United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka Mamlaka ya Maji
Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Morogoro (MORUWASA) kuhakikisha
inaweka mikakati thabiti ya kudhibiti upotevu wa maji.
Agizo hilo
lilitolewa jana Mkoani Morogoro na Mwenyekiti wa Ujumbe wa Kamati hiyo,
Shally Raymond wakati Kamati ilipotembelea miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Mamlaka hiyo.
Alisema Kamati imeshtushwa na upotevu wa maji wa asilimia 40 ambao ni mkubwa ukilinganishwa na Mamlaka nyingine za maji nchini.
"Tunataka
mfanye jitihada za makusudi kupunguza upotevu huu wa maji kwa kuwa maji
haya mnatumia gharama kubwa kwa ajili ya kuyazalisha na kuyatibu hivyo
yanapokuwa yanapotea yanaleta hasara kwa Mamlaka," alisema.
Aidha,
Mwenyekiti hiyo aliitaka Mamlaka hiyo kuchukua hatua za kuwaondoa
wananchi wanaolima na kuishi milimani na karibu na vyanzo vya maji kwa
kuwa wanasababisha uharibifu katika vyanzo hivyo.
"Waelimisheni
kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji ili na wao pia waone kwamba
wanawajibika kuvitunza vyanzo hivyo kwa ajili ya maisha yao ya sasa na
ya baadae," alisema.
Kamati hiyo pia iliitaka Wizara ya Maji
kuhakikisha inakamilisha miradi minne ya maji katika Miji midogo ya
Gairo, Mvomero,Kilosa na Tuliani iliyotakiwa kukamilika mwaka 2012.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA Nicholaus Angubwike
alisema Mamlaka hiyo inalitambua tatizo hilo la upotevu wa maji na
kwamba imeanza mkakati maalum wa kukabiliana na upotevu wa maji.
"Hata
sisi suala la upotevu wa maji ambalo pia linasababishwa na uchakavu wa
mitambo linatuumiza, tumeanza mikakati maalumu ikiwemo kuwakamata wezi
wa maji na kuwapeleka mahakamani," alisema.