Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: - Je, lini barabara ya Ulinzi ya Hifadhi ya Mwalimu Nyerere inayojengwa toka Liwale hadi Mahenge itakamilika?

Supplementary Question 1

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninashukuru kwa majibu mazuri yanayotia tumaini kutoka Serikalini. Vilevile ninashukuru kwenye ile barabara yangu ya Nachingwea – Liwale, tarehe 12 yule mkandarasi anaenda kukagua. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hivyo, nina maswali mawili; barabara hii niliyoitaja inayounganisha Morogoro, tayari TANAPA wameshaanza kuichonga. Sasa tunachotaka kujua; je, sisi tunaweza kuanza kupita hata kabla ya huo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uliotajwa?

Swali la pili, tayari kwenye bajeti iliyopita tunayo barabara yetu ya Nangurukuru – Liwale kilometa 230. Tulishapewa kilometa 72 wananchi wa Liwale wanataka kujua ujenzi unaanza lini? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara hii ya Liwale kwenda Mahenge ambayo inapita katikati ya Hifadhi ya Mwalimu Nyerere, tumetenga fedha kama nilivyosema. Kwa maana ya kutumika kwa sasa waliofanya hiyo barabara ni wenzetu wa Maliasili na Utalii kwa shughuli zao, lakini sisi kama Wizara tunapokwenda kuifanyia upembuzi yakinifu ni kwa maana ya wananchi waweze kutumia.

Mheshimiwa Spika, tuna hakika kama tutakavyokuwa tumefanya usanifu, wenzetu wa maliasili watashauri ijengwe vipi ili iweze kutumika kama barabara ya kiulinzi, pia, iweze kuwahudumia wananchi wote wa Tanzania bila kujali ni wa hifadhi ama siyo hifadhi, ndiyo maana Serikali imetoa fedha ili kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi wa Liwale na Mahenge. Kwa hiyo, itaanza kutumika na wananchi kama itakuwa imekidhi hivyo vigezo.

Mheshimiwa Spika, suala la pili; ni kwamba, Barabara ya Nangurukuru – Liwale tumetenga tuanze ujenzi mwaka huu kilometa 72 kuanzia Liwale kwenda Nangurukuru. Ninataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tayari taratibu za manunuzi za awali zimeanza ili barabara hii ianze kujengwa. Ahsante.