Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: - Je, ni nyumba ngapi zinahitajika kwa Watumishi wa Umma waliopo Vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa ukosefu wa nyumba unasababisha walimu na hao wafanyakazi wa Serikali kuchelewa, lakini katika vijiji vingine kuna nyumba za wananchi ambazo hawaishi huwa wanakuja tu wakati wa sikukuu ikiwemo Christmas. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuziagiza Halmashauri ziingie mkataba na hawa watu wenye ma–bungalow huko vijijini ili waweze kupatia wafanyakazi nyumba za kuishi?

Swali la pili, upungufu ulioandikwa ni mkubwa sana, hata tungejenga kwa miaka 10 bado hatutatosheleza. Serikali inasema nini sasa kuongeza hela zaidi katika mfuko huo wa ujenzi ili hii kazi iende kwa uhakika? (Makofi)

Name

Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shally Raymond.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza kuhusu Serikali ina mpango gani kuingia mkataba. Hili ni jukumu ambalo linaachiwa Halmashauri wenyewe kuweza kuingia mikataba na wenye nyumba ambazo hazitumiki na naamini hili Mheshimiwa Mbunge amelileta kwa sababu kule Mkoa wa Kilimanjaro wengi wanakuwa wapo katika Mikoa mingine na wanarudi kipindi cha mwisho wa mwaka. Kwa hiyo, tutakaa na kuona ni namna gani tunaweza tukazungumza na Halmashauri ambazo zina mazingira kama ya Mkoa wa Kilimanjaro, kuona ni namna gani wanaweza kuingia mikataba hii kwa ajili ya kuweza kuwaweka watumishi wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la hela ya ujenzi. Ni wajibu wa Halmashauri kuanza kuweka fedha, kutenga fedha katika mapato yao ya ndani kwa ajili aya ujenzi wa nyumba za watumishi wa kada ya elimu na afya. Serikali Kuu tayari imeshachukua jukumu kubwa sana, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepeleka fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa maboma, madarasa katika Halmashauri hizo na ukamilishaji wa maboma lakini vilevile katika afya ameshapeleka fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na vituo vya afya.

Kwa hiyo, ni wajibu wao sasa kuanza kuunga mkono jitihada zile za Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga na kukamilisha maboma yaliyojengwa na wananchi kwa ajili ya nyumba za watumishi wa umma. (Makofi)