Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza:- Je, ni kwa namna gani Serikali inalinda afya ya mama mjamzito na mtoto mchanga?

Supplementary Question 1

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini majibu haya ni tamko la sera, ni miongozo ya Serikali, lakini bado huko vijijini akina mama wajawazito wanaendelea kuagizwa kwenda na vifaa vya kujifungulia.

Je, Serikali inatoa tamko gani, kwamba hawa akina mama watakapokosa huduma hizi wachukue hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali imeimarisha huduma na wanawake walio wengi vijijini wanapata hizo huduma.

Je, Serikali ipo tayari sasa kutuletea sheria (kwa sababu haya yote ni matamko na miongozo) Bungeni kwa ajili ya kusimamia huduma hizi za mama na mtoto ziweze kutolewa bure? (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake hili zuri ambao ni ukweli unaogusa maisha ya akina mama wetu kila siku. Swali lake la kwanza kuhusu je, wanapokosa huduma tunafanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwaambie tu kwamba, sheria hiyo ipo. Nitoe tamko kwamba suala la akina mama kupata huduma, mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano ni bure. Pia ni ukweli kwamba kile kipindi ambacho tulikuwa tunapitia kwenye upungufu wa vifaa tiba, pamekuwa pakitokea changamoto hizi ambazo amezisema hapa Mheshimiwa Mbunge. Kama ambavyo nimeeleza kwenye swali la kwanza linalohusu upatikanaji wa vifaa tiba na dawa kutoka kwa Mheshimiwa Halamga, tukiweza kusimamia yale ambayo nimeyasema hapa, nataka kuwahakikishia kwamba suala la akina mama kununua vifaa na vitu vingine havitawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba tu Waheshimiwa Wabunge, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wote kwa pamoja tushikamane kuhakikisha kwenye Kamati zetu za Ulinzi na Usalama, suala la upatikanaji wa dawa na huduma za afya liwe ni ajenda ya kudumu ili tuijadili. Kwa sababu kwa kweli ikikosekana dawa, huduma zikiwa mbaya, watu watakufa. Kwa hiyo, pia ni suala la kiusalama, wote tulijadili kila wakati na kuhakikisha tunalisimamia kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la kwamba tutunge sheria ya kusimamia hili la akina mama kupata huduma, naomba nilichukue tukalitafakari tuone namna ya kufanya, lakini ninaamini Mheshimiwa Mbunge tukikubaliana pamoja sisi Wabunge na Watanzania wote, tukaja na Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, tunakuwa tumepata mwarobaini wa suala hilo. Maana yake kila mama atakapokuwa na bima yake ya afya, kila familia itakapokuwa na bima yake ya afya, basi matatizo haya mengine yatakuwa yameisha, ahsante.