Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: - Je, nini hatma ya madai ya maslahi ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero?

Supplementary Question 1

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, madai ya watumishi wa kilichokuwa Kiwanda cha Sukari Kilombero na process nzima ya ubinafsishaji limebaki kuwa kovu kwenye kidonda kwa wananchi hawa.

Swali langu kwa Serikali; kuna mkataba wa hiari kati ya watumishi hawa na kilichokuwa Kiwanda cha Sukari Kilombero ambao haujatekelezwa mpaka sasa; je, nini hatua za Serikali katika utekelezaji wa hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna kauli ya Serikali ambayo ilitolewa na Waziri Kusila pamoja na Waziri Kimiti walipokutana na watumishi hawa mwaka 2000.

Nini utekelezaji wake ili kutibu majeraha ambayo yametokana na ubinafsishaji wa kiwanda hiki cha sukari?

SPIKA: Mheshimiwa Londo, hilo la pili Mheshimiwa Naibu Waziri anajua kweli ama unazo hizo taarifa hapa?

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, suala hili lipo katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

SPIKA: Hilo ni la nyongeza.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, ni la nyongeza, ndiyo.

SPIKA: Ndiyo, sasa ili yeye aweze kuwa na majibu lazima ajue hao wawili uliowataja walisema nini, ndiyo nauliza Mheshimiwa Waziri hizo taarifa za walichosema anazo? Maana swali lako ni la msingi, lakini sasa nataka kujua yeye anayo? Maana asije akatupa majibu ambayo wale hawakusema.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuwapatia mshahara wa miezi kumi kati ya 40 ambayo ilikuwa ni kifuta jasho kwa watumishi hawa. Sasa utekelezaji mpaka leo hawajatekeleza, nini kauli ya Serikali.

SPIKA: Ahaa, kwa hiyo hicho ndicho walischosema hao wawili?

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kuhusiana na mkataba wa hiari aliousema, unaitwa mkataba wa hali bora kwa mujibu wa sheria. Katika mkataba huu wa hiari, bado ni sawa na mikataba mingine kwa mujibu wa Sheria yetu ya Mikataba Cap. 345, na kama kutakuwa kuna utekelezaji ambao haukufanyika, hilo ni eneo la kwenda kufuatilia na kuweza kushughulikia.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, mtakumbuka kwamba katika kesi hii ilikuwa ni suala ambalo lilihitaji majadiliano katika upande wa wafanyakazi, Chama cha Waajiri, lakini pia uongozi wa kiwanda wakati wanabinafsisha kiwanda hicho. Na katika kipindi hicho mbali na yale ambayo yalizungumzwa kama utatuzi ya mgogoro, kulikuwa kuna mashauri ambayo yalikwenda mahakamani, sasa katika mashauri yaliyokwenda mahakamani kuna uamuzi wa mahakama ambao ulifanyika, kama malipo yatakuwa hayajafanyika, utaratibu wa kisheria ni kufanya execution of decree. Kwa hiyo enforcement of the execution of decree kama haikufanyika, nitawasiliana na Mheshimiwa Mbunge tuweze kuona, kwa sababu mahakama ilifanya maamuzi mahususi, niwasiliane naye, na kama kesi hiyo itakuwa kubwa kwa kiwango chake tutaona namna ya kwenda kushirikiana na kukutana na wafanyakazi hao ili haki yao iweze kupatikana kwa mujibu wa sheria na maamuzi ya mahakama, ahsante.