Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza: - Je, ni kwa nini Serikali haijagawa fedha kwa ajili ya ufugaji wa vizimba vya samaki katika Ziwa Nyasa?

Supplementary Question 1

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa nini Serikali inadhoofisha ustawi wa Ziwa Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma ikiwa pamoja na kuwadhoofisha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma hususani Wilaya ya Nyasa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Rais ametenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuendeleza Maziwa, lakini bilioni 20 hizi zote zinapelekwa katika Ziwa Victoria, je, kwa nini Serikali haiweki uwiano sahihi katika Maziwa yote haya matatu ikiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Nyasa na Ziwa Tanganyika? (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jacqueline Msongozi.

Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali hili kwa ruhusa yako sekunde moja, naomba nitumie fursa hii ndani ya Bunge hili Tukufu, kumshukuru Mwenyezi Mungu na pili kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwangu na kunikabidhi kazi hii ya kuongoza Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Naomba pia niendelee pia kuomba ushirikiano kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu wakati wote wa kutekeleza majukumu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maswali ya Mheshimiwa Msongozi la kwanza juu ya kudhohofisha Ziwa. Nataka nimhakikishie yakwamba Serikali haina mpango wa kudhoofisha Ziwa Nyasa na katika bajeti hii ya 2022/2023 na hata katika bajeti ya 2021/2022 Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inayo mambo iliyofanya katika Ziwa Nyasa ikiwemo ujenzi wa Soko katika Jimbo la Nyasa linaloongozwa na Mheshimiwa Mbunge Engineer Stella Manyanya. Hivi sasa tupo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha hatua za ujenzi wa soko lile ilimradi tuweze kuliruhusu liweze kutumika, lakini kama haitoshi kuhusiana na…

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, tusaidie kufupisha hayo majibu tafadhali.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jibu la pili, uwiano, katika jibu la msingi alilolitoa Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye nampongeza kwa majibu yale mazuri, ni kwamba hatua ya mwaka huu ni hatua ya Ziwa Nyasa. Naomba Mheshimiwa Mbunge Msongozi na Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, lakini pia vilevile na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma wawe na uhakika kwamba sasa zamu yao na wao inafikiwa baada ya hatua hizi za msingi kuwa zimetekelezwa ikiwa ni pamoja na Ziwa Rukwa pia vilevile litafikiwa, ahsante sana. (Makofi)