Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itabadilisha Sera ya Chanjo kitaifa ili kuwakinga watu wengi zaidi badala ya kutibu mtu aliye na ugonjwa tayari?

Supplementary Question 1

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningeomba niweke wazi swali langu lililenga kichaa cha mbwa na kwa sababu kwangu Urambo watu 21 waliumwa na mbwa mwaka jana mwaka 2022 na kati ya hao 21 walioumwa na mbwa 12 walifariki ndio maana nikauliza swali hili. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kichaa cha mbwa kwa kushirikiana na Wizara nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, mtu anaeyeumwa na mbwa mwenye kichaa anatakiwa achomwe sindano tano, na sindano moja ni elfu 30,000. Sindano ya kwanza inabidi alipe 35,000 kwa ajili ya ile ada ya kujiandikisha, sasa wengi wanashindwa kulipa 155,000. Je, Serikali inasemaje kuhusu kupunguza gharama za matibabu? (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu katika hao wagonjwa wake 21, wengi kabisa amekuwa akija kwangu na akihangaika kuhakikisha wanapata tiba. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge sisi na Wizara ya Mifugo tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwanza, sio tu uwepo wa tiba kwa ajili ya watakao kuwa wameumwa lakini mbwa wetu kuhakikisha wanakuwa wanachanjwa na nitumie fursa hii kuwaomba Wakuu wa Wilaya na Wilaya zetu ma DMO kuhakikisha wanashirikiana na wenzetu kuhakikisha mbwa walioko mtaani wanatafuta solutions lakini pia kuhakikisha wenye mbwa wanakwenda kuchanja mbwa wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini amezungumzia suala la gharama 155,000; Waheshimiwa Wabunge ndiyo maana kila wakati hapa tunakuja na Muswada Bima ya Afya kwa wote, leo hapa nilipokaa kwenye kiti change hapa, nina wabunge zaidi ya watatu mmoja anadaiwa milioni tisa mwingine anadaiwa milioni sita na mwingine milioni 4.8, anatakiwa kulipa na wagonjwa wa jimbo lake wameshindwa kulipa. Maana yake ninashukuru tumefanikiwa kuwasaidia Wabunge lakini tunaweza kuwasaidia wangapi? Ndiyo maana wakati wote tunasema na tusisitiza na nitumie fursa hii kuwaomba Wabunge wenzangu kama tunataka kuondokana na matatizo haya ni lazima wote kwa pamoja tukubaliane kwamba suala la bima ya afya kwa watu wote ni la msingi sana ili tuweze kuondokana na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nitumie fursa hii kuwaomba Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuwa mtu yeyote akiumwa na mbwa cha kwanza sisi tunachotaka ni kuokolewa kwa maisha, wasifikirie hela wamtibu mtu ndio suala la fedha lifuate. Waache tabia ya kuwanyima watu tiba eti kwa sababu hawana fedha. Pia MSD, niwaagize MSD kwamba kuanzia sasa hatutategemea kusikia hospitali yoyote mgonjwa amekwenda na hakuna dawa za kusaidia watu walioumwa na mbwa. Tunataka dawa zote za magonjwa ambayo sio magonjwa ambayo yanaoneka kila wakati ziwepo, lakini dawa za kichaa cha mbwa ziwepo kwenye kila hospitali na watu wakiumwa wapewa priority ya kutibiwa mapema, ahsante sana.