Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Emmanuel Papian John

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Primary Question

MHE. EMMANUEL P. JOHN aliuliza:- Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi huko Kiteto baina ya wakulima na wafugaji:- (a) Je, ni lini Serikali itaipatia Kiteto Mahakama ya Baraza la Ardhi ili kesi nyingi ziweze kusikilizwa hapo Kiteto? (b) Je, Serikali ina mpango gani wa kupima ardhi yote ya Kiteto ili kila mtu afahamu mipaka ya eneo lake ili kuepusha mwingiliano wa maeneo usio wa lazima, itafanya hivyo lini?

Supplementary Question 1

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Emmanuel Papian.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na hali ya Kiteto ilivyo na wote mnafahamu, ningependa Mheshimiwa Waziri aniambie ni lini angeweza kufika Kiteto na kuzungukia hayo maeneo kama Waziri wa Ardhi, aweze kuona na kufanya mikutano ya hadhara ili aweze kuzungumza na wananchi wamweleze kero zao zaidi ya hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, naomba Wilaya ya Kiteto ipimwe maeneo yote kwa maana ya kila mtu ajue kipande chake cha ardhi ili kuepusha ile migogoro inayoendelea kwa sababu leo tunaendelea, lakini bado kuna vuguvugu la migogoro inayoendelea. Ahsante.

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBANI NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ameuliza ni lini tutazungukia Kiteto na kufanya mikutano ya hadhara. Naomba nimhakikishie tu kwa sababu zoezi hili la migogoro utatuzi wake utafanyika kwa nchi nzima na kama ambavyo Wizara imeshatoa kitabu cha migogoro, hivyo, muda unakapowadia katika suala zima la kuanza kuzungukia maeneo hayo na Kiteto pia tutafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameulizia ni lini sasa ardhi yote ya Kiteto itapimwa. Kama Waziri alivyotoa kwenye bajeti yake tumeanza na wilaya tatu ambazo ni wilaya za mfano ambazo tunakwenda kuanza nazo kazi na wameshaanza katika Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la upimaji ni suala ambalo linagharimu pesa nyingi na kama tulivyoeleza wakati tunatoa maelezo wakati tunamalizia bajeti, tulisema kwamba, halmashauri pia zinapaswa kutenga pesa kiasi kidogo ili kuweza kuanza upimaji katika maeneo yake, wakati Wizara pia inajipanga katika kuhakikisha kwamba ardhi ya nchi nzima inapimwa.