Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Minara katika maeneo yasiyo na minara na kutatua matatizo ya mawasiliano katika maeneo yenye Minara?

Supplementary Question 1

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante. Kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Lakini yeye mwenyewe anaelewa kwamba kuna kata tisa. Kwa hiyo ukiangalia idadi ya kata ambazo zinashughulikiwa bado nyingi zitakuwa na matatizo yale yale ambayo yanaendelea na kuwapa shida wananchi.

Je, Serikali, kutokana na umuhimu wa mawasiliano kwa upande wa kiuchumi na kijamii, inatoa tamko gani la kuwapa matumaini kata zile ambazo bado zina matatizo ya mawasiliano?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya wananchi wa Urambo, na kwa kweli ameonesha ushirikiano mkubwa pale ambapo Serikali inapohitaji msaada wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba tunatambua kabisa kwamba kuna changamoto ya mawasiliano katika Jimbo hili la Urambo ambapo jimbo hili lenye kata 18; na katika hizo kata 18 kata tisa ndizo ambazo zina changamoto, si kwamba hazina mawasiliano, zina changamoto. Kata hizo ni; Kata ya Uyumbu, Muungano, Vumilia, Busoke pamoja na Songambele. Kata zote hizo tunafahamu kabisa kwamba zina changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidigital tayari tumeanza na kata tatu. kwa hiyo tunaamini kabisa kwamba tunapoenda katika utekelezaji wetu tukishakamilisha kata hizi tatu tunaamini hata zile kata sita ambazo zimebaki tutazifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)

Name

Oliver Daniel Semuguruka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Minara katika maeneo yasiyo na minara na kutatua matatizo ya mawasiliano katika maeneo yenye Minara?

Supplementary Question 2

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Changamoto kubwa inayokabili wananchi wa Ngara ya mawasiliano ya simu ni kuingiliana na nchi jirani za Rwanda na Burundi.

Ninataka kujua, ni nini mkakati wa Serikali ili kutatua changamoto hiyo?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Oliver Semuguruka Mbunge wa Viti Maalum Kagera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kabisa kwamba ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge huyu ameendelea kuwa msumbufu kweli kweli kwa ajili ya kuhakikisha maeneo hayo yanatafutiwa ufumbuzi. Lakini vilevile natambua pia usumbufu ambao nimeendelea kuupata kutoka Mbunge wa Jimbo la Ngara Mheshimiwa Ndaisaba kwa sababu haya maeneo tuliyatembelea na tukagundua kabisa kuna changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo; ya kwanza, si kwamba hatuna minara, kuna maeneo ambayo tuna minara lakini nguvu yake haikuwa inatosha. Hivyo tulitoa maelekezo kwa watoa huduma kuhakikisha kwamba minara yao inakuwa na nguvu ili huu mwingiliano usitokee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna maeneo mengine ambayo hatukuwa na minara ndiyo maana mwaka jana sasa kupitia mradi wa special zone na borders, yaani mipakani na maeneo maalum, tulihakikisha kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo tunaenda kujenga minara yakiwemo maeneo ya Ngara ambapo kuna miradi tisa ambayo inaenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Name

Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Minara katika maeneo yasiyo na minara na kutatua matatizo ya mawasiliano katika maeneo yenye Minara?

Supplementary Question 3

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya changamoto ya mawasiliano ambayo Mheshimiwa Waziri anakiri watu wamekuwa wakinunua bando, kwa sababu ya kuingia na kutoka kwa internet mtu anajikuta bando lake lina-expire kabla wakati hajalitumia. Sasa, kwa sababu hiyo, Je, Serikali haioni ipo haja ya kutengeneza utaratibu bando liwe linachajiwa kwa matumizi kwamba linaisha kwa sababu umetumia badala ya kuchajiwa kwa sababu muda wa lile bando umekwisha?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salome Makamba Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kulikuwa na changamoto hiyo lakini Serikali ikalitambua hilo na njia pekee ya kutatua changamoto hiyo ni Serikali tulitoa maelekezo ya kuhakikisha miradi yote inayojengwa nchini sasa inajengwa ikiwa na uwezo wa kutoa huduma ya internet hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tulibadilisha kanuni zetu pale ambapo unaona kabisa kwamba muda wako unaelekea kuisha lakini bando lako bado linatosha inawezekana ulikuwa umesafiri ukaenda sehemu ambayo haina internet basi utapata fursa ya kuhamisha au kujiunga na kifurushi kingine lakini na ile balance uliyokuwa nayo unai- carry forward.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kupitia hizi njia ambazo Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba inaboresha huduma ya mawasiliano tunaamini kabisa kwamba kupitia njia hizi na mabadiliko ya kanuni zetu itawezesha wananchi kutumia bando lao na mpaka linaisha. Ahsante.

Name

Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Minara katika maeneo yasiyo na minara na kutatua matatizo ya mawasiliano katika maeneo yenye Minara?

Supplementary Question 4

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kata ya Roche, Ikoma, Bukura pamoja na Goribe ni miongoni mwa kata ambazo ziko mpakani kati ya Tanzania na Kenya. Mheshimiwa Waziri nafikiri ulipata ridhaa ya kuzitembelea kata hizi ukaona hazina mnara na hakuna mawasiliano yote katika kata hizi. Nilitaka nijue katika zile minara ambayo umesema wanaitangaza mwezi Juni kama kata hizi nazo zinapata nafasi ya kutangaziwa ili waweze kupata mnara kuboresha na kuweka mawasiliano kwenye maeneo haya ya mpakani na kimkakati?

Name

Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana Mheshimiwa Chege kwa sababu tumekuwa tukishirikiana vizuri sana; na maeneo na kata ambazo amezitaja Mheshimiwa chege tulishafika katika maeneo hayo. Vilevile katika mpango wa utekelezaji wa Tanzania Kidigitali tayari maeneo haya tumeyaingiza na Mheshimiwa Chege tayari anafahamu hilo. Kwa hiyo. kilichobaki sasa ni utekelezaji tu na tayari mkandarasi yuko tayari kwa ajili ya kuanza kazi mara moja kwa ajili ya maeneo hayo katika Jimbo la Rorya. Ahsante.