Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Subira Khamis Mgalu (27 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa nami niweze kuchangia taarifa ya Kamati ya Nishati. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kibali chake na kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge lako. Pia naishukuru sana Kamati yetu ya Nishati na Madini kwa taarifa yake nzuri ambayo iliwasilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri hasa katika Sekta yetu ya Nishati kwa kuwa natambua kabisa na wao wana tambua kwamba sekta yetu ni mtambuka na wezeshi kwa sekta nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zimejitokeza hoja nyingi, lakini naomba nijielekeze kwenye hoja ya umeme vijijini; na hapa naomba nijieleke kwenye miradi kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamesema, kwamba miradi kuna miradi ya REA II ambayo pengine haikukamilika kwa namna moja ama nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeshughulikia na ninavyosema sasa, Wakandarasi mbalimbali wameteuliwa kwa ajili ya kutekeleza miradi REA II ambayo ilikwama. Hapa nasemea kwa Mkoa wa Kilimanjaro na Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, Mama Anne Kilango Malecela na nimtaarifu katika Jimbo la Siha, Jimbo la Siha peke yake lilibakiwa na vijiji vitano tu ambapo REA II sasa ndiyo vinakamilisha. Ndiyo maana naamini Mbunge yule alishawishika baada ya kuona Jimbo zima umeme upo kasoro vijiji vitano, ambapo kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, Mama Anne Kilango Malecela, Mkandarasi Njalita yupo site na anaendelea na kazi ya kukamilisha upungufu uliojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, mikoa mbalimbali yote ambayo ina upungufu kwenye REA II, naomba nitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wakandarasi wale walikuwa hawajamaliza kazi katika kipindi cha uangalizi. Kwa hiyo, nawathibitishia, katika kipindi cha uangalizi ni kwamba Wakandarasi watamaliza upungufu uliojitokeza; na kwenye REA III tunawaahidi kwamba upungufu hautajitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwenye suala la nishati vijijini imejipanga vizuri. Ndiyo maana sasa tumeanza safari ya vijiji vilivyosalia 7,873 na Wakandarasi. Ni kweli kipindi cha miezi sita walikuwa na survey, lakini sambamba na hilo Wakandarasi katika kipindi hicho chote walikuwa wameagiza vifaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana nami kwamba Mikoa mbalimbali ambayo tumefanya ziara Wakandarasi wameanza kazi. Ninaposimama leo kusema ndani ya Bunge lako Tukufu, yapo maeneo vijiji vimeshawasha umeme. Kwa mfano, Mkoa wa Geita, Rukwa, Tanga, Pwani na mikoa mingine, Wakandarasi wapo site na wanaendelea na kazi. Ndiyo maana tarehe 13 tulikutana nao tukawapa maelekezo mbalimbali ya namna ya kuanza miradi hii kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nalithibitishia Bunge Tukufu kwamba tumepokea changamoto ambazo zimeelezwa. Tuwataarifu tu kwamba Wizara hii chini ya Waziri wangu tumejipanga vizuri katika usimamizi. Ndiyo maana kwa sasa ngazi ya Mkoa yupo Engineer pekee kwa ajili ya miradi ya REA; ngazi ya Wilaya yupo Technician kwa ajili ya miradi ya REA; na ngazi ya Kikanda yupo mtu wa REA kwa ajili ya kusimamia miradi hii tu. Kwa hiyo, hii yote imefanywa ili kuboresha usimamizi na kuona changamoto ambazo lizijitokeza REA Awamu ya Pili hazijitokezi tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilithibitishie Bunge lako kwamba kwa sasa hata miradi ya Densfication ambayo lengo lake ni kuvifikia vijiji 305 inaendelea vizuri katika maeneo mbalimbali. Sambamba na hilo, hata mradi huu ambao unaendana sambamba na REA III, huu wa Msongo wa KV 400 wa Mikoa ya Iringa, Dodoma, Shinyanga na Tabora nao unaendelea vizuri ambapo vijiji 121 vitafikiwa na miundombinu ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kama ambavyo Mheshimiwa Mama Anne Kilango amesema, ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, imeongeza usambazaji umeme kwa asilimia 28 miaka miwili; naamini na ninawathibitishia, kwa miaka ambayo tumejipanga 2018/2019, 2019/2020 vijiji vyote vilivyosalia 7,873 vitapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie; tulitoa maelekezo kwamba kisirukwe Kijiji chochote, Kitongoji chochote, Taasisi ya Umma yoyote, iwe Sekondari, iwe Shule ya Msingi, iwe Zahanati. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge wamesema hilo na sisi ndiyo mwongozo ambao tumetoa na nawaomba Wakandarasi wafanye kama ambavyo Serikali imewaelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote na tunawaahidi Utumishi uliotukuka. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili kwa mara ya pili ili niweze kuchangia hoja ya Wizara yetu ya Nishati na nianze kusema naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, pia napenda nimshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ya pekee kwa miongozo yake na kwa kuendelea kuniamini kuhudumu katika sekta hii ya Nishati. Namshukuru pia Makama wa Rais Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mheshimiwa Chief Whip wetu kwa maelekezo mbalimbali anayoyatoa ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, nikushuruku wewe, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge pamoja na Kamati yetu ya Nishati na Madini kwa miongozo mbalimbali mnayotoa katika sekta yetu ya nishati. Kipekee nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa namna ambavyo anaongoza Wizara yetu na kazi nzuri anayoifanya nchi nzima kwa weledi, uaminifu na kipaji ambacho alicho nacho na nimtakie kila la kheri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru familia yangu, mume wangu Juma Mtemvu, wazazi wangu, watoto wangu na familia yote Vilevile nikishukuru chama changu Chama Cha Mapinduzi pamoja na Wajumbe wa UWT, Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Pwani pamoja na viongozi wetu wa Serikali katika mkoa huu na wanachama kwa namna ambavyo wananipa ushirikiano katika majukumu yangu ya Unaibu Waziri lakini pia ya Kibunge ndani ya Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Wabunge wa Bunge hili kwa namna ambavyo wamechangia hoja yetu na mashirikiano wanayotupa siku zote, kwa ushauri wao na maelekezo ya mara kwa mara; kwa kweli wameitendea haki hoja yetu. Takribani Wabunge 100 wamechangia, 50 wamechangia kwa maandishi na wengine 50 wamechangia kwa kuzungumza.

Mheshimiwa Spika, umenipa dakika 15 lakini nataka niseme yote yaliyojadiliwa ndani ya Bunge lako tukufu tumeyapokea, na kwa kuwa majibu yatakuwa ya kimaandishi kwa kila mmoja hoja yake aliyochangia itoshe tu nichangie kwa ujumla wake na kama nilivyotanguliza kusema kwamba nimewashukuru sana. Mjadala wetu huu leo ulijielekeza kwenye suala zima la masuala ya Nishati na hususan asilimia 80 ya waliochangia walijielekeza kwenye mradi wa REA. Mradi wa REA awamu ya tatu ambao umelenga kufikisha vijiji vyote umeme takribani 12,268 ifikapo 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, tumesikia changamoto, tumesikia mlivyotuelekeza, tumesikia namna gani Watanzania wanahitaji nishati hii ifike vijijini. Tumepokea pongenzi; lakini siku zote nasema anayekupongeza anahitaji zaidi. Pongezi mlizozitoa leo mnahitaji tufanye kazi zaidi tuyafikie maeneo mbalimbali, tufikie vijiji vyote 12,068 ili kuweza kuleta tija na tuwaunganishie vijiji vyote. Ila nataka niseme moja, kwamba mradi huu kwa kweli wa REA awamu ya tatu pamoja na hoja kwamba umechelewa. Tumeshawa-categorize wakandarasi, tunatambua wakandarasi ambao wanafanya vizuri na tunatambua wakandarasi ambao bado kasi yao haijawa nzuri. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu, kwamba tunavyopima mradi huu wa REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza na miradi mingine inayoendelea tupime baada ya kuwafungulia letter of credit, ambayo ilikuwa mwezi wa sita mwaka jana 2018.

Mheshimiwa Spika, kwa miezi 24 wa mradi huu, matarijio yetu mradi huu utakamilika Juni, 2020. Kwa kuwa ndani ya Bunge hili na asilimia kubwa ya maswali ninayoyajibu pamoja na Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani yanahusu masuala ya nishati vijijini. Tumeweza kuwahamasisha na kuwasimamia wakandarasi, na hii tunawaahidi wakamilishe mradi ifikapo Desemba, 2019 ili miezi sita inayosalia iwe miezi ya kuunganisha wateja na ya kurekebisha mapungufu mbalimbali. Kwa hiyo niwatoe hofu Wabunge wote waliochangia hoja hii, kwamba pamoja na Watendaji wetu ambao wanafanya kazi vizuri wakiongozwa na Dkt. Khamis Mwinyimvua na Wenyeviti wetu wote wa Bodi zetu hizi. Kwa kweli jambo hili litawezekana na tuahidi tu kwamba itawezekana.

Mheshimiwa Spika, la pili, tumesikiliza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Hotuba hii ilionesha kwamba hakuna jambo lolote ambalo limefanyika; tangu Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani hakuna mradi wowote uliokamilika. Pamoja na kuchangia kwangu, nitaomba mwongozo wako ni nini kifanyike inapotokea hotuba yenye nia ya kupotosha na kulipotosha Bunge lako. Kwanini nasema hivyo, tumesema kwenye taarifa yetu tangu Serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani kwanza kiwango cha uzalishaji wa umeme kimeongezeka. Sasa hivi tuna Mega Watt takribani 1,604 kutoka Mega Watt 1,200 za mwaka 2015. Vilevile tumesema mradi wa Kinyerezi II Extension ulioanza awamu hii ambao umezalisha Mega Watt zaidi ya 244 umekamilika. (Mkofi)

Mheshimiwa Spika, si hivyo tu, mradi wa Makambako - Songea wa KV 220 umezinduliwa, umekamilika. Kana kwamba haitoshi mradi wa kusafirisha umeme wa Iringa – Shinyanga KV 400 umezinduliwa umekamilika. Pamoja na miradi mbalimbali ambayo tumeisema na tumesema, kwamba sasa tunakuwa na Megawatt 300 za ziada tofauti na upungufu wa Mega Watt 100 mwaka 2015. Kwa hiyo ni wazi kabisa Serikali ya Awamu ya Tano imetenda katika kipindi hiki kifupi cha miaka hii mitatu.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa pia utolee mwongozo wako ni suala zima la Taarifa ya Kambi ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuonesha kwamba Serikali inaikwamisha sekta ya nishati na tathmini na namna ambavyo amekuwa amefanya analysis, inashangaza. Nimshauri Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Waziri Kivuli pengine wakati anaandaa taarifa yake ahusishe na watu wa fani nyingine. Kwa sababu utaona namna ambavyo amekuwa anafanya analysis hususan ya fedha zilizopelekwa kwenye Wakala wa Nishati Vijijini (REA) amelipotosha Bunge lako Tukufu. Utaona katika analysis yake aliyoifanya kwa mfano ya mwaka 2015/2016 ameishia Desemba, 2015. Wote tunafahamu mwaka wa fedha wa Serikali unaishia tarehe 30 Juni, hii inafahamika. Unapofanya tathmini ya kuonesha Desemba 2015 unakuwa na hoja binafsi na si hoja ya kulipa uelewa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nataka niitaarifu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa mwaka 2015/2016 Wakala wa Nishati Vijijini ilipokea bilioni mia mbili tisini na tano na arobaini ikiwa ni asilimia 81 ya fedha zilizotengwa. 2016/ 2017 ilipokea bilioni arobaini mia tano tisini na tano ikiwa ni asilimia 75 iliyotengwa. 2017/2018 ilipokea bilioni mia tatu sabini na nne ponti tano ikiwa ni asilimia 80. Mwaka tunaouzungumza 2018/2019 mpaka sasa na hata taarifa ya Kamati yenyewe ambayo Naibu Waziri Kivuli ni Mjumbe wa Kamati hiyo mpaka sasa REA imepokea asilimia 81. Kusema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haiiwezeshi REA, isingewezekana kwa kipindi kifupi cha miezi 36 vijiji takribani 5,019 kupelekewa umeme. Kwa hiyo ni wazi kabisa Bunge lako limepotoshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kana kwamba haitishi, Bunge lako pia limepotoshwa kwenye taarifa ya hasara za Shirika la TANESCO. Tumepokea changamoto zote zilizoelewa, lakini hasara za Shirika la TANESCO zimekuwa zikipungua. 2015/ 2016 zilikuwa bilioni 949, 2016/2017 zimekuwa bilioni 265, 2017/ 2018 TANESCO ilipata hasara ya bilioni 112. Kuliaminisha Bunge lako, na kwa kuwa taarifa hii inaingia kwenye hansard, kwamba hasara za TANESCO zikiwa zimeongezeka hususan awamu ya tano, tutaomba mwongozo wako vinginevyo taarifa ambazo za upotoshaji ziondolewe kwenye hansard ya Bunge ili kupata taarifa sahihi. Niko tayari ku-submit audited report za TANESCO kuthibitisha hoja yangu ninayojenga sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hasara hizo lakini TANESCO imekuwa ikiwekeza kwenye fedha zake za ndani, kwenye miradi ya uzalishaji na miradi ya distribution. Mwaka 2015/2016 TANESCO iliwekeza bilioni 205, mwaka 2016/2017 TANESCO iliwekeza bilioni 220, mwaka 2017/2018 TANESCO imewekeza bilioni 233. Tunaona miradi yote hiyo, ujenzi wa sub-stations line ya Mtwara, kituo cha Maumbika ni fedha za ndani ya TANESCO. Ujenzi wa Sub-station maeneo mbalimbali, uunganishaji wa grid ya taifa kwenye maeneo mbalimbali ni fedha za TANESCO.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa suala zima la LNG. Ni kweli, natambua concern za Wabunge kwamba mazungumzo yamechelewa, lakini nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu mazungumzo haya yalikwama baada ya wabia wa mradi huu kutofautiana. Isingewezekana Serikali ikaendelea na mazungumzo ilhali wabia hawa wametofautiana. Hata hivyo pale kila mbia alipotaka tuzungumze pamoja na Serikali ikatoa baraka zake mazungumzo haya yameanza kwa kasi na yanataraji kukamilika Septemba, 2019. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie dakika chache kueleza uzoefu wa mazungumzo. Mfano Canada ilipojenga LNG yao, mazungumzo yalichukua miaka saba (7), Papua New Guinea ilipojenga LNG yao mazungumzo yalichukua miaka minne (4). Sambamba na hilo hata Msumbiji hapa walichukua mazungumzo mwaka mmoja na nusu lakini pamoja na kwamba mazungumzo haya hayakuingiliana kwenye masuala ya mkataba mkataba. Timu yetu hii tumeshaipeleka nje nchi za Indonesia, tumeipeleka Msumbiji, Papua Guinea, Trinidadi and Tobago na Qatar kwa ajili ya kuona namna gani nchi hizi zilifanikiwa wakati wa haya mazungumzo ya LNG. Kama ambavyo Wabunge wa Mkoa wa Lindi wamesema kwa kuwa mazungumzo yameshaanza na kwamba wawekezaji wanaendelea vizuri ni imani yangu mradi huu mkubwa ambao utatumia takribani trilioni 69, utatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuzungumzia mradi wa Rufiji Hydropower, na kwa kuwa natoka Mkoa wa Pwani ni mdau wa mradi huo.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo imetolewa takwimu hapa, bei ya umeme unaozalishwa na maji ni shilingi 36, bei ya gharama ya umeme unaozalishwa na gesi ni shilingi 147. Mheshimiwa Silinde alitolea mfano kwamba mradi wa Kinyerezi One Extension, bilioni 60 iliyotajwa kwenye kitabu ni fedha za kumalizia. Mradi huu umegharimu Dola za Kimarekani milioni 188 ambapo ni kama bilioni 454. Kutaka kutuaminisha bilioni 60 inaweza kuzalisha Megawatt 150 ni kulipotosha Bunge lako. Hata taarifa yetu ambayo Mheshimiwa Waziri ameisoma, ukurasa wa 34 ilieleza kinaga ubaga kiasi cha fedha iliyotumika. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge pamoja na michango yenu mizuri ninaomba michango hiyo ijielekeze kwenye takwimu zinazotolewa, isiwe na nia ya kupotesha, tunajenga nyumba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli tunategemea kufika uchumi wa kati 2025, tunahitaji umeme mwingi zaidi. Mmetaja miradi mbalimbali lakini gesi hiyo katika taarifa yetu hatujaiacha, uko mradi mpya wa kuzalisha Megawatt 300 katika Mkoa wa Mtwara kwa kutumia gesi. Uko mradi pia Kinyerezi IV na VI ambayo inaandaliwa, inaonesha kwamba gesi hatujaiacha na bado tunaimba huo wimbo kwa sababu gesi inatarajiwa kutumika kwenye viwanda, gesi inatarajiwa kutumika kwenye viwanda vya mbolea, gesi inatarajiwa kutumika kwenye kuendesha magari. Kwa hiyo kusema kwamba sasa hivi wimbo hatuimbi, tunaimba wimbo wa umeme wa bei nafuu kwa ajili ya viwanda na kwa ajili ya kushusha bei ya watumiaji wa umeme wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi binafsi namshukuru Mheshimiwa Rais kwa ujasiri wake. Ndani ya Wizara ya Nishata hatutarudi nyumba, tunatambua umeme ukiwa mwingi tumeshaanza kujenga miundombinu ya kusafirisha, ya kuuziana na nchi za jirani. Leo tunajenga Singida – Namanga kwa ajili ya ku-connect nchi ya Kenya, tuna mpango wa kujenga Masaka Mwanza kwa ajili ya kuunganisha na nchi ya Uganda. Zipo nchi zinahitaji umeme mwingi; umeme ni biashara. Mradi huu ukishakamilika una uwezo wa kuzalisha trilioni 9 kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia bajeti ya Serikali. Kwa hiyo nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge pamoja na maneno yote hatutarudi nyuma, mwendo mdundo katika mradi huu wa Rufiji Hydropower. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi wakazi wa Mkoa wa Pwani hususan Kibiti na Rufiji tunatambua mradi huu, bwawa hili litatusaidia kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tunatambua fursa za ajira lakini tunatambua vijiji 37 vitakavyounganishiwa umeme katika maeneo ya Morogoro na maeneo ya Mkoa wa Pwani. Si hivyo tu, tunatambua kwamba nia ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kutaka bei ya umeme ipungue kutoka senti 11 USD ya sasa na kadri itakavyowezekana. Haya yote yatawezekana baada ya energy mix ya kutosha hususan ya kuongeza umeme wa maji. Tunatambua, na tumepokea maoni ya kutumia nishati ya jadidifu na ndiyo maana tumetangaza tender kuwaalika wawekezaji binafsi Megawatt 950 kwenye upepo, kwenye maji na kwenye makaa ya mawe; na kana kwamba haitoshi, joto ardhi pia.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa nafasi hii, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge, niwashukuru wote ambao mmechangia hoja yetu na tutaendelea kufanya kazi. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa jioni hii kuchangia. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kusimama ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nawashukuru Wapigakura wa Mkoa wa Pwani kwa kukiwezesha Chama chetu kushinda Majimbo yote ya Mkoa wa Pwani, iliyopelekea kutuingiza Wabunge wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Tano pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Naona ameanza kazi vizuri na anasema Serikali yake siyo Serikali iliyochoka; Serikali makini ambayo inakusanya trilioni 1.4; Serikali ambayo inatumbua majibu kadiri inavyoweza; Serikali ambayo imechaguliwa na watu takriban milioni nane; Serikali ambayo ndani ya Bunge hili ina 74% ya Wabunge.
Mhesimiwa Mwenyekiti, Serikali hiyo haijachoka na Chama hicho kinaaminiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye Mwelekeo wa Mpango 2016/2017. Wakati najielekeza, naomba ninukuu hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge hili, ukurasa wa 22 aliposema: “Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umasikini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na salama.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Mwelekeo wa Mpango 2016/2017 kwa kuwa umejielekeza kwenye miradi ya maji; Mradi wa Maji wa Ruvu Juu, Mradi wa Maji wa Ruvu Chini, Mradi wa Maji wa Chalinze, Mradi wa Maji wa Visima Virefu vya Kimbiji na Mpera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono nikiwa na matumaini kwamba miradi hii itakapokamilika; Mradi wa Maji wa Ruvu Juu umekamilika kwa 97%, nina imani maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Mlandizi, Kisarawe na Mkuranga yanaenda kupatiwa maji kutokana na kukamilika kwa miradi hii ambayo nimeitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono mwelekeo wa Mpango huu wa 2016/2017 kwa sababu, suala la elimu; na naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako kwa kuanza mpango wa utoaji wa elimu bure. Natambua wapo baadhi ya Wapigakura wangu wa Mkoa wa Pwani walikuwa wanashindwa kulipa ada ya mitihani ya Baraza la Mitihani; walikuwa wanashindwa kulipa ada ya Sh. 20,000/= mpaka Sh. 70,000/= kwa Shule za Sekondari; walikuwa wanashindwa kugharamia baadhi ya gharama ambazo Serikali imezibeba kupitia capitation. (Makofi)
Kwa hiyo, nasema mwanzo wa safari ni moja. Tumeanza vizuri. Naipongeza Serikali, lakini natambua Serikali ipo sasa, inaangalia changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza awamu hii ya elimu bure. Naiomba Serikali iangalie sana kwenye baadhi ya maeneo, hasa suala zima la uandaaji wa mitihani, suala zima la gharama, umeme, mlinzi katika shule zetu; nina imani mambo yatakuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika suala hili la elimu, natambua Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Bunge hili, tulipitisha Sheria ya Kuanzisha Tume ya Walimu. Naiomba Serikali ya Awamu ya Tano iharakishe uandaaji wa Kanuni ili hii Tume iweze kuwatendea haki Walimu, mishahara yao, kupanda kwa madaraja, lakini pia Serikali iendelee na mpango wa kuzipa Halmashauri zetu kila mwaka milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
Vile vile Serikali ikiangalie sana Kitengo cha Ukaguzi wa Elimu. Kitengo hiki mara nyingi hakitengewi fedha na tunakitegemea sana katika kukagua ubora wa elimu. Kwa hiyo, hayo yakifanyika, ninaamini utoaji wa elimu bure utaenda sambamba na elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu pia umejielekeza kwenye afya vijijini. Kama ambavyo Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ilivyoahidi, kila Mkoa kuwa na Hospitali ya Rufaa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati, naomba Serikali itakapokuja na Mpango ujieleze kinagaubaga, awamu hii itaongeza zahanati ngapi katika vijiji vyetu? Itaongeza Vituo vya Afya vingapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali hii ijielekeze zaidi kwa watoa huduma kwenye Zahanati hizo na Vituo vya Afya. Yapo maeneo katika Mkoa wetu wa Pwani, hasa maeneo kwenye Jimbo la Kibiti, Kiongoroni, Kiechuu, Maparoni; maeneo haya ni maeneo pekee ambayo yanahitaji uangalizi maalum, kwani zipo Zahanati mpaka sasa hazina watoa huduma, hazina Madaktari wala nyumba. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie maeneo yale maalum hasa yale yanayozungukwa na maji, ikiwemo Wilaya ya Rufiji, hususan Jimbo la Kibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Sera za Serikali za kubana matumizi na katika Sera za Mapato. Hapa najielekeza kwenye utaratibu wa retention. Naipongeza Serikali kwa kuamua ku-retain fedha zake na Sheria ya Fedha (Public Finance Act) ya mwaka 2001, ilisema kinagaubaga, fedha zote zitaingia kwenye Mfuko Mkuu (Consolidated Fund).
Kwa hiyo, hapa nampongeza Dkt. Mpango kwa kuja na hili suala kwamba yapo mashirika ya EWURA, TICRA, walikuwa na pesa nyingi zaidi. Yapo mashirika, hata hizi tunazosema zinasimamia mbuga zetu, lakini tulijionea Taasisi ya Ngorongoro, TANAPA; kuna wakati fedha zilitumika kwa kulingana, siyo na bajeti, lakini matakwa ya viongozi wa wakati huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini fedha hizi zikikusanywa kwenye Mfuko Mkuu, lakini naiomba Serikali ijielekeze kuuondoa urasimu. Hazina mjipange kupunguza urasimu na kuzileta pesa hizi kwa mashirika haya kwa wakati uliokusudiwa. Ila ombi langu, Halmashauri zetu tuendelee kukusanya kwa sababu tunayo Mabaraza ya Madiwani yatasimamia, tutafuata Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Halmashauri, tukusanye na tuweze kufanya maendeleo ambayo yanakusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, najielekeza kwenye suala la kilimo. Tulikuwa na utaratibu wa Kilimo Kwanza, lakini pia tulikuwa na utaratibu wa SAGCOT; vile vile kipindi cha BRN kuna baadhi ya maeneo yalichaguliwa kuongeza uzalishaji wa sukari, mpunga na mahindi. Nina imani kabisa, kupitia Mpango huu, naomba kipaumbele pia kiwekwe kwenye kilimo na mipango iliyowekwa hii, BRN, bado ina nafasi ya kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna maeneo ambayo yalitengwa, kwa mfano Wilaya ya Bagamoyo lilitengwa eneo, watu wapo ECHO Energy, wanataka kufanya kazi kwa haraka, tuzalishe sukari nyingi tupunguze pesa tunazozitumia kwa ajili ya uagizaji wa sukari zifanye shughuli ambazo ni za kutoa huduma ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika ujenzi wa viwanda; Wilaya ya Kisarawe tumetenga eneo la viwanda. Tunalo, tunategemea miundombinu ya maji na miundombinu ya umeme ili eneo lile wadau mbalimbali wanaojitokeza waweze kununua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nina imani sana na Serikali. Serikali inaweza! Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi ina uthubutu. Serikali hii, amani ipo. Waliokuwa na nia ya kuvuruga amani ni waliokwenda kwenye Vituo vya Television na kujitangazia ushindi wamepata kura milioni kumi; hawana fomu za matokeo na walikuwa na Mawakala nchi nzima, wanajitangazia kura wakiwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuliokuwa site, tuna uhakika, kura tulizihesabu vituoni, tunajua Wagombea Urais walipata kura ngapi, hakukuwa na utata. Matokeo yaliyotangazwa, Rais Dkt. John Pombe Magufuli alishinda, hatukuwaona mlete ushahidi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna imani Serikali haijachoka, itafanya kazi. Hata hivi karibuni Serikali kupitia utaratibu wa utumbuaji wa majibu, napongeza ilivyotumbua jipu la Hati Fungani. Vipo Vyama vinajidai vinapinga ufisadi, lakini hatukuwaona kwenye majukwaa wakisema kupinga ufisadi. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alijipambanua, alitoa ahadi kwamba yeye atapambana na ufisadi. Wengine hatukuwasikieni! Mlisemea wapi? Leo mkija ndani ya Bunge, mnasema ninyi ndiyo mnapambana na ufisadi, lakini naomba mtoe boriti zilizopo kwenye macho yenu kisha mtazame Vyama vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, napongeza na Bunge hili, wananchi wa Tanzania msibabaishwe na miongozo na kanuni, zimejaa Kanuni nyingi; lakini ukiangalia hata Taarifa yao hiyo waliyoandaa, Mpango huu umeandaliwa kwenye karatasi mbili tu. Zote hizi wameandaa maoni ya Mpango wa Miaka Mitano ambao haujadiliwi sasa! Maoni ya Mpango huu ni kurasa mbili tu. Kuonekana, mmesituka! Hongereni Watanzania. Ahsanteni sana. (Kicheko/Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Pia namshukuru Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Pwani kwa kunipigia kura na kunifanya kuwa Mbunge katika Bunge lako. Niungane na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano kwa kuanza kazi vizuri, nina kila sababu ya kumpongeza kwa matukio yafuatayo machache:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa usimamizi mzuri wa makusanyo ya mapato ambayo naamini yatatekeleza mpango wa maendeleo unaokuja na bajeti hizi ambazo zinaendelea. Pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa fly over na naipongeza Serikali ya Japan ilikuwepo, napongeza kwa uzinduzi wa mradi wa Kinyerezi I pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi kinyerezi II. Pia nampongeza sana Rais Museven kwa kukubali bomba la mafuta kupitia Bandari ya Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nayapongeza haya nikiamini kabisa viongozi wa Mataifa mbalimbali ya nje yana imani na Mheshimiwa Rais wetu, hawana tatizo na kuona kwamba mpaka sasa instruments hazijatoka, kwa sababu wanaamini wao ni kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo pia napongeza fursa ambayo Serikali ya China imeonesha kutaka kutu-support katika ujenzi wa reli ya standard gauge. Naipongeza kwa sababu China wanataka kutoa hela nyingi lakini hawajapata kuuliza instrument ya Waziri wa Mawasiliano wala ya Waziri wa Ujenzi, naamini wao wanaamini hapa kazi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na pongezi hizo, naomba nijielekeze kwenye bajeti. Nampongeza Waziri wa TAMISEMI, pamoja na Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora na Naibu Waziri wameanza kazi vizuri, wanashughulikia masuala ya mishahara hewa vizuri na wanapambana. Nikipitia hotuba ya Waziri wa TAMISEMI pamoja na mikakati ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana, naomba nijielekeze zaidi kwenye sekta ya afya. Katika kujielekeza sekta ya afya nimeona kupitia bajeti hii mkakati wa Serikali wa ujenzi wa vituo vipya vya afya, ujenzi wa zahanati, ukarabati wa hospitali za wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali iangalie sera, Wizara ya Afya nadhani ingekuwa vizuri kama ingepewa jukumu pia la usimamizi wa vituo hivi kwa sababu wao wanasimamia sera. Inapokuwa TAMISEMI na wao wana mambo mengi, lakini changamoto kubwa zipo kwenye maeneo ya vituo vya afya, ziko kwenye maeneo ya hospitali za wilaya na ziko kwenye zahanati. Kwa kuwa TAMISEMI wanaendelea kusimamia, lakini kwa kuwa haihusiani na masuala ya sera, usimamizi kidogo unakuwa hafifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijielekeza zaidi katika ujenzi huo wa zahanati na ukarabati nimeona bajeti ya mwaka 2014/2015 takribani bilioni 263 zilitumika, lakini mwaka 2016/2017 zimetengwa bilioni 27. Naona hiki kiwango ni kidogo nikiangalia changamoto ambazo zinatukabili na nazielekezea changamoto hizo kwenye hospitali yetu ya Wilaya ya Mkuranga ambayo haina X-Ray; kituo chetu cha afya cha Kibiti katika Wilaya mpya hakifanyiwa upanuzi wa jengo la wazazi; kwenye kituo chetu cha afya Mkoani Kibaha changamoto kubwa ni jengo la upasuaji, pia hata kituo cha afya Maneromango, vifaa vya upasuaji vipo, lakini jengo halipo. Nashauri katika kifungu hiki angalau kingeongezwa zaidi ili tuweze kupata huduma nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona wakati nikipitia hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani katika ukurasa wa tatu, nanukuu:
“Kambi Rasmi ya Upinzani inawataka Wabunge wa CCM waache kufanya ushabiki Bungeni”.
Pia katika ukurasa huo huo nanukuu kwamba:
“Vyombo vya Habari vya Umma na Binafsi virushe moja kwa moja mijadala ili wananchi wajue fedha zao zinavyogawanywa katika Halmashauri zao na wajue ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Ibara ya 89 imeipa Bunge wajibu wa kutunga Kanuni za Uendeshaji wa Bunge hili, Kanuni za Kudumu za Bunge, Kifungu 116 zimempa mamlaka Spika kuunda Kamati, pia zimeipa mamlaka Kamati zenyewe kuchagua Wenyeviti wao wa Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Usimamizi wa pesa za Halmashauri (LAAC) na Kamati ya Hesabu ya Serikali (PAC), kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ambazo zinatokana na Katiba zinatakiwa ziongozwe na Wapinzani. Leo wanapoituhumu Serikali kuvunja Katiba, kuvunja taratibu mbalimbali, wao hawajitazami mpaka leo Wenyeviti wa Kamati hizo hawajachaguliwa, leo wanaposema Bunge lioneshwe live lakini wao hawajatimiza wajibu wao zaidi ya miezi minne, Kamati hazijapata Viongozi kutoka Kambi ya Upinzani na mamlaka hiyo ni ya Spika.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekeni Kiongozi unajipangia utaratibu kuteua Wajumbe wa Kamati hukupewa mamlaka hiyo! Ni mamlaka ya Spika kuwapanga Wabunge kwenye Kamati zao kwa vigezo vyao na Kanuni tumetunga wenyewe za Bunge hili. Nilidhani wangetoa ushauri kwamba Kamati zinazoongozwa zipewe mamlaka zenyewe. (Makofi)
MHE. SABREENA H. SUNGURA: Taarifa!
Taarifa....
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa siipokei, kwa kuwa hakujielekeza kwenye Kanuni yoyote na mimi nimesema kama ana ushahidi wa Party Caucus kukutana ili kuchagua viongozi, walichaguliwa ndani ya Kamati husika, hiyo taarifa yake siyo sahihi naomba watimize wajibu wao kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, CAG (Controller and Accounting General) amewasilisha ripoti yake, lakini najua kwa nini hawajachagua mpaka sasa hivi, wamepima maji wameona yana kina kirefu. Mheshimiwa Aeshi endelea na kazi, chapa kazi PAC, umegundua mambo, LAAC nayo endeleeni, chagueni Makamu Mwenyekiti aendelee na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze pia kwenye ukurasa wa mwisho wa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wanaelezea masuala ya vifungu vya Sheria ya Bajeti, kwa kuwa kitabu hiki kinatumika na Wabunge wote na ni upotoshaji, sasa nataka nijielekeze kwenye Public Finance Act hiyo, Kifungu 19 naomba wanavyo-quote Sheria za Fedha wamalizie wasi-quote nusunusu. Kifungu cha 19 kinasema; “If at the close of account for any financial year it is found that moneys have been expended:-
(a) on any expenditure vote in excess of the amount appropriated for it by an Appropriation Act;
(b) for a purpose for which no moneys have been voted and approaprated.
(c) the amount of excess expended or not appropriated as the case may be shall be included in a statement of expenditure.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mwaka wa fedha wa Serikali haujakwisha msiwahishe shughuli, mnapo-quote Sheria mbalimbali za Fedha mmalizie, mme-quote Public Finance Act 18 (a) na 14, kwa nini hamku-quote 19 ambayo ndiyo imetoa mamlaka mwisho wa mwaka wa fedha kama kuna pesa zimetumika za ziada ambazo hazikutengwa ziwasilishwe ndani ya Bunge katika taarifa maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka wa fedha haujakwisha lakini kama pia pesa zilitumika zaidi na naomba kwenye masuala ya barabara, nimeona kwenye kitabu cha TAMISEMI mpango wa ujenzi wa barabara, namwomba tu Waziri wa Fedha mwaka wa fedha wa Serikali ukiisha awasilishe statement, tuipitishe kwa sababu yamefanyika mambo ya heri na mamlaka hiyo anayo, kwa hiyo hakuna uvunjaji wowote wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba niwazungumzie Wabunge Wanawake namna ambavyo hawashiriki vikao vya Kamati vya Fedha Halmashauri za Wilaya. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, Ibara ya 66, imetaja aina za Wabunge wakiwemo Wabunge Wanawake. Wabunge wote wana haki sawa, inashangaza kwamba Wizara ya TAMISEMI Katibu Mkuu anatoa mwongozo wa kuwatoa Wabunge Wanawake ambao wanasimamia maslahi ya wanawake, maslahi mapana na changamoto mbalimbali katika Kamati za Fedha, kama leo wanapoleta milioni hizo hamsini, asilimia 10 ya Vijana na Wanawake, mambo ya sekta ya afya, mambo ya kilimo, Mbunge Mwanamke na yeye ana mchango mkubwa kwenye Kamati ya Fedha ambayo inakutana kila mwezi, Wabunge wana uwezo wa kuchangia hoja na kujenga hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya TAMISEMI tumelisemea kila siku, huu ni mwongozo tu, mtoe mwongozo kuwa Wabunge Wanawake na Madiwani Wanawake, tusibaguliwe na wala tusinyanyaswe, kwa sababu pia Katiba imekataza sheria yoyote inayoonesha ubaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Bajeti na naunga mkono kwamba hakuna uvunjaji wowote wa Kanuni wala wa Katiba, wanaposhutumu na wao wajitazame, wajisahihishe, kidole kimoja kinawatazama. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa fursa asubuhi ya leo kuweza kuchangia bajeti ya Wizara yetu hii ya Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi. Nianze moja kwa moja, kwanza kuwapongeza Walimu wote nchini Tanzania kwa kazi kubwa wanayofanya. Kipekee niwashukuru Walimu hao kuanzia Shule ya Msingi, Sekondari Mtwara Girls na Ndanda High School, Chuoni IFM, Mzumbe University na Walimu wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu kwa namna ambavyo wamenisaidia, nimepata fursa ya kusimama ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba leo, kabla hata sijachangia niliwasiliana na wanafunzi niliosoma nao ambao pia ni Walimu ambapo, changamoto nitakazozichangia hapa na ni maombi yao, ni maombi yaliyotokana na Walimu wenyewe baada ya kuwasiliana nao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, anafanya kazi vizuri; hatua alizochukua dhidi ya Bodi ya Mikopo, hatua alizozichukua dhidi ya TCU, binafsi naziunga mkono. Pia, nampa pole sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufiwa na mama yake mzazi, Mwenyezi Mungu ampe subira na wepesi katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nina matumaini sana ya Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuwa, naamini inaongozwa na Rais wetu aliyepata kuwa Mwalimu, Waziri Mkuu aliyepata kuwa Mwalimu, First Lady aliyepata kuwa Mwalimu, Walimu wana matumaini makubwa sana katika Awamu hii kwamba, jitihada zilizoanzishwa katika Awamu mbalimbali changamoto zao nyingi zitapata fursa ya kutatuliwa katika Awamu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nipongeze kwa utekelezaji wa suala zima la Waraka Namba Tano (5) wa Elimu Bure ambao umeanza mwaka jana Disemba, 2015 mpaka sasa. Nipongeze dhamira ya Serikali ya kutenga kiasi cha bilioni 18 kila mwezi kukabiliana na majukumu mazima ya kutoa elimu kwa Shule za Msingi na Sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Pwani suala hili limetusaidia, ongezeko la uandikishaji kwa ngazi ya mkoa limefikia 150%. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile 50% ya watoto walioongezeka katika Elimu ya Awali na Msingi ni wazi kuwa kuna wazazi ambao ilikuwa inashindikana kabisa kupeleka watoto wao kutokana na changamoto mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwanzo wa hesabu moja. Natambua Roma haikujengwa kwa siku moja. Katika utaratibu mzima wa utoaji wa elimu bure, naiomba Wizara iangalie, isije ikawa utekelezaji wa elimu bure imewapa Walimu Wakuu mzigo mkubwa na Walimu wenyewe bado wanalalamika mishahara bado ni midogo na marupurupu yao mengine; kwa nini nasema hivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji huu wa elimu bure, kuna kipengele cha utawala. Utakuta shule inawezekana ina wanafunzi wachache, lakini gharama za utawala ni moja; kama ni bei ya shajara ni moja, masuala ya mitihani ni mamoja, lakini utakuta ile 10% hasa kwa shule ambazo zina mazingira magumu, mfano shule za Kata ya Kibindu Wilaya ya Bagamoyo, Shule za Delta, Kiongoroni, Mbuchi, Msala, Maparoni Wilaya ya Rufiji! Shule za Wilaya ya Kisarawe zilizopo Vikumburu, Dololo, Kimaramisale, Mafia, Visiwa vya Jibondo, Chole, Mkuranga, Visiwa vya Kwale, Koma, mazingira yao ni magumu kiasi kwa mfano Visiwa vya Rufiji, kuja Makao Makuu ya Wilaya Utete, Mwalimu anatumia 50,000/= nauli. Zilikuwepo boti kwa ajili ya kuwasaidia walimu hawa, lakini zile boti zimeharibika, lakini anaenda kufuatilia cheque kwa ajili ya masuala ya utawala. Kwa mfano kuna shule iko Msala na inapokea 40,000/= asilimia 10 ni 4,000/=, lakini afuatilie hiyo hela mpaka Utete ni 40,000!
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara iangalie mazingira haya magumu na iwatendee haki Walimu, wamelalamika! Walimu sasa wanatumia pesa zao mifukoni kwa ajili ya uendeshaji wa shule. Vile vile suala hili limeathiri masuala ya mitihani; kifungu cha mitihani hakitoshelezi, kwa hiyo, baadhi ya mitihani imepunguzwa! Labda shule zilipanga utaratibu mock ya Kikata, mock ya Wilaya, mitihani ya kila mwezi, ya kila wiki na mitihani hii ilikuwa inasaidia ufaulu. Kwa hiyo, nadhani Wizara iangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Walimu niliowasiliana nao wameomba hiki Chama cha Walimu Tanzania, wamesema chama hiki kimeshasimama, kina miliki jengo, kinafungua benki! Masuala ya kuwakata asilimia ya mishahara yao kwa ajili ya kuchangia chama ambacho kimeshasimama, kina uwezo, naomba Wizara mfuatilie, Walimu wanalalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini chama hiki hakipo wazi! Sisi tumekaa Wilayani, hatuoni msaada mkubwa kwa Walimu wetu, lakini mara nyingi utakuta kwenye masuala ya michakato ya kisiasa kiko mbele, lakini siyo katika kuwasaidia Walimu! Nadhani michango waliyochangia Walimu ingewezekana Chama cha Walimu kingethubutu, sasa hivi kinamiliki benki, kinamiliki jengo kubwa Dar-es-Salaam, kingethubutu hata kuwapunguzia makali ya maisha walimu ambao ni wanachama wao. Kwa hiyo, hilo nalo walimu waliniomba, lakini wamesema sasa hivi chama kimesimama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Walimu wameiomba jitihada za kuimarisha miundombinu. Bajeti ya miaka iliyopita, hususan mwaka jana, kulikuwa na kifungu waziwazi cha ujenzi wa nyumba zao kama 500 kila mwaka.
Nimejaribu sana kuangalia kwenye bajeti ya mwaka huu sioni vizuri, hakionekani waziwazi, lakini bado kuna changamoto kubwa ya miundombinu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Walimu wameniomba, kuna Walimu waliajiriwa Juni, 2015 mpaka leo bado hawajalipwa pesa zao za kujikimu na pesa zao za nauli, inawakatisha tamaa. Walimu pia, wameniomba Serikali iendelee na jitihada za kulipa madeni yao; wanatambua hata mwaka jana mwezi wa 10 baadhi ya madeni yao yamelipwa, lakini kwa kuwa yanajilimbikiza kwa muda mrefu, Walimu wameomba pia suala hili litekelezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Walimu pia wameniomba niwasilishe, utekelezaji wa Waraka wa Posho za Viongozi, sijaliona waziwazi kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri! Walimu Waratibu wa Elimu Kata walipangiwa sh. 250,000/=, Wakuu wa Shule walipangiwa sh. 200,000/=, hizi zinaweza zikawasaidia, naomba hilo nalo litazamwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Pwani tunalo tatizo, baadhi ya shule zetu zina Walimu mmoja mmoja. Mfano Shule ya Gundumu Kata ya Talawanda, Shule ya Kwa Ikonji, Pera, Kata ya Kibindu ina Mwalimu mmoja, lakini shule hizi zina madarasa kuanzia la kwanza mpaka la saba. Kwa mfano kwenye Shule ya Gundumu kuna Walimu wawili wanajitolea kwa sh. 50,000/= lakini tangu Disemba hawajalipwa! Kwa hiyo, mimi binafsi kama Mbunge wao nimeona niwasaidie, nilichukue jukumu hilo ili niweze kuona jinsi Serikali itakavyotusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala la Bodi ya Elimu. Kwanza nakubaliana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya TCU, lakini pia nasikitika hela zaidi ya milioni 700 zilizotumika kwa vijana wale na mimi binafsi siyo Mwalimu, lakini nikiangalia maelezo ya Mheshimiwa Waziri na vigezo walivyovitumia kuwadahili wale na nikirejea maelezo ya Kamati yetu ya Huduma za Jamii, ukurasa wa 11 kwamba, Kamati imebaini kuwa, vijana wengi wenye alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya elimu ya juu wameshindwa kuendelea kutokana na hela hizi za mikopo kuwa si nyingi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo kama wapo vijana wenye elimu, wenye vigezo, wako mitaani wanakosa fursa ya mikopo, tufike hatua ya kuwadahili wanafunzi wenye Arts kusoma masomo ya sayansi kwa ajili ya kuja kutufundishia watoto wetu! Kwenye suala hili kwa kweli, naunga mkono. Nimesema mimi siyo Mwalimu, lakini naamini Profesa Ndalichako amejiridhisha, naamini na Tume aliyoiunda itafanya kazi nzuri, lakini hatua lazima zichukuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, nimalizie kwa kuomba huu ujenzi wa miundombinu, hasa kwenye shule ambazo, kwa mfano tuna Shule ya Mlegele Kisarawe, tuna Shule ya Kidugalo, Tondoroni, Sofu na Kola; shule hizi zina vyumba viwili viwili vya madarasa, lakini zina madarasa kuanzia la kwanza mpaka la saba! Kwa hiyo, utakuta changamoto katika miundombinu ya elimu, bado ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niiombe Serikali, maoni ya Kamati yetu ya Huduma za Jamii ni mazuri sana, hasa uwekezaji kwenye Sekta ya Elimu. Tunapoliandaa Taifa letu kuwa Taifa la kipato cha kati na Taifa la viwanda, tunatarajia kufufua Viwanda vya Nguo, Viwanda vya Kusindika Korosho, tusipoandaa wataalam na tukawekeza zaidi katika Wizara hii, hasa miundombinu yake. Tunaweza tukawa na kila kitu, lakini Taifa litakalokosa wafanyakazi wenye elimu inawezekana hata hii azma nzima tusiitimize. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii niweze kuchangia hoja ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utawala Bora.
Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya ya kuweza kusimama ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili naomba nichukue nafasi kuwapa pole wananchi wenzangu wa Wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji kutokana na matukio yaliyojitokeza, lakini niliona nilisemee hapa kwa sababu tukio la mauaji linaloendelea Wilayani Kibiti na Rufiji kwa kiasi kikubwa limeathiri uendeshaji wa Halmashauri za Kibiti na Rufiji na naiomba Ofisi ya Rais, TAMISEMI waiangalie kwa jicho la huruma Halmashauri mpya ya Kibiti, wameshindwa kukusanya mapato kwa sababu katika maeneo ambayo mauaji hayo yanajitokeza mara kwa mara eneo la Bungu na Jaribu Mpakani ni eneo ambalo lina vyanzo vingi vya mapato na linalochangia mapato kwa kiwango kikubwa.

Kwa hiyo, naomba Serikali itambue Halmashauri ile ni mpya, inahitaji pesa ya uendeshaji wa Halmashauri na ina maeneo maalum ya ukanda wa delta. Kwa hiyo, naomba sana Waziri aitazame Halmashauri ile kwani kwa sasa hata malipo ya posho za Madiwani zitakuwa ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa pia wanaopata madhila hayo ni baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji, naomba pia Mheshimiwa Waziri aangalie namna gani viongozi wa maeneo yale watakavyokuwa wanawajibika. Hapa hapa niwasemee viongozi hawa wa vijiji na vitongoji pamoja na Waheshimiwa Madiwani ambao ni wasimamizi wa shughuli mbalimbali za maendeleo kuwaongezea posho. Kwa mfano, Wenyeviti wa Vijiji hawana posho yoyote. Pia naipongeza Halmashauri yangu ya Chalinze kwa uamuzi wa kuwapa Wenyeviti wetu wa Vijiji shilingi 30,000 kila mwezi kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii pia ni Ofisi ya Rais, naomba nichukue fursa hii kumpongeza kwa dhati Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na kwa Mkoa wa Pwani tunaishukuru ziara yake aliyoifanya mwezi wa Tatu. Ziara ile ilionesha azma yake ya ujenzi wa viwanda nchini kutimia ndani ya Mkoa wa Pwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mazingira mazuri, tunavyo takribani 82 vinavyoendelea kujengwa kikiwemo kiwanda cha tiles ambacho kimekamilika Mkuranga, lakini kuna kiwanda cha tiles kinaendelea Chalinze, lakini pia kuna kiwanda cha usindikaji matunda Msoga, Chalinze. Kwa hiyo, hii inaonesha bado wawekezaji wana imani na Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwamba anaendelea kukubalika na Jumuiya ya Ulaya imeshatoa msaada, imeahidi kuendelea kuisaidia nchi yetu dola milioni 205, ameshasaini. Pia Benki ya Dunia inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya ujenzi wa flyover Dar es Salaam, kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa mwendokasi Dar es Salaam, yote hayo yanaonesha namna gani Mheshimiwa Rais wetu anaaminika na Benki ya Dunia, African Development Bank na wadau mbalimbali wa maendeleo. Tuendelee kumuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye suala la elimu bure. Naipongeza sana Serikali, jambo hili siyo jepesi. Kwa bajeti ya mwaka huu, zaidi ya shilingi bilioni 201 zimetengwa kwa ajili ya elimu bila malipo. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa kutoa ufafanuzi mzuri namna ya kutofautisha elimu bure na elimu bila malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo baadhi ya wananchi wengi tu katika maeneo mbalimbali wameanza kulitekeleza hilo la kutoa michango yao. Hapa naipongeza Halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze, Kibiti, Mkuranga, Mafia, Kisarawe kwa wananchi mbalimbali, tumeanza ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuchangia jitihada za Serikali. Kwenye Halmashauri ya Chalinze ninayohudumu tumetenga shilingi milioni 400 ya ujenzi wa miundombinu kwa mapato ya ndani kwa elimu ya msingi, shilingi milioni 400 ujenzi wa miundombinu kwa mapato ya ndani kwa elimu ya sekondari. Hii inaonesha namna gani sisi wawakilishi wa wananchi; Madiwani na Wabunge tunavyoona umuhimu wa kuisaidia Serikali katika suala zima la elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo naiomba Serikali kwenye suala hili la elimu bure, ukiangalia namna ambavyo hizi fedha zimetengwa kwa uhalisia, uwiano wa wanafunzi katika Halmashauri zetu, uwiano wa walimu na uwiano wa uhaba wa mindombinu; hapa naomba Mheshimiwa Waziri aangalie ile randama kwenye Halmashauri zetu za Mkoa wa Pwani. Kwa mfano, Halmashauri ya Chalinze na Mkuranga inaongoza kwa idadi ya wanafunzi, inaongoza kwa idadi ya walimu, inaongoza na kwa idadi ya uhaba wa miundombinu, kwa hiyo, nadhani katika ule mchanganuo haujakaa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta Halmashauri nyingine idadi yao ni ndogo na hapa nia ni kufanikisha; kwa hiyo, naomba nimletee Mheshimiwa Waziri ile taarifa yetu kamili ya kuonesha namna gani ule mgawanyo ulivyo ili waweze kurekebisha. Ukizingatia hasa Halmashauri ya Mkuranga kwa kweli uhamiaji ulikuwa mkubwa na wanafunzi ni wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo pia naipongeza Serikali hususan Wizara hii ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Afya kwa namna ambavyo wameanza mgao wa vifaa tiba kwenye hospitali zetu. Hivi karibuni tumeona Serikali imenunua vifaa tiba vya thamani ya takribani shilingi 2,900,000,000 ambapo kila Halmashauri itapata vitanda 20, vitanda vitano vya kuzalishia, magodoro 25 na mashuka 50. Kwa kweli hii ni hatua nzuri katika kuboresha huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwenye ukurasa wa 34 wa hotuba ya Waziri wa TAMISEMI, ameonesha ni namna gani Serikali kwa kushirikiana na hizi Wizara mbili itakavyokarabati vituo vya afya 100 ili kuboresha mazingira ya upasuaji kwa ajili ya afya za akina mama. Mpango huu utagharimu shilingi bilioni 63. Naipongeza sana Serikali.

Kwa hapa nizisemee Halmashauri zetu mpya Kibiti na Chalinze; Halmashauri hizi hazina Hospitali za Wilaya, lakini kwa Chalinze bahati nzuri Mheshimiwa Rais wetu Mstaafu wa Awamu ya Nne amejitahidi tumepata majengo kwa Kata ya Msoga, lakini changamoto kubwa ni uhaba wa watumishi. Hatujapatiwa watumishi kwenye hospitali yetu ile ya Wilaya na majengo yamekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata Basket Fund tumepata takriban shilingi milioni 488, lakini mpaka sasa kiasi cha shilingi bilioni 105 kinashindwa kutumika kwa kuwa hakuna hospitali yenye hadhi katika Halmashauri ya Wilaya wakati tunayo tayari na majengo tayari pia yamekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikisemee Kituo cha Afya cha Chalinze. Kituo hiki kinapokea majeruhi wengi, naomba sana Serikali ijitahidi kutuboreshea wodi ya upasuaji, maana hakuna wodi hiyo pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala zima la uwezeshaji wa wananchi, naipongeza sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba Mkoa wangu wa Pwani umepokea shilingi milioni 104 kwenye Mfuko wa Vijana, lakini sambamba na hilo, Mkoa wetu wa Pwani umetoa takribani shilingi milioni 477 ambayo ni asilimia 10 ya mapato yake ya ndani. Hapo naomba nishauri; kwa kuwa marejesho ya mfuko huu hayaonekani wazi wazi kwa kuwa hakuna akaunti maalum, naomba Serikali sasa ione namna ya kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya marejesho tu ya mikopo hii ya asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwa kuwa fedha zinazotengwa ni nyingi, Serikali ione uwezekano wa kuanzisha benki za wananchi katika mikoa yetu. Kwa mfano, mwaka huu tulitenga shilingi 1,800,000,000; mwakani tumetenga shilingi 2,400,000,000; hizi zinatosha kabisa kuanzisha benki za wananchi katika mikoa ili kurahisisha na wakati huo sheria itakuwa imerekebishwa.


Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nadhani pia ile mikopo ya shilingi milioni 50, sijasikia neno kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI, lakini nadhani Wizara yake ndiyo itakuwa inaratibu, inaweza pia ikaongeza nguvu katika mikopo hii ya asilimia 10 kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwasemee walimu pia. Nampongeza sana Mheshimiwa Biteko na Waheshimiwa wote waliosemea hili, lakini hapo niseme tatizo lililopo sasa hivi la uhamisho. Walimu wengi wamepata watu wa kubadilishana nao, lakini vikwazo mbalimbali vinatokea na sekta hii kwa kweli na watumishi wengi wanakwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nampongeza Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa namna alivyosimamia zoezi hili la uhakiki wa wafanyakazi, uhakiki wa vyeti fake, lakini ifike wakati sasa zile haki za kimsingi, hata zile ambazo hazihusiani na masuala ya malipo, walimu wenyewe wameomba kuhama kwa hiari yao, wamepata wa kubadilishana nao, basi TAMISEMI itoe hiyo orodha ili walimu wetu na kikwazo kingine masuala ya ndoa yaweze kufanyika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili siku ya leo, pia nipongeze Wizara hii Mawaziri Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa kazi nzuri naunga mkono hoja hii iliyowasilishwa hapa lakini pia naunga mkono taarifa ya kamati ya bajeti yetu ambayo imewasilishwa hivi punde. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba taarifa iliyotolewa na hata msemaji wa Serikali amezungumza uchumi wetu umeshuka kutoka asilimia 6.9 mpaka asilimia 4.7 na moja ya sababu ambazo zimeelezwa ni changamoto ya ugonjwa huu wa COVID-19, lakini nataka niipongeze kwa dhati Serikali hii ya Awamu ya Sita pamoja na changamoto hiyo na kupitia Wizara hii ya Fedha imekuwa ikiwezesha shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo miradi ya kimkakati kama ambavyo imeelezwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa dhati pia nimpongeze Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuidhinisha fedha takriban bilioni 172, kwa kila Jimbo milioni 500. Nina imani Mkoa wetu wa Pwani utapata bilioni nne na milioni mia tano pamoja na kwamba Meneja wa TARURA wanawasiliana na Wabunge wa Majimbo lakini niwaombe Wabunge wenzangu wa Viti Maluum nasi tusikae nyuma katika jambo hili tulifuatilie kwa sababu pesa hizi zinaenda kusaidia kurekebisha miundombinu ya vijijini wanakoishi wanawake wengi, wanakojihusisha na shughuli za kilimo na kadhalika. Kwa hiyo, nasi tunayo nafasi tutakaporudi baada ya Bunge hili kufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nipongeze uwezeshaji katika sekta ya afya kwa Wizara hii ya Fedha takriban bilioni 121 zimekwenda kwa ajili ya madawa, pia takriban bilioni 43 kwa ajili ya kumaliza miundombinu ya hospitali ambapo watumiaji wakubwa ni akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo yote haya yamefanyika kutokana na makusanyo ya mapato, licha ya mawasilisho ya taarifa ya ukusanyaji wa mapato mpaka mwezi Mei na kuonesha kwamba mapato yaliyokusanywa ni asilimia 82, naomba niishauri Serikali kwamba moja ya jambo ambalo pia hata Mheshimiwa Rais Mama Samia ameahidi kwa Watanzania na ndani ya Bunge hili ni kuendeleza mazuri ya Awamu zilizopita na kuanzisha mazuri mapya. Moja ya jambo la kujivunia mazuri hayo ni katika ukusanyaji wa mapato Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa inafanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo hili jambo ni ahadi ambayo Wizara ya Fedha na Mamlaka zinazohusika hususan TRA na mamlaka zingine hazina budi kutekeleza kwa nguvu za zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili ninawashauri pamoja na kwamba ufanisi unaoesha tunakusanya asilimia 12 ya mapato ukizingatia na Pato la Taifa, katika nchi za Afrika Mashariki tunalingana na Uganda, tunazidiwa na Rwanda Pamoja na Kenya lakini bado tuna nafasi kwanza; tuongeze wigo wa kodi mpya, lakini pili; tuongeze wigo wa walipa kodi, tatu; tuendelee kuziba mianya ya ukwepaji kodi. Pamoja na kwamba mazingira ya sasa hivi na kwamba TRA mmeelekezwa nami naunga mkono maelekezo hayo ya kufanya ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mbinu za kitaalamu na kwa mujibu wa sheria na matokeo tumeyaona lakini suala zima la kuziba mianya ya upotevu wa kodi iwe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa tumeona zikianzishwa nafasi za mabalozi mbalimbali kuhamasisha sekta mbalimbali, nashauri Wizara ya Fedha ili kuimarisha sekta mbalimbali inaweza pia nao wakaja na mabalozi wa kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari kwa Watanzania. Sambamba na hilo niwaombe Watanzania tunayo property tax imerudishwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kila mmoja tuone tuna kila sababu ya kulipa property tax katika mamlaka zetu ili kuwezesha Serikali kufanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe sekta binafsi wameona namna gani Serikali imewasilisha mipango ya kuboresha mazingira ya sekta binafsi, ikiwemo utekelezaji wa mkakati wa kupitia blue print niiombe sekta binafsi ituongoze katika mapambano ya ulipaji kodi wa hiari na uzuiaji wa ukwepaji wa kodi, wao kwa kuwa ni wafanyabiashara wakubwa, wawekezaji, Serikali kazi yake ni kuandaa miundombinu na kwa kuwa tunaamini kuna methali inasema “kwa kungwi kuliwe na kwa mwali kuliwe” kwa hiyo, nao wana nafasi kubwa kuiwezesha Serikali kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa kuwa pia Wizara ya Fedha wamewasilisha maombi ya bajeti ya Ofisi ya Taifa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, niombe yale yote aliyoyashauri kupitia ya bajeti 2019/2020, hususani kwenye mapato na suala nzima la kuwezesha mamlaka za kusikiliza rufaa za kodi, kwa sababu kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya 2019/2020, takribani kuna kesi au mapingamizi ya kodi ya trilioni 360 na CAG ameshauri Serikali iwezeshe kibajeti na masuala mengine ili mapingamizi haya yasikilizwe. Naamini yako mapato kupitia mapingamizi haya ambayo Serikali itayapata.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kwa kuwa Serikali imeandaa mazingira mazuri ya Sekta binafsi, kuna suala la malipo ya wazabuni ya muda mrefu, ripoti ya CAG imesema zaidi ya bilioni 81 hazijalipwa.

Mheshimiwa Spika, pia kuna ucheleweshaji wa malipo ya wazabuni ambayo yanaweza kuwa kichocheo katika kuongeza ukwasi wa pesa kwenye uchumi, inasababisha malipo ya ziada ya gharama za kuchelewesha. Serikali katika ripoti ya CAG inaoneshwa inadaiwa zaidi ya bilioni 14 ikiwa ni tozo za ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali pamoja na kwamba wanakusanya mapato, lakini yapo matumizi ambayo yanatumika kuongeza ukubwa wa matumizi ya Serikali ambayo yangeweza kuepukwa kama mikakati ya kufanya uhakiki wa madai hayo, kuzingatia kifungu cha 51 cha masharti ya jumla ya mkataba, kwamba mkandarasi anapaswa kulipwa ndani ya siku 28, baada ya certificate yake kupitiwa na Meneja wa Mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kama nilivyosema, jukumu la kuinga mkono Serikali yetu ya Awamu ya Sita na kuiwezesha kutekeleza miradi ni la Watanzania wote na tutalifanikisha kwa kulipa kodi. Niwaombe tulipe kodi, lakini niombe pia, zipo taarifa vituo vya mafuta vimeanza wakati mwingine kuuza mafuta hata bila kutoa risiti. Serikali iiwezeshe Mamlaka ya TRA waipe kibali iajiri watumishi wengi zaidi ili wapange kwenye suala zima la ukaguzi, iwawezeshe kifedha. Vile vile Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, iwezeshwe kama ambavyo kwenye bajeti hii imewasilishwa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, mwisho, nawapongeza Fungu Namba 7 la Ofisi...

SPIKA: Mheshimiwa subiri kidogo, kuna taarifa. Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba hotuba anayoitoa Mheshimiwa Mbunge ya kuhusu kulipa kodi kwa hiari ni jambo la msingi sana na tunatamani hata tuongee na wenzetu wa elimu waanze kuwafundisha watoto kuona pride ile ya kulipa kodi kwa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nchi za wenzetu mtu akisahau risiti hata kama alishaenda mbali anairudia, lakini sisi watu wetu bado wanatamani wapewe bei zile zisizo na risiti na kwa maana hiyo namteua kuwa balozi wa walipa kodi kwa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Subira taarifa hiyo unaipokea.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo nimepokea na nimepokea uteuzi wa Balozi wa walipa kodi kwa hiari na nimuahidi Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwingulu Nchemba na Serikali ya Awamu ya Sita nitaifanya kazi hiyo kikamilifu baada ya Bunge hili, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, nitaendelea kuhamasisha kwa Mkoa wetu wa Pwani na kwa Halmashauri ya Chalinze na Halmashauri zote, kupita kila eneo kuhamasisha ulipaji wa kodi ya hiari, property tax, kupitia kwenye vituo vya mafuta.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa heshima hiyo aliyonipa kuwa balozi wa kwanza wa kulipa kwa hiari ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunipa nafasi kusimama ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Masauni, pamoja na watendaji wote kwa maandalizi mazuri, pamoja na Mawaziri wote kwa Wizara mbalimbali ambazo zilikuwa msingi wa kuandaa bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kazi nzuri anayofanya. Waziri Mkuu amekuwa champion wa mazao mbalimbali ya kimkakati, utamuona kwenye mazao ya korosho, pamba, alizeti na mkonge. Katika u-champion wake umesababisha Serikali kuleta marekebisho mbalimbali ya tozo kwenye mazao hayo ili kulinda uwekezaji wa ndani na kuwawezesha wakulima. Kwa hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi anazoendelea kufanya. Na kutokana na uwajibikaji wake unaoendelea, na matokeo mazuri ya bajeti iliyowasilishwa, imenifanya nikumbuke maneno aliyoyasema kwenye hotuba yake baada ya kuapishwa tarehe 19 Machi, 2021 pamoja na huzuni aliyokuwa nayo, Mheshimiwa Rais alisema yafuatayo: nanukuu “Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya yamejidhihirisha kwa kazi mbalimbali zinazoendelea. Sambamba na hilo kwenye ukurasa wa sita wa bajeti aliyowasilisha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amenukuu ahadi ya Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan ya kudumisha mazuri ya awamu zilizopita kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya. Kwa kazi zinazoendelea tumemuona kwenye ujenzi wa SGR, uwekaji wa jiwe la msingi kipande cha Mwanza – Isaka, tumemuona akishuhudia mikataba ya ujenzi wa meli tano Mwanza jioni hii. Tumemuona kwenye uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata dhahabu yote haya yanadhihirisha ahadi yake ya kuendeleza mema yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye masuala ya kuleta mengine mapya ambapo ndipo nitakapojielekeza, napenda niipongeze Serikali kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kuamua kulipa madeni ya Mifuko ya Hifadhi zaidi ya trilioni nane kwa utaratibu wa non-cash special bond isiyotumia pesa, haijapata kutokea. Wastaafu wa nchi hii wanakwenda kupata ahueni hata sisi watoto wa wastaafu tunashukuru kwa hatua hii ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Serikali imekuja na ubunifu wa kuangalia vyanzo vingine vya mapato kwa kuwa na mtazamo wa kuja kutumia masuala ya Euro bond, pia kwa kujielekeza Serikali kufungua soko la ndani la hati fungani kwa wawekezaji wa nje, Serikali kuanzisha bima ya afya Watanzania wote, Serikali kuamua kulipa posho za madaraka kwa Watendaji wa Tarafa na Kata, Serikali kuanza kuzipa mitazamo mipya Halmashauri zetu za Majiji na Manispaa kutumia masuala ya hati fungani katika ku-finance miradi yao ambayo inakwenda kupunguza mzigo wa Hazina kutoa pesa kwa ajili ya Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee katika hilo, nipongeze ubunifu wa kupendekeza vyanzo vya mapato kuongeza Mfuko wa TARURA kwa ajili ya barabara zetu. Hapa nishukuru kwa kiasi cha bilioni nne na milioni mia tano ambazo Mkoa wetu wa Pwani tumezipokea na pendekezo la bilioni 322. Niwaombe Watanzania barabara za vijijini ni kila kitu zinasafirisha malighafi, zitawezesha viwanda vyetu, zitapunguza gharama za uzalishaji, zitawawezesha akina mama kufika kwenye vituo vya afya, zitapunguza gharama za usafirishaji. Kwa muktadha huo naomba nishukuru kwa kusema kwamba barabara ya Chalinze – Nsigi – Talawanda – Bago inakwenda kupata faida hii. Barabara ya Lugoba – Mindukene – Talawanda – Magulumatari, barabara ya Kibiti – Mkongo – Mwaseni inaenda kupata faida ya hela hizi. Barabara ya Bungu – Nyambunda; barabara ya Kimanzichana – Mkamba – Panzui – Msanga, maeneo ya Mkoa wa Pwani ndiyo maana tuna sababu ya kuunga mkono bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii kwa sababu Serikali imekuwa sikivu. Kamati yetu ya Bajeti imependekeza mambo mengi lakini kati ya hayo pamoja na Wabunge wote Serikali imechukua zaidi ya asilimia 70 ya mapendekezo hayo. Hii inaonesha namna gani Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na timu yako, mkiongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, mmeweza kumshauri vizuri Mheshimiwa Rais wetu, naye amekubali mapendekezo hayo leo yapo ndani ya Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima la miradi ya maji; pendekezo la kuongeza tozo kwenye masuala mazima ya mawasiliano kwa ajili ya kusaidia miradi ya maji, naomba Watanzania tuliunge mkono hili jambo kwa sababu maji nayo ni uhai, maji ni kila kitu. Sambamba na hilo, ninaomba tu kutoa ushauri kwenye suala zima la nia ya Serikali ya kufuta msamaha kwenye suala la taa za solar. Katika hili niiombe Serikali yangu Sikivu ilitazame tena hili. Kwa sababu yapo maeneo bado yanatumia umeme wa jua na bado yapo matumaini, kwa mfano maeneo ya Visiwa vya Kibiti, maeneo ya Mbwela Mashariki, Mbwela Magharibi, Maparoni, Salale na Mkuranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Visiwa vya Kwale, Koma, tuna Visiwa vya Bwejuu, Jibondo, maeneo ya Mafia bado tunasubiri umeme wa solar. Kwa hiyo niombe sana tozo hii, vifaa vyote vya umeme viendelee kusamehewa kodi ili kuweza kuwafanya Watanzania wenzetu wanaoishi visiwani waweze kupata huduma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishukuru Serikali kwa mkakati wake wa kuweza kutaka kupandisha vyeo watumishi wa Serikali. Mmetenga bilioni 400 kwenye bajeti kwa ajili ya kupandisha vyeo watumishi 92. Niwaombe tu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Mchengerwa kuzisimamia pesa hizi zitumike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo utaratibu mara nyingi maafisa utumishi wamekuwa wakichelewa kuwapandisha watumishi vyeo, badala yake hela hizi unapofika mwisho wa mwaka zinakuwa zimesalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niunge mkono hatua zote za Kiserikali za kufanya maboresho ya kodi mbalimbali zenye nia ya kulinda viwanda vyetu. Sisi Mkoa wa Pwani tunashukuru ulindaji wa viwanda vya marumaru, vipo viwili tu nchi nzima ambavyo ni kiwanda cha Keda Chalinze na kiwanda cha Goodwill Mkuranga. Tumeona namna ambavyo Serikali mmetia mguu katika marumaru inayouzwa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama vile hiyo haitoshi kwa upande wa akina mama tunashukuru tozo mbalimbali ambazo zimeondolewa kwenye masuala ya kilimo cha mbogamboga na matunda, kwenye masuala ya usindikaji wa maziwa, kwenye masuala ya bima ya mifugo, kwenye masuala ya mazao mbalimbali ambayo ama kwa hakika tunashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimalizie kwa kuwapongeza Kamati yetu chini ya Mwenyekiti kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti hapa ndani. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hatua yake ya kuupa msukumo mradi wa kusindika gesi asilimia Mkoa wa Lindi, mradi wa Mchuchuma Liganga, mradi wa bomba la mafuta, yote haya ambayo yamewekewa hatua za kikodi ili miradi hii iweze kuchangia ajira kwa Watanzania, iweze kuchangia mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Balozi wa kuhamasisha kodi, nimalizie kwa kuwaomba Watanzania kulipa kodi kwa sasa hivi na hatua zinginezo. Niwaombe tuendelee kulipa kodi ni umeme, imepunguzwa sasa hivi 27,000 maeneo yote, kodi ni elimu kwa vijana wetu, Serikali imeongeza zimefikisha bilioni 500 kila kijana wa Tanzania atakayekuwa na sifa za kwenda chuo kikuu atapata mkopo, hiyo ndiyo kodi ya Watanzania. Pia kodi ni barabara kila kijiji cha nchi hii kitapata barabara. Kodi ni madawa tumeona mtazamo wa Serikali wa kumaliza maboma 8,000 na vituo vya afya 1,500 pia kuongeza madawa bilioni 263 zimetengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe wafanyabiashara, mazingira wezeshi katika bajeti hii yameainishwa, mmepunguziwa viwango mbalimbali vya kodi, mmepunguziwa urasimu mbalimbali lakini kubwa Serikali imeweza kutatua mfupa wa asilimia 15 ya gharama za sukari ya viwandani. Wafanyabiashara mmeachiwa ili kuongeza ukwasi kwa uchumi ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sote kwa pamoja tumuunge mkono jemedari wetu, mweledi, mchapakazi, mama yetu kipenzi, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na tunakuombea dua, Mwenyezi Mungu akujalie na tunaamini utatufikisha pale panapostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo kuchangia Muswada wa Fedha wa Mwaka 2020/2021. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na timu yake yote ya Wizara ya Fedha pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Masauni kwa kazi nzuri na ushirikiano mzuri ndani ya kamati yetu. Naunga mkono hoja hii, lakini naishukuru sana Kamati ya Bajeti kwa kutumia muda mwingi wenye nia njema kujadiliana na Serikali na mapendekezo yote ambayo yameainishwa kwenye taarifa yetu yote nayaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maoni machache, kwanza katika Amendment ya VAT, section 81 naipongeza Serikali kwa kutambua bidhaa za mtaji zinazotambulika kwa Sura 84, 85 na 90 ya Kitabu cha Ushuru wa Pamoja wa Forodha kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo hizi zitastahili kupewa vivutio vya hairisho la kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani.

Pamoja na hatua hii ambayo itapunguza gharama za uwekezaji na kuchochea uwekezaji nchini, naomba Mheshimiwa Waziri na timu yake ikajielekeze kwenye masharti ya kupata vivutio vya hairisho hili kwenye Sheria ya VAT hasa section 11(2)(b) ambayo imesema angalau asilimia 90 ya bidhaa ama huduma zinazozalishwa au zitakazozalishwa ziwe zile ambazo hutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini natoa pendekezo hili? Mheshimiwa Spika alielekeza Bunge hili la Kumi na Mbili liwe Bunge ambalo litaleta mapinduzi makubwa kwenye kilimo. Sasa ukiangalia section hii masharti ya kutoa ahirisho la kulipa VAT, wapo wawekezaji kwa mfano wa sekta nzima ya ujenzi wa viwanda vya mbolea, ambapo mbolea inayoingizwa ndani ya nchi inatozwa ushuru wa zero rate na pia inapata msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani. Kwa hiyo, maana yake kama viwanda vya ndani vitazalisha mbolea, inaweza ikakosa fursa hii ya kupata uahirisho wa kodi la ongezeko la thamani. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu ikaliangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilikuwa naomba pia, pamoja na mapendekezo ya Kamati yetu kwenye Sheria ya Wakala wa Meli, sura ya 414, pamoja na nia njema ya kuunda TASAC na kazi zinazoendelea vizuri, lakini naomba Serikali ikatazame kile kifungu Na. 7 na ikatazame Sheria nzima hii, kutokana na maoni ya wadau mbalimbali waliokuja kwenye Kamati ya kuona mwingiliano wa majukumu ya kudhibiti hii sekta na kutenda shughuli zinazohusiana na masuala mazima ya TASAC. Kwa hiyo, naomba Serikali iwasikilize vizuri kwa sababu, wana nia njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ningeomba pia niipongeze Serikali; kwa pamoja tumekubaliana kwenye mashauriano wakafanye marekebisho ya Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania, Sura ya 38 pamoja na kwamba kwa sasa wamefuta ili kufanya marekebisho ya sheria hii kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa spirit ile ile ambayo Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, kupitia bajeti hii na Serikali yake, ameonyesha kupunguza urasimu. Mkatazame uwekezano wa kumpa mamlaka Waziri wa Fedha katika kutoa idhini ya vivutio vinavyoidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya kutoa vivutio, mara nyingi pana kukwama. Kamati ya Kitaifa inatoa vivutio, lakini inapokuja kwenye sheria za kikodi mamlaka ya Waziri wa Fedha yalikuwa bado hajapewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama ambavyo mmetoa sasa, mamlaka ya Kamishina wa TRA na wewe Waziri wa Fedha, kwenye miradi ambayo inatekelezwa na wafadhili, imekupa fursa hiyo ambayo itawezesha kuondoa urasimu na miradi yetu kutekelezwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilipongeze Bunge lako Tukufu, jana limefanya mapinduzi. Nimehudumu Bunge la Kumi, nimehudumu Bunge la Kumi na Moja na leo Bunge la Kumi na Mbili, sijapata kuona bajeti ambayo imepitishwa bila kupigiwa kura ya hapana hata moja. Jana tumepiga kura 94%, lakini 6% wao hawakuwa na msimamo popote. Nini tafsiri yake? Ni kwamba katika bajeti hii ya mwaka 2021/2022, kwa kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri inayofanywa na Baraza lake la Mawaziri, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Bunge tumeridhika kwa kiwango cha juu. Tumeridhika na yale maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwa mara ya kwanza zimeongezwa fedha hapa juu kwa juu ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inamaanisha Mheshimiwa Waziri wa Fedha katikati ataleta supplementary budget ili yale aliyosema, ongezeko la shilingi bilioni 322 kwa Mfuko wa Barabara, ongezeko la shilingi bilioni 70 kwenye Bodi ya Mikopo, ongezeko la shilingi bilioni 50 kwenye madawa na ongezeko la shilingi bilioni 121 kwenye maji. Yote hayo yatawezekana Bunge tena tukifanya mapinduzi kama jana ya kuipitisha sheria hii ya fedha, ambayo imeweka utaratibu sasa wa kuweza kukusanya na kupeleka kwenye mafungu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali, licha ya kwamba imeboresha sheria mbalimbali, lakini kazi inaendelea. Naishukuru kwa sababu zaidi ya Watumishi wa Umma 70,000 washapandishwa vyeo na shilingi bilioni 300 zimetoka. Hongera Mheshimiwa Mchengerwa kwa kazi nzuri hii kutokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Hata punguzo la kodi la 8% kutoka 9% kwenye Muswada wa Fedha huu, lengo ni kumsaidia mfanyakazi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba haitoshi, jambo lingine ambalo limempa credit mama yetu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ni kwenye vyombo vya ulinzi na usalama. Ile punguzo la miaka kutoka 12 mpaka miaka sita, ili askari huyu aweze kupata pension, aweze kuchangiwa; na tunatambua licha ya mambo mazuri, mipango, uwekezaji ambao unahimizwa na Serikali yetu, bila ya ulinzi na usalama mambo haya hayawezekani.

Kwa hiyo, hatua hii ya Serikali ya kuwawezesha vyombo vyetu kupunguza hii miaka ya mkataba, ninaiunga mkono na ninaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba haitoshi, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais alipokuwa Mwanza wakati wa Sherehe za Wafanyakazi, alitoa maelekezo kwamba Bima ya Watoto ambayo ilikuwa inaishia miaka 18 iende mpaka miaka 21. Hili sijaliona katika sheria hii, naomba nalo mlishughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kana kwamba haitoshi, ninampongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa hata marekebisho ya sura ya 178 ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, kwamba ongezeko lolote lipate idhini ya mashauriano baina ya Waziri mhusika na Waziri wa Fedha, lenye nia ya kulinda utozaji holela, nalo pia lina msaada mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naipongeza Serikali kwa kuridhia kutoa mikopo kwenye taasisi zake zinazomiliki zaidi ya asilimia 50, katika marekebisho ambayo yamefanywa ya Ibara ya 13, Taasisi za Umma zinachangia mapato kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Nampongeza Msajili wa Hazina na Wizara ya Fedha kwa kiwango cha mapato yanayopelekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Kumekuwa na ongezeko kubwa.

Kwa mfano, mwaka, 2019/2020 shilingi bilioni 983 zilipelekwa ukilinganisha na shilingi bilioni 161 mwaka 2014/2015. Ni wazi Serikali kwa kutoa fursa hii, itawezesha makampuni, kwa mfano TPDC kuingia mikopo ili kuweza kusambaza gesi na hivyo kuwezesha wanawake kuacha matumizi ya kuni kwa ajili ya nishati ya kupikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, niendelee kutoa pongezi, niwatakie kila la heri Waheshimiwa Mawaziri wote, najua baada ya bajeti hii mnapata kitendea kazi. Niendelee kuwahimiza Watanzania kulipa kodi kwa hiari. Sheria zilizowekwa hapa Mheshimiwa Waziri amefafanua vizuri, tozo itakusanywa; inaenda kufanya nini? Imeweka mikakati ya kuziba mianya ya upotevu, pia imeweka mikakati ya kuongeza vyanzo vya kodi; na kana kwamba haitoshi, imeweka mkakati wa utekelezaji wa blueprint na kuhamasisha shughuli mbalimbali za uwekezaji. Haya yote yanayofanywa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya, naunga mkono hoja. Nawapongezeni sana na kwamba mambo yatakuwa mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nianze kusema naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge wakati wanachangia hoja hii, lilijitokeza suala la utekelezaji wa Mradi wa Rufiji Hydro Power maarufu kama Stiegler’s Gorge. Michango ile ilielezea wasiwasi wao kuhusu utekelezaji wa mradi huu na masuala ya mazingira. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kuwa utekelezaji ni kweli Serikali ya Awamu ya Tano itatekeleza Mradi huu wa Rufiji Hydro Power ambao utazalisha Megawati 2,100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia hata historia mbalimbali za mradi huu tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza mpaka ya Nne na mpaka hii ya Tano, tathmini mbalimbali juu ya mazingira zilifanyika. Katika taarifa zile za tathmini hakuna mahali popote ambapo ilionekana mradi huu usitekelezwe kwa sababu ya mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka nilithibitishie Bunge lako tukufu kuwa mradi huu Serikali zote zilizopita zimefanya tathmini lakini Serikali hii ya Awamu ya Tano imeamua kuutekeleza kupitia mapato ya ndani kutokana na uhitaji mkubwa wa nishati ili kutekeleza uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali imejielekeza kuzalisha Megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020. Ni kweli mpango huu kabambe wa Power System Masterplan umeelekeza miradi midogomidogo ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji, lakini mradi huu na ukilinganisha na gharama ya kuzalisha umeme kwa unit moja kwa kilowati kwa kutumia maji ni Sh.36/=, kwa kutumia gesi ni Sh.147/=, kwa kutumia mafuta ni Sh.346/=, ni wazi utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji ni nafuu. Vile vile kwa kuwa lengo la Serikali ni kupata nishati ya umeme yenye unafuu na Watanzania waweze kuitumia majumbani, viwandani, kwa hiyo, lazima tutekeleze huu mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ambayo imetajwa kwa huu mradi kabambe wa kuzalisha umeme kwa mfano Rumakali, Luhuji, Mpanga, Songwe, Rusumo, Malagarasi, Kakono, ni kweli ipo, lakini hii itatekelezwa baina ya ubia binafsi na wadau mbalimbali. Kwa hiyo, nataka nilitaarifu Bunge lako kwamba kwa kweli naomba watuunge mkono, mahitaji ya umeme ni mengi na Serikali imethubutu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu wake na mradi huu unatekelezeka bila tatizo lolote. Hata sasa wataalam wa chuo kikuu wameshamaliza Environmental na Social Impact Assessment na wataiwasilisha Wizarani na NEMC baada ya wiki moja. Kwa hiyo, naomba tu Bunge lako Tukufu lituunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, lilijitokeza suala la upatikanaji wa nishati au deni la umeme kwa Shirika la ZECO Zanzibar. Naomba niwaarifu wenzetu upande wa Zanzibar kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo na tumeipa kazi EWURA ifanye study ya gharama mbalimbali za kuzalisha umeme ili tufikie muafaka. Naamini Kamati yetu ya Nishati na Madini ilitu-task hiyo kazi na tunaendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu Zanzibar kupitia ZECO wanalipa lile deni kiwango ambacho tunakubaliana, lakini lile deni ambalo hatujafikia muafaka mazungumzo yanaendelea na baada ya miezi miwili utafikiwa muafaka na hili deni litakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wazara hii kwa kazi nzuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa afya njema inayoniwezesha kutoa mchango katika sekta zinazosimamiwa na Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba na Naibu wake pamoja na Makatibu Wakuu na wafanyakazi wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuendeleza Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kujielekeza kwenye tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa sehemu ya bajeti ya maendeleo ambapo hadi tarehe 30, Aprili, 2016 kiasi cha shilingi 5,192,797,589/= tu zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ikiwa ni asilimia 15.9 ya fedha zilizoidhinishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii ya kutopeleka kwa wakati fedha za maendeleo zinaweza kufifisha jitihada ya kuleta mapinduzi ya kilimo itakayopelekea uzalishaji wa malighafi zitakazotumika kwenye viwanda, ambacho ndiyo kipaumbele cha Serikali hii ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali nashauri ijitahidi kupeleka kiasi kilichosalia kwenye Fungu hili la maendeleo la Wizara hii ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kupongeza Wizara, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Bodi ya Korosho, Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Pwani na wadau wengine wa korosho kwa kuwezesha mfumo wa Stakabadhi Ghalani kuanza kutumika tena katika Mkoa wetu wa Pwani. Mfumo huu wa stakabadhi ghalani kwa mwaka huu umepelekea wakulima wa korosho wa Wilaya za Rufiji, Mkuranga, Kisarawe, Bagamoyo na Kibaha kupata bei nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza sana Serikali kwa kuwezesha Vyama Vikuu na Vyama vya Ushirika vyenye madeni ya zamani katika Benki za CRDB na NMB kushiriki katika msimu huu wa korosho na kuweka utaratibu wa kurejesha madeni hayo ya Vyama vya Msingi bila kuathiri hela za wakulima. Naipongeza sana Benki Kuu ya Tanzania kwa kukubali kuwa msuluhishi/mpendekezaji wa utaratibu wa ulipaji wa madeni ya vyama hivyo bila kuathiri utaratibu wa Stakabadhi Ghalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Wizara kuhakikisha pembejeo za zao la korosho (dawa) zinapatikana kwa wakati ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa korosho na hivyo kuipelekea nchi kupata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nianze kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuisimamia Serikali ndani ya Bunge lakini pia na nje ya Bunge kwa kazi mbalimbali anazofanya mikoa mbalimbali. Niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri katika Wizara hii, Mheshimiwa Jenista na Mheshimiwa Angellah Kairuki pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanazofanya lakini pia kwa hotuba ambayo imewasilishwa ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta yetu ya nishati ni nyeti na ndiyo maana kwenye mjadala wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa Wabunge wengi wamepata fursa ya kutoa uchauri, kuelezea wasiwasi wao na wengine pia wamepongeza. Kwa hiyo, kama Wizara tunashukuru kwa pongezi zote na tumepokea changamoto mbalimbali ambazo zimewasilishwa na tunaahidi tutaendelea kuzitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta yetu ya nishati ina mambo mengi; inasimamia suala zima la uzalishaji umeme, usafirishaji na usambazaji. Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia wamejielekeza pia kwenye jambo kubwa la muhimu la usambazaji wa umeme, hususani wamejielekeza kwenye mradi wa REA unaoendelea na wameonyesha changamoto ambazo zipo na wasiwasi pengine huu mradi unaweza usikamilike ndani ya wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwataarifu Waheshimiwa Wabunge, kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Tano, kupitia Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini, inatekeleza miradi mbalimbali ya umeme vijijini. Pamoja na changamoto ambazo zimejitokeza, nataka niwape matumaini kwa kweli huu mradi unaendelea. Tangu tarehe 1 Julai, 2016 mpaka tarehe 30 Machi, 2019 takribani Vijiji 1,969 vimeshapelekewa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichanganya na vijiji ambavyo vilikuwa vimepelekewa miundombinu ya umeme mpaka tarehe 30 Juni, 2016 kama 4,396, tunapozungumza sasa tuna vijiji takribani 6,365 vyenye umeme kati ya vijiji 12,268 na hii ni asilimia 52 ya vijiji vyote kwa mujibu wa takwimu ambayo tumepata kupitia TAMISEMI. Nini maana yake? Maana yake ni kwamba pamoja na changamoto zinazoendelea lakini kazi inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge tunavyoupima Mradi wa REA Awamu ya Tatu, ni kweli mikataba ilianza 2017, sote tulishiriki hapa lakini tarehe kabisa ya kuanza kazi tunaipima pale wakandarasi walipofunguliwa Letter of Credit ambayo ni Julai, 2018. Kwetu sisi mradi una miezi 24 na utakamilika tarehe 30 Juni, 2020. Itakapofika tarehe 30 Juni, 2020 jumla ya vijiji 9,055 vitakuwa vyote vimepatiwa umeme na vitakavyosalia ni vijiji 3,213 ambavyo mpango wake na taratibu zake zimeanza katika Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikijibu maswali mengi na nashukuru pamoja na Waziri wangu mmekuwa mkitupa changamoto mbalimbali lakini kwetu sisi Wizara namna ambavyo tumeweka usimamizi ngazi ya Wizara, Kanda TANESCO na ndani ya REA na hivi karibuni tunaishukuru Seikali ilitupatia fedha tukaipa magari mikoa yote zaidi ya 26 kwa ajili ya usimamizi wa mradi huu na usimamizi ngazi ya wilaya na ma-technician.

Naomba niwatoe hofu hivi karibu tumetoa maelekezo kila wiki kuwasha vijiji vitatu na kila wakati tunapata taarifa. Tumetoa maelekezo ya kuwa kila wilaya kuwa na magenge zaidi ya matano. Kwa hiyo, naomba mtuamini kwamba sisi tunachopambana ni kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba vijiji vyote nchi nzima ifikapo 2021 vipatiwe umeme. Kwa hiyo, mtuamini kwamba uwezo tunao, nia tunayo na nguvu tunayo ya kulisimamia hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoendelea pia tutaliomba Bunge lako Tukufu litaidhinisha mradi, tunaanza densification Awamu ya Pili. Pamoja na kwamba hivi nilivyovitaja ni vijiji lakini ni wazi kwamba miradi kama hii mikubwa kwa Serikali inayofanya miradi mikubwa mingi; ujenzi wa Bwawa la Stiegler’s na ujenzi wa miundombinu mbalimbali lazima kuwe na wigo. Kwa hiyo, baada ya kuona hivyo Serikali imetafakari tunakuja na mradi mwingine wa Ujazilizi Awamu wa Pili ambao utagusa vitongoji. Kwa hiyo, ikifika kwenye kijiji kama umefika kwenye vitongoji vitatu au vinne vimesalia vitongoji ujazilizi unakuja na zaidi ya shilingi bilioni 290 zimetengwa kwa ajili ya kazi hizo pamoja na miradi ya peri- urban kwa Majiji makubwa zaidi ya shilingi bilioni 86 za kuanzia zimetengwa na Serikali yetu ya Awamu ya tano kupitia Wizara ya Nishati na taasisi zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imefanya uamuzi wa kisera, kupitia agizo la Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, baada ya kutafakari upelekaji wa miradi ya nishati vijijini na hoja ya kwamba ikipeleka TANESCO au na wadau wengine kuwe na bei tofauti au ikipelekwa na REA inakuwa na bei tofauti. Serikali imefanya maamuzi kuanzia sasa hivi miradi yote hiyo itapelekewa umeme wananchi wataunganishwa kwa bei ya Sh.27,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niseme wazi kabisa, Serikali itandelea kupambana na wale Vishoka ambao wanawaongezea wananchi bei lakini bei ya kuunganishia umeme ni Sh.27,000. Hii italeta matumaini hata kwa wananchi tunaowaambia wasubiri kwamba TANESCO watapeleka umeme vijijini kwa kupitia Sh.27,000, REA Sh.27,000 na sekta binafsi nayo Sh.27,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo limezungumzwa ni suala la uzalishaji wa umeme. Serikali yetu imefanya mapinduzi kupitia Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, imekuwa na maono ya kuzalisha umeme mwingi ambao utashusha gharama ya umeme. Umeme mwingi utakaozalishwa ni kupitia vyanzo vya maji. Tunao mradi wa Stiegler’s Gorge MW 2,115 tumeshamkabidhi mkandarasi site anaendelea vizuri; Mradi wa Rusumo MW 80 anaendelea vizuri; tumeanza mchakato wa Mradi wa Rumakali MW 358; na Mradi wa Ruhuji MW 222 unaendelea. Kwa hiyo, nataka niseme dhima au mpango huu wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha ifikapo 2025 tunazalisha MW10,000 kwa ajili ya kuhimili uchumi wa viwanda unaojengwa kwa kasi kubwa katika awamu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme dhima hii au mpango huu wa Serikali Awamu ya Tano ni kuhakikisha ifikapo 2025 tunazalisha Megawati 10,000 kwa ajili ya kuhimili uchumi wa viwanda unaojengwa kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine limezungumzwa hapa kwamba Serikali imeacha kutumia gesi, siyo kweli. Serikali inaendelea kutumia gesi kwenye masuala mbalimbali. Gesi katika kuzalisha umeme; na kwa sasa tuna mradi Kinyerezi I Extension Megawati 185; tumemaliza Kinyerezi II megawati 240; kuna mpango wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme Megawati 300 Mtwara pamoja na njia za kuzalisha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukisema eti Serikali imehama kwenye uchumi wa gesi siyo sahihi na hata sasa tunasambaza gesi kwenye viwanda mbalimbali vikiwemo viwanda vya Jimbo la Mheshimiwa kaka yangu Ulega hapa Mkuranga. Tunaongeza viwanda vitano kuvisambazia gesi ili kupunguza gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile mmesikia kiongozi wa Ujerumani ameipongeza Serikali na ameahidi kuleta kiwanda kikubwa cha mbolea na tumeshafikia makubaliano ya bei ya gesi kwenye viwanda vyote vya mbolea. Kwa hiyo, utaona gesi bado ina mchango mkubwa katika uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwamba hivi karibuni pia Mheshimiwa Rais ametuzindulia mradi wetu wa kusafirisha umeme wa Kilovoti 220, Makambako, Songea. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake kwa kazi nzuri anayoifanya na kwenye sekta yetu hatuna shida, hatuna tatizo la pesa. Tumekuwa tukiidhinishiwa na Wizara ya Fedha, nawashukuru sana. Hata ninaposema sasa, zaidi ya asilimia 16 tumeshapata pesa zake. Tunawaahidi tu utumishi uliotukuka na usimamizi wa miradi hii. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi/Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa kuchangia katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Nianze kwa kuunga mkono hoja hii na kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Naibu wake na viongozi wote wa Wizara hii, kwa kazi nzuri wanayoifanya hususan katika ulinzi wa maliasili zetu na vyanzo mbalimbali vya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kuchangia hoja kwa dakika chache ambazo umenipa, lakini nikirejea hutuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuanzia ukurasa wa 18 ambayo imeelezea muktadha mzima wa Rufiji hydropower na nimshukuru Naibu Waziri wa Fedha amesema, sitarejea katika upande lakini nimpongeze sana wake.

Ninachotaka kuwaomba Watanzania na Waheshimiwa Wabunge, kwa kuwa mradi umeanza na tunatarajia mwezi wa Saba kuweka jiwe la msingi na kazi mbalimbli za mazingira wenzeshi, masuala ya mobilization tayari, nadhani itakuwa ni kupoteza muda kuanza kuujadili kwa misingi ya kwamba turudi nyuma, haturudi nyuma. Hilo nataka niliseme wazi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka nirejee kulitaarifu Bunge lako na nilipata kusema, mradi huu mradi huu ulifanyiwa tafiti mbalimbali na kimsingi tafiti zote hakuna tafiti ambayo iliainisha kwamba mradi huu hauna faida yoyote. Kwa sasa tunapotekeleza mradi huu imeshafanyika environment social impact assessment imeshafanyika strategic environment assessment ambazo wenzetu wa Maliasili wanaweza kulisemea vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ninachotaka kusema sisi tumeangalia faida na hasara zake na hususan kwenye kwenye kumpunguzia mtanzania gharama kubwa ya matumizi ya umeme. Tumetathmini vyanzo mbalimbali na kwa kuwa tunatekeleza mpango kabambe wa umeme ambao umeainisha kila chanzo kinatakiwa kizalishe megawatt ngapi ili kufanya ile energy mix ya nchi iwe stable.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nilitaalifu Bunge lako Tukufu kwa kweli kwa namna ambavyo chanzo hiki cha maji kinagharimu shilingi 36, umeme unazalishwa na gesi unagharimu shilingi 147 umeme unazilishwa na mafuta unazalisha Sh.526. Pia ukiangalia gharama za uwekezaji, unapowekeza kwa kutumia imetajwa joto ardhi unatumia Sh. 10,039 kwa megawatt moja tofauti na unapowekeza kwa kutumia maji watumia Sh.6,000 kwa megawatt moja, kwa hiyo utaona hata gharama za uwekezaji zina nafuu kwenye miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, chanzo cha joto ardhi Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza, Wizara ya Fedha imeleta bilioni 32 kununua mitambo ya uchongaji wa visima vya majaribio. Kwa hiyo nataka niseme kwa kweli kwa Serikali yetu kwa energy mix inayoendelea tuna imani kabisa mradi huu mkubwa wa Rufiji hydropower utakaozalisha megawatt 2115 ndiyo mkombozi kwenye uchumi wa viwanda, lakini lile lengo la Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kupunguza gharama ya umeme kwa watumiaji wa kawaida na viwandani litatimia kwa kuwa itakuwa ndiyo mradi mkubwa wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi nchi mbalimbali zilizoweza kujenga mabwabwa makubwa, ikiwemo Ethiopia ikiwemo Unganda, na nchi nyingine zimewezaje na sisi tushindwe kwa ajili tu ya masuala ya mazingira? Kwa hiyo, nikuthibitishie sisi watekelezaji Wizara ya Fedha imetuwezesha, tunaendelea kusimama mradi huu kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara hii kimaandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mawaziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Mheshimiwa Dkt. Hamis Kigwangalla kwa kazi nzuri ya kusimamia mapinduzi makubwa ya uboreshaji wa huduma za afya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zinajieleza kwenye maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la bajeti ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/ 2016 mpaka shilingi bilioni 251.5 kwa mwaka huu 2016/2017. Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017 imetoa matumaini makubwa ambapo mpaka sasa kiasi cha shilingi bilioni 112.19 zilipokelewa MSD. Kati ya hizo, Mkoa wa Pwani Hospitali zetu na Vituo vya Afya tunategemea kiasi cha shilingi bilioni 1.6. Tunawapongeza sana kwa jitihada hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ununuzi na usambazaji wa vitanda vya kawaida 20, vitanda vya kujifungulia vitano, magodoro 25 na mashuka 50 kwa Halmashauri zetu zote vilivyogharimu shilingi bilioni 2.93.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mfuko wa Bima ya Afya ya Pamoja, napongeza hatua zilizochukuliwa na Wizara kuhakikisha kuwa fedha za dawa kupitia Mfuko wa Pamoja zitapelekwa moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma, hatua hii itachangia upatikanaji dawa kwa wakati kwa wananchi wetu. Pamoja na pongezi hizo, katika maeneo machache naomba kushauri yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri yetu ya Chalinze, Wizara ilikubali ombi la kupandisha hadhi Kituo cha Afya Msoga kuwa Hospitali ya Halmashauri. Ombi langu, naomba Wizara ilete watumishi ili kukidhi haja ya kuipandisha hadhi. Kukosekana kwa watumishi wa Sekta ya Afya katika Hospitali hiyo tarajiwa ya Halmashauri, imepelekea pesa za Basket Fund takriban shilingi milioni 90 kati ya fedha zote zilizopokelewa kushindwa kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kusimamia ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne ya kupandisha hadhi Kituo cha Afya Mlandizi kuwa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini na Kituo cha Afya Kibiti kuwa Hospitali ya Wilaya mpya ya Kibiti. Maeneo haya yana wananchi wengi, hivyo vituo hivyo vinazidiwa na idadi ya wagonjwa, lakini kuwa na mgawo ule ule wa hadhi ya kituo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Fedha. Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniamsha salama na kusimama ndani ya Bunge lako na naanza kwa kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na jambo la msingi lililozungumzwa na Waheshimiwa wachache waliopita juu ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011. Najielekeza kwenye Sheria ya Manunuzi ya Umma kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais kupitia hotuba yake ndani ya Bunge hili lakini kutokana pia na mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo asilimia 40 inatarajiwa kutumika kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunatambua wakati ule ilipokuwa chini ya asilimia 40, kwenye asilimia 22 na kuendelea tuliona changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, udhaifu wa taasisi mbalimbali katika usimamizi wa matumizi ya pesa za maendeleo na za kawaida. Leo tulipopokea taarifa ya miscellaneous amendment zinazotarajiwa kuwasilishwa Bungeni kutoonekana kwa Sheria ya Manunuzi ya Umma imetufanya baadhi ya Wabunge tupate mashaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mashaka hayo nikaenda kuchukua taarifa ya PPRA ya mwaka 2014/2015; nikajaribu kupitia kwa kina upungufu uliobainishwa na taarifa hiyo. Pamoja na kwamba taarifa inaonesha masuala ya manunuzi ya umma katika taasisi mbalimbali za kiserikali level of compliance iko juu lakini ukaguzi wa mashirika haya, kwa mfano mwaka 2014/2015 wamekagua jumla ya taasisi za manunuzi 80 kati ya hizo 39 ni za Halmashauri, lakini tunazo Halmashauri 168. Kufanya maamuzi ya kuchelea kuleta marekebisho ya sheria kwa ripoti kwamba labda mambo siyo mabaya si sahihi kwa sababu hata ukaguzi unafanyika kwa taasisi chache.
Kwa hiyo, niombe Serikali iwasilishe Muswada huo tufanye marekebisho kwenye baadhi ya vipengele ili asilimia 40 ya fedha za maendeleo zilete tija na value for money na matumizi hayo yaonekane ili Watanzania wenzetu waweze kufaidika katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo naungana na Waheshimiwa Wabunge, kwa kuwa mimi ni Mbunge wa Viti Maalum na kundi kubwa naloliwakilisha hapa ni wanawake na vijana; na wanawake na Watanzania wengi walikipigia kura chetu kwa matumaini ya ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Tunaamini ahadi hii ikitekeleza itakuwa chachu katika uibuaji wa miradi mbalimbali na pia itakuwa chachu ya mzunguko wa fedha katika maeneo yaliyokusudiwa. Naungana na maoni ya Kamati yangu, Serikali pamoja na changamoto iliyopo, lakini dhima ya kuinua uchumi wa watu wachache au kupitia vikundi vya SACCOS ni muhimu kwa sababu mwisho wa siku watalipa kodi kutokana na shughuli watakazozifanya na itaongeza mapato ya Serikali, huu ni mzungunguko tu.
Kwa hiyo, niombe Serikali iongeze kwani asilimia sita haitoshi na wengine tumeshafanya ziara katika maeneo mbalimbali, wanawake wa Kibaha, Mafia, Mkuranga, Rufiji, Bagamoyo na Kisarawe pamoja na vijana na makundi mengine mbalimbali yanayohusiana na masuala haya ya asilimia 20 wako tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nijielekeze kwenye suala zima la utekelezaji wa bajeti ya mifuko kwa 2015/2016. Tunaweza tukawa na bajeti nzuri, tunaweza tukatenga pesa nzuri kwa maendeleo na matumizi mengineyo lakini kama mifuko hii kwa mfano Mfuko wa NAOT mpaka mpaka Machi, 2016 una asilimia 45 tu. Ofisi hii Kikatiba imepewa dhima ya kukagua matumizi na mapato ya fedha za Serikali. Kwa dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kupambana na ufisadi, kupambana na ubadhirifu, kupambana na maovu mbalimbali na tumeona kasi yake, mchango mkubwa atasaidiwa na Ofisi ya Ukaguzi wa Serikali (National Audit Office). Kwanza niiombe Wizara ijitahidi kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha iweze kuwawasilishia fedha ambazo hawajasilisha mpaka sasa, asilimia 45 mpaka Machi ni kiasi kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna Mifuko ya Mahakama pia asilimia 61, Mfuko wa Bunge asilimia 49 pamoja na interest. Nataka kusema dhima ya mifuko hii ina nafasi kuchangia katika ukuzaji wa uchumi. Kwa hiyo, napenda kusisitiza Serikali ilione hili kwa sababu kama Mfuko wa Ukaguzi utakuwa haufanyi kazi iliyokusudiwa hata uwepo wa Bunge hili katika kazi ya kuisimamia na kuishauri Serikali ambapo msaidizi wetu mkubwa ni Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inawezekana tukapata tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nizungumzie Wizara zingine, kwa mfano mpaka mwezi Machi Wizara ya Kilimo ilikuwa haijapelekewa fedha ya maendeleo. Kama kweli tunataka kuongeza mapato ambapo tunategemea kilimo ndicho kitachangia katika mchango wa Taifa, Wizara hii mpaka Machi kuwa haijapelekewa fedha za ndani ni tatizo. Pia tunayo Wizara ya Afya asilimia 11 tu, hata Wizara yenyewe ya Fedha naomba niisemee pia asilimia sifuri. Wizara hii ina mchango mkubwa katika kusimamia uchumi wa Taifa letu kama ambavyo Wajumbe wengine wamesema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye masuala ya mishahara hewa. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ametoa maelekezo na kwa namna ambavyo kazi imefanyika vizuri na kwa namna ambavyo Serikali imeweza kubaini zaidi ya watumishi hewa 10,000. Hata hivyo, inawezekana kabisa tatizo kubwa ni mfumo. Kwa hiyo, naungana na maoni ya Kamati kwamba Serikali izidi kuangalia mifumo yake hasa LAWSON ambao unatumika katika mishahara, lakini pia EPICA, kuweza kuiunganisha kati ya EPICA9 na LAWSON na isisitize matumizi ya Mkongo wa Taifa. Nadhani kupitia Mkongo wa Taifa masuala ya TEHAMA itaweza kuziunganisha Halmashauri na Serikali Kuu katika mawasiliano ya namna ya kudhibiti watumishi hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tungependa kuona hatua za haraka zimechukuliwa kwa watu waliosababisha kuwa na watumishi hewa. Maana kama tumeshapata idadi ya watumishi hewa 10,000, kiasi cha shilingi bilioni 10 kwa mwaka kilikuwa kinatumika, tunatakiwa tuwajue kinagaubaga na waliohusika wachukuliwe hatua za kinidhamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa niiopongeze Wizara ya Fedha, niendelee kuwaomba…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa jioni ya leo kuchangia Bajeti hii ya Serikali, na nianze kusema naunga mkono hoja. Pia niungane na Waheshimiwa Wabunge wengi kukupongeza wewe binafsi na kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara ya Fedha walioandaa bajeti hii nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kujielekeza kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa saba. Hotuba hii alinukuu hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akifungua Bunge. Naomba ninukuu, kwenye ukurasa wa nane Hotuba ya Mheshimiwa Rais ilijielekeza katika kusema kwamba huduma zisizoridhisha za upatikanaji wa maji, elimu bora na afya ni mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano. Nimejielekeza kwenye hotuba yake, naunga mkono wazo la maombi ya kuongeza tozo ya Sh. 50 kwenye bei ya mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunamalizia bajeti ya mwaka ambao Bunge lilipendekeza tozo ya Sh. 50 kwenye lita moja ya mafuta, bei ya mafuta ilikuwa sh. 2,100 mpaka 2,400. Hapa katikati bei ya mafuta imeshuka lakini hatukuona athari yoyote, hazikushuka bei za usafiri, hazikushuka bei za vyakula, hazikushuka bei za aina yoyote, lakini mpaka sasa bei ya mafuta ni 1,700 hadi 1,900 bado Watanzania wana uwezo wa kuhimili ongezeko la Sh. 50. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini naomba niunge mkono pendekezo hilo ambalo limetokana na Kamati yetu? Ni kutokana na hotuba hii ambayo Awamu ya Tano inajielekeza kutatua kero hizi kubwa za Watanzania. Ukiangalia hotuba yetu kero kubwa ya Watanzania ukiacha maji inayofuatia ni upungufu wa zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka mmoja takribani akina mama 15,000 wanapoteza maisha, akina mama 42 wanapoteza maisha kwa siku, lakini sababu kubwa inayochangiwa kupoteza maisha kwa akinamama hawa ambao ni nguvu kazi ni uhaba wa vituo vya afya, uhaba wa zahanati na uhaba wa vifaa tiba. Pamoja na Serikali kuwa na nia nzuri, bajeti hii ninavyoiona hakuna kifungu cha moja kwa moja kinachoonesha ujenzi wa zahanati, ukarabati au kumalizia majengo yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika kwa nini nasema hivyo? Tuliwasilishiwa mkeka na Wizara ya TAMISEMI ambayo ilikuwa inaonesha takribani bilioni 32 zimetengwa na Halmashauri zetu, lakini ukiangalia vyanzo vya Halmashauri zetu ni own source, Local Government capital grant ambavyo vyote havina uhakika. Ndiyo kusema hata huu mkeka unaoonesha kwamba kuna vituo vya afya vitakarabatiwa, kuna zahanati zitajengwa, kuna wodi zitaongezeka, hauna uhakika kwa sababu chanzo chake hakina uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sisi wote Wawakilishi wa wananchi ndio tunaowasemea wananchi wetu kama walikubali tozo ya Sh. 50 wakati bei iko 2,100 hebu tuwaongezee tozo na kiasi kikubwa itahimiliwa na sisi wenyewe ili tuweze kutenga kiasi cha pesa kuziongezea hizi bilioni 32 ili hali ya vituo vya afya na zahanati zetu iboreke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa viwanda unategemea afya bora ya Mtanzania, lakini wanawake wakiwa ni moja ya nguvu kazi; tunategemea kuanzisha viwanda vya nguo, viwanda vya kubangua korosho; asilimia kubwa ya wafanyakazi ni wanawake, ambao wanahitaji kupata afya bora wakafanye kazi kwenye viwanda hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana na nasema hivyo naunga mkono hoja kwa sababu hata nikiangalia kwenye Mkoa wa Pwani kwenye orodha hii ya mkeka ulioletwa ni wilaya mbili tu; Kisarawe na Mafia. Wakati ninaposimama namkumbuka Daktari wa Zahanati ya Kijiji cha Kitomondo Kibaha Vijijini analala kwenye gari ndogo, hana nyumba na tulimwombea milioni 25 kumalizia nyumba. Tunapochangia Wabunge wanawake sekta ya afya inatuuma, inatugusa. Naomba Serikali ilitazame hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kama nilivyosema kwa sababu hata sasa tuna vituo vya afya 716 kati ya Kata 3,800 ni asilimia 18 tu, maendeleo ni mchakato lakini kama shilingi bilioni 30 katika shilingi bilioni 250 ambazo zitaongezwa kwenye miradi ya maji kwenda kwenye sekta ya afya, kupanga ni kuchagua. Naomba Bunge lako Tukufu kupitia Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tupange mipango hii vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningeomba kujielekeza ni suala zima linalohusu mfuko wa CAG, na mimi naomba niingie kwenye rekodi na naomba kwa sababu naamini Hansard itatumika vizazi vijavyo na ninawapongeza Wabunge wote waliochangia kuomba Serikali itazame jicho la huruma ofisi hii ni wazalendo, tunaliomba hilo kwa sababu tunaamini ni mmojawapo ya nguvu itakayomsaidia Mheshimiwa Rais wetu ambaye amejipambanua wazi wazi kwenye hotuba yake atapambana na ubadhilifu, atapambana na ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ina shilingi trilioni 29, matumizi ya kawaida shilingi trilioni 17, matumizi ya maendeleo shilingi trilioni 11, Ofisi ya CAG kufuatilia hizo hela, shilingi bilioni 18, kwenye matumizi mengineyo. Tuna Halmashauri 168 na mimi nayasema hayo kwa sababu nilishawahi kuwa Mkaguzi miaka kumi, najua adha ya ukaguzi! Najua utaratibu na kukagua unakagua kutokana na Tanzania Auditing Standards na International Auditing Standards, zipo taratibu. Leo tunapopeleka hela mpaka kwenye kijiji CAG anafikaje? Tunapopeleka hela kwenye zahanati, kwenye vituo vya afya, CAG anafikaje? Tunapopeleka hela kwenye pembejeo? (Makofi)
Kwa kuwa kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali, ushauri inategemea, lakini kazi yetu kubwa ni kuisimamia na tunaisimamia kupitia oversight committee. Nikuombe kwa kulinda hadhi ya Bunge lako na kwa kuwa kuisimamia Serikali ni kupitia oversight committee isije tunakuja Bunge lijalo Kamati zako PAC na LAAC zinakosa kazi ya kufanya. Hela hizi nyingi. Naomba sana itazame. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa Fedha anasema ataangalia, ameji-commit lakini mwezi wa 12 mapitio ya bajeti CAG anatakiwa amalize kazi zake, tunaende kwenye kufunga mwaka wa fedha za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona na mimi niingie kwenye Hansard kwamba nimeisemea ofisi hii ili vizazi vijavyo viweze kuona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nimeona nia njema ya Serikali ya kuleta usawa kwenye masuala ya pensheni, nami naunga mkono. Lakini naomba usawa huu ubainishwe kinagaubaga ni makundi gani? Kwa sababu tunayo Sheria ya Retirement Benefits za Viongozi wa Kisiasa walitajwa pale! Lakini ieleweke wazi hata Wabunge wanalipa kodi shilingi 1,200,000 kwa mwezi; kwa mwaka shilingi milioni 15, kwa miaka mitano ni shilingi milioni 75. Wabunge hawa pia wanachangia shughuli mbalimbali za maendeleo. Hata kuzika, madawati tumeunga mkono, vituo vya afya tunaunga mkono, lakini isionekane Watanzania msikubali kuamini kwamba Wabunge eti ni kundi linalojipendelea, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ingekuwa mimi ningewaombea pia wafanyakazi wa Tanzania msamaha kwenye kiinua mgongo chao. Mfanyakazi anafanya miaka 40, miaka 30, anavyostaafu kwanini asipewe kiinua mgongo chake? Kwa kuwa kundi la wafanyakazi, kundi la wanasiasa ni kundi ambalo liko loyal kulipa kodi, kwa nini nisiwatetee? Kwa nini isifike wakati nao wasamehewe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naunga mkono. Najua kuwa kweli kuna changamoto katika misamaha ya kodi, zimetajwa taasisi…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha jioni ya leo kuchangia mapendekezo ya mpango yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha.
Awali ya yote nampongeza Waziri wa Fedha, sisi kama Kamati ya Bajeti tulishirikiana nae vizuri katika kujadili mapendekezo haya. Na naenda moja kwa moja kwenye mchango wangu katika suala zima la kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi wake wa kutoa elimu bure, nikiwaona mamia ya wanafunzi walioongezeka kwenye shule za msingi, sekondari, waliokuwa wanapoteza fursa kutokana na ada na michango mbalimbali na nikiona utayari wa wazazi kuchangia huduma ambazo pengine Serikali haijachangia kwenye ule mchango wa kila mwezi kwa kweli nafarijika. Ndio maana baadhi ya maeneo sisi tumejipanga tunafyatua matofali kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya shule, ujenzi wa madarasa mapya na ndio maana baadhi ya maeneo tumejipanga, tumetengeneza wenyewe madawati pamoja na Waheshimiwa Wabunge acha yale ya kupewa na Bunge. Lakini yapo maeneo tumechangia madawati, tumejenga nyumba za kuhifadhi hayo madawati. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye masuala ya kufungamanisha maendeleo ya viwanda na afya. Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali pia kwa jitihada mbalimbali za uboreshaji wa afya husasan katika tukio la mkutano wa wafadhili wa Kimataifa juu ya afya ya mama na mtoto. Nampongeza sana Mheshimiwa Ummy pamoja na Wizara yake kwa kufanikishwa kufanikisha kupatikana kwa zaidi ya dola milioni 30 kwa ukarabati wa vituo vya afya mia moja. Ukarabati huo utahusu ujenzi wa theatre, maabara ya kuhifadhi damu, wodi ya wazazi, nyumba moja ya mtumishi. Ninaamini itakuwa ni ukombozi mkubwa na Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa imeaanza vizuri. Kwa kuwa tuna vituo 489, vituo 113 ndiyo vyenye fursa hizo ukivijumlisha na vituo hivi mia moja vinabaki vituo 376. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali, natarajia mapendekezo ya mpango huu utakapokuja kuwa kamili na tutakapo kaa Kamati ya Mipango mwezi wa pili, nadhani watakuja na mapango utakaoainisha vituo vilivyosalia namna ya ukarabati na uboreshaji, lakini pia ujenzi wa zahanati mpya kwa ajili ya kupunguza vifo vya akina mama, wajawazito na watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimewasilishwa taarifa mbalimbali; mpango nimeuchangia kwenye Kamati, taarifa zilizowasilishwa kuna taarifa ya Waziri, lakini kuna taarifa ya Waziri Kivuli. Naomba kwa kuwa taarifa zote ni za Bunge na zinajadiliwa na ninapojadili hapa, kambi nyingine huwa wakiona Wabunge wanachingia wanasema anataka Uwaziri. Najua Wizara ile imejaa, Mawaziri wapo wanatosha lakini nachangia ili kuweka sahihi kumbukumbu na kuuacha upotoshaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo ukurasa wa 19, tumeambiwa tulipitisha bajeti hewa na katika ukurasa wa 19, katika maelezo ya Waziri Kivuli anaeleza kwamba, sisi tulipitisha shilingi trilioni 23 kama matumizi. Nataka nimfahamishe kwa kuwa Waziri wetu Kivuli ni mgeni katika Wizara hiyo, alikuwa anahudumu Wizara ya Ardhi, mambo bado hajayajua. Lakini nataka nimfahamishe kuna vitabu Volume III, aliruka fedha za maendeleo kwa Mikoa bilioni 4.3. Pia aliruka fedha za maendeleo kwa ajili ya Halmashauri trilioni 1.3 na trilioni nne, hakuna, hakuna! Kwa kuwa hotuba hii ilichapwa kwenye magazeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mwongozo wako endapo zinawasilishwa hotuba zenye nia ya kupotosha na watu waliondoka wenyewe ndani ya Bunge. Napenda niwataarifu Watanzania hatukupitisha bajeti hewa na hili nimelisemea kwa sababu Mheshimiwa Waziri Kivuli huyu hawezi kuendana sawa na Dkt. Mpango wala Dkt. Ashatu na watendaji wa Wizara ya Fedha waliopoteza muda mwingi kuandaa makaburasha haya, kila kitu kiko sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niweke record sawa na kwa kuwa iligusa pia Kamati; anapozunguza masuala ya bajeti wa kuwasilisha pia maoni ni Kamati. Sasa nashangaa mwenzetu, lakini ninaomba pia wakati mwingine upangaji wa Wizara ziangalie na taaluma pia, nilishangaa Mwanasheria kuwa Waziri wa Fedha, nilishangaa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mapendekezo ya mpango walifanya tathimini ya sekta ya fedha na hapa naomba nijielekeze ni kweli katika taarifa aliyowasilishwa Waziri kunaonyesha mikopo ya kibiashara na shughuli za uchumi kwa quarter iliyoanza Julai zimeshuka na sababu zinazopelekea ni kupungua kwa shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali ikae na mabenki, ikae na sekta za fedha kwa sababu sekta hii inachangia kwenye ukuaji wa uchumi kwa mwaka ambao miezi sita imechangia zaidi ya asilimia 13 inawezekana kupungua kwa fedha katika mabenki hayo inasababishwa na shughuli mbalimbali au maendeleo ya teknolojia ya simu ambazo watu wengi wanatumia miamala ya fedha au masuala ya microfinance. Kwa kuwa inachangia ningeomba sana Serikali isikilizane na sekta hii ya fedha, lakini sekta ya fedha nayo iweke mazingira wezeshi itafute wateja katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho, muda umeisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho lilizungumzwa, ukiangalia umbile la…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Subira, muda umekwisha.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Eeh! Ahsante!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, viongozi hawa wameutendea haki Mkoa wa Pwani. Kwa nyakati mbalimbali wamefika kutufanyia shughuli mbalimbali za uwekaji wa jiwe la msingi, ufunguzi na hata ukaguzi wa viwanda mbalimbali vinavyoendelea kujengwa katika Mkoa wetu wa Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndoto ya Mheshimiwa Rais ambayo imeelezewa kinagaubaga kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwangu mimi naiona ina mwelekeo mzuri wa kutimia. Kwa nini nasema hivyo, ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri na ninampongeza sana kwa kazi nzuri kama nilivyotangulia kusema, katika ukurasa wa 16, tofauti na hotuba ya mwaka jana ameeleza kinagaubaga miradi ya viwanda tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa huo wa 16 mpaka 29 katika moja ya aya kwenye hotuba yake, ameeleza viwanda vikubwa 393 vyenye jumla ya mtaji wa dola za Kimarekani milioni 2000, kama shilingi trilioni 5,000 na ameeleza; ukisoma hotuba yake na ukisoma viambatanisho vyake, majedwali kuanzia 7(b), 7(c) na 7(d) utaona kabisa ni aina gani ya kiwanda, mwekezaji, ajira ngapi zitatekelezeka na ni investment ya kiasi gani. Kwa hiyo, mimi nadhani kwa maelezo yale inatosha kabisa kutoa dira kwamba sera hii ya uchumi wa viwanda inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, naomba nimpongeze Mkuu wetu wa Mkoa wa Pwani, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi kwa kuandaa mazingira wezeshi ya viwanda vyetu. Hapa naomba nisemee viwanda vya chuma vilivyopo Kibaha, cha Kilua, Kibaha Mjini na Mkuranga na ninaomba pia nijielekeze kwenye viwanda vya usindikaji matunda vilivyopo Mboga ambacho kinakaribia kukamilika, Bagamoyo pamoja na Mapinga.

Vilevile naomba nijielekeze, na nipongeze naweka kumbukumbu kwenye Hansard na mimi mwenyewe binafsi baadhi nilivitembelea, Kiwanda vya Vigae kilichopo Mkuranga ambacho ni kikubwa sana, kinatarajia kutoa ajira 4,500. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ninaomba nijielekeze kwenye eneo letu la viwanda la TAMCO na nimeona nia ya Serikali ni njema, na ukiangalia hata bajeti ya maendeleo ya Wizara hii imeongezeka. Mwaka wa jana tulilalamika hapa zilitengwa shilingi bilioni 40, lakini Serikali imeonesha dhamira, imetenga shilingi bilioni 82, ni zaidi ya mara mbili ya pesa ambazo imetengwa mwaka wa jana. Ndani ya pesa hizi zimetengwa kwa ajili ya eneo la viwanda la TAMCO, Kibaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla, eneo lile kama ambavyo limeelezwa na Kamati yenyewe, kama ambavyo Serikali imeeleza namna gani eneo lilivyopangwa, upembuzi yakinifu umekamilika, ramani yake imekamilika, tunatarajia viwanda vya nguo, kuunganisha magari, dawa za binadamu pamoja na viwanda vya aina mbalimbali. Pia ninaiona dhamira ya Serikali, hasa kwa kutumia mifuko ya hifadhi ya jamii kujenga viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulizoea mifuko hii kujenga nyumba mbalimbali ambazo tunaziona sasa hazina soko, lakini dhamira ya kutumia mifuko hii, tumeona ni namna gani mifuko hii inavyoshirikiana ikajenga kiwanda kikubwa cha sukari Mkulazi, naunga mkono. Vile vile tumeona namna gani mifuko hii inayoshirikiana na MSD, TIRDO, Tanzania Investment Bank kujenga viwanda vinavyotumia mazao ya pamba. Kwa hiyo, unaiona dhamira ya Serikali kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba niulize; Wilaya yetu ya Rufiji ina maeneo ambayo tuliyatenga kupitia RUBADA na kuna maeneo yalikuwa yanatolewa na tulikuwa tunatarajia kujenga viwanda vya sukari, Mheshimiwa Waziri sijaona mahali popote alipotaja juu ya ujenzi wa viwanda hivi katika Wilaya yetu ya Rufiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, pia Wilaya ya Kisarawe tulipima eneo (Kisarawe Industrial Park), lipo tayari na tulijitahidi kama Halmashauri na Serikali Wilayani mpaka miundombinu, lakini pia sijaona litajwe popote. Lile eneo lipo sehemu nzuri, limepitiwa na reli ya kati, limepitiwa na reli ya TAZARA, lipo karibu na viwanja vya ndege Dar es Salaam na pia lipo karibu na bandari. Kwa hiyo, unaona mkoa wetu umekaa kama mkoa wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Serikali, mwekezaji yeyote atahitaji athibitishiwe usalama wake, lakini pia anahitaji vivutio mbalimbali. Nina imani baada ya mkutano wa Mheshimiwa Rais na Baraza la Biashara pamoja na sekta binafsi, nina imani majadiliano yatakayoendelea ndani ya Bunge hasa itakapofika wakati wa Finance Bill, vikwazo mbalimbali vya kisheria, vya kodi na vya vivutio nadhani vitapatiwa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza kwenye mchango wangu kwamba wawekezaji wetu hasa wa Mkoa wa Pwani wanahitaji ulinzi wa mali zao. Naiomba Serikali, pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea, lakini kuimarisha ulinzi wa maeneo yetu. Naamini wawekezaji pamoja na nia waliyoonesha, lakini kwa matukio yanayoendelea pamoja na kazi nzuri ya Serikali, yanaweza kabisa kufifisha jitihada hizo za uwekezaji katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote haya yanakwenda sambamba na namwomba Mheshimiwa Waziri, kama ambavyo ameonesha kushirikiana na Waziri wa Wizara ya Maji, basi Wizara ya Kilimo na Mifugo, Wizara ya Fedha, Wizara ya Sheria na Katiba, Wizara ya Miundombinu na Wizara nyingine za kimkakati zijitahidi kufanya kazi kwa pamoja na Wizara ya Nishati na Madini ili kuonesha yale mambo yanayotegemeana na viwanda ili yaweze kufanyika kama inavyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani sisi kama Wabunge, binafsi mimi ninayetokea Mkoa wa Pwani, naamini wajibu wangu ni kuhamasisha wananchi wa maeneo haya kutumia fursa ya viwanda vizuri. Viwanda vyetu vitahitaji rasilimali, niwaombe vijana, wanawake na wananchi wa Pwani kutumia fursa ya viwanda vizuri. Tulime kilimo ambacho kitaleta tija, tujitoe kufanya kazi katika hivyo viwanda ili ajira inavyosemekana, nimepiga mahesabu, ajira katika viwanda vyote vinavyotarajiwa Mkoa wa Pwani ni kama 10,000 zile za moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo ajira chache. Fursa hii isije ikaonekana kwamba viwanda vinajengwa lakini ajira nyingi zinakwenda nje; sitarajii kwamba iwe za Pwani tu peke yake, lakini wote ni Watanzania, tuzitumie fursa hizo lakini wenyewe pia wa Mkoa wa Pwani tuzitumie fursa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nimalizie kwa kuomba Wizara ya Viwanda na Biashara ulipaji wa fidia. Mheshimiwa Mbunge wa Bagamoyo amezungumza leo na hili jambo kwa kweli katika maeneo yale; na maeneo haya ya kimkakati kwa uwekezaji yanasaidia mno, ni maeneo maalum. Tulitembelea eneo maalum la Benjamin Mkapa (Special Economic Zone), tumeona viwanda vya nguo vilivyo pale, tumeona ubora wa bidhaa wanazozitengeneza, tumeona namna gani hata viwanda vile vilivyopo pale Benjamin Mkapa (Special Economic Zone) havijaweza kukidhi soko. Zaidi ya asilimia 30 bado halijakidhi soko la nje. Kwa hiyo, nina imani Serikali ikilipa fidia katika maeneo yote yaliyotengwa nchi nzima na kwa wakati na wawekezaji wakapatikana, uwezo wa kuzalisha bidhaa na kuzisafirisha nje ya nchi upo na masoko yapo.

Mheshimiwa naibu Spika, nimalizie kwa kuunga mkono hoja. Nashukuru sana kwa kazi nzuri inayoendelea kufanywa na naendelea kuamini Sera ya Viwanda, Uchumi wa Viwanda itawezekana. Naendelea kuamini changamoto zilizopo zinaweza zikatatuliwa mezani; na naendelea kuamini Mheshimiwa Rais ana nia njema na ipo siku tutashuhudia mapinduzi makubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Maji. Kwa kuwa dakika ni tano nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Baraza lake la Mawaziri kwa kazi nzuri. Pia mchango wangu niuelekeze moja kwa moja kwenye Mradi wa Maji wa Wami – Chalinze Awamu ya Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na namshukuru sana, na maelekezo yake na namna ya maelezo ya Serikali kwenye hotuba hii, na namna ambavyo mkandarasi yule amepewa siku 100 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa awamu ya tatu; nilikuwa nadhani kwa kuwa changamoto za upatikanaji wa maji Jimbo la Chalinze zimekuwa kubwa, na kwa kuwa mkandarasi huyu anaonekana hata miradi mingine performance yake si nzuri, je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuna haja ya kumbadilisha mkandarasi huyu? Kwa sababu siku alizompa zinakamilika tarehe 31/05 na leo tuko tarehe 11?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa swali la nyongeza nililoliuliza juzi Mheshimiwa Naibu Waziri alinijibu amefikia asilimia 45. Hata hivyo mradi huu unakabiliwa na changamoto nyingi, maji yanayotoka sasa hivi ni machafu, wananchi wanapata taabu, maji hakuna na hata bili wanazopewa wengi wamekatiwa lakini wanaendelea kulipia service charge. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri, na kwa kuwa Jimbo letu la Chalinze na Wilaya ya Bagamoyo kuna wawekezaji wengi wamejitokeza hususan, naomba nimsemee hapa mwekezaji wetu anayejenga kiwanda cha usindikaji matunda pale Msoga, Chalinze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa rasilimali inayohitajika ni maji na kwa kuwa maji sasa hakuna na kiwanda karibu kinafunguliwa, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kukubaliana na makubaliano ambayo yameingiwa mradi wa CHALIWASA pamoja na mwekezaji wetu huyu, kwamba yupo tayari kununua baadhi ya vifaa kwa ajili ya kuboresha mradi ule ili maji yapatikane ambayo mimi nadhani yanaweza yakasaidia kiwanda, yakatusaidiwa na wananchi wa Chalinze?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mradi wa Chalinze autazame kwa macho ya huruma, hali si shwari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwa kupitia bajeti hii kwenye hotuba yake nimeona kwenye ukurasa wa 90 mpaka 92 namna gani ambavyo Serikali imeonesha kabisa chanzo hiki cha shilingi 50 kwa lita moja ya diesel au petrol haitoshi. Kwa hiyo, nadhani kwa kukiri kwao kwenye hotuba hii sasa ni nafasi ya Bunge letu na Kamati yetu ya Bajeti kuweza kuongeza hicho kiwango ambacho Serikali yenyewe imekiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye ukurasa wa 120 Serikali imeonesha kwamba mahitaji ya ujenzi wa miradi mipya ya maji ni makubwa na wameomba wawekezajii wengine au wadau mbalimbali kujitokeza ku- support jitihada hizo na ndiyo maana hapa ninamwomba Mheshimiwa Waziri, nilishamweleza, hivi aone ombi la mwekezaji wetu kuomba kugharamia sehemu za ukarabati wa uchakavu wa miundombinu ya mradi wa maji Chalinze ili waweze kukatana kwenye bili. Kwa nini suala hili linachelewa hivyo? Uwekezaji ule ni zaidi ya bilioni mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Wilaya ya Kisarawe nayo ina changamoto kubwa ya maji, Wilaya ya Rufiji nayo ina changamoto kubwa ya maji. Hivi karibuni kuna binti yetu amepoteza maisha kwa kuchota maji katika Mto Rufiji. Kwa nini sasa Mto Rufiji usitumike kuwa chanzo cha maji katika Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utaona miradi mingi, mfano mradi kupitia DAWASA, upanuzi wa bomba la maji Ruvu Chini na Ruvu Juu yote imepita katika Mkoa wa Pwani lakini kwa bahati mbaya sana hatuna Mamlaka ya Maji ya Mkoa, tunatumia mamlaka ya maji DAWASCO ambayo tunadhani inazidiwa na utoaji huduma za maji katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa hiyo, ningemwomba Mheshimiwa Waziri atueleze, ni kwa nini Mkoa wa Pwani tunakosa kigezo cha kuanzisha Mamlaka ya Maji, wakati ukizingatia vyanzo vingi vya maji vinavyopeleka maji katika maeneo mengine viko katika Mkoa wa Pwani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika kuongezea mchango wangu, kwa nini kata za Mzenga, Mafizi hazina maji wakati ni kilometa 28 kutoka bomba kuu la maji linalopeleka maji Dar es Salaam? Kwa hiyo, ningemwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba bajeti imepungua kwa kiwango hiki nadhani pia atakapokuja kufanya majumuisho atueleze pengine kuna sababu ya msingi. Pengine katika hiyo bilioni 600 tutaongeza maji kwa kiwango cha asilimia ngapi, na Watanzania wangapi wataongezeka katika kupata huduma ya maji kwa bajeti hii iliyopitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bagamoyo Mjini kuna miundombinu ya DAWASA imejengwa pale lakini hawapi maji. Kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashoria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2017/2018.

Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa Tume mbalimbali zilizotajwa muda mfupi uliopita, lakini ripoti zao si Msahafu wala Biblia ambazo haziwezi kubadilishwa. Kwa ujasiri alioonesha kwa kipindi kifupi Mheshimiwa Rais, kwanza cha angalau kutekeleza maamuzi ya kuhamia Dodoma, tangu mwaka 1973, lakini uamuzi wa kuanza ujenzi wa reli ya kisasa, uamuzi wa kuwaondoa watumishi wenye vyeti feki, uamuzi wa kuondoa watumishi hewa, uamuzi wa kuondoa wanafunzi hewa, naamini ripoti ya Profesa Osoro na Profesa Mruma zitafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ripoti hiyo tumefuatilia wengi, kwa kuwa Mheshimiwa Spika, ulihudhuria na kwa kuwa Mheshimiwa Spika ulitoa kauli ya kulitaka Bunge lako kuwa tayari kupokea maelekezo na sheria mpya zitakazoletwa, nina imani mwaka huu mwarobaini wa ripoti mbalimbali umepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ile ripoti ya jana ya Profesa Osoro na ripoti ya Profesa Mruma zilikuwa na mambo mengi. Ukiacha mambo ya kisera, ukiacha mambo ya kisheria lakini yapo mambo ya kiutendaji yaliyosababisha hasara kubwa lazima yashughulikiwe. Kwa mfano, katika ripoti ilisema kiwango cha mrahaba kilichooneshwa kwenye hesabu za makampuni ya Bulyankulu na Pangea zilionesha dola za kimarekani milioni 111, wakati zilizopelekwa Serikalini kama mrahaba kati ya mwaka 1998 mpaka 2017 ni dola za kimarekani milioni 42, tofauti ya bilioni 68. Hili la kiutendaji lazima lishughulikiwe, siyo la kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ripoti imeonesha namna ambavyo wasafirishaji kupitia Wakala wa Meli walivyofanya utapeli wa kutisha, takwimu zinatofautiana baina ya hati za kusafirisha meli na hati za Wakala wa Meli, hili ni jambo la kuachwa? Haiwezekani.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo naunga mkono bajeti hii na naunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais. Naunga mkono bajeti hii kwa sababu, kwanza bajeti ina nia ya kumwondoa Mtanzania kwenda kwenye kipato

cha kati. Pili, bajeti imewagusa Wanawake ninaowawakilisha kitendo cha kufuta VAT kwenye chakula cha mifugo inatosha kabisa mimi kuunga bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitendo cha bajeti hii kuondoa VAT kwenye vipuli vya viwanda ambako Mkoa wangu unaongoza kwa viwanda kwa sasa nina kila sababu ya kuunga bajeti hii. Pia kitendo cha bajeti hii kutoa motor vehicle licence ya mwaka mzima na kupendekeza tozo ya Sh.40/= nikiwaona wanawake wengi wananunua maji kwa elfu moja, kwa elfu mbili, kwa elfu tano dumu, naamini wana uwezo wa kuhimili tozo hii ya Sh.40/= endapo sehemu ya tozo hii itahamishwa kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napongeza namna gani Mheshimiwa Rais wetu anavyosimamia uboreshaji wa mapato. Amesimamia maboresho ya mtambo wa TTMS wa kurekodi dakika zote za simu, tunaona mapato ya simu yameongezeka. Amesimamia uanzishaji wa mfumo wa kukusanya mapato kielektroniki, amesimamia hata kutembelea data center na ameelekeza makampuni yote ya simu yaende kujisajali Dar es Salaam Stock Exchange.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, naomba nipendekeze, Waswahili wanasema ukiumwa na nyoka, ukiona nyasi unastuka. Kwa kuwa, tumeona makampuni mengi ya nje hata taarifa zilizotolewa zinaonesha makampuni mengi ya nje yanatutapeli kupitia transfer pricing, nishauri kwenye soko la Dar es Salaam Stock Exchange, makampuni ya simu, Serikali ilete mapendekezo ya kutafsiri upya maana listed shares ili Serikali yetu ipate fursa ya kuangalia miamala ya makampuni haya hata ile ambayo shares zake nyingi zinatawaliwa na wageni.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Kampuni ikiwa registered Dar es Salaam Stock Exchange ikiuza share zake kwa asilimia 25 ili zile share zote Serikali iwe na nguvu lazima tubadilishe maana halisi ya listed shares ili iende kwenye zile share za makampuni. (Makofi)

Mhehimiwa Spika, sambamba na hilo, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake wa ujenzi wa standard gauge kama nilivyosema. Hata hivyo, nashauri suala zima la kufuta VAT kwenye vipuri liende sio tu kwa viwanda vilivyotajwa vya mafuta peke yake, lakini viguse viwanda vya usindikaji wa korosho, Mkoa wa Pwani tunalima korosho, viguse pia viwanda vya kuzalisha mafuta ghafi hapa nchini kwetu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, lakini nimalizie kama dakika zangu zipo kwenye suala zima la nia ya Serikali ya kufungua Escrow Account kwa ajili ya makampuni yanayotumia sukari ya viwanda. Niombe Serikali ilitazame upya suala hili, makampuni yale yenye viwanda vya kutengeneza vinywaji baridi kwa kweli wamezidiwa, pesa zao nyingi hazijarudishwa kiasi cha bilioni 20, imesababisha viwanda hivi kupunguza wafanyakazi, inasababisha viwanda hivi kupata tabu katika uendeshaji wa shughuli zao. Naomba Serikali itazame upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Serikali ione namna ambavyo itatusaidia wakazi wa Pwani viwanda hivi ambavyo vimeanzishwa vingi na namna ya kutusaidia jinsi ya kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda hivi.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu bajeti hii Mheshimiwa Waziri amesema Mama Lishe watatambuliwa sasa hivi, wauza mboga ndogondogo watatambuliwa. Imani yangu utambulisho huu utakwenda sambamba na huduma za kifedha, utakwenda sambamba na uwezeshaji na naamini kupitia Baraza la Uwezeshaji la Taifa, wanawake wengi watafikiwa, bodaboda wengi watafikiwa kwa kuwa watakuwa na utambulisho rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa spika, mwisho, ni kuhusu Serikali zetu za Mitaa. Niombe sana kwa Mheshimiwa Waziri, nia ni njema ya kufanya mapato yote yakusanywe na Serikali Kuu, lakini niombe urejeshwaji wa mapato hayo uende kwa wakati. Halmashauri zetu nyingi zitashindwa kujiendesha endapo makusanyo yatakayokusanywa kupitia property tax, kupitia

vyanzo vingine vya mabango ambavyo vimekwenda Serikali Kuu kwa nia njema ya kuongeza hayo mapato yatakuwa hayarejeshwi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kushukuru kwamba kwa upunguzaji wa produce cess kwa wakulima wetu, kwa kweli ni suala ambalo ni la msingi. Kila siku tulikuwa tunalisemea lakini namna ambavyo Serikali mmelishughulikia. Mheshimiwa Waziri nakupongeza, bajeti hii imesikiliza maoni ya Kamati, bajeti hii inamgusa mwananchi wa kawaida, bajeti hii imemgusa mkulima na bajeti hii imemgusa mwanamama wa kawaida.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema ambapo nimeweza kusimama ndani ya Bunge hili na pia niwatakie Waislam wote Ramadhan Kareem. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha vizuri bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka wa 2021/2022. Nikimpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba ninukuu sehemu ya kipande cha Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan wakati wa shughuli ya kumuaga Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano kama ifuatavyo; “Tunapokwenda kumpumzisha Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tunaweza kusema bila kigugumizi kuwa tuko tayari kuiendeleza kazi yake nzuri kwa nguvu kasi na ari ile ile.”

Mheshimiwa Naibu Spika, nimenukuu maneno haya ya Mheshimiwa Rais Mama Samia na nampongeza sana, baada ya kuona ahadi aliyoiahidi na uwasilishaji wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu inaenda sambamba. Nasema hivyo kwa sababu nikiangalia majumuisho yake ya mambo ambayo Serikali itajielekeza nayo, akifanya summary ya bajeti yake nzima, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati iliyoanzishwa na Hayati Rais Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mradi huo ni ununuzi wa ndege na Serikali imesema hapa imeshalipia ndege tatu, majadilliano mbalimbali yamefanyika ndani ya Bunge, nayaunga mkono, lakini nataka kusema moja tu, wengi wamekuwa wakinukuu taarifa ya CAG, hata watumiaji wengine wa taarifa hii baada ya kuwasilishwa Bungeni, lakini nataka niseme, tusimuwekee maneno zaidi CAG, kwa sababu kwenye ukurasa wake wa 16 na 17 pamoja na hasara ya Shirika la Ndege hii, CAG hajasema kama uwekezaji huu ni hasara, badala yake ameshauri kudhibiti gharama za uendeshaji pamoja na za kibiashara ili kampuni hii isiendelee kupata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Watanzania tupate tafakuri mpya, kama TANROAD tunaiwekea zaidi ya trilioni tatu kwa ujenzi wa barabara na haiandai taarifa ya kuonyesha kwamba tunahitaji kuona faida na hasara, ni huduma tu kwa sababu barabara zinasaidia sekta nyingine, ufike wakati tuliamini shirika la ndege linatoa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mradi mwingine wa kimkakati ambapo Waziri Mkuu kupitia hotuba yake amesema atauendeleza ni ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na mradi huu CAG amekagua na nataka niseme ni mradi pekee ambao ameukagua wenye kurasa nyingi kama
32. Watumiaji wengi wa ripoti yake wamejielekeza kwenye kipengele kimoja cha kutokuwepo kwa upembuzi wa kina, ningeomba niwashauri waisome vizuri…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Subira Mgalu, subiri kidogo, Mheshimiwa Halima naona umesimama.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, yes. Mheshimiwa Subira ni Mjumbe mwenzangu wa Kamati ya Bajeti…

NAIBU SPIKA: Ngoja nijue ni kuhusu utaratibu, taarifa au kitu gani?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa.

NAIBU SPIKA: Sawa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa taarifa kutokana na alichokisema, nasema hivi Mheshimiwa Subira anafahamu chini ya taarifa ya Msajili wa Hazina ya Mashirika ya Umma ya Serikali, kuna mashirika ambayo yanatoa huduma na kuna mashirika ya kibiashara. ATCL ni shirika la kibiashara, kwa hiyo ni muhimu wakati tunachangia haya mambo, tujue linatoa huduma lakini ni la kibiashara, halijawekwa pale kutoa huduma per se, linafanya huduma then we expect to make profit. Kwa mazungumzo anayozungumza asi-mislead juu ya jukumu la shirika letu la ndege. Ni hayo tu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Subira Mgalu, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokea hiyo taarifa kwa sababu hakunisikiliza vizuri. Ni kweli natambua na yeye ni mjumbe mwenzangu wa Kamati ya Bajeti, nimesema ni kweli shirika la ATCL ni miongoni mwa mashirika 28 ambayo taarifa ya CAG imesema imepata hasara, ni shirika pekee la kibiashara, lakini nimetoa maoni yangu kwamba kama TANROADS tunaiona inatoa huduma inatengeneza barabara ni kwa nini usifike wakati shirika hili ambalo nalo lina wajibu wa kuchochea sekta nyingine kupitia huduma ya usafiri wa anga, kwa nini nalo lisitoe huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee katika mradi huu wa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na ukaguzi mzuri uliofanywa na CAG, nimeainisha kwamba katika kuhuisha upembuzi yakinifu CAG amesema, tathmini ya athari za mazingira imefanyika, usanifu wa kiufundi na utafiti ya geology umefanyika, utafiti wa kitaaluma ufanisi wa miamba umefanyika. Naomba nimnukuu kwenye ukurasa wa 128, maelezo ya CAG namnukuu: “Kulingana na tathmini iliyofanywa hadi sasa, nilibaini kuwa hakuna udhaifu mkubwa wa kiufundi ambao unaweza kuzuia mradi kufikia malengo mahsusi yaliyokusudiwa.”

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi, wasimlishe maneno Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, hiyo ndio ripoti. Katika hili niiombe Serikali, katika moja ya hoja kwenye mradi huu ni makubaliano ya mkataba ya asilimia nne kwa ajili ya miradi ya kijamii ya maeneo yanayotekeleza mradi huu. Wananchi wa Rufiji, wananchi wa Morogoro vijijini wanasubiri kwa hamu mchango wa asilimia nne wa mkandarasi wa gharama ya mradi kwa ajili ya miradi ya elimu na kwa ajili ya miradi ya afya. Kwa hiyo niiombe Serikali hilo lishughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo yalitolewa maoni hapa pamoja na wachangiaji, tuongeze bidhaa ili tuweze kukusanya mapato Zaidi. Mradi huu unaenda kuleta bidhaa ya umeme, umeme utakuwa mwingi ambao unatakiwa uuzwe nchi za jirani na Serikali imejipanga vizuri, inajenga sasa transmission line ya Singida – Namanga ambayo itawezesha kiwango cha umeme kingine kuuzwa nchi jirani tukapata mapato na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze pia katika moja ya kipaumbele cha Mheshimiwa Waziri Mkuu kusimamia makusanyo ya mapato. Katika hili nimwombe Mheshimwa Waziri Mkuu atakapokuwa anapitia, natambua tulipokuwa tunamwona kwenye ziara mbalimbali akija kwenye halmashauri zetu, anakuja na taarifa kabisa na wengi wale ambao waliokuwa wanajihusisha na ubadhirifu wanasimamishwa, wanapisha uchunguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe katika hili kwa kuwa tunatafuta mapato ya nchi yetu na kwa kuwa Serikali imepewa maelekezo na Mheshimiwa Rais Mama Samia ya kupanua wigo wa ukusanyaji mapato; na kwa kuwa katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameainisha namna gani Serikali ina mpango wa kupunguza mashauri katika Mahakama, katika hili naomba niseme, katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, naomba Serikali iimarishe mamlaka za rufaa za kodi. Fedha ya mapato inaweza ikapatikana pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza kwa mujibu wa taarifa ya CAG, kuna kesi zaidi ya 1,097 zenye thamani ya trilioni 360, utaona ni kiasi gani cha fedha zilizopo kwenye masuala ya kesi mbalimbali. Endapo Serikali itaingilia kati na hapa nakumbuka hata Hayati Dkt. John Pombe Magufuli Rais wetu alitoa maelekezo hayo kwamba mamlaka za kodi za rufaa zisikilize hizi kesi haraka ili kama kuna mapato yoyote Serikali iweze kuyapata.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naipongeza sana Serikali na nampongeza sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa kuchangia katika Wizara hii ya Maji na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, pamoja na Naibu Waziri, Engineer Maryprisca. Lakini pia nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa DAWASA kwa namna ambavyo anatuhudumia Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa shukrani, naishukuru Wizara ya Maji pamoja na Serikali kwa kukamilisha mradi wa maji wa Kisarawe, kwa kukamilisha mradi wa maji Mkuranga, lakini kwa ahadi yake ya kuanza upembuzi yakinifu ya kutoa maji ya Mto Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu wanawake wa Mkoa wa Pwani wa Wilaya hizo, watapata tija kubwa na tunaweza kuwatua ndoo kichwani. Sambamba na hilo niishukuru Wizara pamoja na DAWASA na pia kumshukuru sana Rais aliyepita Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa maelekezo ya mradi mpya wa kutoa maji Ruvu, Chalinze - Mboga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika mradi huu kazi inaendelea, lakini wana Chalinze pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo wameniomba pia niombe kasi ya mradi huu iongezeke. Usambazaji wa maji katika maeneo ya Bwilingu, Chalinze Mjini, Pera, Nero na uunganishaji wa wateja wanaomba kama ambavyo Mkurugenzi Engineer Luhemeja ametuambia inawezekana mpaka tarehe 30 Mei, 2021 mradi huu ukikamilika basi ukamilike kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni wa kawaida maombi ya wanawake, pamoja na miradi mingi ya maji lakini gharama za kuunganisha maji ni kubwa sana laki tatu. Wanawake wengi wa vijijini hawawezi kumudu kuitoa kwa wakati mmoja, wanaomba pengine ilipwe kwa installment. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, wanawake wameniomba niombe Wizara ya Maji pamoja na Taasisi zake, itoe elimu kwa namna ambavyo wanasema umetumia unit ngapi, mahusiano yake na ujazo wa maji. Kwasababu, yapo malalamiko ya bili kuwa kubwa na Mheshimiwa Waziri amekuwa akilisemea mara kwa mara, kupitia elimu hiyo wanaweza wanawake na watumiaji wa bili wakawa na uhakika na bili zinazowasilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu, wanawake pia wameniomba, utaratibu pengine wa Wizara ya Maji na Taasisi zake, zianze kutumia prepaid meter kwa ajili ya uhakika wa kile kitu ambacho unatumia maji hayo. Lakini sambamba na hilo, wanawake wameniomba pia na wananchi wa kawaida kwamba, inapotokea na hili hata Katibu Mkuu mama Queen Mlozi ndio amenitumia hapa. Inapotokea umehamia nyumba ambayo mtumiaji alikuwa halipi bili, bili hiyo inapewa kwa mtu aliyehamia kwa hiyo, Wizara na Taasisi zake ziweke mkazo katika kuhakikisha wanakusanya bili kwa mhusika. Lakini kumpa deni ambaye hahusiki na usipolipa maji yanakatwa hilo limelalamikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la nne pia, wananchi wa Kata ya Mpangani, Kibaha Mjini tuna mradi mkubwa wa machinjio na DAWASA walituahidi mradi mkubwa pale, ni miaka mitatu sasa mradi haujajengwa. Na machinjio yale halmashauri inatumia pesa nyingi zaidi ya milioni 40 kwa maji ya ma-bulldozer haya ukizingatia na mapato tu ya milioni 60 kwa hiyo, tunaomba hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa, pamoja na hotuba ya Waziri kuainisha changamoto mbalimbali, lakini ipo changamoto ambayo hata Mheshimiwa Rais aliisisitiza, matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya upatikanaji wa maji safi na salama. Nikuombe Mheshimiwa Aweso, unawazingua wanaokuzingua, lakini kwenye hili la matumizi mabaya naomba endelea na kasi ya kuwazingua. Katika mapitio machache tu ya taarifa ya CAG naomba ukawazingue watu wafuatao: - (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwanza, katika ripoti ya CAG licha ya kwamba tutapata fursa ya kuijadili, lakini kwa kuwa imeainisha matumizi mabaya usichelewe hapa:-

(i) Kuna fedha zaidi za bilioni mbili na milioni 200 zimetumika kwa matumizi mengineyo, ukurasa wa 64 wa taarifa ya CAG ya ukaguzi maalum na amesema mchukue hatua za kisheria;

(ii) Kuna miradi ya thamani ya bilioni nne na milioni 700 haifanyi kazi, haitoi huduma, CAG ameomba mkachukue maamuzi;

(iii) Kuna miradi ya bilioni moja ambapo malipo yamefanyika kwa kazi ambazo hazikufanyika ni ufisadi, kawazingue Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

(iv) Kuna miradi ambayo wakandarasi wameisababishia hasara Serikali na mapungufu ya zaidi ya bilioni 10, nakuomba Mheshimiwa Waziri kashughulikie, kawazingue. Kwasababu, tunazungumza hapa namna tutakavyoongeza mfuko wa Taifa wa maji vijijini lakini tusipofanya jitihada za kutosha kwa hiki kidogo kinachotengwa, zaidi ya bilioni 680 unaziomba leo za maendeleo kwa ajili ya miradi ya maji. Tusiposhughulika na mchwa hawa kwa wakati ni wazi tunaweza tukaona kila siku hela nyingi zinatumika lakini miradi haitoi tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Aweso kasi yako nzuri, Naibu Waziri Engineer anafanya kazi vizuri. Lakini na sio wahandisi pekeyake shirikiana na Wizara ya TAMISEMI wameanza kazi vizuri na wao, hatua zinachukuliwa na mamlaka zingine. Pia, nimemuona Waziri wa Utumishi naye akiagiza TAKUKURU ipitie miradi mbalimbali. Kwa kweli, kama tusipopata muarubaini wa kupambana na pesa zinazotumika vibaya kwenye miradi, tutaona kwamba hela nyingi zinatumika na miradi haifanikiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, Mradi wa WAMI Awamu ya Tatu Chalinze tunapongeza hatua ya Serikali ya kusitisha mkataba na kumpa mkandarasi mpya kazi inaendelea. Lakini kuna maeneo kwa mfano, vitongoji vya Ludiga, Kwaruhombo, Kata ya Kibindu nao tunataka wapate maji ya bomba, maeneo ya Ubena aliyosema Mheshimiwa Mbunge na nakazia hapo hapo naomba mradi huu kama ulivyokusudiwa kwamba utakamilika mwaka huu mwishoni basi ukamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno haya nakushukuru sana kunipa nafasi naipongeza Wizara hii, nampongeza mama yetu mama Samia, nina uhakika atawatua wanawake ndoo kichwani. Na ninamtakia kila la kheri ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa utendaji wake na mipango yake ya kushughulikia tatizo la maji nchini kwetu, pamoja na utendaji wa Mawaziri wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa maandishi utajielekeza kwenye Mradi wa Maji wa Chalinze - Wami uliopo katika Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali juu ya kusuasua kwa mkandarasi wa mradi huu wa Wami - Chalinze na kupelekea hali ngumu ya upatikanaji wa maji Jimbo la Chalinze, wananchi wa Chalinze wangependa kupata ufafanuzi katika maeneo yafuatayo:-

(i) Kwa kweli mradi wa maji Wami – Chalinze Awamu ya Tatu unasuasua, mpaka sasa kuna maeneo ndani ya Jimbo la Chalinze ambayo hayana maji ya bomba kwa zaidi ya miezi sita sasa.

(ii) Tunamshukuru sana Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kutembelea mradi huu wa Wami - Chalinze mwisho wa mwezi Machi, tatizo lishughulikiwe mara moja na maji yawe yanatoka ndani ya siku 100 na mkandarasi alipewa siku 100 ya kuonesha kas yake ya utekelezaji. Je, mpaka sasa ni kiwango gani cha tozo kwa kuchelewesha mradi?

(iii) Je, Wizara baada ya siku 100 alizotoa Waziri Mkuu kuisha na kasi ya mkandarasi kuwa ndogo, Wizara itakuwa tayari kufikiria upya juu ya mkandarasi wa mradi huu wa maji wa Wami - Chalinze Awamu ya Tatu, kwani kama sitakosea kuna kumbukumbu zinaonyesha mkandarasi huyu ana rekodi zisizoridhisha kwenye miradi mingine ya aina hii katika maeneo mengine.

(iv) Uendeshaji wa mradi huu wa maji wa Chalinze, Menejimenti ya CHALIWASA inaonyesha kushindwa kabisa. Uendeshaji wa mradi uko tofauti sana na wakati ukiwa chini ya mkandarasi toka China. Wananchi wengi wa Chalinze wanalalamika sana na bill zinazotolewa. Utokaji wa maji yenyewe usafi wa maji ni shida, waliokatiwa huduma ya maji bado wanachajiwa service charge.

(v) Mamlaka ya Maji Chalinze (CHALIWASA) wamejitoa kuagiza vifaa vya kuunganisha maji hususan mabomba badala yake wameliacha jukumu hili nyeti kwa wateja wa maji wasio na uelewa kitalaam wa ubora wa vifaa vilivyo sokoni hususan mabomba. Je, taratibu na sheria zinaruhusu?

(vi) Kwa kuwa Mji/Halmashauri ya Chalinze sasa ni mji wa viwanda na kuna ujenzi wa viwanda, mfano ujenzi wa Kiwanda cha Tiles Chalinze, ujenzi wa Kiwanda cha Kusindika Matunda, Mboga cha Sayona kinachotarajiwa kukamilika hivi karibuni. Hata hivyo kutokana na tatizo la maji Chalinze linaweza kuathiri kabisa ufanisi wa uzalishaji wa viwanda hivi.

Kutokana na shida hii ya maji Chalinze uongozi wa kampuni hii ulikutana na uongozi wa CHALIWASA kujua tatizo ni nini, hasa moja ya tatizo walisema uchakavu wa pump na machujio ya maji na baadhi ya vifaa. Serikali kwa sasa haina fungu kwa ajili ya kazi hiyo. Kupitia mazungumzo hayo mwekezaji ambaye ni Kampuni ya Sayona Fruits ilionesha utayari wa kuagiza hivyo vifaa nje ya nchi ili uweze kufungwa na hatimaye gharama hiyo ijumuishwe na kukatwa kwa awamu kutoka kwenye bill ya maji ya kiwanda itakayopelekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, menejimenti ya CHALIWASA inashauri iandikwe barua kwa Mawaziri wa Maji na Viwanda ili watoe ridhaa ya mwekezaji aendelee na utaratibu wa kuangiza hivyo vifaa. Mpaka sasa Wizara ya Maji haijatoa mwelekeo au maelekezo yoyote, jambo hili linaweza kufifisha ari za wawekezaji wetu. Kiwanda hiki kinatarajia kuzalisha/kusindika tani 60 kwa siku na kimejengwa kwa gharama ya zaidi ya bilioni 150, na rasilimaji kubwa ni upatikanaji wa maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara kutoa msimamo wake kwenye barua ya maombi iliyoandikwa na mwekezaji Kampuni ya Sayona Fruits kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji kwa maswali ya sera ya Serikali ya viwanda na wananchi wa Chalinze ambao watafaidika kwa uboreshaji wa miundombinu ya mradi huu wa maji Chalinze wa awamu zilizopita za kwanza na pili ambayo ni chakavu.

(vii) Suala la tatizo la maji katika Majimbo ya Kisarawe na Bagamoyo ni kubwa na moja ya sababu ni kumezwa na mipango ya Jiji la Dar es Salaam. Haiwezekani Kisarawe au Bagamoyo huduma za maji ziendeshwe na DAWASCO/ DAWASA ambayo wenyewe wamezidiwa kiutendaji kutokana na mahitaji ya Dar es Salaam na maelezo yake kutokana na wingi wa watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali/Wizara kuunda Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Pwani kama ilivyo kwa mikoa mingine na kuziimarisha kuzifufua Mamlaka za Maji za Wilaya ili ziwe na mamlaka kamili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi wa visima vya Kimbiji na Mpera ambapo ukikamilika unatarajiwa kuzalisha lita milioni 260 kwa siku ambapo maeneo yafuatavyo yatafikiwa; Gongo la Mboto, Chanika, Pugu, Ukonga na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maeneo haya yapo karibu na Kisarawe, naishauri Serikali kuona uwezekano wa kuweza kupata huduma ya maji kutokana na tatizo kubwa la maji maeneo ya Kisarawe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa kuweza kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara, nianze kukupongeza kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti, ninaamini utafanya vizuri kama ulivyofanya Bunge la Kumi na Moja, lakini sambamba na hilo nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa uandaaji mzuri wa hotuba ya bajeti na uwasilishaji mzuri wa Mheshimiwa Waziri ambao bajeti yao kwa kweli imeainisha maeneo mbalimbali na ukizingatia sekta hii ya viwanda ndio muhimili mkuu wa kukuza uchumi, kupambana na umaskini na kuzalisha ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri hotuba yake imeainisha maeneo mbalimbali, lakini kubwa imeanza kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipotoa hotuba yake ndani ya Bunge ambayo ililenga kuchukua hatua mbalimbali katika kukuza uwekezaji na kufanya marekebisho kadhaa katika sera, sheria na kanuni na kuondoa vifungu ambavyo vitabainika kusababisha vikwazo katika uwekezaji, lakini pia vikwazo kwa wafanyabiashara na ninapongea Mheshimiwa Rais tumeona namna ambavyo anaendeleza mafanikio ya awamu ya tano kwenye sekta hii ya viwanda lakini tumeona pia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wizara nyingine katika kuwezesha sekta hii ya biashara na viwanda kuona kwamba inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tumeona Mamlaka ya TRA imefungua akaunti zote walizofungiwa wafanyabiashara, kwa hiyo, tumeona namna ambavyo wawekezaji nao wameanza kurejesha imani yao na mitaji mbalimbali, lakini mchango wangu utajielekeza kwanza kwenye utekelezaji wa mpango wa kuboresha biashara wa blueprint pamoja na mafanikio ya kupunguza tozo zaidi ya 232; lakini ningemuomba Mheshimiwa Waziri kama tunataka mafanikio katika sekta yake hii ambayo itawezesha sekta nyngine ni lazima hatua ya kupunguza muda wa gharama za kupata leseni na vibali ambavyo vimeainishwa kwenye mpango huu wa blueprint utekelezeke kwa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema hivyo ukifanya mapitio ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwanza hata taarifa ya Kamati niipongeze wamewasilisha vizuri nchi yetu kuwa nafasi ya 141 kwa mwaka 2020 kutoka 131 kwa mwaka 2015 ni wazi imeshuka, lakini ninatambua mpango huu wa blueprint umeanza kutekelezwa 2019 lakini ninataka niseme taasisi kwa mfano TRA, Baraza la Mazingira Tanzania, Uhamiaji na masuala ya utoaji vibali vina mchango mkubwa katika kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika ripoti hiyo imeainisha namna gani Mamlaka ya TRA imetumia zaidi ya siku 182 mpaka siku 675 kujibu maombi ya vivutio vya kodi wakati sheria ya uwekezaji ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 imetamka kifungu 16(2),(3),(4) ndani ya siku 14 TIC inapopeleka maombi ya hawa wawekezaji mbalimbali wawekezaji hao wajibiwe, lakini utaona kwenye mamlaka zetu ucheleweshaji ni mkubwa. shilingi bilioni

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia baraza la mazingira uwekezaji wote wa viwanda lazima upatikane mchakato wa uhakiki wa mazingira. Sheria ya NEMC ya mwaka 2018 imeitaka baraza hili kuchukua siku 95 kwenye mchakato huo na kutoa vibali, lakini imekuwa ikichukua siku mpaka 133 mpaka siku 200 na kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ni miradi 5,600 kati ya 13,000 ambayo ilipewa vibali vya maingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaamini pia kaka yangu Mheshimiwa Jafo Mheshimiwa Waziri katika Wizara hii anayo nafasi kubwa kama ambavyo alivyokuwa na nafasi za mamlaka nyingine ili kuwezesha kwamba mpango huu ukamilike na kwa kweli kama watajikita kwenye mpango huu vikwazo vingine vyote ni vyepesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nije kwenye changamoto vya wafanyabiashara, wafanyabiashara pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa lakini bado wanalalamika utitiri wa kodi katika biashara mbalimbali, kwa mfano Mkoa wetu wa Pwani sisi unaongoza kwa viwanda na ninachukua fursa hii kuupongeza uongozi wa Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika maeneo mbalimbali kwa mfano Wilaya ya Mkuranga, viwanda vinavyotengeneza gypsum kwa mfano kiwanda cha KNAUF kinalalamika tozo kubwa ya karatasi ambayo imewekwa kwa ajili ya malighafi ya kutengeneza bidhaa ya gypsum, lakini sambamba na hilo tunavyo viwanda katika eneo la Kibaha, nikupongeze Mheshimiwa Waziri umeainisha namna gani Serikali imeenda kujielekeza eneo letu la TAMCO, lakini na mchango wake wa tozo mbalimbali wa zaidi ya shilingi bilioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo pia zipo changamoto za masuala ya miundombinu wezeshi kwa mfano suala la nishati, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nishati, ni siku tatu zilizopita alitembelea maeneo yale na kuwatia moyo wenye viwanda na kuwaambia mipango ya Serikali namna gani itawezesha umeme wa uhakika wa maeneo haya usio katika katika, lakini tunaomba hatua hii ifanyiwe haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo sisi wana Pwani tunaomba Serikali kwamba viwanda hivi pamoja na kwamba tunaongoza kwa kuwa na viwanda vingi lakini ajira hata zile ambazo zisizohitaji wataalam vijana wengi wamekuwa wakikosa ajira, lakini pia mazingira kazini ya wafanyakazi, pia ujira wa wafanyakazi hawa. Kwa hiyo tunaomba Serikali ishughulikie hayo naipongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kuainisha eneo la uwekezaji la Bagamoyo, lakini pia kwa kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza uzalishaji wa sukari naomba niwakaribishe Wilaya ya Rufiji na Wilaya ya Kibiti yapo maeneo ya kimkakati kwa kutumia Bonde la Mto Rufiji na uwezo wa kujenga viwanda hivyo vya sukari, lakini pia niipongeze Serikali yenyewe kwa kutumia mifuko yake ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika viwanda mbalimbali, lakini katika hili kwa kuwa Serikali imewekeza kwa mfano Serikali imewekeza katika mradi wa Mkulazi CAG ametoa maoni kadri muda wa manunuzi wa mashine unavyochelewa, kiwanda hiki cha Mkulazi kinapata hasara. Niiombe Serikali jambo hili lipo ndani ya uwezo wao wajitahidi ili nchi yetu ijitosheleze kwenye uzalishaji wa sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ninatambua mkakati wa uzalishaji wa vifaa tiba. Ripoti ya CAG imeainisha namna gani Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilivyotumia fedha zaidi shilingi milioni 900 kuanzisha kiwanda hiki katika Mkoa wa Simiyu, lakini mpaka leo zaidi ya siku 500 kibali cha ujenzi wa kiwanda hiki hakijatoka, lakini sambamba na hilo pia kuna Kiwanda cha Chai Mponde kule Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wanataka kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwakuwa ndio yenyewe ambayo imeona iwekeze kwenye miradi ya uwekezaji basi ijitahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimepata maombi au utumishi wa wamiliki wa hoteli, kuna hii hotel levy mpango wa blueprint ulipendekeza kupunguza kwa asilimia mbili, lakini mpaka sasa hivi haijatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaunga mkono hoja, lakini niombe mpango huu utekelezwe mpaka ngazi za Halmashauri, ahsante sana na hongereni na kazi iendelee. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi jioni ya leo kuweza kuchangia mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kusimama jioni ya leo, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan; Makamu wa Rais, Dkt. Mpango; Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote, kwa kazi inayoendelea kufanywa katika kuona kwamba nchi yetu inapiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa maandalizi ya mwongozo wa mpango huu. Na pia nampongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati pamoja na taarifa ambayo imewasilishwa na ninaendelea kuunga mkono hoja ambayo tumewasilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mapendekezo ya mpango ambayo yamewasilishwa inaonesha Serikali imejipanga kukusanya na kutumia zaidi ya trilioni 39 kwa mwaka 2022/2023. Maoni yangu katika item hii ya makusanyo na matumizi kwa kuwa Serikali ina mzigo mkubwa wa miradi mbalimbali ya kimkakati, na kwa kuwa Serikali yenyewe iliahidi kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 kwamba itakamilisha kujifanyia tathmini ya namna ambavyo inaweza kukopesheka kwenye masoko ya kimataifa (sovereign credit rating), naomba mpango ujao sasa itakayouandaa Serikali ije na taarifa mahususi ya kukamilisha tathmini hii ili iweze kuingia kwenye soko la fedha la kimataifa kupitia infrastructure bond, kupitia Eurobond.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kupitia pia hatua ambayo hata Mheshimiwa Rais ameielekeza Wizara ya Fedha hizi municipal bond ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia miradi hii ya kimkakati ambayo inachukua muda mrefu kuweza kuanza kutumika na kuweza walau kuanza kurejesha sehemu ya gharama na Serikali ijikite katika kugharamia shughuli zile za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tukizingatia imeshaongeza ajira mpya, imeshapandisha madaraja watumishi, imeshaongeza kwenye masuala ya mikopo ya wanafunzi, kwa hiyo ni wazi kabisa itahitaji fedha, na ili kuwapunguzia pia Watanzania zile kodi zingine kwa mfano tozo, Serikali ijikite kwenye masoko ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tumeona namna gani Serikali imefanikiwa kwenye huu mkopo wa masharti ya bei nafuu, uwezo wa Mheshimiwa Rais wa kushawishi, wa kujenga hoja ndani ya muda mfupi tumeweza kupata trilioni moja na bilioni 300, ni wazi hata hili pia linawezekana.

Kwa hiyo ninaomba katika mpango unaokuja Mheshimiwa Waziri wajielekeze huko ili kupunguzia gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninaomba katika taarifa yake Mheshimiwa Waziri ameainisha kwenye ukurasa wa 20, ametoa msisitizo kwamba bado kuna mianya ya uvujaji wa mapato, lakini bado pia kuna mianya ya kuvuja mapato kupitia risisti EFD. Nashauri atakapokuja na mpango kamili aeleze kinagaubaga ni namna gani Serikali itadhibiti uvujaji ambao yeye mwenyewe ameusema katika taarifa yake, kwamba hali bado haiyumkiniki, hali bado siyo shwari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze hatua ya Serikali ya kuweza kutoa kibali cha kuajiri watumishi zaidi ya 1,000 wa TRA. Hatua hii iendane na mkakati mahususi watakavyoweza kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nijielekeze kwenye suala zima la mwenendo wa mfumuko wa bei. Katika mapendekezo ya mpango huu yaliyowasilishwa inaonekana bado mwenendo wa mfumuko wa bei upo ndani ya viwango ambavyo vimeainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa, lakini hata hivyo mpaka sasa hivi mfumuko wa bei uko asilimia nne ukilinganisha na asilimia tatu ya kipindi kama hiki mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali ni tete mtaani. Bei za bidhaa cementi, bei za bidhaa nondo, bei ya mafuta, kwa kweli hali bado ni tete. Lakini niishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na nimpongeze Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba, amekuwa akitufahamisha hatua mbalimbali na mwelekeo wa Serikali wa kuweza kuona bei ya mafuta inapungua au hata kama inaongezeka lakini si kwa kiwango kilichokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwa hizi bidhaa za nondo, cementi, mabati, tuiombe Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha nao watuambie, wawaarifu Watanzania mkakati wao wa kuona namna gani bei zinapungua. Na ukizingatia kupitia bajeti ya 2021/2022 Serikali iliweka hatua mbalimbali za kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza leo bei ya nondo ukilinganisha ya Julai kwa tani zinazozalishwa hapa nchini BS 300 ilikuwa milioni moja laki nane thelathini. Tunapozungumza leo mwezi Novemba, kwa tani moja ya nondo ya aina hiyo BS 300 inayozalishwa hapa nchini ni milioni mbili laki mbili themanini, ongezeko la laki nne na nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kuzingatia kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Rais ya hizi pesa za 1.3 trillion, na ujenzi unaoendelea zaidi ya bilioni 500 zimepelekwa kwenye ujenzi. Na ninaomba niikumbushe Serikali ilituletea pesa kipindi cha Aprili na Juni za ujenzi wa madarasa, milioni ileile 20, na sasa hivi kiwango cha ujenzi wa darasa moja ni milioni 20. Naiomba Serikali iliangalie hizi kupanda kwa bei ili isikwamishe utekelezaji wa hizi pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli katika suala zima la mwaka wa fedha huu unaoendelea, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Waziri, mchango wa trilioni moja na bilioni 300 kuchochea uchumi katika maeneo mbalimbali. Mkoa wetu wa Pwani umepata zaidi ya bilioni 17, haijapata kutokea. Kwa hiyo, naomba nimshukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hasa sekta ambazo zimeainishwa ni zile zinazompa fursa mwanamke kupata muda wa kujishughulisha na masuala ya uchumi. Imeshughulishwa sekta ya maji, mitambo ikinunuliwa na visima vikichimbwa maana yake wanawake watapata fursa ya kujishughulisha na shughuli za uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kukushukuru kwa kunipa fursa. Lakini niseme tu kwamba…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, asubuhi ya leo na mimi niweze kuchangia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Serikali kwa marekebisho haya, lakini nampongeza kwa kuwa marekebisho mengi yaliyowasilishwa yamelenga kuimarisha ustawi wa wanawake na watoto, kwa hiyo ninampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, name nianzie kwenye Marekebisho ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353. Napongeza Serikali kwa hatua hizi ambazo zimewasilishwa, hatua kali ambazo zimelengwa kuchukuliwa kwenye makosa ya kumpa ujauzito mwanafunzi, kuoa au kuolewa na mwanafunzi na pia kwa wale ambao wanaficha, wana-facilitate matendo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na adhabu hizi ambazo zimelenga kutekeleza Sera ya Elimu ya Msingi kwa lazima, na pia baada ya Serikali kuamua kabisa kugharamia elimu ya msingi mpaka sekondari, kuna tatizo la msingi kubwa la mdondoko wa wanafunzi. Ukiangalia miaka ya karibuni tatizo la ujauzito kwa wanafunzi siyo kubwa sana mimba zimepungua, lakini tatizo lililopo ni wanafunzi wanaoanza elimu ya msingi wanapofika elimu ya msingi wanapofika darasa la saba wanaomaliza ni wachache sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninatakwimu chache, kwa mfano katika Wilaya yetu ya Rufiji watoto walioanza shule mwaka 2009 ambao walimaliza shule mwaka 2015 walianza shule ya msingi takribani 8,555; lakini waliomaliza ni 4,433 ambao ni sawa na asilimia 52. Kwa hiyo inaonesha zaidi ya asilimia 48 hawakumaliza shule. Inawezekana ni ndoa, inawezekana ni mimba, lakini nashauri Serikali, baada ya marekebisho ya sheria hii, ijielekeze zaidi kutambua chanzo cha mdondoko ambalo tatizo ni kubwa zaidi, wanafunzi wanaoanza siyo wanaomaliza, nusu yake wanaishia njiani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilidhani tuangalie pengine nayo itasaidia kuweka adhabu kali hata wale ambao hawahudhurii madarasani, hajaolewa, hana mimba, lakini wapo majumbani. Tumeona hilo zoezi wakati wa kufuatilia mdondoko wa wanafunzi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninaliunga mkono ni katika Sheria hiyo ya Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Watoto ambayo inalenga kumwokoa mtoto wa kike katika suala zima la ukeketaji. Kutokana na madhara mkubwa ya ukeketaji, naunga mkono adhabu ambazo zimeainishwa, ninaamini kitendo hiki sasa hivi itapunguza idadi kubwa ya watoto wa kike ambao wanakeketwa na wengine siyo kwa hiyari yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naunga mkono marekebisho yanayopendekezwa juu ya suala zima la kuongeza thamani ya kesi za mirathi katika Mahakama za Wilaya Sheria Na. 352. Mirathi imekuwa tatizo kwa wanawake wengi wanakosa haki zao, na kwa kuwa Mahakama Kuu haziko katika ngazi Wilaya na kwa kuwa, kwenda ngazi ya Mahakama Kuu kwa hii sheria ya zamani ilikuwa inawakwaza wanawake wengi pamoja na watoto wao. Kwa hiyo, kuongeza kiwango cha kutoka milioni 10 mpaka milioni 100 kusikilizwa ngazi ya Wilaya ninaona ni ukombozi mkubwa sana kwa wanawake wengi na ninaamini wengi wanatumia fursa hii kufungua kesi ili haki ipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimeona mapendekezo ya marekebisho katika Sheria ya Misitu 323; adhabu mbalimbali zimependekezwa kuongezeka kwa namna ambavyo mtu yoyote atakayekutwa na mazao ya misitu isivyo kihalali. Naunga mkono mapendekezo haya kwa sababu hali ya uharibifu wa misitu yetu tatizo limekuwa kubwa sana, na kwa kuwa uharibifu wa misitu unachangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko ya tabia nchi, tunapata mvua chache, lakini pia tunaigeuza nchi yetu kuwa jangwa, kwa hiyo sheria hii imefika wakati muafaka kabisa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili pia nikumbushie Serikali tulilalamika hapa namna ambavyo mojawapo ya zao la misitu kitanda, kimeongezwa bei kutoka shilingi 8,000 mpaka shilingi 120,000; kwa hiyo naikumbusha katika hilo isiwe adhabu hizi zikatumika pia kuwakomoa wale wanaofanya kihalali na kufanya vijana wengi wanaoshughulika na biashara hizi kihalali wakakosa haki zao.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo pia naunga mkono Marekebisho ya Sheria yanayohusiana na Migogoro ya Ardhi, migogoro hii hasa wanaoathirika wengi ni wanawake, namna ambavyo zile siku za kukata rufaa zimetamkwa sasa kinaga ubaga ili kupata haki kutoka Mabaraza ya Ardhi na Mahakama za Wilaya kwenda Mahakama Kuu, kuna matatizo ya kimsingi sana kwenye Mabaraza haya na watu wengi wanakosa haki zao, kwa kuwa sheria sasa imeainisha ni siku ngapi ambazo anaruhusiwa kukata rufaa katika Mahakama Kuu ili haki ipatikane.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua kabisa wanawake wengi hasa maeneo ambayo tuna migogoro ya ardhi, maeneo ya Mkwapani, Bagamoyo wana migogoro mingi ya ardhi, Kisarawe, Rufiji, Kibiti, Mafia, Mkuranga na Kibaha. Wanawake wanapofika kwenye Mabaraza ya Wilaya, hukumu inapotoka na kwa kuwa, kunakuwa na mkanganyiko na kwa kuwa, wanawake wengi wanaofika Mahakama zile uwezo wao unakuwa mdogo, inachukua muda mrefu kukata rufaa na anapokuwa nje ya kipindi kile haki yake anaikosa. Kwa hiyo ninaunga mkono kabisa kwamba, siku zilizowekwa hizi zitaweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuunga mkono pia mapendekezo ya marekebisho ya Sheria inayohusu Masuala ya Makosa ya Jinai, kutambua ushahidi wa mtoto, ili kama una-credibility ili uaminiwe na haki iweze kutendeka. Tumeona makosa mengi ya jinai wako watoto wanatoa ushahidi, lakini wakati mwingine kwa kuwa sheria haikuweka wazi, sasa kifungu hiki kimewekwa, ninaamini pia watoto watalindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ninaunga mkono mapendekezo ya namna ambavyo wenzetu wa Ustawi wa Jamii wanaweza wakatoa maoni kwa ajili ya kesi mbalimbali zinazohusu watoto. Pia ninaunga mkono namna ambavyo mtoto amelindwa na namna ambavyo adhabu zinazotakiwa kutolewa zihusiane na Sheria ya Mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa name pia ninaungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa kukamilisha safu ya Wakuu wa Wilaya na wote walioteuliwa nawapongeza sana, hata wale walioachwa nawapongeza sana kwa kazi nzuri waliyoifanya katika maeneo mbalimbali, kwa kipindi cha utumishi na Mwenyezi Mungu pia atawajalia mengine na nawatakia kheri katika maisha ya mtaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono Muswada huu.
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (no. 6) Bill, 2021
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuweza kutoa mchango wangu mdogo katika Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbalii (Na. 6) wa Mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. Nakushukuru wewe mwenyewe pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza Serikali na kuonyesha usikivu pamoja na wasaidizi wake; Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Nishati na watendaji mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami naunga mkono hoja ambayo imewasilishwa na Serikali pamoja na maoni ya Kamati yetu. Hususan najielekeza kwenye mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332, na hiki ambacho tunazungumza kufutwa kwa kifungu 83 (b). Kama nilivyotangulia kusema, naipongeza Serikali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuipongeza Serikali, naiomba kwa sababu hapa palikuwa na changamoto, Serikali inatambua yapo makampuni yanayonunua mazao kwa jumla ambayo yana tabia ya kwenye vitabu vyao vya fedha kuongeza kiwango kinachowalipa wakulima wakati kiuhalisia wanawalipa kidogo. Ndiyo maana kukawa na hiyo tafakuri ya nini kifanyike?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, kwa nia hiyo hiyo njema waliyonayo, waendelee kufanya utafiti, ni namna gani makampuni yanayonunua mazao ya wakulima iwe ya ufugaji au uvuvi, itaiwezesha Serikali kupata mapato ya kutosha na kuondoa upotoshwaji unaofanywa kwenye taarifa zao za fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, nawashukuru wawakilishi wa vyama vya wavuvi, wafugaji na wakulima ambao walikuja kwenye kamati yetu kwa nyakati tofauti; na nikushukuru mwenyewe kwa kuridhia Muswada huu uje kwa hati ya dharura kwa maslahi ya Watanzania wetu ambao ambao wengi wapo katika sekta hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia niunge mkono mabadiliko yaliyowasilishwa na Serikali ya kurekebisha Kifungu cha 7 cha sheria ya usimamizi wa kodi, Sura ya 438 kwa kuongeza Kifungu cha 3 kwa nia ya kuhakikisha mradi huu wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Chongoleani Tanga; nasi kama Kamati pamoja na Bunge lako hili tunatambua faida nyingi za mradi huu ikiwemo kuzalisha ajira 10,000, ikiwemo namna ambavyo Serikali itapata mapato ya asilimia 40 kutokana na bomba hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Serikali itakusanya kodi kwa miaka 25 na hata umiliki wa hili bomba kupitia TPDC. Kwa hiyo, inaonesha utayari wa Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza ile miradi ya kimkakati. Katika hilo pia naishauri Serikali kwa kuwa inaendelea na majadiliano ya miradi mingine mikubwa mikubwa ikiwemo la kusindika gesi asilia Lindi, likiwemo la Liganga na Mchuchuma huko. (Makofi)

Mheshimiwa spika, kwa hiyo, kama kuna vikwazo vyovyote katika hatua hizi za awali kwa masuala ya kikodi; na kwa sababu tunataka kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, Kamati ya Bajeti kupitia ruhusa yako na kwa niaba ya Bunge, tupo tayari kuona miradi hii ya kimkakati ambayo ikitekelezeka vizuri itachangia pato la Taifa na kuwezesha sekta nyingine nazo kufanya kazi. Kwa hiyo, napongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kamati tumeshauri, kwa muktadha huo huo Serikali iangalie nayo sheria nyingine mbalimbali; kwa mfano tumezungumzia msamaha wa kodi. Tumeomba Serikali hebu ilitazame hususan katika sekta hii ya viwanda vya dawa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye vifungashio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ulitupa ruksa ya kutembelea kiwanda cha dawa cha pekee hapa nchini cha Serikali kilichopo Keko. Katika ziara yetu ile tumegundua namna gani Serikali imeanza kufanya vizuri. Kiwanda kile sasa hivi kina uwezo wa kuzalisha dawa vidonge milioni sita tofauti na vidonge 1,500,000 lakini imeongeza uzalishaji wa dawa kutoka Paracetamol mpaka dawa zaidi ya 15. Hata hivyo, ina uwezo wa kuingia kwenye masoko ya Kimataifa yakiwemo soko la nchi za SADC, lakini changamoto ambayo walituomba ni Serikai kuangalia hii Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vifungashio.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali itakapotathmini kodi mbalimbali, basi iweze kufanya na hilo ili tuweze kuisaidia hii sekta ya uzalishaji wa dawa hapa nchini, tuweze kujitosheleza na kupunguza gharama za uagizaji dawa nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, naomba nikushukuru sana. Naunga mkono, ahsante sana. Nampongeza tena Mheshimiwa Rais kwa hatua hii na kuwajali Watanzania ambao ndio wengi. Ahsante sana. (Makofi)