Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Primary Question

MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: - Je, ni nini kinachelewesha ujenzi wa barabara kutoka kutoka Tabora – Mambali – Bukene hadi Kangogwa ilihali ilishatengewa bajeti?

Supplementary Question 1

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kipande cha KM 65 katika barabara hii kutoka Nzega, Itobo mpaka Kagongwa, ndicho kitatumika kubeba mzingo mkubwa wa mabomba ya mradi wa mafuta kutoka Hoima - Uganda mpaka Tanga, kwa hali ilivyo sasa barabara ile ni nyembamba, madaraja madogo haiweze kabisa kubeba mzigo huo mzito wa hayo mabomba ya mradi wa bomba la mafuta.

Mheshimiwa Spika, nilishashauri Wizara ya Ujenzi ikae na Wizara ya Nishati pamoja na wenye mradi EACOP ili waweze kuzungumza namna ambavyo hizi KM 65 kutoka Nzega - Itobo na Kagongwa namna ambavyo wanaweza kuzishughulikia kwa haraka ili mzigo huu mzito uweze kupita.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba Wizara imefikia wapi kukuaa na Wizara ya Nishati na hawa wenye mradi EACOP ili kuzungumzia namna kushughulika na hiki kipande cha KM 65 ili mzigo wa mabomba uweze kupita kwenda kwenye site.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Selemani Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukuwe nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Zedi kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia barabara hii na hasa hiki kipande alichokitaja. Katika eneo alilolitaja ndio kutakuwa na kituo kimoja kikubwa sana kwa ajili ya ujenzi wa bomba la mafuta. Kwa hiyo, anachosema barabara ile haiwezi kuhimili kubeba uzito wa magari yanayopita na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo sasa inakuwa ni barabara ya Taifa kwa ajili ya uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kuratibu pamoja na wadau wengine ikiwemo Wizara ya Nishati, EACOP na wadau wengine kuhakikisha kwamba tunaijenga hii barabara ili tutakapoanza kazi hii barabara isije ikawa ni kikwazo kwa maana ya madaraja na upana wa barabara yenyewe.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge taratibu zipo zinaendelea. Ahsante. (Makofi)