Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Primary Question

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. SALIM A. HASHAM aliuliza: - Je, lini Serikali itajenga kwa kwango cha lami barabara ya kutoka Ifakara hadi Mahenge?

Supplementary Question 1

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nashukuru sana Serikali kwa kuanza mchakato wa barabara hizi za kufungua Mkoa wa Morogoro. Sasa kipande cha Ifakara - Lupilo kimetangazwa.

Sasa swali langu la kwanza, je, ni lini kipande cha Lupilo – Mahenge – Liwale kitaanza ujenzi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kipande hiki cha Ifakara – Lupilo kitapita by pass ya Ifakara Mjini ambako wananchi wa Kata ya Mbasa na Katindiuka wamesubiri kwa muda mrefu sana, zaidi ya miaka minne kulipwa fidia na Serikali yao.

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hawa pamoja na hasara ya kusubiri zaidi ya miaka minne? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kipande cha Barabara ya Lupilo – Mahenge - Liwale kina sehemu mbili. Kwanza kuanzia Lupilo hadi Mahenge ni barabara kuu ambayo itakuwa ni sehemu ya ujenzi kwenye barabara hii kubwa ambayo nimeitaja kwa mpango wa EPC, lakini kuanzia Mahenge kwenda Ilonga hadi Liwale tumesema mwaka huu tumeingiza kwenye mpango wa kuanza kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu, maana hiyo barabara haipo lakini Serikali kwa sababu ya maombi ya muda mrefu kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Lindi tumeshaweka kwenye mpango wa kuanza kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu by pass ya Ifakara; hii by pass ya Ifakara ni sehemu ya huo mpango mkubwa na kitakachofanyika sasa ni pamoja na kuhuisha zile tathmini zilizofanyika kwa wananchi ambao wataathirika na mradi huu kwa ajili ya kuwalipa fidia. Kwa hiyo watakuwa ni sehemu ya huo mradi mkubwa ambao tunaenda kuutekeleza, ahsante.