Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ussi Salum Pondeza (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kushiriki katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nijielekeze kwenye maeneo ya Jimbo langu la Chumbuni ambalo lina matatizo ya Kituo cha Polisi ambayo bajeti ya mwaka jana niliyasema na kikaahidiwa kuwa nitapatiwa matengezo na nitapatiwa kituo katika Jimbo langu la Chumbuni Zanzibar, mpaka sasa hivi sijapata. Nilikuwa na kituo kimoja tu kidogo ambacho mpaka sasa hivi nacho hakifai kinavuja, kazi hazifanyiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa zaidi ambalo nataka kulisema hapa leo ni vitendea kazi vya Jeshi la Polisi hususan Zanzibar. Polisi wetu hawana vifaa vya kutendea kazi sana hasa hasa Jeshi letu la Traffic. Unakuta Jeshi la Traffic wanaongoza magari kwa kutumia simu zao za mkononi. Redio hawana, hata sectionnne hazifiki, vitendea kazi ambavyo ni muhimu. Tumeshuhudia Zanzibar mara mbili ama mara tatu Viongozi wetu Wakuu wa nchi, madereva wanaingilia misafara yao kutokana na kutokuwepo kwa taarifa ambazo zinakuwepo kabla,hii yote ni kutokana na ukosefu wa vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Jeshi la Polisi Zanzibar lina deni katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika vikosi vyake vya Jeshi la Kujenga Uchumi yaani JKU ni kitengo cha NIDA mamlaka ya Vitambulisho, wanadaiwa karibu milioni 172 ambazo hawajazilipa mpaka sasa hivi. Nataka kujua leo hapa lini watazilipa fedha hizi milioni 172 katika JKU ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho napenda ambacho napenda kushauri Jeshi letu la Polisi au Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, linaonaje likafikiria kuweka sheria hata wale ambao ni Makamishna wa Jeshi hili. Kwa mfumo uliopo nafahamu wapo Makamishna tisa, kuanzia Kamishna Kaniki, Kamishna Amdan, Kamishna Musa na wengine wapo tisa, wakistaafu anayefahamika kwa mafao ni IGP peke yake. Kwa nini, Jeshi la Polisi lisiwe na mfumo kama Jeshi la Wananchi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo amewasilisha hotuba yake hii ya Wizara ya Nishati na Madini. Pia niwapongeze Watendaji Wakuu wa Wizara hii ya Nishati akiwemo Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wakurugenzi wa REA, TPDC kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi vizuri na wanaweza kufikia yale malengo ambayo sote matarajio yetu ni kuiona Tanzania ya viwanda inakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema maneno haya kwa sababu tunaposema Tanzania ya viwanda tunaitaka bila umeme wa uhakika basi hatuwezi kuipata, lakini kwa kasi ambayo wanakwenda nayo Mawaziri hawa na Watendaji wao, tuna uhakika vission yetu ya 2020 tunao uwezo wa kufikia malengo haya. Tunachotakiwa ni sote humu ndani kama Wabunge kuishauri Serikali na kuwasaidia hawa katika juhudi zao ambazo wanaziendeleza katika kufanikisha upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika ili tuweze kufikia malengo yetu yale ambayo tunayakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nishauri Wizara na Mheshimiwa Waziri kwa upande wa REA. Mimi ni Mjumbe wa Kamati tumetembelea miradi na tumekutana na matatizo mengi ikiwepo scope of work kwa maana kwamba maelekezo yanatolewa kwenye vitabu lakini mkienda field sivyo ilivyo. Hili ni tatizo kubwa ambapo wakandarasi wengi ambao tumewahoji hawana majibu mazuri, wanakwambia mimi scope yangu mwisho hapa, lakini wananchi wanalalamika wanasema katika kijiji chetu mradi umekuja lakini waliopata ni watu wanne, watano hawazidi 10. Kwa maana, hiyo upatikanaji au ile dhana kamili ya kusema wananchi wote watapata umeme wa REA inakuwa haifikiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine nataka nilizungumzie nalo ni kuhusu REA kupewa pesa kwa wakati. Sehemu zote ambazo tumetembelea, miradi tunaikuta imesimama au inasuasua tatizo kubwa ni fedha. Ukiwauliza kwa nini fedha hampati, tumejaribu kuwahoji REA na Wizarani, tatizo kubwa ni Wizara ya Fedha kutotoa fedha kwa wakati. Hili suala linazungumzwa karibu katika kila Wizara kwamba Wizara ya Fedha imekuwa kila pesa ambayo inatengwa lazima iwe inafanyiwa uhakiki, hatukatai kufanya uhakiki, lakini kuna mambo mengine ambayo kama hii REA ambayo iko ring fenced inachukua muda. Kuna time watu hawajalipwa imefika mpaka miezi nane, watu wanasubiri lini watalipwa ili waweze kupata material. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema sasa tuna matarajio ya kufika mpaka mwaka 2020...

TAARIFA . . .

MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sikubaliani naye na taarifa siipokei, hii tunajua ipo na akitaka ushahidi nafikiri kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameeleza, hiyo taarifa yake siipokei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maana kuwa REA lazima wapewe pesa kwa wakati ili tuweze kufikia malengo yetu yale ambayo tumekusudia ya kuhakikisha uchumi wetu unatoka uchumi wa chini na kuwa uchumi wa kati. Hapa kila Mjumbe ambaye amesimama, jambo kubwa ambalo tunalizungumzia ni jinsi gani pesa zitatoka Wizara ya Fedha kuja REA ili wakandarasi waweze kulipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie kwa ruhusa yako ni kuhusu tatizo la deni la Zanzibar. Kuna taarifa ambayo mazungumzo yameanza na yanaendelea kwa sababu imekuwa kuna sintofahamu katika suala la deni la TANESCO, katika taarifa zao wanasema wanadai hivi lakini reality haiko hivyo. Kwa sababu mazungumzo yameanza kufanyika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho naomba hili aliweke wazi limefikia hatua gani na kuna nini ambacho kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni tatizo kubwa sana kwetu Wazanzibar kila mwaka linajirejea hili na inafika pahali watu tunaonekana labda kama vile tunapata kitu cha bure au hatulipi, tunasaidiwa. Kwa sababu sisi tunajiamini na tuna uwezo wa kulipa current bill kabisa kama tunavyolipa sasa hivi, nakutaka Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa aje atoe taarifa hii ya kuhusu Zanzibar tunavyolipa umeme, deni na current bill ambayo tunatumia kila mwaka. Kuhusu suala la bei tutalizungumza baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, sitaki niendelee sana maana nitatoa utamu wa haya maneno yangu ambayo nimemalizia, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi hii. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunijalia afya njema, lakini la pili nataka nizungumzie zaidi hii Wizara yetu ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya mambo ambayo humu kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri ameeleza kuwa kuna Kamati ile ya SMT inayashughulikia, lakini muda mrefu umepita na kila siku tunapata majibu ya kuwa kero hizi zinashughulikiwa. Nataka nijielekeze sehemu moja tu katika huduma ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasemwa Zanzibar tunadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 131, lakini ukweli uliokuwepo hazifiki hata shilingi bilioni 40. Kila mwezi tumekuwa tukilipa current bill still wenzetu upande wa pili ambao ni TANESCO wamekuwa wakituwekea bill ile ile ya kutuambia tunadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 130. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, hivi juzi juzi tu tulipokuwa katika Kamati ya Nishati na Madini tuliweza kui-raise hoja hiyo, Mheshimiwa Waziri upande wa huku akawaita na watu wa Zanzibar, lakini wamekaa bila kupata muafaka wa kusema juhudi hizi zinaendelea kuchukuliwa. Ukweli uliokuwepo na ushahidi upo sisi hatudaiwi zaidi ya shilingi bilioni 133. Cha kushangaza kila mwaka imekuwa kelele Zanzibar inadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 130, Zanzibar hatulipi umeme, lakini ushahidi upo ambapo tunalipa lakini hii kero imekuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeamua kulisema hili kwa sababu hii ni kero ambayo inawakera sana Wazanzibar kwa maana kuna baadhi ya watu hufikia stage ya kusimama humu ndani ya Bunge na kuanza kusema Wazanzibar tunawabeba tu, umeme wanatumia hawalipi, kuna baadhi ya mambo hivi na hivi wao kazi yao ni kupewa tu. Ukweli uliokuwepo hizi kero zingekuwa zinashughulikiwa kwa muda kama ilivyoelezwa katika hotuba ya Waziri basi haya yote yasingekuwa yanajitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa pili imekuwa ni kawaida kuambiwa kila siku vinakaa vikao baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, lakini hakuna hata mara moja ambapo unakuja mrejesho kwamba watu wamekaa na wameamua hivi na kero hii imeisha na imebaki kero hii. Sisi tunaelewa kero ni sehemu ya maisha na changamoto ni sehemu ya maisha, lakini tupewe zile kero ambazo kweli zinatuhusu sisi Wazanzibari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofika mahali jambo tunalifanya kwa kutimiza wajibu wetu, lakini leo hii wenzetu upande wa pili wanafika mahali wakaona kama labda sisi tunasaidiwasaidiwa tu bila kuwa na nguvu yetu wenyewe kusema kweli hatuwezi kujisikia vizuri upande wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilizungumze ni kuhusu mambo ya biashara. Kwenye ufanyaji wa biashara kuna utozaji wa kodi mara mbili. Zanzibar ukinunua mzigo Dar es Salaam let say Tanzania Cable unapeleka Zanzibar huku unalipa VAT na ukifika Zanzibar pia ulipe VAT. Hili suala linawaumiza wananchi wetu wa chini kwa sababu tunalipa VAT mara mbili maana yake tunalipa VAT asilimia 36. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili mwaka 1995 mpaka 2000 halikuwepo, kulikuwa na utaratibu baina ya Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Zanzibar kubadilishana zile tax invoice kwa ajili ya kudai upande wa pili lakini unalipia VAT sehemu moja last destination. Leo hii ukitoa mzigo Zanzibar ambapo umelipia kila kitu ukifika Dar es Salaam lazima pia ulipe. Sasa hili linaonesha jinsi gani sisi upande wa pili tunapata uonevu au tusiseme uonevu tuseme labda kuna jambo ambalo halijakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri katika kikao cha tarehe 28 basi hili ni jambo moja la msingi lichukuliwe kwa umuhimu wake na kwa ufasaha kabisa tupate majibu ya haraka. Kwa sababu wananchi wetu wanafika mahali wanaudharau Muungano wanasema una faida gani maana mtu akinunua tv Dar es Salaam akienda nayo Arusha halipi kodi lakini ukichukua tv Dar es Salaam ukienda nacho Zanzibar inabidi uilipie tena kodi. Hivi ni vitu ambavyo vinaturudisha nyuma sisi kama Wazanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba kuna mambo ambayo yana faida ya Muungano lakini hayaelezwi kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya Muungano ambayo na sisi tunakiri inatusaidia kama MIVARP, tumepata masoko, barabara zimejengwa zote zile ni faida ya Muungano, lakini wananchi wa chini hawana habari kama hivi vitu vinatoka kwenye Serikali ya Muungano. Wanafika mahali wanakwambia kwa style hii sisi Muungano hatuuoni faida yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mzanzibari namba moja nakubali Muungano huu ni mzuri isipokuwa unahitaji kurekebishwa na kero hizi ndogo ndogo ndizo ambazo zinazaa haya mengine yote ya kusema tuna kero na kuona Muungano hauna faida lakini kiukweli una faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri January Makamba kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Kuna baadhi ya mambo mengi ambayo ameyatatua yeye kwa kipindi chake ambayo yalikuwa ni kero kubwa ambazo sisi tunazifahamu.

Tunampongeza sana na tunataka tu kumwambia kwamba, aendeleze juhudi zake kutoka hapa alipofika na haya mengine inshallah Mwenyezi Mungu atamjalia ayamalize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliseme ni kuhusu kodi ya magari. Ukitoa gari Zanzibar lina namba ya ZNZ ukifika nalo Dar es Salaam unazuiwa lakini ukitoa gari Tanzania Bara ina namba za STK, TZD zote zinaenda Zanzibar na zinatumika. Magari yetu Zanzibar yakija Tanzania Bara wanaya-treat kama magari ya nje kitu ambacho siyo cha maana kweli kweli na hii yote ni nchi moja. Unapokuja hapa ukisema nchi yetu ni ya Muungano lakini magari ya Tanzania Bara yakija Zanzibar …

T A A R I F A . . .

MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naipokea taarifa hiyo kwa sababu ndiyo kitu nilichokuwa nakisema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la ushuru hizi ni zile kero ndogo ndogo ninazomwambia Mheshimiwa Waziri January Makamba azitazame. Zile kero ambazo zinatukabili ambazo zinatakiwa kuuweka sawa huu Muungano wetu basi ni kama hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sioni sababu kwa nini gari ikitoka Zanzibar inakuwa treated kama gari ya kutoka nje, lakini gari ya Kenya au Uganda ikifika hapa inapewa kibali na mtu anatumia mpaka anamaliza shida zake. Kwa nini sisi Zanzibar na sisi tusiwe hivyo na hii ni nchi moja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafika mahali tunajiuliza aah au sisi huku tumeegemeaegemea tu, tunabebwabebwa, lakini sisi tuna haki zetu na tumesimama kwa miguu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo Mheshimiwa Waziri nakuomba unapokuja kuhitimisha basi moja ya mambo ambayo tunataka utupe ufafanuzi Wazanzibar ni kuhusu magari na mizigo yao inavyokuja na kwenda jinsi gani VAT inachukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi niwe miongoni wa wachangiaji wa hotuba hii nzuri ya Wizara ya Nishati ambayo kusema kweli inafanya vizuri. Pia nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake, pamoja na Naibu Waziri lakini na watendaji wote wa TANESCO kiujumla wao wanafanya kazi moja nzuri sana ambayo wote tunaikubali. Kiukweli ni wizara ambayo kwa kiasi kikubwa imetutoa tongo machoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina jambo moja ambalo nataka nilielezee au nimpe ujumbe Mheshimiwa Waziri. Kuna tatizo ambalo lipo muda mrefu baina ya TANESCO na ZECO kuhusiana na bei ya umeme. Mimi ni mjumbe wa Kamati na mara nyingi nimekuwa nikilisema hili lakini utaratibu wake au hatua zake zinavyochukuliwa zinachukua muda kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nimeamua kulisema hapa kama jambo mahsusi, ambalo nataka niiambie Serikali yangu na Mheshimiwa Waziri, tatizo ambalo lipo hapa ZECO wanauziwa umeme na TANESCO kwa bei ya Sh.160.4 kwa KV moja. Hata hivyo, kutokana na uchumi wa Zanzibar, ZECO wanasema hawawezi kununua kwa bei hiyo, wana uwezo wa kununua KV moja kwa Sh.130. Hili suala limekuwa linakaliwa vikao muda mrefu bila kupata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo ninaloliona mimi mpaka nikaamua kulizungumzia hapa, kama mtakumbuka ndani ya miaka miwili, mitatu nyuma kuna jambo lilikuwa kubwa zaidi katika mambo ya umeme baina ya ZECO na TANESCO. Hayati Rais aliyepita wa Awamu ya Tano, Dkt. Joseph John Pombe Magufuli aliweza kutufutia Zanzibar deni la shilingi bilioni 22 kitu ambacho leo ukiwauliza Wazanzibar mnamkumbuka vipi Dkt. John Pombe Magufuli basi moja ya jambo ambalo Wazanzibar wataendelea kumkumbuka ni hili la kutufutia deni. Leo hii linakuja jambo lingine dogo hili la bei, kwa nini Waziri usiwaambie watendaji wako wakakaa na watendaji wa kule wakaangalia jinsi ya kulimaliza mapema suala hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, deni lile lilikuwepo mwanzo ambalo lilikuwa linaleta zogo na tafrani humu ndani ya Bunge, kama unakumbuka TANESCO wakija kwenye Kamati yetu tukiwauliza mna madeni mangapi wanasema ZECO tunaidai shilngi bilioni 132; ZECO ukiwauliza wanasema sisi tunadaiwa shilingi bilioni 22 ambazo Hayati Dkt. John Joseph Magufuli alizifuta. Hii ni kwa sababu ZECO walifika mahali wakawa wanalipa current bill tu lakini hawalipi VAT mwisho wa siku TANESCO wanaandika VAT pembeni, hapa tunarudi kulekule. ZECO wanasema tunalipa shilingi 130, TANESCO wanasema shilingi 160.4 baada ya miezi sita na miaka miwili mbele TANESCO watasema wanaidai ZECO shilingi bilioni 54 na ZECO watasema sisi tunadaiwa shilingi bilioni 12. Hili sio jambo zuri na uwezo wa kulitatua Waziri wa Nishati wa Tanzania Bara Mheshimiwa Dkt. Benard Kalemani anao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine zuri ambalo namuamini Waziri, miradi mikubwa na mizuri ya kimkakati ambayo tunaendelea kuisimamia sisi kama wanakamati lakini kwa miongozo yake mambo yanaenda vizuri nashangaa jambo hili dogo linachukua muda mrefu. Kuna Bodi nzuri ya Mzee Kyaruzi sisi tunamuamini kwa uzoefu na maadili aliyokuwa nayo na uwezo aliokuwa nao kiasi cha kuaminiwa zaidi ya vipindi viwili maana yake hili si jambo la kuchukua zaidi ya miezi miwili, mitatu. Hata hivyo, namuamini Waziri na naamini atakapo-windup anaweza akatuletea jibu moja zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia kwa sababu nilisema nina jambo moja mahsusi, mimi katika Jimbo la Msalala nina interest zangu pale lakini nataka niwaambie watu wa REA mpaka leo vijiji 32 tu ndiyo vimepata umeme na vijiji 63 havijapata umeme. Jambo hili linatupa shida na sijui kwa nini wakati uwezo wa kupeleka umeme pale upo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naomba nisichukue muda wako. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa juhudi zake za kuiendeleza nchi katika sera ya Viwanda iliyowekwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa kutekeleza kwa vitendo, kwa kweli viwanda ni kitu muhimu sana kwa maendeleo ya nchi. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuomba sana Serikali yangu ya CCM kujaribu kulimaliza tatizo la Liganga na Mchuchuma kwa kuwalipa fidia wale wananchi wa Ludewa na kuendeleza yale machimbo na kumtafuta mwekezaji mwenye uwezo kwani ni muda mrefu sasa toka tuseme kuna mwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni upatikanaji wa vibali vya uwekezaji wa haraka kwani TIC kuna urasimu sana na hivyo kupeleka wawekezaji kuondoka na kufanya uwekezaji kwenda na mwendo wa kusuasua, hivyo tutachelewa kufikia malengo ambayo tumejiwekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nitumie nafasi hii kwanza kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii kuchangia leo hii katika Bajeti yetu hii ya Ulinzi.

Mheshimiwa Spika, vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi letu hili la Wananchi wa Tanzania, mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza pia Rais wetu wa Zanzibar kwa majukumu yake na ushirikiano ambao anautoa katika kuhakikisha amani inaendelea kutawala katika nchi yetu, lakini katika kushauriana na Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni mama yetu Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza yale majukumu ya amani na ulinzi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii sasa kukupongeza wewe Waziri kwa jinsi ambavyo unafanya kazi katika nafasi hii muda mchache lakini jinsi gani umetufikisha hapa na umelifikisha hapa Jeshi letu hili katika kuongoza. Nakushukuru sana na tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, mimi leo hapa nataka nitoe ushauri ambao nahisi ukiuchukua ikikupendeza itatusaidia sana katika Jeshi letu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa kwanza ni katika kuhakikisha nafasi zile za ajira zinapotokea uliendeshe Jeshi kama ilivyo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaani nafasi za ajira zinapotoka, umesema katika hotuba yako, nimekusikia, lakini unavyosema wewe na inavyochukuliwa haiko hivyo. Nina ushahidi, ukihitaji nitakupa, jinsi gani ambavyo hata mgawanyo wa ajira unapotoka katika Serikali yetu hi ya Muungano, tuna asilimia 79 kwa 21, lakini mgawanyo hauko hivyo, kama ambavyo washauri wako au watendaji wako labda wanakuelezea unakwenda sawa, lakini hauko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nimekuwa nikisimama mara nyingi nikiuliza maswali yangu kuhusu Wizara yako, ni jambo la mipaka ya makambi ya Jeshi. Hili umelizungumza kuwa mmeanza, umetuonesha mpaka picha kuwa mnapima. Lakini kiuhalisia mipaka bado ni jambo moja ambalo linasumbua sana baina ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wananchi siyo kama Jeshi hawalipendi, Jeshi wanalipenda kwa sababu ni Jeshi lao na linafanya kazi vizuri, lakini sasa inapofika mipaka wakijenga tokea asili yao ilivyokuwa Jeshi wanasema sisi mpaka hapa, lakini hakuna mwenye hati. Jeshi tatizo kubwa ambalo lipo, lina makambi mengi hayana hati miliki, lakini wananchi wapo ambao wana hati lakini Jeshi kwa heshima yake au kwa nguvu zake ambazo ipo na tumeipa sisi, na ndivyo tunavyopenda Jeshi letu liwe lina nguvu, basi huwa linafanya mpaka mwisho wanavyotaka wao.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine ambalo nataka pia nikushauri. Kiwanda chetu cha Nyumbu kinafanya mambo mengi, lakini yote kwa yote, fedha hakipati kwa muda, lakini na Serikali haitoi fedha kukiimarisha Kiwanda chetu cha Nyumbu kuhusu vifaa vyetu vinavyoweza kutengenezwa pale.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nishauri, leo hapa sina haja ya kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri, kazi yangu kubwa ni kumshauri yale ambayo nahisi ana mapungufu katika Wizara yake ila na ni kuboresha ili jeshi letu liendelee kuwa bora. SUMA JKT wamefanya kazi nzuri na wamefanya kazi kubwa katika nchi yetu hii lakini tatizo lao nalo kama Kiwanda cha Nyumbu bajeti wanaomba na pesa wanazoomba hawazipati kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri, tukiziimarisha taasisi zetu mbili hizi Nyumbu na SUMA JKT tukiwapa fedha ambazo wanataka na kwa wakati basi zita-create hata ajira ambazo tumesema zipo rasmi na ambazo sio rasmi, basi wana uwezo wa ku- create, kwa sababu wamefanya mambo mengine ambayo sitaki niyarudie wachangiaji wengine wamesema hapa, mpaka Ikulu yetu ambayo tunajisifia sasa hivi kubwa, nzuri, lakini imefanywa chini ya usimamizi wa SUMA JKT na ni vitu ambavyo vinawezekana, lakini wakiwezeshwa ndio itaonekana. Sasa ni jukumu la Waziri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka labda nimshauri Waziri na ushauri wangu sio jambo kubwa sana, jinsi ambavyo zinavyotoka nafasi zile za vyeo, majengo, basi yatoke kwa uwiano na yatoke kwa wakati, lakini sana vyeo. Kuna maafisa ambao wanatoka kwenye JWT lakini wanafanya kazi katika SMZ ambao wamechukuliwa kwa ajili na wao ni Watanzania kama sisi, lakini unapofika wakati wa kuwa na wao wafikiriwe kwenye vyeo, kidogo wanasahaulika. Ningependa hili nalo Mheshimiwa Waziri alichukue kwa sababu yote hii inatokana na nini? Jeshi letu hili la Muungano linafanya kazi huku na huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho, ikimpendeza Mheshimiwa Waziri, Jeshi lina hospitali ya Bububu kule Zanzibar ambayo ndio hospitali kubwa na hospitali ya viongozi wa ngazi ya juu na ya mwisho ikitokea wamepata matatizo au wana shida yoyote hata Mawaziri kama huyu akija, basi hospitali yao ya mwanzo huwa ni ya Bububu ambayo ni ya Jeshi, lakini ukiingalia hali yake sio nzuri kabisa, ina hali mbaya inahitaji ukarabati mkubwa na vifaatiba, vile vile na hata yale majengo yake hayako sawa, yaani ukiangalia hadhi yake na ya Jeshi letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hospitali ile haviko sawa. Kwa hiyo, ushauri wangu nafikiri nitakuwa nimechangia pale ambapo Waziri anahitaji mchango wa sisi kama Wabunge, naomba leo mchango wangu uwe huu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono asilimia mia moja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi hii niwe mmoja wa wachangiaji wa bajeti yetu hiii muhimu ya Wizara ya Nishati.

Mhemiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuifanikisha Wizara hii kwa kuipatia fedha kwa wingi na kuweza kufikia malengo yake. Pia, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa REA, Mkurugenzi wa TANESCO Ndugu Maharage Chande na wafanyakazi wao wote kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakiitendea haki Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, leo hii mimi nimesimama, na mara nyingi zaidi ya miaka mitatu minne nilikuwa nikisimama jambo langu kubwa lilikuwa ni kuhusu bei ya umeme Zanzibar. Lakini mimi ninayofuraha, pamoja na Wazanzibari wote jinsi ambavyo Wizara hii chini ya usimamizi wa viongozi hawa na Katibu Mkuu wao Mramba, kuweza kukubaliana na Serikali ya Zanzibar kuweka bei sawa pamoja na Tanzania bara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili tunawapongeza sana. Leo nitakuwa na mambo mawili ambayo yanataka Mheshimiwa Waziri utakapo wind up unipe status yake limefikia wapi.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na mpango wa TANESCO wameongea na Wizara ya Nishati ya Zanzibar kuhusu kupeleka cable nyingine ya umeme, kwa sababu cable iliyokuwepo sasa hivi inakaribia kuzidiwa kwa kuwa ina megawatts 100 na sasa hivi tuko abourt 80 na kuendelea. Pia, kutokana na hali ya uchumi wa Zanzibar ambayo Rais wetu wa kule Dkt Hussein Ali Mwinyi ya Uchumi wa Blue uwekezaji umekuwa mkubwa sana. Sasa uwekezaji huu hautoweza kufanikiwa kama itakuwa hatuna umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri, kama tulivyoweza kuzungumza kwenye Kamati yetu; kwanza na-declare kwamba mimi ni mjumbe wa Kamati hii; kwa hiyo, mengi yanayozungumzwa humu na ambayo ameyazungumza Mheshimiwa Waziri ni kweli, na yote ameyafanya ni kutokana na ushirikiano ambao sisi tunampa ushauri halafu na wao wanauchukua na wanaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana watu wa TANESCO, kwa upande wao wamekuwa wakiwasaidia sana watu wa ZECO, zaidi pale inapotokea hitilafu ya umeme mdogo au ukatikaji wa umeme upande wa Bara, yaani Ras Kilomoni kwa ajili ya kwenda Unguja na Majani Mapana Tanga kwa ajili ya Kwenda Pemba, nawapongeza sana wafanyakazi wa TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, isipokuwa kwa kumalizia tu na si ka ajili ya muda kwa sababu leo hii katika jambo ambalo umetufurahisha Wabunge ni jinsi ambayo umetuelekeza kujibu hoja na kuuliza swali. Twende moja kwa moja; na mimi ndiyo maana nimeanza moja kwa moja, na huu ni mwendokasi. Nakupongeza sana kwa hili. Style hii tukiendelea nayo tutaweza ku-manage muda wetu. Waheshimiwa Wabunge tuko wengi na kila mmoja anataka kuchangia; na ili tuweze kuchangia ni lazima tu manage time. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hongera sana na bila kusahau nataka nikwambie jambo lako ni letu sisi sote Wabunge humu ndani. Tuko na wewe, na tunajua una jambo lako lakini ni letu sisi. Ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nakupongeza wewe, Mheshimiwa Waziri na Wizara yote, naunga mkono asilimia. (Makofi)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI: Mheshimiwa Spika, kwanza naanza kwa kumshukuru Mungu kutujalia uhai na afya njema na hivyo kuweza kuhudhuria vikao vinavyoendelea vya Bunge letu hili.

Mheshimiwa Spika, naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya yeye na mtaalam wake, kwa jinsi wanavyofanya vizuri kwa muda aliokaa, kuna mambo mengi mazuri ambayo ameyafanya.

Mheshimiwa Spika, nampongeza kwa kanuni mpya alizozitunga kwa Wizara, zimeifanya Wizara yake ionekane jinsi gani inafanya kazi kwa maslahi mapana ya wanyonge. Nampongeza pia Mheshimiwa Waziri kwa kuanzisha (Tourism One Stop Centre) ambalo limejengwa jengo la mamlaka katika Mji wa Arusha.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa programu ya ujirani mwema kwa kuchangia miradi ya vijiji zaidi ya 30 vinavyozunguka hifadhi kwa kuwachimbia visima, zahanati, vyumba vya madarasa na mambo mengine. Changamoto pia haziko kuhusu mifugo inayoingia kwenye hifadhi, adhabu zake ni kweli zinahitaji kuboreshwa zaidi kwani utaratibu uliopo haukidhi kwani haijakaa vyema.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, wanyama wanaoingia utaratibu ungekuwa Wizara kutoa mwongozo wa kuwa wale ambao mifugo yao imeingia kwenye hifadhi basi wao ndio wapewe kipaumbele ili kuondoa dhana ya rushwa kwenye zoezi hili.

Mheshimiwa Spika, mwisho nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wao jinsi wanavyofanya kazi vizuri.