Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: - Je, lini Bandari ya Karema itafunguliwa na kuanza kufanya kazi kwa kuwa ujenzi umekamilika kwa asilimia 87?

Supplementary Question 1

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili bandari iweze kufanya kazi vizuri, inahitaji kuwa na barabara ya lami kutoka bandarini, lakini pia inahitaji kuwa na reli kwa ajili ya kubeba mizigo. Kwa kuwa barabara ya lami kutoka Karema kwenda Mpanda bado haijakamilika, na kwa kuwa Serikali bado haijajenga reli kutoka Karema kwenda Mpanda;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kujenga reli pamoja na barabara ya lami ili kuwezesha kubeba mizigo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuwa na bandari ambayo haifanyi kazi, ambayo haina meli, ni sawa na kuwa na nyumba ambayo haikaliwi na mtu. Ziwa Tanganyika halina meli inayofanya kazi sasa hivi, MV. Liemba haifanyi kazi na MV. Mwongozo haifanyi kazi;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inajenga meli ili ziweze kubeba mizigo kutoka Kongo na nchi za jirani?

Name

Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Answer

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Bandari yetu ya Karema inatakiwa ifungamanishwe na barabara kwa kiwango cha lami pamoja na reli. Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka wa fedha ambao tunauanza wa 2023/2024, kati ya kilometa 112 zote zimekwisha tangazwa na itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuifungua bandari hii ya Karema – Ikola mpaka Kagwira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anataka kujua meli katika Ziwa Tanganyika. Kama ambavyo tuliweza kuwasilisha bajeti yetu siku ya Jumatatu na Jumanne, tuliweza kutoa commitment kwamba kati ya Ziwa Tanganyika, meli tatu tunaendelea kuzikarabati, hususan Meli ya MT. Sangara inayobeba mafuta ambayo iko asilimi 90, pia kuna Meli ya MV. Liemba ambayo tayari mkataba wake tutasaini mwezi Juni, na MV. Mwongozo tumepata mkandarasi mshauri atakayeweza kuishauri Serikali namna gani ya kuifanya hii meli i-balance maana ilikuwa na shida ya stability.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo pia tumetenga fedha kwa kutengeneza meli kubwa mbili, moja ya mizigo itakayobeba tani 3,500 na nyingine ni ya kubeba abiria 600 pamoja na tani 400 ambayo kwa ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma, mlisema ikiwezekana ziwe mbili, na sisi Serikali tukasema tunakwenda kulifanyia kazi hili. Kwa hiyo hii ni mipango na tunakwenda kufanya katika mwaka wa fedha ujao, ahsante.