Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:- Je, lini Serikali itaweka wazi vigezo vya kubaini kaya maskini zinazostahili kupokea msaada wa TASAF?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nitaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwa kuwa, umaskini unatofautiana kutokana na mahali kwa mahali. Maskini wa jamii ya wafugaji, makazi siyo kitu cha msingi kwake, lakini maskini wa mahali pengine makazi inawezekana ikawa ni kitu cha msingi kwake. Kwa hiyo, ni lini Serikali itaona haja ku-standardize hivi vigezo vya kuzipata kaya maskini ili jamii ile iepukane na migogoro? (Makofi)

Swali langu la pili, nitazungumzia vile vipengele vinne vya Miradi ya TASAF na nitazungumzia suala zima la Public Work Program kwamba, kwa kuwa miradi hii inapokamilika inakabidhiwa katika mitaa au vijiji. Ni lini sasa Serikali itaweka utaratibu maalum kuhakikisha kwamba wanashirikishwa wanakijiji wote au jamii yote ili miradi ile iwe vipaumbele kwa jamii husika badala ya zile kaya zilizolengwa? Ahsante sana. (Makofi)

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanaisha Ulenge, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza juu ya ku - standardize vigezo. Utaratibu wa kupata wahusika au wafaidikaji ni utaratibu kwanza shirikishi. Wananchi wanashirikishwa katika ngazi ya kijiji, wanajadili juu ya taratibu zao, wanajadili juu ya vigezo na kutambua wapi ambao wanatakiwa kufaidika katika mradi huo. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie, tunapokwenda hata kwenye jamii ya wafugaji, wafugaji wenyewe wanashirikishwa ili kuweza kutambua na kutanabaisha vipaumbele vyao. Hivyo pia tunapokwenda kwenye jamii za wakulima na jamii mbalimbali. Kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba taratibu ziko wazi, vikao vinayokaa ni shirikishi na wanavyohitaji wananchi ndivyo ambavyo mradi wetu wa TASAF unakwenda kusimamia.

Swali la pili juu ya vipaumbele ambavyo vipo katika maeneo yetu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyokuwa nimejibu katika swali la msingi na maelezo ya ziada katika swali lake la kwanza la ziada, kwa uhakika kabisa nataka nimuhakikishie yeye na kulihakikishia Bunge lako kwamba tunapokwenda katika vijiji mambo yote yanayotakiwa na wanayohitaji wananchi ndiyo kipaumbele cha mradi huo wa TASAF na siyo vinginevyo.