Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:- Je, kuna mpango gani wa kuchukua hatua kwa Watumishi wanaoripoti na kuondoka bila kufanya kazi Wilayani Tunduru?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa kutokana na Waraka huo wa Serikali sina uhakika sana kama unazingatiwa kwa Wilaya ya Tunduru, kutokana na mwaka jana tulipata Walimu wa Shule za Msingi 56 na waliohama ni 57. Je, Serikali ina mpango gani wa kutufidia wale waliohama?

Swali la pili, je, Serikali haioni haja ya kutoa Waraka maalum kwa ajili ya Tunduru pekee kwa kuwa wale wote wanaohama labda inawezekana kutokana na mazingira waliotokea na wanayokwenda kuyakuta hawakubaliani nayo.

Je, Serikali haioni haja ya kutuletea ama kuajiri waajiriwa ambao wanaotokana na maeneo yale ili waendelee kubaki pale na kupunguza kero hiyo ya kuomba kuhama? Ahsante.(Makofi)

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu kilio cha wananchi wa Tunduru kilishafikishwa katika Ofisi zetu mbili zote ikiwemo Ofisi ya Rais, Utumishi ili kuweza kuyashughulikia na hizo taratibu kufuatwa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali, kwa maana ya kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi hilo jambo tumeshalichukua na tutakwenda kulifanyia kazi na Mheshimiwa Mbunge tutakapokuwa tayari tutakujulisha ili upate kujua hatua ambayo zimefikiwa katika jambo la kufidia hili gap lililopo katika upande wa walimu wako.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili nataka kumhakikishia Mbunge kwamba siyo taratibu za Serikali kutengeneza Waraka kwa ajili ya Halmashauri moja au Wilaya Moja. Waraka ni kwa ajili ya Tanzania nzima ili kuweza kukabiliana na changamoto iliyopo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imechukua kilio hicho na inakwenda kukifanyia kazi na itakapokuwa tayari tutakuja kumjulisha yeye pamoja na Bunge lako.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri naona umesimama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba niongezee majibu mazuri aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru juu ya eneo linalohusu watumishi kuwa wako kwenye harakati za kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine muda mwingi kuliko hata kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, wewe ni Mbunge unajua kinachotokea, jambo hili linapaswa kupatiwa majibu ya uhakika kwa sababu ni kweli kabisa kwamba watumishi wengi wanapangiwa mahala na wanakwenda kule kwa mipango ya harakati za kuanza kuondoka toka siku waliyofika. Ni ukweli kwamba huwezi ukazuia mobility ya watumishi wa umma kwa sababu wao ni binadamu kuna changamoto na mambo mbalimbali yanayowasibu pia.

Mheshimiwa Spika, wapo baadhi ya watumishi ambao wao ni wanandoa wanachangamoto kubwa unamkuta mume yupo Kigoma, mke yuko Mbeya familia hii inapata changamoto ya kutokuwa Pamoja, pia watumishi hawa hawatafanya kazi kwa ufanisi kwa sababu muda mwingi wanafikiria juu ya mwenza wake yuko mbali.

Mheshimiwa Spika, jambo hili wacha tulichukue tusijibu kwa haraka tukae na mamlaka za ajira na hasa TAMISEMI ili tuweze kutengeneza mfumo mzuri, tuangalie pengine inawezekana huko Tunduma ambako wanahama walipelekwa ambao hawapendi Tunduma lakini wako wengi wanaopenda kwenda Tunduma kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, tutajaribu kutengeneza utaratibu tuone tunaweza tukafanyeje bila kuvunja umoja na mshikamano wa Taifa letu kwa sababu pia kuwapangia watu kutoka sehemu aliyotoka huko huko itakuwa ni jambo, lakini wapo wanaoweza kuwa wanapenda kwa kiasi fulani, tunaweza tukafanya maamuzi hayo kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, ahsante sana. (Makofi)