Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Primary Question

MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, lini Serikali itapandisha hadhi barabara ya Kwinji - Kilindi Asilia hadi Kimbe?

Supplementary Question 1

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri tu. Nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sababu barabara hii inaunganisha Kata tatu. Kata ya Msanja, Kata ya Kilindi Asilia na Kata ya Kimbe, ni Kata ambazo zina uzalishaji mkubwa sana wa mahindi na kipindi cha mvua inakuwa ni shughuli kubwa magari kupita. Sasa kwa sababu suala hili liko Serikalini; Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuelekeza Mkoa sasa kufanya tathmini hiyo na iweze kupandishwa hadhi barabara hiyo?

Swali la pili ni kwamba barabara hii ina madaraja mengi na ina vivuko vingi sana na kipindi cha mvua haipitiki. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kutoa maelekezo kwa TARURA ili maeneo haya yaweze kurekebishwa na Wananchi wa Wilaya ya Kilindi waweze kupata huduma ya Serikali? Ahsante. (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kigua, swali la kwanza kuhusu kuelekeza mkoa; kama nilivyokuwa nimesema kwenye majibu yangu ya msingi kwamba, taratibu za kupandisha au kuteremsha barabara kuwa ya Mkoa ni taratibu za kisheria. Hivyo basi, ningeshauri Mkoa wa Tanga waanze kuchukua hatua stahiki za kupandisha barabara hii kwa kukaa Mheshimiwa Kigua kule Kilindi kupitisha kwenye DCC yao na ikitoka DCC iweze kwend RCC na baadaye kwenda kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa, kisha waweze kuandika kwa Waziri mwenye dhamana ya barabara ambaye ni Waziri wa Ujenzi ili na yeye aweze kutuma timu ya kufanya tathmini ili barabara hii iweze kupandishwa kuwa ya Mkoa. Nitakaa na Mheshimiwa Kigua tuone tunafanya vipi na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi ili barabara hii iweze kuanza huu mchakato wa kupandishwa.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la madaraja na vivuko ambavyo vinahitajika sana. Ni kweli nikiri kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa uzalishaji na wananchi wa kule Kilindi kwa ajili ya kutoa bidhaa zao mashambani Mheshimiwa Mbunge amekuwa akilifuatilia sana, tutakaa naye vilevile kuona ni namna gani tutapata fedha kwenye bajeti ya TARURA hii inayokuja 2023/2024 ili kuweza kutengeneza vivuko zaidi kwa sababu tayari katika mwaka huu pekee wa fedha tunaoumaliza tulitengeneza boksi Kalavati 15, drift ndefu yenye mita 15 lakini imechongwa vilevile kilometa 21 kwenye barabara hii, lakini kwa sababu ina urefu wa kilometa 47 tutakaa tuone ni namna gani tunaendelea kutengeneza maeneo hayo yaliyosalia. (Makofi)