Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Primary Question

MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: - Je, ni Vijana wangapi hawana ajira nchini na Serikali imewaandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi?

Supplementary Question 1

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Moja; Serikali ina makakati gani wa dharura wa kudhibiti biashara holela, uingiaji wa mikataba mibovu na usimamizi hafifu wa sheria ambazo kasoro hizo zinasababisha ajira nyingi za Watanzania kupotea?

Mbili; kwa nini Serikali isiachane na utaratibu wa sasa hivi wa baadhi ya ajira kupatikana kwa njia ya uteuzi na badala yake ajira zote zikapatikana kwa njia ya ushindani, ajira za Viongozi na ajira za Watendaji, Mawaziri, Wakurugenzi na Makatibu Wakuu na Watendaji wengine wote wa Serikali ili kuiwezesha Serikali kupata Viongozi wenye uwezo usiotiliwa mashaka katika nafasi mbalimbali za Serikali? (Makofi)

Name

Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameeleza ni mkakati gani ambao Serikali imeendelea kuchukua kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hakuna mikataba mobovu pia utumiaji mzuri wa fedha ambazo zinaenda kwenye maeneo ya uwekezaji ili kuweza kulinda ajira za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayofuraha kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba tayari Serikali kupitia vyombo vyake muhimu imekwisha kuanza kuchukua hatua na mtakumbuka Mheshimiwa Rais katika nyakati zote amekuwa akichukua hatua katika kuimarisha vyombo vyetu vinavyosimamia sheria, ikiwemo Mahakama lakini pia Polisi, TAKUKURU kwa maana ya PCCB (Prevention and Combating Corruption Bureau) ambayo inapambana na maswala ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine Serikali imeendelea kuweza kuchukua hatua kwa wale ambao wamekuwa wakiingiza katika mikataba mobovu, hatua mbalimbali zimekwisha kuchukuliwa na Serikali tayari ina Mahakama maalum kuchukua hatua kwenye masuala ya rushwa. Kwa mfano, tunayo Mahakama ambayo inasimamia masuala ya makosa ya kiuchumi, ambayo hii mojawapo ni kudhibiti haya ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake pili ameeleza kwamba ajira kwa nini zisipatikane kwa njia ya ushindani badala ya uteuzi jinsi ilivyo. Kwa sasa, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza namna na mfumo wa uendeshaji wa Serikali na inatambua uwepo wa ajira ambazo zinapatikana kwa utaratibu ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema wa ushindani lakini pia zipo ajira zinazopatikana kwa njia ya uteuzi kulingana na provisions zilizopo katika Katiba, zipo pia ajira ambazo zinapatikana kwa utaratibu wa kuomba ama kuzipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo katika kupanua wigo wa ajira, Serikali imekwisha kuchukua mikakati ya kuhakikisha tunatafuta ajira ndani na nje ya nchi. (Makofi)