Ibara hii ni haya yafuatayo; Muswada wa Sheria kwa ajili ya lolote kati ya mambo yafuatayo; kutoza kodi au kubadilisha kodi kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kupunguza.”

Sasa katika madaraka haya na ukisoma na hizi nyingine ni lazima uisome na hiyo. kwa hiyo, kuamua kuwatambua Watanzania wakajulikana kwa shughuli wanazozifanya ili waweze kupata msaada wa Serikali labda lingehojiwa msaada wa Serikali uko wapi dhidi ya hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nasema…

MHE. KABWE Z. R. ZITTO:Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Simbachawene pokea taarifa.

T A A R I F A

MHE. KABWE Z. R. ZITTO:Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa George Simbachawene, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti aangalie taarifa ya Kamati ambayo yeye mwenyewe ameiongoza ambayo imesomwa hapa Bungeni ukurasa wa 27 aya ya 4.1 kuhusu namna ambavyo mamlaka zinajiamulia kukusanyakusanya mapato bila consultation ya Wizara ya Fedha na Bunge hili kuleta sheria, arejee katika hilo kabla hajanijibu mimi ndiyo atajua kwamba nilichokuwa nakiongea mimi ni kile ambacho kamati imeleta hapa.

SPIKA: Mheshimiwa Simbachawene unapokea hiyo taarifa?

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, anavyoitafsiri ni tofauti, tumezitaja kabisa; tumesema Wizara, taasisi/mamlaka ya mikoa na wilaya. Ni kwa sababu ya vile vikodi/vitozo vidogo vidogo ambavyo vinahitajika kwa mujibu wa sheria Serikali i-coordinate siyo kila mamlaka itoke na kodi/ tozo yake, zinaleta shida na kero kwa wananchi na huu ndiyo ulikuwa ushauri kwa Serikali na bahati nzuri Serikali ilishaupokea ushauri huu kutoka kwenye Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini tunakopa leo? Lakini pia lazima nieleze ipo tofauti kati ya Deni la Taifa na Deni la Serikali; hapa tunachanganya mambo. Deni la Serikali ni lile ambalo Serikali imekopa kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana na lina utaratibu wake. Haiwezekani ikasemekana eti halieleweki, sheria ipo inakuwaje deni liwe halieleweki? Deni la Serikali linaeleweka vizuri kabisa ingawa Serikali pia ina udhibiti wa Deni la Taifa lakini Deni la Taifa linahusisha pia mikopo ya sekta binafsi. Kwa hiyo, lazima kuelewa namna ya ku-balance, isijeikachukuliwa yote kwa ujumla wake halafu ikawachanganya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inadaiwa hapa kwamba eti sisi tunakopa sana na pengine deni hili limeongezeka. Madeni tunayolipa leo kama nchi yalikopwa toka awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi hii, kwenye ule mkeka yapo madeni na Kamati yako iko well informed. Vipo vitu tunavipata kule na mimi namshukuru Mungu kuwepo kwenye Kamati hii nimejifunza mambo makubwa ambayo nilikuwa siyajui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, madeni tunayolipa leo ni ya miaka ya 1980, 1990 yaani ya siku za nyuma ndiyo tunalipa leo na haya tunayokopa sisi yatalipwa huko mbele, lakini lazima tuhakikishe tunakopa kwa ajili ya kitu gani. Sasa tunapokopa kwa ajili ya reli ambayo watoto wetu wataikuta kwa miaka 100 ijayo, tunapokopa kwa ajili ya kuzalisha umeme ambao wajukuu zetu wataukuta, kuna ubaya gani! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukopaji una uwiano wake na uwiano muhimu ni kipimo cha debt to GDP ratio. Deni ukilinganisha na GDP (Pato la Taifa), kwa mfano Tanzania nilishanishe tu kidogo, Marekani debt to GDP ni asilimia 106.1; Kenya debt to GDP ni asilimia 52; Zambia debt to GDP ni asilimia 54; Ugiriki debt to GDP ni asilimia 179 yaani GDP yao inaingia kama mara mbili na zaidi, lakini Tanzania debt to GDP yetu ni asilimia 32, tupo chini ya wengine wote. Kwa hiyo deni letu ni himilivu, tena bado tuna nafasi ya kukopa ili tuweze kuwekeza, cha msingi ni kuwekeza kwa ajili ya watoto wetu na wajukuu zetu na vizazi vijavyo, hicho ndicho cha msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yamesemwa mambo hapa…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. DAVID E. SILINDE: Achana nae unapoteza muda.

SPIKA: Mwakajoka nini tena? Maana yake hiyo shule…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, unajua amejisahau…

SPIKA: Ngoja kidogo, subiri, hujaruhusiwa bado.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Unasikia mzee amejisahau anasema kwamba…

SPIKA: Hujaruhusiwa kwanza, nitakupa nafasi.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Aah sorry.

SPIKA: Usiwe unaongea kabla hujapewa nafasi. Nilikuwa nasema kwamba shule hii inayotolewa na lawyer kwa Zitto economist ilitakiwa...; Mheshimiwa Zitto ni Mwakajoka amesimama kwa hiyo…, Mwakajoka nakupa dakika moja. (Makofi/Kicheko)

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika,mimi nampa taarifa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza kwamba anazungumza kama Waziri, ajue kabisa kwamba sasa hivi ni Mbunge wa kawaida, kwa hiyo, anatakiwa kutoa michango yake. (Makofi)

SPIKA: Aah! Yaani kwa kweli umechezea wakati wangu, hapa wanaongea professionals na Mwakajoka hujawahi kuniandikia professional yako ni nini hasa? Mheshimiwa Simbachawene endelea. (Kicheko)

MBUNGE FULANI: Darasa la nne huyo.

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, nataka Mwakajoka afahamu kwamba kila Mbunge wa CCM ni Waziri mtarajiwa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri wakati mwingine tukafahamu historia ya uchumi wa nchi yetu na namna tunavyoujenga. Tulipopata uhuru tulijenga uchumi wa kijamaa na mpaka leo misingi ya kijamaa hatujaiondoa kwenye Katiba hii. Ukisoma Ibara ya 9 inaeleza vizuri namna ya kujenga uchumi wetu, kwa sababu ya muda sitainukuu, lakini nataka wafahamu kwamba ni tofauti na baada tulipofika mwaka 1967 tukajenga uchumi mwingine, lakini pia tumejenga uchumi wa aina tofauti katika kipindi cha kila awamu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, leo hii tunajikuta tunasahihisha makosa ya uchumi wa soko huria ambao ulikuwa ni fashion na sera ya mashirika ya fedha duniani including World Bank. Tumefika tulipofikana inadaiwa kwamba hatujapiga hatua kubwa ukilinganisha na wenzetu kwa sababu ya aina ya uchumi tulioujenga. Mataifa ya Asia ambayo yali-harmonize ujamaa na ubepari na ndiyo maana Wachina wanasema wanajenga scientific socialism leo, ndiye aliyefanikiwa kupiga hatua.

Mheshimiwa Spika, kwa ninavyoona mimi, ninaona kama Serikali ya Awamu ya Tano inaenda kwenye aina ya ujenzi wa uchumi wa scientific socialism. Mwelekeo huu ni sahihi, ndiyo uliofanya nchi za Asia, Malaysia, Singapore, Bangladesh na zingine kupiga hatua kubwa kiuchumi including China yenyewe na nchi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tupewe nafasi kama Chama cha Mapinduzi, tuipeleke hii nje, tufike mahali tuje tupimwe kwa kura za wananchi na nataka niwaambie Watanzania kwamba leo hii ukitaka kujenga nyumba, lazima ujinyime kabisa, ni lazima tujinyime kidogo ili tuweze kujenga nchi yetu, haiwezekani tukawa tunafanya sherehe huku tunafanya maendeleo, haiwezekani. Ni lazima tukubali, tusikilizane, tulete utulivu tuone nchi inavyojengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania ni mashahidi, kila mahali nchi hii inajengwa, katika kila sekta nchi inajengwa, sasa ni lazima tujenge nchi, haya mambo mengine yatakuja tu. The highest good in life is happiness, Plato alisema, we will be happy kama tumejenga misingi ya uchumi imara. Tumefika tulipofika leo kwa sababu hatukuweka misingi imara sana ingawa awamu zilizopita zilifanya kazi nzuri, lakini kila regime ina fashion yake, let’s follow this fashion. Twende tumuunge mkono Rais, tujenge misingi ya uchumi na mimi naamini ndani ya miaka 10 na kama tutaendelea kumchagua Magufuli kuwa Rais wa nchi hii, tutayaona makubwa ambayo hatukuwahi kuyafikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi/Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri waliyochangia na kusema ukweli michango pamoja na kwamba ni siku moja lakini michango ni mingi mno. Umetuendesha vizuri na tumepata wachangiaji 25 waliopata kusema. Lakini pia tumepata wachangiaji wengi walioweka kwa maandishi. Niseme tu kwa kweli michango yote tunaithamini na tutaichukua yote kwa ajili ya kuifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nafahamu pia wako ambao hawakusema lakini pia hawakuandika ila kwa namna moja ama nyingine tumekuwa tukikutana wakieleza yao. Nataka niseme tu wote michango yenu tutaitumia katika kuhakikisha kwamba tunaboresga utendaji kazi na kuleta mabadiliko katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, nianze na mchangiaji wa kwanza ambaye ni Kamati yenyewe ya Nje, Ulinzi na Usalama. Michango na maoni yote ya Kamati ya Nje, Ulinzi na Usalama kamati inayoongozwa na Mheshimiwa Zungu, yote kabisa tunaichukua kama ilivyo na sisi kwetu ni suala la kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, Kamati hii ina watu wenye weledi, tunafanya nao kazi kwa karibu na tukijifungia kule tunafundana kweli kweli. Ndiyo maana mengi hapa hayajasemwa lakini hata ambayo hayakuja hapa sisi tunayafahamu na tunayafanyia kazi kwa kadri walivyotuelekeza. Kwa hiyo, nawashukuru sana Wajumbe wa Kamati wote kabisa na hotuba yenu yote sisi tumeichukua na tutaifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, sio rahisi sana kujibu hoja zote zilizosemwa hapa kwa maandishi na wale waliosema na kwa hivyo nitajaribu kusema baadhi ya zile ambazo kwa mujibu wa uzito wake basi zinapaswa kutolewa majibu hapa.

Mheshimiwa Spika, zimezungumzwa changamoto za vyombo vyote, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto, juu ya changamoto ya vitendeakazi, changamoto ya makazi ya askari, ofisi zenyewe (vituo) au makambi ya magereza. Yamezungumzwa hapa masuala ya maslahi ya watumishi, upungufu wa watumishi kwa maana ya askari. Yote haya ukiyaangalia kwa namna yalivyo, ni suala la fedha. Kama bajeti ikiruhusu tunaweza tukamaliza matatizo haya yote na tufahamu kuwa nchi yetu hii ni kubwa, Wilaya nyingi bado hazina huduma muhimu, hatuna vituo vya polisi, hatuna makambi kwa ajili ya magereza na nchi inapanuka na kila siku tunaanzisha maeneo ya utawala mapya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme changamoto hii tunaichukua kama Serikali na kadri bajeti zinavyokwenda tutakuwa tunapungua changamoto na mtaona hata katika kitabu chetu cha hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani tumeweka fedha nyingi sana kwenye development sasa. Kubwa ni kwamba fedha hizo zipatikane na tuweze kutekeleza miradi hiyo, inayoendelea na ile ambayo itatekelezwa kwa fedha hizi ambazo tunaziomba safari hii.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, changamoto ni nyingi, zote mlizozisema, nyingi zinahitaji fedha. Kama fedha hakuna, hakuna muujiza hapo. Na siwezi kusema kwamba nitafanya kwa sababu ni fedha ndiyo itakayofanya. Kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge mtuelewe, kadri Serikali itakavyokuwa inapata fedha tutaendelea kupunguza changamoto mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tunayo magari takribani 357 ambayo yataingia wakati wowote kwa ajili ya Jeshi la Polisi. Tutajitahidi tugawane kwa kuangalia uzito wa maeneo yetu mbalimbali. Safari hii tutaangalia maeneo ya vijijini zaidi na ya mipakani ambako huko ndiko kuna changamoto nyingi sana. Nimeongea na IGP amesema kweli kabisa this time tutayapeleka magari haya vijijini zaidi kuliko hata mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia katika ujenzi wa makazi ya askari katika kila jeshi tumepanga kiwango cha fedha ambazo zitakwenda. Kuna ambao wana shilingi bilioni sita, bilioni tatu, bilioni mbili; zitatusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto hii ikiwemo na kusaidia miradi inayoendelea sasa. Tumepewa fedha nyingi sana ambazo kusema kweli zitatusaidia sana, Dodoma tu hapa tunajenga nyumba nyingi tu, lakini na mikoa kadhaa tutajenga nyumba nyingi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaambie Waheshimiwa Wabunge changamoto hizi tunazifahamu kama Serikali na kusema ukweli askari wetu wanaishi katika makazi ambayo hayafai ukilinganisha na mabadiliko ya uchumi na kadiri tunavyokwenda kwenye uchumi wa kati, haiwezekani sekta nyingine zimekuwa sana elimu, afya lakini sekta hii ya ulinzi bado hatujaikuza kulingana na mazingira tunayokwenda nayo. Bado kuna majengo ya kikoloni yanaonekana, lock up za kikoloni, cell za kikoloni, bado tuna kazi kubwa ya kufanya. Mimi niseme natambua sana michango ambayo imetolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, yako mengine ambayo yamezungumzwa ni very specific. Kuna hili lilizungumza juu ya mafunzo yale ya utayari ya askari polisi. Yale mafunzo siyo mafunzo kama mtu anaenda kusomea kazi mpya. Ni mtu anaenda kufanya mafunzo ya utayari, ukakamavu, sasa ile ni sehemu ya kazi. Hizi Sh.10,000 ambazo wanapewa kila siku kama ration allowance huwa ni kwa ajili ya askari huyo kupata chakula. Kwa hiyo, awe yuko ofisini, barabarani, likizo au ypo kwenye training ya mafunzo hayo ni hela hiyohiyo ndiyo anayotakiwa kula.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sasa ukisema unamlipa nyingine wakati ana hela ya kula na ameenda kwenye mafunzo ya utayari, jamani, unajua kuna utofauti kati ya vyombo hivi vya kijeshi na civil service ya kawaida. Hawa wanajeshi utayari ni sehemu ya kazi yao, yaani kunyakua, kuruka kichura na kadhalika ni sehemu ya shughuli yao sio mafunzo kama mafunzo mapya. Kwa hiyo, anapokwenda pale anahama na ileile Sh.10,000 yake anaenda kuila akiwa kule kwenye yale mafunzo kwa sababu ukimlipa utakuwa umemlipa double payment na kwa mujibu wa sheria za Serikali ni makosa mtu kumlipa malipo mara mbili kwa ajili ya jambo hilohilo. Kwa hiyo, chakula hicho atakula akiwa nyumbani, kwenye mafunzo au akiwa popote. Hiyo ndiyo PGO inavyosema na ndiyo sheria ya nchi inavyosema. Sasa kama ni suala la huruma ya kwangu mimi Simbachawene ningesema tu kwamba walipwe lakini sasa ni sheria kwamba amepewa ration allowance ataila popote pale atakapokuwa.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni juu ya kazi ya Jeshi la Polisi na lawama ambazo wamekuwa wakipewa. Nataka niwaambie ndugu zangu, ukiangalia katika takwimu na ukiangalia level ya uhalifu katika nchi yetu tuna nafuu kubwa sana. Leo katika hotuba yangu nimesema makosa ya usalama barabarani yamepungua kwa asilimia 36.4 na makosa ya jinai za kawaida yamepungua kwa asilimia 15.9. Hii maana yake ni kwamba vyombo hivi vinafanya kazi vizuri kwa kushirikiana na wadau wengine. Lawama za mtu mmoja- mmoja kwa tabia yake na hulka yake hizo haziwezi kuepukika zipo katika kila sekta. Hawa askari polisi ni binadamu, ni watoto wetu tuliowalea wenyewe na tunawajua wanavyofanana; tunawajua kwa sababu ni ndugu zetu, kwa hiyo, siyo kosa la mtu mmoja lifanye jeshi zima la polisi likawa halina maana.

Mheshimiwa Spika, hapa nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao kwa kweli mmesema sana juu ya hali za maisha ya vijana hawa wanaofanya kazi nzuri na kwamba zinatakiwa kuboreshwa pengine tutawatoa kwenye utendaji mbovu, mtu anaingia ana -stress, anakuja pale badala ya kum-arrest mtu vizuri anam-arrest vibaya kwa sababu yuko traumatized kiasi kwamba akili yake haiko vizuri. Kwa hiyo, tushirikiane kwa pamoja na mimi nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa mfano, sisi Jeshi letu la Polisi limejitahidi sana kufanya kazi vizuri kwa kushirikiana na majeshi mengine na wadau wengine. Ukiangalia takwimu, kwa mfano, kuna namna ambayo unaweza uka-rate ukaangalia jinai ikoje na makosa yakoje, Kingereza wanasema incarceration rate. Incarceration rate ni pale unapohesabu katika population ya watu laki moja ni watu wangapi wako magerezani au wamezuiwa wanasubiri aidha kesi au wamehukumiwa.

Sasa ukiangalia Marekani incarceration rate ni 727, Kenya 81, Uganda 124, Brazil 193, Tanzania 59. Maana yake katika Watanzania laki moja wanaokuwa wamezuiwa magerezani ni wachache. Hii maana yake ni kwamba vyombo hivi vinafanya kazi nzuri na ndiyo namna pekee ya kuweza kutathmini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge na nieleze kwamba kwa yale ya marekebisho waliyosema tutaendelea kuchukua hatua kwa wale ambao hawana uadilifu. Mambo yote yanafanyika kwa mujibu wa utaratibu, mtu anapokiuka taratibu kusema kweli tutachukua hatua kali. IGP hapa kila siku lazima kuna watu wanakuja ofisini kwangu kukata rufaa amewafukuza. Ukitaka kuwarudisha anakwambia haiwezekani huyu mimi najua hafai kuwa askari polisi. Ninyi wenyewe Wabunge ndiyo mnaonipigia simu Mheshimiwa Mbunge ndugu yangu amekuwa hivi, amekuwa hivi, huku tunakwenda kwa mujibu wa sheria na hili ni jeshi, huku ni discipline asilimia 100. Kwa hiyo, tutajitahidi na tutachukua hatua kuhakikisha tunakuwa na jeshi lenye weledi lakini lenye nidhamu pia.

Mheshimiwa Spika, limezungumziwa suala la ucheleweshaji wa malipo ya wastaafu na hapa ni kwa majeshi yote. Nataka niwaambie malipo ya wastaafu sasa hayachelewi sana, kama yanachelewa ni pamoja pia na malipo ya wastaafu wengine. Mimi nizungumzie ile ya kufungasha mizigo na kumrudisha askari aliyestaafu kwao; hii ilikuwa ina tatizo kwa muda wa miaka kadhaa, kwa kweli ilikuwa haijalipwa, lakini Mama yetu Mheshimiwa Rais Samia Hassan Suluhu alipoingia tu kama kuna document ya kwanza niliyompelekea ofisini kwake ilikuwa ni kumuomba fedha hizi na sasa ameruhusu na zimeanza kutoka. Uhamiaji wameshapata shilingi milioni 65, Polisi wamepata shilingi bilioni 3 na Magereza wamepata shilingi milioni 812, tumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Sasa tutaanza kuwalipa wale wastaafu ambao walikuwa hawajapewa fedha zao kwa ajili ya kufungasha mizigo na kurudi nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lilizungumzwa jambo ambalo lilikuwa sensitive kidogo kwa sababu ni gender sensitive; suala la taulo za kike kwa askari na kwa wafungwa. Bado jambo hili si la kukurupuka na kulisemea kwa sababu tukisema kwa askari ambao wana mshahara na wana malipo mengine kama hizo allowance, ration allowance na vitu kadhaa, wataibuka na walimu hapa, watasema kwani sisi walimu wa kike hizi taulo na sisi vipi? Kwa hiyo, maeneo mengine na sekta nyingine wataibuka, lakini acha tulichukue kwa sababu ni jambo la gender kwa sababu pia kuna jeshi mojawapo hapahapa nchini linafanya hivyo. Tujiulize wenzetu wamefanyaje, wamechukua wapi, basi tutaelewana na tunaweza tukaja na suluhisho lakini ni muhimu zaidi kwa wafungwa magerezani. Kwa wafungwa magerezani hili nadhani tulichukue tuone namna tunavyoweza kuwashirikisha wadau kuweza kutatua tatizo hili kwa sababu wale hawana alternative means, wamefungiwa mle hawana njia, asiyekuwa na uwezo anafanyaje? Hili tunalichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ilizungumzwa juu ya Graduate Sergeant kufanya kozi ya graduate. Sergeant huyu kama ni graduate ukienda moja kwa moja ukawa Inspector umeruka sana. Zamani utaratibu ulikuwa ni huu uliorudi sasa wa kwamba lazima apitie kwenye Sergeant course ndiyo aende kwenye Inspector. Ukimaliza Sergeant course siyo mtu mdogo anaongoza askari 30. Kwa hiyo, mimi niseme tu utaratibu huu mpya acha tuuone unavyokwenda, lakini hata watakaokuwa na diploma wanaweza wakafanya hii Sergeant course kwa sababu majukumu yale hawezi kushindwa kubeba mtu mwenye diploma. Kama anaweza kubeba mwenye degree na mwenye diploma anaweza kubeba.

Mheshimiwa Spika, kwa harakaharaka nizungumzie suala la tozo za zimamoto, ukaguzi wa majanga ya moto na kutoa ithibati. Tozo hii ni kweli imelalamikiwa ni kubwa na Kamati ime-raise concern kubwa sana kwamba ukaguzi ukifanywa gharama zile ni kubwa. Tunafikiri na kwa sababu ni suala la Kanuni zilizo chini ya Waziri tutajaribu kuona, tupitie upya, tutashirikiana na Kamati yenyewe ili tuweze kuja na Kanuni rafiki ili tupanue na wigo wa watu wanaoweza kulipa. Hili hatuwezi kulifanya ndani ya mwaka huu, tulifanye kwa mwaka huu kwa ajili ya mwaka wa fedha unaokuja kwa sababu Kanuni za Fedha zinatukatalia.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine lililozungumzwa ni upekuzi magerezani. Upekuzi huu unafanyika kwa mujibu wa sheria. Kama kuna wanaofanya kinyume na sheria inavyotaka, wanafanya makosa na pale tutakapopata taarifa za malalamiko mahsusi tuna uwezo wa kuchukua hatua kwa wale waliofanya upekuzi huo.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine lililozungumzwa ni suala la Uhamiaji. Uhamiaji na hasa mipakani ambapo wamelalamika sana, niseme tu hata inapozungumzwa habari ya Kitambulisho cha Taifa cha NIDA unaweza ukapata kitambulisho lakini bado ukawa…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Waziri anapoongea hapa ni elimu kubwa sana kwenu ambayo itawasaidia hata ninyi kufafanua baadhi ya mambo kwa wananchi. Sasa mtu unakuwa uko hapa hapa unapiga story wakati yanatolewa majibu ambayo ndiyo kero za wananchi, ni vizuri sana mkakaa mkasikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, endelea.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, wamesema kwamba maeneo ya mipakani kuna ubaguzi, wanahojiwa waseme nne, waimbe wimbo wa Taifa; hizi ni technique tu za kutaka kujua huyu ni nani na huyu ni nani. Kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wa mikoa ya mipakani tunafahamu kwamba wakati mwingine kati ya nchi hii na nchi hii kutofautisha ni kitu kigumu sana, lakini ni kautaratibu tu fulani siyo conclusively kwamba kenyewe anatosha kuweza kumtia mtu hatiani. Kinachofanyika ni zaidi ya hapo, tunataka kujua pia umezaliwa wapi, wazazi wako walikuwa wapi, hayo tumekuwa tukifanya na ndio kazi ya Idara ya Uhamiaji. Tukifanya hivyo tunagundua kabisa, mtu mwingine anakwambia mimi mama yangu alifia hapa lakini tukienda nchi ya pili tunaenda kukuta mpaka mama yake na kwao mpaka tunajua kila kitu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya tunayafanya kwa weledi mkubwa na Waheshimiwa Wabunge naomba mtuamini. Kwa sasa tunadhani pengine tukipata vitambulisho hivi vya Taifa ndiyo tumepata uraia wa Tanzania; uraia wa Tanzania una Sheria yake ya Uraia na unamchakato wake. Kitambulisho hiki ni procedure tu ya kuwatambua na vinatolewa hata kwa wakimbizi na wahamiaji wa kazi. Kwa hiyo, ukipata kitambulisho hiki siyo muarobaini kwamba wewe umeshamaliza sasa hutaulizwa, hapana! Utaulizwa na utanyang’anywa hata hicho kitambulisho kama umepewa tukigundua kwamba wewe siyo raia wa Tanzania kwa sababu ziko haki za Mtanzania na ziko pia haki za mtu anayeishi Tanzania ambaye siyo raia wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, suala la NIDA. Kwa sasa tulikuwa tunamalizia vitambulisho vya first generation kwa maana ya ile backlog ya zamani. Ndiyo maana kasi yetu pamoja na kufunga mashine haijawa kubwa kwa sababu kwa sasa tunazalisha vitambulisho kama 32,000 kwa siku. Lengo letu lilikuwa ni kuzalisha vitambulisho 140,000 kwa siku endapo tungekuwa tunatumia vitambulisho vya second generation. Sasa vile vya first generation bado tulikuwa na backlog ya vitambulisho kama 4,500,000 (raw card) ambazo ni lazima tuzimalize, tusipozimaliza ile ni fedha tutapata hasara. Kwa hiyo, mtaona speed inasuasua lakini badaye tutatoa vitambulisho kwa speed kubwa.

Mheshimiwa Spika, mimi nina uhakika kwamba hadi Julai, August, backlog yote iliyokuwepo ya 25,000,000 tutakuwa tumemaliza kabisa. Kwa target ya 25,000,000 tumetoa vitambulisho 7,000,000, tuliokwishawatambua ni 18,000,000. Tuna uhakika kazi ya utambuzi kama imefanyika basi kazi ya kufyatua vitambulisho itafanyika kwa speed.

Mheshimiwa Spika, changamoto ni nyingi, ukitaka kununua wino mchakato wa manunuzi, ukitaka kununua raw card mchakato wa manunuzi, ukitaka kufanya sijui nini mchakato wa manunuzi. Kwa hiyo, michakato hii ya manunuzi ndiyo inayochelewesha mambo kwenda lakini sasa ndiyo sheria za nchi tutafanyaje? Hata hivyo, kwenye eneo hili nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Julai na Agosti watu wote waliokuwa wamechukuliwa alama za vidole, wametambuliwa watakuwa wamepata vitambulisho vyao.

Mheshimiwa Spika, sasa ilielezwa hapa juu ya kadi mbovu 427,000 zilizokuwa zimeonekana wakati Mkaguzi wa Hesabu za Serikali alipopita kwenye Ofisi za NIDA. Kadi zile zilikuja mwanzo kabisa wakati NIDA haijaanza kuzalisha hata kitambulisho hata hiki kimoja. Walipoangalia specification wakaona haziendani na zilizokuwa zimeagizwa, kwa hiyo, mkandarasi akaambiwa kadi zako hizo hatuzitaki, tunazozitaka sisi ni hizi. Kwa hiyo, ilikuwa ni yeye juu yake kuja kuchukua kadi zake kwa sababu hatuzihitaji pale lakini kwa sababu sasa zimeshafutwa kwa mujibu wa sheria na tumeandikiana tayari hakukuwa na mawasiliano mazuri kati ya Ofisi ya CAG na Ofisi ya NIDA juu ya namna ambavyo zile kadi zilikuwa abandoned pale maana hazina specifications tunazozihitaji. Kwa hiyo, zinatakiwa hata kuteketezwa yaani hazihitajiki. Kwa hiyo, eneo hilo ndivyo ambavyo ninaweza kulisemea.

Mheshimiwa Spika, maeneo mengine ambayo yamesemwa ni yale ya jumla, kama nilivyosema tutajitahidi kuyafanyia kazi na kuhakikisha kwamba yote yaliyosemwa na Waheshimiwa Wabunge tunayazingatia. Vinginevyo nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wachangiaji wote, nina vikaratasi hapa vina michango mingi sana lakini niseme tu tutazingatia yale waliyoshauri.

Mheshimiwa Spika, niongelee hili la mradi wa Dar City, zile nyumba za Kunduchi na Msasani ambapo Kamati pia na wenyewe walisema. Tulielewana na Kamati, tunamalizia mchakato wa mwisho ili negotiation kati ya yule mbia na Serikali uweze kumalizika kwa sababu pale ni kwamba mkataba ule unavunjika. Mnapovunja mkataba kunakuwa kuna mambo mengi, investment ile ilikuwa ya miaka 70, investment ile ilikuwa ya hela nyingi kwa hiyo, Wizara ya Fedha na Wizara yangu zinaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba tunamaliza mkataba ule bila Serikali kuingia kwenye kesi mbaya au kuvunja mkataba kwa kukiuka taratibu.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kukushukuru sana wewe na Waheshimiwa Wabunge wote. Nimshukuru Naibu Waziri wangu na Maafisa wote wa vikosi vyote ambao wanafanya kazi kwa karibu sana pamoja na mimi.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nami ni mara yangu ya kwanza kuzungumza ndani ya Bunge lako Tukufu, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya na uhai mpaka kufika siku ya leo, lakini kwa namna ya pekee sana nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini na kunipa jukumu hili la kuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu ninaeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Rais kwamba kazi hii nitaifanya kwa umahiri mkubwa, kwa uadilifu mkubwa na jitihada zote katika kuhakikisha kwamba namsaidia Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kazi yake iweze kuwa na mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru tena Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango kwa namna ambavyo anamsaidia Mheshimiwa Rais pia anatusaidia na Waheshimiwa Mawaziri katika kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru sana Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa namna alivyofanya mageuzi makubwa kule Zanzibar na kufanya Zanzibar iwe kama inavyoonekana sasa katika hali nzuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ambae ndiyo mwenye hoja hii ambayo iko mbele tu nianze kabisa kwa kuiunga hoja hii mkono kwa ailimia 100 na ninawasihi na kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote kama ambavyo mmekuwa mkifanya tuendelee kuiunga mkono hoja hii, maana hoja hii Mheshimiwa Waziri Mkuu pia anashika Fungu la Bunge na kwa hivyo tusipoiunga mkono sijui tutaendeleaje na shughuli zetu hapa, kwa hivyo niwaombe na niwasihi pia tuunge mkono hoja hii ili mambo yetu yaweze kwenda sawa sawa.

Mheshimiwa Spika, nami naamini katika hili ni pande zote na hata wenzetu wa Upinzani walio wachache watatusaidia katika kuunga mkono hoja ili shughuli ziweze kufanyika na tutekeleze majukumu yetu ambayo wananchi wametuleta humu ndani.

Mheshimiwa Spika, ninakupongeza wewe kwa namna unavyoliongoza Bunge pia Mwenyekiti wetu wa Kamati ambapo mimi ninadondokea katika Kamati mbili. Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati ya UKIMWI na magonjwa yasiyo ambukiza, Wenyeviti wangu hawa wawili pamoja na Wajumbe wa Kamati hizi tumeshirikiana nao vizuri sana katika maandalizi yote ya bajeti hii na hata katika hotuba walioitoa yote yale ambayo wameyasema niseme kwa ujumla wake kwa kuwa siyo rahisi kuyajibu moja moja tunayachukua yote na tutaendelea kufanyanao kazi kwa pamoja na kuhakikisha kwamba yale wanayotushauri, yale wanayosimamia yote tunayatekeleza kadri Mungu atakavyoweza kutujalia.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya mambo yanayosemwa hapa mengi yanadondokea katika taarifa za Kamati, nianze tu kupongeza taarifa zote na kwamba baadhi ya hoja ambazo zimezungumzwa na hasa Kamati ya Katiba na Sheria, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama alikuwa na maelezo ambayo yalibeba ujumbe wa Kamati na kutoa maoni mbalimbali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nami nitayajibu kwa mujibu wa Kanuni (99) (2) Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Januari mwaka 2016 ambaye inaruhusu kujadili utekelezaji wa bajeti za Wizara.

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ilikuwa ni suala la kupanua wigo wa wapiga kura, idadi inayopiga kura ni wachache, kwa hiyo Kamati ina maoni kwamba lazima kazi ifanyike ili kuweza kupeleka elimu na kutia hamasa ya wanachi wengi kupiga kura kadri inavyowezekana, hili tunalichukua pia Kifungu cha Sheria Na. 4(c) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura 343 kinatoa jukumu hili kwa Tume ya Uchaguzi kuhakikisha kwamba inatoa elimu kwa wapiga kura na kuhakikisha kwamba idadi ya wapiga kura inaongezeka na kuwa ya kutosha kulingana na idadi ya population ya nchi.

Mheshimiwa Spika, pia hakujafungwa taasisi na asasi za kiraia na viongozi mbalimbali wa kijamii msisitizo wangu hapa na wenyewe tuchukue jukumu la kuhakikisha kwamba tunawaelimisha wananchi wetu umuhimu wa kushiriki katika zoezi la kupiga kura, kwa sababu ndiyo mahala pekee ambapo kwa maoni na uchaguzi wao wanakuwa na maoni yao ya jumla nini wanataka katika Taifa lao litokee.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine la pili, ambalo ni maoni ya Kamati ni kuhuishwa kwa daftari la wapigakura. Sheria ya uchaguzi Sura 343 ya Tume ya Uchaguzi inapaswa kuboresha daftari hili mara mbili kila baada ya uchaguzi na kabla ya uchaguzi unaofuata na jambo hili limekuwa likifanyika na kwa hivyo niendelee kusisitiza tu kuendelea kufanyika kwa jambo hili kwa maana ni jambo la msingi kuhakikisha kwamba daftari hili linaboreshwa kila mara.

Mheshimiwa Spika, pia ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itoe elimu kwa Wasimamizi na Wasaidizi wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa na wagombea kuhusu sheria zinazosimamia uchaguzi. Sheria ya Vyama vya Siasa Sura Na. 258, Ofisi ya Msajili inajukumu la kutoa elimu hii kwa umma, kwa Wagombea, kwa Vyama vya Siasa ili kuhakikisha kwamba demokrasia inasimamiwa katika misingi ya kisheria lakini na kudumisha amani.

Mheshimiwa Spika, eneo la Nne ilikuwa ni kuhuisha taarifa za vyama vya siasa katika register za kisheria, hili ilizungumzwa na Kamati niendelee kusema tu ofisi ya Msajili huwa inapaswa kufanya kazi hiyo, jambo muhimu hapa ni kwa vyama vyenyewe vya siasa kuhakikisha kwamba vinatoa taarifa zao kwa wakati kwa Msajili ili ziweze kuingizwa kwenye record na madaftari hayo.

Mheshimiwa Spika, pia eneo lingine la tano ilikuwa ni Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kuendelea kuimarishwa lakini pia kasoro ndogondogo za usajili wa mapato, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Kamati kwamba tutaendelea kuboresha na kuhakikisha kwamba maduhuli yanakusanywa lakini pia kuboresha ofisi hii, Serikali imetenga fedha kiasi katika bajeti iliyopita kiasi cha Shilingi Bilioni 2.5 ambazo Serikali imeahidi kuzitoa katika mwezi huu wa Aprili, lakini Mkandarasi amekwishapatikana na shughuli ya ujenzi inaendelea na katika bajeti hii ya mwaka 2022/2023 Shilingi Bilioni 1.8 zimetengwa kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Spika, masuala mbalimbali yanayohusiana na masuala ya Kamati ya UKIMWI yalisemwa hapa na Kamati na yaliwasilishwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Toufiq kama ambavyo Naibu Waziri Ummy Nderiananga amejaribu kuelezea na nimpongeze sana kwa majibu mazuri, hili ni jembe langu nalitegemea sana, msimuone mkimya lakini ni mashine kubwa sana hiyo, mimi ninamuita chawa wangu wa nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri Nderiananga amejaribu kueleza vizuri niongeze kusema tu kwamba tutajitahidi sana kufanya mapitio ya Mkakati wa Nne wa Kitaifa katika kuhakikisha kwamba mapato ya mfuko huu wa UKIMWI yanakuwa ya kutabirika, kwa hiyo, tutajitahidi sana.

Mheshimiwa Spika, katika kufanya hivyo tutaendea pia na Serikali itaendelea kutoa fedha kama ilivyoahidiwa ile Shilingi Bilioni Moja ambapo mwezi Aprili itatolewa hiyo fedha lakini pia bajeti iliyotengwa kwa ajili ya magonjwa yasiyoambukiza ya Shilingi Bilioni 10.9 ndiyo fedha iliyotengwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 83, hii ni hatua kubwa ambayo itatusaidia.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine ni eneo la matumizi udhibiti wa madawa ya kulevya. Baada ya mafanikio makubwa yaliyofanywa na taasisi hii inayozuia na kudhibiti madawa ya kulevya hasa madawa ya viwandani, kimbilio kubwa la watumiaji wa madawa ya kulevya hapa nchini limeenda zaidi kwenye matumizi ya madawa yanayolimwa hapa nchini kama bangi. Hali hii ya matumizi ya bangi hapa nchini kwa kweli inatishia amani na mimi nafikiri ipo haja kila mmoja akatimiza wajibu wake.

Mheshimiwa Spika, namna ambavyo tunalichukulia jambo hili na namna ambavyo hali ilivyo huko mtaani bangi inaonekana kama ni sigara ya kawaida au ni kama ni kitu cha kawaida, wote hapa ndani wengi ni wazazi na tuna watoto wetu na jambo hili tunalijua hata kwa kuangalia ama ni kwa jirani yako ama mahala popote mnapopita katika vijiji vyetu na mitaa yetu, hali si nzuri.

Mheshimiwa Spika, ninatoa rai sisi kama viongozi pamoja na kushirikiana na taasisi iliyopewa jukumu hilo lakini viongozi wa dini, taasisi sizizo za Serikali tushirikiane katika kukomesha matumizi ya madawa ya kulevya, sio ajabu kwa kweli kwa sasa ukajikuta pengine matumizi ya madawa hayo yanafanywa pengine hata na watu wenye nafasi kubwa. Hali hii ikiendelea tutakuwa na Taifa gani kesho.

Mheshimiwa Spika, hii nimeamua leo kuzima ukimya kwa sababu kwa kiasi fulani nanaifahamu hali hii, hali sio nzuri. Nitoe rai kwa wadau wote na hasa sisi viongozi kuhakikisha kwamba tunalizungumza jambo hili hadharani. Imekuwa kama ni fashion na hasa, sasa unakuta matumizi haya yanafanywa na watoto wa kike zaidi kuliko hata watoto wa kiume, hali ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, niliona niliseme hili na hili haliwezi kupelekewa lawama kwa mtu mmoja kwanza kuna mafanikio makubwa ya kudhibiti ambayo yamefanywa na taasisi yetu, lakini wamekimbilia kwenye haya yanayolimwa ambayo yanapatikana ndani ya nchi na kwa hivyo tushirikiane katika kuhakikisha kwamba tunapelekea elimu ya madhara yanayotokana na madawa ya kulevya.

Mheshimiwa Spika, ukiwa na kijana wako anayevuta bangi leo ujue baada ya miaka 10 mpaka 15 huna mtu wa maana tena. Kwa hiyo, madhara haya ni madhara kwa familia lakini kwa madhara kwa Taifa pia. Nilidhani niseme haya kwa sababu hatuna namna na zaidi ya kusema na kuomba ushirikiano kwa wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, tarehe 23 na tarehe 24 Machi nilikwenda Geneva kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, nilipokuwa kule kabla ya mkutano na hata baada ya mkutano moja ya kati ya mambo niliyokuwa nakutana nayo na wadau wengi walikuwa katika ule mkutano ni namna walivyo na tamaa ya kufika Tanzania lakini kuona Tanzania inayoongozwa na Rais Mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata maelezo yangu ndani ya Baraza lile la Haki za Binadamu kila Mjumbe aliyesimama kuchangia juu ya Tanzania alikuwa anasifia juu ya hatua zilizochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika masuala ya kulinda haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie huko nje tunavyoonekana siyo kama tunavyojifikiria, heshima yetu imekuwa kubwa. Nami nataka niseme pengine kuongozwa na mwanamke kuna baraka zake kwa sababu mimi siyo mara ya kwanza kusafiri na kuwakilisha nchi yangu kwenye taasisi za Kimataifa, tulikuwa tukipata taabu kidogo kuelezea baadhi ya mambo lakini sasa unakuta mtu anakuelezea yeye mazuri yaliyopo Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ninataka nisema kwamba Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametupa unafuu na wepesi katika kuilezea Tanzania, pia amekuwa na bahati katika kuifanya Tanzania iwe branded kama ni Taifa la watu wastaarabu, Taifa linaloendelea na ndiyo maana hata taasisi nyingine kama Taasisi ya Africa Development Bank ambayo imetoa nishani kwake, tuzo kwa Rais wetu kwa sababu ya kusimamia ujenzi wa miundombinu, hii ni zawadi na tuzo kwa Taifa zima, Rais anapewa kama nembo tu, lakini tunasifiwa kwa sababu ya mafanikio makubwa ambayo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge pamoja na changamoto tunazozipata na tunazozipitia katika kipindi hiki cha majanga mbalimbali ya dunia, ambayo Tanzania hatupo peke yetu tusivunje umoja wetu, tusivunje mshikamano wetu, tuendelee kushirikiana, tuendelee kupendana na kuhakikisha kwamba zile changamoto tunajadiliana na kukubaliana pamoja ili tuweze kusonga mbele kwa mafanikio makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno haya, nimalizie kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu nimuahidi Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba nitatoa ushirikiano na kufanyakazi kumsaidia na kuanzia kwa wakati huu ambao ninasimama hapa ninaanza na hili la kuunga mkono hoja yako Mheshimiwa Waziri Mkuu, na ninaamini Waheshimiwa Wabunge wote watakuunga mkono Mheshimiwa Waziri Mkuu, hongera sana kwa hotuba nzuri uliyoitoa.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, Dkt. Tulia Ackson, Waheshimiwa Wabunge, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha na kutuongoza katika kusimamia mjadala wa Bunge wakati wa hoja ya Bajeti Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao na hasa Kamati ambayo inaongozwa na watu mahiri sana Dkt. Mhagama pamoja na Makamu wake. Kwa kweli Kamati hii imetusimamia vizuri na hata kufikia hatua kwa kweli Kamati inastahili sifa kwa sababu tumetumia nao muda mwingi lakini pia wamekuwa watu wema sana katika kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya yote yamefanyika kwa sababu wachangiaji wote wamejikita katika kutuwezesha kutekeleza majukumu tuliyokasimiwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sambamba na kutatua changamoto za waajiri, watumishi wa umma na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu na tumesikia katika michango ya Waheshimiwa Wabunge waliyowengi hakuna ambaye hakumpongeza Mheshimiwa Rais. Tunawashukuru sana kwa pongezi zenu kwa Mheshimiwa Rais na tutazifikisha salamu hizi ingawa alikuwa anasikia. Bila shaka sote tunafahamu dunia ipo katika mazingira magumu sana kutokana na majanga mbalimbali, lakini nchi yetu iko salama salimini. Iko salama kiuchumi, kijamii, kiulinzi na iko salama kidemokrasia na ndiyo maana nchi imetulia chini ya Uongozi wa Mama yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, michango iliyosemwa hapa mingi pamoja na Kamati kuwa imekuwa na mchango wa uongozi, lakini ni kama imejirudia kwenye maeneo yaleyale yaliyosemwa na Kamati, tukiichukua michango yote. Wachangiaji waliyochangia kwa kuongea ni 25 na waliyochangia kwa kuandika ni wawili uki–group michango hiyo yote unaikuta imejikita katika maeneo takribani 15.

Mheshimiwa Spika, maeneo haya 15 ni haya yafuatayo na kwa sababu ya muda pengine nisipate fursa ya kuweza kuyamaliza lakini michango hii ilikuwa ni mizito, ni muhimu kwa Taifa letu, ni muhimu kwa umoja wa Taifa, ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu, lakini pia ni muhimu kwa ustawi wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa maneno ya dakika 20 sidhani kama naweza nikatosheleza sana, lakini nitajaribu hata hivyo kupitia baadhi ya maeneo kwa haraka ili angalau iweze kuwasaidia Waheshimiwa Wabunge kuweza kutupitishia bajeti. Tukishapitisha bajeti maana yake siyo kwamba tumefika mwisho wa kuwasikiliza, tutaendelea kuwasikiliza na kuboresha eneo hili.

Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu masuala ya ajira kwa utumishi wa umma ni mhimili muhimu sana katika usalama wa nchi. Watumishi wa UMMA NA UTUMISHI WA UMMA kwa ujumla ni rasilimali muhimu sana katika maendeleo na mshikamano na umoja wa Taifa lolote lile. Mathalani ili kuweza kuajiri watu wanaotosha, ili kuweza kuwalipa mishahara watumishi wakaridhika kabisa, kabisa, hakuna nchi imefikia kiwango cha asilimia 100. Katika kila nchi yako madai, watu wanadai kwa viwango tofauti na pengine nchi yetu inaweza ikawa imefikia hatua nzuri sana katika kuutunza na kuusimamia utumishi wa umma tofauti hata na nchi nyingi zinazotuzunguka. (MakofI)

Mheshimiwa Spika, mnasikia wenyewe baadhi ya nchi sasa hivi hata kulipa mishahara ni tatizo, lakini sisi wananchi wetu wanalipwa mishahara. Kama mishahara kulipa ni tatizo utazungumzia ajira mpya? Siyo rahisi kuzungumzia ajira mpya. Kama kulipa mishahara ya watumishi siyo rahisi, utasimamia utendaji wa kazi? Siyo rahisi kuusimamia utendaji wa kazi. Kwa hiyo, tujivunie na tujipongeze kwamba mpaka sasa pamoja na changamoto za kidunia na majanga mbalimbali, Taifa letu na nchi yetu iko salama na tunaenda vizuri. (MakofI)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema nitoe mfano tu, mishahara lazima iendane na pato la Taifa, haipangwi tu, lazima unapoipanga mishahara iendane na mapato ya ndani ya nchi yetu na uwezo wa uchumi. Tunaweza tukalipana tunavyotaka, liko Taifa moja duniani siwezi kulisema hapa, limewahi kuamua kupanga mishahara kadri ya maneno, wakaachana na uhalisia, Taifa lilianguka na mpaka leo Taifa hilo halijawahi kusimama, liko America huko. Halijawahi kusimama pamoja na u–giant wake kwa sababu walikosea tu kwa kipindi cha makubaliano ya hela, baadaye kutoka kule ikawa ni ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mathalani kwa mwaka 2020/2021, Bajeti ya Mishahara ilikuwa ni trilioni 7.7, wakati mapato ya ndani yalikuwa ni trilioni 24, hii ni sawa sawa na asilimia 32. Mwaka 2021/2022, Mishahara ilikuwa ni trilioni 8.1, wakati mapato ya ndani yalikuwa ni trilioni 26.3. Mwaka 2022 Mishahara ilikuwa ni trilioni 9.8 na pato la Taifa lilikuwa ni trilioni 28, sawa sawa na asilimia 34. Sasa hivi kwa Bajeti ya 2023/2024 tutakwenda trilioni 10.8 wakati mapato ya ndani ni trilioni 31, tayari asilimia 35.

Mheshimiwa Spika, kuna standards za Kimataifa, uki – break hiyo ni lazima utaingia kwenye crisis ya uchumi. Maslahi haya tunayopigia kelele, walipwe vizuri, wafanywe nini watu hawa hawazidi milioni moja, ni laki tano na sitini plus. Sasa tukitaka hawa wapate sana maana yake tusimamishe miradi mikubwa ya maendeleo. Tunazungumzia idadi ya watu chini ya milioni moja, chini ya Watanzania walio sasa karibu milioni 62. Sasa hapa tunazungumza maslahi ya watu hawa tu, ingawa wanafamilia zao, lakini tunazungumzia maslahi ya hawa watumishi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuwe makini tunapotaka kuzungumzia maslahi, tuangalie pia na miradi na mambo mengine ambayo yatabeba uchumi huu ili kujenga uchumi na baadaye tuje tumalize haya yabebe na maslahi ya watumishi. Kwa hiyo hatuwezi kwenda kwenye perfections a hundred percent, lakini tumejitahidi na tuko vizuri kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliona nianze hapa ili tuwekana vizuri, tunaweza tukadai chochote kile tukasema chochote kile, lakini tufahamu kwamba lazima tuendane na uwezo wa uchumi wetu katika kuweka maslahi ya watumishi wetu.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili lililozungumzwa ni nafasi za kazi kugawanywa katika halmashauri ili kuwe na usawa katika kuajiri watumishi wa umma. Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la Mwaka 2008, kifungu cha 4(2) inatamka kuwa ajira zinatakiwa kuwa za ushindani na zifanyike kwa kuzingingatia miundo ya kiutumishi (Schemes of Services).

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge hapa wamezungumza kwa hisia kubwa sana kwamba tugawane kwa sababu hatuoni uhalisia, hazigawanywi sawasawa. Hata hivyo, nataka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, kwamba huko nyuma hatukuwa na Sekretarieti ya Ajira na tatizo lilikuwa kubwa kuliko hili la leo. Ni bora leo tumeweka Sekretarieti ya Utumishi wa Ajira na kuweka ajira zetu ziwe centralized, tunaweza tukaona hata hayo mapungufu.

Mheshimiwa Spika, huko nyuma tulikokuwa hata hayo mapungufu kuyaona ilikuwa ni vigumu. Tunafahamu zilikuwepo baadhi ya taasisi ambazo ulikuwa unakuta watu wa ukanda fulani, watu wa maeneo fulani ndiyo wameajiriwa pale, leo kuna hata afadhali unaweza ukasema Hapana, mbona kwangu sijaona, mbona kwangu sijaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo msukumo wa haya yote na tulipofika pamoja na pengine mapungufu ya mfumo ulioko sasa, lakini tumefika hapa kwa sababu wanaomaliza katika vyuo na kutegemea kuajiriwa na Serikali ni wengi kuliko nafasi zilizopo. Nilikuwa naongea na Waziri wa Elimu tunavyo Vyuo vya Ualimu mathani 35 vya Serikali, weka na vya binafsi tuchukulie kila chuo wakamaliza wanafunzi 200 tu katika hivyo vyuo 35, tutakuwa na wahitimu wangapi? Watakuwa karibu 7,000.

Mheshimiwa Spika, hapa hatujaweka na vyuo binafsi, so in average tuna wahitimu wa nafasi za Ualimu kwa ngazi tofauti tofauti karibu 15,000 kila mwaka. Ajira za Walimu zinazotoka mathalani zilizotoka kwa mwaka 2022/2023 ni 13,000, tayari wahitimu wamezidi idadi ya nafasi zilizopo. Kwa hiyo kumbe kuna makosa ambayo tuli–over plan na mkumbuke kwa nini Walimu?

Mheshimiwa Spika, Walimu wamekuwa wengi kwa sababu tulikuwa na uhaba wa Walimu wakati tulifungua shule nyingi, shule za kata ambazo zikahitaji Walimu, tukakosa Walimu, ndiyo tukaja na vodafasta, we had no Teachers. Tuliposema hivyo vyuo vikafunguka, kila mtu anajua huku ndiyo kwenye mikopo, kwenye nini? Ndiyo sababu tukapeleka wanafunzi wengi na fursa zikafunguka pale, sasa tumewa–over training Walimu. Kwa hiyo kuna haja ya kufanya u–turn na kupunguza. Sasa hili ni jambo ambalo sekta na yenyewe watatusaidia katika kufanya hayo.

Mheshimiwa Spika, sasa hili siyo jambo la kiutumishi peke yake, lakini jambo ni kwamba tuna walimu wengi lakini nafasi ni kidogo, kwa hiyo ugomvi huu wote na mivutano hii yote inatokana na sababu hiyo. Niseme tu kwa sababu ya nafasi ndogo tutajitahidi, ni bora tukabaki katika mfumo uliopo tukauboresha kwa kutumia mawazo haya mlioyasema, kuliko tukazichukua hizi nafasi mkasema tugawane. Nilikuwa naangalia kwenye group letu la party caucus tukigawana tutapata kila mmoja 112, haya nipeni mimi nichukue 112 niende nazo kwenye Jimbo langu la Kibakwe, nikifika nazo tu pale Kibakwe kila mmoja anajua Mbunge ndiyo anaetoa hizi ajira, wanakuja kujaa kwangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nikishapewa hizo ajira 112 ambazo mmenigawia za Jimbo la Kibakwe, Mfuko wa Jimbo wenyewe mnajua Madiwani tunavyohangaishana nao, kwa hiyo Madiwani na wenyewe watasema tugawane, kama ni 112, unapata 20 haya tugawane kila mmoja kila Diwani anapata Watatu, ikifika kule Diwani nae ataambiwa Mwenyekiti wa Kijiji atasema tugawane, automatically zitakuwa hazitoshi na tutaleta crisis na ugomvi zaidi, isipokuwa tunachoweza kufanya ambacho tunafikiria kwenda kufanya ni kutumia mawazo haya ya kuhakikisha kwamba waajiriwa wa nchi hii wanatoka maeneo yote kwa sababu utumishi huu ni utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnakumbuka Waheshimiwa Wabunge, tunayo Majimbo yetu na tumekuwa tukiomba vibali vya Halmashauri kupata ajira na tumekuwa tukipewa zile ajira 15, 16 za wale Watendaji wa Vijiji na nini na nini. Niambieni nani, zimebaki katika Jimbo lake zote? Zikifika kule Mkuu wa Wilaya anataka Ndugu yake awepo, Mkuu wa Wilaya anatoka Kibakwe? Afisa Utumishi hatoki Kibakwe, anataka ndugu yake awemo, DSO anataka ndugu yake awemo, Mkurugenzi anataka ndugu yake awemo, Afisa Mipango anataka ndugu yake awemo. Hawa wote hawatakuwa wametoka Nkasi, hawa wote watakuwa wamekuja na vyeo vyao na wao watakuwa ndiyo wanakaa kwenye ile panel na ndiyo wenye nguvu, wanazichukua zile zote matokeo yake wa pale Nkasi, wa pale sijui Peramiho hapati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hilo lenyewe tuko kule sisi limetushinda. Tukisema tuchukue zile ndiyo kabisa! Kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wazo ni zuri, acheni tukae tutulie. Suala la Utumishi wa Umma ni suala la usalama wa nchi. Nchi hii imewekwa katika misingi mizuri sana na haya mambo yanayochipuka ni ya mtu mmoja mmoja lakini kuna ukweli kwa maneno haya mnayosema ninyi Viongozi mnaowakilisha watu kwamba kuna upendeleo tunaona kuna harufu, hawezi akawa mtu mzima hapa nikasema haupo haiwezekani! Yako maeneo upendeleo upo na yapo maeneo yako vizuri, lakini lazima turekebishe na kurekebisha kwenyewe hatuwezi kuvunja kitu ambacho kipo kizuri, tukaanzisha ambacho hatukijui hatma yake.

Mheshimiwa Spika, nakubaliana tutachukua mawazo haya, will make a system ambayo hata katika uombaji tu pale tuta–control. Hebu waombe wenye address inayojulikana kama anatoka Dodoma Mjini au maeneo haya hatuzungumzii makabila sisi tunazungumzia originality ya mtu alikosomea na wazazi wake na alikozaliwa, hilo linawezekana kufanyika na zikapatikana katika mtandao na msambazo ambao upo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetengeneza mifumo, bajeti hii ya safari hii ni bajeti ya mifumo. Tunataka kuimarisha nguvu ya mifumo. Kuna mifumo mipya iliyojengwa zaidi ya 15. Mifumo hii itatusaidia sana katika kudhibiti. Nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kusimamia na kuanzisha mifumo hii ambayo mingi yake bado hatujaanza kuitekeleza kwa asilimia 100, lakini ipo mifumo mipya.

Mheshimiwa Spika, ipo mifumo ambayo itatusaidia katika kusimamia utendaji kazi wa watumishi, iko mifumo itakayotusaidia katika kuhakikisha mtumishi mmoja mmoja yuko wapi na anafanya nini, iko mifumo ambayo itatusaidia suala la ulipaji wa mishahara na taarifa za kila mtumishi na uki-press mimi nilifanyiwa majaribio na nimeweza kuona just press in real time you get wherever you want, wapi kuna upungufu wapi kunaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tunaupungufu wa walimu wa hesabu, masomo ya sayansi 11,336. Ajira zilizotoka za Walimu ni 13,000. Ukitaka hapa ugombane hapa na Waheshimiwa Wabunge useme tunaajiri walimu wa masomo ya sayansi tu, hapa watu wao wana masomo ya arts, nini na nini utasikia vurugu, hata huko kwenye maofisi ni vurugu. Wanaanza tuweke kidogo, lakini kimsingi tunao walimu wa masomo ya arts wengi wamepitiliza hatuna hata pa kuwaweka. Tulio na shida nao ni hawa wa masomo ya sayansi, Chemistry, Physics, Biology na Hesabu.

Mheshimiwa Spika, tuchukue basi haya tuamue hapa, tuchukue zote hizi tuseme tunawapa walimu wa hesabu kupunguza gap, utasikia tu. Kwa hiyo, nasema Waheshimiwa Wabunge tuachieni tutafakari Serikali hii ni Serikali yenu. Ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na Bunge hili hauishii kwenye kupitisha mafungu tu ya bajeti hii, uendelee hata nje ya hapa na nina wakaribisha na Mheshimiwa Spika nimechukua maoni yako, lazima tulete semina, kwa sababu moja kati ya misingi ya utawala bora ni uwazi. Moja kati ya misingi muhimu ya utawala bora ni uwazi. Hatutaficha chochote tutaleta hata mifumo ambayo bado hatujaimalizia kwa ajili ya majaribio tuje tufanye semina na Waheshimiwa Wabunge waone hali halisi ilivyo ili wakitushauri tushauriane vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo ni mengi lakini muda ni mdogo hata hivyo yamesemwa maeneo mengi sana. Ucheleweshaji wa uwasilishwaji wa michango ya katika Mifuko ya Jamii wastaafu, hili tutaendelea kulisimamia. Tumetengeneza mifumo ambayo itahakikisha ina - link na PSSSF na mishahara ambapo mfumo huo wenyewe ukiubonyeza tu hivi hakuna mtu anayeweza akafanya chochote hata yule wa PSSSF anaweza asifanye chochote mpaka mwajiri atoe mchango wake na muajiriwa naye atoe mchango wake iingie kwa pamoja. Haipokewi tofauti tofauti. Kwa hiyo, hiyo itafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine lililozungumzwa ni watumishi wa umma kukaimu nafasi za uongozi kwa muda mrefu. Hili tatizo linawezekanika ni la kiutendaji tu, ni very administrative tutaliwekea utaratibu ambao tutahakikisha kwamba na lenyewe hili linakwisha. Watu wanakaimu muda mrefu na wakati wengine wana sifa. Watu wanakaimishwa wakati hawana sifa na watu wanazulumiwa wenye sifa kuingia. Kwa hiyo, kote kuna matatizo. Mtu anakaimu na sheria inasema kukaimu mwisho ni miezi Sita, lakini mtu anakaimu miaka 10. Sasa huyo ni Kaimu huyo si tayari tu na wakati huo ukimleta mwingine unaleta ugomvi na conflicts kubwa sana ambazo zinapelekea. Kwa hiyo, nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kwamba eneo hili tunalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matumizi ya kanzidata katika kuajili watumishi wapya ili kupunguza gharama za Serikali. Yes, haya mawazo yalikuwa ni ya Waheshimiwa Wabunge ya bajeti iliyopita na Mheshimiwa Jenista Mhagama aliyachukua na wamekwenda kutekeleza, kanzidata ipo hawarudii tena kufanya interview na sasa tukaongeza mpaka na muda wa kukaa kwenye kanzidata kufika mwaka mmoja, ile system inafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, mimi niliambiwa na Waheshimiwa Wabunge nisaidie kuna kijana wangu alifanya interview na nini na nini, nimeshangaa jana ananishukuru. Ananishukuru nini? Anasema amepata ajira, kumbe wali- upload jana, walitoa jana, wametoa. Sikufanya mimi ila nashangaa nashukuriwa na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi na ninyi kuna watu wanawashukuru lakini hamkufanya chochote. Ni system ya Sekretarieti ya Ajira inafanya kazi katika merits kwa uwazi na kwa ukweli. Kwa hiyo, hili jambo limefanikiwa ni mawazo yenu. Amini Serikali, muamini kwamba kuna watu wakweli, ingawa kama kuna wazembe ni wachache wanaotupotosha.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine lilikuwa ni usaili unaoendeshwa kufanyika ngazi ya Kanda badala ya Dodoma ikijumuisha matumizi ya TEHAMA. Mfumo upo tayari, tumetengeneza mfumo unaitwa online aptitude testing system ambao huu mfumo sasa watafanya usaili hukohuko kwenye Kanda wala hakuna sababu ya kuja Dodoma. Watafanya kwenye Mikoa watafanya kwenye Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo jingine ni kuajiri kwa kigezo cha miaka, kwa Jeshi USU, hili tutajaribu kuwasiliana na Wizara ya Kisekta, tuweze kuona changamoto inatokana na nini je, ni lazima kweli kuangalia umri kwa sababu miaka ya 28 mtu akifanya kazi miaka 30 atakuwa na miaka mingapi? Tuangalie tutawasiliana na Wizara ya Kisekta.

Mheshimiwa Spika, pia kuhusu ajira za kujitolea. Ni kweli kulikuwa hakujawekwa utaratibu mahsusi kwa ajili ya ajira za kujitolea. Ziko nchi ambazo ajira za kujitolea volunteers ndizo zinazoendesha na zinazosaidia na ku – supplement gap ya Watumishi wa Umma. Kwa nini sisi tukiwa tuna watu wengi na tume-train sisi wenyewe kwa hela za Serikali, watu wana ujuzi badala ya kumkuta mtu anafundisha na anapenda kufundisha unamkuta anaendesha bodaboda. This is not right!

Mheshimiwa Spika, nadhani tukubaliane Waheshimiwa Wabunge na sisi Serikali tunachukua mawazo haya ni lazima tukatengeneze mfumo mahsusi utakao angalia pia hata wanachostahili hicho kidogo, kwa sababu huyu mtu hawezi kujitolea asipate kitu kabisa hataweza kwenda. Anahitaji kufua, anahitaji usafiri. Lazima kuwe kuna utaratibu ambao tuuweke ikibidi hata kutenga bajeti kidogo tutenge tuseme tunahitaji wangapi wa afya, wangapi wa elimu halafu waweze kupata na wafanye kazi huku wakingojea kuajiriwa. Unakuta hawa walioajiriwa pengine hata siyo wazuri sana kuliko hawa wanaojitolea. Inauma wakati mwingine unapokuta haya yanatokea, hili tumelichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, urejeshaji wa michango ya watumishi walioondolewa kazini wa kubainisha kuwa na vyeti vya kugushi. Mpaka sasa hivi madai 11,896 yenye jumla ya Shilingi Bilioni 35.02 yamelipwa kati ya madai 12,662. Waheshimiwa Viongozi wenzangu, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Serikali hii inaongozwa na Mama huyu ana huruma sana, jambo hili lilikuwa limekwisha, kukubali kutoa Bilioni 35 ni huruma ya Mheshimiwa Rais. Alisema wapeni fedha zao kwa sababu walifanya kazi lakini jambo lilikuwa limeisha.

Mheshimiwa Spika, katika muda wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu, mambo mengi ya kiutumishi yaliyokuwa yanapigiwa kelele yametatuliwa. Kwa upande wa Watumishi na Vyama vyao vya Watumishi wenyewe huko wanaimba tu ‘iyena iyena’ ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu, haya mengine tunayoyasema huku wala huko hayapo kwa sababu wamefanyiwa mambo ambayo hawakuyatarajia. Kweli kabisa tuwe wakweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ni nyongeza ya mishahara imefanyika, kama ni malimbikizo yamelipwa, hakuna ambacho hakijaguswa niwaambie ukweli Waheshimiwa. Sasa nyingine ni kurudisha posho ya kufundisha teaching allowance. Teaching allowance hii iliingizwa kwenye mishahara kwa sababu ilikuwa haina impact katika mafao. Kwa hiyo, ikaamuliwa na wahusika wenyewe Walimu kwamba hii posho mnayotupa hai - effect positively mafao yetu. Kwa hiyo, utaratibu ikaonekana basi kuwasaidia angalau wawe na kitita angalau kizuri iingizwe kule kenye mshahara. Imeingizwa tushasahau sasa tunakuja kudai tena. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge wacha tukatafakari, tuwaulize na wenyewe maana hapa kuna walimu mliostaafu, Walimu wenyewe wako kule nje, ninyi mmekuja kuwasemea. Tumewasikia mmewasemea, lakini tukawaulize na wao mnasemaje tunyofoe huku tuwaletee huku au tuiache huku isaidie kwenye mafao? Watasema wao kwa sababu wana vyama vyao.

Mheshimiwa Spika, waraka wa mwaka 2014 kuhusu viwango vya mshahara, posho wa viongozi wa elimu unaotekelezwa kwa Wakuu wa Shule lakini hautekelezwi kwa Wadhibiti Ubora. Wadhibiti Ubora kulikuwa kuna mkanganyiko wa viwango, mkanganyiko wa viwango ikaonekana huu waraka ukasitishwa na Wizara ya Elimu tutawasiliana na Wizara ya kisekta ambao hawa wadhibiti ubora wako kwao, kwamba baada ya kusitisha wamekuja na solution gani na kwenye hotuba yao wanaweza wakaja kuisema vizuri.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuhamisha umiliki wa ndege za Wakala wa Serikali TGFA kwenda Kampuni ya Ndege ya Tanzania. Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Viongozi wenzangu kulikuwa kuna sababu za msingi sana za kiusalama pia usalama wa rasilimali hizi za Watanzania. Pengine mawazo yale na sababu zile zinaweza zikawa zimepitwa na wakati na pengine wazo hili la kuzifanya ndege hizi zimilikiwe sasa na ATCL kwa sababu ni shirika la Kiserikali, TGFA ni wakala wa Serikali, ATCL ni Wakala wa Serikali. Mimi sioni kama kuna tatizo just give us time. Tuje tuangalie zile sababu ambazo siyo rahisi kuzisema, tukaangalie tuweze kufanya hilo kwa sababu limesemwa bajeti iliyopita na limesemwa na bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhakikisha kwamba vyuo vinatoa kozi ambazo zinaendana na soko la ajira hili nimelisema, Wizara ya Elimu sasa hivi ipo kwenye mchakato wa kubadilisha mitaala na nini, lazima tuangalie pia na demands yetu. Waheshimiwa Wabunge haya yataisha tukiwa na Tume ya Mipango. Waheshimiwa Wabunge Tume ya Mipango inakuja waraka umeshatayarishwa mimi nimekwishapitisha nangojea kwenda Baraza la Mawaziri likipitishwa wakati wowote naingia nao pale kwenda kuleta iwepo hapa na ipitishwe ndani ya Bunge hili kama Spika ataruhusu na kutoa nafasi.

Mheshimiwa Spika, tuwe na Tume ya Mipango that is why are training teachers bila kujua mahitaji yetu na hata tukijua mahitaji hatuweki conditions za kujua tunahitaji nini na nini, lakini pia hata katika sekta nyingine na ndiyo maana human capital is a very basic resource katika nchi, bado inakuwa hatuijui sawa sawa kwamba tunataka nini hatutaki nini, ndiyo maana tunahitaji reform kubwa na reform basically itafanywa na mifumo ya kidigitali na artificial intelligence, lazima tufike hatua hata usaili na nini tuweke maswali pale mtu afanye asahishiwe siyo na binadamu na awe selected na artificial intelligence, badala ya kufanywa na binadamu kwa sababu huku tunatuhumiana. Kwa hiyo hili wala halina tatizo, tutahakikisha kwamba vyuo vinatoa kozi ambazo kwa kweli zina uhitaji wa watu na vile ambavyo vimehama kwenye malengo yake ya msingi vinarudi katika malengo ya msingi.

Mheshimiwa Spika, eneo la 15 ni Sera, Sheria na Taratibu na Nyaraka za Utumishi wa Umma kupitiwa kwa wakati. Mapitio yanafanyika, tutaendelea kupitia maeneo haya na kuhakikisha kwamba tunaleta mabadiliko ili reforms hizi ziendane kwanza tubadilishe sera, tubadilishe sheria na mimi nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge katika muda ambao kama Mheshimiwa Rais ataendelea kuniacha nikabaki katika Wizara hii, ambacho na mimi ninachotaka kuacha kama legacy ni kuhakikisha kabisa tunaubadilisha mfumo wa utumishi wa umma, njia pekee tayari msingi umekwishawekwa na Waziri aliyenitangulia kuhusu mifumo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la 16 na la mwisho ni kusimamia na kutoa mafunzo maalum kwa Watumishi wa Umma ili kuwezesha utendaji kazi unaozingatia weledi na ustadi. Mafunzo yanatolewa sana lakini tunaotoa mafunzo tunaelewana? Mafunzo yanatolewa sana, kila bajeti hapo kila mliyopitisha kwenye mafungu yenu kuna mafunzo, kuna kujenga uwezo, kuna kufanya nini, lakini tufike hatua sasa tuwe na a committed public service, a committed one na mtu ajue miiko na vitu ambavyo haviruhusiwi katika utumishi wa umma. Tusichanganye utumishi wa umma. Kama unataka kuwa tajiri nenda kafanye kazi kwenye private sector. Kwenye utumishi wa umma hauji kutafuta utajiri unakuja kutoa service ni wito. Tusichanganye kabisa (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mawazo mengine ya kufikiria tunaweza tukaufanya utumishi wa umma ukawa kama udalali wa kuuza vitu fulani fulani sokoni, haiwezekani! Lazima utumishi wa umma uwe na miiko na mtu ajiulize niingie au nisiingie? Lazima uwekwe ugumu fulani wa utumishi wa umma. Huwezi ukamfanya kila mtu akawa Sheikh, huwezi ukamfanya kila mtu akawa Mchungaji. Ni lazima kuwe kuna sababu ambayo inakufanya wewe uwe mtumishi wa umma. Sasa hizo ndiyo lazima tufike huko, siyo kila mtu ni mtumishi tu wa umma.

Mheshimiwa Spika, yapo maeneo ambayo lazima tulazimishe watu kuyasomea. Leo hii kuna baadhi ya maeneo tumekosa watumishi kabisa, hili siyo jambo la ajabu hata Marekani best brain huwa wanazi- retain siyo kwamba wao hawana watu ila wanajua this is the best brain na hapa kwenye eneo hili ni gumu. Ndiyo maana nendeni Marekani, nendeni wapi, nendeni kokote huko mtakuta Watanzania Wabobezi ndiyo wanaofundisha kwenye Vyuo Vikuu, ndiyo wanaoendeha taasisi muhimu kule, ni kwa sababu watu wana retain best brain, kwa sababu duniani kuzidiana akili ni kitu cha kawaida.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutasimama na hayo na tuta-train watu wetu, wako watu wengine watasoma hata kama hawataki. Tukijua una akili utasomeshwa hiki ili uje ufanye kwa lazima, wamekuwa wakifanya hivyo hata Awamu zilizopita. Mwalimu Nyerere alifanya hivyo, Awamu ya Pili ya Ali Hassan Mwinyi imefanya hivyo, Awamu ya Tatu imefanya hivyo, Awamu ya Nne ya Kikwete imefanya hivyo. Kuna watu lazima walazimishwe kusoma! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Chamuriho huyu alilazimishwa kusoma, tena hayo masomo aliyoyasomea hayakuwa yake, akaambiwa utasoma hiki unachoambiwa kusoma, leo hii kwenye nchi ukitafuta watu walio na ubobezi katika eneo la usimamizi wa miradi ya kiinjinia huwezi kumuacha Mheshimiwa Chamuriho, lakini do we have them in the University of Dar es Salaam or other Universities? Will you find other genius? Bado tunatakiwa kulazimisha watu wetu katika kujenga mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na watu ambao wanaweza ku-deliver na kusimamia kama nchi ili tuweze kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nirudie tu kusema nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kusema kwa kuandika na wale ambao hawakusema kwa sababu niliziona hisia zao, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge yote mliyoyasema hapa, yote kabisa tunayachukua kwa uzito mkubwa sana na tuhakikishe kwamba nchi yetu inapata maendeleo na ustawi, kwa sababu rasilimali muhimu ni watu, kuhakikisha wanafanya kazi na uaminifu na uadilifu.

Mheshimiwa Spika, suala la utawala bora hakuna champion wa utawala bora kama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Nimekusikia Mheshimiwa Aida Khenani hayo ni mambo madogo, makubwa yamekwisha tatuliwa, haya madogo tunawaachia watu wa chini huku watayafanya lakini nataka nikuhakikishie Rais wetu hana ubaguzi kwa misingi ya Vyama, Rais wetu hana ubaguzi kwa misingi ya dini, wala kwa misingi ya makabila wala ukanda. Ameamua kujenga nchi moja, ameamua kujenga nchi yenye mshikamano, tuendelee kumuunga mkono na nikuhakikishie jambo hilo tutalishughulikia ili tuweze kuacha kuwa na manung’uniko ya mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika baada ya maneno haya, naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kabisa kuipongeza Serikali na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kuleta Muswada huu mzuri ambao kwa hakika unataka kuiokoa nchi hii ili isipate matatizo ambayo nchi za wenzetu zimepata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulianza Mfumo vya Vyama Vingi mwaka 1992 na kwa hiyo, kutoka 1992 mpaka sasa ni takribani miaka 27. Tumefanya chaguzi mara tano na katika chaguzi hizi tumeshuhudia mambo mengi. Tumeshuhudia watu wakiumizana, watu wakifa, watu wakimwagiwa tindikali na fujo nyingi sana. Vile vile tumeshuhudia kutokuwepo demokrasia ndani ya vyama vya siasa. Katika kipindi hiki tumeshuhudia pia rasilimali za vyama kuwa rasilimali za watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vipo vyama inawezekana likitokea la kutokea, watu wawili au watatu tu wakiondoka, wakiwa hawapo, hivyo vyama vinakosa mali kabisa kwa sababu hata hawajui ziko wapi. Katika mazingira haya na upungufu huu, bila shaka ndiyo maana Serikali ikaamua kuleta Muswada huu.

Mheshimiwa Spika, Muswada huu ni matokeo ya kujifunza kwetu mambo mengi yanayotokea. Nimewasikiliza wachangiaji waliopita na hasa rafiki yangu Mheshimiwa Zitto, amezungumza juu ya jambo la demokrasia, lakini demokrasia bila mipaka ni fujo. Demokrasia ni mfumo au utaratibu unaoweka utawala kwa uchaguzi na ukishauweka huo utawala kwa uchaguzi kuna mifumo mingi; iko constitutional democracy, iko representative democracy na iko direct democracy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, indirect democracy inakuwa kila jambo lazima mpige kura; katika representative democracy wanachaguliwa viongozi kama hivi tulivyo sisi kwa niaba ya Watanzania wengine kwa ajili ya kuamua mambo yao na kusimamia masuala ya utawala. Katika mazingira haya, mnapomaliza uchaguzi, shughuli zote za siasa zinakuja Bungeni. Zikija Bungeni huku ndiyo tumepewa mpaka na kinga ya kusema tunayotaka tuseme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawaambia pande zote mbili, kama uchaguzi umekwisha, kwa nchi maskini kama yetu ambayo bado wako watoto wanakaa chini, ambayo bado kuna matatizo watu hawapati dawa, tunataka tuendelee kulumbana na kufanya siasa wakati uchaguzi umepita, tutaendelea kuwa masikini na hatuwezi kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata aliyeshinda ana haki yake na aliyeshindwa ana haki yake. Wakati wewe umeshinda; tuchukulie Mheshimiwa Zitto umeshinda uchaguzi, unaongoza nchi, halafu sisi akina Simbachawene tunaanzisha Movement for Change, tunaanzisha Sangara, tunaanzisha operesheni, nchi haitulii, nchi inahema juu kwa juu, utaongoza vipi? Utaiongozaje hiyo nchi? Kwa hiyo, ni vigumu sana haya mambo kuya-equate unapochukulia nadharia za kidemokrasia na hali halisi ya dunia ya leo…

SPIKA: Mheshimiwa Simbachawene, bahati nzuri Mheshimiwa Zitto hawezi kuwa Rais wa Nchi, haiwezekani. Endelea tu Mheshimiwa. (Kicheko/Makofi)

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, katika mazingira hayo, hakika tunapaswa tujiulize, maana ziko nchi ambazo hazina hata vyama vingi. China kuna chama kimoja kikubwa kinafanya vizuri; na China sasa ndiyo Taifa kubwa lenye uchumi mkubwa duniani. Sasa katika mazingira haya lazima na sisi tujiulize, vyama vyetu lazima viwekewe mipaka na kurekebishwa baadhi ya mambo ili twende sawa. Ndiyo maana Serikali inaleta Muswada kama huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Msajili wa Vyama vya Siasa ndio referee na role yake ni impartial. Unapozungumzia juu ya vikundi vya ulinzi, wote tunajua humu, mbona hatutaji tu! CUF wana blue guard, CHADEMA wana red brigades, CCM wana green guard; hivi vitu ni hatari kwa Taifa. Kwa hiyo, huwezi kusema Muswada huu unapendelea upande mmoja, sheria inakata kotekote. Humu tupo Wabunge wengi wa CCM, lakini tunasema, tunaona umuhimu wa kutunza amani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako maeneo ambayo yameguswa na Muswada huu ambayo kwa kweli kabisa na hasa yanayompa nguvu ya kusimamia mchezo huu wa siasa, yanayompa nguvu Msajili kufanya kazi ya u-referee wake vizuri, ni ya muhimu sana, lakini unashangaa yanapingwa.

Mheshimiwa Spika, unasema training na capacity building za ideology; ideology ni kitu cha hatari sana. Ndicho tunachozungumza, leo hii tujiulize Janjaweed ilitokea wapi? It was ideology teachings. Janjaweed ambayo leo hii Western Sudan na Eastern Chad ni matatizo makubwa na inasambaa kote; leo hii Al-Qaeda ni tatizo la dunia, it is these teachings ambazo hazikuwa controlled ndizo zilizotufikisha hapo, ndizo zilizoifikisha dunia hapo. Kuna Mungiki, imewatesa wenzetu wa Kenya vibaya mno; lakini IS imemwondoa Gaddafi kwa kumuua kinyama kweli kweli. Wanasema wanapigania ideology ya Uislam, wakati na Gaddafi ni Muislam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siasa ina vitu vingi, ukiviachia hivi kama huvioni unakuja kulia baadaye. Hizi ideology, teachings hazikatazwi kwa mujibu wa sheria hii, tumesema zitolewe taarifa kwa Msajili watakavyofundisha na wanachotaka kufundisha halafu ataruhusu au atakataa kulingana na hali ilivyo ya hizo ideologies wanazotaka kufundisha au itikadi au vyovyote mnakavyoweza kusema. Hazijakatazwa, kuwekewa utaratibu huu tu ndiyo jambo baya! Hapana, bila shaka pengine wengine wanafikiri tuna nchi nyingine ya kwenda, lakini nchi yetu ndiyo hii hii, tusipoilinda ilivyo, hatuna pa kwenda sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanazungumzia suala la uzingatiaji wa matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Vyama vya Siasa katika kutekeleza na kufanya shughuli zetu zote za uendeshaji wa demokrasia nchini. Jambo hili ndilo limekuwa tatizo kubwa kwamba wengine wanafuata kidogo, wengine wanajitahidi, tunataka kuwe na uwanja ulio sawa. Napo hapa kuna tatizo?

Mheshimiwa Spika, vipo vyama hapa viliungana vika- form coalition, sina uhakika kwenye ugawanaji wa baadhi ya makubaliano waliyoyafanya kama wengine hawakuumizwa. Muswada huu unaweka schedule ambayo inaweka utaratibu wa makubaliano ambapo waliopata madhara ni vyama ambavyo tunajua, lakini kama mtu aliyeumia anasema yeye hajaumia, inakuwa vigumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiangalia nikiwa upande wa CCM na nikiwaangalia wenzetu, naona wao wanauhitaji zaidi Muswada huu na Sheria hii kuliko sisi, wana hali mbaya sana hawasemi. Sasa kama hivyo ndivyo na hawaoni hii, bila shaka sasa hiki kinachotaka kufanywa na sheria hii ambacho kinataka kunyanyua zaidi institutional party, badala ya chama cha mtu, wenzetu wanaiona hiyo siyo sawa, bila shaka hawajui wanachokifanya. Mimi ninavyoona angalau CCM tuna an institutional system political part, lakini si ajabu wao wanahitaji zaidi kwa kweli, kwa maoni yangu wanahitaji zaidi Sheria hii kuliko tunavyohitaji sisi CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako mambo mengi yamesemwa lakini moja kati ya masuala mengine ya msingi yanayoletwa na sheria hii, ni masuala ya vyama kuzingatia Katiba zao. Kumekuwa na tatizo la vyama kutokuzingatia Katiba na wakati huo huyo Referee aliyepewa hiyo kazi anakuwa hana uwezo, Sheria hii inampa uwezo wa kusema sasa bwana fuata Katiba yako ulisema hivi, lakini pia wameweka na nyongeza nyingine ya kwanza hapa ambayo inasema italeta basic matters for which provisions of the constitution of the parties shall contain. Hasa Katiba zitakuwa na mfumo ambao unafafana, zina mfumo ambao vitu muhimu vyote vipo na hivyo Msajili itakuwa ni rahisi sana kuvisimamia vyama hivyo na kuamua hata ugomvi ambao umeweza kutokea hapa na Msajili anashindwa kupata namna ya kufanya. Sasa nadhani kama nilivyosema vyama vingine vinahitaji zaidi Sheria hii kuliko pengine hata CCM.

Mheshimiwa Spika, Sheria hii inazungumzia kumzuia mtu asiye raia kujishughulisha na masuala ya siasa za nchini mwetu. Hivi wewe leo kweli unaweza ukatoka hapa ukaenda Marekani ukasema wewe unataka kupata haki ya kuanzisha chama, unataka kupata haki ya kufanya nini, ni ngumu mno. Sisi hatuwezi kuacha milango hii wazi na ndiyo maana Sheria hii inakuja kuuziba huu mwanya kwa sababu tunajua yanayotokea. Nami niseme tu ukicheka na nyani, utavuna mabua. Tunajua yanayotokea, tunajua ambavyo vyama hivi vinaweza vikatumika katika kuingiza watu wasio na nia njema na nchi yetu, tunapozima mianya hii ubaya wake ni nini na wameonesha kidole sana kwa upande wa CCM, lakini nasema hivi, wana haki ya kufanya hivyo kwa sababu nchi hii ikiparaganyika watakaodaiwa na Watanzania ni sisi CCM, maana ndiyo tunaoongoza nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo niwasihi na niwaombe wana CCM wenzangu tushikamane na tuhakikishe kwamba sheria hii inapita kwa sababu ya uhuru wa nchi yetu, amani ya nchi yetu na kwa sababu ya uimara wa demokrasia katika nchi yetu. Tusipofanya hivyo sisi ndiyo tutakaoulizwa kuliko mwingine yeyote yule, wenzetu wengine wanaweza wakawa wanatafuta namna ya kuingia kiurahisi, lakini sisi tunaona suala la siasa ni lingine lakini maisha ya nchi yetu, maisha ya watoto wetu na maisha ya wajukuu zetu ndiyo kitu cha maana kuliko hata mchezo wa siasa tunaocheza humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata mchezo wa mpira wenyewe una sharia, mchezo wowote duniani una sharia na taratibu zake na hata kuna kadi unapewa ya njano, baadaye unapigwa red, kwa nini? Kwenye utaratibu wa kuendesha jambo sensitive hili ambalo linatunza mhimili wa amani na utulivu wa nchi tusiliwekee utaratibu, ni jambo zuri na naunga mkono hoja, sheria hii Waheshimiwa Wajumbe na Waheshimiwa Wabunge tuipitishe kama ilivyopendekezwa kwa marekebisho ya Serikali. (Makofi)
The Fire and Rescue Force (Amendment) Bill, 2021
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niwashukuru Wabunge wote kwa michango mizuri ambayo inaboresha zaidi Muswada wetu ambao uko mbele yako. Kipekee sana ninashukuru maoni ya Kamati ambayo pamoja na yale ambayo tumeyafanya katika Kamati, pia wametueleza maeneo mengine muhimu ya kuzingatia nami niseme tu maoni ya Kamati yote ambayo wametoa katika taarifa yao tumeyapokea na tutayazingatia.

Mheshimiwa Spika, suala la elimu kama walivyosema ni kweli lazima tuendelee kutoa elimu kwa sababu majanga ya moto yanaendana sambamba na maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji. Kadri tunavyowekeza kwenye majengo marefu, kadri tunavyojielekeza kwenye majengo ya kisasa na kutumia umeme sana ndipo tunapopata majanga zaidi ya moto. Zamani huko ukisikia kibanda kimeungua shambani ni upepo ulivuma ikawa hivi basi, lakini kwa sasa ni majanga ambayo yanaambatana na hasara kubwa. Hivyo, elimu itaendelea kutolewa na tutazingatia sana maoni ya Kamati ambayo imetoa kwenye kamati lakini pia na Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa kwamba kimsingi sheria huwa hairudi nyuma sheria inaanzia pale ilipotungwa kwenda mbele na ni matakwa ya Katiba yetu.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge na wananchi wasiwe na wasiwasi kwamba baada tu ya kutungwa sheria hii basi matakwa ya marekebisho haya yataanza moja kwa moja kuanza kwenda kuwagusa hata wale ambao walijenga nyumba zao kabla ya kutungwa kwa sheria hii hapana, sheria hai-apply retrospective sheria inaanzia pale ilipotungwa kwenda mbele.

Mheshimiwa Spika, hii ni pamoja na adhabu zilizosemwa lakini ni pamoja na matakwa ya kuzingatiwa katika majenzi, hakuna nyumba itakuwa condemned kwa sababu eti haina kitu fulani na kitu fulani lakini kubwa hapa ni kwamba majanga haya ya moto yanapotokea yanasababisha hasara kubwa, kwa hiyo hata kama hauguswi na sheria hii kuanzia hapa ilipofikia lakini kwa kuwa sasa tumeleta sheria na tuna utaalamu na tumeanzisha jeshi hili kamili, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji basi ujuzi ule wa Jeshi hili utumike katika kufanya kutoa ushauri na ili kuweza kuwasaidia wadau wetu wananchi pia na wawekezaji kuhakikisha kwamba wanafanya marekebisho kwenye majengo yao hata kama siyo lazima lakini kwa kweli ushauri wetu ni huo kwamba ikitokea janga ya moto kwenye majengo tusianze kulaumiana, ooh! kwamba kwa sababu hatukuguswa na sheria basi hatuwezi kufanya marekebisho ya kuweka ving’amua moto lakini pia kuweka matakwa ya mahitaji ya ushauri ya Kikosi cha Jeshi la Zimamoto.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote waliozungumzia na hapa nimpongeze sana Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, pia Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda wamezungumza kwamba sasa Jeshi limeshakuwa Jeshi na kama limekuwa Jeshi basi liwe na tabia ya kijeshi na kwamba matukio yanapotokea tunataka tuone mabadiliko ya kwamba tumekwenda kwenye Jeshi na watu wako active. Kimsingi kuzima moto ni uwekezaji pia unatakiwa Jeshi hili tulipe vifaa tuwekeze uwekezaji mkubwa tusizungumzie tu kuzima na maji siku nyingine tuzungumzie kuzima kwa kutumia helikopta na vitu kama hivyo. Sasa haya yote yanahitaji uwekezaji na niwashukuru sana Waheshimiwa Wajumbe kwa kuliona hilo na kwa kuweza kushauri mambo ya kuzingatiwa siku za usoni.

Mheshimiwa Spika, suala la kumiliki silaha limesemwa hapa ni kweli kwamba silaha hizi tutazitungia Kanuni hazitaanza tu hivi bila kuweka Kanuni nzuri. Kwa sababu tutashangaa kweli kumuona Askari wa Zimamoto hakuna tukio la moto hakuna hatari yoyote iliyopo katika mazingira yaliyopo halafu na yeye ana bunduki ameshika hivi anatembea nayo, italeta mgongano mkubwa sana lazima tueleze katika Kanuni kwamba bunduki itatumika wakati gani, itaruhusiwa na nani, na nani anayeambatana katika tukio wakati wengine wameshika silaha za kuzima moto lazima kuwe kuna wengine ambao wana kazi ya kuwalinda hawa wanaofanya ile kazi. Kwa hiyo, siyo kwamba wote watakuwa na bunduki kunakuwa hakuna tofauti kati ya Polisi na Zimamoto, lakini silaha ya kwanza ya Askari wa Zimamoto na Uokoaji ni kuwa na zana za kufanyia kazi ya kuzima moto au kuokoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, silaha inalinda hawa wanaofanya lakini na mali zile zinazokwenda kuokolewa kwa sababu tumejifunza na kuona kwamba kunatokea uvamizi na watu wanapora vitu wakati wa matukio kama haya na Askari wetu wanakuwa wako katika eneo la tukio wanashindwa kudhibiti kwa sababu hawana vitu vinavyoweza kusababisha wananchi wakaogopa kusogea katika matukio hayo.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo limesemwa Mheshimiwa Njau amesisitiza kuhusu elimu kutolewa pia nimesahau Mheshimiwa Mohamed Haji amesisitiza vyombo hivi kufanyakazi kwa pamoja. Ni kweli hili jambo la msingi sana kama vyombo hivi vitakavyokuwa viko chini ya Wizara moja na vyote sasa vinakuwa Majeshi havitafanya kazi kwa ushirikiano basi itakuwa fujo. Kwa sababu wakati Jeshi la Zimamoto wanakwenda kuzima moto mawazo yao ni kuzima moto, ni lazima katika mawasiliano hayo hayo Jeshi la Polisi na lenyewe linatoka kuja sehemu ya tukio likija kulinda watu na mali zao, hili ni kweli lazima tuliweke vizuri katika utaratibu ili lisije likaleta mgongano. Wale wakasema bwana ninyi si mna kila kitu ninyi endeleeni tu huko nasi tunaendelea na shughuli zetu hapa! Ni kweli kabisa kwamba tutatengeneza utaratibu ambao vyombo hivi vitafanya kazi kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine limeguswa na ni hili la majengo ya mita 12, kupitisha michoro yao kwa Zimamoto ili ipate ithibati na ushauri wa kitaalam wa namna ya kujenga. Hili jambo utaliona kama ni la kawaida ukiona matatizo yanayotokea kwa mabweni kwa mfano, mtu anaamua kujenga tu bweni la shule anaweka watoto wetu mle ndani, hajapata ushauri na watoto wale wana matukio mengi ya moto yanatokea huko, kimsingi kama wangepata ushauri Jeshi la Zimamoto ndiyo lenye utaalam wa kusema katika mchoro huu mnaotaka kujenga inatakiwa kuwe kuna milango minne kwa ukubwa wa jengo hili au kuwe kuna milango mitatu, uwekwe mwingine hapa mwingine uwekwe hapa.

Mheshimiwa Spika, utakuta pia hata nyumba zetu tunazojenga unajenga mimi najifungia kule master bed room kule umeji-seal kule kabisa, umeweka kabisa hakuna hata namna ya kujiokoa hata likitokea janga, lakini pia hujaweka ving’amuzi vya moto lakini hawa wataalam wetu hawa wana ujuzi wa kushauri kwamba katika mchoro wako huu hapa unapaswa kuwa na mlango, hapa unapaswa kuwa kuna dirisha kubwa, hapa unapaswa kuweka kitu hiki kwa sababu moto ukitokea utaweza kujiokoa kwa stahili hii.

Mheshimiwa Spika, hivyo matakwa haya pamoja na kwamba tumesema ni kwa ajili ya majengo marefu kupitisha ili kupata ithibati hii na ili uweze kupata building permit vyombo hivi vitashirikiana kwa sababu vyote ni vyombo vya Serikali, nasi katika Jeshi la Zimamoto itabidi tuweke utaratibu kama mtu anataka kupitishiwa fomu zake zile apitishiweje, zifanyweje, tutaweka utaratibu ambao hautakuwa na urasimu mkubwa ili kuondoa changamoto ambayo Waheshimiwa Wabunge wana wasiwasi nayo, lakini kubwa hapa ni ule ushauri utakaotolewa na chombo hiki kwa watu wanaowekeza na kupata hasara yanapotokea majanga.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Fakharia Shomari amesema fire hydrants zipo lakini tunaelewa kwamba wananchi wengine wamejenga maeneo ambayo fire hydrants zilipaswa kuwepo na kwamba leo amesema wasije wakapata usumbufu sheria hii itakapoanza kutumika. Kama nilivyosema generally, Wabunge wengi mmezungumzia suala la elimu, elimu itaanza kwanza na baadaye kama ilivyo utaratibu sheria hii yetu inaendeshwa kwa Kanuni na huwezi kuchukua hatua yoyote ya kisheria kutokana na sheria hii ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na namna ya utendeji kazi wake kama hujampelekea kwanza notice ya kwanza kuna (a), kuna (b), na (c) ambayo ndiyo inayokuja kusema sasa hapa tunaweza tukachukua hatua. Kwa hiyo kimsingi hapa kutakuwa kuna mengi yamezungumzwa na kama mtu hajafanya kwa maksudi na alifanya bila kujua, itajulikana na kusema ukweli hawawezi wakatendewa hayo na wasiwe na wasiwasi kwa sababu kama tulivyosema sheria kimsingi haitumiki kwa kurudi nyuma kabla ilipokuwa haijatungwa.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine limezungumziwa na Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan ilikuwa ni hawa Voluntary Fire Fighters, kwenye marekebisho haya tumeweka hawa Zimamoto wa Kujitolea. Wazima moto wa kujitolea hawa wametajwa na wametambuliwa na sheria lakini eneo lingine amezungumzia juu ya renumbering ya ile clause 11(b) ni kweli alikuwa yuko sahihi, kulikuwa kuna makosa ambayo tumeyaona na Attorney General anaona namna atakavyofanya.

Mheshimiwa Vita Kawawa amezungumzia kuiongezea bajeti Jeshi la Zimamoto ili kuweza kufanyakazi yake vizuri na kwa ufanisi, hili ni kweli na wote waliosema hilo nakubaliana nao, kusema kweli ili kuweza kufanya fire hydrants hizi ziweze kufanyakazi zake vizuri lazima kushirikiana na taasisi zingine za maji lakini na taasisi za Majiji au Halmashauri kwa pamoja ndiyo tuweze kufanya vizuri na hii imesemwa hata katika sheria.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu pia amezungumzia kuwepo kwa Kanuni na Kanuni hizi zitakapotungwa basi zifanyike haraka na ziletwe Bungeni, hili tulikubaliana hata kwenye Kamati kwamba Kanuni hizi zitakapotungwa tunajaribu kushauriana ili tuweze kutengeneza Kanuni nzuri zitakazofanya sheria hii itekelezeke bila kuwa na changamoto za usumbufu lakini pia tulete ufanisi na kuepusha majanga ya moto hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa ufupi kwa kweli hayo ndiyo nimeona Waheshimiwa Wabunge wamechangia na ninawashukuru sana wote waliochangia na wengine ambao hawakuchangia na wote tunawashukuru kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninashukuru kwa michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge ambayo katika kuchangia wamegusa maeneo ambayo na sisi Wizara ya TAMISEMI ndio ambayo tunayatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ambalo nataka nitoe ufafanuzi kama sehemu ya mchango, ni suala la elimu bila malipo. Elimu bila malipo imesemwa sana na wachangiaji wengi na kwa namna ilivyokuwa inasemwa ni kama vile elimu bila malipo ni programu maalum ambayo imewekwa, ina fedha zake na kwamba sasa suala la utoaji wa elimu nchini hakuna mpango mwingine wowote ni elimu bila malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hili siyo sawa sawa lakini elimu bila malipo dhana na falsafa yake ilikuwa ni kujaribu kuondoa gharama za mapema hasa kwa wazazi na hasa wale wazazi wasiokuwa na uwezo kutakiwa kuchangia michango mingi sana ili watoto wao waweze kupata elimu. Jambo hili lilikuwa baya zaidi pale ambapo linawaweka kwenye jukumu la kwanza kabisa wale watoto wanaoandikishwa darasa la awali na darasa la kwanza, wazazi wao walipaswa kulipa kulingana na mpango uliowekwa na shule kiasi cha kuanzia shilingi 10,000 hadi shilingi 100,000. Sasa jambo hili liliwafanya wazazi wengi sana washindwe kuwaandikisha watoto wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuonesha tu namna ambavyo ongezeko la wanafunzi limekuwa kubwa kutokana na kuondolewa kwa gharama hizo ambazo sasa Serikali inazilipa, utaona kwa mfano kwa mwaka 2014 uandikishaji wa wanafunzi wa awali na darasa la kwanza ulikuwa kwa jumla yao walikuwa 915,000. Mwaka 2015 tulipoanza kuchukua gharama hii Serikali na kuzuia wazazi kutoa pesa hii ili wawaandikishe watoto, uandikishaji wa darasa la kwanza na awali walifika jumla ya 2,200,637. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 waliongezeka zaidi watoto kwa sababu wazazi wameondolewa ule mzigo na udahili wa watoto wa darasa la kwanza na darasa la awali ulifika 2,909,894. Kwa mwaka 2017 umeongezeka zaidi kwa maana ya kwamba sasa wazazi wameshaona kwamba Serikali imewapokea huu mzigo wa kulipa zile gharama za awali, udahili wa darasa la awali na darasa la kwanza kwa mwaka 2017 hadi Machi juzi tulivofunga usajili, tumeandikisha watoto 3,188,149. Kwa upande huu kwamba sasa tunampatia kila mtoto wa Tanzania elimu sasa hili tumefanikiwa, kinachobakia ni changamoto ya kuboresha tu kutoa elimu iliyo bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge waliosema kwamba hii elimu bure imesaidia na ninawapongeza sana Wabunge wanaoliona hilo. Kitendo cha Serikali kupokea mzigo huu ikiwa ni pamoja na kulipa ada kwa wanafunzi wa Sekondari, kulipa ada wale waliokuwa wanasoma shule za bweni walikuwa wanatakiwa kulipa ada shilingi 70,000 na wale wa kutwa walitakiwa kulipa ada shilingi 40,00 Serikali inazilipa hizi fedha siyo tena zinalipwa na wazazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na gharama za mitihani wa kidato cha pili ilikuwa ni shilingi 10,000 na mitihani mingine ya Taifa ya form four ilikuwa ni shilingi 50,000 gharama hizi pia Serikali imezichukua. Kwa hiyo, utaona wazazi wamepata nafuu kubwa sana pia wanafunzi wengi sasa hawafukuzwi shuleni kwa ajili ya kwenda kufuata michango hii na hawazuiliwi vyeti vyao na Baraza la Mitihani kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inagharimia kwa kutoa shilingi 10,000 kwa mtoto wa shule ya msingi na shilingi 25,000 kwa mtoto wa shule ya sekondari kwa ajili ya uendeshaji wa shule ambazo fedha hizi zinapelekwa moja kwa moja shuleni. Jambo hili limewapa faraja sana wazazi na kuondoa mzigo kwao, kwa hiyo wazazi wamebakia tu na jukumu la kuhakikisha kwamba watoto wao wanakuwa na sare na vitu vinavyowasaidia ili kujifunza ikiwa ni pamoja na madaftari, kalamu na vitu vingine vidogo vidogo pamoja na nauli kwa wale wanaokwenda shuleni na kurudi, lakini na kuhakikisha kwamba watoto wao wanakula wale ambao hawakai shule za bweni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inatoa hela ya chakula kwa ajili ya wanafunzi walio bweni. Kwa mwezi Serikali inatumia kiasi cha shilingi bilioni 20.8 kwa kila mwezi kwa ajili ya kugharamia gharama ambayo ingepaswa kulipwa na wazazi au walezi wa wanafunzi hawa. Mafanikio haya ni makubwa sana na hii nirudie kuwaomba Waheshimiwa Wabunge ambao tunafahamu kwamba bado tunalo jukumu kubwa ikiwa ni pamoja na majukumu mengine yanayohusiana na kuwasaidia watoto wetu ili waweze kupata elimu nzuri. Siyo kweli kwamba kwa sababu elimu bila malipo basi gharama zote Serikali imechukua na kila kitu ni Serikali hapana, hakuna programu hiyo, hatujawahi kupitisha mpango huo hapa, lakini jambo hili ilikuwa ni kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi wa watoto ili waweze kupata haki yao ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mafanikio haya sasa tunapata tatizo jingine na ambalo nalo limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi nalo ni suala la miundombinu katika utoaji wa elimu. Tuna upungufu mkubwa sana sasa wa madarasa na tuna upungufu mkubwa sana wa nyumba za walimu na tunao upungufu bado wa matundu ya vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwashule za msingi upungufu wa madarasa ni 119,275 na kwa sekondari upungufu wa madarasa ni 7,458 na kwa nyumba za walimu kwa shule za msingi upungufu ni nyumba 182,899 na kwa sekondari ni nyumba 69,811. Hali kadhalika tuna upungufu wa matundu kwa shule za msingi na sekondari ya vyoo. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine nchini, kuhakikisha kwamba tunaendelea kusaidiana na Serikali kama tulivyofanya siku za nyuma kwa kushiriki katika miradi iliyopangwa katika maeneo yetu kwa kushirikiana na wananchi ili tuweze kuisaidia Serikali kupunguza kazi hii/mzigo huu ambao uko mbele yetu. Hata hivyo, Serikali tunapanga bajeti kwa mfano kwa mwaka unaoisha tulipanga karibu kiasi cha shilingi bilioni 59 kwa ajili ya uimarishaji wa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naendelea kutoa rai na kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na kuwaomba wananchi wote wa Tanzania, nchi yetu inafuata siasa ya ujamaa na kujitigemea, kila mmoja analo jukumu la kuhakikisha kwamba anashiriki katika kujenga nchi yetu. Sote tunajua, miundombinu ya elimu inatusaidia siyo tu Taifa kupata wanafunzi na wananchi walioelimika pia wazazi wanafanya uwekezaji kwa sababu watoto hawa ni wa kwao. Kwa hiyo, tushirikiane na Serikali kwa sababu bado mzigo huu ni mkubwa na Serikali peke yake haiwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote ambao wanaojitolea kwa namna moja au nyingine na wadau wengine wote nawashukuru, tuendelee kushirikiana ili kupambana na upungufu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ahotuba yake nzuri sana na niwapongeze pia Mawaziri Mheshimiwa Jenista na wasaidizi wake wanafanya kazi nzuri sana tunawaona na tunawatia moyo endeleeni hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote ile duniani inaongozwa kwa dira na kwa sisi Tanzania dira yetu ni ya 2025 na kwa sasa tunatekeleza dira ya miaka mitano na katika miaka mitano tumekuwa tukitoa hapo kila mwaka tunatoa kipande na tunatekeleza. Kwa sasa tuna Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2018/2019, nichukue nafasi hii kupongeza sana, nimeona orodha ya miradi ya kimkakati. Niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kwamba, miradi hii kwa kweli, iko barabarani na iko sambamba kabisa na vision yetu ya 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kokote kule na hasa kwenye nchi ambazo zimeendelea na zilizopata uhuru karibia na sisi Tanzania, nyingi sana zimepiga hatua na shabaha zao kufikiwa kwa sababu ya maamuzi ya dhati. Sisi hapa udhati wetu wa maamuzi, napata mashaka. Wakati standard gauge leo inajengwa wengine wanasema hiyo haina umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunajenga barabara na miundombinu inayounganisha, hapa tulikuwa hatuna barabara kwa mfano ya kutoka Iringa kupitia Dodoma kwenda mpaka Babati sasa tunaungana na Arusha; na hiyo nayo haina maana, lakini watu wanapita humo humo haina maana. Wakati wanafunzi wanalipiwa gharama kubwa sana na Serikali karibu kila mwezi shilingi bilioni 22 na ushee hilo nalo linaonekana halina maana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sidhani kama ni sahihi sana kwa sababu kama tutasema kila jambo tunabeza, kila jambo jema linabezwa, basi maana yake ni kwamba hatujui tunakokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, rai yangu Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba, hebu wakati mwingine tuzungumze kama Watanzania na pengine masuala haya ya dira yafundishwe hata kwenye shule za msingi, kwenye sekondari, kwenye vyuo vikuu yafundishwe kwa sababu hata ukimwambia Mtanzania hapa anayemaliza degree ya chuo kikuu kwamba hivi dira yetu sisi mpaka tunapofika mwaka 2025 tunataka tuwe tumefika wapi, unaposema suala la uchumi wa kati wengine hatuelewani, ama kwa makusudi, lakini nadhani iko haja ya kusisitiza watu kupata elimu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi ambazo zimepiga hatua kwa shabaha zao walizoziweka hazikuwa legelege na kuwa na mawazo ambayo yanasigana kama sisi. Wakati jambo zuri ndege zinashuka hapa, ndege tatu zimefika tunasubiri hizo mbili zije, tayari wameanza kusema ndege ni za nini? Sasa unashindwa kuelewa hivi wanajua tunakokwenda? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kujenga uchumi bila kuwa na national carrier, uchumi wa kisasa unajengwa kwa njia za usafirishaji. Kwa hiyo, nisihi sana kwamba, si ajabu hata humu Wabunge wengine wenzetu hawajui tunakwenda wapi na ndio maana wanavuta kamba tunakotaka kuelekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisihi kwamba kama tunataka kuwa Japan, kama tunataka kuwa kama China, ni lazima tuweke dira. Wenzetu Wachina juzi wameamua kuwa na Rais wao wa maisha. Uamuzi ule usifikiri ni wa kitoto ni uamuzi wa watu waliofikiri sana. Wameona kwamba Xi Jinping amekuja na ku-address kwa hotuba zake tatu tu. Ameeleza msingi wa vision yao wanayoitaka. Na sisi leo tunaye Magufuli ambaye anatupeleka kwa vitendo kwa kuangalia tunataka kuelekea wapi, lakini wako watu wanabeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Xi Jinping kwa hotuba tatu analibadilisha Taifa lenye watu wengi duniani la China, kumwamini kwamba anastahili kuwa Rais wa maisha, lakini sisi Magufuli anayetenda haya tunayoyaona makubwa tunasema hatuelewi anataka kutupeleka wapi. Kwa hiyo, niseme tu rai yangu, Mheshimiwa Waziri Mkuu nchi hii ni yetu wote ni Watanzania, lakini pale yanapofanyika mambo mazuri ni lazima wote tuunge mkono kama Watanzania tusikatishane tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnafanya kazi nzuri na kubwa sana, mnafanya kazi ya kujitolea kweli kweli lazima tuwapongeze. Mheshimiwa Waziri Mkuu nakupongeza wewe binafsi kwa kazi nzuri unayofanya. Imani yangu ni kwamba watanzania hawa ni vizuri sasa tukawaeleza tunayoona picha ya tunakokwenda.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wake kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Kuhusu barabara ya kutoka Mbande – Kongwa – Mpwapwa – Kibakwe hadi Chipogoro; barabara hii ni ahadi ya Mheshimiwa kujenga kwa kiwango cha lami. Hatua kadhaa zilianza kuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kuweka alama za “X”. Kinachotusikitisha ni kuona haipo katika mpango wowote katika orodha ya barabara mbalimbali ulizozitaja katika hotuba yako. Aidha sijaona fedha yoyote iliyotengwa kwa ajili ya shughuli yoyote ya maandalizi ya ujenzi. Hakika tumeshindwa kuelewa nini hatima yetu kwa majimbo ya Mpwapwa na Kibakwe, Mheshimiwa Waziri tunaomba msaada wako, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kalemani mdogo wangu, Naibu wake Mheshimiwa Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Ndugu Mwinyimvua na watumishi wote wa Wizara ya Nishati, hongera sana kwa kazi nzuri mnayoifanya na napenda nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia sasa inapima uwezo wa uchumi wa nchi kwa kuangalia uwezo wake wa kuzalisha na kutumia umeme. Kwa hiyo, ukitaka kupata kipimo kizuri cha kujua nguvu ya uchumi wa Taifa fulani, unaangalia wana uwezo gani wa kuzalisha nishati na wana uwezo gani wa ku-consume nishati hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe takwimu, nchi ya kwanza kwa kuzalisha umeme yaani energy per capital ni Iceland, nchi ya 73 ni China, nchi ya 137 ni Tanzania, nchi ya mwisho ni Eritrea. Katika grouping walizozifanya kwa clusters sisi ni wa 137 na uwezo wetu wa kuzalisha umeme ni megawatt 1,500. Ukiangalia kwa kiwango hiki utaona kwamba tunapozungumzia kupeleka umeme vijiji vyote zaidi ya 12,000, tunapozungumzia uchumi wa viwanda na kwamba mpaka mwaka 2020 tufike uchumi wa kati ni ndoto kama hatuna energy ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha wakati Serikali inafanya juhudi kubwa sana ya kuzalisha umeme na sera ya dunia ya nishati, The World Energy Policy is power mixing. Lazima uwe na vyanzo vya aina zote ili hiki kikitetereka unakitumia hiki, hiki kikitetereka unakitumia hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwelekeo huu tunaokwenda wa kwenda uchumi wa viwanda ambapo pande zote mbili za Bunge tunakubaliana, hatuwezi kufika huko kama bado suala la uzalishaji wa umeme kwa nchi yetu siyo suala la kufa na kupona. Ni lazima liwe suala la kufa na kupona, ni lazima tuzalishe umeme wa aina yoyote ili tuweze ku-fit kwenye hicho tunachokitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Mchumi na wakati mwingine napenda kusikiliza hotuba ili nijifunze kwa sababu kujifunza hakuna mwisho. Inanisumbua napoona hata wabobezi wa uchumi waliopo humu wana-undermine jitihada hizi zinazofanyika. Sababu zenyewe zinazotolewa, nimesikiliza sana wasemaji wengi wanasema tuache Stiegler’s Gorge, tusizalishe umeme huu mradi ulioanza kufanyiwa study mwaka 1972 mpaka leo haujatekelezwa, tuachane nao na sababu wanazozitoa ni kwamba kwa kuwa tuna gesi hatuna haja ya kuzalisha umeme huu kwa sababu gesi tunayo tuzalishe umeme wa gesi. Wakati wanajua kabisa kwa sasa hivi the leading generation katika nchi ya energy ni gesi ambayo ina megawatt zaidi ya mia saba na arobaini na kitu, inayofuatia ni hydro ambayo ina mia nne themanini na kitu karibu 500, zinazofuatia ni ndiyo biomass na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa sisi suala la kuzalisha umeme wa hydro ni la kufa na kupona. Miradi mingi ya hydro duniani huwa inapata upinzani mkubwa na hupata upinzani mkubwa kwa sababu tu umeme wake ni wa bei rahisi na unaweza ukaiibua nchi hiyo kutoka kwenye umaskini na kuwa nchi yenye uchumi stable. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Waganda wanajenga Bujagali upinzani ulikuwa mkubwa, wakasema tunajenga kwa pesa zetu na wakajenga kwa pesa zao. Vyanzo vya maji yanayozalisha umeme ule wa Bujagali, Kabahale ni vyanzo vya Mto Nile ambapo kuna siasa nyingi na international affairs nyingi lakini bado wame-generate umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, installed capacity ya Ethiopia ni megawatt zaidi ya 4,000 na wamezi-tap kwenye Mto Nile wakajenga mradi, unazalisha umeme na walikataa kusaidiwa na mtu yeyote wakaamua kuzalisha kwa pesa yao. Hivi sasa Ethiopia wana mradi unaoitwa The Grand Ethiopian Renaissance Dam ambao utazalisha megawatt 6,450 na wanachukua Mto Nile. Sisi tunazuiwa na Watanzania wenzetu wanaosema ni wazalendo, kukata miti square kilometer 1,400. (Makofi)

TAARIFA . . .

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji ni mdogo wangu na nampenda sana rafiki yangu, alipokuwa anagombea Urais Chuo Kikuu nilimsaidia pia. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunapaswa kulichukua jambo hili kwamba siyo la kisiasa, ni jambo letu sote na ushindi wa kujengwa kwa chanzo hiki cha umeme iwe ni wa kwetu sote. Ili tuweze kufika kwenye uchumi wa viwanda, kwanza ili tuweze kupeleka umeme kwenye vijiji vyetu vyote zaidi ya 12,000 tunahitaji zaidi ya megawatt 2,500 ambazo hatuna. Sasa anayesema anataka umeme wa REA kijijini kwake ndiyo huyo anayekataa chanzo chenye bei nafuu kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania katika ukanda huu wa East Africa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi. Niseme tu kwa niaba ya Serikali, maoni ya kamati hizi mbili ambazo ni muhimu sana, ambazo zinafanya kazi ya kufuatilia (over site function) zimefanya kazi zao vizuri sana na ninawapongeza sana. Nampongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Mheshimiwa Kaboyoka, taarifa yake nzuri na Wajumbe wote wa Kamati hiyo. Kipekee sana nimpongeze dada yangu Mheshimiwa Grace Tendega kwa ripoti nzuri sana. Nawapongeza pia Makatibu wa Kamati, wamefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yamesemwa mambo mengi makubwa yenye nia ya kuishauri Serikali, kama ambavyo wajibu wa Bunge umesemwa kwa mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nasi kama Serikali, kazi yetu kwa muktadha huu ni kupokea taarifa hizi ambazo baadaye kupitia kiti chako zitapitishwa na kuwa maazimio ya Bunge; kwa hiyo, Serikali kazi yake itakuwa ni kwenda kuyapitia na kuyatekeleza kwa kadri kanuni za Bunge zinavyotaka, ambapo huko tutakutana Serikali pamoja na Kamati na kujaribu kutekeleza na kuteta taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kwa mujibu wa utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wangekuwepo Mawaziri wote na pengine wangepata fursa ya kusema hapa, wangeweza kupunguza mzigo ambao umesemwa, lakini tunafahamu ziko taratibu. Nakushukuru na kukupongeza pia wewe kwamba umetuongoza vizuri na Serikali tumepata kusikia, lakini kwa michango ya Waheshimiwa Wabunge, unazo Kamati makini. Kwa kweli ni watu makini na wamefanya kazi yao vizuri; nasi upande wa Serikali tutajitahidi kufanya nao kazi vizuri ili tuhakikishe kwamba tunamsaidia Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Rais wa Awamu ya Sita hayuko tayari kuona fedha za Serikali zinachezewa, hayuko tayari kuona Serikali inaingia mikataba mibovu. Amesema ukitaka kujua true colors zake, chezea fedha ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutafanya kazi hii kwa uaminifu mkubwa upande wetu wa Serikali kwa kadri kila sekta ilivyoguswa ili kuhakikisha kwamba ripoti hizi za Kamati zinatendewa haki ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nirudie tena kuwapongeza Kamati zote mbili kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uamuzi wake wa Kuendeleza Mji wa Dodoma na Kuupa Hadhi ya Jiji
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia. Nawashukuruni sana. Waheshimiwa Wabunge wote kwa pande zote mbili kimsingi ni kama wameunga mkono hoja yangu na hoja ya Wabunge wa Mkoa wa Dodoma ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuamua Dodoma kuwa jiji. Kimsingi ni kama wamepongeza na wameunga mkono hoja hii nawashukuruni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tulileta hoja hii? Tulileta hoja hii ya kuomba azimio hili lipitishwe na Bunge kwa sababu ni utaratibu wa kawaida wa mabunge duniani. Pale ambapo Serikali imefanya jambo zuri, ni jambo zuri la kidiplomasia pia kuungwa mkono na Bunge lake ili kuonesha kwamba Bunge na Serikali viko pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uamuzi wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi ulifanywa mwaka 1973, ni miaka 44 mpaka 2017. Rais huyu wa Awamu ya Tano baada ya kupita Marais wengi, yeye ameamua kwa vitendo kwamba tunahamia Dodoma, Serikali inahamia Dodoma mambo ambayo tayari yameshafanyika. Kwa hiyo, tunapotaka kupongeza ni kwa sababu sisi Wabunge wa Dodoma tunaona faida inayopatikana na ninyi wenzetu Wabunge mnaona yanayoendelea kwamba Dodoma inashamiri na inaenda kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoona matembe yaliyokuwa karibu na mji yanaondoka, tunapoona watu wanazidi kujenga nyumba bora, tunapoona miundombinu mbalimbali inazidi kuimarishwa, tunapoona idadi ya watu inaongezeka, tunapoona Wabunge badala ya weekend kuondoka kwenda Dar es Salaam mnabaki Dodoma, sisi mlitaka tufanye nini badala ya kuomba tupitishie Azimio hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tumeomba Azimio hili lipitishwe na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wote tuunge mkono, kwa sababu Rais huyu amefanya jambo kubwa na sisi Wabunge wa Dodoma tunataka Watanzania wafahamu kwamba Wabunge wa Dodoma tumefurahishwa na jambo hili na tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Afrika ijue kwamba Wabunge wa Dodoma na wananchi wa Dodoma tumefurahishwa na jambo hili, tunataka dunia ijue kwamba Wabunge wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla tumefurahishwa na jambo hili na ndiyo maana tunaleta azimio hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ilipotangazwa kuwa jiji ilikuwa haijakidhi vigezo na ile siku ya Uhuru ikatangazwa Dar es Salaam kuwa Jiji. Ilikuwa haina hata vigezo hata kimoja. Tuna Jiji la Mbeya, Jiji la Tanga, Jiji la Arusha na Jiji la Mwanza. Ni vigezo vipi vilivyokamilishwa ilhali ikiwa Dodoma iwe nongwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakata niseme tu Waheshimiwa Wabunge, mimi nimewaomba na Wabunge wa Dodoma tunawaomba wenzetu Wabunge muunge mkono azimio hili kumpongeza Mheshimiwa Rais na yale yote mliyoyasema Waheshimiwa Wabunge na kwenye maazimio
tumesema; kwenye Azimio namba mbili tumeiomba Serikali kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi miundombinu mbalimbali ili kukidhi vigezo hivyo ambavyo vina upungufu. Kwa sababu hakuna kitu ambacho kimekamilika hata katika miji mingine ambayo imetangazwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa Dodoma kwa sababu ya hadhi yake ya Makao Makuu ambayo hakuna anayebisha hata mmoja, basi hivi vyote tunaamini vitakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, nasi wananchi wa Dodoma na kwa niaba ya wenzangu Wabunge wa Dodoma, hususan Mheshimiwa Spika ambaye ameruhusu Azimio liweze kusomwa, tunasema hivi, zawadi yetu kwa Mheshimiwa Rais Magufuli itakuwa ni kubwa mwaka 2020, ndiyo ahadi tunayoitoa kwake. Tunamshukuru kwa haya makubwa anayoifanyia Dodoma, tunamshukuru kwa kututoa gizani na sasa ametuweka kwenye mwanga. Ninawaomba kwa sababu na nyie Waheshimiwa Wabunge wote ni sehemu ya maendeleo ya Dodoma, mtuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja tena.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. GEOGRE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii ya Mipango na Fedha kwa kazi nzuri wanayofanya na sisi tunasema kama Wabunge wa chama kilichopewa dhamana na Watanzania kuongoza nchi hii, tuko nyuma yao na wasiwe na hofu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa mengi juu ya uchumi wa nchi yetu. Leo nianze kwa kumuunga mkono nakubaliana sana mawazo ya mchangiaji aliyepita rafiki yangu Bashe kwa maeneo aliyogusa amefanya kazi nzuri ya kibunge na ni mfano mzuri wa Wabunge wengi ambao tunachangia michango yetu hapa inayokwenda sawasawa kabisa na tunachotakiwa kuwafanyia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labla pengine nilikuwa nikisikiliza wenzangu wanavyochangia wakihoji uwezo wa kuweka mipango ya nchi yetu na kuendesha uchumi wa nchi na wengine wakijaribu kubeza yanayofanyika. Nataka niwahakikishie na hasa Wabunge wenzangu wa CCM. Tusivunjike moyo watanzania wanatuelewa wanaona barabara zinajengwa, wanaona zahanati zinajengwa, wanaona vituo vya afya vinajengwa wanaona watoto wao wanasoma bure, wako pamoja na sisi na wanatuelewa sana tuendelee. Usitegemee adui yako akakusifia na ukiona anakusifia basi jambo hilo uliache, ukiona anakupinga jambo hilo lifanye sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitumie Bunge lako kukumbusha misingi ya uchumi wa nchi yetu unapangwaje. Maana hapa zimekuwa zikielezwa theories mbalimbali za uchumi na wengine hata siyo Wachumi na hata mimi na-declare kwamba siyo Mchumi, lakini nataka nijadili uchumi kwa legal perspective, kwa sababu mipango na uendeshaji wa uchumi haji nao tu Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa sababu ni Waziri, ipo kwenye sheria na katiba hakurupuki tu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango akaja tu na mambo hapa akasema imekuwa hivi imekuwa hivi, hapana.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka nisome katiba na naomba niisome kwa ukamilifu maeneo yanayo-guide mipango na uendeshaji wa uchumi wa nchi yetu; ili tukiwa tunazungumza tuwe tunaelewana, maana wako wengine wana nadharia za kibepari, wako wengine wana nadharia za kijamaa hatuwezi kuelewana sisi wana TANU na ASP tunajua tulikotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu Ibara ya tisa (9) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema hivi:

“Lengo la katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, naendelea anasema katika Ibara hii ya 9: ...Hivyo Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote inawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha...

Mheshimiwa Spika, naruka (a), naruka (b) kwa sababu ya muda naenda (c):

(c) kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine; (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niruke zote niende (i) inasema:

(i) kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada za kuondosha umaskini, ujinga na maradhi;

(j) kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi.”

T A A R I F A . . .

MHE. GEOGRE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, nia yake ilikuwa ni kuona kwenye TV umeonekana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nimenukuu eneo hili theories tunazozitoa nyingi hapa kila mtu anatoa theory yake na anachukua mfano best practice ya nchi anayoiona yeye. Wakati asili ya uchumi wa Taifa lolote, asili ya mipango ya uchumi wa Taifa, mipango ya maendeleo ya Taifa lolote inatokana na historia yake. Sisi Watanzania kwa asili ni wajamaa na fikra zetu sisi ni za kiumoja umoja na ujamaa jamaa, huwezi kuwabadilisha Watanzania hapo.

Mheshimiwa Spika, leo hii mtu akija na mawazo ya purely ubepari, basi hatokani na misingi ya Kitanzania, ingawa katika Ibara hii ya tisa (9) inasema tutafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea kwa kuzingatia mazingira na mabadiliko ya wakati. Ndiyo maana katika sheria zetu tumetambua baadhi ya misingi ya kibepari, tukatunga sheria ya PPP kwamba wakati mwingine Serikali itapaswa kufanya biashara na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, tukapima tukaweka sheria ya ubinafsishaji kwamba tukaribishe sekta binafsi iingie kufanya kazi na Serikali. Ndiyo maana tuna viwanda na ndiyo maana shughuli mbalimbali zinazofanywa na sekta binafsi, lakini katika katiba hii inatukataza kupeleka njia kuu za uchumi mikononi mwa watu wachache maana huo ni unyonyaji. Ndiyo maana tunapokuwa tunazungumza mambo haya ni lazima twende kwa kiasi maana nchi yetu kwa asili na hata fikra za watu, utamaduni wa watu wanafikiria… (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. GEOGRE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, nikubaliane kwamba wakati mwingine mtu unapochangia ukakatizwa katizwa inaondoa ladha nzima, lakini nime-cite hapa Katiba yetu na naomba nirudie maana sasa sina namna na kwa hiyo hata hotuba yangu haitakwisha.

Mheshimiwa Spika, eneo la katiba hili linazingatia kwamba ambavyo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa, kwa kuzingatia mazingira yalimo katika Jamhuri ya Muungano. Mazingira yatakavyojitokeza tutabadilika kulingana na ndiyo maana sisi hatuwezi kusema ni wajamaa per se au mabebari per se. Ukitaka kutengeneza misingi ya uchumi wa Tanzania haiwezekani ikafafana na nchi nyingine that’s what I want to say! Ni lazima itokane na asili ya watu wale ndiyo maana kwenye miaka ya 90 mpaka 2000 tulipoingia kwenye sera ya ubinafsishaji, tulipobinafsisisha wengine walipotaka kutuondoa madarakani wakasema hawa wameuza viwanda, wakati wao wenyewe wanasema tukumbatie sekta binafsi, wakasema tumeuza viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii tulikuwa tuna Shirika la Ndege ambalo tumejaribu kucheza na sekta binafsi tukaingiza South Africa wakachukua baadhi ya hisa na nini likashindwa kwenda. Tumeamua Serikali ya Awamu ya Tano kununua ndege zetu imekuwa nongwa. Leo hii tunayo reli ambayo tumeamua kuijenga sisi wenyewe kama nchi na kwa kuanza na fedha zetu wanasema kwa nini tusiwape sekta binafsi waweze kufanya mambo yenye gharama kubwa. Huku wakiona kabisa kwamba yako baadhi ya mabehewa ya watu binafsi yanayotembea kwenye reli…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia ni lazima Watanzania tuunge mkono tijihada hizi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano maana mengi haya yanayofanywa leo yalikwishashindikana kwa formula hizo wanazozisema. Ndiyo maana tunasema tuungane mkono kwa sababu hakuna kanuni moja ya uendeshaji wa uchumi na uchumi unatokana na historia ya watu wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kabisa kukushukuru kwa kusimamia vizuri mjadala huu na pia kwa shughuli zote ambazo unafanya kwa Bunge hili na kwa nchi hii tutakukumbuka sana na historia yako itabakia. Ni katika kipindi chako mambo makubwa na mengi yanafanyika katika nchi ambayo nchi hii inaweka msingi mzuri wa kwenda mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili namshukuru sana Kamati ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Salum Rehani, Mbunge wa Uzini kwa kazi kubwa na maoni mengi mazuri ambayo wameyatoa, nasi kama Serikali kusema kweli baadhi yake tunakubaliana nayo na tutayachukua.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa waliochangia na kugusa Wizara ya Mambo ya Ndani sio wengi sana, lakini kwa hawa wachache wamezungumza mambo ambayo yanagusa maeneo makubwa na kwa sababu ya muda nitajaribu kuongea kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wakimbizi tulionao hapa nchini ni wengi, hadi jana walifikia kiasi cha tunawakimbizi hapa nchini 293,931. Katika idadi hii, wakimbizi wengi zaidi wanatoka Burundi ambao wako 217,501.

Mheshimiwa Spika, jitihada kubwa zinafanyika kuhakikisha kwamba wakimbizi hawa wanarudishwa makwao. Mwezi Novemba, 2019 mwaka jana yalifanyika makubaliano kati ya UNHCR, Serika ya Tanzania na Burundi juu ya utaratibu mpya. Kwa sababu pamoja na wale waliokubali wenyewe kwa hiari yao kurudi kwao, lakini logistic namna ya kuwarudisha nyumbani imekuwa kidogo zina mchakato mgumu. Kwa hiyo, tumekubaliana kuweka malengo kwamba kila wiki tutarudisha wakimbizi 2,000, ni imani yangu kwamba kama hili likitoka tukalisimamia, basi idadi kubwa ya wakimbizi watakuwa wameondoka nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia jambo la pili ambalo lilizungumzwa hapa ni juu ya vitambulisho vya Taifa jukumu ambalo linafanyika na NIDA. Kazi kubwa imefanyika sana tu, kwa sababu mchakato wa kutoa vitambulisho vyenyewe kuwakabidhi wananchi ni wa mwisho kabisa; lakini kuandaa mpaka kufikia kutoa vitambulisho, ndiyo kazi ngumu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kazi hii imefanyika, lengo letu ilikuwa ni kutoa vitambulisho milioni 24,200,000. Katika usajili, tumesajili 20,131,014, alama za kibaolojia tumeweza kuchukua 18,157,624, lakini kuingiza kwenye mfumo, tumeingiza 16,240,341. Kwa hiyo, utakuta kwamba karibu tumefanya kwa haya yote yote kwa kiasi kikubwa vizuri, kasoro ile hatua ya mwisho. Kwa upande wa vijijini tumeweza kuhakiki wananchi 15,488,766, pia tumetoa namba za utambulisho 13,872,281, lakini vitambulisho tulivyovitoa ni vichache na sababu kubwa ni mtambo wa kuzalishia vitambulisho hivi.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa jitihada kubwa inafanywa kukamilisha mtambo ambao tayari umenunuliwa, una kasoro kidogo ambazo ni chache, unarekebishwa na tunaufunga pale Kibaha ili tuweze kutoa vitambulisho vingi; na uwezo wa mtambo huo ni kutoa vitambulisho 9,000 kwa siku moja. Kwa hiyo, ninaamini kwamba tutaweza kufikia malengo.

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu, zimezunguziwa jitihada za kupunguza mahabusu. Jitihada kubwa zimefanyika lakini hata hivyo, pamoja na kufanyika jitihada hizo za kupanua Magereza hasa na kurekebisha miundombinu ya Magereza ni lazima pia jitihada nyingine hizi tuweze kuziendeleza. Tumeamua kuunda Kamati ya kusukuma kesi, pia DPP anazunguka katika Magereza na kuhoji mahabusu waliokaa muda mrefu ili kesi zao ziweze kusikilizwa kwa haraka. Kwa hiyo, jitihada zote zinaweza zikasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni hili la uhuru wa kuamudu ambao upo kwa mujibu wa Katiba. Hoja iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni kwamba, pamoja na uhuru huu lakini lazima tuangalie namna ya kuudhibiti au kuuwekea utaratibu uhuru huu. Nakubaliana kabisa kwa asilimia 100 kwamba kanuni zetu hazioneshi namna nzuri zaidi ya kuweza kuweka mfumo mzuri wa udhibiti wa uhuru wa kuabudu. Serikali haiingilii kamwe na wala haitaingia kamwe uhuru wa kuabudu, lakini kuweka utaratibu unaohakikisha amani na usalama ya wanaoabudu ni jambo la msingi.

Mheshimiwa Spika, tumejaribu kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine, wenzetu kwa mfano Nigeria wenyewe hawana masharti yoyote, lakini tunaona yanayotokea huko. Wenzetu wa Rwanda wameweka utaratibu na wameweka hata elimu ya mtu anayeweza kutoa au kuanzisha ministry au huduma ya namna hiyo, lazima awe na aina fulani ya elimu. Wenzetu Kenya walijaribu wakaenda nalo lakini hawakulimaliza na Uganda vilevile na wenyewe wanaendelea nalo.

Mheshimiwa Spika, nasi nadhani iko haja ya kuchukua maoni haya na kubadilisha hata kama siyo sheria, basi kanuni zilizopo kwa haraka ili tuweze kuwa na mfumo mzuri wa namna ya kuabudu. Sitaki niseme zaidi ya hapo kwa sababu, ni leo hii mchana nimekutana na wahusika wa dhehebu lile la Calvary Assemblies of God ambao Boniphace Mwamposa anafanya kazi katika lile dhehebu na kwamba ile huduma anayoitoa siyo huduma iliyosajiliwa nasi hatuna usajili wa huduma ile, lakini ile ni slogan tu; lakini yeye amesajiliwa na wenye lile dhehebu wamekuja wamekiri kwamba ni mtumishi wao, ni mfanyakazi wao, ni kiongozi ambaye anahudumu Dar es Salaam na Kilimanjaro na amekuwa akifanya hivyo mara zote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea na hatua nyingine za jambo lile kama kioo na Mwalimu wa mengine yasitokee huko mbele ya safari.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kuwashukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mheshimiwa Sadiki Muradi pamoja na Makamu Mwenyekiti Kanali Mstaafu Masoud Ali Khamis pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwa umoja wao na kwa ushirikiano pamoja kuwa na Serikali katika kuhakikisha kwamba azimio hili linafikia hatua hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru sana Msemaji wa Kambi ya Upinzani Mheshimiwa Cecil Mwambe kwa kutoa maoni mazuri ambayo kimsingi kwa pande zote mbili Kamati pamoja na Upinzani wameunga mkono hoja hii. Pia niwashukuru wachangiaji wengine wote waliozungumza na wale walioandika kimsingi hakuna hata mmoja aliyepinga azimio la matumizi ya zebaki yaani The Minamata Convention on Mercury.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa pongezi hizi na na kwa kuwa hakuna aliyepinga nataka nisema kwa ujumla wake tu kwamba mengi yaliyosemwa yamelenga zaidi katika kuonesha namna gani sasa kama tumeshakubaliana kwamba zebaki ni kitu kibaya, kina madhara kwa binadamu kwa afya ya binadamu na mazingira. Pia yako madhara ambayo yanaonekana na yanatokea na tunayafahamu na mifano tunaijua. Lakini pia liko kundi la wachimbaji wadogo ambao wao wanaathirika moja kwa moja kwa sababu wanaichezea zebaki kwa kuishika kwa mikono hapa tuna kazi ya kufanya na ndio maana Jumuiya ya Kimataifa na dunia imeona ikae na kuja na mapendekezo ya makubaliano haya ambayo leo tumeyaridhia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi suala la zebaki ni suala gumu kwa sababu viko vitu ambavyo hatuna namna bado tunahitajika kutumika kutumia zebaki kwa sababu ya aina ya teknolojia ambazo bado tunazihitaji kwa ajili ya huduma, kwa ajili ya matibabu, kwa ajili ya mila na kwa ajili ya baadhi ya utengenezaji wa vitu vingine ambavyo tunavihitaji. Na teknolojia mbadala wa vitu hivyo haujapatikana, kwa hiyo itatutuchukua muda kidogo na ndio maana hata katika kuridhia na hata azimio lenyewe linazungumzia juu ya kuondokana na matumizi ya mercury kidogo kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ifikapo kwa 2030 kusudia la mkataba huu ni kuhakikisha kwamba tuwe tumeondoka kabisa, sasa haya ni malengo na kimsingi the legal status ya convention hizi za Kimataifa huwa sio kwamba unapokuwa haujafikia level unaadhibiwa, lakini kutoingia na kukubali na kuridhia mikataba kama hii unaweza ukakosa faida za kushirikiana na wenzako duniani katika kuondokana na jambo ambalo si zuri kama ilivyo zebaki.

Kwa hiyo, kimsingi mimi nikubaliane na Wabunge wote na niseme tu kwamba Serikali imejipanga chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kuhakikisha kwamba tunakuwa na mpango mkakati wa kutekeleza azimio hili na tumekwishaanza maandalizi ya mpango mkakati huo na ifikapo mwezi ujao tutakuwa tayari tumeukamilisha mpango mkakati ambao utakuwa na majibu ya hoja nyingi sana zilizoulizwa na Waheshimiwa Wajumbe namna ambavyo tutaweza kuondokana na matumizi ya zebaki kwa sababu ya ubaya ambao wote tumedhihirisha hapa kwamba ni kitu kibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuomba na kusihi Waheshimiwa Wajumbe wakubaliane na maoni haya yaliyotolewa na watu wote pia msimamo wa Serikali katika kuamua kuridhia azimio hili ili tuwe pamoja na dunia tusiweze kukosa fursa nyingine za ushirikiano wa kusaidia na wenzetu duniani katika kuondokana na matumizi ya zebaki ambayo ni mbaya kwa afya ya binadamu lakini pia kwa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumshukuru Naibu Waziri Mheshimiwa Mussa kwa kushirikiana na mimi na kunisaidia na hata tumeweza kulifikisha azimio hili mahala hapa na kwa kumalizia nichukue nafasi hii kukuomba wasihi Waheshimiwa Wajumbe na Wabunge wote waweze kuridhia azimio hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Kutekeleza Itifaki ya Cartagena (Nagoya – Kuala Lumpur Supplementary Protocol on Liability and Redress on Cartagena Protocol on Biosafety) pamoja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Haki Miliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. (Protocal for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeder’s Rights) in The Southern African Development Community – SADC) pamoja na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Marrakesh wa mwaka 2013 unaowezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu au ulemavu unaomfanya mtu kushindwa kusoma (The Marrakesh Treaty to Facilitate Access to Published Work For Persons Who Are Blind, Visually Impaired or Otherwise Print Disabled)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kujumuisha au kusema kwa kifupi kwa yale ambayo yamechangiwa. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Bishara na Mazingira, Mheshimiwa Saddiq Murad na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Col. Mstaafu Masoud Ally pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Aidha, nawashukuru pia Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Eng. Joseph Mwalongo pamoja na Naibu Katibu Mkuu Balozi Joseph Sokoine na wataalam wote wa Wizara Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushiriki na kuandaa azimio hili hadi hatua hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi wachangiaji wengi kwa pande zote mbili za Kamati ikiwepo upande wa Upinzani ni kama vile wameunga mkono Nyongeza la Azimio hili la kuhusiana na masuala ya Bioteknolojia. Kusema kweli, ingawa ilielezwa hapa kwamba tumechelewa, lakini upande wa Upinzani wamesema kwamba tulipaswa kuacha kuridhia kwa sababu tumefanya hivyo kwa haraka na pengine wadau hawakushirikishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio hili ni nyongeza tu la Azimio la Cartagena ambalo Tanzania iliridhia mwaka 2003. Nyongeza hii ilitokana na namna ambavyo hatua za uwajibikaji na ulipaji wa fidia kwa wale watakaoathirika na matumizi ya bioteknolojia ambapo kulikuwa na mvutano na kikawekwa kifungu cha 27 ili nchi ziweze kwenda kutafakari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nyongeza hii kutoka mwaka 2003 mpaka 2019 ni miaka takribani 16. Kwa hiyo, tathmini na tafakari zimefanyika sana na ndiyo maana sasa limekuja kuwekwa humu kuwa eneo au sehemu ya Azimio lile la Cartagena ambalo ilipitishwa mwaka 2000 na Tanzania tuliridhia mwaka 2003.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwatoe mashaka kwamba ushirikiswaji haukufanyika. Siyo kweli, ushirikiswaji ulifanyika kwa kiasi kikubwa sana na kwamba hatua hii ni muhimu sana kwa sababu hatuna namna yoyote ya kuzuia madhara yanayotokana na bioteknolojia. Sisi Tanzania basically, hatujaanza kutumia bioteknolojia, lakini hatuna namna ya kuzuia kwa sababu bioteknolojia inaweza kukuathiri kwa namna nyingi; inaweza kuwa direct or indirect. Bidhaa zake tunazitumia na wapo watu inawezekana wameathirika. Kwa hiyo, kusema tusiridhie au tusite ni kuendelea kujiweka katika mazingira ambayo watu wetu wakipata madhara, hatuwezi kupata fidia au hawawezi kufidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza tumechelewa, lakini sasa tumeamua na Bunge lako limeamua kukaa na kujadili na kwa kiasi kikubwa wameunga mkono. Kwa hiyo, nawashukuru sana, akiwepo mchangiaji mmoja Mheshimiwa Eng. Chiza ambaye amezungumzia kuhusiana na suala la utafiti kwamba tafiti zimeondolewa. Kwenye ule utafiti umeweka msamaha kwa hatua za kisheria kwa utafiti katika matumizi ya bioteknolojia au shughuli za kitafiti kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu, pande zote; kwa upande wa Upinzani, Kamati na Waheshimiwa Wabunge wote wametoa maoni mazuri. Sisi kama Serikali tumejipanga na maoni yale yaliyotolewa tutayazingatia kwamba lazima tujenge uwezo wa wataalam kubaini madhara lakini pia jamii kupata elimu ya faida na madhara ya bioteknolojia. Maoni haya yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge tumeyachukua na tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa dhati kabisa kwa kunipa nafasi ya mwisho kwa leo hii na bila shaka ndiye mchangiaji wa mwisho kwa maana ya wachangiaji wa kawaida katika bajeti ya Serikali. Nianze kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Manaibu Makatibu Wakuu na Viongozi wa Taasisi zote na Idara zote zilizoko chini ya Wizara hii kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya ya kuhakikisha kwamba, tunakuza uchumi wa nchi yetu, ili tuweze kupata matunza tunayoyataka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nianze kupongeza kwa Serikali kutekeleza kwa vitendo ahadi ya kuhamishia Serikali Dodoma kama Makao Makuu ya nchi. Ni jambo kubwa ambalo liliahidiwa kwa muda mrefu, lakini limetekelezwa na tunaona kasi yake ambavyo Dodoma inabadilika na mimi kama Mwanadodoma kwa niaba ya Wananchi wa Dodoma niseme jambo hili limetufurahisha. Tunaona namna ambavyo tumepata faida ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja na imebadilisha maisha ya watu wetu. Serikali imelifanya jambo hili bila kutumia gharama kubwa, lakini lina tija kubwa sana kwa Wananchi wa Dodoma na sisi tunaoishi Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu na nilitaka niwataarifu Wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwamba, kwa bajeti ya mwaka huu jumla ya pesa itakayoingia Dodoma kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya barabara tu ni bilioni 175. Bilioni 175 zitapitia TANROADS, zitapitia Halmashauri ya Jiji ya Dodoma na zitapitia kwenye Fungu lile la miradi ya Miji ya Kimkakati, ukijumlisha zote ni kwamba, bilioni 170 na ushee zinaingia Dodoma kwa ajili ya kutengeneza barabara ikiwepo barabara ya mzunguko. Hili si jambo dogo, ni jambo kubwa na tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, limezungumzwa jambo hapa lililokuwa linahusianisha maendeleo ya watu dhidi ya maendeleo ya vitu na jambo hili limetafsiriwa vizivyo likinukuu Kauli ya Mwalimu Nyerere na ni upotoshaji mkubwa. Na kama kungekuwa kuna Profesa anasahihisha mtihani kwa watu waliokuwa wanachangia wakienda na mtizamo wa hoja hiyo wote wangepata sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alichokisema Mwalimu ni kwamba, maendeleo ni lazima yawe yale yanayotambua pia hali ya usawa, haki na utu kwa maana ya dhana ya usawa, haki na utu kwa sababu ya element za kikoloni zilizokuwepo wakati huo wakati wakoloni wanatuambia tutawafanyia hiki, tutawafanyia hiki, hamna haja ya kudai uhuru kwa sababu, tutawafanyia kila kitu. Akasema hapana, lazima utu wetu, haki, viwepo ndipo tuone uzuri wa maendeleo. Leo kilichotafsiriwa hapa ni kama vile usijenge barabara, lakini uvae nguo nzuri, usijenge nyumba, lakini upulizie perfume, ndicho wanachozungumzia, hiyo sio hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa Shivji alipokuwa anaongea katika mdahalo wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere tarehe 25 Machi, 2017 aliondoa utata wa jambo hili. Na katika maeneo aliyosema, alisema namnukuu, “Hakuna kitu kinachoitwa maendeleo ya vitu kutokana na ukweli kwamba, vitu havijiendelezi.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia alipokuwa anahitimisha akasema, uhuru bila maendeleo ni ulaghai uliosukwa na walionacho. Uhuru bila maendeleo ni ulaghai uliosukwa na walionacho kwa hiyo, ili uweze kuitafsiri vizuri kati ya maendeleo ya watu na maendeleo ya vitu katika falsafa za kisasa za mendeleo kwa maana ya maendeleo huwezi ukatenganisha hivi vitu viwili. Na ukitenganisha utapata tatizo maana tunajenga miradi mikubwa kwa ajili ya kujenga msingi wa uchumi wa nchi yetu. Tunajenga Airport ili tupate kuingiza fedha zaidi kila kinachofanyika, tunajenga barabara, tunajenga madaraja, tunajenga mradi wa kuzalisha umeme, ili hivi vijenge msingi wa uchumi wetu, uchumi wetu bado ni mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka Serikali iende kwenye kuzalisha chuma la Liganga, ili tuweze ku-export chuma tupate fedha nyingi. Hii yote ni katika kujenga msingi wa uchumi maana uchumi wetu ni mdogo, lakini hapa mtu anasema eti kwa nini hamuongezi mishahara? Uchumi huu mdogo unaongezaje mshahara?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima uanze kujenga uchumi wa nchi kwanza, msingi wake wa uchumi ndio uongeze mshahara, utaongeza hewa tu. Hapa sasa hivi ninyi Waheshimiwa Wabunge na wengi wetu tumeajiri wafanyakazi wa ndani, tumwambie Mheshimiwa Dkt. Mpango hapa aweke kima cha chini shilingi milioni moja kama tutaweza kulipa kwa uchumi tulionao, uchumi wetu hauwezi kubeba. Kwa hiyo, Rais anaposema nipewe muda tuweke mambo sawasawa halafu tutaongeza mshahara kwa kiwango kizuri, lazima tuelewe msingi wake ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati ya moyo wangu ninaamini Serikali inafanya vizuri. Mheshimiwa Dkt. Mpango endeleeni tukamilishe miradi hii mikubwa, ili tuweze kutatua tatizo la msingi na baadaye uchumi wetu uweze kukua, tulionao uchumi wa sasa ni mdogo mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Vile vile kipekee sana namshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini na sasa amenipa kuisimamia Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nampongeza tena Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Zungu kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizipongeze sana Kamati zote mbili; Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati ya Utawala na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, dakika moja tu. Waheshimiwa Wabunge, kwa mujibu wa Kanuni ya 34(5), ninaongeza muda bila kulihoji Bunge mpaka shughuli yetu itakapomalizika.

Endelea Mheshimiwa. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Wajumbe wa Kamati zote mbili; Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati ya Utawala na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa kazi nzuri wanazofanya. Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama na Mheshimiwa Chaurembo, pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ambao kimsingi kwa upande wetu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Kamati ya Katiba na Sheria ikiongozwa na Mheshimiwa Mhagama, na wewe mwenyewe Makamu Mwenyekiti, mmekuwa watu wa karibu sana nasi, mnafanya kazi yetu iwe nyepesi, nanyi ni walezi wazuri. Kwa hakika mara zote hata wakati mwingine msipotuita tunajikuta tunawa-miss kwa sababu, tukifika kwenye Kamati yenu mnatusaidia sana katika kuhakikisha kwamba jukumu letu la Serikali linakwenda sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa mengi na Kamati. Kwa hakika kama ingekuwa hakuna ulazima wa kusema, wala hakukuwa na sababu ya kusema. Ilikuwa ni kusema amina, amina, amina, kwa sababu, tunatakiwa tu tuyachukue, tuyapokee na kwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimeona niguse tu maeneo machache, hasa moja tu la hatua kubwa ambayo imefikiwa na Mhimili wa Mahakama. Katika jukumu ambalo pia ninalo kama Waziri wa Katiba na Sheria ni pamoja na kusimamia mhimili huu. Unaposimamia mhimili ni kitu kikubwa sana, na hasa mhimili huu wa Mahakama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilifahamishe Bunge lako Tukufu na wananchi wa Tanzania kwamba, mhimili huu umepiga hatua kubwa sana katika maendeleo ya kimtandao. Wamepiga hatua kubwa sana kiasi kwamba, sasa unaweza ukasajili kesi yako ukiwa nyumbani na simu yako na ukasajili shauri lako, lakini unaweza ukapata majibu yote ukiwa nyumbani wala usitoe hata hatua moja nje ya nyumba yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna uwazi mkubwa katika uendeshaji wa mashauri ambapo unaweza ukasikiliza shauri lako na wala usifike hata Mahakamani. Maendeleo haya ni makubwa na wakati mwingine tunasema tumeenda mbele kuliko hata uelewa wa wananchi wa kupokea huduma yenyewe hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameenda zaidi sana kwamba, yako malalamiko ya wananchi kuhusu kutokutendewa haki au rushwa na mambo mengine na mhimili huu wa Mahakama. Yenyewe hiyo wameweka ukurasa mahususi ambao unaweza ukaingia na ukaandika uko wapi? Umetendewa nini? Uki-post tu pale, mfumo mzima wa Mahakama, viongozi wote wanaona, kwamba kuna mahali, mfano Tandahimba au wapi, kuna hakimu au kuna mtu mwenye wajibu wa kutoa haki amefanya hiki na hiki. Ni hatua kubwa mno Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunafikiri ikitupendeza na nilikuwa naongea na Mkuu wa mhimili huu, Jaji Mkuu - Prof. Ibrahim Juma, pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Ole-Gabriel, wakasema ikipendeza na kama kutakuwa na nafasi tupate fursa ya kuja kutoa semina kwa Wabunge ili muone mifumo hii na system hizi zinavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakapopata muda na kama muda utaruhusu, basi Bunge lijalo tupate slot hata angalau siku moja tuje tufanye semina hiyo ili Wabunge mwelewe iwe rahisi kwenda kuwaeleza wananchi hatua kubwa ambayo imefanywa na mhimili huu wa Mahakama. Yamesemwa pia maeneo mengine ya namna ambavyo taasisi kama ya RITA, NIDA, Uhamiaji, PSSF, Bima ya Afya, Bodi ya Mikopo na mifumo mingine kwamba, iunganishwe ili iweze kusemana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie kwamba, maandalizi ni makubwa. Hatua kubwa imefikiwa na sasa mifumo hii inasema kwa pamoja na mawasiliano yapo na mahusiano yapo, yanaendelea kujengwa kwa mifumo zaidi ili kuhakikisha kwamba, mawasiliano ya vifo, usajili, utambuzi na vyote hivi vinapatikana katika mfumo wa pamoja katika Serikali.

Niwahakikishie tu kwamba, hatua hii imefikiwa na Wajumbe wa Kamati mmelisema hili sana na nirudie kusema, tunaendelea nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema, yote mliyoyasema hakuna hata moja ambalo tutafuta. Tunayachukua kama yalivyo na tunahakikisha kwamba tunayatekeleza. Tutakapokutana mwezi wa Tatu tutawapa mrejesho wa hatua tutakayokwenda na ninyi mtatushauri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na nianze kwa kuzipongeza Kamati zote mbili; Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji pamoja na Kamati ya Miundombinu kwa kuwasilisha hoja zao leo asubuhi na kwamba tumepata michango ya kutosha. Kusema kweli Kamati hizi zinafanya kazi nzuri sana. Nianze kwa kuunga mkono hoja za Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, nina maoni katika maeneo mawili. Kwenye mapendekezo ya Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji kwenye aya ya 3.3, ukurasa wa 60, limetolewa pendekezo linalohusiana na kuimarisha dhana ya ushirika nchini. Katika pendekezo hilo, Kamati imesema Serikali ilete Bungeni marekebisho ya sera na sheria za ushirika; wamezitaja na zile sheria.

Mheshimiwa Spika, nataka kushauri azimio hili lirekebishwe kidogo ili kusiwe kuna ulazima wa Serikali kuleta sera humu Bungeni kwa sababu siyo utaratibu. Kwa hiyo, isomeke, “Serikali iangalie upya au ipitie upya Sera ya Ushirika nchini ya mwaka 2002 na kuleta marekebisho ya sheria.” Isomeke hivyo, litakuwa azimio linaloweza kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili linahusiana na pendekezo la aya ya 3.6 ambayo imeelezea umuhimu wa kuwa na chombo cha Kitaifa cha Kudhibiti, Kuratibu na Kusimamia Kipango ya Kaendeleo ya nchi yetu. Ilikuwa ni concern kubwa ya Bunge hili hata wakati wa Bunge letu la Bajeti, walieleza haja ya kuwa na Planning Commission (Tume ya Mipango) ambayo kama kumbukumbu tunazo, basi tunakumbuka tuliivunja na kufuta ile sheria mwaka 2018.

Mheshimiwa Spika, maoni haya kwa sababu yametolewa na safari hii yamekuja kwa mapendekezo ya Azimio la Kamati, nataka tu niwape taarifa Waheshimiwa Wabunge na Kamati inayohusika kwamba Serikali ililichukua jambo hili kwa uzito mkubwa toka wakati ule na kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wiki hii kama siyo wiki iliyopita, aliagiza tuanze mchakato wa kuunda Tume ya Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ingekuwa siyo kuvunjwa kwa sheria ile kwa uzima wake, tulitaka tutafute namna ya urahisi wa kwenda kwenye hiyo, lakini kwa kuwa mchakato wake ni lazima uanze kutoka mwanzo, ianze sheria, tupitie stages zote, tunatarajia mpaka kwenye Bunge la mwezi wa Nne angalau tufanye first reading. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pengine ikilipendeza Bunge lako na kwa mamlaka uliyonayo, tunaweza tukaenda kwa speed utakayoona inafaa ili tuweze kuwa na Planning Commission katika nchi, itusaidie kupanga mipango yetu hii mikubwa ambayo kwa kweli tunaitekeleza, lakini unaiangalia uratibu wake hauna chombo kikubwa chenye uzito wa Kitaifa wa kuweza kuratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitamani nichangie maeneo haya mawili, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Kamati husika kwa michango mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi, na nianze kwa kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya UKIMWI, Dawa za Kulevya na Magonjwa Yasiyoambukiza, Mheshimiwa Fatma Toufiq pamoja na Kamati yote kwa ujumla. Tunafanya nao kazi vizuri, na niseme tu kwa kweli maazimio yote saba ambayo wameyaleta katika taarifa yao, sisi Serikali tunayapokea yote kwa mikono miwili na tunahakikisha kwamba tunakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niseme tu katika kuchangia katika maazimio haya yaliyogawanyika katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni eneo la UKIMWI ambapo Kamati hii na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wanaonisikia, tumemaliza mkakati wa nne wa mapambano dhidi ya UKIMWI, na sasa tumetengeneza mkakati wa tano. Katika mkakati huu wa tano, msisitizo mkubwa utakuwa ni kutoa elimu juu ya kupima virusi vya UKIMWI pia kufuatilia VVU wale watoro, ufuasi wa dawa na tohara kwa wanaume. Hayo ni maeneo ambayo yatatiliwa mkazo mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kuimarisha afua za udhibiti wa VVU na UKIMWI na hasa kwenye mikoa ile ambayo maambukizi yamefika asilimia zaidi ya 4.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kutoa elimu kuhusu unyanyapaa na ukatili wa kijinsia ili kupunguza hofu kwa waathirika. Eneo lingine ni kujenga uwezo wa Kamati za UKIMWI na kuhakikisha kuwa Kamati hizi zinakuwa na uwezo na kuchukua hatua na kutoa ushauri unaostahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho katika eneo hili la UKIMWI ni kuhakikisha kuwa vituo vya kutoa huduma ya afya ya mama na mtoto vinatoa elimu pia kwa wamama wajawazito ili kuhakikisha kwamba maambukizi yale hayatoki kwa mama kwenda kwa mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni eneo la magonjwa yasiyoambukiza, ambapo hapa kulikuwa na azimio na azimio moja ambalo limesisitiza zaidi kwamba magonjwa haya ambayo hayaambukizi yanaweza tu kupungua pale ambapo elimu itatolewa kwa wananchi, na pia kuhimiza michezo shuleni. Sisi kwa ujumla tumepokea azimio hili na kazi kubwa ya Serikali ni kwenda kulitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni kuhusu Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Hapa yako maazimio mawili na msisitizo mkubwa umekuwa ni umuhimu wa kuhakikisha kwamba sera ya kudhibiti dawa za kulevya na mapambano dhidi ya dawa ya kulevya inatiliwa mkazo na kuhakikisha kwamba inakamilika. Niseme tu hatua za utayarishaji wa sera hii zimekamilika na sasa tuko katika kupeleka kwa wadau ili tuweze kupata maoni na baadaye sera hii itakuwa imekamilika. Nataka niwahakikishie Bunge na Kamati kwamba tuko katika hatua za mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala zima ambalo limezunguzwa hapa pamoja na michango ya Wabunge ni umuhimu wa kuweka waratibu wa masuala ya UKIMWI katika Halmashauri zetu za Wilaya. Dawa za kulevya hazina uratibu kule kwenye ngazi za chini. Kwa hiyo, maoni haya yaliyotolewa, nadhani hata kama siyo sehemu ya azimio lililosemwa katika maandishi, lakini ni jambo zuri la kulichukua na sisi Serikali nadhani ni administrative, ni kusema tu katika kwamba masuala ya UKIMWI na dawa za kulevya, tutajaribu kuliangalia katika Serikali tuone namna gani litakavyotekelezwa, lakini siyo jambo baya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilizungumzwa hapa juu ya mradi wa DHS ambao ulikuwa ni mpango ambao unafuatilia na kuangalia hali ya UKIMWI katika makundi mbalimbali. Mheshimiwa Mchafu amezungumza suala hili akasema haishirikishi watoto katika utafiti huu. Ni kweli, nadhani pengine ni upungufu. Tujaribu kuona kwa program hii ambayo kwa kweli inaisha na sasa tunakuja DHS nyingine, tutaangalia namna ambavyo tunaweza tuna- include suala la watoto kuingia katika utafiti huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya iko kwenye mchakato wa kuanzisha mpango mkubwa sana ambao utakuja na utafiti mkubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI na madhara yake. Kimsingi nao nadhani wamelichukua hili, tutashirikiana kwa sababu tunafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kwamba katika mpango unaokuja basi tunahakikisha na watoto wanaingia katika nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Vinginevyo, naunga mkono hoja ya Kamati kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kupongeza Kamati hizi tatu kwa kazi kubwa sana na nzuri ambayo wamefanya. Kusema ukweli wamefanya Bunge hili leo lichangamke kwa sababu ya kazi kubwa ambayo imefanywa na Kamati hizi tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, LAAC wamekuja na Maazimio sita, PIC imekuja na maazimio 11, na PAC imekuja na maazimio saba. Serikali tumeyachukua maazimio yote positively na kusema kweli ni kazi ya Serikali kwenda kuyafanyia kazi. Napenda nikuhakikishie kwamba tumeyasikia, na pia tumesikia michango ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii iliyofanyika leo inatokana na ripoti ya CAG ya mwaka 2019/2020. Huu udhaifu mliousema hapa, ni ya 2019/2020. Sasa taarifa ambayo sisi tunaamini imeandaliwa na CAG na ikapokelewa na Mheshimiwa Rais, na ikaletwa humu Bungeni, na mmeifanyia Kazi mkaitendea haki, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wakati anapokea taarifa hii, alisema maneno yafuatayo: “Kumekuwepo na mifumo mingi Serikalini, mifumo ambayo haisomani, na kila mmoja ukitengeneza mfumo unauruhusu uchotaji wa fedha.” Pia akaendelea kusema, “kuna usimamizi usiokuwa na weledi Serikalini unaosababisha wizi.” Mwisho wa kunukuu. Akaagiza CAG, PCCB na DPP wachukue hatua bila kuogopa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, kwa taarifa hii na michango hii na mapendekezo ya Maazimio haya ya Kamati, Mheshimiwa Rais naamini atayapokea kwa mikono miwili na atahakikisha kwamba haya yote yanaenda kusimamiwa na kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa niaba ya Serikali kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, na hasa Bunge hili ambalo kimsingi ni Bunge la CCM. Kama Bunge la CCM linaikosoa Serikali yake katika chombo muhimu, maana yake Bunge hili linaaminika na wananchi. Kwa hiyo, michango yenu Waheshimiwa Wabunge na maazimio haya, ni kazi ya Serikali kufanyia kazi. Tumeyapokea na naomba kuwahakikishia kwamba tunakwenda kuyafanyia kazi na tutarudisha hapa taarifa wakati kama huu mwaka unaokuja na mtaona mabadiliko makubwa sana Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo hapa yamezungumzwa ni aibu. Accounting Officer huyo huyo anachelewa kulipa, mradi unakuwa penalized, halafu yeye mwenyewe anasaini malipo ya kumlipa tena Mkandarasi huyo huyo. Haiwezi kuwa sawa sawa. Ni lazima tuseme, na tuje tueleze ndani ya Bunge hili, nani alichelewesha? Nani amechukuliwa hatua? Hatua zionekane kweli zikichukuliwa, siyo zisemwe tu zimechukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuweke mfumo wa sasa ambao utaruhusu kwamba yule anayekosea Serikalini anaadhibiwa; na yule anayefanya vizuri, anapongezwa na kusifiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nataka niwahakikishie tumewasikia, nami na wenzangu tunaunga mkono hoja hizi za Kamati na Serikali iko tayari kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza sana siku ya leo pia ni siku nyingine kubwa ambapo Bunge limefanya kazi kubwa likijadili taarifa za Kamati ambazo zina majukumu mengi na nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama pamoja na Makamu wake na Wajumbe wa Kamati hiyo, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rweikiza pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo wamefanya kazi kubwa sana, taarifa zao kama mmeona zinatofautiana maazimio mathalani ya Kamati ya Katiba na Sheria ni maazimio 22 ni maazimio mengi sana, na kwa hiyo niwapongeze sana Kamati hii kwa kazi kubwa ambayo wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi siwezi kuchambua yote, lakini niseme sisi tumepokea kama Serikali na kazi yetu sisi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na uratibu lakini yapo ambayo tuna husika na Kamati hii kwa sababu na sisi tunawajishwa na hii Kamati ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamegusia maeneo kadhaa lakini moja hili la Ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali nataka niwapongeze sana Kamati namna ambavyo wameliweka azimio hili, sisi kwetu ni kazi kwa sababu Ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali ni ofisi ambayo kwa kweli inahitaji kuangaliwa sana na Serikali tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba tunaijengea uwezo ili iweze kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza tu nataka niwahakikishie Wajumbe wa Kamati na Bunge lako tukufu kwamba Serikali ina mpango wa kuifanya Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali kuwa Wakala wa Serikali. Tunataka kuifanya hivyo ili iwe na uwezo wa kufanya shughuli zake kibiahsara, kufanya shughuli zake kwa kufanya maamuzi yenyewe ya ndani kuliko ambavyo ilivyo sasa ambapo mambo mengi wanakuwa hawawezi kuyaamua kwa hiyo kasi ya utendaji wao inapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Serikali inajenga kiwanda kikubwa cha kisasa hapa Dodoma ambacho kitafungwa mitambo ya kisasa na kutakuwa kuna uwezo wa hela kuanzia kununua vitendea kazi maana yake pia eneo la vitendea kazi kama makaratasi yanakuwa ni changamoto kwao na wanashindwa kupata kazi na kuzifanya kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie kwamba hili tumelipokea kwa mikono miwili na tunaenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumzia pia utoaji wa maeneo ya ujenzi wa Mji Mkuu wa Serikali kule Mtumba hadi sasa tumetwaa ekari 2030.88 na tumelipa fidia na fidia hii imeenda vizuri, nataka tuwahakikishie tu kwamba kama kutakuwa kuna haja ya kutwaa eneo lingine hakuna tatizo hamjasikia kelele yoyote Mji wa Serikali tutaendelea kufanya kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo imefanya kazi kubwa sana, ni mimi nimewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati hii, naifahamu kazi hii, wameweza kuchambua sheria 685; siyo jambo dogo na wakabaini dosari 45. Wamefanya kazi kubwa na Kamati hii pamoja na mambo mengine pia imeweka azimio humu kwamba baadhi ya Wizara wakielekezwa wanakuwa hawatekelezi yale maazimio na maelekezo ya Kamati hasa kwenye sheria ndogo ambazo zina dosari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaelewe Waheshimiwa Wabunge kwamba sheria hizi ndogo ndio zinazowagusa watu ambao tunawawakilisha humu ndani kwa hiyo ni lazima maelekezo yanapotoka basi sisi Serikali tunatakiwa tuwe active kuhakikisha kwamba tunafanya mabadiliko au tunajadiliana na Kamati na kueleza sababu kwa nini sheria ziko hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu letu la uratibu kama Ofisi ya Waziri Mkuu litaendelea, tuliwakumbusha, nataka niwahakikishie Kamati kwamba tutaendelea kuwakumbusha tena ili maazimio haya yote toka tumeanza shughuli ya taarifa za Kamati yaweze kutekelezwa kwa kiwango kikubwa ili tukikutana mwakani kipindi kama hiki tuweze kuwa tunazungumza lugha ambayo hata kama hatukutekeleza yote lakini angalau tunasema kuna kazi fulani imefanyika kwa upande wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na ninaomba nimuunge mkono kabisa Mheshimiwa Kigua kwa hoja yake. Hoja yake iko wazi na ni halisi na Watanzania karibu wote wanaguswa na madhara ya upandaji wa bei za mafuta, na jambo la dharura huwa linatatuliwa kwa njia ya dharura. Kwa hiyo, nataka nikubaliane sana na wote wanaozungumza kutatua jambo hili kwa njia ya dharura huku tukiendelea na mipango ya muda wa kati na muda mrefu. Kwa sasa shida ipo na wananchi wanaumia sasa hivi tunavyozungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan halali kwa sababu ya jambo hili; Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango halali; Mheshimiwa Waziri Mkuu halali; na Waheshimiwa Mawaziri na viongozi hatulali kwa sababu jambo hili naamini limetugusa sote na ndiyo maana hata Wabunge hamlali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapokuwa na jambo kama hili, la kwanza ni maelewano kati yetu viongozi, jambo ambalo tayari nayaona mafanikio makubwa kwamba Bunge sasa na Serikali tunashikamana pamoja kujadili positively namna ya kutatua tatizo. Huu ni ushindi wa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana jana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, ameitisha kikao cha Mawaziri wachache, inawezekana tulikuwa wachache, lakini tulijadili jambo hili kwa uzito mkubwa mno na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri akija atazungumza; na hata ile taarifa iliyotokana na kikao kile imezungumza baadhi ya namna ambavyo Serikali itachukua mawazo ya Wabunge katika kutatua tatizo hili.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini…

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, hapa unachangia kama Mbunge. Kwa hiyo, Mbunge anatoa taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Neema Mgaya.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji aliyetoka kuchangia hivi punde; kutokana na unyeti wa suala hili na michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge walioomba suala hili litatuliwe kwa uharaka kutokana na unyeti wa jambo hili, haoni kwamba kuna umuhimu sasa Bunge liahirishwe ili Serikali ipate muda wa kuchakata jambo hili vizuri na ikiwezekana kesho asubuhi mrudi na majibu ambayo yatakwenda kuwapa unafuu wananchi wetu? (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Neema hiyo haiwezi kuwa taarifa ya Waziri, kwa sababu yeye hana uwezo wa kuahirisha Bunge. Pia wakiulizwa; nilimwona Mbunge mwingine naye kauliza maswali kama Serikali imjibu. Hapa Serikali inachangia, mwenye hoja ni Mbunge. Mheshimiwa Omari Kigua ndio mwenye hoja, ndiyo maana atahitimisha yeye. Kwa hiyo, hawa hawawezi kuulizwa maswali ya kujibu na hata Mheshimiwa January Makamba atakaposimama anachangia, siyo anajibu hoja za Wabunge. Msianze kusema haikujibiwa hoja yangu, hapana. Mwenye hoja yuko kule na ni Mbunge.

Mheshimiwa Simbachawene, malizia mchango wako.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwamba Serikali tunaliangalia hili jambo na tunahitaji kwa kweli kutafakari kwa uangalifu mkubwa kwa sababu mnafahamu nyie wote Waheshimiwa Wabunge na tumeshiriki kutunga hapa sheria za fedha mbalimbali. Kuna maeneo ambayo huwezi kugusa kwa sababu ni statutory; yapo kwa mujibu wa sheria na yanatupatia mapato.

Mheshimiwa Spika, leo hii katika maamuzi ya jambo hili tukienda kwa fujo fujo, tukienda bila kutafakari, tujue kwamba tunaenda kuathiri miradi ya maji, tunaenda kuathiri miradi ya barabara, tunaenda kuathiri miradi ya ujenzi wa reli na tunaenda kuathiri miradi mingi ya TARURA. Kwa hiyo, tuwe makini. Haya yote ndiyo yanayotugusa na ni kipimo kwetu sisi Wabunge juu ya kuwaletea maendeleo wananchi wetu na tumeahidi na yapo kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, lazima tuwe makini.

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na mawazo yanayotolewa kwamba tuangalie masuala ya tozo na nini, lakini tumejaribu kuangalia hata hayo ni sehemu kidogo sana, kwa hiyo, inaweza isilete hata huo unafuu. Umakini mkubwa upo, lakini nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla, lazima tukipewa nafasi kama Serikali, muda siyo mrefu tunaweza tukaja na majibu kwa sababu Rais hawezi kushindwa kutupatia majibu Watanzania kwa sababu yeye ni Rais, ana uhalali wa kuamua chochote, hawezi akashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali haiwezi ikashindwa kupata majibu. Kwa msaada huu wa mawazo ya Wabunge, haiwezekani tukashindwa kupata majibu. Mimi naamini tutapata majibu na tutajitahidi kabisa kupunguza kwa namna yoyote ile. Kupata majibu ni kupunguza bei. Ni kupunguza bei, hakuna njia nyingine, ni kupunguza bei. Tunapunguzaje? Tutafanyaje? Njia zote zitatumika kuhakikisha kwamba, tunapunguza. Kama ni ku-subsidize, kama ni kufuta kodi au vyovyote vile, tutafanya, maana sisi ndio tunaotunga sheria na tuko hapa wote na Rais yupo, analiona hili tatizo. Waziri Mkuu yupo, Makamu wa Rais yupo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini tutatoka salama, Waheshimiwa Wabunge watuamini Serikali. Nami nataka niwahakikishie kwamba, tukipewa muda siyo mrefu tunaweza tukaja na majibu.

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Simbachawene kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Bilakwate.

T A A R I F A

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kumpa taarifa mchangiaji anayeendelea na mchango wake: Pamoja na Serikali kuchukua hatua za dharura kupunguza bei ya mafuta, lazima Serikali iangalie huko vijijini ambako ndiko kuna wananchi ambao wanapata shida. Bidhaa zinapanda, lakini sehemu nyingine zinapanda siyo kwa sababu ya kupanda kwa mafuta.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu haiwezekani kitu kilichokuwa kinauzwa shilingi 2,000/= leo hii kimepanda zaidi ya asilimia 200. Kwa hiyo, pamoja na hatua mnazochukua kama Serikali, lazima mwangalie bidhaa huko chini ambazo zimepandishwa zinaendana na uhalisia?

Mheshimiwa Spika, ahsante.

SPIKA: Haya, ahsante sana. Mheshimiwa George Simbachawene.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Bilakwate kwamba gharama nyingi za maisha zinapanda kwa sababu leo hii tunavyozungumza kutokana na maendeleo ya nchi hii ambapo hakuna kitongoji hakina chombo cha moto; hakuna kijiji hakina vyombo vya moto; kila mahali kuna vyombo vya moto; na kwa hiyo, usafiri ni karibu kila mahali. Ukitaka kutoa mazao shambani kwenda sokoni utapakia kwenye pikipiki, utapakia mgonjwa kwenye chombo cha moto. Kwa hiyo, kila kitu kitaguswa tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni kweli tunafahamu kama Serikali na kwamba ni lazima tujitahidi kutumia njia yoyote kuhakikisha kwamba bei ya mafuta inapungua kama jambo la dharura.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Kigua na kwamba Serikali tunachohitaji kwa kweli ni muda wa kutafakari, tukikurupuka hapa tutaharibu na mambo mengine ambayo kwa kweli yapo na tulishayapanga sote kwa kushirikiana, na mengine ni mambo yaliyopitishwa na Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kabisa kwa kuunga mkono hoja iliyoko mbele yetu. Kusema kweli, kama mtu wa Dodoma aliyeko nje ya Bunge amesikiliza hotuba ya mzungumzaji aliyepita, ndugu yangu Mheshimiwa Mchungaji Msigwa, Msigwa anajitafutia chuki isiyokuwa na sababu na watu wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kwanza Mheshimiwa Mchungaji Msigwa anafahamu wazi kabisa na Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania wanafahamu kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekamilisha mpango wa kuhamia Dodoma, iko kwenye asilimia 99, yaani zoezi limekwisha. Serikali imehamia Dodoma, Wizara zote ziko Dodoma, Waziri Mkuu yuko Dodoma, Makamu wa Rais yuko Dodoma amebakia Rais tu yaani biashara hii imekwisha. Jambo likiwa limekwisha mimi nadhani njia nzuri ya mtu mstaarabu ni kupongeza tu kwamba kazi imefanyika vizuri na mambo yote yanaendelea vizuri na hakuna ambalo limeshindwa kufanyika. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, taarifa yake siipokei, kwa sababu uamuzi wa kuhamia Dodoma kwa mara ya kwanza ulifanywa na Serikali ya kikoloni mwaka 1959, na kwa mara ya pili ukafanywa mwaka 1973 na Serikali ya Awamu ya Kwanza na sababu ni hizi zilizopo kwenye preamble kwenye Muswada huu. Sababu hizi za kwenye preamble zimejitosheleza na zinaonesha ukubwa na uzito wa uamuzi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa faida kubwa kwa Watanzania sababu ni kwamba Dodoma ni katikati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuweka Makao Makuu ya nchi Dodoma ni kutafuta urahisi wa kuwahudumia Watanzania. Ni rahisi kwa Watanzania kutoka katika kila pembe ya nchi yetu kuja Dodoma na kurudi kwa gharama nafuu lakini pia ni rahisi kwa Serikali ku-monitor maendeleo na matatizo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja…

T A A R I F A . . .

MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE: Mheshimiwa Spika, tatizo langu wanaonipa taarifa wote ni marafiki zangu, sasa inakuwa shida.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba sababu hizi zitabakia kuwa valid kwa namna yoyote ile. Mimi nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa uamuzi wake wa dhati wa kuamua kwamba sasa kweli tunahamia Dodoma. Wala hakuja na jambo jipya, hili jambo amelikuta lakini yeye ameamua kulifanya kwa vitendo na ndiyo maana tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu hata katika Ilani zetu zote hakuna Ilani ambayo imewahi kuacha kusema tutaendelea kutekeleza mpango wa Serikali wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma, hakuna Ilani imewahi kuacha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi nikupongeze wewe, Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na historia itakukumbuka katika jambo hili kwa kusimama kidete na kusema lazima ije sheria inayotaka uamuzi wa kuhamishia Makao Makuu Dodoma isiwe tena inawekwa kwenye kanuni bali kwenye sheria iliyotungwa na Bunge. Hakika sisi Wana-Dodoma na wananchi wa Dodoma tunakupongeza sana kwa kusimamia jambo hili kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze Wizara ya TAMISEMI pamoja na wadau wote walioshiriki kutengeneza Muswada huu wa sheria hii ambayo tunaipitisha hapa inayo-declare kwamba Dodoma ndiyo Makao Makuu. Ni sheria fupi, ina kurasa mbili, lakini iko loaded, huwezi ukachezea tena habari ya Makao Makuu Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kifungu kile cha 4 inazungumza ugumu wa kubadili tena mawazo haya, yaani hata angekuja nani hawezi kubadili mpaka mabadiliko yale yaweze kupitishwa na theluthi mbili ya Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungani wa Tanzania. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba Serikali imeona ilipe uzito jambo hili kama inavyotoa uzito kwenye vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni heshima kwa uamuzi huu na uamuzi huu kwa kweli umewekewa misingi mizito na mikubwa sana. Tunashukuru sana TAMISEMI kwa kusimamia na kuleta declaration hii ambayo ina uzito unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kifungu hichohicho cha 4(3), kinasema kwamba sheria nyingine zinazoendesha Mamlaka
za Serikali za Mitaa zitapaswa zizingatie uzito wa Makao Makuu na kwa hiyo Makao Makuu haya haitaendeshwa kwa sheria hizi zilizokuwepo na hivyo ni lazima zitungwe sheria nyingine ili ziweze kufanya Makao Makuu itambulike na kuwa na hadhi yanayostahili, hili ni jambo jema. Kwa sababu hii ilikuwa ni declaration basi ifanyike haraka hizi sheria nyingine zinazozungumzwa ziweze kutungwa zinazoendana na uzito wa Makao Makuu maana kwa sheria zilizopo hatuwezi tukaendesha Makao Makuu kwa ufanisi kama ambavyo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudie tena kusema, duniani moja kati ya mikakati na kitu cha kujivunia cha kila nchi katika maamuzi ya mambo yao huwa ni uzito na asili na historia ya nchi hiyo. Kwa sisi Tanzania kulitekeleza jambo hili ambalo liliasisiwa na Baba wa Taifa letu la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwetu sisi hii ni ibada na tutatoka tunajivunia. Leo au kesho sheria hii ikipitishwa tutakuwa tumefanya ibada kubwa na sifa hizi ziende kwa Watanzania wote, kwa viongozi wetu wa Chama cha Mapinduzi na wazee wetu, waasisi wa Taifa letu ambao ni wengi kwa kweli na wengine wako hai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yeyote anayebeza mpango huu anaibeza historia ya nchi yetu. Maamuzi haya yalifanywa kwa uzito maana hata nchi kubwa kama China waliamua kuhamisha Makao Makuu kwa gharama kubwa. Nchi kama Nigeria wameamua kufanya hivyo. Ni kwa sababu wanataka kutekeleza mambo yanayolenga maslahi yao, historia na utamaduni wao. Kwa hiyo, sisi kufanya haya leo kwa gharama ndogo kama ilivyotokea, kwa kweli tumejitoa na tumetoa mchango mkubwa na niipongeze sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 5) ACT, 2021
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana sana sana kwa kunipa nafasi; na kwa kuwa iliyokuwa Idara na ambayo sasa Bunge lako linakaa kwa ajili ya kutunga kuifanya iwe jeshi kamili, ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na ndiyo practice inaonesha kwa nchi wanafanya hivyo.

Mheshiumiwa Spika, niseme ukweli, hata kwa hali ilivyo sasa, ukimwangalia Kamishna Jenerali na wale Askari wote na wamevaa vyeo, tayari wana sura ya kijeshi na wanashiriki katika vikao vya Kamati mbalimbali za Ulinzi na Usalama sambamba na vyombo vingine vya kijeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini leo hii tunataka kutunga sheria hii? Unaposema jeshi, maana yake ni nidhamu. Tunataka chombo hiki sasa kiwe na nidhamu, kifanye kazi kwa amri. Chombo kinachokuwa kinafanya kazi kama Jeshi kinakuwa chini ya Amiri Jeshi Mkuu. Kwa ilivyokuwa, kilikuwa ni kama hakipo chini ya Amiri Jeshi Mkuu, lakini kinafanya kazi na Amiri Jeshi Mkuu. Sasa tunarasimisha kwa sababu kila kitu kipo sawa sawa. Tayari tunakiona kama Jeshi na tayari wanavaa sare ya kijeshi na wana vyeo vya kijeshi, kasoro tu kulikuwa kuna upungufu wa kukifanya kuwa jeshi kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa leo hapa kuna mjadala kwamba kwa kufanya Idara hii kuwa jeshi tunavunja Katiba, la hasha! Nadhani wanaofikiri hivyo wameji-misdirect kwenye Kifungu cha 147 (4) ambacho kimetoa tafsiri ya mwanajeshi. Kilipotoa tafsiri ya mwanajeshi kikasema, maana yake ni askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la kujenga Taifa. Wao wakadhani majeshi yalifungwa hapa, hakutakiwi Tanzania kuundwa jeshi lingine. Hapa ilikuwa ni tafsiri ya mwanajeshi kwa maana ya majeshi yaliyokuwepo wakati huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuanzisha leo jeshi: Je, tunavunja Katiba? Kibali hicho tunakipata wapi? Tunakipata kwenye Ibara ya 147 (1) na ya (2). ya (1) inasema: “ni marufuku kwa mtu yeyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa Serikali kuunda au kuweka Tanzania Jeshi la aina yoyote.” Kwa hiyo, ni Serikali ndiyo inayoweka Jeshi la aina yoyote iliyokuja na Muswada hapa Bungeni ni Serikali na Mkuu wa Serikali ni Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, twende ya pili ya 147(2) inasema hivi Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza kwa mujibu wa sheria kuunda na kuweka Tanzania majeshi ya aina mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wa Tanzania hapo ndiyo ina qualify zaidi kwamba sasa kumbe Serikali ina uwezo wa kuweka majeshi haikuishia kwenye ile kwamba baada ya yale tuliyoelezwa kwenye 147(4) basi iishie pale pale hapana bali yanaweza kuwekwa kwa mujibu wa sheria. Sheria inatungwa na nani? na Bunge 151 inasema kuhusu tafsiri sasa ukienda 151 inasema Jeshi maana yake nini? Jeshi maana yake ni lolote kati ya majeshi ya Ulinzi na ni pamoja na Jeshi lolote jingine lililoundwa na katiba hii au kwa mujibu wa sheria na linalotawaliwa kwa amri ya Jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amri ya Jeshi inatolewa na nani? Na Amiri Jeshi Mkuu. Jeshi lolote maana yake kati ya haya yaliyowekwa kwenye Ibara ya 147(4) na lingine lolote litakalokuja kwa mujibu wa kutungwa sheria bungeni. Kwa hiyo, nadhani kwa wanasheria wazuri nadhani wanafahamu na wameelewa sasa tukibakia hapa tunataka kuleta utata utakuwa ni utata. Lakini nadhani tumeelewana na hata wenzetu waliotoka kwenye kamati kule nadhani wameelewahapa tulikuwa tunanogesha mjadala lakini kimsingi katiba ni maandishi lakini yanahitaji pia tafsiri ya mtu aliyesomea kutafsiri sheria,

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, 2022
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE NA URATIBU): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba nichukue nafasi hii kwanza kabisa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote, najua wapo waliochangia kwa kusema, lakini wapo ambao hawakuweza kuchangia, lakini wameshirikia na sisi katika mjadala wa hoja iliyokuwa mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati. Kama ulivyoona hapa uelewa unasumbua juu ya Muswada huu basi hata huko kwenye Kamati tulikuwa na sisi tunapata shida lakini hatimaye baadaye tulianza kuelewana. Kama pia ulivyoona hapa namna michango ilivyokuwa inaendelea kila mtu anazidi kuwa mbunifu zaidi na hasa katika kujua tofauti ya maafa na majanga ni nini. Wapo wengine wanachanganya majanga na maafa wanajua ni kitu kimoja.

Mheshimiwa Spika, majanga ni yale ya asili au yale yanayotokana na sababu za binadamu, yanapotokea ndio yanasababisha maafa. Maafa ni matokeo ya majanga. Sasa huwezi kutunga sheria ya majanga, yaani wewe unaweza ukatunga sheria ya kuzuia tropical cycle hapana ila effect yake ndio unaweza ukatunga sheria ya kuweza kui-manage. Kwa hiyo duniani kote standard sheria ziko hivyo, wanazungumzia sheria Disaster Management Act, kwa hiyo na sisi tumefuata utaratibu huo.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni sheria yetu hii inahusika na matukio haya kabla, katika level hiyo hiyo kama ya majanga, lakini kabla je, njia gani tunaweza tukapunguza majanga kutokuweza kutokea, yale ambayo kibinadamu tunaweza. Baadaye, wakati yanapotokea majanga na wakati majanga haya yamekwishasababisha sasa madhara ambayo sasa yanaitwa sasa maafa, lakini na namna tutakavyorudisha madhara au kupunguza madhara ya maafa, hapa ndiko tunaweka sheria. Sheria kama sheria haiwezi ika-exhaust everything na ndio maana tuweka nafasi ya Waziri kutunga kanuni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kazi hii nzuri iliyofanyika ya marekebisho makubwa, sheria hii imekuwa na marekebisho makubwa, lakini kwa kweli sifa zote wapewe Kamati yetu, Kamati ya Katiba na Sheria. Wamekuwa walimu wetu wazuri, wametusaidia sana katika ushauri na kwa kuwa sisi Serikali ndio tulikuwa wenye hoja hata hili jedwali la marekebisho tuliloleta kwa kweli ni kazi kubwa iliyofanywa na Kamati. Kwa hivyo nawashukuru Kamati kwa kushirikiana na wataalam wetu wa Wizara tumeweza kufika hatua hii leo hapa.

Mheshimiwa Spika, wachangiaji walio wengi wamepongeza na nimeanza kuwashukuru Wajumbe wa Kamati kwa sababu wamekuwa walimu humu wakielezea uzuri na maeneo mazuri ambayo yamewekwa katika sheria hii. Niwatoe mashaka kwa maeneo machache ambayo yameonyesha kwamba pengine watu hawakuweza kuyaona.

Mheshimiwa Spika, nianze na wote waliochangia ambao ni kama 12, lakini sio rahisi sasa kwa muda niliopewa kuweza kurejea kila mmoja alichokisema labda yale ambayo yalitia wasiwasi sana kwa ajili ya uelewa wa Wabunge pia na Watanzania wanaotusikiliza.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kuchauka alizungumzia jambo lililokuwa lina-reflect tukio lililomkuta yeye, tukio halisi na ni kweli, tumpe pole sana lakini kimsingi lile lilikuwa ni kosa, watu walifanya uhalifu, haliwezi kuwa janga. Watu walikuja wakafanya uhalifu, wakaharibu mali, kwa hiyo wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Linapokuwa janga ni mpaka liwe linachukua sura ya ukubwa wake na haliwezi kurejesheka kwa namna nyepesi, lakini gari utaenda utanunua unakuwa na gari, nyumba utaenda utajenga utakuwa na nyumba, lakini ulikuwa kwa jirani alikusaidia pengine au ulihamia nyumba yako nyingine ya pili. Kwa hiyo halijawa janga. Kwa hivyo nijibu na lile la kusema nani anapanga kiwango kwamba hili ni janga au siyo janga.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa zile kamati tulizoziweka linapowazidi level ya mtaa au Kijiji wanaenda level ya juu kidogo kutoa taarifa. Kwa hiyo zile kamati zinawasiliana level zote wilaya, mkoa mpaka Taifa kulingana na uzito na ukubwa au pengine teknolojia au vifaa vinavyoweza kutumika.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limeguswaguswa ni maelezo aliyotoa Mheshimiwa Salome Makamba. Alijaribu kurejea baadhi ya maeneo, lakini yale yote mashaka yake yako covered na huu Muswada kwenye sura ya tano, masharti ya jumla. Kwa mfano, alisema fedha zikipatikana zinaweza zisifanyiwe shughuli nyingine. Kifungu cha 36(2) kinasema:

“Mtu ambaye atakusanya michango au misaada kwa ajili ya jamii iliyoathirika na maafa na kutoiwasilisha katika kamati….”, yaani fedha yoyote itakayokusanywa kwa ajili ya maafa itakwenda kushughulika na suala hilo tu na sasa tumeliweka kuwa kosa na mtu huyu atachukuliwa hatua. Kwa hiyo tume- improve tumetoka kwenye ile level ambayo ulikuwa na mashaka nayo.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni lile ambalo alizungumzia suala la kinga ya kutokushtakiwa, kinga hii imewekwa kotekote, liko eneo hapa tumesema, kifungu 37:

“Endapo kosa limetendwa chini ya sheria hii na taasisi au kampuni, mtu yeyote ambaye wakati kosa hilo linatendwa alihusika na usimamizi wa taasisi au kampuni hiyo atachukuliwa kuwa yeye ndiye aliyetenda kosa…”

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, atashtakiwa yeye kama yeye kwa sababu hiyo. Pia tukaenda tukasema kuna nature na aina ya matatizo, gari inaungua, mtu yuko ndani, umeamua kuchukua chuma kigumu ukavunja kioo, ukamtoa katika nia yako hiyo njema umesababisha tatizo la mtu yule pengine kuumia zaidi kinyume na matarajio. Nia ilikuwa njema lakini limetokea vinginevyo, ndio tukasema lazima tuwape kinga. Hii ni standard law kwa mwanasheria yoyote anajua, katika sheria yoyote na hasa wale wataalam wa sheria zile za Law of Torts, provisions kama hizi ni lazima zinakuwepo nia njema yaani lazima iwe nia njema. Kwa hiyo tumewapa kinga hao, kwa sababu ya hiyo nia njema. Inapimwa kwa kuangalia vitu vingi sana, sasa is a science, tukienda sasa huko tunafika mbali, lakini kimsingi sheria nyingi tunaziandika hivyo kwa madhumuni hayo.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine ni lile ambalo limesemwa na Waheshimiwa Wabunge hapa, juu ya maeneo yale ambayo yatagusa watu kupata uelewa na uwajibikaji. Tumeweka masuala ya majanga isiwe watu wanasema tu, Ofisi ya Waziri Mkuu au mtu fulani, ili watu wote waweze kushiriki. Kwa hiyo, nakubaliana kabisa na wale waliosema kwamba, elimu izidi kutolewa watu wajue na zile angalau standard equipment katika hizi Kamati katika Mikoa na katika maeneo yetu kuwa na vifaa vya msingi hata vya kuweza kusaidia.

Mheshimiwa Spika, unakuta Wilaya nzima haina hata maturubai. Yaani likitokea tatizo ni Wilaya nzima na ni chombo cha utawala kabisa kiko pale kuna Mkuu wa Wilaya, kuna nani, lakini hawana maturubai ambapo hata watu wakipata matatizo ya mvua tu mnaanza kutafuta Red Cross! sasa tunaonesha kwamba, hatuna utayari. Kwa hiyo, utayari huu ni jukumu la kila mmoja na tumesema kwenye sheria hii kwamba, sasa itakuwa ni lazima kwamba, lazima hizi mamlaka zetu hizi za utawala ambazo zimewekewa mfumo huu wa sheria hii basi ziwe na wajibu wa kuwa na mazingira haya ya maandalizi.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema awali, siyo rahisi kuyajibu yote, lakini yale ambayo pengine yatahitajika ufafanuzi tunaweza tukafanya hivyo kwa maandishi, lakini kimsingi nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri ambayo imelenga kujenga. Kipekee nirudie tena kuwashukuru sana Kamati yetu chini ya viongozi wetu mahiri Mheshimiwa Dkt. Joseph Mhagama pamoja na Mheshimiwa Najma Giga, wametusimamia vizuri na tumetoka na sheria nzuri. Mimi naamini changamoto yetu itakuwa ni utekelezaji tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutajitahidi sana Serikali katika kutunga kanuni, tutunge kanuni ambazo zitakuwa zinasaidia katika utekelezaji chanya wa sheria hizi. Wengi wamesisitiza kwamba, kwenye kanuni kwa kweli, tujaribu kutengeneza kanuni zitakazosaidia kupunguza changamoto za watu wetu ambazo ni ndogondogo katika misingi midogomidogo, lakini ndizo zinazowagusa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya ninaomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango wa Mwaka 2023.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, na mimi kama wenzangu nikutakie kila la kheri kwamba unakwenda kugombea nafasi ya kuwa Spia wa Bunge la Dunia. Nafasi hii ni kubwa na kwa hiyo kwa kweli Watanzania wote tuungane kumwombea Mheshimiwa Spika wetu Dkt. Tulia Ackson ili akaipeperushe bendera ya nchi yetu. Heshima hii kwa kweli siyo yako, wala siyo ya familia yako, ni heshima ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuhitimisha nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama kiongozi wetu wa Taifa letu la Tanzania, lakini kama ambaye amebeba dhamana ya Watanzania wote katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata maendeleo na shabaha zake zote na malengo yetu ya kupambana na maadui watatu; ujinga, umaskini na maradhi yanashughulikiwa kikamilifu na katika kufanya hivyo Mheshimiwa Rais ndiyo maana amekuja na azma ya kuhakikisha kwamba tunaanzisha Tume ya Mipango katika kuifanya mipango ya nchi yetu iweze kuratibiwa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chimbuko la suala hili, kwanza kabisa ni Mheshimiwa Rais mwenyewe, lakini pia na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili. Katika bajeti zetu mbili zilizopita Waheshimiwa Wabunge walizungumza sana juu ya umuhimu wa kuwa na Tume ya Mipango na kwa umuhimu huo, Serikali yetu sikivu na Mheshimiwa Rais akaamua kuanzisha mchakato huu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipoanzisha mchakato huu alitoa maelekezo ya kwamba Tume hii ifanyiwe mchakato wa haraka na Waheshimiwa Wabunge leo hii tukipitisha sheria hii Mheshimiwa Rais ataisaini na itaanza kutumika tarehe 1 Julai kwa sababu anaisubiri kwa hamu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo rasilimali nyingi kama Taifa. Tunao watu, Watanzania ambao wameelimika vizuri sana, lakini tunayo rasilimali ardhi, lakini tunayo amani katika nchi yetu, lakini tunazo rasilimali mbalimbali hata kuzitaja ni nyingi mno. Tuna mito, mabonde, bahari, misitu, wanyama, madini na tuna kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vitu hivi bila kufanyiwa utaratibu wa kuhakikisha kwamba vinasimamiwa na kuratibiwa vizuri unaweza ukavikuta badala ya kusaidiana katika kuleta maendeleo vinagombana na ndiyo maana imeelezwa hapa na Waheshimiwa Wabunge ambao kwa kweli nataka niwashukuru takribani Wabunge wote 15 wamechangia huku na huku na jumla ya hoja zilizotolewa hapa ni nyingi na naamini hata ambao hawakusema wangeweza kuyasema haya haya juu ya umuhimu wa hii sheria ya kuanzisha rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Bunge, Tume ya Mipango kwa ajili ya kutekeleza mipango ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia. Niwashukuru sana kwa sababu hakuna hata mmoja aliyepinga, lakini niishukuru sana Kamati. Kamati hii ni Kamati yenye watu weledi, ni Kamati yenye watu makini. Kamati hii imekuwa ndiyo chachu ya mafanikio makubwa ya maboresho ya Muswada huu mpaka hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uzito wa kazi ya Kamati, lakini usikivu wa Serikali, unauona kwa marekebisho mengi iliyofanya kupitia kwenye majedwali ya marekebisho. Ukiona majedwali ya marekebisho yalivyo marefu ujue Kamati imefanya kazi yake kubwa, lakini majedwali yakiwa marefu maana yake Serikali nayo imekuwa sikivu. Kwa hiyo nataka niwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi katika kuhitimisha sijaona ambalo halijasemwa hapa na Waheshimiwa Wabunge hata ambao walikuwa hawajasoma vizuri na wako nje ya Kamati, Wajumbe wa Kamati wamejitahidi sana kujibu na niwashukuru sana Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Kyombo na Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Mhagama, lakini pia na Wajumbe wengine wote ambao wamejitahidi kutoa ufahamu mkubwa walioupata kwa wale ambao walikuwa hawajapitia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako maeneo yamesemwa kwamba Rais anawezaje kuwa yuko kwenye Tume lakini huku ni kwenye kifungu kile cha 7, ni kwamba ile kuwajibika kwenye taarifa kwenye Baraza la Mawaziri tumekifuta, kwa sababu Serikali imekuwa sikivu na Kamati imefanya kazi yake sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi hakuna controversy yoyote katika Miswada yote miwili na kwenye huu wa Usalama wa Taifa, kimsingi Wabunge wote wameunga mkono. Eneo hili ambalo limeleta kidogo mjadala la kinga dhidi ya Maafisa wetu wa Usalama wanapokuwa wakitekeleza kazi zao, ni wakati wakitekeleza kazi zao kwa majukumu yaliyosemwa kwa mujibu wa sheria. Siyo wewe ni Afisa wa Usalama unakwenda kugombana huko mtaani, umeitumia silaha yako vibaya, eti ukasema una kinga, hapana. Sheria itachukua mkondo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazungumzia kinga katika kulinda usalama wa nchi na pengine tuna underrate jukumu la chombo hiki, kwa sababu pengine tunafikiria domestically, lakini chombo hiki kinalinda usalama wa nchi dhidi ya maadui wa nje zaidi. Kinalinda usalama wa nchi yetu juu ya mipango yetu ya maendeleo. Vita siku hizi ipo kwenye uchumi zaidi, chombo hiki kinalinda usalama dhidi ya mipango yetu ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kimsingi ni kama tumekubaliana na kwa wale Waheshimiwa Wabunge ambao walikuwa wana wasiwasi lakini pia wananchi walioko huko nje tunaona mijadala mbalimbali hakika ni kwa vile hawajapata fursa ya kupitia yale mambo mazuri ambayo Kamati hii imesimamia lakini Waheshimiwa Wabunge wanayafahamu, taratibu tunaweza tukakuta na wenzetu tuko pamoja kwa sababu hakuna jambo lililofanywa hapa kwa nia yoyote ile mbaya. Msingi mkubwa ni amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu, lakini na kulinda nchi yetu kama jukumu la kila Mtanzania na wenzetu hawa wamepewa jukumu hilo na kwa hivyo lazima tuwakinge dhidi ya mambo fulani fulani ambayo wanaweza wakawa wanatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la kinga limesemwa sana na huko mtaani kwamba wana kinga kwa sababu watafanya jambo fulani. Tunazungumzia kinga dhidi ya magaidi, katika kutekeleza jambo hili anapopambana na magaidi mtu wa Usalama wa Taifa halafu ikatokea silaha yake imefyatuka imemuumiza mtu, wewe unasema achukuliwe hatua lakini umemkinga nurse akimchoma sindano mgonjwa akafa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinga hizi zimetolewa katika sheria mbalimbali katika nchi yetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja Mheshimiwa Waziri:

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: …na Waheshimiwa Wabunge wote wanafahamu. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na kupitia kwao Watanzania wote tuna jukumu sisi kama Watanzania kuhakikisha kwamba tunalinda nchi yetu dhidi ya maadui walio ndani na walio nje ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kumalizia, naomba niwashukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini Katibu Mkuu wa Uwekezaji Dkt. Tausi Kida; CPD Onorius Njole; pia Katibu Mkuu Ikulu, Ndugu Mululi Mahendeka; Katibu Mkuu, Ofisi ya Utumishi kwa ushirikiano pamoja na utaalam wote waliotupatia katika kuhakikisha kwamba jukumu hili tunalitekeleza kuhakikisha kwamba sheria hizi zinatungwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo kupitia muda huu ulionipa, sasa nichukue nafasi hii kutoa hoja kwa Miswada yote miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Yatokanayo na Urekebu wa Sheria wa Mwaka 2023 .
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, na mimi kama wenzangu nikutakie kila la kheri kwamba unakwenda kugombea nafasi ya kuwa Spia wa Bunge la Dunia. Nafasi hii ni kubwa na kwa hiyo kwa kweli Watanzania wote tuungane kumwombea Mheshimiwa Spika wetu Dkt. Tulia Ackson ili akaipeperushe bendera ya nchi yetu. Heshima hii kwa kweli siyo yako, wala siyo ya familia yako, ni heshima ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kuhitimisha nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama kiongozi wetu wa Taifa letu la Tanzania, lakini kama ambaye amebeba dhamana ya Watanzania wote katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata maendeleo na shabaha zake zote na malengo yetu ya kupambana na maadui watatu; ujinga, umaskini na maradhi yanashughulikiwa kikamilifu na katika kufanya hivyo Mheshimiwa Rais ndiyo maana amekuja na azma ya kuhakikisha kwamba tunaanzisha Tume ya Mipango katika kuifanya mipango ya nchi yetu iweze kuratibiwa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chimbuko la suala hili, kwanza kabisa ni Mheshimiwa Rais mwenyewe, lakini pia na Waheshimiwa Wabunge wa Bunge hili. Katika bajeti zetu mbili zilizopita Waheshimiwa Wabunge walizungumza sana juu ya umuhimu wa kuwa na Tume ya Mipango na kwa umuhimu huo, Serikali yetu sikivu na Mheshimiwa Rais akaamua kuanzisha mchakato huu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alipoanzisha mchakato huu alitoa maelekezo ya kwamba Tume hii ifanyiwe mchakato wa haraka na Waheshimiwa Wabunge leo hii tukipitisha sheria hii Mheshimiwa Rais ataisaini na itaanza kutumika tarehe 1 Julai kwa sababu anaisubiri kwa hamu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo rasilimali nyingi kama Taifa. Tunao watu, Watanzania ambao wameelimika vizuri sana, lakini tunayo rasilimali ardhi, lakini tunayo amani katika nchi yetu, lakini tunazo rasilimali mbalimbali hata kuzitaja ni nyingi mno. Tuna mito, mabonde, bahari, misitu, wanyama, madini na tuna kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vitu hivi bila kufanyiwa utaratibu wa kuhakikisha kwamba vinasimamiwa na kuratibiwa vizuri unaweza ukavikuta badala ya kusaidiana katika kuleta maendeleo vinagombana na ndiyo maana imeelezwa hapa na Waheshimiwa Wabunge ambao kwa kweli nataka niwashukuru takribani Wabunge wote 15 wamechangia huku na huku na jumla ya hoja zilizotolewa hapa ni nyingi na naamini hata ambao hawakusema wangeweza kuyasema haya haya juu ya umuhimu wa hii sheria ya kuanzisha rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Bunge, Tume ya Mipango kwa ajili ya kutekeleza mipango ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia. Niwashukuru sana kwa sababu hakuna hata mmoja aliyepinga, lakini niishukuru sana Kamati. Kamati hii ni Kamati yenye watu weledi, ni Kamati yenye watu makini. Kamati hii imekuwa ndiyo chachu ya mafanikio makubwa ya maboresho ya Muswada huu mpaka hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uzito wa kazi ya Kamati, lakini usikivu wa Serikali, unauona kwa marekebisho mengi iliyofanya kupitia kwenye majedwali ya marekebisho. Ukiona majedwali ya marekebisho yalivyo marefu ujue Kamati imefanya kazi yake kubwa, lakini majedwali yakiwa marefu maana yake Serikali nayo imekuwa sikivu. Kwa hiyo nataka niwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi katika kuhitimisha sijaona ambalo halijasemwa hapa na Waheshimiwa Wabunge hata ambao walikuwa hawajasoma vizuri na wako nje ya Kamati, Wajumbe wa Kamati wamejitahidi sana kujibu na niwashukuru sana Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Kyombo na Mwenyekiti Mheshimiwa Dkt. Mhagama, lakini pia na Wajumbe wengine wote ambao wamejitahidi kutoa ufahamu mkubwa walioupata kwa wale ambao walikuwa hawajapitia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako maeneo yamesemwa kwamba Rais anawezaje kuwa yuko kwenye Tume lakini huku ni kwenye kifungu kile cha 7, ni kwamba ile kuwajibika kwenye taarifa kwenye Baraza la Mawaziri tumekifuta, kwa sababu Serikali imekuwa sikivu na Kamati imefanya kazi yake sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi hakuna controversy yoyote katika Miswada yote miwili na kwenye huu wa Usalama wa Taifa, kimsingi Wabunge wote wameunga mkono. Eneo hili ambalo limeleta kidogo mjadala la kinga dhidi ya Maafisa wetu wa Usalama wanapokuwa wakitekeleza kazi zao, ni wakati wakitekeleza kazi zao kwa majukumu yaliyosemwa kwa mujibu wa sheria. Siyo wewe ni Afisa wa Usalama unakwenda kugombana huko mtaani, umeitumia silaha yako vibaya, eti ukasema una kinga, hapana. Sheria itachukua mkondo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazungumzia kinga katika kulinda usalama wa nchi na pengine tuna underrate jukumu la chombo hiki, kwa sababu pengine tunafikiria domestically, lakini chombo hiki kinalinda usalama wa nchi dhidi ya maadui wa nje zaidi. Kinalinda usalama wa nchi yetu juu ya mipango yetu ya maendeleo. Vita siku hizi ipo kwenye uchumi zaidi, chombo hiki kinalinda usalama dhidi ya mipango yetu ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kimsingi ni kama tumekubaliana na kwa wale Waheshimiwa Wabunge ambao walikuwa wana wasiwasi lakini pia wananchi walioko huko nje tunaona mijadala mbalimbali hakika ni kwa vile hawajapata fursa ya kupitia yale mambo mazuri ambayo Kamati hii imesimamia lakini Waheshimiwa Wabunge wanayafahamu, taratibu tunaweza tukakuta na wenzetu tuko pamoja kwa sababu hakuna jambo lililofanywa hapa kwa nia yoyote ile mbaya. Msingi mkubwa ni amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu, lakini na kulinda nchi yetu kama jukumu la kila Mtanzania na wenzetu hawa wamepewa jukumu hilo na kwa hivyo lazima tuwakinge dhidi ya mambo fulani fulani ambayo wanaweza wakawa wanatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la kinga limesemwa sana na huko mtaani kwamba wana kinga kwa sababu watafanya jambo fulani. Tunazungumzia kinga dhidi ya magaidi, katika kutekeleza jambo hili anapopambana na magaidi mtu wa Usalama wa Taifa halafu ikatokea silaha yake imefyatuka imemuumiza mtu, wewe unasema achukuliwe hatua lakini umemkinga nurse akimchoma sindano mgonjwa akafa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinga hizi zimetolewa katika sheria mbalimbali katika nchi yetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Dakika moja Mheshimiwa Waziri:

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: …na Waheshimiwa Wabunge wote wanafahamu. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge na kupitia kwao Watanzania wote tuna jukumu sisi kama Watanzania kuhakikisha kwamba tunalinda nchi yetu dhidi ya maadui walio ndani na walio nje ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kumalizia, naomba niwashukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini Katibu Mkuu wa Uwekezaji Dkt. Tausi Kida; CPD Onorius Njole; pia Katibu Mkuu Ikulu, Ndugu Mululi Mahendeka; Katibu Mkuu, Ofisi ya Utumishi kwa ushirikiano pamoja na utaalam wote waliotupatia katika kuhakikisha kwamba jukumu hili tunalitekeleza kuhakikisha kwamba sheria hizi zinatungwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo kupitia muda huu ulionipa, sasa nichukue nafasi hii kutoa hoja kwa Miswada yote miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.