Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: - Je, nini mpango wa Serikali katika kuharakisha kesi za mauaji ambazo huchukua muda mrefu kusikilizwa?

Supplementary Question 1

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza niipongeze sana Wizara ya Katiba na Sheria kwa hatua mbalimbali ambazo wanachukua za kuboresha mfumo wa katiba na sheria nchini.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa watuhumiwa wengi wa makosa ya mauaji wanakaa rumande kwa muda mrefu sana wakisubiri mashauri yao kusikilizwa na watuhumiwa wengi wengine wanafia rumande wakisubiri kesi zao. Naomba kujua ni kwa nini Serikali isiteue Majaji wa muda mfupi ad hoc judges au acting judges wakasikilize mashauri haya kwa haraka?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa kesi nyingi za mauaji zinacheleweshwa kwa sababu ya Idara ya Upelelezi kuchelewa kufanya wajibu wake, aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya. Je, ni lini Serikali italeta Bungeni sheria ya kuweka ukomo wa makosa ya mauaji ambayo upelelezi haukamiliki? Ahsante.

Name

Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nipende kumjibu Mheshimiwa Mbunge maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza pamoja na uhaba wa Majaji tulionao, bado sisi kama Serikali Waziri wakishauriana na Mheshimiwa Jaji Mkuu, wamefanya zoezi la kuwaongezea mamlaka wale Mahakimu ambao ni wa mahakama hizi za ngazi mbalimbali ambazo zinaendesha kesi ambazo hazina mamlaka wao kusikiliza kesi za mauaji. Kwa hiyo, tunao Mahakimu nje ya Majaji 153 ambao wameongezewa mamlaka za kusikiliza kesi za mauaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukiliangalia suala la kesi hizi upande wa mahakama haina kuchelewesha kesi, isipokuwa kwenye eneo hili la upelelezi ambalo kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, tumeamua kuunda timu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo tumemshirikisha Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, pamoja na Ofisi ya DPP, kuharakisha upelelezi wa hizi kesi ili kuhakikisha kwamba zinaisha kwa wakati. Mpaka sasa tayari timu iko mikoani na inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mpaka kufikia mwishoni mwa Mei, hili suala la mrundikano wa kesi utakuwa umekwisha.

Mheshimiwa Spika, hili suala la kuja na sheria, bado tuna taratibu na kanuni na sheria vilevile zinazoonyesha kipindi cha upelelezi cha kesi, lakini matukio ni mengi sana kwa sasa hivi, kwa hiyo, kila siku kesi za mauaji nyie wenyewe mtakuwa mashahidi zinazaliwa kila siku. Kwa hiyo, ndiyo maana tumekuja na huu mkakati ambao tutakuwa tunatumia hawa Mahakimu ambao hawapo katika vigezo vya kusikiliza kesi za mauaji kuwaongezea nguvu. Vile vile tutahakikisha kwamba tunakimbiza hizi kesi na zinakwenda kumalizika kwa wakati, bila kuchelewesha aina yoyote kesi za mauaji.