Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha kuvuja kwa mitihani nchini?

Supplementary Question 1

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali bado tabia ya kuvujisha mitihani imeendelea. Ni vipi Serikali inaenda kukomesha tabia hii? Nadhani ndiyo swali langu la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mara nyingi tumeshuhudia wazazi na watoto wasio na hatia kubebeshwa mzigo wa kufutiwa matokeo na muda mwingine shule kufungwa. Ni kwa namna gani Serikali itaondoa mzigo huu kwa wazazi na watoto wasio na hatia? (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, nitajibu maswali mawili yote kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa suala la uvujaji wa mitihani halipo, mara ya mwisho mitihani ilivuja mwaka 2008 na ulikuwa ni mtihani mmoja wa somo la hisabati Kidato cha Nne. Kutoka mwaka 2008 hakujawahi kutokea uvujaji wa mitihani.

Mheshimiwa Spika, kinachotokea ni udanganyifu katika mitihani kwenye baadhi ya maeneo, kwa sababu suala la mitihani ni suala la mchakato ambayo inahusisha utungaji wa mitihani, ufungaji wa mitihani, usafirishaji wa mitihani lakini baadaye tunakwenda kwenye vituo vya kufanyika mitihani. Kwa hiyo, matukio ya udanganyifu kwenye baadhi tu ya maeneo baada ya mitihani kufunguliwa na kuingia kwenye vyumba vya mitihani, vijana au Walimu au Wasimamizi wamekuwa labda wakiingia na nyaraka ambazo hazitakiwi kwenye ufanyikaji wa mitihani, pale ndipo inatokea udanganyifu wa mitihani. Lakini suala la uvujaji wa mitihani tulishalitokomeza kama Serikali na sasa hivi tunapambana na suala hili la udanganyifu wa mitihani ndipo tunaona kwamba wale wanaohusika kwenye udanganyifu ndiyo wanaochukuliwa hatua.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Name

Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha kuvuja kwa mitihani nchini?

Supplementary Question 2

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali moja la nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kuongeza posho kwa usimamizi wa mitihani, kwa sababu zoezi la usimamizi wa mitihani ni gumu wakati mwingine linagharimu ustawi wa maisha ya msimamizi husika?

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maimuna Mtanda Mbunge wa Newala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Hivi sasa taratibu za usahihishaji wa mitihani tunakwenda kubadilika kwa sababu tunakwenda kwenye e-marking. Tumeanza kwa mitihani ya Darasa la Saba na sasa hivi tuko kwenye pilot ya mitihani ya Ualimu na baadae tutakwenda kwenye mitihani ya Form Four na Form Six. Kwa hiyo kwanza tutapunguza sana gharama za Walimu kusogea kwenye maeneo yale ambayo tunasahihisha mitihani badala yake mitihani itakuwa inasahihishwa huko huko Mikoani.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo wakati tunakwenda kuboresha mifumo hii ya usahihishaji wa mitihani vilevile tunakwenda kuboresha na posho zile za wasahihishaji wa mitihani na wale wataokuwa wanasimamia mitihani hii. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi hili tayari liko kwenye bajeti zetu na linakwenda kukaa sawasawa. Nakushukuru sana.

Name

Maryam Azan Mwinyi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha kuvuja kwa mitihani nchini?

Supplementary Question 3

MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali inachukua hatua gani ya kudhibiti udanganyifu badala ya kusubiri udanganyifu ndiyo mnatoa adhabu?

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maryam kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyozungumza kwenye majibu yangu ya msingi jukumu letu kama Wizara, jukumu letu kama Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatoa elimu ya kutosha ya athari za udanganyifu wa mitihani kwa wasimamizi vilevile kwa wale wanafunzi ambao kwa namna moja au nyingine wanaathirika kwa kiasi kikubwa kwenye zoezi hili. Kwa hiyo, jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunatoa elimu watu wasifanye udanganyifu katika mitihani kwa sababu athari zake ni kubwa kwa wao wenyewe binafsi lakini na kwa Taifa kwa ujumla. Nakushukuru sana.

Name

Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha kuvuja kwa mitihani nchini?

Supplementary Question 4

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali inatumia Polisi kusimamia mitihani ya wanafunzi. Je, haioni kwa kutumia Polisi wanafunzi wanapata taharuki na kushindwa kufanya mitihani yao kwa uhuru? ahsante.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Yustina kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge. Polisi hawaendi kusimamia mitihani, kwa sababu hakuna Polisi ambaye anaingia kwenye chumba cha mtihani. Polisi ni sehemu ya kikosi kazi au ni sehemu ya Kamati zetu ambazo zinaratibu pamoja na kuhakikisha kwamba usalama wa kituo cha mtihani pamoja na uhifadhi wa mitihani yetu. Lakini hakuna Polisi ambaye anaingia ndani ya chumba cha mtihani na kuanza ku-invigilate wale wanafunzi wakati wanaendelea na mchakato wa mtihani. Lakini wako pale kwa mujibu wa sheria kuhakikisha kwamba usalama wa kituo pamoja na usalama wa mitihani yetu pale inapohifadhiwa pamoja na ufanyikaji inakwenda sawasawa lakini siyo kuingia ndani ya kituo au darasa ambalo mitihani inafanyika.

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Primary Question

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: - Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha kuvuja kwa mitihani nchini?

Supplementary Question 5

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Suala la uvujaji wa mitihani ni ukosefu wa maadili wa kuanzia anayeandaa, mratibu na anayesimamia. Sasa nataka kujua mkakati wa Serikali ambao unaenda kusaidia suala hili la ukosefu wa maadili ni upi? ahsante. (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Sima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi kwamba uvujaji wa mitihani kwa mara ya mwisho ulitokea mwaka 2008. Na kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili ni suala la kimaadili na sisi kama Serikali wajibu wetu ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kutoa elimu kuanzia kwa wale ambao wanaotunga mitihani vilevile wale wanaofunga, wanaosafirisha mpaka wale ambao wanakwenda kusimamia zoezi hili la ufanyikaji wa mitihani.

Kwa hiyo tunafahamu ni suala la kimaadili na tumekuwa tukitoa mavunzo ya athari za uvujaji wa mitihani kwa namna moja au nyingine, lakini nimwondoe wasiwasi kwa kiasi kikubwa na kama tukichukua takwimu kwa mara ya mwisho tukizungumza hilo suala la udanganyifu tu mwaka 2011 udanganyifu ulifanyika kwa wanafunzi 9, 736.

Mheshimiwa Spika, lakini mwaka 2021 ni wanafunzi 393 tu ndio ambao walifanya udanganyifu kwenye mitihani. Kwa hiyo tunaendelea kudhibiti na tunaamini baada ya muda si mrefu tunaweza tukapata achievement kubwa kuhakikisha kwamba hakuna mtu ambaye atajihusisha na udanganyifu wa mitihani.