Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 1

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa majibu ya Serikali, swali langu lilisema ni lini? Sasa Serikali wanasema wapo kwenye hatua za kukamilisha utaratibu wa financial. Sasa nataka kufahamu, huu utaratibu wa financial utakamilika lini ili kuweza kutoa pesa kwa ajili ya kujenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami kwa sababu Wilaya ya Nachingwea na Wilaya ya Masasi na Wilaya nyingine pale hazijaunganishwa kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kuna barabara ambayo pia inaendelea kujengwa kwenye eneo hilo hilo kati ya Nanganga – Ruangwa, inaunganisha hizo Wilaya mbili, lakini jengo la Chama cha Mapinduzi, Ofisi ya Kijiji, Msikiti pamoja na majengo ya wananchi mbalimbali yalivunjwa sawa sawa na hii barabara ninayoisema ya Nachingwea – Masasi: Ni lini Serikali italipa fidia kwa watu hawa waliopata athari za kuvunjiwa majengo yao kwa sababu ya ujenzi wa barabara? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na suala la kwanza ambalo pia umetaka nitoe maelezo kwa Waheshimiwa wote. Ni kweli tuna barabara nane ambazo zimeingizwa kwenye mpango wa EPC + F. Katika barabara nane, barabara itakwenda kwa Mpango wa PPP ambayo ni barabara ya Kibaha - Chalinze hadi Morogoro. Hiyo itaingia kwenye PPP na barabara zilizobaki hizo saba ambazo ni pamoja na hii niliyoisoma ya Masasi – Nachingwea hadi Liwale zimeingizwa kwenye Mpango wa EPC + F.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ni mfumo ambao ni mpya ambapo wakandarasi wanatafuta fedha, wanajenga, halafu Serikali inatafuta utaratibu wa namna ya kuja kuwalipa kwa makubaliano ambayo yatakuwepo. Sasa kuna sehemu mbili; kuna sehemu ya Engineering ambayo ni Wizara ya Ujenzi wanakwenda na wakandarasi wanaangalia, wana-bid, wanaagalia kwa upande wa ufundi na kuona kwamba wamekubaliana, halafu baada ya hapo sasa, wanapeleka hiyo mikataba Wizara ya Fedha ili kuona kama kwa kuingia nao mikataba hiyo Serikali itakuwa imefanya jambo sahihi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mfumo ambao ni mpya ambao ni lazima Serikali iende kwa umakini sana ili tusije tukaingia kwenye mkataba ambao hatukujipanga vizuri. Kwa hiyo, kuna umakini mkubwa sana ambao unafanyika ili tuweze kwenda na miradi hii mikubwa ambayo kama tutaijenga, basi tutakuwa tumepunguza kero nyingi sana za usafiri. Tumechukua barabara nyingi zile ambazo ni ndefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa idhini yako nitataja barabara chache. Ni Barabara ya kutoka Ifakara – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo hadi Namtumbo. Tuna barabara ya Mafinga hadi Mgororo, tuna barabara ya Kongwa – Kibaya hadi Arusha, tuna barabara ya Karatu hadi Arusha, tuna barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom hadi Sibiti. Pia tuna barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Liwale; na tuna barabara ya Igawa – Songwe hadi Tunduma. Hizo ni baadhi ya barabara ambazo zimeingia kwenye mpango huu. Kwa hiyo, ukiangalia ni barabara kubwa ambazo tungetamani tuzijenge kwa wakati mmoja kwa utaratibu huu wa EPC +F, ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara inayotoka Dodoma kwenda Iringa ina mashimo, yaani haipitiki, ni shida tupu.

Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kwenda kufukia tu yale mashimo badala ya kusubiri muda eti ya kuikwangua barabara yote kiasi ambacho itachukuwa muda mrefu? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ntara, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara ya Dodoma – Iringa ina mashimo lakini atakubaliana nami kwamba jitihada zimekuwa zikifanyika sana za kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo ni korofi yanazibwa na yanaendelea kuzibwa. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zina madaraja. Kwanza, ukiangalia madaraja yapo mengi, sasa wakati tunajenga hiyo barabara traffic haikuwa imetegemewa kama ilivyo sasa. Kwa hiyo sasa hivi bado tunaendelea kufanya economic design kuona namna ya kuboresha hiyo barabara kwa sababu sasa imeoneka ni barabara ambayo inapitisha traffic nyingi lakini pia kuna magari mengi makubwa na mazito ambayo yanapita kwenye hiyo barabara, ahsante. (Makofi)

Name

Timotheo Paul Mnzava

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Vijijini

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 3

MHE. TIMETHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ukizingatia kwamba kazi ya upembuzi na usanifu ulikamilika muda mrefu: Ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuijenga kwa lami barabara ya kutoka Korogwe – Dindira – Bumbuli mpaka Songwe?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema ni kweli barabara hiyo ni muhimu na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tusubiri bajeti tutakayoisoma, naamini kuna mapendekezo ya kuianza kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Name

Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 4

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Kilosa kwenda Mikumi inaungana na Mji wa Kilosa ambako kuna uwekezaji wa mabilioni ya hela station ya SGR lakini kipande hiki kimekuwa kimeingia kwenye bajeti kwa miaka mitano mfululizo bila utekelezaji. Sasa kwa kuwa sisi wengine hatujui kuruka sarakasi ndani ya Bunge, ni lugha ipi ambayo unataka tutumie kuwaeleza Serikali barabara hii ni muhimu kutengenezwa?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba Serikali ilishaanza kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami hadi Kilosa na tumetenga na tumeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuendelea kwenda Ulaya hadi Mikumi na ni azma ya Serikali kuunganisha hii Barabara ya Morogoro kutoka Dodoma kwenda Morogoro na Morogoro kwenda Iringa kupitia Kilosa hasa tukitambua umuhimu wa hiyo barabara kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafahamu na ndiyo maana imeanza kutenga fedha na hata kwenye kipindi hiki cha bajeti nina hakika hiyo barabara itaendelea kutengewa fedha ili kuijenga japo siyo yote lakini kwa awamu.

Name

Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea kwa kiwango cha lami?

Supplementary Question 5

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, napenda kujua ni lini Barabara ya Omugakorongo kwenda mpaka Murongo itajengwa ukizingatia Wilaya ya Kyerwa haina lami hata kilometa moja ukiachana na lami ya mchongo ambayo iko Nkwena? Nataka kujua ni lini kwa sababu imechukua muda mrefu?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anatropia, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja ya Omugakorongo hadi Murongo tunavyoongea sasa hivi iko kwenye hatua za manunuzi na nina hakika kabla ya kumaliza mwaka huu wa fedha barabara hiyo itakuwa imeanza na nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii itaanza kujengwa upande wa Murongo kuja Omugakorongo ili tuweze kujenga lile Daraja la Mto Kagera ambao unapakanisha sisi na Uganda.