Parliament of Tanzania

Contributions By: Hon. Dr. Abdallah Saleh Possi

All Contributions

The Access to Information Bill, 2016

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uhai siku ya leo. Nimepata hii fursa ya kuchangia huu muswada, nitachangia kwa haraka haraka baadhi ya mambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kusema ukweli ni kwamba kwa Taifa letu hili la Tanzania lenye watu zaidi ya milioni 50, lenye mikoa mingi, mipaka kuanzia Mara mpaka Ruvuma, Katavi mpaka Pemba, haiwezekani hata siku moja, hata ingetokea mtu aangalie television zote, asome magazeti yote kwa siku akagundua, akapata habari zote za nchi; hata kama angepita kwenye mbao za matangazo kwenye ofisi zote za Serikali zilizopo katika eneo analoishi. Ndiyo maana sasa kuwe na utaratibu maalum wa kumwezesha Mtazania kupata habari pale anapoihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wanaweza wakawa wamefanya tafiti ama za kitaaluma, ama za masuala mengine na utagundua ukweli ni kwamba siyo kila taarifa utaipata kwenye vyombo vya habari au utaipata kwenye notice za matangazo au kwamba utakwenda tu ikawa hapo hapo.
Kwa mfano, huwezi ukaenda leo ukasema naomba taarifa inayohusiana na historia ya elimu maalum Tanzania toka mkoloni mpaka mwaka 1980, halafu ukategemea utaipata hapo hapo; au huwezi uka-expect kwamba Afisa wa Serikali atajua tu wewe ukifika taarifa unayotaka ni hiyo.
Kwa hiyo, ni lazima kuwe na utaratibu maalum. Kwa maana hiyo, sheria hii inarahisisha sasa upatikanaji wa taarifa mbalimbali kinyume na baaadhi ya Wabunge wengi waliodhani kwamba hii taarifa, maana waliishia kwenye mfano mmoja kwamba labda inahusiana na taarifa za masoko au vikao vya Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na ukweli huo, ni lazima tutenganishe vitu viwili; sheria hii, nilikuwa nashangaa kidogo, mtu anaongelea hili as if waandishi wa habari sasa kabla ya kutoa taarifa yoyote, lazima wa-apply taarifa, hapana. Hiyo ingekuwa unreasonable, haikuwepo wala hata kabla ya kipindi cha mwaka 1984 wakati hatujawa na Bill of Rights. Pia kuliwa na mkanganyiko wa kuchanganya mambo ya Whistleblowers na muswada huu. Ni vitu viwili tofauti. Hapa tunazungumzia Mwananchi ambaye anataka taarifa. Whistleblowers ni mtu ambaye tayari ana taarifa, the two do not go together.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine na bahati nzuri kwenye taarifa ya Upinzani walirejea katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaozungumzia haki za kisiasa na haki za kiraia ambao kwa kweli Ibara ya 19 ya Mkataba huo inazungumzia haki ya uhuru wa habari. Cha kusikitisha, labda ni kwa bahati mbaya, wengi waliorejea hapo, wakasahau kurejea dokezo namba 34 la mwaka 2011 linalotolewa na Kamati ya Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ambalo lilikuwa linatolea ufafanuzi kuhusiana na Ibara hiyo hiyo 19 ya huo mkataba ambao ni Ibara yetu ya 18 ya Katiba. Kama wangefanya marejeo hapo, mkanganyiko mwingi na vijembe vingi vilivyokuwa vinatolewa visingekuwepo kwa sababu ufahamu ungekuwa umeimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niende haraka haraka tu nitoe mfano. Nimesema kwa mfano, muswada huu hauna haja ya kuzuia habari, kwa sababu ukisoma kwa mfano Ibara ya 4, 5 na 9 inakuonesha. Kifungu cha 5 ni wajibu wa mwenye taarifa kutoa taarifa; kifungu cha 9, kikisomwa na marekebisho, bahati mbaya kuna watu walijitapa kwamba wamesoma, wameelewa jana, lakini walichokuwa wanachangia kinaonesha kwamba hata haya marekebisho ambayo Mwenyekiti aliweka pale mezani, hawakutaka kuyasoma. Ukisoma na marekebisho, kifungu cha 9 kinasema; sheria itakapoanza kazi ndani ya miezi 36, Maafisa wote ni lazima waweke hizo taarifa hadharani. Hata kama kwa sababu moja au nyingine wasipoziweka, haimzuii, haiathiri haki ya mtu kupata taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 11 kinaonyesha kwamba of course mtu ukiandika taarifa bado unaweza ukajibiwa kwamba hili tayari linajulikana liko public. Maana yake nii? Ina-imply kwamba kuna uwezekano bado, licha ya sheria hii kutokea kwa mtu kupata taarifa kwa njia nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitumia busara tu, hivi ni kweli kwa muswada huu tunataka kudhani kwamba mwandishi wa habari akitaka kumhoji Mbunge au Waziri ni lazima aombe ruhusa kwa kupitia sheria hii hapa? Sidhani na that is not correct. Pia ukisoma vizuri Ibara ya 12 inakwambia hakuna chochote kwenye sheria hii kitakachomzuia mtoa taarifa kutoa taarifa kwa njia nyingine zaidi ya zile ambazo zimeelezewa katika muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema mwanzo lile la Whistleblowers, nasikitika sana hasa kwa wale ambao wanasema waliisoma muswada huu vizuri, hawakupitia Kifungu namba 23, hawakupitia ibara ya 23(1), hawakupitia Ibara ya 24. Ibara ya 23 inasema, hakuna atakaye adhibiwa iwapo atatoa taarifa inayoonyesha kuwa mtu ametenda kosa. The same na Ibara ya 24, hamna atakayeadhibiwa kwa mtu ambaye ametoa taarifa akiwa na nia njema. Kuna watu wakasema, anaadhibiwa vipi mtu akiwa amepewa taarifa mbovu? Jamani eeh, kwenye kanuni za adhabu kuna defence ya sheria inaitwa mistake of fact.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu akitembea hapa akaokota box, kumbe lile box lina hela, hatahukumiwa kwamba ameiba pesa, kwa sababu in his mind alichoona ni box. Kwa hiyo, ukipewa taarifa wewe ukaamini ni kweli na ukaitoa chini ya kanuni za adhabu hutaadhibiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kilichosemwa kingine hapa, aidha ni ....
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kengele ya kwanza au ya pili?
Aah ya kwanza, okay. Niendelee na mambo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ile exemption ya Ibara ya 6, kuna mtu mmoja alisimama jana akasema kwa mfano mambo ya faragha, kwamba hii ina mpango wa kuzuia maslahi ya viongozi. Faragha ni haki pia iko kwenye Katiba.
Kwa hiyo, hatuwezi tukaona haki moja tukaacha haki nyingine. Bahati nzuri hata katika huo Mkataba wa Umoja wa Mataifa ambao bahati nzuri Kambi ya Upinzani wame-refer, moja ya limitation to the right of freedom of information ni privacy. Sasa nashindwa kuelewa kwa nini hayo hayakuoneka, yanaonekana hapa? That is either double standard au unasoma ukiwa biased.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia na masuala ya usalama. Kuna watu wanaona kama hili jambo geni. Kwa bahati nzuri katika hotuba yao waka-refer kwa mfano, jamaa wa WikiLeaks Julian Assange, kitu ambacho hawakusema, Julian Assange sasa yuko katika hifadhi ya kisiasa kwenye Ubalozi wa Ecuador kwa sababu Marekani wanamtafuta, alitoa taarifa zinazohatarisha usalama wake. Ni Marekani hiyo hiyo ambayo jana tuliambiwa hapa kiongozi wake George Washington aliyetoa definition ya democracy, hawazungumzii kuhusu Snowden aliyetoa taarifa za usalama, lakini leo taarifa za usalama za Tanzania zinaonekana ni kuzuia uhuru wa vyombo vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba tu niseme kwamba ni vizuri tunapochangia miswada tusome, tuielewe na tuwe wakweli. Siyo tabia njema kwa kiongozi aliyeaminiwa na hata aliyejigamba kwamba ameelewa kitu anachoki-present kusema mambo ambayo ukiangalia mara moja unagundua kwamba he was simply not serious katika homework yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, naomba nimalizie kwa kuunga mkono hoja.

The Media Services Bill, 2016

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kusema naunga mkono hoja na nataka kusema maneno machache. Nitafafanua ile dhana inayoongelewa kana kwamba uhuru wa habari ni absolute, ni limit less, kwamba hauna mipaka yoyote ile. Ila nianze tu kwanza kwa ujumla kwa dhana nzima ya haki za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mwenyewe ni mtu wa haki za binadamu, naamini huko, lakini tuna nadharia mbalimbali, wapo wanaosema haki za binadamu ni absolute, hazina mipaka, lakini wapo wengine wanaosema kuna mipaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja wa jumla sana, unaweza usihusiane na uandishi wa habari. Kuna watu wanasema katika nadharia hiyo hiyo ya haki za binadamu, basi mtu atakuwa na haki pia kuwa na mapenzi ya jinsia moja, lakini hatakuwa na haki ya kuoa wake wawili upande mmoja. Upande mwingine wa dunia kuna watu wanasema aaa’ unaweza ukaoa wake wawili lakini hiyo ya mapenzi ya jinsia moja hatutaki kwa sababu ni kinyume na utamaduni wetu na sisi tuna haki zetu wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wengine wakaenda mbali sana, katika dunia hii ambayo watu wana interest tofauti huwezi ukawa una mipaka kwa sababu unaweza ukajikuta haki yako moja inavuruga haki ya mtu mwingine. Sasa na hilo linajikita katika nadharia nzima ya sheria, wapo wasomi wa zamani wanasema pale ambapo hakukua na sheria binadamu alikua anaishi katika state of confusion, state of anarchy, kwamba kila mmoja anafanya analotaka matokeo yake na usalama unapungua. Sasa katika mambo hayo yote mawili lazima kuwe kuna balance kati ya haki pamoja na mipaka yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije katika dhana ya uhuru wa habari. Nafahamu katika ibara ya 18 ya Katiba, lakini bahati nzuri Katiba yetu ukiisoma ile sehemu ya haki za binadamu (Bill of rights) lazima uisome na kifungu cha 30(1) (2), maana yake nini? Haki zote zilizokuwemo mle ikiwemo haki ya habari ina- certain restrictions. Moja ya restriction hizo ni kuangalia masuala yanayohusu maadili (morality), usalama wa nchi, lakini haki za watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu hiki hakikuja kwa bahati, tayari hapo maamuzi ya Mahakama Kuu yanasema Tanzania kwa sababu ilisaini Mikataba mbalimbali ya Kimataifa, basi ninavyotafsiri katika hii ni vizuri kuangalia na Mikataba mingine ya Kimataifa inasemaje, mimi nitaangalia Mikataba miwili lakini pia nitaangalia Azimio moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba hii miwili ni Mkataba wa Haki za Binadamu wa Afrika (the African Chart of Human and People’s right), lakini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kisiasa na za Kiraia. Kwa sababu mikataba hii ina chanzo katika Universal declaration of human rights ambayo wataalam wanasema ni azimio ambalo lina desturi za sheria za kimataifa nitakuja huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, the African Charter kweli inaonesha Ibara ya 9(1), uhuru wa habari. Ukiangalia ibara ya 27(2) inazungumzia kuhusu limitations, ukienda ibara ya 29 moja ya uwajibu ni watu kutokufanya mambo ambayo yatahatarisha usalama wa nchi zao wenyewe. Nasema hivi kwa sababu kuna watu walikuwa wanazungumzia mambo ya uchochezi na nini, tutakuja huko baadaye. Mambo haya pia yanajitokeza katika ibara ya 19(3) ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kiraia, lakini pia na Ibara ya 20 ya mkataba huo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema haya yana asili yake katika Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, kwa hiyo ukizisoma ibara ya 18 na ibara ya 30 utagundua kwamba kila haki ina mipaka yake. Sasa kwa nini kuna mipaka? Huwezi ukasema kwa sababu kuna uhuru wa habari, basi mtu aandike aseme sasa watu wachinjeni watu wa kabila fulani, sasa ni wakati wa jeshi kupindua nchi; haiwezekani, haiko hivyo Marekani, haiko hivyo Urusi, haiko Uingezereza, haiko Tanzania na haitakuja kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo tu la public or state interest tuangalie mfano unaoendelea leo. Leo ukiangalia CNN ya Marekani au ukiangalia ABC wanavyoelezea wao kuhusu vita ya Syria ni tofauti kabisa na inavyoelezewa kwenye labda Russian Television, kila mmoja anaelezea kutokana na state interest. Sasa sisi ni watu gani ambao hatujui state interest na hatutaki ku-protect our state interest kupitia media. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikumbushe kitu kimoja kabla sijasahau Mheshimiwa Tundu Lissu alituongelea hapa kuhusu Nyalali Commission. Bahati nzuri ripoti tunayo hii hapa na tukaangalia ukurasa wa 48 na ukurusa wa 49. Ukurasa wa 48 ulikuwa unazungumza kuhusu News Paper Act, mapendekezo, akasema tu kwa mfano the Act be amended according to allow more freedom of the press and expression and relaxation of censorship of information, nitatafsiri baadaye. Ukurasa wa 49 ulikuwa unazungumzia kuhusu Tanzania News Paper Agency Na. 14 ya mwaka 1976.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Okay, the monopoly of the news correction and dissemination (SHIHATA) should be abolished, the provisions of the Act that violate freedom of the constitution and press should be repealed. Sasa haya ndiyo yalikuwa mapendekezo, wapi waliandika kuhusu accreditation?
Mheshimiwa Tundu Lissu wapi waliandika kwamba vifungu vyote vya sheria hizo cha kwanza mpaka cha mwisho viondolewe na visirudishwe tena? Ni wapi katika mfumo wa sheria kwamba sheria haiwezi ikawa repealed na kurudishwa tena?
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umekwisha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwanza? Okay, baada ya kusema hayo nisahihishe mambo mawili yaliyokosewa au yaliyosemwa kimakosa na Mheshimiwa Mbilinyi na Mheshimiwa Kubenea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbilinyi jana alivyoanza alisema eti tafsiri ya media kwenye Muswada eti ni chombo cha habari za ki-electronic. Chombo cha habari cha electronic kwenye huu Muswada wa kisheria maana yake ni electronic media, tafsiri ya media kwenye Muswada huu kwa Kiswahili ipo kule nyuma, ni sekta ya habari. Sasa iwapo mtu hapa anasimama kama Waziri Kivuli wa Habari halafu anashindwa kuona tofauti kati ya media na chombo cha habari cha electronic, haya ndiyo tunasema sasa umuhimu wa kuzingatia viwango na weledi unahitajika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kubenea naye akaja na analysis yake moja, ile statement ukiisoma kweli ni sahihi, lakini ukifikiria kwa sekunde mbili kuna tatizo kubwa la uchambuzi. Alisema hivi, kwamba Uhuru wa habari ni kitu tofauti kwa hiyo kuna haki ya uhuru wa habari, lakini hakuna haki ya kuwa daktari, kweli hakuna haki ya kuwa daktari kama vile hakuna haki ya kila mtu kuwa mwanataaluma ya habari; kuna haki ya kupata habari, kuna haki ya afya kwenye mikataba mingine, lakini hakuna haki ya kuwa mwanahabari na hakuna haki ya kuwa daktari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama analysis hii ndogo mtu nguli anayejitamba hapa ni mwandishi wa habari wa siku nyingi anashindwa kuwa nayo, basi inaleta matatizo kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini labda niwakumbushe tukio moja dogo tu linalosema ni kwa nini tuwe na weledi. Mwaka fulani alipouwawa Kamanda wa Polisi wa Mwanza bwana Henry Barlow, ikachapishwa picha ya dada mmoja kwenye magazeti, mengine yanaheshimiwa sana akasema huyu alikuwa ni chanzo cha ugomvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri kuna watafiti wakasema mbona hii picha ilichapishwa kwenye website ya kimarekani na sisi wabishi tuka-google kweli tukagundua yule mama alikuwa ni binti wa Kimarekani, taarifa ilikuwa inahusu obesity but somehow mtu tu anapata courage ya kwenda kwenye internet photocopy, weka kwenye gazeti na Watanzania wote wanaaminishwa kwamba eti huyu alikuwa ni chanzo cha mgogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia hayo, utaona ni kwa nini tunahitaji weledi na professionalism. (Makofi
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa muda.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa afya ambayo ndiyo nyenzo muhimu katika ufanyaji kazi wa kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa imani yake aliyoonesha kwangu kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu. Nasema ni heshima kubwa sababu nafahamu changamoto iliyoko miongoni mwa jamii ya watu wenye ulemavu. Namwahidi sitomwangusha, nitafanya kazi kwa uadilifu mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake thabiti. Namshukuru pia kwa miongozo yake ya kila siku, ambayo siyo tu kwamba imetupa ari lakini imetujenga katika uongozi na naamini ni Waziri Mkuu imara na Wanaruangwa wamepata mwakilishi mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Antony Mavunde. Kutoka kwa hawa wawili nimejifunza kwamba umoja ni nyenzo muhimu katika kutatua changamoto mbalimbali na nafahamu kwamba Wanaperamiho na Wanadodoma Mjini wamepata Wawakilishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakupongeza wewe na kukushukuru pia kwa ushirikiano wako uliotupa siku zote tulizokuwa hapa Bungeni. Nawapongeza Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge wote. Sasa kwa mujibu wa kanuni 99(2) ya Kanuni za Bunge, Toleo la mwaka 2016 nijibu baadhi ya mambo mbalimbali yaliyoongelewa kuhusu watu wenye ulemavu. Nitayajibu kwa ujumla wao kwa sababu baadhi ya mambo yamerudiwa rudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimetolewa hoja kuhusu elimu katika mambo mbalimbali. Niseme tu, tayari Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa watu wenye ulemavu, jitihada zimekuwa zikifanywa. Binafsi nimefanya ziara katika maeneo mbalimbali, nimeona kuna dalili njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi yangu itazidi kuwasiliana na Wizara ya elimu ili kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata elimu sawa na watu wengine, katika suala hilo hilo la elimu limezungumziwa jambo linalohusu Vyuo vya Elimu ya Ufundi kwa Watu Wenye Ulemavu. Ni dhima ya Serikali kuboresha elimu katika Vyuo hivi hasa kupitia Program ya Kukuza Ujuzi inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Niseme tu, haya hayataishia hapa. Vyuo vingine vyovyote vinavyotoa Elimu ya Ufundi, vina jukumu pia la kuhakikisha elimu yao ni shirikishi na tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu ili Vyuo vya VETA pia viweze kutoa elimu shirikishi kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa pia suala la ajira. Niseme tu Sheria Na. 9 ya mwaka 2010, lakini pia na Sheria ya Ajira ya Employment and Labour Relations Act vinazungumzia kuhusu ajira kwa watu wenye ulemavu. Niseme tu na nikumbushe kwamba ni marufuku kwa mujibu wa sheria zote hizi mbili, mtu kuachishwa tu kazi eti kwa sababu ya ulemavu. Ukweli ni kwamba waajri wana jukumu la kuweka miundombinu na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyakazi wenye ulemavu, yaani kwa Kiingereza ni reasonable accommodation. Kwa hiyo, natoe tu wito kwa watu wenye ulemavu kulizingatia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa pia suala kuhusu majengo ya umma (accessibility). Ofisi yangu imeshaanza kuwasiliana na itaendelea kuwasiliana hasa na TAMISEMI lakini pamoja na Idara na Taasisi nyingine za Serikali ili kuhakikisha kwamba majengo ya umma yanafikika kirahisi kwa watu wenye ulemavu. Hili ni suala la kisera lakini pia ni suala la kisheria lipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inatekelezwa na Serikali iliyoko madarakani kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumziwa pia masuala yanayohusu mauaji wa watu wenye Ualbino, niseme tu hili ni suala ambalo lilianza toka miaka ya 2006. Nashukuru Mungu kwa sasa limepungua, lakini nafahamu suluhisho thabiti la mauaji haya ni watu kuondokana na imani potofu. Watu mara nyingi wanaangalia hili suala kwa uchache wanafikiri ni ushirikina, lakini tunakwenda mbali zaidi, tatizo kubwa ni binadamu kufikiria kwamba mtu mwenye Ualbino ni mtu tofauti. Once imani hiyo inapotoka, basi usalama sahihi ndiyo utapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashirikiana na wadau mbalimbali na itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwa na mpango madhubuti wa kuondoa unyanyapaa na tayari tuko katika stage za awali za kuandaa mpango huo ambao once ukifanikiwa baada ya miaka mitano tuna uhakika hali itakuwa nzuri ili wale wanaoishi katika vituo maalum, sasa waweze pia kujumuika na wenzao kwa sababu tunafahamu ni kinyume cha sheria, ni kinyume cha haki za binadamu kwa watu kuwekwa kwenye makambi pasipo sababu maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limezungumziwa suala la kodi na incentives mbalimbali kwa watu wenye ulemavu. Hili ni wazo zuri na teknolojia inapoendelea, inarahisha mambo mengi. Haijaandikwa popote kwamba chombo cha usafiri cha mtu mwenye ulemavu kiwe ni bajaji peke yake. Kwa hiyo, pale ambapo ataweza kuendesha gari, basi Ofisi ya Waziri Mkuu itawasiliana na Wizara ya Fedha ili kutengeneza utaratibu maalum kwamba yale magari ambayo yatakuwa ni nyenzo nzuri ya kujongea kwa watu wenye ulemavu, basi incentives zipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia utaratibu kwa sababu nafahamu experience ya nchi nyingine, utaratibu huu ulikuwa abused kwa mara ya kwanza, lakini walijitahidi wakaweka sawa. Kwa hiyo, ni wazo zuri na tutaendelea kulifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine hapa ambalo kidogo itabidi nilielezee kwa kirefu ni kuhusu makazi ya Watu Wenye Ulemavu. Hoja zilizotolewa, yaliitwa makambi, sidhani kama ni lugha nzuri sana, ni Makazi ya Watu Wenye Ulemavu. Haya yana historia ndefu; yalikuwa ni makazi ya wazee na wasiojiweza na watu wenye ulemavu na ukiangalia historia yake hasa, yalianza kuwatunza waathirika wa ugonjwa wa ukoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba dhamira ya Serikali hasa ukizingatia sheria na mikataba mbalimbali ya haki za binadanu na hasa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006 ni kuhakikisha kwamba mtu mwenye ulemavu anashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na siyo kuwekwa kwenye makambi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu pia kutokana na changamoto mbalimbali, wapo watu wachache kwa namna moja au nyingine watahitaji msaada fulani. Kwa hiyo, niseme tu kwa wale wanaoishi katika makambi haya kwa sasa Serikali itajitahidi kuyaboresha makambi haya, tayari tulishaanza mawasiliano na Wizara ya Ardhi ili kuzuia uvamizi katika baadhi ya haya maeneo na huduma nyingine zimendeelea kuboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, dhima kuu ni kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanaishi katika jamii shirikishi. Kwa hiyo, nikumbushe tena, Halmashauri zina wajibu wa kuwasaidia watu wenye ulemavu ambao hawana msaada lakini jamii pamoja na familia kisheria vyote hivi vina jukumu la kuwasaidia na kuwatunza watu wenye ulemavu ambao watahitaji msaada. Ila kwa hali halisi ni kwamba suala la ulemavu ni suala mtambuka na watu wenye ulemavu wana haki ya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limeongelewa suala la kuwezesha watu wenye ulemavu kiuchumi. Niseme tu kwamba kuna baadhi ya mambo kwa kweli yanahitaji tu kubadilisha namna ya kufikiri.
Kwa mfano, tunapozungumzia asilimia kumi ya bajeti ya maendeleo ambayo inakwenda kwa vijana na akinamama katika Halmashauri mbalimbali, hakuna kikwazo chochote cha sheria kwa Mtendaji wa Serikali kutoa kipaumbele maalum kwa watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niweke msisitizo tu na niseme kwamba kwa sababu watu wenye ulemavu ni watu ambao waliachwa nyuma kwa muda mrefu na kwa sababu affirmative action (kipaumbele maalum) kimekuwa ni jambo la kawaida cha kuwakwamua watu walioachwa nyuma kwa muda mrefu, imefanywa hapa katika jinsia lakini hata katika zile nchi ambazo zili-suffer ubaguzi wa rangi, yalifanywa hivyo kwa makundi maalum yaliyobaguliwa kutokana na hali zao. Hivyo basi, kutokana na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu na Katiba ya Nchi na Mikataba mbalimbali na sera nitoe maagizo tu kwa Watendaji wote wa Serikali, sasa kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu siyo option kwa sababu ni suala la lazima ili kuhakikisha kwamba usawa halisi kwa watu wenye ulemavu unapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme tu kwamba, naunga mkono hoja na niwatakie heri Mawaziri wote na Viongozi wote wa Serikali katika kuchapa kazi, waendelee kufanya kazi vizuri. Nitoe ushauri tu kwa wenzangu wa upande wa pili, wapo watu wanaosema kwamba utakuwa una busara sana if you try to hide a bit of your stupidity. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMEVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nitakwenda haraka haraka. Kwanza, moja kwa moja niseme tu kwamba naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri. Ninachokisema hapa ni kuboresha tu kwa sababu nafahamu kazi waliyokuwa nayo na yapo mengine tutaendelea kuwasiliana vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika kuboresha huko, yameongelewa hapa kuhusu masuala ya accessibility ya facilities kwa watu wenye ulemavu. Sitayarudia aliyosema Mheshimiwa Mama Macha na wengine ila nitaboresha tu kwamba ni vizuri sasa pia kuangalia ni namna gani tunaboresha teknolojia kwa ajili ya wale watu wenye uhitaji wa viungo bandia. Nasema haya nikifikiria idadi kubwa ya watu ambao walikatwa viungo vyao, watu wenye Ualbino ambao watakuwa wakihitaji kuwa productive na nimeona ugumu au ughali wa masuala haya ya vifaa bandia. Kwa hiyo, in future for purpose ya kuboresha, ni vizuri tuangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la pili ambalo nataka kuliweka sawa ni suala la NHIF. Ni utaratibu wa bima yoyote ile duniani kuwa na exemptions; haiwezi ika-cover vitu vyote lakini sasa tuangalie zile life saving instruments; vitu kama pace makers na vingine kwa sababu ni very expensive lakini visipokuwa covered hivi, maana yake kuna watu wanaweza wakapoteza maisha na purpose ya bima ni ku-save life.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo pia ni muhimu sana, najua tumefanya mawasiliano lakini nasema hivi kwa kukumbusha zaidi; ni kwamba kuhusiana na mafuta maalum ambayo yanawakinga watu wa Ualbino kuepukana na skin cancer ni very cheap na bahati nzuri yameanza kutengenezwa hapa katika PPP, kwa hiyo, suala ni kuhakikisha kwamba kuna utaratibu maalum wa MSD kuhakikisha inayanunua mafuta haya na Halmashauri zetu kuyasambaza mafuta haya. Hili likifanyika, ina maana rate ya skin cancer itakuwa imepungua sana na kwa maana hiyo, zile gharama za watu kwenda Ocean Road hazitopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lastly, of course nimeshawasiliana na baadhi ya watu, lakini kutokana na muda sitaweza sana, naomba tu tuwe tuna mawasiliano ya mara kwa mara ili kuona ni namna gani early cancer prevention treatment inaweza ikafanyika kwa kutumia gesi ya nitrogen ambayo kwa sasa inatumika hasa kwa upande wa wanyama. Ila technology inaonesha kwamba hii inaweza ikazuia sana skin cancer na wapo watu ambao wanafanya hivi, wanawatumia Madaktari wetu wa Kitanzania, suala ni kuangalia namna gani tuna- sustainable policy, ili wale wafadhili wakiondoka, basi wataalam wetu waendelee kulifanya hili kama ni jambo endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ulikuwa ni mchango wangu, naomba kuunga mkono hoja.

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema machache kuhusu bajeti ya Wizara inayohusika na Mawasiliano na Uchukuzi. Kuna mambo mawili hatuwezi tukakwepa na wala hatuwezi tukaingiza siasa inapokuja katika masuala ya mawasiliano ambayo ni sheria na teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumzia sheria nina maanisha Sheria za Kimataifa na Kitaifa na nianze kwa kusema kwamba Tanzania mwaka 1983 ilikuwa mwanachama wa WIPO (World Intellectual Property Organization) na kwa maana hiyo, ndio maana tuna sheria ambazo zinalinda haki za watu waliotoa ubunifu wa aina mbalimbali katika teknolojia, kwa lugha rahisi ni patents.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu tunakubali kwamba Tanzania haiwezi ikajifungia na tupo katika kisiwa kinachoitwa globalization, kwa hiyo, ni wajibu wa Tanzania kulinda patents za wabunifu mbalimbali wa Hitanzania na wa Kimataifa. Na ndio maana suala la kukataza matumizi ya simu fake sio utashi tu wa TCRA au sio siasa tu, ni wajibu wa kisheria za kwetu za ndani, lakini pia na za kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sisi sote, Wabunge tuna nia moja ya kuhakikisha kwamba tuna act kama viongozi kuhakikisha kwamba Taifa linakwenda katika mstari ulionyooka, basi ni rai yangu kwa Wabunge wote kuunga mkono suala hili. Na katika kusema hivyo niweke wazi kwamba maendeleo ya teknolojia sasa yamewafanya pia baadhi ya wajanja kuwa haraka zaidi kutumia teknolojia hiyo hiyo kuingiza simu fake, ndio maana kwa wale wanaofuatilia wanakumbuka mwaka 2014 Ujerumani zilikamatwa Samsung Galaxy, Uingereza pia hivyo hivyo, tena kule ulikamatwa mpaka mnara fake uliokuwa unaingilia mawasiliano ya watu. Mwaka jana tu pale China kabla ya IPhone, nafikiri, kutoa toleo lao jipya, China zilitoka mpya na watu wakaamini kwamba zile ndio zilikuwa ni sahihi, maana yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya yote tusiwe na ile dhana ya kudhani kwamba TCRA wanaweza wakaweka watu bandarini na airport kuzuia simu fake. Njia pekee ya kuzizuia ni njia ya matumizi ya teknolojia kama hivi wanavyotaka kufanya kwamba, kuzima simu fake, kuzidhibiti zisiweze kutumika. Na hii naamini inafanyika kwa manufaa ya wananchi wote kwa sababu, wananchi sasa watakuwa wana pata kitu halisi kulingana na fedha yao kwa sababu nina amini ni wizi kumuuzia mtu kitu cha shilingi 700,000 wakati ukweli ni kwamba ni cha shilingi 200,000 kwa sababu kilitengenezwa kwa low quality au kinaweza kikawa kwa quality isiwe low sana, lakini ukweli ni kwamba kime-infringe patent ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo naunga mkono hoja ya Waziri. Ahsante sana.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's