Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Primary Question

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga campus ya Chuo Kikuu Mzumbe katika Mkoa wa Singida?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; katika Wilaya ya Manyoni tuna uhitaji mkubwa sana wa chuo ambacho kinaweza kikatoa elimu ya afya katika ngazi ya cheti na diploma. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba, sasa wanasogeza kampasi ya chuo cha afya cha ngazi ya certificate and diploma katika Wilaya ya Manyoni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, kuna uhitaji mkubwa sana wa Wahadhiri katika vyuo vikuu vyetu na vyuo vya kati; na kwa kuwa, hivi karibuni Serikali imekuwa ikitumia mfumo wa usaili kuwapata Wahadhiri, hususan Tutorial Assistants, je, Serikali haioni haja ya kurudi kwenye mfumo wa zamani ambapo vijana waliokuwa wakipata first class walikuwa wakibakizwa vyuoni na kuendelezwa? Ahsante sana.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na jambo la kwanza, swali lake la kwanza analozungumzia suala la chuo cha afya. Naomba tuubebe ushauri wake tuweze kuangalia namna gani ya kufanya upande wa hivi vyuo vya afya, tukishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Afya au na taasisi nyingine binafsi, tuweze kuangalia namna bora ya kufanya katika upatikanaji wa vyuo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Dkt. Chaya, pale katika jimbo lake katika wilaya yake tayari sisi kama Wizara ya Elimu, kama Serikali, tumeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha VETA ambavyo huenda baadaye tukatohoa tu na hizo kada za afya vilevile zikaweza kufundishwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anazungumzia suala la wahadhiri. Ni kweli zamani tulikuwa na utaratibu katika vyuo vikuu, wale wanafunzi wanaofanya vizuri huwa wanabaki palepale chuoni kwa ajili ya kuwa Wahadhiri. Utaratibu huu hapa katikati ulisitishwa ili kuweza kuweka ushindani kwanza, lakini vilevile kuondoa upendeleo kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo, mamlaka yale sasa yalikasimiwa au yalipelekwa moja kwa moja kwenye Tume ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kutoa vibali vya kuajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokea ushauri huo hata wakati tunakusanya maoni wakati wa mapitio ya mitaala suala hili lilizungumzwa sana. Kwa hiyo, tuachie kama Serikali twende tukalifanyie kazi, ili tuweze kuangalia namna bora ya kurudisha utaratibu ambao utakuwa mzuri na kutoa fursa kwa kila Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Name

Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Primary Question

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga campus ya Chuo Kikuu Mzumbe katika Mkoa wa Singida?

Supplementary Question 2

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Mkoa wa Njombe ndio Mkoa ambao hauna chuo kikuu wala chuo cha juu na Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Njombe tarehe 9 Agosti, 2022 alipokea ombi la wazee wa Njombe kuhusu kujengewa chuo kikuu katika Mkoa wa Njombe na Mji wa Njombe. Je, Serikali itaanza lini mchakato wa kuhakikisha kwamba na sisi tunapata chuo kikuu?

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli Mheshimiwa Rais alifanya ziara katika Mkoa wa Njombe, tarehe 9 Agosti, 2022 na miongoni mwa ahadi alizozitoa ni ujenzi wa kampasi mojawapo ya chuo kikuu pale Njombe, ingawa katika mgawanyo huu wa miradi ya HEET katika mikoa ambayo haitapata fursa katika awamu hii ya kwanza ni Mkoa wa Njombe. Kwa vile tayari Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alishatoa hiyo ahadi na sisi kama Serikali ahadi hii ya Mheshimiwa Rais tunaendelea kuifanyia kazi, hivyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mwanyika na wananchi wa Mkoa wa Njombe, tuko njiani kuja Njombe na tutahakikisha kwamba, tunaleta taasisi ya elimu ya juu katika Mkoa wa Njombe.