Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: - Je, lini Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro itakuwa Jiji?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Licha ya majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kufuatana na swali la msingi, nilikuwa natanguliza tu, maombi yatakuja, tayari tumeshaongelea, kwa hiyo, yatakuja. Yakija naomba mtufikire.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza. Manispaa yetu ya Morogoro ina kata 29 lakini ina tarafa moja. Kata zake ni kubwa sana: Je, Serikali haioni kuwa inaweza angalau ikatupatia tarafa ya pili kusudi kuwe na tarafa mbili kwa sababu kata ni nyingi sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Kwa sababu mkazo wa Serikali sasa hivi ni kuimarisha miundombinu pamoja na huduma za jamii; miundombinu ya Manispaa ya Morogoro bado siyo mizuri hasa kwa upande wa Barabara: Je, ni lini Serikali itaweza kuwapa fedha na kuwaongezea kusudi barabara zetu za Manispaa ya Morogoro ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuongezwa tarafa ya pili. Naomba kumshauri Mheshimiwa Mbunge na pia kuishauri Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kufanya vikao kwa ajili ya maombi hayo kama ambavyo amesema juu ya maombi ya kuwa Halmashauri ya Jiji. Utaratibu uko wazi. Kikao cha kwanza ni cha Bodi ya Ushauri ya Wilaya (DCC), baada ya hapo maamuzi yenu yanapelekwa katika kikao cha Mkoa, yaani Bodi ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na baada ya hapo tunakwenda kumwasilishia Mheshimiwa Waziri ili sasa maamuzi ya kugawa Halmashauri yenu au Manispaa yenu ili mweze kupata tarafa ya pili na taratibu nyingine kwa ajili ya kuwa jiji ziweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, hilo ni jibu kwa swali la kwanza. Swali la pili, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali kupitia TARURA imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inaimarisha miundombinu katika majiji yetu, Manispaa zetu na Halmashauri zetu zote zilizopo ndani ya nchi yetu. Hivyo nataka nimhakikishie tena Mheshimiwa Mbunge kupitia Halmashauri yake, watengeneze bajeti yao, watengeneze vipaumbele vyao, watuletee Ofisi ya Rais, TAMISEMI na tutakwenda kufanyia kazi.