Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Antipas Zeno Mgungusi (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza naunga mkono hoja, lakini pili napenda nijikite kwenye hii hotuba ukurasa wa 46 ambao unazungumzia masuala ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa Serikali, hasa Wizara ya Maliasili, Waziri na wasaidizi wake kwa kuongeza idadi ya wageni kutoka 2015 mpaka sasa hivi 2021 idadi ambayo imetajwa pale sambamba na mapato yameongezeka kama ambavyo imetajwa kwenye hotuba kwa wale waliopitia, lakini pamoja na hayo niseme tu kwamba, hii dira ya Rais, maono yake ya kutaka kuongeza idadi ya wageni kutoka milioni moja na kitu mpaka milioni tano mwaka 2025 itafikiwa tu kama Wizara na wataalam wake wakitoa ushirikiano wa kutosha, lakini hasa kubadilisha mind set kwa maana ya kwamba, lazima tukubaliane utalii ni biashara. Kwa uzoefu tu wa kawaida kumekuwa na hali ya kwamba, uhifadhi umekuwa unashindana na utalii ndani ya Wizara na taasisi zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni kwamba, kunapokuwa na changamoto ya bajeti kwenye Wizara pamoja mashirika, lakini bajeti ya kwanza kuonewa ni ya utalii, lakini hasa ya masoko, kwa maana ya tourism promotion. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake na wengine kwenye mashirika waanze kubadilika kwa maana ya kuona utalii ni biashara, lakini pia utalii ndio unamlea uhifadhi. Shughuli zote za doria za magari, za mafuta, uniform za wapiganaji, posho na vitu vingine vinanunuliwa au vinalipwa kutokana na makusanyo yanayotokana na utalii. Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu waweze kutoa kipaumbele kwenye bajeti za utalii kuliko vinginevyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata Bodi yetu ya Utalii ambayo sasa ndio inayofanya masoko imekutana na changamoto ya bajeti kwa miaka mingi. Tumekuwa tunajitahidi inawekwa fedha nyingi, lakini fedha ambayo inatoka kwa utekelezaji inakuwa ni ndogo sana, hali ambayo inafanya tusiweze kushindana kama ambavyo inapaswa. Ukiangalia wenzetu nchi jirani ya Kenya, wengine wa Afrika Kusini na Wamoroko wanafanya vizuri zaidi kitakwimu, wanaingiza wageni wengi, lakini hawana vivutio vingi kama ambavyo sisi tunavyo Watanzania. Kwa hiyo, utalii ni biashara, lazima tukubali kwamba, utalii ndio unalea uhifadhi, ili uhifadhi ufanyike kwa kiwango tunachokipenda, basi tupate fedha kwanza kutoka kwenye utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niwashukuru wafanyabiashara kwa maana ya wakala wa utalii. Wao ndio wamekuwa wakileta wageni kwa zaidi ya asilimia 80 hapa nchini. Kwa hiyo, niombe tu Wizara iendelee kushirikiananao kwa ukaribu kujifunza kuona wenzetu wanachokifanya, ili wageni waweze kuja kwa wingi kufikia hili lengo la Rais la kufikisha wageni milioni tano mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kumekuwa na changamoto ya migogoro ya mipaka ya ardhi. Sisi kwetu Bonde la Kilombero tuna changamoto nzuri kidogo niseme kwa sababu, kuna hili suala la mradi wetu wa umeme wa Nyerere, Stiegler’s George. Ni mradi mkubwa wa kitaifa ambao sote tunaupenda na tunautakia heri, hatuko tayari kumuona mtu yeyote ambaye anaharibu, lakini sisi watu wa Bonde la Kilombero imeonekana tunatoa sehemu kubwa ya maji ya mradi ule, kwa hiyo, kwa maana yake ni kwamba, baadhi ya maeneo ambao tulikuwa tunalima muda mrefu na kufuga kwa sasa yanakwenda kuathirika. Suala la uhifadhi limekuwa serious sana na Serikali kwa hiyo, baadhi ya vitongoji vyetu vya Jimbo la Malinyi, Ulanga na Mlimba vitaenda kupotea kwa maana ya vinafutika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji kimoja cha Ngombo ambacho kipo Malinyi nacho kwa msimamo wa Serikali lazima kifutwe kwa sababu, inasemekana ndio chanzo cha maji mengi ambayo yanakwenda Stiegler’s. Pengine sisi hatuna pingamizi sana, niiombe Serikali, Waziri Mkuu yupo hapa na ndugu yangu Dkt. Ndumbaro, Waziri, yuko hapa tutatoa ushirikiano kadiri inavyotakiwa, lakini naomba tu tusaidike kwa maana ya Kijiji cha Ngombo kibaki, lakini kwa masharti ili tusiharibu uhifadhi. Kwa hiyo, tuko radhi kupunguza idadi ya mifugo. Serikali tutashirikiana nayo kupunguza hata matrekta na masuala mengine ambayo tunaona yanachangia kuharibu uhifadhi, ili mradi wetu huu mkubwa usikwame, lakini naomba Serikali itufikirie wananchi waweze kubaki kwa masharti ambayo watayatoa au ambayo tutaafikiana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, maeneo ya ziada ya kulima kwa Jimbo zima la Malinyi imekuwa ikitusumbua. Kuna mpaka wa mwaka 2012 uliwekwa, badaye kuna mpaka mwingine mpya 2017, yote hayo inasemekana hayapo kwenye GN, lakini niombe Serikali, hatubishani nao, lakini naomba tufikiriwe angalau mita 700 tu kutoka kwenye mpaka ule wa 2017 tuweze kupatiwa ili tuweze kuendeleza shughuli zetu za uchumi. Sasa hivi Malinyi imesimama, watu hawalimi, tunasubiri hatma ya mwisho ya Serikali kutuambia mustakabali wetu ukoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliambiwa kuna Mawaziri wanane wale watakuja kutoa hatima, lakini muda unazidi kwenda watu hawana cha kufanya, majibu yanatakiwa na mimi kama Mbunge majibu sina. Kwa hiyo, niwaombe Serikali basi itoe official statement tuweze kujua nini ni nini na nini kinachofuata, maana sasa hatujui hatima yetu. Kwa hiyo, nashukuru sana, naamini Wizara na Waziri Mkuu watashirikiana kuweza kutufikiria sisi watu wa Malinyi, Ulanga na Kilombero.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni suala la changamoto ya miundombinu ya barabara. Kwetu Malinyi kuna barabara kubwa ambayo tunaisubiria, maarufu kama Barabara ya Songea, lakini Kiserikali inaitwa Lupilo – Malinyi – Londo – Namtumbo, kilometa 296 ambayo itaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma kupitia Wilaya ya Malinyi na Namtumbo.

Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Serikali kiujumla kutufikiria hili jambo liweze kuanza kwa uharaka ili tuweze kutokea Songea na mikoa mingine. Jambo hili likifanyika itakuwa imetusaidia kukuza uchumi wa Malinyi na Ulanga Kilombero kama mbadala wa kilimo ambacho sasa inaelekea tunaenda kuacha kutokana na changamoto ya mpaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nitoe shukrani kwa Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, hasa kunisaidia wakati nimeumwa Novemba, Disemba. Nilipata huduma nzuri Ofisi ya Bunge ilinisaidia, lakini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Sokoine Morogoro, walinisaidia nilipata huduma nzuri kwa hiyo, nimesema nichukue wasaa huu kuwashukuru. Mwisho wazazi wangu Mzee Zeno Mgungusi na mke wake Theopista Nghwale na mke wangu Mariam Ali Mangara aka mama Moringe nawashukuru wote kwa kunipa ushirkiano.. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa nafasi. Nina masuala kama matatu; la kwanza ni sakata la KADCO na Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro; la pili, suala la TIC kwa maana kwenye Muswada wa Uwekezaji; na la mwisho, suala nguvu za Kamati zako za Bunge ambazo sisi tunazitumikia dhidi ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mtumishi mstaafu, nilibahatika kufanya kazi Wizara na Maliasili na Utalii. Kipindi changu nikiwa Wizarani nilishiriki katika shughuli za kufanya utafiti wa hali ya utalii nchini na bahati nzuri nilikuwa napangwa Kiwanja wa Ndege cha Kilimanjaro kwa miaka takribani mitano mfulululizo. Utafiti huo tulikuwa tunafanya watu wa Idara ya Utalii ya Wizara ya Maliasili, Commission ya Utalii ya Zanzibar, Idara ya Uhamiaji Tanzania pamoja na Benki Kuu.

Mheshimiwa Spika, kipindi chote sehemu yangu nilipangiwa Kilimanjaro ndipo nilipata kuufahamu ule uwanja na kuifahamu KADCO. Kwa bahati mbaya sikubahatika kipindi kile kuifahamu KADCO vizuri mpaka juzi baada ya kuisoma taarifa ya CAG na baada ya kualikwa kwenye Kamati ya PIC kuweza kusikiliza haya masuala yanakwendaje.

Mheshimiwa Spika, kimsingi KADCO kwa sasa ni kama kigenge au kibubu cha watu kufanyia maisha nje ya mfumo wa Serikali. Kinachonisikitisha sikuona kama Katibu Mkuu wa Wizara ile au watu wa Wizara kama wanaumwa na hali hii. Sinema zinazoendelea KADCO wao wako comfortable kabisa, wanapumua vizuri na wanaendelea kula vizuri kana kwamba hakuna kinachoendelea mpaka CAG, Wabunge na wadau ndio wanakuja kuona matatizo ya mle ndani, jambo ambalo linasikitisha sana.

Mheshimiwa Spika, katika ushirki wangu wa kikao, tunamhoji Katibu Mkuu na watu wake ambao walikuja jopo zima pale, Waraka wa Baraza la Mawaziri Na.5 wa mwaka 2009, ulitoa maelekezo kuwa tutanunua hisa zote za KADCO kutoka kwa wale wabia ambao walikuwa wajanja wajanja. Tutanunua kwa 100% baada ya kumaliza zile hisa, umiliki uende kwa TAA. Aidha, iendelee ku-operate kama kampuni tanzu ya TAA au KADCO ifariki kabisa uwanja uendeshwe direct na TAA kama wanavyofanya Kiwanja cha Dar es Salaam na viwanja vingine, lakini jambo hilo halikufanyika.

Mheshimiwa Spika, tunawauliza watu wa Wizara kwa nini hamjatekeleza maagizo haya? Wanajibu, Waheshimiwa mnajua tulikuwa na mchakato wa kutafuta mbia mpya wa kuendesha. Tukawaambia KADCO nani anawapa mamlaka ya kutafuta mbia, nadhani lilipaswa liwe ni jambo la Wizara na Mkuu wa masurufu (Accounting Officer) wa Wizara ni Katibu Mkuu pengine wangefanya wao. Hata hivyo wanasema kwamba huu mchakato tulikuwa tunafikiria kutafuta mtu. Hali ambayo inaonesha kabisa mashaka na kuna nia ovu ya wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuliwahoji, kama kuna mchakato wa kutafuta mtu mpya, sasa hivi ni miaka 12, maana ni mwaka 2010 ndio tulinunua hisa zote, hivyo kampuni imekuwa ya Serikali kwa 100%. Hadi leo tunazungumza mwaka 2022 ni miaka 12, mnachakata kwa miaka mingapi kumtafuta mtu wa kuendesha? Hawana majibu yaliyonyooka, wanaongea vitu ambavyo havieleweki. Nilitamani kumshawishi Mwenyekiti tuwafukuze kwenye kikao. Kwa hekima ya Mheshimiwa Hasunga, alisema tuwasikilize mpaka mwisho, tuone inakuwaje?

Mheshimiwa Spika, tukasema kama kweli huo mchakato ulikuwepo, mmetangaza wapi kwamba jamani tunatoa tangazo, tunatafuta mbia, tunatafuta mtu wa kuendesha Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, mna tangazo ambalo mmelitoa juu ya hili? Halipo. Katika mazingira yoyote inaonekana kabisa kuna nia ovu, hawa watu hawana nia nzuri na ni mchongo tu, wanataka watupige na waendelee kutupiga zaidi.

Mheshimiwa Spika, kituko kingine, wanajibu sasa hivi tuko kwenye mchakato wa ku-renew mkataba wa uendeshaji, ile concession agreement. Awali ile concession agreement ilikuwa baina ya wale wawekezaji na Serikali. Sasa hivi wawekezaji hawapo uwanja ni wetu tangu awali na KADCO imekuja kwetu kwa 100%, Mkataba Serikali inataka isaini na nani? Maana yake wanajadili Serikali kuingia makubaliano ya kuendesha uwanja na jini au hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna muda huwa nawaambia wenzangu tukiwa tunazungumza, muda mwingine Mungu akikusaidia ukiwa huna akili unaishi kwa amani sana, lakini ukiwa na akili utapata stress. Maana upeo wako ukiwa mfupi unaona kila kitu sawa tu, nyeupe na nyekundu ni sare, ndefu na fupi unaona ni sawa tu. Kwa hiyo wenzetu ambao hawana akili wanaishi sawa kuliko sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nakishangaa, kwa maana baada ya sisik kuinunua ile kwa 100% nilitarajia Katibu Mkuu wa Wizara ndiye Mkuu wa Masurufu na watu wake waiagize moja kwa moja KADCO iende TAA, maana, KADCO pamoja na kwamba tumeinunua haiwezi kujipeleka yenyewe na watendaji ambao wako pale wananufaika na KADCO, hawawezi kujipeleka na kusema tumekuja TAA. Ni Katibu Mkuu wa Wizara (KM) anatakiwa aiagize iende, lakini hafanyi hivyo, hakufanya hivyo na anapumua na ana amani tele kabisa, ni kituko. Kwa hiyo, mambo haya yanakera na ni mambo ya wazi kabisa, inaonesha kuna nia ovu, kitu ambacho sisi sote hatukukubaliana.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, kwa hekima za Mheshimiwa Hasunga ambaye alikuwa anakaimu Uenyekiti katika kile kikao alisema, Waheshimiwa hebu tuwape muda kidogo, maana wenyewe waliomba walisema, tunahitaji muda tukajadiliane tutaleta majibu. Tukasema kwa nini mlete majibu mkishajadiliana, mnajadiliana na nani? Katibu Mkuu wa Wizara tuko naye hapo mbele, Mwenyekiti wa Bodi na Bodi yake ya KADCO yuko pale, Mkurugenzi wa KADCO yuko pale, Mwanasheria wa KADCO yuko pale, timu nzima ambayo wanayojua hili sakata wako pale. Pembeni mnaenda kujadiliana na nani ili mtuletee majibu baada ya wiki moja? Ni vitu ambavyo havieleweki. Bahati nzuri kwa hekima za Mwenyekiti, Mheshimiwa Hasunga alisema tuwavumilie kwa wiki moja, Ijumaa inayofuata watuletee majibu. Akasema pia Mheshimiwa Mgungusi tutakualika tena, uje ushiriki na hicho usione kwamba leo tunakwepesha. Hata hivyo, mpaka kesho, mpaka mwakani, hawakuleta majibu.

Mheshimiwa Spika, hapa kuna picha mbili, nia ovu ya moja kwa moja, kwamba wanapiga mchongo, lakini pia ni dharau kwa Kamati yako ya Bunge. Kwa hiyo, pamoja na mambo hayo yote, nashauri kwenye sakata hili tuagize ukaguzi maalum ukafanyike kuhusu KADCO kuanzia mwaka 2010 tangu tumenunua hisa kwa 100%.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kirefu KADCO hawakuwa na Mwanasheria. Kituko kingine wana-hire huduma mtaani kwa maana wana Mwanasheria wao private mtaani na wanalipa. Ukiangalia zile legal services za kila mwezi unaweza ukazimia, bora usijue. Kwa hiyo, siwezi nikasema mengi, naomba tukubaliane ukaguzi maalum ukafanyike kule KADCO, wanaweza wakaona vituko vya hatari.

Mheshimiwa Spika, kingine niseme tu, kama ikiwapendeza, naomba Katibu Mkuu wa Wizara ajitafakari kwa maana ya sehemu ya Uchukuzi, Mwenyekiti wa Bodi ya KADCO ajitafakari, maana ni nje ya mamlaka yangu, lakini nashauri tu wajitafakari, Mkurugenzi wa KADCO na safu yake, Menejimenti nzima ijitafakari. Kwa suala la KADCO naomba niishie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kwenye Muswada wa Uwekezaji. Suala la TIC- Kituo cha Uwekezaji Tanzania. Kwenye ule Muswada ambao tulipitia Wizara ya Viwanda na Biashara katika kipengele cha Board Members, Wajumbe wa Bodi ya TIC tulipendekeza kuwepo na Wizara ya Mambo ya Nje kama moja ya member wa ile Bodi ya TIC. Kwa sasa kuna Wizara zimetajwa, Wizara ya Fedha ipo, Wizara ya Ardhi, TAMISEMI ipo lakini Wizara ya Mambo ya Nje haipo kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya TIC. Kwa hiyo, sisi tulipendekeza, lakini sasa Serikali nadhani hawakuichukua hii, wakaacha kama ilivyokuwa awali.

Mheshimiwa Spika, naona haja ya Wizara ya Mambo ya Nje kuwepo TIC kwa sababu gani? Tunapozunguzma Uwekezaji mkubwa leo Foreign direct investment zinatoka nje, makampuni makubwa yanatoka nje na leo hii mnajua sera yetu sisi ya kimataifa ni diplomasia ya uchumi. Tunawataka Mabalozi wapambane kuacha siasa bali watafute wawekezaji kuja Tanzania. Wawekezaji wanakuja na mitaji yao au pengine wanakopa lakini wanaingia hapa nchini, wangependa kuona mwenyeji wao yupo kwenye huduma zao. Mwenyeji wao ni Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Mabalozi. Inawezekanaje katika Bodi ya Wakurugenzi ya TIC hakuna mtu wa Wizara ya Mambo ya Nje, lakini kuna TAMISEMi? Nawaza sijui kwa nini kuna TAMISEMI au kwa sababu ya ardhi, wanamiliki maeneo, lakini Wizara ya Ardhi ipo!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tulipendekeza aidha, iongezeke Wizara ya Mambo ya Nje kwenye Bodi au apunguzwe mmoja, apunguzwe hata TAMISEMI, Wizara ya Ardhi anamwakilisha, lakini hakuna sababu ya msingi ya kufanya Foreign Affairs asiwepo kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya TIC, maana hata wawekezaji wanapoona wanalalamika au hawahudumiwi vizuri mwenyeji wao yupo wanabanana naye pale inapendeza, kuliko mtu wa Mambo ya Nje akienda kulalamikiwa na wawekezaji wake ambao amewaleta na yeye aanze kuuliza pembeni hai-make sense kwa hali ya kawaida. Hivyo, napenda kushawishi Bunge kama litakubaliana Wizara ya Mambo ya Nje iongezwe kwenye Bodi ya Wakurugenzi pamoja na ile Kamati ya Kitaifa ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ni suala la nguvu za Kamati zako za Bunge ambazo tunazihudumia dhidi ya watendaji wa Serikali. Nimekuwa na uzoefu mdogo tangu nimekuwa nikifanya kazi za Kamati miaka hii miwili ya Ubunge, watendaji wa Serikali mara nyingi hawako serious. Wanakuja kwenye Kamati tunakaa nao, unaona kabisa hawako serious. Kuna watu ni Maprofesa na elimu kubwa lakini wengi unakuta hawa-own taarifa ambazo zinazokuja. Tunauliza maswali ya kawaida kabisa very obvious, hawawezi kusema mpaka unabaki unashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatoa maelekezo kwa mfano Bunge la Bajeti, tunawaambia Bunge lijalo mje na taarifa fulani, fulani wanaitikia ndio Waheshimiwa. Session inayokuja mnakutana hawaleti, yaani kama wametuzoea au wanatuweza hivi. Muda mwingine watendaji wanaambiana kwamba wewe peleka tu taarifa hata zikiwa kubwa, Waheshimiwa Wabunge huwa hawasomi. Waambie tu Mheshimiwa, Mheshimiwa huwa hawasomi. Sasa bahati mbaya wanakosea njia, siku hizi watu wanasoma sana na hata kukesha inapolazimu watu tunakesha, we read between lines, hata wakileta vitabu vikubwa tunasoma na tunafuatilia.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa Wabunge wenzangu ambao ni Mawaziri na Naibu Mawaziri, sisi ni wenzenu. Tupo kuwasaidieni kuhakikisha kwamba tunasaidia hii nchi na inakwenda mbele, there is nothing personal. Mara nyingi utakuta Mawaziri au Naibu Waziri, hawatumii muda mwingi kubanana na watendaji wao. Sijui wanazoeana? Baadaye unakuta Kaibu Mkuu anamwingiza chaka, Waziri anakuja kukaangwa kwa ajili ya mambo ya watendaji wake. Naibu Waziri anakaangwa kwa ajili ya Mkurugenzi fulani aliye chini ya Taasisi zao, kwa nini? Wasiwachekee, sisi tukija kwenye Kamati tunakaza, wakitulaumu sawa, mahusiano yetu ya urafiki yakivunjika sawa, lakini you need to be serious kuwasimamia watendaji.

Mheshimiwa Spika, naomba uwatie moyo Wabunge wako kwenye Kamati kwamba waendelee kufanya kazi seriously. Mtu anashindwa kujibu halafu baadaye wanaongea pembeni kwamba hili suala ni zito sana, msilijadili sana maana huwezi kujua kwa nini halitatuliwi kwa miezi yote halitatuliwi, kutakuwa kuna kit utu. Wanataka kama kuanza kutishatisha watu, lionekane jambo sijui ni la nani? Halipo. kinachokuja kwenye Kamati tunajadili na tunakaza na watalifanyia kazi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa leo nashukuru sana, lakini nasisitiza Katibu Mkuu wa Uchukuzi na timu yake wajitafakari. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Awali ya yote, naomba uniruhusu niweze kutoa shukrani kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya TAMISEMI ingawa siyo Wizara hii, lakini waliweza ku-attend dharura ya Malinyi ya mafuriko ya maji yaliyoathiri barabara zetu. Fedha zimetolewa, sasa wakandarasi wapo site wanatatua tatizo Wanamalinyi watakuwa na amani hawataathirika tena na masuala ya mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hii nina mambo mawili au matat. La kwanza, Jimbo langu la Malinyi lina changamoto ya mawasiliano, sehemu kubwa ya jimbo huwezi kupatikana, karibia asilimia thelathini au arobaini ya Jimbo ndiyo wanapatikana hewani, lakini zaidi ya asilimia sitini, sabini hakuna mtandao voice na data ndiyo kabisa ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi ninavyozungumza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi hazipatikani kwa maana huwezi kumpata mtu hewani akiwa kwenye Ofisi hizo mpaka jioni wakirudi mtaani ndiyo unaweza wakapatikana. Kwa hiyo, naona Wizara inanisikiliza naomba walichukulie hili jambo kwa udharura watu Malinyi waweze kusaidika tuweze kupata mawasiliano kama maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia changamoto ya cyber-crimes kwa maana ya wizi wa mtandao umeendelea kuwepo. Mnakumbuka tulifanya usajili wa line kwa njia ya vidole ili kuweza kudhibiti changamoto hii, lakini mpaka leo hii bado watu wanafanya utapeli na namba ambazo zinatumika kufanya utapeli bado zinapatikana hewani mpaka hivi ambavyo ninazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi ni muhanga wa jambo hili, watu wame-forge akaunti kwenye mitandao ya facebook wanawatapeli watu kuna masuala ya ajira mtume nauli na kadhalika ili ufanyiwe mipango, namba ambazo zinatolewa watu wanapiga bado zipo hewani na watu wanaendelea kutapeliwa fedha. Nimefanya majaribio kadhaa rasmi kwa maana ya kuripoti Polisi miaka miwili iliyopita, tumeandika barua, nimepewa RB naambiwa watu wa cyber wanafuatilia lakini mpaka leo wanaendelea kutapeliwa na tunachafuliwa heshima zetu. Sasa mimi ni
kiongozi nina access ya kusema, sijui watu wangapi kwenye nchi hii wanakumbana na adha ya namna hii na hawezi kusema. Kwa hiyo, naomba Wizara ilichukulie jambo hili serious.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ni suala la mawasiliano ya simu katika vivutio vya utalii kwenye National Parks, Game Reserve na maeneo mengine. Kwa mfano, Hifadhi kama ya Mlima Kilimanjaro tuna watalii wengi wanapanda lakini asilimia 90 ya mlima ule mawasiliano hakuna. Watangazaji wazuri wa utalii ni watalii wenyewe, watalii wa ndani na watalii wa nje, watu wanapanda milima wanapenda ku-share experience yao moja kwa moja, watume picha kwenye mitandao, wafanye live video calls kuwahamasisha wengine lakini jambo hili haliwezekani kwa maana ya kwamba network hakuna kabisa mlimani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe tu Mheshimiwa Waziri alichukue hili washirikiane na Wizara ambayo ni mlaji ya Maliasili wahakikishe Mlima Kilimanjaro ambacho ni kivutio chetu kikubwa mawasiliano yawepo muda wote hasa ya data. Jambo hili linaendelea hata kwenye hifadhi zingine Ruaha, Ngorongoro maeneo mengine ya misitu yote yana changamoto kubwa za network. Kwa hiyo, naomba suala hili lichukuliwe kwa uzito kusaidia watalii kui-enjoy na kuwashawishi wenzao kwa kuona kwenye mitandao uzuri wa vivutio vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo changamoto pia ya doria, askari wetu ambao wapo porini wanafanya doria kulinda maliasili za nchi yetu, wanakutana na changamoto kubwa ya mawasiliano. Siyo mara zote radio call zinafanya kazi vizuri lakini mawasiliano ya simu yanaweza kuwa rahisi kuhakikisha watu waliopo kule porini wanafanya kazi vizuri, wanatoa taarifa kwa wakati, muda mwingine ni rahisi hata ku-track majangili, mambo ya kuviziana ni ya kizamani sana lakini technology ndiyo inafanya kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Wizara inanisikia walichukue jambo hili, hata majangili ambao wapo porini wanapanga mipango unaweza ukawa-track kupitia technology. Maeneo makubwa ambayo yanaathari ya ujangili hayapatikani kwa simu tunatumia tu radio call. Kwa hiyo, naomba Serikali ilichukue suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo mchango wangu ni huu, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Awali ya yote nakupongeza wewe kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti, lakini pia umetosha kwenye kiti kana kwamba ni mzoefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nitoe shukrani kwa Wizara ya Maliasili. Pamoja na changamoto nyingi za Bonde la Kilombero, nimekuwa tukipishana nao mara nyingi tunagombana, lakini walau kwa kidogo tunashukuru kwamba wametoa idhini wananchi wetu waliolima kule waweze kuvuna kipindi hiki ambapo mpunga upo tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo, niseme tu, natoa pongezi kwa Watendaji wa Jeshi USU la Uhifadhi, Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro Daktari Manongi; Kamishna wa TFS, Profesa Silayo Dos Santos, Kamishna Kijazi wa TANAPA, ambaye kwa sasa amepanda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara. Nawapongeza kwa utendaji mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote kwa yote, niseme utalii nchi hii unakumbana na changamoto kubwa mbili; ya kwanza, ni utegemezi wa aina moja ya utalii kwa maana ya utalii wa wanyamapori ndiyo sehemu ambayo tumelalia sana. Changamoto ya pili ni utangazaji wa utalii usiotosheleza. Kipande hicho hicho cha utangazaji wa utalii na chenyewe kina changamoto mbili; ya kwanza ni ufinyu wa bajeti; na ya pili ni ubunifu usiotosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika suala la kutegemea utalii wa aina moja, zaidi ya asilimia 80 au 90 ya watalii wanaokuja Tanzania wanaenda kwenye Hifadhi ya Taifa, kwenye Mapori ya Akiba na maeneo mengine mbalimbali ambayo tumejaliwa kuwa nayo. Ila ukiangalia takwimu za nchi ambazo zinafanya vizuri duniani na Afrika kiutalii kwenye kumi bora zote za Afrika, zimetajwa hapa asubuhi; Morocco, South Africa na maeneo mengine hawana vivutio vingi kwa maana ya wanyamapori, hawana hifadhi nyingi nzuri kama za kwetu, lakini wanafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili linatakiwa liifikirishe Wizara, Serikali na nchi kwa maana tunakoelekea utalii wa wanyamapori unaweza ukapotea na utalii mwingine mbadala ndiyo ambao unashika hatamu. Kwa hiyo, naomba Wizara ichukue hili kama changamoto. Tuna vivutio vya asili; ukiangalia beach ya Lake Tanganyika, kule Kirando na Kipili Nkasi, ukiangalia tuna kimondo pale Mbozi, Olduvai Gorge kule Ngorongoro na maeneo mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii wa kitamaduni ni vitu ambavyo vinapendwa sana na watalii wengi. Kwa hiyo, naishauri Serikali tujikite kwenye maeneo hayo. pamoja na kwamba tunafanya utalii wa wanyamapori, lakini utalii mbadala hasa wa kitamaduni uweze kuzingatiwa na kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya utangazaji wa utalii, nilizungumza suala la kibajeti, ni kweli bajeti yetu ni finyu, Bodi ya Utalii ambayo ina dhamana ya kufanya matangazo, imekuwa ikitoa fedha ambazo siyo toshelezi kulinganisha na nchi shindani, lakini hata hicho hicho kidogo hatufanyi ubunifu kuweza kukitumia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu hata tufanye vyovyote vile hatuwezi kuwa na fedha nyingi kama nchi nyingine ambazo zimetajwa saa zile, lakini ubunifu ndiyo kila kitu. Nitolee mfano, kufanya matangazo ya utalii kwenye Media kubwa kama CNN kwa dakika moja haipungui milioni 200, 300 na kuendelea. Ukweli ni kwamba tunaweza tusimudu sana, lakini ubunifu ni kwamba television zote kubwa; CNN na Aljazeera na wengine wana vipindi vya Makala kwa maana ya documentaries, wanaonyesha uhaba wa maji Afrika, Sudan, Tanzania na kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kufanya lobbying tukatumia documentaries, tukawaalika wakafanya kama documentary kuonesha vivutio vyetu, sisi tunakuwa tumepitia humo humo, tukaonwa na dunia nzima kwa bei rahisi ambayo pengine inaweza ikawa bure kabisa kuliko kutegemea kujaza bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bajeti ndogo ambayo imekuwa ikitolewa kwa ajili ya Bodi ya Utalii, maisha yangu yote ambayo nimekuwa Wizarani haikuwahi kutolewa hata kwa asilimia 90. Bajeti inatengwa, lakini fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya utekelezaji kazi ni ndogo mno. Kwa hiyo, katika hali hii hatuwezi kushindana na mataifa mengine ambayo yametutangulia Afrika na dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuongezea kwenye ubunifu, nilikuwa naishauri Serikali, jambo hili Wizara ya Maliasili isaidiwe na Serikali kiujumla, kwa maana kwenye balozi zetu; watalii wengi tunawategemea wanatoka kwenye mataifa ya nje, tunawaagiza mara kadhaa mabalozi wafanye kazi kuleta watalii Tanzania, lakini unaweza ukakuta wenyewe hawana uelewa mkubwa juu ya suala la utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nishauri Wizara ya Maliasili na Mambo ya Nje wakashirikiana, tuwapeleke waambata wa utalii kwenye balozi zetu. Kuna waambata wa jeshi, kuna waambata wa idara, wapo kwenye balozi. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Mambo ya Nje na Maliasili zishirikiane tuwaweke Maafisa Utalii kwenye balozi zetu waweze kuwasaidia mabalozi kuweza kutangaza nchi yetu. Kinyume na hapo, tutaishia kuwalaumu mabalozi tu, lakini kazi haitaonekana kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikihama kwenye eneo hilo, kuna suala la vita dhidi ya ujangili. Mara nyingi kumekuwa na malalamiko na Jeshi USU la Hifadhi kutokana na kutotosheleza kwa manpower, kwa maana wapiganaji ni wachache. Mara kadhaa TANAPA, Ngorongoro, TFS na TAWA wamekuwa wakilalamika pengine na kuhitaji nguvu kazi kwa ajili ya ziada. Niseme, jambo hili tuli-support lakini ushirikiano uwe mkubwa kwa Serikali kiujumla wake. Tukimwachia Maliasili peke yake hataweza kulingana na manpower aliyonayo. Kwa hiyo, naomba tu, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Maliasili kuunganishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, wafanye ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vijana wanamaliza JKT, wanakaa kwenye makambi yetu, wanajitolewa miaka miwili kumwagilia maua, kupanda bustani; wamekuwa trained, wale ni askari, wachukuliwe, wapate short course kidogo ya uhifadhi, waripoti kwenye Jeshi USU la Uhifadhi, wakisimamiwa na Maafisa wa kule waweze kufanya operation ambazo zinapaswa hizo za kisheria. Kinyume chake tutalia suala la kuongeza askari, inaweza ikachukua miaka mingi tusiweze kumudu kupata idadi toshelezi, wakati tayari tuna nguvu kazi ya JKT au Jeshi la Wananchi Wapiganaji ambao wapo tu sasa hivi ambao ni ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hili jambo lisiachiwe Wizara ya Maliasili peke yake, askari wengine watumike, wapate course ya muda mfupi. Kule watalipwa tu posho kwenye paramilitary ile ya conservation, mishahara yao itaendelea kwenye majeshi yao ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano kwenye suala la TFS kwa maana Wakala wa Huduma ya Misitu, wamekutana na changamoto kubwa za kihifadhi. Doria zimekuwa ngumu, changamoto ni kubwa, askari wanalemewa hasa kwenye misitu yetu ambayo ipo karibu na mipaka. Kule Kigoma Misitu ya Makere Kusini na Kaskazini, majangili wamekuwa wakiingia kufanya uvunaji haramu wa misitu, TFS wanalemewa. Mara kadhaa kumekuwa na incidents wapiganaji wanazidiwa, wengine wanauliwa, mambo kama haya huwa hatutangazi, huwa hayasemwi, lakini yapo. Kwa hiyo, kuna haja ya Jeshi la wananchi au JKT kuongeza nguvu kwa TFS na Jeshi la Uhifadhi kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuna suala la muundo mzima wa conservation paramilitary, Jeshi USU la Uhifadhi. Sasa kwa sababu masuala mengi ni ya kijeshi, siwezi kuyasema hapa, lakini nimeandika kitabu changu cha Maisha Yangu ya Uaskari kama Afisa wa Jeshi USU, humu kuna madini mengi. Naomba Wizara wakichukue, watapata vitu vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwa upendeleo, Jeshi la Uhifadhi kwa sasa lina-operate differently kwa maana ya kila…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)